Sayyid Hassan Nasrullah

Kutoka wikishia
Sayyid Hassan Nasrullah

Sayyid Hassan Nasrullah (Kiarabu: السيد حسن نصر الله) (1339 H.Sh - 1403 H.Sh), ni mwanazuoni wa Kishia na mwanasiasa mashuhuri kutoka Lebanon, yeye ni Katibu Mkuu wa tatu wa Hizbullahi na ni mmoja wa waanzilishi wa kikundi hicho. Katika kipindi chake cha uongozi, klicho anzia mnamo mwaka 1992 hadi 2024 B.K., Hizbullahi iliimarika na kuwa miongoni mwa nguvu za ukanda wa mashariki ya kati. Moja ya mafanikio makubwa chini ya uongozi wake, ni; ukombozi wa kusini mwa Lebanon wa mwaka 2000 kutoka katika ukaliwaji wa kimabavu wa utawala wa Kizayuni, kuachiliwa kwa wafungwa wa Lebanon na urejeshwaji wa miili ya mashahidi kutoka Israel mnamo mwaka 2004, pamoja na ushindi dhidi ya Israel katika vita vya siku 33 vya mwaka 2006. Kwa mafanikio haya, Sayyid Nasrullahi alijipatia umaarufu mkubwa na kupewa jina la "Sayyid wa Mapambano" kutokana na ushujaa wake.

Aidha, kutokana na uongozi wake thabiti na ushindi dhidi ya Israel, Sayyid Nasrullahi alitambuliwa kuwa ni kiongozi mwenye ushawishi mkubwa zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu na Mashariki ya Kati. Sayyid Hassan Nasrullah alipata elimu yake ya kidini katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq, na baadaye katika Chuo cha Imamu Al-Muntadhar huko Baalbak. Yeye alikuwa ni mmoja wa wanafunzi wa Sayyid Abbas Musawi, pia alihudhuria alijipatia baadhi ya masomo mengine ya kidini kutoka wanazuoni wengine mashuhuri kama vile; Sayyid Mahmoud Hashimi, Sayyid Kadhim Haa’iri na Muhammad Fadhil Lankarani katika mji wa Qom nchini Iran.

Kuanzia mwaka 1975 hadi 1982 B.K., Sayyid Hassan Nasrullahi alikuwa ni mwanachama wa kikundi cha harakati za Amal, moja ya vyama vya kisiasa vya Kishia nchini Lebanon. Hata hivyo, ilipofika mwaka 1982 B.K., akishirikiana na kundi la wanazuoni wapambanaji, alijitenga na harakati hizo na kuanzisha kikundi cha Hizbullahi ya Lebanon. Baada ya kuuawa kwa Sayyid Abbas Musawi tarehe 16 Februari 1992 B.K., Sayyid Nasrullahi aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Hizbullahi, nafasi aliyo aliendelea nayo hadi kuuawa kwake mwaka 2024 B.K./1403 H.Sh. Katika kipindi cha uongozi wake, Sayyid Hassan Nasrullahi alikutana na viongozi wa Iran na maafisa wake kwa ajili ya mazungumzo na kujenga ushirikiano wa karibu na viongozi hao, huku mara kadhaa akikutana ana kwa ana na kiongozi mkuu wa mhimili wa muqawa (mapambano) (Ayatullah Khamenei) nchini Iran.

Sayyid Hassan Nasrullahi aliuawa shahidi tarehe 6 Mehr 1403 H.Sh. (27 Septemba 2024 B.K.) kufuatia shambulio la mabomu lililofanywa na utawala wa Kizayuni katika eneo la Dhahiyah, kusini mwa Beirut. Kufuatia tukio hilo viongozi mbalimbali walitoa salamu za rambirambi wakionesha hisia zao juu ya maafa hayo. Miongoni mwa viongozi wa kidini na kisiasa waliotua salamu za rambirambi baada tukio hilo ni pamoja na; Ayatullah Khamenei (Kiongozi Mkuu wa Iran) na Ayatullah Sistani (wanazuoni wakuu wa kidini nchini Iraq). Wengine walio onesha hisia zao juu ya tukio hilo kwa kutoa salamu za rambirambi ni wanazuoni wakuu wa vyuo viwili maarufu vya Najaf nchini Iraq na Qom nchini Iran akiwemo; Makarim Shirazi, Nouri Hamedani, Ja’afar Subhani, Shubeiri Zanjani, Jawadi Amuli na Bashir Hussein Najafi. Taarifa za maombolezo zilimiminika kutoka serikali za mataifa mbalimbali, maafisa wa ngazi za juu, na makundi mbali mbali ya mapambano, kikiwemo kikundi cha Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, Harakati ya Jihad al-Islam ya Palestina, Ansarullah ya Yemen, Fat'h, Asa'ib Ahl al-Haq, kikundi cha Harakati za Amal cha Lebanon, kikundi cha Tayyaru Al-Hikmati Al-Watani cha Iraq, pamoja na kikundi cha Harakati za Sadr kilichoko nchini Iraq. Kufuatia tukio hilo, Iran ilitangazwa siku tano za maombolezo ya kitaifa, huku Lebanon, Syria, Iraq na Yemen zikitoa siku tatu za maombolezo ya kitaifa. Aidha, maandamano na mikutano ya kulaani mauaji hayo yalifanyika katika nchi mbalimbali kama ni ishara ya kukemea na kulaani shambulio hilo la kigaidi.

Kabla ya kuuawa shahidi, mara kadhaa Sayyid Hassan Nasrullahi alinusurika katika majaribio ya mauaji yaliyofanywa na majeshi ya Israel, ikiwa ni pamoja na mashambulizi yaliyotokea miaka ya 2004, 2006, na 2011 B.K. Licha ya hatari na vitisho hivyo, Nasrullahi aliendelea kuongoza harakati zake bila taharuki, akiwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Israel.

Aidha, mnamo mwaka 1997 B.K., Sayyid Muhammad Hadi (mwanawe mkubwa), aliuawa shahidi wakati wa mapambano na majeshi ya Israel, tukio ambalo liliongeza msimamo na dhamira ya Nasrullahi katika kuendeleza harakati za kupinga uvamizi wa Kizayuni.

Sayyid wa Mapambano Katika Mapambano Dhidi ya Ukaliaji wa Israel

Sayyid Hassan Nasrullah, kiongozi mashuhuri na mwenye heshima kubwa nchini Lebanon, [1] alijipatia jina la «Sayyid wa Mapambano» kutokana na mchango wake muhimu katika Harakati ya Hezbullah. Uongozi wake ulipelekea ukombozi wa kusini mwa Lebanon mwaka 2000 B.K., baada ya miaka 22 ya ukaliaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika maeneo hayo, na baadae ushindi mkubwa katika vita vya siku 33 vya mwaka 2006 B.K. Mchango huu ulimfanya kuwa kiongozi wa kimkakati na kielelezo muhimu cha upinzani dhidi ya ukaliaji wa Israel. [2] Kutokana na mapambano yake dhidi ya Israel na ushindi wa mara kwa mara, Sayyid Hassan Nasrullahi ametambuliwa kama kiongozi maarufu katika ulimwengu wa Kiislamu. [3] Yeye amegeuka kuwa ndiye kiongozi anayependwa zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu [4] na ameonekana kama kiongozi jasiri na mwenye ushawishi mkubwa zaidi katika Asia Magharibi. [5] Umaarufu wake unatokana na hotuba zake zenye hamasa na haiba yake ya kipekee ya uongozi aliyokuwa nayo, ambayo imevutia heshima na kupelekea mapenzi kutoka kwa watu wa Lebanon na mamilioni ya wafuasi katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu. [6] Kwa mujibu wa ripoti ya EuroNews ikinukuu kutoka Associated Press, Nasrullah alipata heshima kubwa kutoka kwa watu wa Lebanon na mamilioni ya watu katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu. [7] EuroNews ilimtaja Nasrullahi kama mshirika wa karibu zaidi wa Iran na ndiye adui sugu wa Israel. [8]

Hotuba ya Sayyid Hassan Nasrullah Labik Ya Hussein ina maana...

Uongozi Wake Akiwa Katibu Mkuu wa Hizbullahi ya Lebanon

Baada ya kuuawa shahidi kwa Sayyid Abbas Musawi mnamo tarehe 16 Februari 1992 B.K. (27 Bahman 1370 H.Sh.), Sayyid Hassan Nasrullahi alichaguliwa kwa kauli moja na wanachama wa Hizbullahi kushika nafasi ya Ukatibu Mkuu wa chama hicho. [9] Akiwa na umri wa miaka 32 wakati wa uteuzi wake, Nasrullahi aliiongoza Hizbullahi kwa ustadi kabisa, chini ya uongozi wake, harakati za kikundi hicho zilizidi kupata nguvu na kuwa na ushawishi mkubwa katika ukanda wa Mashariki ya Kati. [10]

Inasemekana kwamba Hizbullahi, chini ya uongozi wa Sayyid Hassan Nasrullah, iligeuka kuwa nguvu ya kikanda katika eneo la Mashariki ya Kati, [11] ikifanikiwa katika uwanja wa mapambano dhidi ya Utawala wa Kizayuni. Miongoni mwa mafanikio yake makubwa ni pamoja na; ukombozi wa kusini mwa Lebanon mwaka 2000 B.K., ushindi katika vita vya siku 33 mwaka 2006 B.K., na kushindwa kwa makundi ya kigaidi mwaka 2017 B.K. [12] Nafasi muhimu ya Sayyid Hassan katika kuachiliwa kwa wafungwa wa Lebanon na urejeshaji wa miili ya wapiganaji wa muqawama (upinzani) kutoka mikononi mwa Israel mwaka 2004 B.K. ilitambulika kama ni nafasi msingi katika kuimarisha hadhi ya Hizbullahi. [14] Chini ya uongozi wa Sayyid Hassan, Hizbullahi pia ilionekena kujihusisha katika harakati za siasa, ambapo baadhi ya wanachama wake waliweza kushinda uchaguzi na kupata nafasi katika Bunge la Lebanon, wakionyesha uwezo wao wa kuathiri siasa za kitaifa na kuongeza ushawishi wao katika muktadha wa kisiasa wa Lebanon. [15]

Sayyid Hassan Nasrullah alikuwa mmoja wa walengwa wa tageti za mauaji ya kigaidi ziliyowekwa na Israel, ambapo inasemekana kwamba; kuanzia mwaka 2006 B.K.,[16] Sayyid Hassan Nasrullah alilazimika kuishi maisha ya siri ili kujikinga na vitisho vya mauaji kutoka kwa majeshi ya Israel. [17] Mara nyingi hotuba zake zilifanyika kupitia mtandao na video konferensi. [18] Nasrullahi aliiona Hezbullah kama ni mwiba katika jicho la Marekani na kama kizuizi muhimu dhidi ya mipango ya ukaliaji wa kimabavu wa Israel, akisisitiza umuhimu wa harakati za kikundi hicho katika kulinda uhuru na usalama wa Lebanon na eneo zima la Mashariki ya Kati. [19]

Hotuba ya Sayyid Hassan Nasrullah Siku ya Ashura 1434 Hijria


Kwa nafsi zetu, maisha yetu, watoto wetu na mali zetu, tunamwambia Imamu Hussein (a.s): «Labbaika ya Hussein». Kamwe hatutatengana na agano (ahadi) zetu wala kuacha mwito huu... Kwa wale wote madhalimu, wavamizi, mafisadi, wale wanaojitafutia maslahi yao binafsi na wale wanaodhani kuwa wataweza kuvunja nia, dhamira na uthabiti wetu, tunawaambia kuwa sisi ni watoto wa yule Imamu, wa wale wanaume, wanawake na vijana waliosimama pamoja na Hussein katika Siku ya Ashura, wakinena pamoja na Imam Hussein kuiambia historia maneno yasemayo: «هَیْهات مِنّا الذِّلّة» "Hapana! Kamwe hatutakubali udhalili".[20]

Uhusiano Wake na Makundi Mbali mbali ya Upinzani

Katika wadhifa wake akiwa Katibu Mkuu wa Hizbullahi ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullahi alikuwa na uhusiano wa karibu mno na mhimili wa upinzani (ushirika wa makundi ya upinzani kutoka Yemen, Iran, Iraq, Syria, Lebanon na Palestina).[24] Yeye alikuwa ni mshirika muhimu wa viongozi wa Iran na makundi ya wapambanaji wa Kipalestina kama vile Hamas. [21] Baada ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza kufuatia lililoitwa Kimbunga cha al-Aqswa, Nasrullahi alianzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Israeli kutoka katika eneo la kusini mwa Lebanon, ili kusaidia na kuunga mkono muqawama (upinzani) wa Kipalestina, akitangaza kwamba; mapambano yake hayo yangelidumu hadi mwisho wa vita vya Gaza. [22] Aidha, wakati wa uongozi wake, Hizbullahi ya Lebanon ilijenga uhusiano mzuri na wa kirafiki na kikundi cha Harakati cha Amal cha Lebanon, ikionyesha umoja wa kisiasa na kijeshi kati ya makundi hayo mawili katika kukabiliana na changamoto za kikanda. [23]

Uhusiano Wake na Iran

Sayyid Hassan Nasrullah alikuwa na mahusiano ya karibu na ya kirafiki na Iran pamoja na viongozi wake. [23] Mara kadhaa alisafiri kwenda Iran na kukutana na viongozi wa nchi hiyo, jambo lililoimarisha mshikamano kati ya Hizbullahi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mara ya kwanza, aliyokutana na Imam Khomeini katika Husainiya ya Jamaran ilikuwa ni mwaka 1360 H.Sh (1981 B.K.). [24] au 1361 H.Sh. (1982 B.K.), [25] kisha akakutana naye tena mnamo mwaka 1365 H.Sh. (1986 B.K.), alipokwenda yeye pamoja na wanachama wa Hizbullahi nchini humo kwa lengo la kuimarisha uhusiano, na kupata ushauri wa kisiasa na kijeshi. Mkutano wake wa mwisho na Imam Khomeini ulifanyika miezi michache kabla ya kifo cha Imamu, wakati wa mgogoro kati ya Harakati za Amal na Hizbullahi, ambapo Sayyid Hassan alifika kwa Imamu Khomeini kwa nia ya kutafuta mwongozo wa kiroho na kisiasa kutoka kwake. [26]

Kama ilivyoelzwa katika riwaya ya maisha ya Nasrullah; Uhusiano wa karibu kati ya Sayyid Hassan Nasrullah na Ayatullah Khamenei ulianza rasmi mnamo mwaka 1365 H.Sh. (1986 B.K.). [27] Tangu wakati huo Nasrullah alikuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na viongozi wa kijeshi na kisiasa wa Iran, akiwemo Qassim Suleimani na Hussein Amir-Abdullahian, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran. [28]

Sayyid Hassan Nasrullah aliiona Iran kama ni mshirika muhimu na msaidizi mkuu wa Hizbullahi, na aliendelea kuitetea Iran kila ilipohitajika. [29] Miongoni mwa matukio hayo ni baada ya shambulio la Israel kwenye Ubalozi Mdogo wa Iran huko Damascus mnamo Farvardin 1403 H.Sh. (Aprili 2024), ambapo Nasrullah alisisitiza haki ya Iran kujibu mashambulizi hayo na kuonesha imani kwamba ni lazima Iran italipiza kisasi dhidi ya Israel. [30] Sayyid Nasrullahi anasema kwamba; ni fakhari kwa Hizbullahi kuwa na Urafiki na mahusiano ya karibu na Iran. [31]

Mnamo Novemba 2009 B.K., Sayyid Hassan Nasrullah alitangaza na kuwasilisha waraka mpya wa kisiasa wa Hizbullahi, ambao uliweka wazi kwamba moja ya misingi na wajibu muhimu wa chama hicho, ni uaminifu na kujitolea kwa uongozi wa Wilayat al-Faqih wa nchini Iran. [34] Waraka huo ulidhihirisha uhusiano wa karibu wa Hizbullahi na mfumo wa utawala wa Iran, ukionyesha kuwa uongozi wa Iran ulikuwa ndiyo nguzo ya muhimu ya kisiasa na kiitikadi kwa harakati za Hizbullahi. Kulingana na ripoti za Al Jazeera [35] na EuroNews, [36] baadhi ya wataalamu wa siasa na wapinzani wa Hizbullahi walimwona Nasrullahi na chama chake kama wakala wa Iran, wakihusisha harakati zake kama ni uwakilishi wa maslahi ya Iran nchini Lebanon.

Sayyid Hassan Nasrullahi
Sayyid Hassan Nasrullah akitoa kauli ya akisisitiza msimamo wa Hizbullahi katika mapambano yake dhidi ya maadui wa Mashariki ya Kati na harakati zao za kikoloni: alisema: Tunaamini kuwa Yazid wa zama hizi, ambaye tuna wajibu wa kukabiliana naye kwa misingi ya Karbala, misimamo ya Husseini, na ujasiri wa Zainab, ni ile mipango wa Marekani na Wazayuni. Mipango hii ni tishio kwa umma wetu, ustaarabu wetu, dini za mbinguni, mataifa yetu, pamoja na yale yenye heshima na utukufu mbele yetu. Nasi kama ilivyokuwa hapo awali, tumejizatiti na tutaendelea kujizatiti kwa kufuata misingi ya Husseini na Zainab dhidi ya Yazid huyu wa kisasa. Mapambano haya yatabaki kuwa kipaumbele chetu cha juu kabisa.[37]

Elimu na Maisha Yake

Sayyid Hassan Nasrullah alizaliwa katika moja ya mitaa ya mashariki mwa Beirut mnamo tarehe 31 Agosti 1960 [38] au 1962, [39] sambamba na tarehe 8 Shahrivar 1339 H.Sh au 1341 H.Sh. [40] Baba yake alikuwa akiitwa «Sayyid Abdulkarim», na mama yake «Nahdiyya Safiyyu al-Din». [41] Asili ya familia hii inarejea kwenye kijiji cha Al-Bazuriyya, kilichoko katika wilaya ya Suur, kusini mwa Lebanon, ila baadae familia hii ilihamia Beirut. [42] Baadhi ya vyanzo vimeeleza kuwa Sayyid Hassan alizaliwa katika kijiji cha Al-Bazuriyya. [43] Sayyid Hassan Nasrullahi alikuwa na alikuwa na ndugu watatu wa kiume na dada watano, naye ndiye ndiye mtoto wa kwanza katika familia yao. [44] Wakati wa ujana wake, Sayyid Hassan alishirikiana na ndugu zake katika kufanya kazi katika duka la mbogamboga la baba yao, shughuli iliyomfundisha nidhamu ya kazi na maisha ya kijamii akiwa kijana. [45]

Historia ya Sayyid Hassan Nasrullah

Nasrullahi alianza elimu yake ya msingi katika skuli ya Al-Najah, iliyoko katika eneo liitwalo Al-Tarbawiyya. Hata hivyo, mnamo Aprili 1975 B.K. (sawa na 1354 H.Sh.), vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipoanza nchini Lebanon, familia yake ilihamia kijijini Al-Bazuriyya kusini mwa nchi hiyo. Huko, Nasrullahi aliendelea na masomo yake ya sekondari katika mji wa Al-Bazuriyya, akiweka msingi wa elimu yake licha ya mazingira magumu ya vita na maisha ya uhamaji. [46]

Kulingana na maelezo ya Sayyid Hassan Nasrullahi mwenyewe, tangu akiwa mtoto alionyesha shauku kubwa katika elimu ya kidini na malezi ya kiroho. Licha ya upinzani kutoka kwa wazazi wake, [47] mnamo mwaka 1976 B.K. (sawa na 1355 H.Sh.), akihamasishwa na Sayyid Muhammad Gharawi, imamu wa mji wa Al-Suur na mwanafunzi wa mwanazuoni maarufu Sayyid Muhammad Baqir al-Sadr, Sayyid Hassan Nasrullahi alihamia mji wa Najaf nchini Iraq. Alienda huko ili kujifunza elimu za kidini. Sayyid Muhammad aliandika barua ya kumbulisho kwa Ayatullahi Sadr, ambaye alimkabidhi Sayyid Abbas Musawi jukumu la kusimamia maendeleo ya kielimu na mahitaji ya Sayyid Hassan. [48] Mnamo mwaka 1978 B.K., Sayyid Hassan alimaliza masomo yake ya awali ya kidini, lakini baada ya miaka miwili ya huko Najaf, alilazimika kurejea Lebanon kufwatia shinikizo la serikali ya Baath ya Iraq lililomlazimisha kufanya hivyo. [49] Baada ya kureja Lebanon, mnamo mwaka 1979 B.K. (1357 H.Sh.), Sayyid Hassan alianzisha shule ya Imamu al-Muntadhar katika mji wa Baalbak. Huko, aliendelea na masomo yake ya kidini huku akiwa ni mwalimu aliyetoa mafunzo kwa wengine. [50]

Mnamo mwaka wa 1989 B.K. (1367 H.Sh.) [51] au 1990 B.K. (1368-1369 H.Sh.), [52] Sayyid Hassan Nasrulahi alisafiri kwenda mji wa Qom, nchini Iran, akabaki huko kwa muda wa mwaka mmoja akiendelea na masomo yake ya juu ya kidini. [53] Akiwa huko, Sayyid Hassan alihudhuria masomo ya wanazuoni tofauti maarufu, ikiwa ni pamoja na; Sayyid Mahmoud Hashimi, Sayyid Kadhim Ha’iri na Muhammad Fadhil Lankarani, ambao walimpia elimu ya kina katika fani mbali mbali za kidini. [54] Sababu ya kurejea kwake kutoka Qom kwenda Lebanon inahusishwa na uvumi wa kuongezeka kwa mgogoro kati ya Hizbullahi na harakati za kundi la Amal. [55]

Licha ya kujikita zaidi katika elimu ya dini, Sayyid Nasrullahi pia alipitia mafunzo mbalimbali ya kijeshi na kushiriki kozi mbali mbali za ukomavu wa kijeshi, jambo lililochangia kuimarisha uwezo wake wa kiulinzi na kimapambano. Hii ilimwezesha kusimama imara kama kiongozi shupavu, mwenye maarifa ya kijeshi na kidini, katika harakati za Hizbullahi. [56]

Mke na Watoto

Mnamo mwaka wa 1978 akiwa na umri wa miaka 18, Sayyid Hassan Nasrullah alifunga ndoa na bibi Fatima Yassin. Katika ndoa hiyo, wanandoa hawa walibahatika kupata watoto wanne: watatu kati yao ni watoto wa kiume walioitwa; Muhammad Hadi, Muhammad Jawad na Muhammad Ali, pamoja na mtoto mmoja wa kike ailiyeitwa Zainab. [58] Mtoto wake mkubwa, Sayyid Muhammad Hadi, aliuawa shahidi mnamo tarehe 12 Septemba 1997 (sawa na tarehe 22 Shahrivar 1376 H.Sh.) katika mapambano dhidi ya majeshi ya Israel kusini mwa Lebanon. Mwili wake uliangukia mikononi mwa Wazayuni, lakini mwaka mmoja baadaye, kufuatia operesheni ya kubadilishana wafungwa kati ya Israel na Hizbullahi, mwili huo ulirejeshwa Lebanon. [59]

Kuuawa Kwake

Makala Asili: Kuuawa Shahili kwa Sayyid Hassan Nasrullahi
Salamu za Rambirambi za Ayatullahi Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu wa Iran


Mujahidi mkuu, kiongozi wa harakati za mapambano katika eneo hili, mwanazuoni mashuhuri wa kidini, na kiongozi wa kisiasa mwenye busara, Mheshimiwa Sayyid Hassan Nasrullahi, radhi za Mwenye Ezi Mungu zimshukie, alifikia daraja ya shahada katika tukio la usiku wa jana nchini Lebanon na kupaa kuelekea mbinguni. Sayyid shujaa wa mapambano tayari ameshapokea ujira na malipo ya miaka mingi ya jihadi katika njia ya Mwenye Ezi Mungu kupitia mapambano matakatifu. Kwa kweli shahada baada ya juhudi kama hizi ndio tunzo ya msingi ya kazi kama hiyo. Ulimwengu wa Kiislamu umempoteza mtu muhimu na mashuhuri mno; upande wa mapambano nao umepoteza kiongozi wa kipekee; na Hizbullahi ya Lebanon imepoteza kiongozi nadra mno. Lakini, baraka za uongozi wake wa miaka mingi wa hekima na jitihadi zake kamwe hazitapotea. Msingi aliouanzisha Lebanon na kuelekeza fikra za msingi huo kwenye vituo vingine mbali mbali vya mapambano, katu hautafutika kutokana na kifo chake, bali utaimarika zaidi kupitia baraka za damu yake pamoja na mashahidi wengine wa tukio hili. Pigo la upande wa mapambano kwa utawala wa Kizayuni, ambao uko katika hali ya kuzorota na kufifia, litakuwa na nguvu zaidi kwa uwezo na nguvu za Mwenye Ezi Mungu. Dhati ovu ya utawala wa Kizayuni haitaweza kujipatia ushindi katupitia tukio hili. Sayyid wa mapambano hakuwa ni mtu wa kawaida tu, bali alikuwa ni njia na itikadi, na njia hii itaendelea daima bila kuzorota. Damu ya shahidi Sayyid Abbas Musawi haikupotea bure, basi pia damu ya shahidi Sayyid Hassan haitapotea bure. Kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, mapambano haya yataendelea kupata nguvu zaidi, na damu za mashahidi hawa zitakuwa ndiyo taa ya mwanga kwa waliosalia katika njia ya jihadi. Huu ni mwito wa dhati kwa jamii nzima ya Kiislamu, kwa Waislamu wa Lebanon, pamoja na wale wote walioko katika mstari wa mbele wa mapambano dhidi ya dhulma na ukandamizaji. [60]

Sayyid Hassan Nasrullahi, siku ya Ijumaa tarehe 6 Muharam 1403 (sawa na 27 Septemba 2024), alifariki shahidi kutokana na mashambulizi ya anga yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni katika eneo linalokaliwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia liitwalo Dhahiyah, kusini mwa Beirut nchini Lebanon. [61] Jeshi la utawala huo lilidai kwamba lilikuwa likilenga kituo cha miongozo ya na mahali pa mikutano ya Hizbullahi. [62] Baada ya shambulio hilo, jeshi la Israeli lilitangaza kifo cha Sayyid Hassan Nasrullahi pamoja na baadhi ya makamanda wengine, ikiwa ni pamoja na Ali Karaki. [63] Hizbullahi ilithibitisha kifo cha Sayyid Hassan Nasrullahi katika tangazo lililotolewa tarehe 7 Muharam 1403 Hijiria. [71]

Mwitikio wa Watu Mashuhuri na Viongozi Kufuatia Mauaji ya Sayyid Hassan Nasrullahi

Habari za kifo chake zilitangazwa hadharani katika baadhi ya maeneo ya makaburi matakatifu, kama vile katika haram ya Imamu Ridha (a.s) [65] na haram ya Imamu Ali (a.s). [66] Taarifa za Hizbullahi kuhusiana na kifo chake zimekuja zikisema kwamba: "Sayyid wa mapambano, mja mwema Sayyid Hassan Nasrullahi, shahidi mwenye heshima za hali ya juu, kiongozi shujaa, mwenye busara, mwenye ufahamu na muaminifu, tayaria amesha jiunga na msafara wa milele wa mashahidi wa Karbala na kukaribishwa katika uwanja wa radhi za Mwenye Ezi Mungu." Kulingana na taarifa kutoka katika mitandao ya habari za Kiarabu ni kwamba; utawala wa Kizayuni ulitumia karibu mabomu 85 ya chini ya ardhi yenye uzito wa tani moja au mbili katika shambulio lililopelekea mauaji yake, wakati ambapo mkataba wa Geneva unakataza matumizi ya mabomu kama hayo. Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, mwili wa Nasrullahi ulikuwa salama, na sababu ya kifo chake ilikuwa shinikizo au mapigo yaliyotokana na mlipuko au kutokana na gesi za sumu zilizotumika katika shambulio halo.

Shahada ya Said Hassan Nasrullahi iliamsha mwitikio mkubwa kutoka kwa viongozi wa mbali mbali wa kidini na kisiasa. Kuna viongozi kadhaa walitoa salamu za rambirambi kufuatia tukio hili. Miongoni mwa waliotoa salamu za rambai mbai ni pamoja na Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran. [67] Wanazuoni maarufu wa kidini walio onesha hisia zao na kutoa salamu za rambi rambi ni kama vile; Sayyid Ali Sistani, [68] Nasser Makarim Shirazi, [69] Hussein Nuri Hamadani, [70] Jafar Subhani, [71] Sayyid Musa Shuabiri Zanjani, [72] Abdullah Jawadi Amuli, [73] Bashir Hussein Najafi [74] na Hussein Wahid Khurasani [75] pamoja na Jumuiya ya Walimu wa Chuo cha Kiislamu cha Qom (Jaamiatu Al-Mudarrisina) [76] na Jumuia ya Kimataifa ya Ahlul Bayt (a.s). [77]

Salamu za rambirambi na matamko ya kulaani mashambulizi ya Israeli zilikuja kutoka serikali mbalimbali duniani, vikundi vya upinzani, na vyama vya kisiasa, vilionekana kulani kufuatia tukio la kuuawa kwa Sayyid Hassan Nasrullahi. Iran, Urusi, Iraq, Yemen, [78] Cuba [79] na Venezuela [80] zilitoa taarifa rasmi za huzuni na kulani tendo hilo, huku vikundi kama kikundi cha Harakati za Hamas, Kikundi cha Kiislamu cha Harakati za Jihadi cha Palestina, kikundi cha Harakati ya Ansarullah ya Yemen na kikundi cha Harakati cha Fat’hu, kikundi cha Asaibu Ahlu Al-Haqqi, pamoja na kikundi cha Harakati cha Amal, vilisimama nan a kuonesha mshikamano wao. Aidha, viongozi wa Harakati mbali mbali kama vile; Said Ammar Hakim na Muqtada al-Sadr, walijiunga na wengine kulaani mashambulizi hayo ya Israeli. [81] Chama cha Jamaat Islami Pakistan na Chama cha Jamiat Ulamaa-Islam Pakistan ni miongoni mwa walitoa taarifa wakionesha huzuni zao kufuatia kifo cha Said Hassan Nasrullahi na kulaani mashambulizi ya Israeli. [82]

Kufuatia tukio hilo, Iran ilitangaza siku tano za maombolezo, [83] huku Lebanon, [84] Syria, [85] Iraq [86] na Yemen [87] zikitangaza siku tatu za maombolezo kwa umma. Siku ya Jumamosi, vyuo vya dini vilifungwa nchini Iran, na wanafunzi wakafanya maandamano ya kulaani ukatili wa utawala wa Kizayuni. 88] Kumbi za sinema na michezo ya kuigiza pia zilifungwa nchini Iran kwa ajili ya maombolezo ya tukio hili.[89]

Raia wa mataifa mbali mbali kama vile Iran, [90] Pakistan, Yemen, Jordan, Morocco, Ukingo wa Magharibi (Palestina), Bahrain na Iraq walitoka na kufanya maandamano wakilaani mauaji ya Sayyid Hassan Nasrullahi na kuonyesha uungwaji mkono wao kwa Hizbullahi. [91]

Masoud Pezeshkian, Rais wa Iran, pia naye alitoa rambirambi zake kufutia kuuawa shahidi kwa Sayyid Hassan Nasrullahi, katika taarifa yake alieleza akisema kuwa; amri ya shambulio hilo la kigaidi ilitoka New York, akisisitiza kwamba Marekani haiwezi kujiondoa kwenye lawama za kushirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israeli.

Mnamo tarehe 1 Oktoba 2024, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran, katika kujibu mauaji ya viongozi Sayyid Hassan Nasrullahi na Ismail Haniyeh, lilianzisha operesheni maalumu iliyopewa jina la Waadu Saadiq ya 2, ili kulipita kisasi mauaji hayo. Katika operesheni hiyo, jeshi la Iran lilishambulia vituo vya kijeshi na kiusalama vya Israeli kwa makombora kadhaa kama ni jawabu ya hujuma hizo zilizofanya na serikali ya Israeli. [92]

Majaribio ya Mauaji Yaliyofeli

Kwa mujibu wa ripoti kutoka baadhi ya mashirika ya habari ni kwamba; kutokana na ushindi wa Sayyid Hassan Nasrullah dhidi ya Israeli, na kuimarika kwa nguvu za Hizbullah chini ya uongozi wake kama Katibu Mkuu, ilipelekea kupata vitisho vya mara kwa mara na hata kushambuliwa kwa mashambulizi ya kigaidi kutoka utawala wa Kizayuni. Majaribio kadhaa ya mauaji yaliyofanywa dhidi yake ni kama ifuatavyo:

  • 2004: Jaribio la kumuuwa kwa kumtilia sumu iliyo wekwa kwenye chakula.
  • 2006: Mashambulizi ya mabomu yaliyofanywa na ndege za kivita za Israeli kwenye jengo alilokuwa akiishi Sayyid Nasrullahi. Mnamo Aprili 28 mwaka huo, kikundi cha kigaidi kilichopanga kutekeleza shambulizi la bomu dhidi ya gari la Sayyid Hassan Nasrullah kilikamatwa, na hivyo kuzuia jaribio hilo.
  • 2011: Mripuko ulitokea kwenye jengo lililodhaniwa kuwa Sayyid Hassan Nasrullah alikuwa ndani yake, shambulizi lililofanywa na ndege za kivita za Israeli.

Shughuli na Majukumu ya Kisiasa: Kutoka Harakati za Amal Hadi Hizbullah

Sayyid Hassan Nasrullah alianza kushiriki katika shughuli za kisiasa tangu akiwa na umri mdogo. Ufuatao ni muhtasari wa shughuli zake za kisiasa:

  • Kujiunga na Harakati za Amal (1975): Sayyid Hassan Nasrullah alijiunga na harakati za Amal tokea mwaka 1975, baada tu ya kumaliza masomo yake ya sekondari, akiongozwa na upendo wake kwa Imamu Musa Sadr. Yeye alijiunga na kikundi hicho akiwa pamoja na kaka yake, Sayyid Hussein, aliyekua kiongozi wa harakati hizo katika mji wa al-Bazuriyya. [93]
  • Mwanachama wa Kamati ya Kisiasa (1982): Mnamo mwaka 1982, Sayyid Hassan alikua ni mwanachama wa kamati ya kisiasa ya harakati za Amal huku akishika jukumu muhimu katika siasa za eneo la Baqaa. [94]
  • Kuanzisha Kundi la Hizbullahi (1982): Mnamo mwaka huo huo wa 1982, baada ya uvamizi wa Lebanon uliofanywa na majeshi ya utawala wa Kizayuni, na kukataliwa kwa mpango wa amani kati ya Israel na baadhi ya viongozi wa harakati za Amal, Sayyid Hassan pamoja na baadhi ya wanafunzi wapiganaji kama vile Sayyid Abbas Moussa na Subhi Tufaili, waliamua kujitenga na harakati za Amal na kuanzisha msingi wa kwanza wa Hizbullah nchini Lebanon. [95]
  • Kiongozi wa Hizbullah Katika Kitongoji cha Baqaa (1985): Mnamo mwaka 1985, Sayyid Hassan aliteuliwa kuwa kiongozi na mwakilishi wa Hizbullah katika eneo la Baqaa, akichangia katika uimarishaji wa harakati hizo. [96]
  • Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji (1987): Katika mwaka 1987, Sayyid Hassan alikua ni mwenyekiti wa kamati ya utendaji ya Hizbullahi na mwanachama wa baraza la maamuzi la kundi hilo. [97]
  • Mwakilishi wa Hizbullahi nchini Iran (1989-1990): Wakati wa uwepo wake mjini Qom, Sayyid Hassan alikua ndiye mwakilishi wa Hizbullah nchini Iran, na ndiye aliye husika na ufuatiliaji wa shughuli za Hizbullahi nchini humo. [98]
  • Katibu Mkuu wa Hizbullahi (1992): Mnamo mwaka 1992, baada ya kuuawa kwa Sayyid Abbas Mussawi, Sayyid Hassan alichaguliwa kuwa katibu mkuu wa Hizbullahi, na kuendelea na uongozi wake wa kisiasa na kijeshi katika harakati mbali mbali za kikundi hicho. [99]
Sayyid Hassan Nasrullah

Mnamo mwaka wa 1360 Shamsia, Sayyid Hassan Nasrullahi alipata ruhusa ya kukusanya fedha za kidini na kushughulikia masuala ya kidini kutoka kwa Imamu Khomeini. [100] Hii ilimuwezesha kujijenga kama kiongozi wa kidini na kisiasa katika jamii ya Kiislamu. Aidha, Sayyid Hassan alikuwa ni mwakilishi na wakili maalumu wa Ayatullahi Khamenei katika Beirut na eneo la Jabal ‘Amil. [101]

Kazi Andishi na Sanaa Kuhusiana na Sayyid Hassan Nasrullah

Kuna kazi nyingi andishi zilizo andikwa kuhusiana na; maisha, tabia, na uongozi wa Sayyid Hassan Nasrullah, zikijumuisha vitabu, filamu, makala, na hata nyimbo. Baadhi ya kazi hizi muhimu ni kama ifuatavyo:

Vitabu

  • Kitabu: Sayyid Aziz Zindeginame Khodgofte Hujjatu Al-Islam Sayyid Hassan Nasrullah (Wasifu binafsi wa Hujjat al-Islam Sayyid Hassan Nasrullah), kilichokusanywa na Hamid Dawoodabadi. Ayatullah Khamenei, katika maoni yake juu ya kitabu hichi, aliandika akisema: "Kila jambo linalochangia kumfahamu zaidi na kumheshimu Sayyid huyu mpendwa ni zuri na kwa upande wangu binafsi, ni jambo linaniletea furaha."
  • Kitabu: Sayyid Hassan Nasrullah: Inqilabe Junubi (Mapinduzi ya Kusini), kilichoandikwa na Rif’at Sayyid Ahmad na kutafsiriwa na Asma Khajezaadeh, kilichochapishwa na taasisi ya Nashr Ma'arif huko Qom mwaka 1394 SH.
  • Zabur Muqaawimat (Zaburi ya Ukombozi); kitabu kinachozungumzia mwongozo wa maisha, misimamo, na mitazamo ya Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Huzbollah ya Lebanon, kilichoandikwa na Muhammad Hussein Bazi na kutafsiriwa na Mostafa Allahyari, kilichochapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1387 SH na Shirika la Uchapishaji la Tablighi Islami.
  • Azadtariine Marde Jihan (Mwanamme Huru Zaidi Duniani); kitabu kilichoandikwa na Rashid Jafarpoor.
  • Nasrullahi; mahojiano ya kipekee kati ya Muhammad Rdhaa Za’iri na Sayyid Hassan Nasrullah.
  • Rahabariye Inqilabi Sayyid Hassan Nasrullahi (Uongozi wa Mapinduzi wa Sayyid Hassan Nasrullahi); kitabu kilichoandikwa na Azita Bidqi Qurrebaagh [102]

Nyimbo na Filamu za Hati Elezi za Matukio ya Kweli (Documentary)

Kumekuwa na filamu na nyimbo mbalimbali zinazohusiana na Sayyid Hassan Nasrullahi, zikilenga kuonyesha ustadi wa uongozi wake, mapambano dhidi ya Israeli, na ushawishi wake katika harakati za Hizbullahi. Wapenzi na wafwasi wa Hizbullahi, wameandika nyimbo kadhaa katika kuakisi ujumbe wa mapambano na upinzani dhidi ya dhulma, zikimtukuza Sayyid Hassan kama kiongozi wa ukombozi. Pia kuna rikodi kadhaa za filamu za hati elezi, zitoazo zitoazo picha halisi ya Sayyid Nasrullahi kama kiongozi wa kidini na kisiasa. Miongoni mwa filamu hizo ni kama ifuatavyo:

  • Filamu ya Negahi be Zindegi Sayyid Hassan Nasrullahi (Mwangaza wa Maisha ya Sayyid Hassan Nasrullahi): Hii ni filamu iliyorushwa na kituo cha habari cha “Shabake Khabar”, ikitoa uchambuzi wa kina kuhusu maisha ya Sayyid Hassan Nasrullahi, ikijikita kwenye uongozi wake na ushawishi wake ndani ya Hizbullahi.
  • Filamu ya Munadiane Azadi (Wanadiaji Uhuru) (sehemu inayohusiana na Sayyid Hassan Nasrullahi): Filamu hii pia ilirushwa na “Shabaka Khabar”, ikiangazia nafasi ya Nasrullahi kama kiongozi wa mapambano dhidi ya Israeli na mchango wake katika harakati za uhuru.
  • Filamu ya Nasrullahi dar Cheshme Dushmaanaan (Nasrullahi Katika Macho ya Maadui): Hii ni filamu ya dakika 50 iliyotayarishwa na shirika la habari la “Shabakatu Al-Mayadeen”. Filamu hii imetayarishwa kupitia hotuba za Sayyid Hassan Nasrullahi na imetumia picha na uchambuzi kutoka kwa wataalamu na wachambuzi wa Kiyahudi wa Israeli.
  • Filamu ya Hikaayaat Hassan (Hikaya za Hassan): Hii ni filamu iliyorushwa na kituo cha habari cha Shabaka Al-Arabiya, ikimuelezea Sayyid Hassan Nasrullahi. Filamu ambayo ilipelekea meneja wa “Shabaka Al-Arabiya” kuondolewa madarakani kwa sababu ya kuruhusu kurushwa kwa filamu hiyo.

Nyimbo na Video za Muziki kuhusiana na Sayyid Hassan Nasrullah

Kuna nyimbo na video mbali mbali za muziki zilizo tungwa na kuimbwa kuhusiana na Sayyid Hassan Nasrullah, zikieleza uongozi wake, mapambano dhidi ya udhalimu, pamoja na nafasi yake muhimu kama kiongozi wa Hezbollah. Miongoni mwazo ni kama ifuatavyo:

  • Nyimbo iitwayo «Nasrullahi» iliyotungwa na kuimbwa na Ali Nafari [103]
  • Video ya muziki wa Kiarabu iitwayo «Ya Nasrullahi» iliyotungwa na kuimbwa na Ali Al-Attar.
  • Video ya muziki wa Kiajemi iitwayo «Ma Baz Mi-Gardim» (Tunarudi Tena) iliyotungwa na kuimbwa na Aliridha Alizadeh. [104]
  • Video ya muziki wa Kiajemi iitwayo «Waqt-e Mujazat» (Wakati wa Adhabu) iliyotungwa na kuimbwa na Hossein Redhai. [105]
  • Video ya muziki wa Kiajemi na Kiarabu iitwayo «Aashiqan-e Qadimi» (Wapenzi wa Zamani) iliyotungwa na kuimbwa na Omid Manawi. [106]
  • Video ya muziki iitwayo «Amanatdar Banu-ye Dimashq» (Mlinzi wa Bibi wa Damascus), kazi ya lugha mbili (Kiajemi na Kiarabu) iliyotungwa na kuimbwa na Mujtaba Minutan na Haamid Mahdharnia. [107]
  • Wimbo «Ya Sayyidi» na «Lilsayyid Rabb Yuhmiihi» uliotungwa na kuimbwa na Bassam Shams.
  • Wimbo wa Kiarabu «Ahbaai» uliotungwa na kuimbwa na Julia Boutros, mwimbaji wa Kikristo wa Lebanon (2006).
  • Wimbo "Ya Nasrullahi" uliotungwa na kuimbwa na Alaa Zalzali, mwimbaji wa Lebanon (2007). [108]

Nyimbo hizi zimekuwa maarufu katika ulimwengu wa Kiislamu, zikitangaza ujumbe wa ujasiri, mapambano dhidi ya udhalimu, na kuakisi heshima ya uongozi wa Sayyid Hassan Nasrullahi. Nyimbo za hamasa zinaakisi mapambano na uthabiti, hasa miongoni mwa wafuasi wa Hezbollah na jamii za Waislamu wa mataifa mbalimbali.

Makala Zinazo Husiana

Rejea

Vyanzo