Nenda kwa yaliyomo

Israel

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Utawala wa Kizayuni)
Makala hii inahusiana na utawala unaoikalia kwa mabavu Palestina. Ili kujua kuhusiana na Palestina na kukaliwa kwake kwa mabavu angalia makala za Palestina na kukaliwa kwa mabavu Palestina.

Israel au Utawala wa Kizayuni (إسرائيل أو الكيان الصهيوني) ulitangaza uwepo na kuanzishwa kwake 1948 ukiwa na aidiolojia ya Uzayuni. Utawala huo ulifikia hilo baada ya kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina. Waislamu wanaitambua Israel kuwa ni utawala bandia na adui mkuu wa Uislamu. Marajii Taqlidi wa Kishia wanatambua kuwa, ni haramu kufanya muamala wa aina yoyote na kuwa na uhusiano na Israel na wanataka utawala huo ghasibu ufurushwe na kufukuzwa kutoka Palestina.

Baadhi ya maeneo ya ziara ya Kishia yaliyoko huko Israel ni pamoja na Maqam Raas al-Hussein (palipowekwa kichwa cha Imam Hussein) Ashkelon, maqam ya Imam Ali katika njia ya Quds kuelekea Jaffa, eneo la ziara liinalonasibishwa na Fatma binti ya Imam Hussein (a.s) na eneo jingine la ziara linalonasibishwa na Sukaina binti ya Imam Hussein (a.s).

Inaelezwa kuwa katika baadhi ya vyuo vikuu vya Israel kuna masomo ya Kuujua Uislamu na Kuujua Ushia. Chuo Kikuu cha Jerusalem, Haifa, Tel Aviv na Bar-Ilan vimetajwa kuwa vituo muhimu vya utafuti kuhusu Uislamu huko Israel.

Nchi nyingi za Kiislamu kama Indonesia, Pakistan, Syria, Iraq, Malaysia, Saudi Arabia, Yemen na Iran (baada ya mapinduzi) haziutambui utawala wa Kizayuni na wala hazina uhusiano wa kisiasa na kibiashara nao.

Kuanzishwa kwa Israel na kuikalia kwa mabavu Palestina kulikuwa na matokeo kama vile mauaji na kuwa wakimbizi watu wengi wa Palestina, kuundwa kwa mhimili wa muqawama (mapambano) na harakati za wananchi huko Palestina na maeneo yanayoizunguka na maandamano katika maeneo mbalimbali duniani. Kwa mujibu wa ripoti, hadi kufikia mwaka 2023 chini ya asilimia 15 ya Palestina (inayojumuisha Ukanda wa Gaza na sehemu zilizotawanyika za eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan) ndizo zilizokuwa zimesalia mikononi mwa Wapalestina. Kwa maana kwamba, asilimia kubwa ya ardhi ya Palestina ilishaporwa na kughusubiwa na Wazayuni.

Wazayuni wakiwa na lengo la kuhalalisha kuasisi Israel huko Palestina wametaja sababu kadhaa na miongoni mwazo ni kuwa, Mayahudi ni kaumu na jamii teule na Palestina ni ardhi iliyoahidiwa Wayahudi. Kwa muktadha huo, kuwafukuza Waarabu Wapalestina ni haki ya Mayahudi na Wazayuni. Ngano ya Holocaust na kaulimbiu ya "Ardhi bila watu ni kwa ajili ya watu wasio na ardhi" ni sababu zingine zilizotajwa za kuhalalisha uvamizi wao huko Palestina.

Upinzani wa Maulamaa wa Kishia dhidi ya Israel

Wanazuoni wa Kishia daima wamekuwa wakipinga kuasisiwa Israel na kulaani jinai zake. Kwa mtazamo wa baadhi ya Marajii Taqlidi kama vile Sayyid Muhammad Hadi Milani, [2] Imam Khomeini [3] na Muhammad Fazil Lankarani, [4] ni haramu kufanya muamala wowote na Israel kama ambavyo matumizi ya bidhaa za Israel zake ni haramu pia. Kundi jingine kama vile Sayyid Mohsen Hakim, Sayyid Abul-Qassim Khui, Ayatullah Buroujerdi, Sayyid Abdul Hussein Sharafuddin, Sayyid Abul-Qassim Kashani [5] na Imam Khomeini [6] sambamba na kulaani jinai za Israel, wametaka kufukuzwa kwa utawala huo kutoka Palestina. Abdul Karim Zanjani, mmoja wa mafakihi wa Kishia wa karne ya 14 Hijria baada ya tangazo la kuanzishwa utawala wa Israel na vita baina ya Israel na Waarabu mwaka 1948, alitoa fat’wa ya Jihadi dhidi ya utawala huo. [7]

Imam Khomeini ameitambulisha Israel kama adui mkuu wa Uislamu, Qur'ani na Mtume (s.a.w.w), ambayo haisiti hata kidogo kufanya jinai yoyote na uporaji katika mataifa ya Kiislamu. [8]. Kwa mtazamo wa Murtadha Mutahhari, Israel ndiye adui mgumu na hatari zaidi wa Waislamu. [9]

Imamu Khomeini

Ninachukulia kuunga mkono mpango wa uhuru wa Israel na kutambuliwa kwake kama janga kwa Waislamu na mlipuko kwa serikali za Kiislamu, na ninaona kuupinga kama faradhi kubwa ya Uislamu.[1]

Imam Mussa Sadr anauchukulia utawala wa Israel kama kielelezo kamili cha ukiritimba na kuhodhi mambo, udhalimu, uvamizi na ukatili. [11] Ayatullah Khamenei pia ameitambulisha Israel kuwa ni utawala wa ghasibu, mtenda jinai, [12] mwongo, [13] muuaji wa watoto na mnyongaji, [14] bandia [15] na adui khabithi na muovu zaidi kwa Uislamu na ubinadamu. [16]

Uhusiano wa Mataifa ya Kiislamu na Israel

Uhusiano kati ya nchi za Kiislamu na Israel nao umekuwa wa kupanda na kushuka. Nchi nyingi za Kiislamu kama Indonesia, Pakistan, Syria, Iraq, Afghanistan, Algeria, Bangladesh, Kuwait, Lebanon, Libya, Malaysia, Oman, Qatar, Somalia, Saudi Arabia, Tunisia, Yemen na Iran (baada ya mapinduzi), haziutambui rasmi utawala wa Kizayuni wa Israel. [17]

Pamoja na hayo, baadhi ya viongozi wa nchi za Kiislamu wameanzisha uhusiano wao wa kawaida na Israel. Miongoni mwa mataifa hayo ni Misri, Jordan, Bahrain, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Sudan na Morocco. [18] Uturuki imechukuliwa kuwa nchi ya kwanza ya Kiislamu kuanzisha uhusiano na ushirikiano na Israel. Uturuki iliitambua rasmi Israel mnamo Machi 1949 na kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia nayo mwaka wa 1952. [19]

Mnamo Machi 1950, Iran iliitambua rasmi Israel na kuanzisha uhusiano wa kisiasa na utawala huo. [20] Miaka miwili baadaye na baada ya kuingia madarakani Muhammad Mosaddeq, Iran ikakata rasmi uhusino na Israel. [21] Katika kipindi cha utawala wa Reza Pahlavi, uhusiano kati ya Iran na Israel ulianza tena na mnamo mwaka 1346 Hijria Shamsia, ubalozi wa Israel ulianza kazi rasmi nchini Iran, na ulidumu hadi ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. [22] Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979 uhusiano wa Israel na Iran ulivunjwa na ubalozi wa Israel ukabadilishwa na kuwa ubalozi wa Palestina. [23]

Masomo ya kuujua Uislamu na kuujua Ushia katika Israel

Ushia na Iran yamezingatiwa kuwa miongoni mwa masomo ya utafiti wa vyuo vikuu vya Israel. [24] Imekuja katika kitabu cha “Eslam Pezhohi Dar Israil (Utafiti wa Uislamu Israel) kwamba: Israel imetoa kipaumbele kwa kiasi kikubwa katika shughuli zake za utafiti kwa Uislamu kwa kuhamasisha vituo vya kielimu na shakhsia mahiri duniani kufanya utafiti kuhusu Uislamu, madhehebu za Kiislamu, Waislamu na jamii za Kiislamu. [25]

Kwa mujibu kitabu cha utafiti kuhusu Shia na watafiti wa Kishia wanaozungumza Kiingereza, Chuo Kikuu cha Kiebrania cha Jerusalem, mojawapo ya vyuo vikuu muhimu zaidi Israel, kilichoko Baytul-Muqaddas kina kitivo maalumu katika masomo ya Shia. [26] Chuo Kikuu cha Tel Aviv ndio kikubwa zaidi miongoni mwa vyuo vikuu vya Israel, pia kina kitengo maalumu cha utafiti wa masomo ya kuujua Uislamu na kuujua Ushia. [27]

Picha ya jalada la kitabu Islam Pezuhesh Dar Israel, kilichoandikwa na Akbar Mahmoudi

Kitabu cha Belief and Law in Imami Shi'Ism (imani na fiqhi katika Shia Imamiyyah) kilichoandikwa na Etan Kohlberg, [28] Shia Imamiyyah Ba Negahe Be Sunnat Revai Anan, kilichoandikwa na Joseph Elias [29] na “Kalam, Falsafe Va Erfan Shia Davazdah Emami” kilichoandikwa na Zabinah Schmidtke, ambaye alishinda Tuzo ya Dunia mwaka wa 2002 ya kitabu cha mwaka cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, [30] ni miongoni kazi muhimu za watafiti wa Ushia wa Israel.

Hali ya Mashia na Maeneo ya Kishia katika Palestina Inayokaliwa kwa Mabavu

Hakuna takwimu sahihi za idadi ya Mashia wanaoishi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel. Kituo cha Takwimu cha Quds inayokaliwa kwa mabavu kimetangaza kuwa, idadi ya Mashia rasmi mwaka 2007 ilikuwa 600; hata hivyo takwimu hizi hazijatambuliwa kuwa ni makini; kwa sababu Mashia wengi huficha itikadi yao ya Ushia kwa hofu na wasiwasi wa kumbuliwa na vyombo vya usalama vya Israel.Mtandao wa Kanali ya Saba ya Yemen ulitangaza idadi ya Mashia katika mwaka huo huo kwamba ni watu 6,000. Idadi hii imeripotiwa kuwa inafikia hadi 10,000 [31].

Inasemekana kwamba tangu kutangazwa kwa uwepo wa Israel, Mashia wamekuwa wakiishi Israel, na vikundi vya Kishia kama vile "Watoto wa Abdul-Rafi" na "Mashia wa Kweli" wanafanya harakati zao kwa siri. [32] Takwimu za Waislamu wanaoishi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) hadi kufikia mwaka 2022 ilikuwa 1,728,000. [33]

Maeneo Yanayonasibishwa na Ahlul-Bayt katika Ardhi Zinazokaliwa kwa Mabavu

Madhabahu ya Raas al-Hussein huko Ashkelon, Palestina.

Miongoni mwa vituo vya Kishia huko Israel ni maqam Raas al-Hussein huko Ashkelon ambacho baadhi ya watafiti wamekieleza kuwa ni ziara muhimu na mashuhuri zaidi na wamekinasibisha na Ahlul-Bayt (a.s). [34] Sababu ya kuwa mashuhuri na umuhimu wa eneo hilo ni kuwa, kwa mujibu kauli, kichwa cha Imamu Hussein kimezikwa hapo. [35] Inaelezwa kuwa, kichwa cha Imamu Hussein kilihamishiwa Cairo katika nusu ya pili ya karne ya sita Hijria; lakini maqam ya Raas al-Hussein huko Ashkelon ingali inaheshimiwa na watu wanafanya ziara katika eneo hilo. [36]

Kuna maeneo mbalimbali pia ambayo yananasibishwa na Imam Ali (as) na miongoni mwa maeneo hayo ni maqam na eneo la ziara ya Imam Ali katika njia ya Quds kuelekea Jaffa (Tel Aviv) ambalo limebomolewa, maqam ya Imamu Ali katika mji wa Nablos, katika mji wa Acre na Lud. [37] Katika mji wa al-Khalil kuna eneo la ziara linalonasibishwa na Fatma binti wa Imam Hussein (a.s) na katika mji wa Tabariya kuna eneo la ziara ambalo linanasibishwa na Sukainah binti ya Imamu Hussein (a.s). [38]

Kukaliwa kwa mabavu Palestina na kutangazwa rasmi kuundwa Israel

Makala Kuu: Kukaliwa kwa Mabavu Palestina

Mnamo Mei 14, 1948 baada ya kufikia mwisho kwa mamlaka na usimamizi wa Uingereza kwa Palestina, [39] David Ben-Gurion, baba na mbunifu wa utawala wa Israel, [40] alitangaza katika ukumbi wa mkutano wa jiji la Tel Aviv mamlaka ya kujitawala na kuanzishwa kwa taifa la Kiyahudi la Israel. [41] Baada ya hapo, kukaliwa kwa mabavu Palestina kukawa kumeanza rasmi. [42]

Mchakato wa Israel kuikalia Palestina kwa mabavu, kutoka 1917 hadi 2020. Rangi nyeupe: Maeneo yaliyochukuliwa.

Siku moja baada ya tangazo la kuwepo na kuanzishwa Israel, majeshi ya nchi tano za Kiarabu (Misri, Lebanon, Syria, Jordan na Iraq) [43] yaliingia vitani na Israel ili kuunga mkono Palestina [44]. Baada ya vita hivi, maeneo yaliyotekwa yalifikia 78%. [45].

Kwa mujibu wa ripoti, hadi kufikia mwaka 2023 chini ya asilimia 15 ya Palestina (inayojumuisha Ukanda wa Gaza na sehemu zilizotawanyika za eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan) ndizo zilizokuwa zimesalia mikononi mwa Wapalestina na maeneo mengine yalikuwa tayari yamekaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni. [46]

Siku ya tangazo la kuwepo (kuanzishwa) kwa Israel inajulikana kama siku ya «Nakba» au «Maafa» kati ya Wapalestina, na wanalaani siku hii kila mwaka kwa kufanya maandamano. [47] Israel kutokana na kuikaliwa kwa mabavu Quds na Palestina inajulikana kama utawala vamizi wa Quds au utawala ghasibu wa Israel. [48]

Matokeo ya Kutangazwa Uwepo wa Israel

Kutangazwa rasmi uwepo wa Israel na kukaliwa kwa mabavu Palestina kumekuwa na matokeo mabaya kwa Palestina na ulimwengu wa Kiislamu. Baadhi ya matokeo hayo ni:

Kuuawa na kufanywa wakimbizi wananchi wa Palestina: Kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha upashaji habari cha Palestina ni kuwa, kufuatia kukaliwa kwa mabavu Palestina kuanzia 1948 mpaka 2023, zaidi ya Wapalestina 100,000 wameuawa. [49] Kituo hiki kikilinukuu Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) kimetangaza kuwa, idadi ya wakimbizi wa Kipalestina hadi kufikia mwaka 2020 ilikuwa milioni 6.4. [50]

Kuundwa mhimili wa muqawama na harakati za wananchi: Baada ya kukaliwa kwa mabavu Palestina na maeneo yanayoizunguka, kuliundwa na kuanzishwa harakati na asasi mbalimbalii kama vile Harakati ya Fat'h mwaka 1959, [51] Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) mwaka 1964, [52] Harakati ya Jihad al-Islami mwaka 1979, [53] na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS mwaka 1987 [54] huko Palestina na Harakati ya Amal mwaka 1975 [55] na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah mwaka 1982 huko nchini Lebanon [56] kwa ajili ya kukabiliana na Israel.

Wananchi wa Palestina katika kipindi chote cha kukaliwa kwa mabavu ardhi zao walianzisha mapambano mara chungu nzima dhidi ya Israel. [57] Kuibuka Intifadha tatu huko Palestina: Intifadha ya kwanza (Intifadha ya Mawe) ilikuwa mwaka 1987, Intifadha ya Pili (Intifadha ya al-Aqswa (Septemba 2000 na Intifadha ya Tatu (Intifadha ya Quds) mwanzoni mwa Oktoba 2015. [58]

Kadhalika angalia: Mhimili wa Muqawama

Malengo ya Kuasisiwa Israel

Kuasisiwa nchi kubwa (Israel Kubwa) yenye utambulisho wa Uyahudi ikiwa na nguvu na udhibiti wa eneo la Mashariiki ya Kati ndilo lengo la kwanza na muhimu zaidi la lililotajwa la kuasisiwa utawala wa Kizayuni wa Israel. [59] Roger Garaudy, mwandishi, mwanasiasa na mustabsir (mtu ambaye ameingia katika Ushia) wa Kifaransa anaamini kwamba, lengo la kimsingi la Wazayuni ni kuhajiri Mayahudi wote na kuelekea katika «ardhi ahidiwa» [60] na kuanzisha dola la Kiyahudi katika Palestina. [61] Imamu Khomeini anaamini kuwa, lengo la kuasisiwa Israel katika ardhi za Palestina ni kuudhibiti ulimwengu wa Kiislamu na kuzikoloni ardhi za Kiislamu. [62]

Sababu za Wazayuni za Kuasisi Israel

Murtadha Mutahhari

Wanadai kwamba, miaka 3000 iliyopita watu wawili katika sisi (Daud na Suleiman) walitawala kwa muda huko…Katika kipindi chote hiki cha miaka 2000 ni lini ardhi ya Palestina ilikuwa ikimilikiwa na Wayahudi?...kabla ya Uislamu pia haikuwa milki yao kama ambavyo baada ya Uislamu pia haikuwa mali yao. Siku ambayo Waislamu waliikomboa Palestina, ardhi hiyo ilikuwa ikimilikiwa na Wakristo na sio Mayahudi. Kimsingi Wakristo walifikia suluhu na mapatano na Waislamu. Moja ya vipengee vilivyokuwako katika hati ya mkataba wa amani ni kwamba, msiwaruhu Mayahudi kuingia hapo. Imekuwaje mara ghafla ardhi hiyo imechukua anuani ya nchi ya Mayahudi? [63]

Wazayuni wametaja sababu na uhalalishaji wa kuikalia kwa mabavu Palestina na kuanzisha taifa la Israel huko, ambalo pia linajulikana kama simulizi au hekaya za Israel [64] Sababu hizi zina vipengele vya kidini na visivyo vya kidini: Moja ya sababu zao za kidini ni kwamba, Palestina ndio ile «ardhi iliyoahidiwa» [65], ambapo suala la kupatwa ardhi hiyo kizazi cha Ibrahim (a.s) limekuja katika Agano la Kale. [66] Kwa mtazamo wa Wazayuni ni kuwa, kuwafukuza wengine kutoka katika ardhi ambayo imeahidiwa watu maalumu sio tu kwamba, ni haki kufanya hivyo bali ni taklifu (jukumu). [67]

Tukio la Holocaust (mauaji dhidi ya mayahudi) ni miongoni mwa sababu zisizo za kidini za Wazayuni ambazo wanazitumia kuhalalisha na kuifanya kuwa sababu kuu ya kuasisiwa dola la Israel; [68] mpaka imefikia kuelezwa kuwa, kuanzishwa dola la Israel lilikuwa jibu la Mwenyezi Mungu kwa mhanga mkubwa. [69] Mayahudi wanaamini kwamba katika tukio hili, Wayahudi milioni sita waliuawa na Adolf Hitler katika Vita vya Pili vya Dunia. [70] Tukio hili liliwafanya Wazayuni kupiga kelele za kuonewa na kudhulumiwa kuomba fidia kutoka kwa jamii ya kimataifa. Wazungu walifikiria kuanzisha dola huru kwa ajili yao kwa kisingizio cha kufidia uharibifu huu. [71] Pamoja na hayo wakosoaji wa madai haya ya Mayahudi wanapinga idadi na takwimu zinazotolewa kuhusiana na idadi Mayahudi waliouawa katika vita hivyo. [72]

Vita na Mauaji

Makala Kuu: Orodha ya Vita vya Israel Dhidi ya Waislamu

Israel imewashambulia mara kwa mara watu wa Palestina na Lebanon na nchi za Kiislamu za eneo hilo na kuanzisha vita ambavyo vimepelekea vifo vya idadi kubwa ya raia na kusababisha uharibifu mkubwa. [73]

Maeneo ya makazi yaliyoharibiwa na Israeli katika vita vya siku 33 (Dhahiya, kusini mwa Beirut, 2006)

Pia, Israel imewashambulia mara kwa mara watu wa Ukanda wa Gaza; ikiwa ni pamoja na vita vya siku 22 mwaka 2008, vita vya siku 8 mwaka 2012, na vita vya siku 51 mwaka 2014. [74] Mnamo Oktoba 2023, Israel ilishambulia Ukanda wa Gaza kujibu operesheni ya kijeshi ya Kimbunga cha al-Aqswa iliyotekelezwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na imeua zaidi ya Wapalestina 40,000 na kujeruhi maelfu ya wengine. [75]

Mauaji ya Umati

Makala Kuu: Orodha ya mauaji ya Israel

Katika kipindi cha kuikalia kwa mabavu Palestina, Israel imefanya mauaji mengi sana huko Palestina na maeneo yanayoizunguka. Baadhi ya mashirika ya habari yametaja hadi kesi 120. [77] Kulingana na ripoti ya Kituo cha Habari cha Palestina, kutoka 1948 hadi 2023, zaidi ya Wapalestina 100,000 wameuawa na Wazayuni. [78] Jinai za Israeli dhidi ya Wapalestina na mauaji ya raia na watoto ambayo yametekelezwa na utawala wa Kizayuni yameitwa kuwa ni mauaji ya halaiki. [79]

Mauaji kwa Malengo ya Kisiasa

Kwa mujibu wa takwimu za vyombo vya habari, Wazayuni wa Israel katika kipindi chote cha kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel wamefanya mauaji 2700 yenye malengo ya kisiasa. [80] Katika ripoti iliyopewa jina la "The World's Deadliest Killers" (Wauaji Wabaya Zaidi Duniani), gazeti la lugha ya Kiingereza la Independent la Ireland limeliita Shirika la Kijasusi la Israel (Mossad) "mashine ya mauaji ya kikatili ya Israel".[81] Mauaji haya ya malengo ya kisiasa ya utawala wa Israel hayakuishia Palestina na viongozi wa kijeshi na wanaharakati wa muqawama tu; bali yamewalenga na kuwaua viongozi wengi wa kisiasa na wanasayansi katika maeneo mbalimbali ulimwenguni. [82]Baadhi ya watu na shakhsia waliouawa na utawala wa Kizayuni wa Israel ni: Sayyid Abbas Mousavi, Katibu Mkuu wa pili wa Hizbullah nchini Lebanon, Emad Mughniyeh, mmoja wa makamanda wa Hizbullah, Ragheb Harb, kiongozi wa kidini wa Kishia anayejulikana kwa jina la Sheikh wa Mashahidi wa Muqawama nchini Lebanon, Samir Kuntar, mmoja wa wanachama wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO), Fat’hi Shaqaqi, mwanzilishi wa Harakati ya Mapambano ya Jihadul Islami na Sheikh Ahmad Yassin mmoja wa viongozi wa Hamas. [83] Kulingana na nyaraka na ripoti, Shirika la Ujasusi la Israel (Mossad) pia lilihusika katika mauaji ya wanasayansi wa nyuklia wa Iran kama vile Ali Mohammadi, Shahriari, Ahmadi Roshan, Rezainejad na Fakhrizadeh. [84]

Kukiuka Sheria na Maazimio ya Kimataifa

Ramani ya Israel na maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu.

Israel imetambulishwa kuwa imevunja rekodi ya kupinga maazimio ya Umoja wa Mataifa. [85] Inasemekana kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha maazimio zaidi ya 102 kutoka 1948 hadi 2016, na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lilipitisha maazimio 104 ya kuilaani Israel kutoka mwaka 2006 hadi 2023. [86] Marekani ikiwa na lengo la kuiunga mkono Israel, imepiga kura ya turufu mara 30 dhidi ya maazimio ya Umoja wa Mataifa ya kulaani Israli kutoka 1972 hadi 1996. [87]

Miongoni mwa maazimio yaliyopasishwa kulaani hatua za Israel ni:

  • Azimio nambari 3236 la 22 Novemba 1974: Azimio hili lilipasishwa likieleza haki ya Palestina kujiainishia hatima na mustakabali wake, haki ya mamlaka ya kujitawala Palestina na haki ya wakimbizi wa Kipalesrina kurejea katika ardhi zao; hata hivyo Israel imelikanyaga azimio hilo na kukataa kulitekeleza. [88]
  • Azimio nambari 3234 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la 23 Disemba 2016: Azimio hili lilipasishwa likilaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa. [89]
  • Azimio nambari 242 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa: Katika azimio hili lililopasishwa 22 Novemba 1967, baraza la Usalama lilitaka kuondoka vikosi vya utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi zilizokaliwa kwa mabavu mwaka 1967. [90]

Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu

Baada ya kukamilika kwa mazungumzo haya ya nyuklia, nimesikia Wazayuni katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu wakisema kwamba, kwa muda huu, kwa mazungumzo haya, tutakuwa huru na kuondokana na wasiwasi na Iran kwa miaka 25 ... ninajibu ... nyinyi [Israel] hamtaiona miaka 25 ijayo. Inshallah, Mwenyezi Mungu akipenda, mpaka miaka 25 ijayo kwa tawfiki ya Mwenyezi Mungu, hakutakuwa na kitu kinachojulikana kwa jina la utawala wa Kizayuni katika eneo. [91]

Bibliografia

Makala Kuu: Orodha ya vitabu kuhusu Palestina na Israel

Kumeandika vitabu mbalimbali kuhusiana na historia ya kuundwa Israel, siasa, vita na masuala yanayohusiana na hayo. Baadhi yavyo ni:

  • Daneshnameh Soyonism va Israel: Kitabu hiki kimeandikwa kwa lengo la kuutambua Uzayuni na Israel. Kitabu hiki cha mijalada 6 kimeandikwa na Majid Safataj Gardavari.
  • Siyasat Da Diyanat Dar Israel: Mwandishi Abdul-Fattah Madhi, mtarjumi Gholamreza Tahami.
  • Tu Zodtar Bokosh: Mwandishi Ronen Bergman, mtarjumi Vahid Khidhab. Kitabu hiki ni simuzlizi za vikosi vya operesheni na kijasusi za Israel za miaka 60 ya mauaji ya Shirika la Kijasusi la Israel (MOSSAD).
  • Majaray Felestin Va Israel: Mwandishi Majid Safataj.
  • Dah Ghalat Mashuhur Darbaray Israel (vitu vingi ambavyoi watu wanadhani ni sahihi kumbe sio kweli): Mwandishi Ilan Pappe, mwanahistoria wa Kiisrael. Mtarjumi Vahid Khidhab. Katika kitabu hiki kunabainishwa na kukosolewa ngano kumi na itikadi zisizo sahihi kuhusiana na Israel. [92] Moja ya itikadi hizo zisizo sahihi ni kuwa sawa Uzayuni na Uyahudi na chuki dhidi ya Uzayuni na chuki dhidi ya Uyahudi maudhui ambayo imejadiliwa katika mlango wa tatu wa kitabu hiki na kutolewa hoja za kuonyesha kuwa sio sahihi. [93]
  • Islam Pezhohi Dar Israil: Mwandishi Akbar Mahmoudi. Katika kitabu hiki kumetambulishwa vituo muhimu zaidi, shakhsia, athari na uhakiki kuhusiana na utafiti kuhusu Uislamu na kuujua Uislamu huko Israel. [94]

Rejea

  1. Khomeini, Sahifa Imam, 1389 S, juz. 16, uk. 293

Vyanzo