Nenda kwa yaliyomo

Mdahalo wa Imamu Ridha (A.S.) na Imran Sabi

Kutoka wikishia

Mdahalo wa Imamu Ridha (a.s) na Imran Sabi (Kiarabu: مناظرة الإمام الرضا (ع) مع الصابئة) Ni Mdahalo wa kihistoria na ni mojawapo ya mijadala muhimu ya kiakida kuhusiana na uwepo wa Mwenye Ezi Mungu na sifa Zake. Mdahalo huu uliwahusisha watu waili muhimu nao ni Imamu Ridha (a.s) na Imran Sabi’i, mwanazuoni maarufu wa wakati huo. Mdahalo huu ulifanyika kwa ombi la Khalifa wa Abbasiyya (Bani Abbas) aitwaye Maumun, ambaye alikusanya wanazuoni wakubwa kutoka dini mbalimbali, zikiwemo Ukristo, Uyahudi, Zoroastrianism (Umajusi), na Sabi’ina (Sabianism), ili kujadiliana na Imamu Ridha (a.s) kwa kina na busara.

Katika mazungumzo haya, Imran Sabi’i alizua maswali mengi yenye uzito kuhusiana na asili ya Mwenye Ezi Mungu, na Imamu Ridha (a.s) naye alijibu kwa ufasaha na ufahamu wa hali ya juu, akitumia mantiki na ushahidi wa kina kabisa. Majibu haya ya Imamu Ridha (a.s) yalimridhisha sana Imran Sabi’i, kiasi ya kwamba ilibidi akubaliane na Uislamu kwa kutamka shahada mbili na kuingia katika kusilimu. Hadithi hii, inayosimulia tukio hili muhimu, imeripotiwa na Sheikh Saduq katika vitabu vyake vya Tawhid na Uyunu Akhbar Al-Ridha, ambavyo vinaendelea kuwa ni rejeo muhimu kwa wanafunzi na watafiti wa masuala ya kidini. Mdahalo huu si tu kwamba unaonyesha umahiri wa Imamu Ridha (a.s) katika kujadiliana kwa hekima, bali pia unaakisi uwezo wake kielimu katika kujibu maswali magumu ya kiitikadi.

Muktadha na Vichochezi vya Kuundwa kwa Mdahalo

Mdahalo maarufu kati ya Imamu Ridha (a.s) na Imran Sabi, umeliohifadhiwa katika urithi wa Hadithi za Kishia, unafafanua jinsi Imamu Ridha (a.s) alivyohusika katika mjadala wa kina na wanazuoni kutoka dini mbalimbali. [1] Hadithi hii, iliyosimuliwa na Hassan bin Muhammad Naufali, inatoa mwanga juu ya mazingira ya kihistoria yaliyosababisha mdahalo huu muhimu. Hili lijiri pale Imamu Ridha (a.s) alipokuwa akielekea Marw kutoka mji wa Madina, ambapo Khalifa wa Abbasiyya, Maamun, Khalifa wa wakati huo alipoamua kuandaa mjadala wa kiakida ili kupima maarifa na hekima ya Imamu Ridha (a.s), akiwa mjini Marw. Katika maandalizi haya, Maamun alikusanya wanazuoni na wanaakida mashuhuri kutoka dini tofauti, wakiwemo Jathaliq, kiongozi wa Wakristo, Ras al-Jalut, kiongozi wa Wayahudi, pamoja na viongozi wa Wasabaiyya na Wazoroastria (Wamajusi). [2] Lengo hasa la Maamun lilikuwa ni kuanzisha mjadala wa kidini ambao ungeleta changamoto kwa Imam Ridha (a.s) mbele ya umma ulioko katika mjadala huo.

Baada ya matayarisho hayo, Maamun alimwalika rasmi Imamu Ridha (a.s) kushiriki katika mdahalo huo. Kwa unyenyekevu na ujasiri, Imamu Ridha (a.s) alikubali mwaliko huo na siku iliyofuata akahudhuria mbele ya Maamun na wanazuoni hao. [3] Katika mjadala huo, Imamu Ridha (a.s) aliwapa changamoto wanazuoni hao kwa hoja za kiakida na baada ya mjadala wa kina, aliwashinda kwa hoja zake zenye nguvu za kimantiki. [4] Baada ya kuwashinda wanazuoni wa Kikristo, Kiyahudi, na Kizoroastria, Imamu Ridha (a.s) aliigeukia hadhara na kutoa mwito kwa yeyote ambaye alikuwa na shaka na Uislamu aulize maswali yake bila woga. Hapo ndipo Imran Sabi’i, ambaye alikuwa amejadili dhana ya umoja wa Mungu na wanaakida wengi huko Kufa, Basra, Sham na visiwani kwa jumla (maeneo ya Tigris na Euphrates), bila kupata majibu ya kuridhisha, alipo nyanyuka. Alimwomba Imam Ridha (a.s) kujadiliana naye juu ya mada hiyo nyeti, na kwa moyo mkunjufu na hekima, Imam Ridha (a.s) alikubaliana na ombi hilo. [5] Mdahalo huu unafahamika kama mojawapo ya midahalo muhimu zaidi katika historia ya Kishia, ukidhihirisha umahiri wa Imamu Ridha (a.s) katika kueleza na kutetea misingi ya imani ya Kiislamu kwa njia ya hoja za kiakili na za kidini.

Maswali ya Imran Sabi

Katika mdahalo wa Imam Ridha (a.s) na Imran Sabi, Imran aliuliza maswali mengi kuhusu Mungu, baadhi ya ambayo ni kama ifuatavyo:

  • Ni kitu gani cha kwanza kuwepo kabla ya kuwepo kitu chochote? [6]
  • Je, kitu hicho kinajitambua, kupitia hudhurio lake ndani yake mwenyewe? [7]
  • Uumbaji wa Mungu ni wa namna gani na nini maana ya kuumba na kuna aina ngapi za kuumba? [8]
  • Je, uumbaji wa Mungu huleta mabadiliko fulani ya hali ya Mungu? [9]
  • Kitu gani kitacho tuwezesha kuelewa uwepo wa Mungu? [10]
  • Mungu ni nini? [11]
  • Je, Mungu yupo ndani viumbe au viumbe viko ndani Yake? [12]
  • Je, umoja wa Mungu unajulikana kwa kuelewa asili Yake au kwa kuelewa sifa Zake? [13]
  • Mungu yuko kwenye kitu gani? Je, kuna kitu kinachomzunguka? Na je, Anaweza kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine? [14]

Matokeo ya Mdahalo

Kwa mujibu wa Hadithi iliyosimuliwa na Hassan bin Muhammad Naufali, baada ya Imamu Ridha (a.s) kutoa majibu ya kina kwa maswali yote ya Imran Sabi’i, Imran alihisi kuridhika na kuamua kukubali maelezo ya Imamu Ridha kuhusiana na uwepo wa Mwenye Ezi Mungu. Jambo lilipelekea kubadili imani yake kwa kutamka shahada mbili na kuingia katika Uislamu. Katika hatua inayofuata, Imamu Ridha (a.s) aliridhika na silka za Imran, na kwa heshima kubwa alimwalika nyumbani kwake kwa ajili ya chakula cha usiku. Aidha, alimtunuku mavazi mapya, kipando cha kusafiria, na dirhamu elfu kumi kama ni zawadi ya kwa ajili yake. [15]

Kwa mujibu wa simulizi hii, baada ya mdahalo huo, Imran Sabi’i alikabiliwa na wanazuoni wa dini mbalimbali, walikuwa wakimtembelea na kujadili naye juu ya masuala ya kidini. Imran alithibitisha umahiri wake katika mijadala hiyo kwa kuendelea kushinda mmoja baada ya mwengine. Katika hatua nyingine, Khalifa Maamun alitoa dirhamu elfu kumi kwa Imran kama ni ishara ya kuthamini mchango wake, na Imamu Ridha (a.s) akamteua Imran kuwa ni msimamizi wa sadaka katika eneo la Balkh. [16]

Vyanzo vya Hadithi

Maelezo ya mdahalo yaliporipotiwa kwa mara ya kwanza na Sheikh Saduq (aliyeishi kati ya 305 na 381 Hijria) katika vitabu vyake vya Tawhidi [17] na Uyunu Akhbar Al-Ridha. [18] Ahmad bin Ali Tabarsi, aliyeishi katika karne ya sita Hijria, alifupisha kisa hichi katika kitabu chake Al-Ihtijaj. [19] Aidha, Allama Majlisi amekinukuu kisa hichi katika kitabu chake Bihar al-Anwar, ila ni kunukuu kutoka vitabu hivyo viwili vya Sheikh Saduq. [20]

Uhalali wa Sanad (Hati) ya Hadithi

Wataalamu wa elimu ya rijali (wajuzi wa elimu ya nasaba za wapokezi wa Hadithi) wana mitazamo tofauti kuhusiana na mnyororo wa wapokezi wa Riwaya hii. Baadhi yao wanawakubali wapokezi wote na kudai kuwa ni waaminifu, huku wengine wakiwahesabu baadhi yao kuwa si waaminifu (madhaifu). [21] Aidha, sanad ya Hadithi hii ni mursal, ambayo inamaanisha kwamba baadhi ya wapokeza wa mnyororo wa wapokezi wake hawajatajwa. Jambo linaloifanya Hadithi hii kuwa ni dhaifu kwa upande wa sanad. [22] Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wanaamini kwamba licha ya udhaifu katika sanad yake, ila bado Hadithi hii inakubalika. Hii ni kwa sababu Sheikh Saduq ndiye aliye inukuu Hadithi hii, na yeye alikuwa hanukuu Hadithi, ila baada ya kuwa na uhakika kwamba zinatoka kwa Maasumina. [23]

Matini ya Riwaya na Tafsiri yake

Imam Al-Ridha (a.s.) akasema: "Enyi watu, ikiwa kuna mmoja yenu anaye pinga Uislamu na anataka kuuliza, basi na aulize bila ya kuona haya." Hapo, Imran al-Sabi’i alisimama, akiwa ni mmoja wa wajuzi wa theolojia, na kusema: "Ewe mwerevu kuliko wengine, kama usingealiomba maswali, nisingeweza kukuuliza maswali yangu. Nimeingia miji kadhaa ikiwemo; Kufa, Basra, Shamu, na visiwani (maeneo ya Tigris na Euphrates), na nimekabiliana na wanatheolojia kadha wa kadha, ila sikupata mtu anayeweza kunithibitishia uwepo wa Mungu usio na mwenza, ulio simama bila kuhitaji kitu katika uwepo wake. Je, unaweza kunipa ruhusa ya kuuliza maswali?"

Imamu Al-Ridha (a.s) alimjibu Imran al-Sabi na kusema, "Ikiwa Imran al-Sabi yupo miongoni mwa watu hawa, basi ni wewe." Imran akasema, "Ndio, ni mimi." Imamu akamwambia, "Uliza, ewe Imran, lakini uwe na msawa na mwenye isafu na wala usipotoshe au kudhulumu." Imran akasema, "Wallahi, ewe bwana wangu, sikusudii chochote isipokuwa nataka unithibitishie jambo ambalo nitaweza kulishikamana nalo bila kuwa na njia ya kulipinga." Imamu akasema, "Uliza ulitakalo." Watu wakaanza kujikusanya na kukaribiana zaidi. Imran al-Sabi akauliza kwa kusema: "Nipe habari za wa kwanza kuwepo na kile alichokiumba."

Imamu Al-Ridha (a.s) alimjibu Imran na kusema, "Umeuliza, basi elewa. Ama kuhusiana na Yule Mmoja (Mwenyezi Mungu), Yeye ni Mmoja daima, hakikuwepo kitu chochote pamoja naye, yupo bila mipaka na wala sifa za ziada. Na atabaki hivyo milele. Kisha aliumba viumbe tofauti, wenye sifa na mipaka mbalimbali, hakuumba viumbe hivyoa kwa hakuviegemeza kwenye kitu fulani, wala kuvitumbukiza kwenye kwenye kitu chenye mipika fulani, wala hakuviweka juu kitu vikazungukwa na kitu hicho, na wala hakuiga kutoka mahala fulani katika uumbaji wake.

Na baada ya hapo, Mwenyezi Mungu aliumba viumbe kwa namna na mitindo tofauti, vikiwemo aina safi na visizo safi, vyenye tofauti na vinavyo fanana, pia aliumbarangi na ladha tofauti. Alifanya hivyo bila ya kuwa na haja yoyote kwao au kwa sababu ya kutaka kufikia daraja au nafasi fulani kupitia uumbaji huo. Wala uumbaji huo, haukumletea ziada wal mapungufu yoyote ndani yake. Je, unaelewa hayo? Imran Alijibu, "Ndio, naapa kuwa nimeelewa, ewe bwana wangu".

Imamu aliendelea kumwabia; Pia fahamu ya kwamba ingekuwa Mwenye Ezi Mungu ameumba viumbe kwa sababu ya mapungufu haja au kwa kuwa anavihitajia viumbe hivyo, basi angeliumba tu vitu ambavyo angeweza kutumia katika kutimiza mahitaji yake. Na pia, katika hali hiyo, ingefaa aumbe mara nyingi zaidi ya vile alivyoumba; kwani kadiri msaada na wasaidizi wanavyokuwa wengi, ndivyo mtu anavyokuwa na nguvu zaidi. Na pia, katika hali hiyo, mahitaji yasingekoma; kwani kila uumbaji unavyo endelea kukuwa ndivyo mahitaji yanavyo kuwa makubwa zaidi. Na kwa sababu hiyo, nasema: viumbe havikuumbwa kwa sababu ya mahitaji ya Mola. Bali, uumbaji viumbe, ni uhamishaji wa Mwenye Ezi Mungu kutoka hali moja kwenda nyengine, huku akivipa viwango tofauti vya utukufu kati yavyo, bila ya kuwa na haja ya kile kilicho bora zaidi miongoni mwavyo, wala kilicho chini hakukiweka chini kwa kutaka kulipiza kisasi dhidi yake. Hii ndiyo sababu ya uumbaji wake.

Imran aliuliza: "Je, Muumba huyo ambaye ni Mwenye Ezi Mungu, aliitambua dhati kake mwenyewe binafsi yake?"

Imamu (a.s) alijibu kwa hekima na busara: "Hakika, elimu na ufahamu wa kitu chochote hujengwa juu ya kutofautisha kati ya vitu viwili, na ndio sharti ya kutambulika kwa uwepo wake. Katika kipindi kile cha kabla ya uumbaji, kulikuwa na uwepo wa Mwenye Ezi Mungu pekee, bila kitu kingine chochote cha kuweza kufanyiwa ulinganisho au tofauti. Hivyo basi, hapakuwa na haja ya kuwepo kwa tofauti au umuhimu wa utambuzi wa kila kimoja kwa ajili ya kuthibitisha uwepo wake. Hapo awali kulikuwa na uwepo mtupu, usio na mipaka, ambapo hakukuwa na kitu chochote cha kutofautisha mipaka ya kila kimoja. Je, umeelewa, Imran?"

Imran alijibu kwa unyenyekevu: "Ndiyo, ewe bwana wangu. Basi sasa niambie, kwa njia gani Mwenye Ezi Mungu alijua kile alichokijua? Yaani, kwa chombo gani alitambua kile alichokijua? Je, ilikuwa ni kwa kupitia dhamira au kuna kitu kingine tofauti na hicho?"

Imamu alijibu kwa hekima akimwambia: “Iwapo elimu ya Mwenye Ezi Mungu ingeweza kufikiwa kupitia 'dhamira' (ambayo ni ile sura inayopatikana katika fikra), je, hivi kuna uwezekano wa kuweka mipaka kwa ajili ya kutambua hiyo 'dhamira'?"

Imran alijibu kwa ukweli: "Hapana, haiwezekani."  Imamu akaendelea kwa ufasaha zaidi: "Hivyo basi, hiyo 'dhamira' ni nini hasa?" Imran, akiwa katika hali ya kutafakari, hakuweza kutoa jibu.

Imamu aliendelea kusisitiza: "Hakuna tatizo katika kutojua. Sasa, ikiwa nitakuuliza kuhusu 'dhamira' hiyo kuwa je hivi kuna uwezekano wa kuitambua kwa kutumia 'dhamira' nyingine? Ukisema ndiyo, basi utakuwa umekanusha madai yako mwenyewe, ewe Imran. Je, si sahihi kusema kwamba huyo 'Mmoja' au 'Dhamira' haielezeki? Na si kweli kwamba hueleweka kupitia matendo yake, jee kitu kingine kinaweza kusemwa na kudhaniwa juu yake? Jee kweli ni haki kumdhania Yeye, dhana zinazo shikamana na pande au sehemu mbalimbali kama wanavyo weza kufikiriwa viumbe? Hivyo basi, elewa vizuri jambo hili na weka maarifa yako juu ya msingi huo sahihi."

Imran aliuliza kwa kina: "Je, unaweza kunifahamisha kuhusiana na mipaka ya uumbaji wa Mwenye Ezi Mungu, maana yake, na aina zake?" Imamu alijibu kwa hekima kwa kumfafanulia akisema: "Umeuliza swali lenye uzito, sasa zingatia vizuri ili uelewe vyema: Mipaka ya uumbaji wa Mungu inahusisha aina sita. Kwanza, kuna vile vinavyoweza kuguswa, kupimwa uzito, na kuonekana. Pili, kuna kitu kisichokuwa na uzito ambacho ni roho. Tatu, kuna aina nyingine inayoweza kuonekana lakini haina uzito, haiwezi kuguswa wala kuhisiwa, haina rangi wala ladha, haina ukubwa, umbo, au sura. Na miongoni mwa haya yote kuna matendo na harakati zinazounda vitu, na kuvibadilisha kutoka hali moja kwenda nyingine, kuongeza na kupunguza; lakini matendo na harakati hizo hupita bila kuwa na muda zaidi ya inavyohitajika kwa ajili yake. Kwa hivyo, wakati kitendo kinapokamilika, kinaondoka na kupotea, lakini athari yake hubaki, sawa na jinsi maneno yanavyotamkwa na kuondoka huku athari yake ikibaki."

Imran, akichochewa na jibu hilo la kina, akauliza: "Ikiwa Muumba ni 'Mmoja', na hakuna kitu kingine chochote zaidi yake, wala hakuna kilicho simama sambamba naye. Sasa je, uumbaji wa viumbe hivhyo hautambadilisha?" Imamu alijibu kwa busara: "Uwepo wa Mwenye Ezi Mungu ni wa tangu, na wala Yeye habadiliki kwa kuumba viumbe hivyo; lakini viumbe hubadilika kwa jinsa ya matakwa ya Mungu yanavyo wabadilisha. Ila Yeye hubaki kuwa Mmoja, wa milele, bila kubadilika, huku viumbe wake wakiendelea kubadilika na kufuata mpangilio wake wa kimaumbile."

Imran aliuliza: "Sisi tumemjua Mungu kwa kupitia njia gani?" Imamu alijibu kwa uwazi: "Kupitia vitu vingine tofauti na Yeye Mwenyewe." Imran akauliza kwa hamu: "Ni vitu Hivyo?" Imamu akajibu kwa ufasaha: "Ni matakwa Yake, jina Lake, sifa Zake, na vitu vyengine vinavyohusiana na hivyo. Vyote hivi ni viumbe vilivyoumbwa na kupangwa kupitia mipango ya Mungu."

Imran akaendelea na maswali: "Yeye ni nani hasa?" Imamu alijibu kwa kina: "Yeye ni nuru, maana yake ni kwamba anawaongoza viumbe wake wote, iwe ni wa mbinguni au wa ardhini. Kwa upande wangu, hakuna haja wala wajibu wa kueleza zaidi isipokuwa kuthibitisha umoja Wake."

Imran, akiwa na mashaka, akauliza: "Je, si kweli kwamba kabla ya uumbaji, Mungu alikuwa kimya, kisha akaanza kusema?" Imamu alijibu kwa mtindo wa tafakuri: "Kimya kina maana pekee yake pale ambapo kuna maneno yaliyotangulia, na hivyo, kimya hakiwezi kuwa na maana ya mazungumzo au hali yoyote ya kiakili bila kuwepo kwa vitu vya awali." Kwa mfano, hawezi kusemwa kwamba taa imekuwa "kimya." Hali kadhalika, hatuwezi kusema kuwa taa "imeangaza" kwa maana kwamba mwangaza na kung'aa si sifa ya taa yenyewe, na si sawa kuihisabu sifa hiyo kuwa ni miongoni mwa matendo ya taa hiyo. Kwa hiyo, tuanapo angazwa ndipo tunaposema kwamba taa inatupa mwangaza, na tunamaanisha kwamba mwangaza umeenea kwetu kutoka katika taa hiyo, na sisi tumepokea mwangaza huo. Hivyo, kwa kutumia mwangaza huo, unaweza kuona vitu vizuri na kupata ufahamu zaidi katika shughuli zako.

Imran alisema: "Nilidhani kwamba Muumba, kuumba viumbe kunakoleta mabadiliko ndani ya kazi Zake, humbadilisha kutoka katika hali moja kwenda nyengine." Imamu alijibu kwa kusema: "Unadhaniaje  jambo ambalo haliwezekani, iweje Muumba abadilike, haiwezekani Yeye kubalidilika bila kuwepo kitu kitakachombadilisha. Je, umewahi kuona moto ukijibadilisha wenyewe? Au umewahi kuona joto likijichoma wenyewe? Au umewahi kuona mtu mwenye kuona akaliona jicho lake mwenyewe?" Imran alijibu kwa uaminifu: "Hapana, sijawahi kuona."

Imran akaendelea kwa kusema: "Sasa, naomba unifafanue: Je, Muumba yumo ndani ya viumbe, au viumbe vimo ndani Yake?" Imamu (a.s) akamjibu: "Yeye ni zaidi ya hayo. Siyo kwamba Yeye yupo ndani ya viumbe wala viumbe haviko ndani Yake. Bali Yeye amezikiuka hali zote." Kisha aliongeza akisema: "Nitakufafanulia kwa msaada na nguvu za Mwenye Ezi Mungu."

Imamu akmtaka Imran atoe jawabu akimwambia: "Niambie, je, wewe uko ndani ya kioo au kioo kiko ndani yako? Ikiwa hakuna hata mmoja wenu aliye ndani ya mwingine, jinsi gani unaweza kujiona kwenye kioo?" Imran alijibu: "Kupitia mwangaza ulioko kati yangu na kioo." Imamu akaendelea kumuuliza: "Je, unaweza kuona mwangaza huo kwa njia yoyote nyingine zaidi ya jinsi unavyo uona kwa macho yako kwa kupitia kioo?" Imran alithibitisha akisema: "Ndiyo, nauona." Imamu akasema: "Tuoneshe sisi jinsi unavyo uona mwangaza huo." Imran hakutoa majibu.

Imamu akaendelea kumwambia: "Kwa mtazamo wangu, mwangaza bila ya kuwemo ndani ya mmoja wenu, umeweza kukufanyeni kila mmoja kumuona mwenziwe. Hii ni mfano mwingine ambao wajinga hawawezi kuelewa. Suala la Mungu liko juu zaidi ya mfano huu niliokupa”. Hapo Imamu akageukia upande wa Maamun na kusema: "Wakati wa sala umewadia."

Imran alizungumza kwa unyenyekevu akasema: "Bwana wangu, tafadhali usikatishe maswali yangu. Moyo wangu umekuwa mwepesi kutokana na majibu yako. Imamu (a.s) alijibu: "Tutasali sala zetu kisha tutarudi tena kwenye majadiliano yetu." Baada ya hapo, Imamu aliinuka, na Mamun naye akaondoka. Iamamu (a.s) akasimama kwa ajili ya sala na watu nao wakasimama nyuma ya Muhammad bin Jaafar wakasali jamaa huku Imamu akiwa ndani na watu wengine wakiwa nje ya eneo hilo. Kisha Imamu akarudi mahali pake na kumuita Imran, akamwambia: "Weka wazi maswali yako."

Imran akauliza: "Tafadhali nieleze: Je, umoja wa Mungu unaweza kueleweka kwa kupitia dhati Yake au ni kwa kupitia sifa na alama zake?" Imamu akamjibu: "Mungu, Muumba mmoja, ndiye yule aliyepo tangu na tangu, daima ni mmoja na hana mwenza. Yeye ni mmoja na wala hapana mwingine sambamba naye. hadirikiki wala si kwamba hatambuliki, si mwenye ampuli moja wala mwenye sampuli tatanishi. Yeye si kumbukumbu iliomo akilini wala msahauliwa wan je ya akili, na si kitu ambacho jina la kitu ambacho jina la kitu chengine limo ndani yake. Si kwamba uwepo wake umeanza wakati maalum katika kuwepo kwake, na wala si wa kuambiwa atasalia hadi wakati maalum, wala si mtegemea kitu chengine au kwamba uwepo umeenea hadi kufikia mpaka wa kitu chengine. Hakufichika katika kitu chengine pembeni yake, hayo yote ni kabla ya uumbaji wa viumbe vyake; kwa kuwa hakukuwa na kitu kingine kando yake kabla uumbaji wake, sifa yoyote unayoinasibisha kwake ni sifa unayoizua na kuitengeneza na ni tafsiri inayo kusaidia kuelewa umoja wake."

Pia, elewa ya kwamba uanzilishi (uumbaji), matakwa, na jaala (irada) ni majina matatu ya kitu kimoja; na uumbaji au uanzilishi wa kwanza kabisa, ambayo ni jaala (irada) na matakwa yake, vilikuwa ni herufi alizo ziweka kama asili na msingi wa kila kitu na ndiyo mwongozo kwa kila chenye kufahamika na ni mwangaza kwa kila jambo lenye utata. Kwa kupitia herufi hizo, kila kitu, iwe ni haki au batili, kitendo au kitendwa, chenye maana au kisicho na maana, hutenganishwa na kufahamika, na mambo yote yamekusanywa juu ya herufi hizo. Katika uumbaji wa herufi hizi, hakukuwekwa maana wala uwepo wenye vipimo vyenye mipaka maalumu, isipokuwa uwepo wake binafsi, kwa sababu uwepo wao ulianzishwa kwa mfumo wake anzilishi, na nuru, hapa, ndiyo kitendo cha kwanza cha Mwenye Ezi Mungu; Mungu ambaye Yeye mwenyewe ni nuru ya mbingu na ardhi, na herufi hizo zilitoka katika ulimmwengu fikirika zikaingia katika ulimwengu wa vitendo, herufi hizo ndiyo msingi wa maneno, na ibara zote ni za Mungu alizwafundisha viumbe wake. Herufi hizi ni thelathini na tatu: ishirini na nane kati yao zinaashiria lugha (lahaja) za Kiarabu. Kati ya herufi ishirini na nane, ishirini na mbili zinaashiria lugha za Kisiria (Syriac) na Kiebrania. Kati ya herufi hizo, tano zinapatikana katika lugha mbalimbali za watu wa ngeni zisizohusiana na lugha tatu za mwanzo, zitumiwazo katika maeneo tofauti, lugha hizo zimesambaa na kuenea maeneo mbali mbali. Na hizo ni herufi tano zilizotenganishwa na herufi ishirini na nane, hivyo kufanya idadi ya herufi kuwa thelathini na tatu. Na hizi herufi tano, kwa sababu maalum, hazifai kuzungumzwa zaidi ya vile tulivyoeleza. Kisha Mwenye Ezi Mungu alizifanya herufi hizo kuwa ni "kitendo" chake baada ya kuzihesabu na kuzipangia mipango maalumu, kama ilivyo katika Aya takatifu isemayo: (Kun faya kun ; کنْ فَیکونُ), (Nayo ni kauli ya Mungu isemayo “kuwa” na papo hapo kitu huumbika na kutokea). "Kun" ni sifa na uumbaji wa Mungu, na kile kinachozalishwa kutokana na kauli ya “Kun” ni kitendo na ni kiumbe. Uumbaji wa kwanza wa Mungu Mtukufu ni uanzilishi, ambao hauna uzito wala mwendo, hausikiki, hauna rangi, wala hauhisiwi. Kiumbe wa pili ni herufi ambazo hazina uzito wala rangi, ila zinaweza kusikika na kusifika, lakini haziwezi kuonekana. Kiumbe wa tatu ni kitu kihisiwacho kwa hisia zote, kinachoweza kuonjeka na kuonekana. Mwenye Ezi Mungu Mtukufu alikuwapo kabla ya uumbaji wake, kwa sababu kabla ya Mungu Mtukufu hapakuwa na mwengine aliye pamoja naye, na hakuna kitu chengine kilichokuwepo sambamba naye. UUmbaji wake ulikuwepo kabla ya herufi, na herufi hazionyeshi kitu chengine isipokuwa zinajidhihirisha zenyewe tu.

Hapa Maamun aliuliza: Je, inawezekanaje kwamba herufi hizo ziwe hazionyeshi kitu chengine isipokuwa zenyewe tu? Imamu alijibu: Kwa sababu Mungu Mtukufu huzifnay kuwa na uwezo wa kuashiria maana fulani. Kwa mfano pale Mungu anapozikusanya herufi kadhaa, kwa mfano herufi nne au tano au sita au zaidi au chache zaidi, huwa ni kwa ajili ya maana mpya iliyoanzishwa ambayo haikuwepo hapo awali.

Imamu alipojibu swali la Maamun, Imran, aliuliza akisema: “Vipi sisis tunaweza kutambua kwa undani zaidi juu ya suala hili?” Imamu naye akamwambia: “Ili kuelewa jinsi herufi zinavyofanya kazi, ni muhimu kutambua kwamba kila herufi isimamayo peke yake, huwa haina maana kamili zaidi ya kuwa ni alama ya maandishi tu. Alisema, "Kwa mfano, unapotamka herufi moja baada ya nyingine kama vile; 'ا، ب، ت، ث، ج,' herufi hizi zikiwa zimesimama peke yakee huwa hazina maana yoyote ile zaidi ya kuwa ni alama za maandishi zinazojitegemea."

Hata hivyo, Imamu (a.s) aliendelea kufafanua kuwa, unapozichukua herufi hizi na kuziunganisha kwa mpangilio maalum ili kutengeneza neno au jina, hapo herufi hizi huanza kubeba maana maalum inayohusiana na neno au jina hilo. Hii inamaanisha kuwa, herufi zinapounganishwa kwa usahihi, zinaweza kuunda neno lenye maana, ambalo linaweza kuwakilisha kitu, dhana, au sifa fulani.

Imamu aliongeza kuwa, herufi hizo zinapopangwa kwa utaratibu fulani, zinaweza kuonesha jina au sifa ambayo huashiria kitu au dhana maalum. Kwa maneno mengine, herufi hizi, zikijumuishwa pamoja kwa namna maalum, zinapata uwezo wa kubeba na kutoa maana fulani; lakini, kila herufi ikiwa peke yake, haina maana yoyote zaidi ya kuwa ni alama tu.

Baada ya maelezo haya, Imam alimgeukia Imran na kumwuliza, "Je, umeelewa?" Naye akajibu “Ndio”

Imamu akendelea kufafanua kuhusiana na sifa na majina ya Mwenye Ezi Mungu, akasema kwamba: “Sifa haziwezi kuwepo bila ya kuwepo msifiwa wa sifa hizo, na jina haliwezi kuwepo bila maana ya jina hilo. Hivyo, sifa na majina ya Mwenye Ezi Mungu zinabeba maana ya ukamilifu na uwepo wake, lakini sio kama vile sifa ziashiriazo mipaka ya vitu ambavyo vinaweza kupimwa au kufafanuliwa kwa njia za kawaida kama vile; umoja, wingi, uzito, rangi, pembe nne, uwili, utatu, usita n.k.  Kwani hizo ni sifa za kimaada, kwa hiyo haziwezi kutumika katika kuelezea au kuhimili welewa wa dhana ya Mwenye Ezi Mungu.

Imamu aliendelea kusema kwamba: “Majina sifa na za Mungu zinaonesha uhusiano na ukamilifu wake, na kwa kupitia sifa na majina hayo, watu wanaweza kumfahamu Mungu. Hata hivyo, Mungu mwenyewe hawezi kueleweka kikamilifu kwa kutumia njia za kimaada kama vile kumuona kwa muono wa macho au kumhisi kwa mguso wa mikono. Ila yeye hufahamika kwa kupitia dalili na ishara hizi za sifa na majina Yake. Imamu aliendelea kufafanua kwa undani zaidi na kusema kwamba; hakuna kitu chochote miongoni mwa viungo vya hisia kama vile; kuona, kusikia, au kugusa, kinachoweza kumwelezea au kudiriki Mwenye Ezi Mungu kikamilifu. Mungu ametakasika na ni mtakatifu alioje, na hawezi kupimwa au kueleweka kikamilifu na viumbe kwa kutumia vipimo vya akili zao, au kwa kutumia vigezo vya kidunia na kimaada. Nalo hili halihitaji hoja, kwani ni jambo lililo wazi kabisa. Kwa hiyo sifa za Mungu ni vielelezo vinavyomwongoza mtu kwenye welewa wa kumtambua Mwenye Ezi Mungu. Hivyo basi yeye hueleweka kupitia majina yake, na kupitia viumbe vyake tunaweza kusimamisha hoja juu ya uwepo wake. Tunaweza kusimamisha hoja tosha kwa yule mwenye kiu ya kumwelewa Mola wake, na wala hatakuwa na haja ya kutumia hisia zake za kimwili kama vile; kumuona kwa macho, kumsikia kwa masikio, kumgusa kwa mikono yake au kumzunguka Mola wake kinaga ubaga kupita moyo na roho yake. Na kama mjina na sifa zake zisigekuwepo katika kuashiria uwepo wake, basi waja wake wasingekuwa na uwezo wa kumwelewa Mola wao. Waja mwamuabudu Mola wenu kupitia sifa zake kama ni ashirio lake yeye, na kama mngelikuwa mnaabudu maana za sifa hizo, basi mngelikuwa hamumuabudu Allah ambaye ni Mmoja tu. Kwani sifa zake ni tofauti na Yeye mwenyewe, jee umeelwa? Imran akajibu “Ndio nimeelewa, lakini fafanua kwa mapana zaidi.” Hapo Imamu akasema: "Usije ukajaribu kusema maneno ya wapumbavu waliopotoka na wasio na nuru nyoyoni mwao; ambao wanadhani kwamba Mwenye Ezi Mungu yupo kwa ajili ya kutoa thawabu na adhabu Siku ya Kiama tu, na wala hayupo duniani humu kwa ajili ya kutiiwa na kutoa matumaini kwa waja wake. Na kama uwepo wa Mungu usingekuwa na faida duniani humu isipokuwa kuzidisha matatizo na mapungufu kwa waja wake! Basi hata huko Akhera pia asingekuwepo (asingekwa na faida yoyote). Lakini wale wenye mawazo kama hayo wamepotea njia, na wamekuwa vipofu na viziwi kuhusiana na haki, bila ya wao wenyewe kujua kwamba wako katika hali hiyo. Aya ifuatayo ni yenye kuthibitisha jambo hili: ‘Na aliye pofu ulimwenguni humi, basi hata Akhera pia ni kipofo, na aliyepotea njia zaidi’ (Suratu Al-Isra, Aya ya 72)."

Pale Aya inapotaja upofu, haimaanishi upofu wa macho bali ni upofu wa kuto ona ukweli. Wenye hekima wanatambua kwamba haiwezekani kusimamisha hoja juu ya uwepo wa ulimwengu wa Akhera isipokuwa kwa kupitia yale yanayoonekana ulimwenguni humu. Na mtu yeyote anayejaribu kuelewa Akhera kwa mawazo yake mwenyewe, bila mwongozo wa ulimwengu huu, huyo atakuwa anatengana na ukweli halisi katika kuielewa Akhera. Hii ni kwa sababu Mwenye Ezi Mungu ameiweka elimu ya utambuzi wa Akhera mikononi mwa wenye akili, elimu, na ufahamu.

Imran akauliza: "Je, tende la uumbaji lenyewe ni kitu kiumbe asu si kiumbe?" Imamu akajibu: "Ni kiumbe tulivu ambacho hakiwezi kueleweka kutokana na utulvu wake. Kwa hiyo, ni kiumbe kwa sababu ni kitu kilichozaliwa na kuumbwa na Mwenye Ezi Mungu, na hivyo kikawa kiumbe. Kwa maneno mengine, kuna aina mbili tu za uwepo; uwepo wa Mwenye Ezi Mungu na uwepo wa viumbe vyake, na hakuna kitu cha tatu katikati. Kila kitu kilicho umbwa na Mwenye Ezi Mungu, hakiwezi kukwepa hali ya ukiumbe. Uumbaji (viumbe) wa Mwenye Ezi Mungu ima; tulivu au sio tulivu (vinavyo badilika badilika), ima tofauti au sawa (vifananavyo), kinachojulikana au kisichojulikana. Chochote kinachoweza kupimika, ni kiumbe cha Mwenye Ezi Mungu Mtukufu. Tambua kwamba chochote kiundwacho na fahamu zako, ni maana inayoweza kueleweka kupitia hisia, na kila hisia inaonesha kitu kile kile ambacho Mwenye Ezi Mungu amekiwekea uwezo wa kueleweka. Kisha elewa ya kamba; ufahamu unatoka moyoni. Na elewa ya kwamba; Yule Mwenye Ezi Mungu, ambaye ni mmoja na anayeendelea kuwepo, hana vipimo wala mipaka. Yeye ameumba kiumbe chenye vipimo na mipaka maalumu. Na kile kilicho umbwa na Mungu kiuhalisia ni vitu viwili: kipimo na kitu chenye kipimo, na kauna hata kimoja kati yavyo chenye rangi wala uzito na wala haviwezi kuonjeka, ns kila kimoja alikifanya kuwa ni njia ya kuelewa kingine, kisha vyo viwili akaviweka katika hali ya kueleweka bila ya kuhitaji kitu chengine kwa ajili ya kuvielewa vitu hivyo. Hakuuumba kitu chochote kama kitu kimoja, chenye kujitegemea wenyewe, bali alitaka vitu hivyo view ni hoja na ishara iashiriayo kuthibitisha uwepo wake. Mwenye Ezi Mungu ni mmoja na pekee. Hana mwenze ambaye angeliweza kumsaidia, kumlinda au kumuhifadhi. Hata hivyo, viumbe kwa idhini na mapenzi ya Mwenye Ezi Mungu, vinahifadhiana na kulindana vyenyewe kwa wenyewe. Watu wamehitilafiana juu ya suala hili, na hadi walipoangukia katika fadhaifu na kupotea, kisha wakajaribu kutoka kwenye giza kwa kutumia giza, kwa sababu wao walimpachika Mwenye Ezi Mungu kwa sifa zao za kibinadamu, na hivyo badala ya wao kuongoka na kuifikia haki, wakawa wamo katika mifazaiko na hatimae kupotea. Kama wao wangelimsifu Mwenye Ezi Mungu kwa sifa zake mwenyewe, na viumbe kwa kwa kutumia sifa zao wenyewe, basi wangelikuwa wamefanya insafu, na wasingeshindana (wala kuzozana). Lakini kwa kuwa walikuwa wakitafuta kitu ambacho ambacho hawakuwa na uwezo wa kukielewa, hatimae walijikuta wamekwama njiani bila ya mafanikio. Na Mwenyezi Mungu humuongoza amtakaye na kumweka katika njia iliyonyooka."

Baada ya hapo Imran alisema: "Ewe bwana wangu, nashuhudia kwamba Yeye ni yupo kama ulivyomfafanua; lakini kuna swali jengine moja limebakia." Imamu akamwambia: "Uliza". Imran akauliza akisema: " Je Mwenyezi Mungu Hakimu yupo wapi? Je, hivi kuna kitu kinachomzunguka? Je, hubadilika katika hali moja kwenda nyengine? Au je huondoka sehemu moja hadi nyingine? Au anahitaji kitu chochote?" Imamu akajibu: "Hili ni moja ya maswali magumu zaidi yanayoulizwa na watu mbali mbali, ambayo hayawezi kudirikiwa na wenye upungufu wa akili na wasio na maarifa, lakini wale wenye busara na insafu hawatashindwa kulielewa jambo hili. Hivyo basi, zingatia kwa makini na uelewe jibu langu juu ya swali lako, ewe Imran:

Kwanza kabisa, kama (Mwenyezi Mungu) angeumba viumbe kwa sababu ya haja ya kuwategemea, basi ingekuwa ni sahihi kusema kwamba Yeye huhama akiwaendea viumbe wake kwa sababu anawahitaji; lakini Yeye hakuumba kitu chochote kile eti kwa sababu alikuwa anakihitaji. Yeye daima yuko thabiti, na hayupo ndani ya kitu chochote, wala juu ya kitu chochote; isipokuwa viumbe wake ndiwo wanao shikamana huku mmoja akimsaidia mwingine, na mmoja kuingia ndani ya mwengine, huku baadhi yao wakiwa wanatoka kutoka kwa wengine. Mwenye Ezi Mungu Mtukufu kwa uwezo wake ndiye anaye shikilia na kuhimili kila kitu. Hivyo basi, haiwezekani Yeye haingii ndani ya kitu chochote wala kutoka kwenye kitu chengine. Yeye hachoshwi na tendo la kuvihimili viumbe vyake wala hashindwi na jambo hilo. Wala hakuna hata kiumbe kimoja kinachojua jinsi tendo hili linavyofanyika, isipokuwa Mwenye Ezi Mungu mwenyewe pamoja na wale ambao aliwowapa maarifa ya utambuzi wa jambo hilo, nao ni manabii wa Mwenye Ezi Mungu, na walio na siri za Mwenye Ezi Mungu, walinzi na wahifadhi wa sheria zake. Amri zake hutekelezwa kwa kufumba na kufumbua, bali ni zaidi ya hapo. Anachotaka, huamuru tu kwaa husema: "Kuwa", na kitu hicho huwepo kwa matakwa na amri ya Mwenye Ezi Mungu. Hakuna kiumbe chake chochote kilicho karibu naye zaidi kuliko chengine, wala hakuna kitu kilicho mbali zaidi naye kuliko kingine. Je, umeelewa, Imran?"

Hapo Imran akasema: "Ndiyo, mkuu wangu, nimeelewa na nashuhudia kwamba Mwenye Ezi Mungu Mtukufu ni kama ulivyomfafanua na kuuelezea kwa upweke wake, na nashuhudia kwamba Muhammad ni mja wake ambaye alitumwa na nuru ya uongofu na dini ya haki." Kisha akageuka kuelekea Qibla, akasujudu na akasilimu. [25]

Mada Zinazo Husiana