Nenda kwa yaliyomo

Harakati ya Ansarullah ya Yemen

Kutoka wikishia
Ansarullah

Harakati ya Ansarullah ya Yemen (Kiarabu: أنصار اللّه اليمنية) au Wahouthi ni harakati ya kisiasa na kidini ya ya wafuasi wa madhehebu ya Zaydiya nchini Yemen ambayo ilianzishwa mnamo 1990 na kudhibiti sehemu ya ardhi ya nchi hiyo. Ansarullah inachukuliwa kuwa imeathiriwa na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na fikra za Imam Khomeini. Kuundwa kwa serikali ya Houthi kunachukuliwa kuwa ni muendelezo wa serikali ya Uimamu wa Zaidiya nchini Yemen, ambayo ilianzishwa katika karne ya tatu Hijria na kuendelea kwa zaidi ya miaka 1100.

Kukabiliana kwa harakati hii na Marekani na muungano wa serikali ya Yemen na nchi hii kulipelekea kutokea mapigano kati ya Ansarullah na serikali ya Yemen. Vuguvugu hili lilimpoteza mwanzilishi wake Hussein Houthi katika vita vya kwanza na serikali ya Yemen, lakini likapata mafanikio katika vita vilivyofuata. Sambamba na kuanza mwamko wa Kiislamu, Wahouthi waliweza kupata udhibiti wa Sana'a, mji mkuu wa Yemen. Saudi Arabia ililenga Ansarullah chini ya kivuli cha muungano wa Waarabu ili kudhibiti tena maeneo yaliyotekwa, ambayo yalishindwa kutokana na muqawama na kusimama kidete harakati hii.

Katika kukabiliana na mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza na mauaji ya raia wa Palestina, Ansarullah ililenga shabaha Palestina inayokaliwa kwa mabavu pamoja na meli za Israel katika Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden. Harakati hii iko kwenye orodha ya ugaidi ya Baraza la Usalama na baadhi ya nchi za Kiarabu na Marekani.

Wasifu na Nafasi

Ansarullah ya Yemen ni vuguvugu la kidini lenye mfumo wa kisiasa na kidini. [1] Madhehebu ya wanachama wa vuguvugu hili ni madhehebu ya Jaroudiyya, mojawapo ya madhehebu ya Zaidiyya, ambayo yanahesabiwa kuwa madhehebu ya karibu zaidi na Mashia Ithnaashariya. Harakati hii iliasisiwa kwa ajili ya kuendeleza utawala wa Uimamu wa Zaydiya uliokuwa umeanzishwa na Yahya bin Hussein, aliyekuwa na lakabu ya Al-Hadi ilal-Haq (aliyekufa: 298 AH) na iliendelea kwa zaidi ya miaka 1,100.[3]

Kiini cha mwanzo cha vuguvugu hili kilikuwa kikundi cha kitamaduni kilichoitwa Shabab Al-Muumin Association, ambacho kilianzishwa mwaka wa 1990. [4] Baada ya Hussein Badreddin al-Houthi kuwa kiongozi wa kundi hili, alianza shughuli yake ya kisiasa kwa kubadilisha jina na kuwa Kikundi cha Shabab Al-Muumin [5] na kuanzisha harakati zake za kisiasa. Harakati za kitamaduni za kikundi hiki ziliongezeka kati ya 1992 na 2004 na kuanza harakati zake za kijeshi. [6] Kutojali na kupuuza serikali ya wakati huo Yemen maeneo ambayo wakazi wake ni Wahouthi, ushawishi na upenyaji wa makundi ya Kisalafi na Kiwahabi na kuenea kwa fikra zao katika maeneo hayo, ambayo yalionekana kuwa tishio kubwa kwa Wahouthi, kumezingatiwa kuwa sababu ya kuundwa kwa kundi hili. [7] Kiwango cha idadi ya Wahouthi nchini Yemen kinatajwa kuwa takribani 40%. [8] Jina la Houthi, ambalo linatumika kwa vuguvugu hili na viongozi wake, linatokana na jina la mji unaoitwa Houth kusini mwa Sa'adah. [9]

Muundo wa Kitaasisi

Mbinu ya utawala ya Ansarullah ya Yemen inatokana na mbinu ya jadi ya Zaidiyya, utawala wa nasaba (wa kifamilia), na baadhi ya vyombo vya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vinazingatiwa katika fremu ya mfumo wa jamhuri. [10] Ansarullah ya Yemen ina asasina idara tatu za utekelezaji ambazo ziko chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa kiongozi wa harakati hii:

  • Baraza za Kisiasa: Hiki ni kitengo cha utekelezaji ambacho kina jukumu la kusimamia mahusiano ya harakati hii na makunbdi na vyama vingine vya kisiasa pamoja na jumbe za kidiplomasia na asasi za kieneo. Kinafanya tathmini, uchambuzi wa kisiasa na kutoa ripoti.
  • Baraza la Utendaji: Baraza hili linaundwa na vitengo vinavyohusiana na wananchi kama idara ya utamaduni malezi, idara ya kijamii, kitengo cha habari, masuala ya wanawake na mikoa.
  • Idara ya Kazi za Kiserikali: Kusimamia kamati za Ansarullah katika asasi za utekelezaji na kuandaa sera na sheria ni miongoni mwa majukumu ya asasi hii. [11]

Uhusiano na Iran

Badreddin Houthi alipokuwa nchini Iran

Harakati ya Ansarullah nchini Yemen inachukuliwa kuwa imeathiriwa na Imam Khomeini na mapinduzi yake, ambayo yaliletwa na Hussein Houthi kama kielelezo kwa watu wa Yemen. [12] Makabiliano ya harakati hii na Marekani na Israel yanazingatiwa kuwa yameathiriwa na fikra ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. [13] Iran inatambulishwa kama muungaji mkono wa kifedha na kijeshi wa Ansarullah ya Yemen. [14] Inasemekana kwamba wakati Badreddin Houthi alipokuwa nchini Iran, vijana wa Yemeni walipata mafunzo ya kijeshi, kiusalama na kidini nchini Iran. [15] Wapinzani wa Ansarullah ya Yemen, wanaitambua harakati hii kuwa nguvu ya Iran nchini Yemen. [16]

Vikwazo vya Kieneo na Kimataifa

Idadi kadhaa ya wanachama wa Ansarullah ya Yemen akiwemo Abdul-Malik al-Houthi mwaka 2014 na kuendelea walijumuishwa katika orodha ya vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Mnamo 2022, Baraza la Usalama lililiwekea vikwazo vya silaha Harakati ya Ansarullah. [17] Mwaka huo huo, Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Ndani wa mataifa ya Kiarabu, liliiweka Harakati ya Ansarullah ya Yemen katika orodha yake ya makundi ya kigaidi. Nchi nyingine, kama vile Marekani, zilitangaza vuguvugu hili kuwa kundi la kigaidi. [18]

Viongozi wa Ansarullah

Tangu Harakati ya Ansarullah ya Yemen ianzishe harakati zake mpaka kuunda serikali, imeongozwa na viongozi mbalimbali. Wafuatao ni baadhi ya viongozi hao.

Hussein al-Houthi

Makala asili: Hussein al-Houthi
Hussein Badreddin al-Houthi, kiongozi wa Ansarullah

Hussein al-Houthi ni mtoto wa Badreddin al-Houthi [19] ni muasisisi na kiongozi wa kwanza wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen. [20] Alikuwa mfuasi wa madhehebu ya Shia Zaidiyyah na akiwa ameathirika na fikra na mitazamo ya Imamu Khomeini, aliliweka suala la uadui dhidi ya Marekani na Israel katika nara zake na alibainisha kadhia ya Palestina kuwa ni katika masuala yanayopewa kipaumbele na yeye na harakati yake. Hussein al-Houthi aliauawa shahidi katika vita vya kwanza vya Wahouthi na serikali ya Yemen mwaka 2004. [21] Fikra na miatazamo yake ya kiitikadi ndio iliyopelekea kuanzisha Harakati ya Ansarullah. [22]

Badreddin al-Houthi

Makala asili: Badreddin al-Houthi

Badreddin al-Houthi alikuwa mmoja wa Marajii wa Shia Zaydiya; anatambuliwa kama Kiongozi wa Kimaanawi wa Harakati ya Ansarullah. [23] Akiwa pamoja na baadhi ya Maulamaa wengine wa Kizaydiya wa Yemen walisimama kukabiliana na upenyaji wa fikra za Kiwahabi. [24] Badreddin alikuwa muungaji mkono wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na alifahamika kuwa aliathirika na fikra za Imamu Khomeini (r.a). Kutokana na mashinikizo na vitisho vya Mawahabi, aliondoka Yemen na kuelekea Iran na kipindi fulani alibakia katika mji wa Qom. Uwepo wake huu, ukawa utangulizi wa kufahamu zaidi Ushia na Mapinduzi ya Kiislamu. [25]

Abdul-Mlaik al-Houthi

Makala asili: Abdul-Malik al-Houthi
Abdul-Malik al-Houthi, kiongozi wa tatu wa Ansarullah

Abdul-Malik al-Houthi ni kiongozi wa tatu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen, baada ya kaka yake Hussein na baba yake Badr al-Din, kufikia nafasi hii. [26] Kulingana na ripoti, alichaguliwa na babake kwa ajili ya kushika wadhifa huu. [27] Wengine wanasema kwamba uongozi wake kwa harakati ya Ansarullah ulianza mwaka 2010 (mwaka alioaga dunia Badr al-Din al-Houthi), [28] na wengine wanasema 2004 (mwaka ambao Hussein Houthi aliuawa) [29] na wengine wanasema 2006 [ 30].

Ushindi dhidi ya serikali ya Yemen, [31] kushindwa kwa mashambulizi ya muungano wa Waarabu dhidi ya Yemen yakiongozwa na Saudi Arabia, [32] shambulio la kombora la Ansarullah na ndege zisizo na rubani dhidi ya Israel na meli zake katika Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden [33] na kukabiliana na Marekani na Uingereza katika bahari hizi mbili ni miongoni mwa matukio ya wakati wa uongozi wa Abdul-Malik al-Houthi. [34]

Makabiliano ya Wahouthi na serikali ya Yemen

Harakati ya al-Houthi ilikuwa ikiitambua serikali ya Yemen kuwa kibaraka wa Marekani na kukosoa kuwepo kwa ubaguzi, umaskini, utegemezi wa serikali, na uingiliaji wa wageni katika masuala ya Yemen. [35] Baada ya tukio la Septemba 11 na mashambulizi ya Marekani dhidi ya Afghanistan na Iraq na uwepo wake wa kijeshi katika eneo na Ghuba ya Aden, harakati hii ilichukua msimamo dhidi ya Marekani [36] na kauli mbiu yao maarufu inayojulikana kama Sarkha ilipigwa dhidi ya Marekani na Israel. [37] Baadhi ya watafiti wanasema kuwa, kauli mbiu ya Sarkha dhidi ya Marekani ambayo mkuu wa serikali ya Yemen aliichukulia kuwa inamlenga yeye, pamoja na kushadidi harakati za kijeshi za harakati hiyo na kukataa kwa Hussein al-Houthi kutoa majibu kuhusu shughuli za harakati hiyo ndio sababu za kuibuka mapigano kati ya serikali ya Yemen na harakati hii na kutokea vita. [38] Makabiliano ya kijeshi ya Ansarullah ya Yemen na serikali ya nchi hiyo yalipelekea kutokea vita kadhaa:

  • Vita vya kwanza: Vita vya kwanza vya serikali ya Yemen dhidi ya Wahouthi vilipelekea kuuawa Hussein al-Houthi. Kuuawa wanajeshi watatu wa serikali na jaribio la kumkamata Hussein al-Houthi ni mambo yaliyotajwa kuwa sababu ya kutokea vita hivyo. Vita hivi vilifanyika katika mkoa wa Marran mnamo 2004. [39]
  • Vita vya pili: Kukataa kumaliza mivutano kulisababisha kutokea vita vya pili mnamo 2005 vilivyodumu kwa miezi miwili. Hatimaye, serikali ya Yemen ilitangaza ushindi na vita vikaisha. Wigo wa vita hivi ulikuwa mpana kuliko vita vya kwanza. [40]
  • Vita vya tatu: Mivutano iliyobakia ya vita ya pili ilisababisha kutokea vita vya tatu. Wigo wa vita hivi, vilivyoanza mwishoni mwa 2005 na kumalizika mwanzoni mwa 2006, ulipanuliwa hadi katika mji wa Saadah. [41]
  • Vita vya nne: Kuhamishwa kwa Wayahudi wa jimbo la Saadah na jaribio la kuanzisha serikali ya Kishia katika jimbo hili na Wahouthi kulipelekea kutokea vita vya nne. Wigo wa vita hivi, ambavyo vilifanyika mwaka 2007, uilienea mpaka nje ya mkoa wa Saadah. Vita hivi vilifikia tamati kwa upatanishi wa serikali ya Qatar. [42]
  • Vita vya tano: Vita hivi vilianza mwaka wa 2008 na vilihusisha majimbo ya Sana'a na Amran. Tangazo la upande mmoja la serikali la kusitisha mapigano lilipelekea kufikia mwisho vita hivi. [43]
  • Vita vya sita: Wahouthi walituhumiwa kuwateka nyara raia wa kigeni, na vita vya sita vikaanza Agosti 2009. Utumiaji mkubwa wa serikali wa mashambulizi ya anga na kuingia kwa Wahouthi katika ardhi Saudi Arabia na kuwaua wanajeshi wawili ni miongoni mwa sifa za vita hivi. Kuondoka kwa Wahouthi kutoka Saudi Arabia mnamo 2010 ndiko kulikokuwa mwisho wa vita hivi. [44]

Mwamko wa Kiislamu na Mapinduzi 2011

Maeneo yanayodhibitiwa na Ansarullah (rangi ya kijani)

Sambamba na kuanza mapinduzi ya mwamko wa Kiislamu katika baadhi ya nchi za Kiislamu, wananchi wa Yemen nao walianzisha harakati za kuipindua serikali na Wahouthi wakaitumia fursa hiyo. [45] Matokeo ya matukio hayo ikwa ni Wahouthi kuweza Machi 2011 kuudhibiti mji wa Saadah na kuchukua mamlaka na udhibiti wa mkoa huo. [46] Wahouthi walikuwa wakipinga mchakato wa makubaliano ya kisiasa na wakataa uchaguzi wa mapema wa rais na hawakumtambua Rais mpya aliyechaguliwa. [47] Baada ya Wahouthi kuungana na Ali Abdallah Saleh, mwaka 2014 waliudhibiti mji mkuu Sanaa. Mwaka 2017 Ali Abdallah Saleh kutokana na kufanya mazungumzo na muungano wa Saudia, alituhumiwa na Wahouthi kwa kufanya khiyana na akauawa katika mapigano na vikosi vya Wahouthi. [48]

Mapigano ya kijeshi na mataifa ya kigeni

Ansarullah ya Yemen imekuwa na mapigano ya kijeshi na nchi nyingi za kigeni, ambazo baadhi yake tunazitaja hapa chini:

= Mashambulio ya Saudi Arabia na Mataifa Yaliyounda Mungano Dhidi ya Ansarullah

Rais wa Yemen Abdu Rabbuh Mansour Hadi na Waziri Mkuu wake Khalid Mahfoudh Bahah walijiuzulu kutoka nyadhifa zao. [49] Kisha akaenda Aden na kuunda serikali ya muda. Mnamo Machi 26, 2015, muungano wa nchi za kikanda ukiongozwa na Saudi Arabia, kwa kumuunga mkono Mansour Hadi, ulianzisha mashambulizi makali ya anga na baharini dhidi ya Yemen, ambayo yaliharibu miundombinu mingi, vituo vya kijeshi na vya kiraia nchini Yemen. [50] Lengo la mashambulio haya lilikuwa ni kuyaondoa majimbo ya Yemen kutoka kwa udhibiti wa Ansarullah na kurejesha tena silaha za serikali kutoka kwa harakati hii. [51]

Baada ya mashambulizi ya anga ya muungano huo, awali Ansarullah ilichukua udhibiti wa maeneo tofauti ya Yemen ili kukabiliana na kundi la kigaidi la Al-Qaeda na vikosi vinavyoshirikiana na muungano huo. Baada ya takriban miezi miwili ya uchokozi wa muungano wa Saudia, kulifanyika operesheni kadhaa dhidi ya Saudi Arabia. Pamoja na upanuzi wa mashambulizi ya muungano, Ansarullah ya Yemen ilitumia makombora ya balistiki dhidi ya Saudi Arabia kwa lengo la kusimamisha mashambulizi. [52] Wahouthi walifanya mashambulio ya kijeshi mara kadhaa dhidi ya maeneo tofauti kwa kutumia makombora ya balistiki na ndege zisizo na rubani. [53]

Mashambulio dhidi ya Israel na Meli zake Kujibu Mashambulio ya Mabomu Dhidi ya Gaza

Katika kuunga mkono watu wa Gaza dhidi ya mashambulizi ya Israel, harakati ya Ansarullah ya Yemen ilichukua uamuzi wa kushambulia na kulenga maeneo mbalimbali ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa makombora na ndege zisizo na rubani. [54] Wahouthi pia walishambulia meli za Israel na meli zingine zilizokuwa zikielekea katika bandari za Israel (Palestina inayokaliwa kwa mabavu) katika Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden. [55] Marekani na Uingereza zilifanya mashambulizi kadhaa ya anga dhidi ya Ansarullah nchini Yemen, ambayo, kulingana na baadhi ya vyombo vya habari vya magharibi, hayakuweza kuwazuia Wahouthi kuendelea kutekeleza mashambulizi haya. [56] Hatua hii ya Ansarullah ilifanyika kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya Israel dhidi ya raia, maeneo ya makazi, na vituo vya matibabu huko Gaza na kuzingirwa kwa mji huu. [57] Mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yalifanywa kufuatia operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqswa (Oktoba 2023) iliyotekelezwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS). [58]

Rejea

Vyanzo