Nenda kwa yaliyomo

Teolojia ya Shia Imamiyya

Kutoka wikishia
Makala hii inahusiana na Elimu ya teolojia katika Madhehebu ya Shia Imamiyyah. Ili kujua kuhusu elimu ya teolojia baina ya Waislamu angalia elimu ya teolojia (ilm al-Kalam ).

Teolojia ya Imamiyyah (Kiarabu: الكلام الإمامي) au Elimu ya Kalam ya Imamiyyah, ni mojawapo ya shule (au Madhehebu) za kiteolojia za Kiislamu, ambapo kipengele muhimu zaidi kinachoitofautisha na kuipambanua (Elimu ya Kalam ya Imamiyyah, au Elimu ya Teolojia ya Imamiyyah), ni itikadi yake katika suala la Uimamu. Elimu ya Teolojia (ilm al-Kalam) ya Imamiyyah, katika njia na vyanzo vyake, hutumia: Qur’an Tukufu, Sunna za Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Maimamu Maasumin (a.s), na Hoja za kiakili. Inasemekana kuwa mwanzo wa kudhihiri Teolojia ya Imamiyyah unasadifiana na siku za mwanzo kabisa baada ya kufariki kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), kwa maana hapo ndipo ulipoanza mjadala kuhusu moja ya masuala muhimu ya teolojia, yaani suala la Uimamu na Ukhalifa baada ya Mtume (s.a.w.w).

Baadhi ya watafiti wanaamini kwamba Imam Ali (a.s) alikuwa shakhsia ya kwanza Muislamu ambaye alizungumza kuhusu masuala kama vile: Dhati ya Mwenyezi Mungu na sifa zake, Kutokea (kuibuka) na Ukale na Uwepo wa Mwenyezi Mungu ambao ni Basit.(Yaani: Uwepo wa Mwenyezi Mungu ni uwepo Rahisi – na uwepo Rahisi ni ule uwepo usiokuwa na Sehemu – kwa ibara nyingine: Uwepo wake (s.w.t) hauna mchanganyiko wowote bali ni uwepo rahisi ambao haujumuishi au hauundwi na sehemu mbili au zaidi kama ilivyo kwa viumbe wake, ambavyo uwepo wao umeundwa kwa mchanganyiko wa sehemu mbalimbali kama vile uwepo wa kimaada (yaani: Mwili) na sura (yaani: Nafsi na Roho), na – Mas’ala ya – kumpwekesha Mwenyezi Mungu) na Wingi (miungu). Baada ya Amirul Muuminina Ali bin Abi Talib (a.s), Maimamu wengine (a.s) waliibua mijadala juu ya masuala ya kiteolojia na kujadiliana na wanateolojia na wanazuoni wa Dini na Madhehebu nyinginezo, ambapo ilikuwa wakiulizwa maswali mbalimbali na kutatua ishkalati mbalimbali kuhusiana na masiala mbalimbali za Elimu ya Teolojia, na waliwalea na kuwaibua wanateolojia mashuhuri kama vile Hisham bin Hakam na Muumin al-Taq.

Baada ya zama za Ghaiba, Teolojia ya Imamiyyah iliendelea kukua na kupanuka kimaendeleo kupitia vipindi mbalimbali vya kihistoria na kwa kuundwa na shule nyingi za kiteolojia, ambazo zilijikita katika mitazamo mitatu tofauti ifuatavyo: Mtazamo wa Maandiko (Maandishi), Mtazamo wa Mantiki (Akili) na mtizamo wa mchanganyiko kati ya Mantiki na Masimulizi (ya Kimaandiko). Usuli au Misingi ya jumla ya Teolojia ya Imamiyyah ni zaidi ya ile Misingi Mitatu ya jumla. Kwa maana kwamba: Teolojia ya Imamiyyah, mbali na kuamini Misingi mitatu ya jumla ambayo ni Tawhidi, Utume na Ufufuo, ambayo shule nyinginezo za Teolojia ya Kiislamu pia zinaiamini, inajumuisha Misingi nyingine miwili, yaani: Uimamu na Uadilifu, na hiyo ni Misingi Miwili muhimu ambayo inaitofautisha shule ya Teolojia ya Imamiyyah na Shule nyingineo za Kiislamu (katika Elimu hii ya Teolojia).

Baadhi ya vitabu muhimu vya kiteolojia vya Imamiyyah ni kama ifuatavyo: Awael al-Maqalat, Tas’hih al-Etiqad, Tajrid al-Etiqad na Kashf al-Murad. Waandishi wa vitabu hivi wanahesabiwa kuwa miongoni mwa wanateolojia mashuhuri wa Imamiyyah, ambao ni: Sheikh Mufid (Aliyezaliwa mwaka 336 hijiria au 338 Hijiria na kufariki mwaka 413 Hijiria) Sheikh Tusi (Aliyezaliwa mwaka 385 AH na kufariki mwaka 460 AH), Khawaja Nasir al-Din al-Tusi (Aliyezaliwa mwaka 597 AH na kufariki mwaka 672 AH) na Allama al-Hali (Aliyezaliwa mwaka 648AH na kufariki mwaka 726 AH).

Ufafanuzi Kuhusu Teolojia ya Imamiyyah

Teolojia ya Imamiyyah ni miongoni mwa Madhehebu ya Teolojia ya Kiislamu ambayo katika masuala ya Imani, yanatumia na kuegemea katika njia hizi na vyanzo hivi muhimu vifuatavyo:

  1. Qur’an Tukufu.
  2. Sunnah za Mtume (s.a.w.w) na Maimamu Maasumina (a,s).
  3. Na dalili za kiakili.

Madhehebu hii ya Kalam (Madhehebu ya Kiteolojia) imekua na kuendelea katika maingiliano na tamaduni zingine na ustaarabu mwingine, na kuwa chini ya ushawishi wa tamaduni hizo na ustaarabu huo [1]. Inasemwa kwamba kwa mujibu wa vyanzo vya kihistoria na nyaraka za hadithi (na riwaya), suala la Uimamu ndio utambulisho mkuu wa Madhehebu ya Teolojia ya Imamiyyah miongoni mwa Madhehebu nyinginezo za kiteolojia ya Kiislamu [2]. Hata hivyo, baadhi wamezingatia suala la Tawhidi inayotokana na (au ambayo chanzo chake ni: Qur’an Tukufu, Hadith za Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Maimamu wa Shia Ithna Asharia (a.s) kuwa ndio msingi mkuu wa masuala yote ya kiteolojia ya Imamiyyah na (kwamba msingi huo ndio) utambulisho wake. [3]

Chimbuko au Mwanzo

Mwanzo wa kudhihiri kwa Teolojia ya Imamiyyah inachukuliwa (na kukadiriwa) kuwa ni siku za mwanzo kabisa baada ya kifo cha Bwana Mtume (s.a.w.w) [4], kwa sababu suala la kwanza kabisa la kiteolojia lililoibuliwa miongoni mwa Waislamu katika kipindi hicho, lilikuwa ni suala la Uimamu na Ukhalifa baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), ambalo ziliibuka nadharia mbili za jumla (baina ya waislamu), nazo ni hizi zifuatazo: Nadharia ya kwanza: Kwamba mrithi (Khalifa) wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) anateuliwa na Mwenyezi Mungu kupitia Mtume wake Muhammad (s.a.a.w). Nadharia ya pili:Kwamba kuteuliwa kwa Khalifa wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni suala ambalo wameachiwa Waislamu, kwa maana hilo ni chaguo la Waislamu. [5]

Imam Ali (a.s) na kundi la wazee katika Muhajirina na Ansari walikuwa wakiiunga mkono nadharia ya kwanza, na wakataja sababu kuu mbili za hoja yao: Sababu ya kwanza: Ni Maandiko (au Hadithi) zilizokuja (na kupokewa) kutoka kwa Mtume (s.a.w.w). Sababu ya pili: Ni ubora wa Imam Ali (a.s) [6]. Pia, katika masuala kama vile Sifa za Mwenyezi Mungu, Qadhaa na Qadar, Jabri na Tafwidh, ambayo ni miongoni mwa masuala ya kiteolojia (kiitikadi) ya zamani zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu, Mashia pia wamekuwa waanzilishi katika masiala hizo. [7]

Inasemekana kwamba Imam Ali (a.s.) alikuwa shakhsia wa kwanza wa Kiislamu ambaye kwa mara ya kwanza kabisa aliibua masuala ya kina na muhimu ya kiTeolojia kama vile: Dhati ya Mwenyezi Mungu na sifa zake, Uumbwaji (kutokea) na Ukale, Urahisi wa uwepo wa Mwenyezi Mungu (Yaani uwepo ambao ni Basit, usiokuwa na muunganiko au mjumuiko wa sehemu, "Simple existence, without parts"), na upweke na wingi (na hii ni masiala inayohusia na mjadala usemao kuwa: Je Mungu ni mmoja au kuna miungu wengi na tofauti tofauti?!) [8]. Kulingana na kauli ya Murtaza Mutahari, mojawapo ya sehemu muhimu na za msingi za Nahj al-Balaghah ni Masuala yanayohusiana na Teolojia, na ukitizama katika jumla ya Hotuba zake, Barua zake na Maneno mafupi mafupi ya Hekima, utaona kwamba mada hizi zinazohusiana na Teolojia zimejadiliwa ndani yake takriban mara arobaini. [9] Baada ya Imam Ali bin Abi Talib (a.s), Maimamu wengine kama vile Imam Sajjad (a.s), Imam Baqir (a.s), Imam Swadiq (a.s), Imam Ridha (a.s), Imam Jawad (a.s) na Imam Hadi (a.s), walijadili juu ya masuala mbalimbali ya kiteolojia. Maswali na ishkalati mbalimbali viliibuliwa (kuhusiana na Teolojia), kwa lengo la kutetea mafundisho ya Uislamu, ambapo walifanya mijadala mbalimbali na wanateolojia na wasomi wa dini mbalimbali na hata wa madhehebu nyinginezo, lakini pia waliwalea kielimu na kuwazoeza wanafunzi wao wengi katika elimu hii ya Teolojia [10].

Misingi ya Jumla ya Teolojia ya Imamiyyah

Teolojia ya Imamiyyah, mbali na Usuli/ Misingi mitatu ya jumla ya Tawhidi, Utume na Ufufuo, ambayo shule zingine za kiteolojia za Kiislamu zinaiamini pia [11], wanayo Misingi mingine ambayo inawatofautisha na Shule zingine za Kiteolojia [12], Misingi hiyo ni kama ifuatavyo:

  • Uimamu: Wanateolojia wa Imamiyyah, wanakubaliana kwamba Uimamu ni cheo na nafasi ambayo Mwenyezi Mungu (s.w) amewapa baadhi ya waja Wake wateule [13]. Vile vile wanaafikiana juu ya imani hii kwamba baada ya kifo cha Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w), Imam Ali bin Abi Talib (a.s) alipata Uimamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t), na akawa mrithi wa moja kwa moja wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), na baada yake, nafasi ya Uimamu ilitolewa kwa Imam Hassan (a.s), na kisha Imam Hussein (a.s), na baada yake, nafasi ya Uimamu inashikiliwa na Maimamu Tisa (a.s) kutoka katika kizazi chake (yaani, Kizazi cha Imam Hussein (a.s), ambao ni: Imam Sajjad (a.s), Imam Baqir (a.s), Imam Swadiq (a.s), Imam Kadhim (a.s), Imam Ridha (a.s), Imamu Jawadi (a.s), Imam Hadi (a.s), Imam Hasan Askary (a.s) na Imam Mahdi (a.t.f.s) [14].
  • Uadilifu: Mashia, pamoja na Mu'tazila [15], wanaamini Wema na Ubaya wa kiakili [16]. Uzuri (wema) wa kiakili na ubaya wa kiakili maana yake ni hii kwamba: Akili (ya Mwanadamu), bila kujali uwepo wa hukumu na amri ya Mungu, hutambua "Uzuri" (wema) na "Ubaya" (Uovu) wa vitendo [17]. Kwa maana kwamba: Mwenyezi Mungu (s.w.t) hata asiposema kisheria kuwa tendo fulani ni ovu (baya) au ni zuri (jema), Akili ilivyo katika asili yake inaweza kutambua na kuhukumu uzuri na ubaya wa matendo ya Mwanadamu. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) hatendi kinyume na ile hukumu ya akili, na ni kwa ajili hiyo husemwa kuwa Yeye (s.w.t) ni Mwadilifu [18]. Yaani hafanyi lolote (s.w.t) isipokuwa lililo jema (na zuri). Hatendi tendo ovu (baya), na wala hawabebeshi waja wake chochote kinachopita uwezo wao (au kuwa nje ya uwezo wao), na wala hamlaumu wala kumuadhibu (mja wake) isipokuwa kwa dhambi zake [19]. Kwa sababu ya kuamini maana hii ya uadilifu, Shia na Mu’tazila wameitwa Al-Adliyyah [20].Kinyume na rai hii, Asha’ira wanaamini Wema (Uzuri) na Ubaya (Uovu) wa Kisharia [21], yaani: Wanasema kwamba chochote anachoamrisha Mwenyezi Mungu ndio Chema (Kizuri na cha kheri), na anachokikataza ndio kibaya, kwa mantiki hiyo, anachofanya Mwenyezi Mungu kinakuwa ni Hasan (Kizuri) [22].

Vipindi vya kihistoria vya Teolojia ya Imamiyyah

Muhammad Safar Jibraili (Msomi wa Teolojia na mwalimu wa Elimu ya kiteolojia) katika kitabu chake: "Mwenendo wa Maendeleo ya Teolojia ya Shi'a" amechunguza ndani yake vipindi vya kihistoria vya Teolojia ya Imamiyyah kwa kuangazia vipengele viwili ambavyo ni Muundo na Manhaji, navyo ni kama ifuatavyo (23):

Muundo

Kwa upande wa mageuzi ya kimuundo, Teolojia ya Imamiyyah inajumuisha hatua kadhaa zifuatazo:

  • Uundaji: Mwanzo wa hatua hii, ambayo ndani yake masuala ya kiteolojia yalijadiliwa kwa njia isiyo ya kiuandishi (yaani hayakuwa ni masuala yaliyo katika mfumo wa uandikwaji, hakuna kitabu wala maandishi yoyote kuhusiana na masaili hizo za kiteolojia, hii ilikuwa ni hatua ya mwanzo kabisa ya uundwaji wa masuala ya Elimu ya kiTeolojia). Hatua hii inazingatiwa kuwa ilikuwa katika siku za mwanzo kabisa baada ya kifo cha Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) [24].
  • Upanuzi: Baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w) hadi mwanzoni mwa karne ya pili ya mwandamo wa Hijiria [25]. Katika kipindi hiki, Teolojia ya Imamiyyah ilianza na Imam Ali bin Abi Talib (a.s), kisha ikaendelezwa na Maimamu wengine (a.s), na ikafikia kilele chake katika kipindi cha Imam Baqir (a.s) na Imam Swadiq (a.s) [26]. Hisham bin Hakam, Hisham Ibn Salim, Muumin al-Taq na Humran bin Aayyan ni miongoni mwa wale ambao Imam Swadiq (a.s) aliwataja kwa cheo cha Mwanateolojia [27].
  • Uhariri wa Maudhui: Karne ya 2 na 3 ya mwandamo wa Hijiria [28]. Kwa mujibu wa kauli ya Ibn Nadim, mwandishi wa Kitabu cha Bibliografia katika karne ya nne ya mwandamo Hijiria, anasema kwamba: Mtu wa kwanza ambaye alikusanya kazi ya kuandika maudhui juu ya somo la Teolojia, alikuwa ni Ali bin Ismail Maithami (ambaye alikuwa ni mmoja wa wapokezi wa Riwaya wa Imam Ridha (a.s), na alifariki mwaka 215 Hijiria) [29]. Aliandika kazi mbili zenye majina haya: Kitab al-Imamah na Kitab al-Istighaq [30]. Baada ya kazi hiyo, pia aliandika risala kuhusu maudhui mbalimbali za kiteolojia, hasa kuhusu Tauhid na Uadilifu [31].
  • Ufafanuzi na mpangilio wa Maudhui: Karne ya 3 na ya 4 ya mwandamo Hijiria [32]. Katika hatua hii, ambayo ni mwanzo wa kipindi cha Ghaiba, wanaTeolojia wa Imamiyyah walieleza masuala ya kiTeolojia yanayoegemezwa kwa Madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s), na hii ni kutokana (au ni kwa sababu ya) kuibuka kwa Madhehebu pinzani ya kifikra, kama vile Mu'tazila na Asha’ira, hivyo (Wanateolojia wa Imamiyyah) walieleza na kuzifafanua Maudhui za KiTeolojia na kuzipanga katika mada au maudhui maalum na kujibu ishkalati zote zilizotolewa [33].

Katika kipindi hicho, Abu Sahl Nobakhti aliandika kitabu kiitwacho Al-Tanbiyhi kuhusu Uimamu [34], Ibn Quba Al-Razi aliandika Kitabu alichokiita Al-Ansaf juu ya Maudhui hiyo hiyo [35], na Sheikh al-Saduq aliandika kitabu alichokiita Al-Tawhiyd kuhusu Maudhui ya Sifa (za Mwenyezi Mungu) na kukanusha Tashbih [36], na pia aliandika kitabu kilichoitwa Kamal al-Din wa Tammam Al-Niimah, kuhusiana na maudhui ya Ghaiba [37].

  • Muundo: Karne za 5 na 6 [38]. Teolojia ya Imamiyyah iliundwa katika kipindi hiki kupitia wanateolojia watatu maarufu wa Shia, ambao ni: Sheikh Mufid, Sayyid Murtaza na Sheikh Tusi. [39].
  • Mabadiliko na mageuzi: Karne ya 7 na 8 [40]. Awamu hii ilianza kwa kuibuka kwa shule ya teolojia ya Hillah, hasa kwa kazi za Sadid al-Din al-Hammsi, na kufikia kilele chake kupitia kwa Khawaja Nasir al-Din al-Tusi [41].

Khawaja Nasir al-Din al-Tusi alibadilisha Teolojia ya Imamiyyah kwa kuleta mbinu mpya na ya kiubunifu akitumia misingi na kanuni za kifalsafa [42]. Aliunda mpangilio mpya katika uwasilishaji wa masuala ya kiteolojia kwa kuandika kitabu alichokiita: “Ufupisho wa Imani” “Tajridul Iitiqadi (Abstraction of Belief), kutokana na kazi hiyo, aliwashawishi wanaTeolojia wengi waliomfuatia [43].

  • Hatua ya ufafanuzi na Muhtasari: Karne ya 9 hadi 14 [44]. Kazi Nyingi za kiTeolojia zinazopatikana katika kipindi hiki ni zile zinazohusiana na Ufafanuzi (Sharhi) na Mukhtasari wa kazi zilizopita, hasa kitabu cha Tajrid al-Itiqad [45]. ni sehemu ya kazi hiyo. Kitabu cha Shuwa’rqu al-Ilham, ambayo ni sharhi (ufafanuzi) ya kina ya kitabu cha Tajrid al-Itiqad, kinachukuliwa kuwa mojawapo ya kazi maarufu za kipindi hiki [46].
  • Hatua ya Matengenezo na mabadiliko: Kuanzia nusu ya pili ya karne ya 14 [47]. Kipindi hiki kilianza na Sayyid Jamal al-Din Asad Abadi, ambapo yalianzishwa ndani yake masuala mapya katika teolojia, na kimeendelea (kipindi hicho) hadi sasa kwa kushamiri tafiti mbalimbali za kiTeolojia za wanaTeolojia kama vile Muhammad Jawad Balaghi, Sayyid Hebatuddin Shahrashtani, Sayyid Muhammad Hussein Tabatabai na Murteza Mutahari [48].

Manhaji (Njia)

Baadhi ya Manhaji (njia) za kawaida (au ambazo ni maarufu zaidi) za Teolojia ya Imamiyyah ni kama zifuatazo:

  • Maandiko: Hii ni Manhaji katika Elimu ya Teolojia ya Imamiyyah ambayo msingi wake huu kwamba utafiti unaruhusiwa kufanyika ndani ya mawanda ya vyanzo vya simulizi tu (na si vinginevyo), na akili (kwa kujitegemea kivyake) kama chanzo cha elimu haihusiki kamwe katika kufanya uchanganuzi na kuleta tafsiri ya habari na uchunguzi wa mafundisho ya dini [49]. Manhaji (njia) ya Maandiko inachukuliwa kuwa inafuata mwenendo wa hadithi za Shia katika zama za Maimamu Maasum (a.s), hususan katika zama za Imam Ridha (a.s) [50]. Mtazamo huu (au Manhaji hii) baadae ilikuja kuchukuliwa kuwa ndio mkondo mkuu wa Shule ya Teolojia ya Mji wa Kielimu wa Qom wakati wa zama za Ghaiba, kupitia wanaTeolojia kama vile Sheikh Sadouq na Muhammad bin Hassan Saffar al-Qummi [51].
  • Mrengo wa Mantiki ya Taawili: Katika Manhaji hii (au Mrengo na muelekeo huu), akili (mantiki) inachukuliwa kuwa ni chanzo cha kutambua, kuthibitisha na kutathmini mafundisho ya dini. Na pale ambapo dalili ya kiakili na ya hakika inapopingana na dalili ya kunukuu (masimulizi), basi katika hali hiyo itatangulizwa (na kupewa kipaumbele) dalili ya kiakili, na dalili ya kunukuu (masimulizi) itatafsiriwa na kufanyiwa taawili [52]. Baadhi ya watafiti, wameitambulisha (na kuielezea) Familia ya Nobakhti kama mwanzilishi wa Mlengo au Manhaji ya Kimantiki katika Teolojia Imamiyyah kutokana na ujuzi wao wa Falsafa ya Kigiriki na Teolojia (Teolojia) ya Mu'tazili [53].Manhaji hii (au Mlengo huu wa Kimantiki) ilikuwa ndio mtiririko mkuu wa Shule ya Teolojia ya Baghdad, ambayo ilifikia kilele chake kwa kazi (nzuri) za wanaTeolojia kama vile Sheikh Mufid, Sayyid Murtaza, na Sheikh Tusi. [54] Baada ya hapo, (Manhaji hii ya Kimantiki na Taawili ya Maandiko) iliendelea katika Shule ya Teolojia ya Hillah. [55].
  • Mrengo wa Mantiki ya Falsafa: Katika mtazamo huu (au Mlengo huu au Manhaji hii), MwanaTeolojia anaeleza (anafafanua), anaimarisha, na anafanya ulinzi wa kutetea mafundisho ya kidini kwa kutumia mbinu na akili ya kifalsafa. [56] Kulingana na kauli ya Murtaza Mutahari, urazini wa kifalsafa (yaani: Akili na Mantiki ya Kifarsafa) ulijitokeza kupitia (Mwanatheolijia maarufu) Khawaja Nasir al-Din al-Tusi kwa uandishi wa kitabu alichokiita: Tajrid al-Etiqad katika Teolojia Imamiyyah. [57]. Na baada ya yake, (Manhaji hii) iliendelezwa na wanaTeolojia wengine wa Kishia, kama vile Muhaqqiq Lahiji. [58] na wengine wengi.

Tofauti na Mashirikiano ya Teolojia ya Imamiyyah na Madhehebu Zingine za Kiteolojia

Katika baadhi ya masuala ya kiteolojia, na vilevile katika namna ya kushughulikia masuala haya, tunaikuta Teolojia ya Imamiyyah ikiwa na tofauti kadhaa lakini pia kukiwa na mambo kadhaa yanayofanana na madhehebu nyinginezo za kiteolojia ya Kiislamu, hasa Madhehebu ya Mu'tazila na Asha’ira. [59]

Katika Masuala ya Kiitikadi (Kiimani): Baadhi ya masuala yenye utata (na ikhtilafu) ya Teolojia ya Imamiyyah kwa kulinganisha na mitazamo mingine ya kieolojia ni kama ifuatavyo:

  • Usawa wa Dhati na Sifa: (Kwa kwaana kwamba: Sifa za Dhati za Mwenyezi Mungu ni sawa na dhati yake tukufu). Imamiyyah (Shia Ithna Asharia) na baadhi ya Muutazila wanaitikadia na kuamini kuhusu Sifa za Dhati Tukufu za Mwenyezi Mungu (s.w.t), ambazo ni Elimu, Uwezo, na Uhai, kwamba ziko sawa na Dhati ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) [60]. Lakini Asha’ira, wao wameenda kinyume na nadharia hiyo, kwa sababu nadharia yao ni hii kuwa Sifa za Dhati za Mwenyezi Mungu ni Qadim (za zamani, au za tangu na tangu) na zinaongezeka juu ya Dhati ya Mwenyezi Mungu. [61]
  • Wema na Ubaya wa Kiakili: Imamiyyah na Muutazilah ni miongoni mwa wale wanaosema nadharia hii ya Wema na Ubaya wa Kiakili; wakati Asha’ira na baadhi ya Shia wa mlengo wa Akhbari (Akhbariyuna) wao wanakataa na kukanusha kabisa nadharia hii ya "Wema na Ubaya wa Kiakili". [62]
  • Kutenzwa nguvu na Hiari: Mu'tazila wanaamini katika nadharia ya Tafwidh Yaani, wanaamini kwamba mwanadamu halazimishwi kufanya matendo yake na anayafanya kwa kujitegemea kabisa na kwa kuegemea katika uwezo wake na hiari yake. [63] Kwa upande mwingine, Asha’ira wanaamini katika nadharia ya uchumaji. [64](Mukhtasari wa maana ya nadharia hii ya Kasbu ambayo asili yake ni mtazamo wa Asha’ira Abul Hassan al-Ash'ari, ambaye katika ufafanuzi wake juu ya Nadharia ya Kasbu (upataji uchumaji), anasema kwamba: Kwa hakika, kitendo cha Mwanadamu kinatendeka kwa sababu ya nguvu zile alizokuwa nazo mtendaji kiasi kwamba kupitia nguvu hizo chumo linalopatikana ni tukio kutoke. Yaani, ukitenda, chumo lake ni kuwepo tukio hilo lililotokana na kutenda kwako, na hukutenda ispokuwa kupitia nguvu za kutenda zilizopo ndani yako. Kwa maelezo hayo, wanasema kwamba Mwenyezi Mungu, anapo umba kitendo, huumba pia nguvu ndani ya mwanadamu ili kitendo hicho kiwepo kupitia uwezo na nguvu hiyo ndani ya Mwanadamu, nadharia hii inaitwa nadharia ya Kasbu, yaani: Kuchuma, kwa maana: Tukio ni chumo lililotokana na kitendo cha Mja kupitia zile nguvu alizopewa ndani yake ile zimsaidie kuleta au kuzalisha matukio kupitia matendo yake.Natija na mtizamo huu ni kwamba: Mwenyezi Mungu ameumba mwanadamu na matendo yake pia!). Kwa mujibu wa nadharia hii ya Kasbu, Mwenyezi Mungu ameumba vitu vyote, hata matendo ya Mwanadamu, na mwanadamu ni mchumaji tu (au mpokeaji tu) wa matendo yake kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na kwa sababu hii, matendo ya mwanadamu yamo katika nuru ya uwezo na mzunguko wa nguvu ambapo pindi anapotaka kutenda tendo lolote, basi Mwenyezi Mungu huumba ndani yake nguvu hiyo na kumfanya atende kwa nguvu hiyo wakati wa kutenda kwake tendo lolote .[65] (Kwa ibara nyingine watu wa nadharia hii wanataka kusema kuwa Mwanadamu hana hiari ya kuamua katika matendo yake, bali anatenda kwa kutenzwa nguvu pasina kujitegemea katika kuamua kutenda au la. Na hii ndio Jabri yenyewe). Kinyume na mitazamo hii miwili (Mu’tazila na Asha’ira), Shia Imamiyya wanaamini katika nadharia inayoitwa Jambo ni kati ya mambo mawili au (Al-Amru bainal Amrayni), na hii ni nadharia mahususi kwa Shia Imamiyyah. [66] Kulingana na nadharia hii (Shia Imamiyyah), katika matendo ya Mwanadamu ambayo ni matendo kwa hiari yake mwenyewe na kwa mapenzi yake, irada mbili zina athari ndani yake, yaani: Irada yake (matakwa yake kama mwanadamu) na Irada (Matakwa) ya Mwenyezi Mungu (s.w.t), vinaathari katika matendo hayo ya Mwanadamu. Lakini irada hizi mbili moja iko mbele nyingine ndio inafuatia na wala haziko sambamba [67].
  • Ihbat (Kubatilika): ((Ufafanuzii: Maana ya ihbat, katika lugha ni: Kubatilisha au kubatilika, kuharibu, kufanya kitu kisiwe na kazi wala faida yoyote. Na katika istilahi maana yake ni: Kubatilika kwa matendo mema ya mja kutokana na madhambi makubwa aliyoyatenda, na kutoweka kwa malipo (au thawabu) za matendo yake yaliyotangulia ikiwa ni matokeo mabaya ya dhambi zake alizozifuatisha baada tu ya kutenda mema hayo. Imamiyyah na Asha’ira hawakubaliani na Nadharia hii ya Ibhat (kuharibika na kubatilika kwa malipo – thawabu – ya ibada na matendo mema kutokana na athari ya dhambi) na wanaona kuwa hilo ni halali na sahihi katika baadhi ya madhambi makhsusi tu, kama dhambi ya ushirikina (hii ndio inaweza kufuta mema na mazuri ya mja); lakini Mu’tazila kwa upande wao wanaamini kwamba dhambi huharibu na kubatilisha malipo (thawabu) ya matendo yetu yaliyotangulia [68]
  • Kutenda dhambi kubwa: Kwa mujibu wa Imamiyyah na Asha’ira, mtu anayetenda dhambi kubwa ni Muumini, lakini ni Fasiki. Kwa maana: Muumini, anapotenda dhambi kubwa, anabakia kuwa ni Muumini, lakini Muumini ambaye ni Fasiki. Khawarij (wasiokuwa Madhehebu ya Ibadhi) wanamchukulia mtu kama huyo (Muumini aliyetenda madhambi makubwa) kuwa ni Kafiri. Mu’tazila pia wanaamini kwamba mtu huyo si Muumini wala si Kafiri; badala yake, wanamhesabu kuwa yupo katika daraja kati ya Ukafiri na Imani, jambo ambalo wanaliita kuwa ni (Nafasi kati ya nafasi mbili) Manzila Bainal Manzilatain. [69]

Katika Manhaji (Njia)

Kwa mtazamo wa Manhaji, pia kuna tofauti (ikhtilafu) na kuna mambo ambayo yanafanana (Mushtarak) kati ya Teolojia ya Imamiyyah na baadhi ya madhehebu zingine za kiteolojia [70] Inajulikana wazi kuwa Teolojia ya Mu'tazila, ambayo inaegemea zaidi katika njia (manhaji) ya urazini (Akili na Mantiki), imevuka mipaka, kiasi kwamba wafuasi wa madrasa ya Mu'tazila, katika hali ya kutokea kwa mgongano kati ya Akili ya kimantiki na Riwaya (Masimulizi), wanafasiri na kuifanyia taawili dhahiri ya riwaya (masimulizi) ili kuipendelea Akili ya kimantiki na kuitanguliza mbele ya riwaya (maandiko). [71] Kwa upande mwingine, Ahlul-Hadith ambao ni sehemu ya Wanazuoni wa kiTeolojia, katika masuala ya imani na itikadi, wanazingatia na kutegemea dhahiri ya (au mwonekano wa) maandiko(riwaya), na wanapinga vikali tafsiri na taawili yoyote na uchambuzi wowote ule wa akili ya kimantiki katika masuala ya imani na itikadi. [72] Madhehebu ya kiteolojia ya Asha’ira na Maturidiyyah pia yamechukua manhaji ya kati kwa kati ambayo ni mchanganyiko wa Akili ya Kimantiki na Manukuzi (yaani: Maandiko au riwaya au masimulizi). [73]

Kwa mujibu wa kauli ya Murtaza Mutahari, Teolojia ya Imamiyyah si kama Teolojia ya Ahl al-Hadith, ambao kimsingi wanakanusha matumizi ya Hoja na Akili za Kimantiki katika masuala ya imani na itikadi za kimadhehebu (kidini). Na pia sio kama zilivyo fikra za Asha’ira ambazo huchukua uasilia wake kutoka kwenye msingi wa Akili na kuifanya akili (ifuate au) iwe chini ya dhahiri ya maandiko. Teolojia ya Imamiyyah inaipa nafasi maalum Akili ya Kimantiki; Lakini pia inaichukulia nadharia ya akili ya kimantiki ya Mu'tazili kuwa ya kupita kiasi na kuvuka mipaka. Tafakuri ya Mu'tazili ni ya kiakili; lakini inategemea mabishano (au inaegemea kwenye mabishano ya kimijadala); hali ya kuwa Teolojia ya Imamiyyah (hasa baada ya Khawaja Nasir al-Din al-Tusi) inaelekea kwenye njia (na manhaji) ya Kimantiki ya Uthibitisho (kwa maana: Manhaji ya kiakili inayoegemea kwenye hoja dalili zenye kuthibitisha jambo kwa hoja imara za kiakili zisizopingika). [74] Bila shaka, kumekuwepo pia na vikundi vingine kama vile Akhbari (Akhbariyuna) katika (sira au) mwenendo wa kifikra wa Shia, ambao (hawa kwa upande wao) walitegemea dhahiri ya maandiko pekee ili (iwawezeshe) kuelewa mafundisho ya kiitikadi [75]

Kazi Muhimu za Kiteolojia na Wanateolojia Wakubwa

Baadhi ya vitabu muhimu vya kiteolojia vya Imamiyyah ni kama vifuatavyo: Awael al-Maqalat, Tas-hih al-Itiqad, Tajrid al-Itiqad na Kashf al-Murad. [76] Waandishi wa vitabu hivi, kwa mtiririko huo (hapo juu) ni: Sheikh Mufid (336 au 338-413 AH), Sheikh Tusi (385-460 AH), Khawaja Nasir al-Din al-Tusi (597-672 AH) na Allamah al-Hilli (648-726 AH). Wanazuoni hawa (Mwenyezi Mungu awarehemu) wanachukuliwa kuwa miongoni mwa WanaTeolojia mashuhuri mno wa Imamiyyah. [77] Yafuatayo, ni maelezo na ufafanuzi kuhusiana na baadhi ya vitabu hivi na vingine vya kiTeolojia vya Imamiyyah:

  • Kitab al-Tauhid: Kitabu hiki ni mkusanyo wa hadithi (au riwaya mbalimbali) kuhusu Tawhidi na elimu juu ya Dhati ya Mwenyezi Mungu(s.w.t), Sifa zake, Majina yake, na Matendo yake. Pia kuna masuala mengine mbalimbali ya kiTeolojia, ambapo ni kitabu kilichotungwa na kuandikwa na Sheikh Saduq (r.a). [78] Al-Itiqadat: Kitabu hiki pia kimeandikwa na Sheikh Saduq(r.a). Mwandishi (Sheikh Saduq) katika milango 45 ya kitabu hiki, na mwanzoni mwa kila mlango, ameeleza masuala muhimu zaidi ya kiitikadi ya Shia Imamiyyah kwa kuyaweka chini ya anuani isemayo: "Mlango wa Itikadi katika..." [79] Kitabu kiitwacho: Tas-hih al-Itiqadat al-Imamiyyah kwa maana: Kitabu kinachojihusisha na kusahihisha masuala ya Itikadi za Imamiyyah, kilichotungwa na Sheikh Mufid (r.a), ni miongoni mwa vitabu vya kiTeolojia vya Shia Imamiyyah, ambavyo viliandikwa kwa lengo la kufanya mapitio na utafiti wa kina juu ya kitabu cha Iitiqadat cha cha Sheikh Saduq (r.a) [80]
  • Al-Ihtijaj ala Ahal Al-llijaj: Kitabu hiki ni miongoni mwa vitabu vya masimulizi (riwaya) ya Shia vilivyoandikwa na Ahmad Bin Ali al-Tabarsi (r.a), ambaye alikuwa ni Mwanateolojia na Mwanasheria wa karne ya 6 Hijiria. Kitabu hiki kina riwaya mbalimbali za Maimamu Maasumin (a.s), ambapo maudhui ya riwaya hizo ni dalili na hoja mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na Maimamu Maasumin (a.s) katika kukabiliana na mitizamo, hoja na fikra za wapinzani. [81]
  • Tajridul Etiqad: Baadhi ya sifa na vipengele vya kitabu hiki cha Khawaja Nasiruddin al-Tusi ni kama ifuatavyo: Ubainishaji wa masuala ya kiteolojia kwa njia ya uthibitisho(wa kidalili), uvumbuzi katika mpangilio na nidhamu ya masuala ya kiteolojia, na kuchanganya baina ya masuala ya kiteolojia na falsafa. Sifa hizi zimekitofautisha kitabu hiki na kazi nyingine za kiTeolojia zilizofanyika kabla yake, na zimeziathiri (kwa athari chanya) kazi zingine za kiTeolojia zilizofanyika baada yake. [82] Fafanuzi (Sharhi) nyingi zimeandikwa kuhusiana na kitabu hiki cha Tajrid al-Etiqad, [83] ambapo Kitabu kiitwacho: Kashf al-Murad kilichoandikwa na Allamah al-Hilli kinachukuliwa kuwa ndio Kitabu cha kwanza kabisa na muhimu zaidi kilichotoa ufafanuzi (na sharhi) muhimu juu ya kitabu hiki. [84]
  • Manshur Aqaid Imamiyyah: (Ilani ya Itikadi ya Imamiyyah): Hiki ni kitabu kilichoandikwa kwa lugha ya Kifarsi. Kimeandikwa na Ayatollah Ja'far Subḥānī (Mwenyezi Mungu Amhifadhi), ambaye alieleza kwa ufupi Itikadi ya Kishia katika mfumo wa sura kumi na misingi mia moja na hamsini za itikadi. [85].

Rejea

Vyanzo