Nenda kwa yaliyomo

Zinaa

Kutoka wikishia
Makala hii inahusiana na moja ya vielelezo vya uchafu na maovu. Ili kufahamu kuhusiana na maana hii angalia makala ya mambo maovu.

Zinaa au Uzinzi (Kiarabu:الزنا) ni kujamiiana (kukutana kimwili) baina ya mwanaume na mwanamke bila ya kuweko mkataba wa ndoa baina yao. Tendo la zinaa ni katika madhambi makubwa na kuwa kwake haramu ni katika mambo yaliyo wazi na bayana na ambayo hayana shaka ndani yake. Adhabu ya zinaa au mzinifu inatofautiana kulingana na mazingira yake. Adhabu ya mseja na kapera (mtu ambaye hajaoa au hajaolewa) ni kuchapwa mijeledi 100, adhabu ya mzinifu mwenye mume au mke ni kupigwa mawe na adhabu ya kufanya zinaa na maharimu wa nasaba na kubaka ni kifo.

Kwa mujibu wa fat'wa za mafakihi, kitendo cha zinaa kinathibiti kwa mzinifu kukiri bayana na kuweko ushahidi wa mashuhuda na zinaa haithibiti kwa kufanyiwa vipimo vya kidaktari. Kuna hukumu mbalimbali kuhusiana na zinaa. Miongoni mwa sheria na hukumu hizo ni kwamba, kufanya zinaa na mwanamke aliyeolewa au aliyeko katika eda ya talaka rejea, hupelekea kuwa haramu milelele kwa maana kwamba, wawili hao katu hawawezi kuoana tena.

Utambuzi wa Maana

Zinaa au uzinzi katika fasili na maana ya mafakihi ni mwanamke na mwanaume kukutana kimwili (kujamiiana) bila ya kuweko mkataba wa ndoa baina yao (ni kujamiiana mwanamke na mwanaume ambao kimsingi sio mke na mume na hakujafungwa ndoa baina yao), au mwanaume kutokuwa mmiliki wa mwanamke (kama mwanamke atakuwa ni mtumwa) au kutokuweko shubha ya nikaha (kudhani kwamba ni mkewe kumbe siye) au umiliki. [1] Katika hali hii, kukutana kimwili kwa aina hizi kunahesabiwa kuwa ni kufanya zinaa na ili kuthibiti hivyo, uume wa mwanaume unapaswa kuwa umeingia katika utupu wa mbele au wa nyuma wa mwanamke kwa kiwango cha kichwa chake (mpaka katika sehemu ya kutahiria). [2]

Zinaa; Dhambi Kubwa

Wanazuoni wa Kiislamu wameihesabu zinaa kuwa ni katika madhambi makubwa, [3] na kueleza kwamba, uharamu wake ni katika mambo ambayo yako wazi na yasiyo na shaka katika dini. [4] Swahib al-Jawahir, msomi na fakihi wa Kishia wa karne ya 13 Hijiria anasema, dini zote zina mtazamo mmoja kuhusuu zinaa kuwa haramu. [5] Kwa mujibu wa kitabu kitakatifu, kukatazwa zinaa ni moja ya amri kumi za Mungu alizopatiwa Nabii Mussa (as) [6] na katika baadhi ya mazingira adhabu yake ni kupigwa mawe. [7]

Kuna Aya saba ndani ya Qur'an Tukufu ambazo zinazungumzia zinaa pamoja na hukumu zake. [8] Katika vitabu vya hadithi kuna hadithi ambazo zimetengwa ambazo zinazungumzia maudhui hii tu. [9] Katika hadithi zinaa inatajwa kuwa sawa na kumuua Mtume na kubomoa Kaaba [10] na kumetajwa matokeo yake mabaya duniani na akhera. Miongoni mwa athari za zinaa hapa duniani ni, maisha kukosa baraka, [11] kuondoka nuru ya kidhahiri, umri kuwa mfupi, umasikini [12] na kifo cha ghafla. [13] Ama kwa upande wa athari za akhera inaelezwa kuwa ni, kuhesabiwa kwa ugumu (hesabu ya mtu kuwa ngumu Siku ya Kiyama), kukumbwa na ghadhabu za Mwenyezi Mungu na kubakia milele katika moto wa jahanamu. [14]

Falsafa ya kuharamishwa zinaa ni kama vile kuzuia kuchanganyika nasaba, kumlinda mwanadamu, kuzuia kuenea maradhi na kuleta utulivu na usalama katika jamii. [15]

Adhabu

Katika maandiko ya fikihi kuna dhabu tatu zilizobainishwa kwa ajili ya mzinifu ambapo kila moja ya hizo hutekelezwa kulingana na hali ya mzinifu. Nazo ni kupigwa mijeledi (viboko), kuuawa na kupigwa mawe.

"Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini". Kwa mujibu wa Aya hii, kundi miongoni mwa waumini linapaswa kushuhudia wakati wa kutekelezwa hukumu na adhabu hii dhidi yao. [17]

  • Kuuawa: Adhabu ya kuzini na maharimu wa nasaba (kama mama, dada na binti), kuzini kwa kubaka (kutumia nguvu na vitisho), [18] kuzini mwanaume asiye Muislamu na mwanamke wa Kiislamu, na kukakariwa zinaa mara kadhaa baada ya kupigwa mijeledi ni kuuawa. [19]
  • Kupigwa mawe: Adhabu ya mzinifu mwenye mke au mume ni kupigwa mawe. [20] Kwa sharti kwamba, aliyezini awe baleghe, mwenye akili na huru. [21] Aliyehukumiwa adhabu ya kupigwa mawe anapaswa kufanya ghusli, kisha kwa mwanaume atachimbiwa shimo na kufukiwa hadi usawa wa kiuno na kwa mwanamke atafukiwa hadi usawa wa kifua na kisha atapigwa mawe mpaka afe. [22] Adhabu ya mwanaume mzee mwenye mke na mwanamke mzee mwenye mume ambao wamezini ni kupigwa mijeledi 100 na kisha baada ya hapo wapigwe mawe. [23]

Kuzini ndani ya eneo takatifu kama msikiti na Haram za shakhsia wakubwa wa kidini na kuzini katika wakati mtukufu kama ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani hupelekea adhabu kuwa kali zaidi ambapo mbali na adhabu zilizoainishwa, kuna adhabu zingine ambazo huainishwa na mtawala (taazir) na adhabu ni hiyo hiyo kama mwanaume atazini na maiti ya mwanamke. [24]

Adhabu za Kiislamu za zinaa, zinatekelezwa katika sheria za nchi za Kiislamu kama Iran, Saudi Arabia na Pakistan. [25]

Njia za Kuthibitisha

Kwa mujibu wa Fat’wa ya mafakihi kuna njia mbili za kuthibitisha kwamba, kumefanyika tendo la zinaa ambazo ni kukiri (ungamo) mhusika mwenyewe na nyingine kutolewa ushahidi wa mashuhuda.

  • Ikirari (ungamo): Kuthibiti zinaa ni kupitia ikirari, ungamo na kukiri mhusika. Mbali na masharti jumla na ya lazima ya taklifu (kama kubaleghe, akili, hiari na kuwa huru) ni sharti akiri mara nne kwamba, amefanya zinaa. [26]
  • Ushahidi: Ili kuthibiti zinaa ni sharti kuweko na ushahidi nao ni kutoa ushahidi wanaume wanne waadilifu kwamba, waliona kwa macho yao wakati wa kufanyika kitendo cha kujaamiana kwa mbele au kwa nyuma. Kama sio wanaume wanne, kwa mujibu wa kauli mashuhuri, wanaume watatu na wanawake wawili. [27] Ushuhuda wa wanaume wawili na wanawake wanne unathibitisha kuchapwa mijeledi tu na sio kupigwa mawe (rajm). [28] Ushuhuda wa mashahidi utakuwa na itibari na kutekelezwa adhabu pale utakapokuwa unafanana, yaani watoe ushahidi wa kushuhudia kitendo hicho sehemu moja na katika zama moja. Kwa maana kwamba, kusiweko na mgongano na hali ya kupingana katika ushahidi wao. Kinyunme na hivyo, watoa ushahidi watapatiwa adhabu ya qadhf ambayo ni kumtuhumu mtu kwa zinaa au liwati. [29]

Kwa mujibu wa fat'wa za mafakihi ni mustahabu kwa mashahidi kujiepusha na kitendo cha utoaji ushahidi wa zinaa. Kadhalika ni mustahabu kwa kadhi kutumia kinaya na kutoa ishara ya kuwashajiisha mashahidi ili waache kutoa ushahidi wa zinaa. [30]

Baadhi ya Hukumu za Kifiq'h za Zinaa

Baadhi ya hukumu za kifiq'h za zinaa ni:

  • Kwa mujibu wa nadharia mashuhuri ni kuwa, nasaba haipatikani kwa zinaa. Kwa msingi huo na kwa mujibu wa mtazamo wa Kisheria mtoto wa zinaa hanasibishwi kwa mwanaume wala mwanamke. [31] Hata hivyo baadhi ya mafakihi wa zama hizi kama Imam Khomeini na Ayatullah Khui wao wana mtazamo mwingine. [32]
  • Endapo mwanamke mwenye mume atazini kabla ya kuchukua talaka kwa mumewe, kwa mujibu wa fat'wa mashuhuri ya mafakihi atakuwa haramu milele kwa mawanaume ambaye amezini naye. [33] Hata hivyo baadhi ya Marajii kama Sayyid Mussa Shubairi Zanjani wanaamini kwamba, mwanamke huyu hawi haramu milele kwa mwanaume huyo. [34]
  • Kwa mujibu wa mtazamo mashuhuri baina ya mafakihi, kuzini na mama au binti ya mwanamke, haiwi sababu ya yeye kuharamishiwa kumuoa mwanamke huyo; kwa sharti kwamba, kitendo cha zinaa kiwe kimefanyika kabla ya ndoa baina yao. [35]
  • Mwanamke mseja (ambaye hajaolewa) kama atazini kwa mujibu wa nadharia mashuhuri hana eda; [36] lakini mwanamke mwenye mume ambaye amepata ujauzito wa zinaa kisha mumewe akampa talaka, anaweza kuolewa baada ya kumalizika eda; hata kama atakuwa hajajifungua. [37]
  • Endapo mume atamtuhumu mkewe kwa zinaa, kama baina yao kutafanyika liana, basi mwanamke yule atakuwa haramu milele kwa mwanaume yule. [38]
  • Kama mzinifu atakimbia wakati wa kutekelezwa hukumu dhidi yake, kama adhabu yake ilikuwa ni kupigwa mawe na hilo lilithibiti kwa ikirari na ungamo lake, kwa mujibu wa mtazamo mashuhuri, hatoadhibiwa tena (kwa maana kwamba, hakuna haja ya kumtafuta na kumkamata na kisha kumuadhibi tena); lakini kama adhabu yake itakuwa ni kuchapwa mijeledi au kupigwa mawe kulikothibiti kupitia ushahidi wa mashuhuda, atakamatwa na kurejeshwa kwa ajili ya kuadhibiwa. [39]
  • Kuchapwa viboko na kupigwa mawe kunathibiti pale mfanya zinaa anapokuwa na elimu ya kuwa haramu kitendo hicho. [40]
  • Mazingira ambayo aliyezini anafutiwa adhabu: Kuzini kwa shubha (aliyezini atakapodhani kwamba, anafanya tendo la ndoa na mkewe), madai ya kuweko mahusiano ya mume na mke, kulazimishwa (kulazimishwa kufanya tendo la zinaa kwa kutishwa na kadhalika) [41], na kutubu aliyefanya zinaa kabla ya tendo la zinaa kuthibiti kwa kadhi (mtoa hukumu). [42]
  • Adhabu ya zinaa ni haki ya Mwenyezi Mungu. Kwa msingi huo utekelezaji wake hautegemei takwa la mtu, na kadhi anaweza kutekeleza adhabu hii kwa kutegemea elimu, ufahamu na maarifa yake. [43] Kadhalika ushahidi wa kujitolea (bila ya takwa na maombi ya kadhi) wa kuthibitisha zinaa unakubaliwa. [44]

Rejea

Vyanzo

  • Bahrani, Yusuf bin Ahmad. Al-hadaiq al-Nadhirah fi Ahkami al-Itrah al-Thahirah, Editor: Muhammad Taqi Irawani dan Sayid Abdul Razzaq Muqram, Qom, Kantor penerbitan Islami berafiliasi dengan Jamiah mudarrisin Hauzah Ilmiyah Qom, 1409 H.
  • Haidari, Abbas Ali. Zina, Insiklopedia Dunia Islam (juz.21), Teheran, 1395 HS.
  • Khomaini, Ruhullah. Tahrir al-Wasilah. Dar al-Kutub al-Ilmiyah, Ismailiyan, 1408 H.
  • Khui, Abul Qasim, Takmilatu Minhaj al-Shalihin, Nashr Madinah al-Ilm, Qom, 1410 H.
  • Majlisi, Muhammad Baqir, Bihar al-Anwar, Beirut. Dar Ihya al-Turath al-Arabi, 1403 H.
  • Najafi, Muhammad Hassan, Jawahir al-Kalam fi Sharhi Sharai' al-Islam. Dar al-Kutub al-Islamiyah dan al-Maktabah al-Islamiyah, Teheran. 1362 1369 HS.
  • Shahid Thani, Zainuddin bin Ali, Al-Raudhah al-Bahiyah fi Sharhi al-Lum’ah al-damasyqiyah, Penerbitan Davari, Qom, 1410 H.
  • Shahid Thani, Zainuddin bin Ali, Masalik al-Afham Ila Tanqih Sharai' al-Islam, Muassasah al-Ma’arif al-Islamiyah, 1413 1417 H.
  • Shubairi Zanjani, Sayyid Mussa, Risalah Taudhih al-Masail, Qom, Salsabil, 1388 HS.
  • Tabatabai Yazdi, Muhammad Kazhim, Al-urwah al-Wutsqa. Muassasah al-Nashr al-Islami al-Tabiah li Jamaati al-Mudarrisin, Qom, 1418 1420 H.
  • Tusi, Muhammad bin Hassan, Al-Tibyan fi Tafsir al-Qur’an, Riset: Ahmad Qashir Amili, Beirut, Dar Ihya al-Turats al-Arabi, Tanpa tahun.