Akhera

Kutoka wikishia
KIFO NA UFUFUO ni uhalisia, ukweli na uhakika usiokwepeka; Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea

Akhera (Kiarabu: الآخرة) ni ulimwengu baada ya kifo na mauti na ni ulimwengu ujao baada ya maisha ya dunia. Akhera iko mkabala wa maisha ya dunia. Imani na itikadi ya uwepo wa ulimwengu wa Akhera hutambulika kuwa ni miongoni mwa misingi ya dini ya kiislamu na mtu ambae haamini uwepo wa Akhera basi hawi muislamu. Qur'an Tukufu imetilia mkazo na msisitizo sana juu ya suala la Akhera na kwamba kuamini uwepo wa Akhera ilikuwa ni miongoni mwa misingi ya Mitume wote waliotumwa na Mwenyezi Mungu. Na inasemekana kuwa zaidi ya theluthi moja ya aya za Qur'an zinahusiana na suala la Akhera.

Katika vitabu vya kitheolojia vya waislamu imezungumziwa Akhera chini ya utambulisho au anuani Ufufuo(Marejeo ya kiama) na zimetolewa dalili mbali mbali za kiakili na za kunukuu kwa ajili ya kuthibitisha masuala hayo. Wanazuoni wa kiislamu kwa kujitegemeza kwenye aya za Qur'an wamesema kuwa Akhera ni ulimwengu ulio tofauti kikamilifu na ulimwengu wa kidunia na wamebainisha na kuweka wazi sifa pekee za ulimwengu wa akhera, na miongoni mwa sifa pekee za Akhera ni kubakia milele (kuwa na maisha ya milele), kuwepo kwa tofauti kati ya watu wazuri na watu wabaya, kulipwa kwa mujibu wa matendo na kulipwa na kufaidika na neema za Akhera kwa msingi wa ustahiki.

Baadhi ya wanazuoni wa kiislamu wanaamini na kuitakidi kwamba Akhera huanza tu baada ya kukoma na kumalizaka kwa maisha ya dunia, ama kundi fulani la wanazuoni wengine wanaitakidi kwamba ulimwengu wa Akhera hata hivi sasa upo na unauzunguka ulimwengu wa dunia.

Maana ya Akhera

Akhera katika lugha ina maana ya mwisho, baada ya na nyingine,[1] na makusudio ni huo ulimwengu mwingine ambao hufuatia baada ya maisha ya dunia.[2] Qur'an Tukufu kwa ajili ya kuueleza ulimwengu baada ya kifo mara nyingi hutumia neno Akhera na neno hilo limetumika mara 104, na wakati mwingine hutumia maneno kama vile (Nyumba ya Akhera), (Ulimwengu mwingine) na (Siku ya Akhera) (Siku nyingine).[3]

Umuhuimu waa kuamini uwepo wa Akhera

Itikadi na imani ya uwepo wa Akhera ni miongoni mwa misingi ya dini na ni sharti moja wapo la kuwa muislamu, kwa maana kwamba mtu ambae hatokubali itikadi na sharti hilo haingii katika hesabu ya waislamu.[4] Kwa mujibu wa maneno ya Murtadha Mutwahari ni kuwa, itikadi hiyo ni miongoni mwa mafunzo muhimu sana ambayo manabii wote walikuwa wakiwaita watu na kuwalingania kwayo baada ya Tawhiid (Upweke wa Mwenyezi Mungu) na kwamba kitu muhimu sana walicho kuwa wakiwalingania watu ilikuwa ni kuamini na kuitakidi uwepo wa ulimwengu wa Akhera.[5]

Na kwa mujibu wa maneno ya Muhammad Taqiy Misbah Yazdi ni kwamba zaidi ya theluthi moja ya aya za Qur'an zinahusiana na suala la Akhera.[6] Suala la kuamini na kuitakidi ulimwengu wa Akhera ndani ya Qur'an imebainishwa kuwa ni miongoni mwa mihimili na nguzo muhimu za wito wa mitume wote. Na kwa mujibu wa aya nyingi za Qur'an suala la kuitakidi uwepo wa Akhera pembezoni mwa imani ya Mwenyezi Mungu na imani ya Utume ni moja ya misingi na nguzo tatu za dini ya kiislamu.[7] Na kwa mujibu wa imani na itikadi ya madhehebu zote za kiislamu ni kwamba kuamini na kuitakidi uwepo wa Akhera ni miongoni mwa mambo ya dharura na ya lazima ya dini ya kiislamu na mtu ambae hataamini na kuitakidi jambo hilo basi haingii na hahesabiwi katika waislamu.[8]

Vitabu vya kitheolojia vya waislamu vimezungumzia pia ulimwengu wa Akhera kwa anuani (Nguzo ya ufufuo na marejeo ya kiama).[9] Barzakh, Kiama, Swiraat, Hisab, uombezi, pepo na moto ni miongoni mwa mambo yanayo fungamana na Akhera vitu ambavyo vimeelezwa na kuandikwa kwenye Qur'an, hadithi na vitabu vya maulamaa wa kiislamu na kwa mujibu wa Qur'an hapana budi kuitakidi na kuamini vitu hivyo.[10]

Dalili na uthibitisho wa uwepo wa Akhera(Ufufuo)

Wanazuoni wa kiislamu wanacukulia kwamba miongoni mwa dalili na uthibitisho muhimu sana wa kuwepo kwa ulimwengu wa Akhera ni thibitisho za kunukuu ukiwemo wahyi(ufunuo), kwa maana kwamba ile hali ya mitume ambao ni wenye kuhifadhiwa na maasumiin kutoa habari kuhusiana na ulimwengu wa Akhera na kuwaita pia kuwalingania watu kwenye jambo hilo, ni uthibitisho tosha wa kuwepo kwa ulimwengu wa Akhera.[11]

Na miongoni mwa thibitisho za kunukuu kuhusiana na suala hili na kuhusu uwepo ulimwengu wa akhera ni aya ya 7 ya surat at-Taghaabun isemayo: (Sema: ndio, naapa kwa jina la Mola na Mwenyezi Mungu, bila shaka kitasimama kiyama…..)[12]

Kwa mujibu wa maneno ya Murtadha Mutwahari ni kuwa kinyume na thibitisho za kunukuu pia kuna thibitisho zingine nyingi kwa ajili ya kuthibitisha ulimwengu wa Akhera thibitisho ambazo kwa uchache ni (Ishara na alama ) za kuthibitisha uwepo wa ulimwengu wa Akhera. Na bwana huyu ametaja njia tatu kuhusu jambo hili: 1-Kumfahamu na kumtambua Mwenyezi Mungu. 2-Kutambua na kuufahamu ulimwengu na 3-kuitambua nafsi na roho ya mwanadamu.[13]

(Hoja ya hekima / برهان الحکمة) na (hoja ya uadilifu / برهان العدالة) ni miongoni mwa thibitisho za kiakili ambazo wanazuoni wa kithiologia huzitoa na kuzizungumzia kwa ajili ya kuthibitisha uwepo wa ulimwengu wa Akhera.[14]

Katika uthibitisho wa hekima(hoja ya hekima / برهان الحکمة), husemwa kwamba; haipatani au haiendani na hekima ya Mwenyezi Mungu kuweka mipaka ya maisha ya mwanadamu kwa maisha haya ya kidunia, maisha ambayo yana uwezekano wa kutokuwa na kikomo; Kwa sababu Mwenyezi Mungu alimuumba mwanadamu ili kumfikisha kwenye ukamilifu mkubwa iwezekanavyo, na kufikia ukamilifu mkubwa zaidi hakuwezi kupatikana katika ulimwengu huu; Kwa sababu thamani inayokuwepo ya ukamilifu wa ulimwengu mwingine haiwezi kulinganishwa na ukamilifu wa kidunia.[15]

Ushahidi na uthibitisho wa uadilifu(hoja ya uadilifu / برهان العدالة) pia unasema: kwa kuwa katika ulimwengu huu wema na waovu hawaoni malipo na adhabu ya matendo yao inavyostahiki, basi uadilifu wa Mwenyezi Mungu unahitaji kuwepo ulimwengu mwingine ambao kila mtu atapata anachostahiki humo.[16]

Sifa pekee za Akhera na tofauti kati yake na dunia

Kwa mujibu wa maneno ya Murtadha Mutwahari ni kuwa kuna mamia ya aya za Qur'an zenye maudhui zihusianazo na zenye mafungamano na ulimwengu wa Akhera, kama vile ulimwengu baada ya kifo, siku ya kiama, namna ya kufufuliwa wafu, mzani wa matendo, hesabu, kuhesabiwa kwa matendo, pepo na moto, na kubakia milele kwa ulimwengu wa Akhera.(18) Wanazuoni wa kiislamu kutokana na msingi wa aya mbali mbali za Qur'an ni kwamba Akhera ni ulimwengu unao tofautiana kikamilifu na ulimwengu wa kidunia na wanaamini kuwa katika ulimwengu wa Akhera kuna nidhamu inayo tofautiana kikamilifu na nidhamu ya ulimwengu wa dunia.[17]

Katika Akhera watu wote kuanzia mwanzo wa kuumbwa kwa ulimwengu hadi mwisho wa ulimwengu huo, watu wote watafufuliwa na kuishi kwa wakati mmoja.[18] Katika ulimwengu huo wanadamu wote ima watakuwa katika saada na wema usio na kikomo na kila watakacho taka watapatiwa ima watakuwa katika mahangaiko yasiyo na mipaka mahangaiko ambayo hawatapata kinyume na kile walicho kichuma na wanacho kistahili, ama katika dunia ni maisha na kifo, kuwa nacho na kutokuwa nacho, kupata na kukosa, kufanikiwa na kutofanikiwa, kuwa na maisha ya raha na kuwa na maisha ya tabu, na furaha na tabu, ghadhabu na furaha vyote vimechanganyika na viko pamoja katika maisha ya dunia.[19]


Sifa zingine pekee za Akhera kwa msingi wa aya za Qur'an na riwaya za Ahlulbaiti ni kama zifuatazo:

  • Maisha ya milele: Kwa mujibu wa Aya mbalimbali za Qur'an Akhera ni ulimwengu usio na mwisho na usio na kikomo na ni ulimwengu wa milele. Kama mfano imefafanuliwa na kubainishwa katika aya ya 34 ya Surat Qaf ya kwamba katika Akhera watu wa peponi watapewa bishara ya kwamba: (Hivi leo ni siku ya kubakia milele) vivyo hivyo imekuja katika kitabu Ghurarul-hikam kutoka kwa Imamu Ali(a.s) imenukuliwa kama ifuatavyo: (Dunia ni yenye kumalizika na kutoweka na akhera ni ya milele na sio yenye kutoweka).[20]
  • Kutenganishwa kwa watu wema na watu wabaya:Kwa msingi wa aya kadhaa za Qur'an ni kwamba katika Akhera watu wema na watu wabaya watatenganishwa: (Enyi watenda madhambi siku ya leo jitengeni au tenganeni na watu wema,[21] watu ambao walimkufuru na kukataa uwepo wa Mwenyezi Mungu, wataswagwa na kupelekwa motoni, ili mwenyezi Mungu aweze kutenganisha watu watwaharifu na wasio watwaharifu.[22] (Waumini watakuwa katika furaha na wataingia peponi na makafiri watakuwa na ghadhabu na hasira na wataingia motoni).[23] Watu ambao walikuwa wakimuogopa na walikuwa na hofu na Mola wao, watapelekwa peponi makundi kwa makundi.[24] Na watu waovu wakiwa na kiu kubwa wataswagwa na kupelekwa kwenye moto wa hajannam.[25]
  • Kupata malipo ya matendo: Kwa msingi wa aya mbali mbali za Qur'an ni kwamba mwanadamu atayaona matokeo na natija ya matendo yake aliyo yafanya katika dunia: (bila shaka haraka sana atayaona matokeo ya matendo yake na juhudi zake. Kisha atapatiwa malipo ya matendo yake kikamilifu na bila shaka yoyote).[26] Hivyo basi kila ambae atafanya wema hata kama ni kiasi cha tembe moja ya wema ataiona, kwa maana atayaona matokeo yake na natija yake, na kila ambae atafanya ubaya kwa kiwango cha ncha ya tembe ya ubaya na uovu basi natija yake ataiona.[27]
  • Malipo yatazingatiwa msingi wa ustahiki wa mtu: Kinyume na duniani, katika Akhera kila mtu atapewa na kulipwa kwa msingi wa ustahiki na atapewa anachostahili, Imekuja katika hadithi kutoka kwa Imamu Ali (a.s): (Hali ya duniani hufuata matukio na mambo yafanyikayo na hali ya Akhera hufuata anachostahiki mtu).[28]

Wigo wa Akhera

Ama kuhusiana na wigo wa Akhera kuna tofauti za kinadharia na kuna nadharia mbalimbali:Baadhi wanaamaini kwamba Akhera huanzwa kwa kufariki kwa mwanadamu na kuingia kwake kwenye ulimwengu wa Barzakh, ama kuna watu wengine ambao ulimwengu wa Barzakh hawautambui kuwa ni miongoni mwa ulimwengu wa akhera na wanaitakidi kuwa: Akhera huanza baada ya kumalizika ulimwengu wa Barzakh.[29] Vivyo hivyo wanatheologia wanaitakidi kwamba Akhera ni baada ya ulimwengu wa dunia, kwa maana kwamba Akhera ni baada ya kumalizika kwa maisha ya dunia ndipo yanaanza maisha ya Akhera, ama wanafalsafa wanaitakidi kwamba Akhera hivi sasa ipo, katika muendelezo wa maisha ya dunia kwa maana kwamba wakati ambapo dunia ipo, akhera nayo ipo na ni muendelezo wa maisha ya dunia kwa maana daraja ya uwepo wa Akhera ni mkubwa zaidi na Akhera inaudhibiti na kuuzunguka ulimwengu wa dunia. Moja ya aya zenye kutegemewa na kundi hili ni aya ya 49 ya Surat al-Tawbah isemayo: «وَ إِنَّ جَهَنَّمَ لَمُحِيطَةٌ بِالْكَفِرِين» (kwa hakika jahannam imewazunguka makafiri).[30]

Osia wa Qur'an na riwaya kuhusiana na Akhera

Katika aya mbali mbali za Qur'an na riwaya kuna osia na maelezo mbali mbali kuhusiana na Akhera kiasi kwamba baadhi ya maelezo hayo ni kama yafuatayo:

  • Hayakuwa maisha ya dunia isipokuwa ni mchezo na upuuzi na maisha ya Akhera ni kwa ajili ya wenye kumcha na kumuogopa Mwenyezi Mungu ni mazuri zaidi. Je, hamlifahamu hilo?[31]
  • Kwa hakika maisha ya Akhera ni kwa ajili ya wale ambao hawapendi kujitweza katika dunia.[32]
  • Mtu mwenye kuikumbuka na kuitaja sana Akhera basi madhambi yake yatapunguzwa.[33]
  • Dunia ni shamba la Akhera.[34]
  • Mtu ambae siku yake nzima hima yake kubwa ni Akhera, Mwenyezi Mungu ataweka katika moyo wake hali ya kujitosheleza na kutohitajia na matendo yake atayafanya kuwa ni yenye nidhamu na hataondoka dunia isipokuwa akiwa amepata riziki yake kikamilifu.[35]

Kitabu cha pekee

Moja ya kitabu pekee kuhusiana na Akhera, ni kitabu kiitwacho Manaazilul-akhera (vituo vya Akhera) kilicho andikwa na Sheikh Abbas Qomi ambae ni miongoni mwa wanazuoni wa karne ya kumi na nne. mtunzi huyu katika kitabu hiki amebainisha na kufafanua kwa ufasaha hatua za ulimwengu wa Akhera kiasi kwamba kwa mujibu wa kitabu hicho hatua za ulimwengu wa Akhera ziko kama ifuatavyo: Kifo na mauti, kaburi, barzakh, kiama na swiraat. Katika kitabu hiki pia ameongelea miizaan, hisabu na kuhesabiwa katika Akhera na adhabu ya jahannam na amezungumzia utendaji wa baadhi ya matendo ya kiibada na kuchunga baadhi ya masuala ya kimaadili na kwamba ni muhimu kwa ajili ya kuvuka kwa urahisi katika hatua za Akhera na kuusia kufanya hivyo ili kurahisisha kuvuka katika hatua za Akhera.

Kitabu hiki cha Manaazilul-akhera kimetarjumiwa kwa lugha ya kiarabu, kingereza, kituruki, kiswahili na urdu.

Rejea

  1. Mujtahid Shabestariy, (Aakherat) uk. 133
  2. Sha'araaniy, Nathri Tuubaa, 1389 S, uk. 15.
  3. Mujtahid Shabestariy, (Akherat) uk. 133.
  4. Mutwahari, Maj'muue Aathar, 1377 S, 1418 H, juz. 2 uk. 501.
  5. Mutwahari, Maj'muue Aathar, 1377 S, 1418 H, juz. 2 uk. 501.
  6. Misbahu Yazdiy, Aamuzesh Aqaid, 1384 S, uk. 341.
  7. Mujtahid Shabestariy, (Aakherat) uk. 133.
  8. Mujtahid Shabestari, (Akherat) uk. 133.
  9. Mutwahari, Maj'muue Aathar, 1377 S, 1418 H, juz. 2 uk. 501.
  10. Mujtahid Shabestariy, (Aakherat) uk. 133.
  11. Mutwahari, Maj'muue Aathar, 1377 S, 1418 H, juz. 2 uk. 502-503.
  12. Misbahu Yazdiy, Aamuzesh Aqaid, 1384 S, uk. 389.
  13. Mutwahari, Maj'muue Aathar, 1377 S, 1418 H, juz. 2 uk. 503.
  14. Misbahu Yazdiy, Aamuzesh Aqaid, 1384 S, uk. 364-366.
  15. Misbahu Yazdiy, Aamuzesh Aqaid, 1384 S, uk. 364.
  16. Misbah Yazdiy, Aamuzesh Aqaid, 1384 S, uk. 365.
  17. Tazama: kitabu cha Twabatwabai. Al-miizaan, 1417 H, juz. 20, uk. 148; Misbah Yazdiy, Aamuzesh Aqaid, 1384 S, uk.411.
  18. Misbahu Yazdiy, Aamuzesh Aqaid, 1384 S, uk. 411.
  19. Twabatwabaiy, Al-miizaan, 1417 H, juz. 20, uk. 148.
  20. Aamudiy, Ghurarul-hikam, 1366 S, uk. 134.
  21. Surat Yaasin, aya 59.
  22. Surat al-Anfaal aya 36-37.
  23. Misbah Yazdiy, Aamuzesh Aqaid, 1384 S, uk. 415.
  24. Surat az-Zumar aya 73.
  25. Surat Maryam aya 84
  26. Surat an-najmi aya 40-41.
  27. Surat az-Zalzalah aya 7-8.
  28. Aamudiy, Ghurarul-hikam, 1366 S, uk. 148.
  29. Khorasaniy, (Aakherat) uk. 98.
  30. Khorasaniy, (Aakherat) uk. 98-99.
  31. Surat al-Qasas aya 83.
  32. Aamudiy, Ghurarul-hikam, 1366 S, uk. 146.
  33. Ibnu Abi Jamhuur, Awaali lliaaliy, 1405 H, juz. 1, uk. 267.
  34. Ibnu Abi Jamhuur, Awaali lliaaliy, 1405 H, juz. 1, uk. 267.
  35. Ibnu shu'ubah Al-harraniy, Tuhaful-uquul, 1404 H, 1363 S, uk. 48.

Vyanzo

  • Qur'an Tukufu
  • Ibnu Abi Jamhuur, Muhammad bin Zainud-din, Awaali lliali Al-aziiziyah fil-ahaadithid-diiniyah, kilicho hakikiwa na Mujtaba Iraqi, Qom, Daru sayyidis-shuhadaa lin-nashri, chapa ya kwanza mwaka 1405 H.
  • Ibnu shu'ubah Al-harraaniy, Hasan bin Aliy, Tuhaful—uquul anir-rasoul, kilicho hakikiwa na Ali Akbar Ghaffariy, Qom, Jaamiatul-mudarrisiin, chapa ya pili, mwaka 1363sh/ 1404 H.
  • Aamudi, Abdul-waahid, Tasniifu Ghurarul-hikam, kilicho hakikiwa na Mustwafa Dirayatiy, Qom, Daftar tablighaat islaami, chapa ya kwanza, mwaka 1366 S.
  • Khorasaany, Ali, (Aakherat) Daairatul-ma'aarifil-qur'anl- kariim, j1, Qom, Muassasat Bustani kitaab, chapa ya tano Biita.
  • Sha'araaniy, Abul-hasan, Nathri tuuba, Lughatnaameh qur'an kariim, kilicho hakikiwa na Sayyid Muhammd Ridhaa ghiyaathi kirmaaniy, Qom, Bun'yaad farhangi Mahdi maw'uud, chapa ya kwanza, mwaka 1389 S.
  • Twabatwabai, Sayyid Muhammd Husein, Al-miizaan fii tafsiiril-qur'an, Qom, Daftar Intishaaraat islaamiy, chapa ya kwanza, mwaka 1417 H.
  • Mujtahid shabestariy, Muhammad, (Aakherat), Daairatul-ma'aarif buzorgi islaami, j1, Tehran, Markaz Daairatul-ma'aarif buzorgi islaami, chapa ya pili, mwaka 1374 S.
  • Misbah Yazdiy, Muhammad Taqii, Aamuzesh Aqaaid, Tehran, Amiir kabiir, chapa ya kumi na nane, mwaka 1384 S.
  • Mutwahariy, Murtadhaa, majmue aathar, j2, Tehran, Intishaaraat swadraa, chapa ya saba, mwaka 1377 S/1418 H.
  • Makaarimu Shiraaziy, tafsiiru namuune, Tehran, Darul-kutubil-islaamiyah, chapa ya kwanza, mwaka 1374 S.