Qadhf

Kutoka wikishia

Qadhf (Kiarabu: القذف) ni mtu kumtuhumu mwenzake kwa tuhuma ya zinaa au liwati. Mafakihi wametaja masharti kama vile baleghe, akili na Uislamu kwa ajili ya kuthibitisha qadhf na kutekeleza adhabu. Adhabu ya qadhf (tuhuma ya zinaa au liwati) ni viboko 80, hata hivyo adhabu hiyo hutekelezwa pale mtu aliyetuhumiwa atakaposhtaki na kudai hilo. Kadhalika, adhabu hiyo hudondoka na kutotekelezwa pale mtuhumiwa wa tuhuma hiyo asipodai adhabu dhidi ya aliyemtuhumu, au atakapoyaunga mkono na kuyathibitisha madai ya mtuhumu au mtoa tuhuma atakapotoa ushahidi wa wazi wa kuthibitisha tuhuma zake.

Qadhf (tuhuma ya zinaa au liwati) ni moja ya madhambi makubwa na ina hukumu maalumu, kama vile kutokubaliwa ushahidi wa mtoa tuhuma ya zinaa au liwati, na kwa mujibu wa kauli mashuhuri ni kwamba, mtu ambaye imetekelezwa dhidi yake adhabu ya tuhuma ya zinaa au liwati mara tatu, akirejea mara ya nne adhabu yake ni kuuawa.

Utambuzi wa maana na nafasi

Qadhf ni mtu kumtuhumu mwingine kwa zinaa na liwati. [1] Qadhf katika lugha maana yake ni kurusha mawe, maneno n.k [2] Inaelezwa kuwa, mtu anayefanya qadhf na kutoa tuhuma ya zinaa au liwati kimsingi anakuwa anarusha maneno mabaya na yasiyofaa kwa wengine. [3] Katika fiq’h mtu anayetoa tuhuma hii anajulikana kwa jina la Qadhif na mtu ambaye ametupiwa vna kurushiwa tuhuma hiyo anafahamika kwa jina la Maqdhuf. [4]

Kutoa tuhuma ya zinaa au liwati ni miongoni mwa madhambi makubwa [5] na katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w), yametajwa kuwa ni madhambi saba yenye uharibifu . Madhambi mengine sita yanayotimiza idadi ya madhambi hayo saba ni uchawi, ushirikina, kuua nafsi, kula mali ya yatima, kuchukua riba na kukimbia kutoka vita katika hali ya jihad. [6] Maudhui ya Qadhf imejadiliwa katika vitabu vya kifiqhi milango ya adhabu za kisheria (zisizo za kimali ambazo zimeainishiwa baadhi ya madhambi maalumu). [7] Pia, vifungu vya 245 hadi 261 vya sheria ya adhabu ya Kiislamu ya Iran, ambavyo vimechukuliwa kutoka katika fiqhi ya Imamiyya, vimeelezea tuhuma hii pamoja na adhabu yake. [8]

Adhabu

Adhabu ya tuhuma ya zinaa au liwati kuchapwa viboko (mijeledi) 80 [9] ambapo hilo linatimia kwa ushahidi wa wanaume wawili waadilifu au kukiri na kuungama mara mbili kwa aliyetoa tuhuma hiyo. [10] Hoja ya hukumu hii ni: ((وَالَّذِينَ يَرْ‌مُونَ الْمُحْصَنَاتِ ثُمَّ لَمْ يَأْتُوا بِأَرْ‌بَعَةِ شُهَدَاءَ فَاجْلِدُوهُمْ ثَمَانِينَ جَلْدَةً وَلَا تَقْبَلُوا لَهُمْ شَهَادَةً أَبَدًا ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ؛ ; Na wanao wasingizia wanawake mahashumu (wanaoheshimika), kisha wasilete mashahidi wanne, basi watandikeni bakora thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao tena, na hao ndio wapotovu)). [11] Hoja na ushahidi mwingine ni hadithi [12] na Ijmaa (maafikiano). [13]

Kadhalika ushahidi wa mtu ambaye ametoa tuhuma ya zinaa na liwati kwa mwingine na akashindwa kuthibitisha katu haukubaliwi. [14]

Adhabu kali

Kwa mujibu wa kauli mashuhuri ni kwamba, mtu ambaye imetekelezwa hukumu ya qadhf (tuhuma ya zina au liwati) dhidi yake mara tatu, endapo itatokea mara ya nne, basi hukumu yake ni kuuawa. [15] Hata hivyo, Ibn Idrissa Hilli anaamini kwamba, ambaye imetekelezwa hukumu ya qadhf (tuhuma ya zina au liwati) dhidi yake mara mbili, endapo itatokea mara ya tatu, basi hukumu yake ni kuuawa. [16]

Mazingira ambayo adhabu ya qadhf haitekelezwi

Adhabu ya qadhf (tuhuma ya zina au liwati) haitekelezwi katika mazingira haya yafuatayo:

  • Mtuhumiwa au mrithi wake (endapo aliyetuhumiwa ataaga dunia) atamsamehe mtoa tuhuma.
  • Mtoa tuhuma atakapotoa ushahidi wa wazi wa kuthibitisha madai yake.
  • Mtuhumiwa atakapokiri tuhuma dhidi yake.
  • Endapo tuhuma ya zinaa (uzinzi) au liwati itapelekea kulaaniana mke na mume kwa lafudhi maalumu. [17]

Kwa nini kuweko adhabu ya Qadhf

Ayatullah Nassir Makarem Shirazi anasema katika tafsiri ya Nemooneh: Lengo la kutekelezwa adhabu ya tuhuma dhidi ya zinaa au liwati (baada mtoa tuhuma kushindwa kuthibitisha tuhuma yake) ni kulinda heshima za watu na kuzuia ufisadi wa kijamii na kimaadili wa tuhuma ya zinaa au liwati (Qadhf). Endapo watu mafisadi watatoa tuhuma chafu na mbaya dhidi ya wengine na kisha wasiadhibiwe, bila shaka, hadhi na heshima ya watu itakuwa hatarini na hilo kupelekea watu kuwa na mitazamo mibaya baina yao na hivyo kuifanya familia kusambaratika. [19]

Masharti ya kutekelezwa adhabu ya Qadhf

Kumebainishwa masharti maalumu kwa ajili ya kuthibitisha na kutekeleza adhabu ya Qadhf kwa kila mmoja wapo yaani mtoa tuhuma na aliyetuhumiwa. Endapo itatokea kwamba, sharti moja kati ya masharti hayo halipo, adhabu ya Qadhf haitatelelezwa na mtoa tuhuma ataainishiwa adhabu ya Taazir (ambazo mtawala wa Kiislamu ndiye mwenye jukumu la kuainisha adhabu hizo). [20] Kubaleghe, akili timamu, kusudio na hiari ni miongoni mwa masharti yanayopaswa kutimia kwa mtoa tuhuma. [21] Kwa muktadha huo, kama mtoto au kichaa atatoa tuhuma ya zinaa au liwati kwa mtu, haitatekelezwa dhidi yake adhabu ya Qadhf bali atapewa adhabu ya kumuadabisha (hukumu ya taazir). [22] Kadhalika kama mtu atatoa tuhuma ya zinaa au liwati dhidi ya mtu kwa kusahahu au kwa kulazimishwa haitatekelezwa kwake adhabu ya tuhuma ya zinaa au liwati. [23] Baadhi wamesema kuwa, mtoa tuhuma anapaswa kuwa na ufahamu na welewa kuhusu kile anachokisema. [24] Mafakihi wanaamini kuwa, sharti la anayetuhumiwa anapaswa kuwa na mwenza (mwanaume au mwanamke mahashumu na mwenye heshima zake). [25] na Makusudio ya Ihsan ni kubaleghe, kuwa na akili timamu kuwa na uhuru (uhuru ambao ni mkabala na utumwa), Uislamu na utakasifu.; [26] hata hivyo ihsan imekuja pia kwa maana ya kuwa katika ndoa. [27]

Kadhalika ili kutekeleza adhabu ya Qadhf, ni lazima aliyetuhumiwa atake hilo kutoka kwa mtawala wa kisheria, kwani adhabu ya Qadhf ni katika haki za watu na mtawala wa kisheria anaweza kutekeleza haki ya mtu pale mwenye haki hiyo atakapotoa ombi. [28] Ili kuthibitisaha adhabu ya Qadhf, maneno ya tuhuma yanapaswa kuwa wazi na kwa sura iliyozoeleka na yatoe ashirio la zinaa au liwati. [29]

Hukumu zingine

Baadhi ya hukumu zingine za Qadhf ni:

  • Mtu ambaye anatoa tuhuma ya zinaa au liwati kwa kundi fulani la watu, endapo wote kwa pamoja watataka itekelezwe adhabu ya Qadhf dhidi ya mtoa tuhuma, itatekelezwa adhabu moja tu (viboko 80 tu), lakini kama kila mmoja atawasilisha ombi la adhabu kivyake, itatekelezwa adhabu ya kila mmoja dhidi ya mtoa tuhuma. [30] Kadhalika mtu ambaye atamtuhumu mwanamke fulani kwamba, amezini na mwanaume fulani, endapo wawili hao watawasilisha kwa pamoja ombi la kutaka adhabu ya Qadhf dhidi ya mtoa tuhuma, mtoa tuhuma ataadhibiwa mara moja na kama watawasilisha mashataka kila mtu kivyake, basi ataadhibiwa mara mbili. [31]
  • Baba ambaye atamtuhumu mwanawe kwa zinaa au liwati, hataadhibiwa adhabu ya Qadhf, bali atapatiwa adhabu ya taazir. [32]
  • Adhabu ya Qadhf inarithiwa; kwa maana kwamba, kama mtuhumiwa ataaga dunia, haki ya kutaka kutekelezwa adhabu ya Qadhf itamfikia mrithi. [33]
  • Endapo watu wawili watatoleana tuhuma ya Qadhf baina yao, adhabu ya Qadhf itaondoka na wote wawili watapewa adhabu ya taazir. [34]