Mdahalo kati ya Imam Ridha na Jathaliq

Kutoka wikishia

Mdahalo kati ya Imam Ridha na Jathaliq (Kiarabu: مناظرة الإمام الرضا عليه السلام مع الجاثليق) mwenye imani ya Kikristo, ulikuwa ni mjadala wa mazungumzo ya kina uliojadili mada muhimu za kielimu, likiwemo suala la Unabii wa Mtume wa Muhammad (s.a.w.w) pamoja na asili ya kibinadamu ya Yesu Kristo. Mazungumzo haya yalifanyika katika kikao kilichoandaliwa kwa agizo la Khalifa wa ukoo wa Abbasiya aitwaye Maamun, ambapo wanazuoni wa dini za Kiyahudi, Kikristo, Zoroastria (Kimajusi) na Kisaabi’i walishiriki katika mdahalo huo pamoja na Imam Ridha (a.s).

Hadithi ya mdahalo huu inasimulia tukio la kihistoria lililozungumzwa kwa kina katika vitabu vya Tawhidi na Uyoon Akhbar al-Ridha, ambavyo viliandikwa na Sheikh Saduq, mwanazuoni maarufu wa Kiislamu wa kutoka madhehebu ya Kishia. Kwa mujibu wa maelezo ya Hasan bin Muhammad Naufali, mpokezi wa Hadithi hii, Imamu Ridha (a.s) alijenga hoja nzito katika kuthibitisha Unabii wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), akitumia dalili zitokazo katika Injili, kitabu kinachoheshimiwa na Wakristo. Imamu Ridha (a.s) alitumia Aya za Injili kuonesha wazi kuwa Yesu Kristo hakuwa Mungu, bali alikuwa ni mwanadamu aliyetumwa na Mwenye Ezi Mungu. Katika mazungumzo haya ya kina, Imamu alitoa ufafanuzi wa kina na wa kielimu, akionesha tofauti kati ya Uungu na ubinadamu, na kueleza kwa hoja na ithibati makini kuwa Yesu alikuwa mjumbe wa Mwenye Ezi Mungu, si Mungu mwenyewe. Hivyo, Hadithi hii inatoa mwanga juu ya ujuzi na elimu ya Imamu Ridha (a.s) paomja na uwezo wake wa kubainisha ukweli kupitia maandiko ya kidini yalioko katika dini nyengine.

Kulingana na riwaya hii, Jathaliq, ambaye alikuwa ni mmoja wa viongozi wa kidini wa Kikristo, alishindwa wazi katika mdahalo huu wa kielimu. Alishindwa kutoa majibu sahihi na yenye nguvu kwa maswali na hoja zilizowekwa mbele yake na Imamu Ridha (a.s). Katika mdahalo huu, Imamu Ridha alionyesha maarifa yake ya kina na uwezo wa kubainisha ukweli kwa kutumia hoja za kiakili na msingi wa maandiko ya kidini. Jathaliq, kwa upande wake, alishindwa kuleta ushahidi wa kutosha au kuendeleza majadiliano kwa ufanisi, na hivyo alishindwa kuthibitisha hoja zake au kupinga kwa mafanikio kile alichokuwa akishawishisha. Hali hii ilionyesha kwa wazi mtindo wa majadiliano na umakini wa Imamu Ridha katika kujenga na kuthibitisha mitazamo yake, huku akimwacha Jathaliq bila majibu ya kutosha na hali ya kushindwa katika mdahalo huo.

Muktadha na Vichochezi vya Mjadala

Mdahalo wa Imamu Ridha (a.s) na Jathaliq umetajwa katika hadithi inayosema kwamba; mjdala huo ulihudhuriwa na wanazuoni wa dini mbalimbali, wakiwemo wa Kikristo, Kiyahudi, Kizoroastria (Kimajusi), na Kisabi’i. Katika mjadala huu, Imamu Ridha (a.s) alionyesha umahiri wake wa kiitikadi na uwezo wake wa kujenga hoja madhubuti dhidi ya mawazo na imani za dini hizi, akiweka wazi msingi wa Uislamu na kumjibu kila hoja iliyotolewa na wapinzani wake kwa hekima na ujuzi wa hali ya juu kabisa. [1] Kulingana na ripoti ya Hassan bin Muhammad Naufali, mpokezi wa Hadithi hii, mdahalo huu uliandaliwa kwa ombi la Khalifa Maamun wa kutoka ukoo Abbasiyya. Pale Imamu Ridha (a.s) alipoondoka Madina kuelekea Marw kwa mwaliko wa Maamun, Khalifa aliwaalika wanazuoni na wanafikra wa dini mbalimbali ili wakusanyike kwa ajili ya mjadala wa kidini na Imamu Ridha (a.s) huko Marw. Mjadala huu wa kina juu ya masuala ya kiitikadi, ulihudhuriwa na wanazuoni kadhaa kutoka dini mbali mbali. [2] Naufali alieleza kwamba lengo kuu la Maamun kuandaa kikao hichi lilikuwa ni kumjaribu Imamu Ridha (a.s). Ma'mun alitaka kupima maarifa, hekima, na uwezo wa Imam Ridha (a.s) katika kujibu hoja na changamoto kutoka kwa wanazuoni wa dini mbalimbali. Kwa kuwaleta pamoja wanafikra wa Kikristo, Kiyahudi, Kizoroastria, na Kisabii, Maamun alikuwa na hamu ya kuona jinsi Imamu Ridha (a.s) atakavyo shinwa kutetea imani za Kiislamu mbele ya hoja tofauti za kidini, na hivyo kuthibitisha udhaifu wake ili kumshusha hadhi yake kama ni kiongozi wa kidini wa juu katika jamii. [3]

Jathaliq, ambaye alikuwa kiongozi mkuu wa Wakristo, ndiye aliye fungua mjadala na Imamu Ridha (a.s) katika kikao hichi. Mbali na Jathaliq, viongozi wengine kama Ra's al-Jalut, kiongozi wa Wayahudi; viongozi wa Masabi’ina; Hirbidh, kiongozi mkuu wa Wazoroastri (Wamajusi); na Imran Sabi’i pia walihudhuria na kushiriki katika mjadala huo wa kidini. Kila mmoja wao alikuja na maswali na changamoto zake, wakitaka kujua maoni ya Imamu Ridha (a.s) kuhusu masuala mbalimbali ya kiitikadi na kidini. [4]

Mbindu za Imamu Ridha (a.s), Nidhamu, na Heshima Juu ya Uhuru wa Maoni

Mwanzo mwa mjadala, Jathaliq anamwambia Maamun, ambaye alimtaka aanze mjadala, kwamba hawezi kujadiliana na Imamu Ridha (a.s) kwa sababu yeye hakubalianai na kitabu cha dini ya Kiislamu wala nabii wa dini hiyo. Alisema hayo huku akihoji kwa kusema kwamba; ni vipi mjadala unaweza kufanyika bila kuwepo misingi ya pamoja. Imamu Ridha (a.s) akamjibu kwa hekima, akimweleza kwamba; katika mjadala wao, atatumia hoja zake kwa rejea kitabu cha Injili, ambacho ni kitabu kitakatifu cha Wakristo. Kusikia hivyo, Jathaliq akakubali pendekezo hilo, lakini pakawekwa sharti kwamba; askikatae chochote kitakachotolewa kutoka kwenye Injili hiyo. Hivyo, mjadala unafanyika kwa kutumia maandiko ya kitabu hicho. [5] Katika mazungumzo hayo, Imamu Ridha (a.s) mara kadhaa alitumia Injili kuthibitisha ukweli wa hoja zake na kuwathibitishia Wakristo usahihi wa maneno yake kwa kutumia maandiko yao wenyewe.[6] Akiwa kikao humo, Imamu Ridha (a.s) alitoa tangazo kwa kila apingaye Uislamu ambaye anataka kuuliza maswali fulani, basi anaweza kuuliza maswali yake bila woga na bila kujali nafasi ya Imamu Ridha (a.s) na mamlaka aliyonayo katika kasri la Maamun. Uhakikisho huu ulitolewa kwa nia ya kuwafanya wapinzani wajisikie huru kuuliza maswali yao. Wapinzani walikiri kuwa, kama siyo uhakikisho huo wa wazi kutoka kwa Imamu Ridha (a.s), basi hawangethubutu kuuliza maswali yao kwa hofu ya kudharauliwa au kushindwa katika mjadala huo. Hivyo, uhakikisho huo uliwapa ujasiri wa kushiriki kikamilifu katika mjadala huo. [7] Mojawapo ya sifa muhimu katika mijadala ya Imamu Ridha (a.s) na wapinzani pamoja na wataalamu wa dini mbalimbali ilikuwa ni dhamira ya kuendelea na majadiliano hadi kufikia hitimisho la kina, bila kuyakatisha au kuyaacha nusu. Imamu Ridha (a.s) alihakikisha kuwa kila hoja ilijadiliwa kwa kina na kufafanuliwa kikamilifu. Hata kama mjadala ulikatishwa kwa muda kwa ajili ya kusali au sababu nyinginezo, mara tu baada ya sala kumalizika, mjadala huo ulikuwa unaendelezwa tena. Hii ilionesha uwazi, uvumilivu, na utayari wa Imamu Ridha (a.s) katika kusikiliza na kujibu maswali na hoja zote zilizoletwa mbele yake, kuhakikisha kuwa kila kitu kinafikishwa hadi mwisho kwa kina kabisa na hitimisho linapatikana. [8]

Maudhui

Katika mazungumzo kati ya Imamu Ridha (a.s) na Jathaliq, mjadala ulijikita hasa katika masuala mawili makuu: Suala la kwanza ni Kuthibitisha Unabii wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), Imamu Ridha (a.s) alijaribu kuthibitisha ukweli wa unabii wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) kwa kutumia hoja kutoka katika Injili, kitabu kitakatifu cha Wakristo. Alieleza jinsi unabii wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ulivyoandikwa na kutabiriwa katika maandiko ya awali, akitumia mifano na Aya zilizotajwa ndani ya Injili. Suala la pili ni swali kuhusu je, Nabii Isa (a.s) ni Mungu au ni Mwanadamu: Imamu Ridha (a.s) alijibu maswali kuhusu hadhi ya Nabii Isa (a.s), na kufafanua vya kutosha ikiwa yeye alikuwa ni Mungu au mwanadamu. Alitumia mashiko kutoka katika Injili na maandiko ya dini nyingine kuthibitisha kuwa Nabii Isa (a.s) alikuwa ni mwanadamu na sio Mungu kama alivyodai Jathaliq, huku akionesha jinsi mafundisho haya yalivyopotoshwa au kufasiriwa vibaya. Katika mjadala huu, pia yalijadiliwa masuala mengine kama vile: Idadi ya Wanafunzi wa Karibu wa Nabii Isa (a.s): Imamu Ridha (a.s) alijadili idadi ya wanafunzi wa karibu wa Nabii Isa (a.s), na kutoa maelezo kuhusu nafasi yao katika historia ya dini ya Kikristo. [9] Kupotea kwa Nakala Asili ya Injili: Imamu Ridha (a.s) alizungumzia kuhusu kupotea kwa nakala asili ya Injili, akionyesha jinsi nakala hizi za awali zilivyopotea na jinsi tafsiri na tafakari za baadaye zilivyobadilishwa au kupotoshwa. [10] Mjadala huu ulifanyika kwa kina na kwa umakini, huku Imamu Ridha (a.s) akijitahidi kufafanua na kuonyesha ukweli wa jawabu zake katika mada zote zilizojadiliwa.

Imam Ridha (a.s) ili kuthibitisha unabii wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), alileta mifano kutoka kwenye Injili na Torati ambayo inaashiria kuja kwa nabii mwenye ishara za Mtume Muhammad (s.a.w.w). Miongoni mwa mambo aliyosema ni:

  1. Unabii Katika Injili: Imamu Ridha (a.s) alieleza kwamba katika Injili, Yohane Mbatizaji (John the Baptist) alitangaza kuhusu dini ya Muhammad ambaye ni Mtume wa Kiarabu. Alisema kwamba Masihi alimtaja Muhammad na alitoa habari za kuja kwake baada yake. Imamu Ridha (a.s) aliongeza kwamba habari hizi zilikuwa ni sehemu ya mafundisho yaliyotolewa kwa wanafunzi wa Masihi, ambao walimwamini. [11]
  2. Utabiri wa Faraklita (Paracletus): Aidha, Imamu Ridha (a.s) alirejelea maandiko ya Injili ambayo yanaeleza kwamba Yesu alisema: “Mimi nitakwenda kwa Mungu wenu na Mungu wangu, na kwamba Faraklita (Mfariji (Paracletus)) atakuja baada yangu”. Faraklita ni jina linalotumika katika Injili kumaanisha Mfariji ambaye anatabiriwa kuja baada ya Yesu, na Imamu Ridha (a.s) alionyesha kwamba; jina la Faraklita linahusishwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w). [12]

Katika kupinga imani ya Wakristo kwamba Yesu ni Mungu, Imamu Ridha (a.s) alileta hoja mbili muhimu:

  1. Hoja ya Kwanza: Imamu Ridha (a.s) alieleza kwamba kama Yesu angekuwa Mungu, basi asingepaswa kusimamisha sala wala kufunga. Akasema kwamba; ibada kama sala na kufunga zina maana ya mtu kutafuta msaada au huruma kutoka kwa mwingine. Kwa hivyo, kama Yesu alikuwa Mungu, haingekuwa na maana kwake kusimamisha sala au kufunga kwa ajili ya mtu mwingine, kwa sababu Mungu hana haja ya kuomba msaada au kufanya ibada kwa ajili ya mwingine. Hii inadhihirisha kuwa Yesu, kwa hali hii, alikuwa binadamu na hakuwa Mungu. [13]
  2. Hoja ya Pili: Jathaliq alidai kwamba Yesu ni Mungu kwa sababu alifufua wafu, aliponya wagonjwa, na kuwarejeshwa vipofu mwanga wa macho yao. [14] Imamu Ridha (a.s) alijibu hoja hii kwa kusema kwamba; manabii wengine pia walifanya miujiza kama hiyo. Kwa mfano, Elisha alifufua wafu na kuponya wagonjwa, na nabii Ezekieli alifufua watu 35,000 baada ya miaka 60 ya kifo chao. Imamu Ridha (a.s) alionyesha kwamba kama uwezo wa kufanya miujiza ungeweza kuthibitisha Uungu, basi manabii hawa pia wangeweza kuhisabiwa kuwa ni Waungu, jambo ambalo Wakristo hawakubalianai nalo. Hivyo, uwezo wa kufanya miujiza hauwezi kuwa ni uthibitisho wa Uungu. [15]

Matokeo ya Mjadala

Kulingana na muktadha wa Hadithi, Jathaliq hakupata majibu kwa baadhi ya maswali yaliyoulizwa na Imamu Ridha (a.s) katika majadiliano haya na mara kadhaa alionekana akibaki kimya bila kusema kitu. Hapa kuna baadhi ya matokeo muhimu ya mjadala huu:

  1. Hoja ya Sala na Kufunga: Wakati Imamu Ridha (a.s) alipo mwambia Jathaliq kwamba; kama kweli Yesu alikuwa ni Mungu, basi kulikuwa na haja gani ya Yesu huyo kusimamisha sala na kufunga, katika sali hili Jathaliq alibaki kimya na hakuwa na majibu. [16] Hoja hii ilionyesha kwamba ibada za Yesu hazingekubaliana na hali ya Uungu wake.
  2. Ushahidi Kutoka katika Injili: Pale Imamu Ridha (a.s) alipoleta ushahidi kutoka ndani ya maandiko ya Injili kuhusiana na utume wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) na ubinadamu wa Yesu, Jathaliq alimuomba Imam Ridha ruhusa ya kutokujibu maswali haya, [17] akionesha kwamba alikuwa hana majibu juu ya hoja zilizowasilishwa mbele yake.
  3. Ukurasa wa Hatimisho: Mwishoni wa majadiliano, Jathaliq alikiri kwamba hakuwa na matarajio ya kukutana na mtu kama Imamu Ridha (a.s) miongoni mwa wasomi wa Kiislamu. [18] Hii ilionesha heshima yake kwa maarifa ya Imamu Ridha (a.s) na kwa kiasi kikubwa alikubali kuwa Imamu Ridha alishinda mjadala kwa hoja zake makini.

Vyanzo vya Hadihti

Matini ya majadiliano kati ya Imamu Ridha (a.s) na Jathaliq kwa mara ya kwanza kabisa imeripotiwa kutoka katika vitabu viwili viitwavyoTawhidi na Uyuni Akhbar al-Ridha, [19] [20] vilivyoandikwa na Sheikh Saduq (aliyeishi kati ya mwaka 305 na 381 Hijiria). Vitabu hivi vinashikilia nafasi muhimu katika nyanja za elimu ya dini na Hadithi. Riwaya ya tukio hli imaelezea kwa kina kabisa ndani vitabu viwili hivyo. Katika Ihtijaj, kitabu kilichoandikwa na Ahmad bin Ali Tabarsi, aliyeishi katika karne ya sita Hijria, kuna muhtasari wa juu ya majadiliano haya. [21] Kitabu hichi kinatoa kiasi fulani cha mwangaza kuhusian na mazungumzo kati ya Imamu Ridha na Jathaliq. Vilevile, Alama Majlisi, mmoja wa wanazuoni maarufu wa Kiislamu, ameinukuu Hadithi hii kutoka kwenye vitabu vya Tawhid na Uyuni Akhbar al-Ridha vya Sheikh Saduq. [22]

Uhalali wa Hati ya Hadithi

Katika utafiti uliofanya na wanazuoni wa fani ya wa elimu ya rijali, ambayo ni sayansi inayochunguza uaminifu wa wapokezi wa Hadithi, kumebainika kuwepo kwa mitazamo tofauti kuhusiana na mlolongo wa wapokezi wa Hadithi hii. Wengine wamewahisabu wapokezi wote wa Hadithi hii kwan ni wapokezi waaminifu, wakati baadhi ya wanazuoni wamehesabu baadhi yao kuwa ni madhaifu wasio aminika vya kutosha. [23] Zaidi ya hayo, msururu wa wapokezi wa Hadithi hii ni mursal, kwa maana ya kwamba; baadhi ya wapokezi wake hawajatajwa kwa majina ndani ya msururu huo. Hali ambayo inaathiri uhalali wa Hadithi, na hivyo kutumbukizwa kwenye kapu ya Hadithi dhaifu, kutokana na mapungufu hayo katika msururu wa wapokezi wake. [24] Hata hivyo, baadhi ya wanazuoni wanakubaliana na dosari hizo wakisema kwamba; ingawa Hadithi hii ina udhaifu katika msururu wa wapokezi wake, ila bado inakubalika na inaweza kutegemewa na kufanyiwa kazi. Hii ni kwa sababu Hadithi hii imesimuliwa na mwanazuoni maarufu (Sheikh Saduq), ambaye hakuwa akisimulia Hadithi asizokuwa na uhakika nazo, bali alikuwa akinukuu zile tu azlizokuwa na uhakika nazo kwamba zimesimuliwa na Maasumina (watu walio toharishwa). Kwa hiyo, licha ya udhaifu unaopatikana katika msururu wa wapokezi, ila bado hadithi hii inakubalika kutokana na usahihi na uaminifu wa msimuliaji wake. [25]

Matini na Tafsiri Yake

Maa'mun alimgeukia Jathaliq na kumwambia: "Ewe Jathaliq, huyu ni Ali bin Musa bin Ja'afar, binamu yangu na mtoto wa Fatima, binti wa Nabii wetu na ni mwana Ali bin Abi Talib, rehma za Mwenye Ezi Mungu ziwe juu yao. Ningependa uzungumze naye, ujadili naye, uweke hoja zako mbele yake, ila usiache kuwa na insafu."

Jathaliq alisema: "Ewe Amiri Al-Muuminina, nitajadili vipi na mtu anayetoa hoja kutoka katika kitabu ambacho sikubaliani nacho na kutumia maneno ya Nabii ambaye mimi simuamini?" Imamu aliuliza: "Ewe Mkristo, ikiwa nitakuletea hoja kutoka katika Injili, je, utazipokea na kukubaliana nazo?" Jathaliq akajibu: "Je, hivi nitaweza kukataa kile kisemwacho na Injili? Naapa kwa Mungu ya kwamba, hata kama moyoni utadhikina na jambo hilo, ila bado nitalazimika kukubali tu." Imamu akasema: "Sasa, uliza chochote unachotaka, na utapata jibu lako."

Katika majadiliano hayo, Jathaliq aliuliza: "Una imani gani kuhusiana na unabii wa Isa na kitabu chake? Je, unapingana na viwili hivyo?" Imamu alijibu kwa utulivu: "Ninakubaliana na unabii wa Isa na kitabu chake, na pia yale aliyowaahidi wafuasi wake na yaliyoafikiwa na wanafunzi wake. Hata hivyo, nakataa kumtambua Isa yeyote yule ambaye hakukiri unabii wa Muhammad (s.a.w.w) na kitabu chake, na ambaye hakuwapa umma wake habari na bishara njema kumhusiana naye."

Jathaliq akauliza: "Je, kwani si kila hukumu inahitaji mashahidi wawili waadilifu?" Imamu akathibitisha kwa kusema: "Ndiyo, bila shaka". Jathaliq akaendelea: "Basi, lete mashahidi wawili waadilifu kutoka kwa wale ambao hawatoki katika imani yako, ila wanakubalika ndani ya Ukristo. Na sisi pia tutaleta mashahidi wawili waadilifu kutoka kwa wale ambao si waumini wenzetu". Imamu akakubali kwa utulivu kabisa, akamwambia: "Sasa umezungumza jambo lililo sawa. Je, unakubali ushahidi wa mtu mwadilifu aliyekuwa na heshima kubwa mbele ya Isa?" Jathaliq akatulia na kuuliza: "Mtu huyo mwadilifu ni nani? Tafadhali, taja jina lake." Imam akajibu kwa upole: "Unasemaje kuhusiana na Yohanna wa Mbatizaji?" Jathaliq, kwa mshangao na heshima, alisema: "Ah! Umetaja mtu aliyekuwa akipendwa sana na Isa."

Imamu akamwambia: "Nakuapia kwa jina la Mungu, je, hivi Injili haijasemwa kwamba Yohanna alisema: 'Masihi alinitaarifu kuhusiana na dini ya Muhammad Mwarabu na akanipa habari njema kwamba atakuja baada yake, nami pia nilitoa bishara hiyo njema kwa wanafunzi wake, ambapo nao waliamini?'"

Jathaliq alikubali na kusema: "Ndiyo, Yohanna alinukuu akielezea kwamba; Yesu Masihi alisema kuwa atakuja nabii ambaye ameashiriwa, na pia alitoa habari njema kuhusiana na familia yake na mrithi wake. Lakini hakutaja ni lini hili litatokea, wala hakuwataja kwa majina ili tuweze kuwafahamu." Imamu akasema: "Ikiwa hapa patakuwa na mtu anawezaye kusoma Injili naye akakusomea sehemu zinazohusiana na Muhammad, familia yake, na umma wake, je, utaamini?" Jathaliq akajibu: "Hilo ni jambo zuri." Imamu akamgeukia Nastasus wa kutoka nchi ya Roma na kumwuliza: "Je, unaweza kusoma sehemu ya tatu ya Injili kwa usahihi?" Nastasus akajibu: "Ndiyo, nimeihifadhi yote kikamilifu."

Baada ya hapo Imamu alimwelekea Raasu al-Jalut na kumuuliza: "Je, umewahi kusoma Injili?" Raasu al-Jalut akajibu: "Ndiyo, nimeisoma." Imamu akaendelea kusema: "Nitakusomea sehemu ya tatu ya Injili. Ikiwa kuna kitu chochote kuhusu Muhammad, familia yake, na umma wake, basi wafikiana na ukweli huo. Ila kama hakuna kitu kama hicho, usikubaline nami juu ya hili."

Imam akaanza kusoma sehemu hiyo, na alipofikia mahali palipomhusu Mtume Muhammad (s.a.w.w), alisimama na kumwambia Raasu al-Jalut: "Nakusihi kwa haki ya Yesu na mama yake, je, unakubali kuwa mimi ni mjuzi wa Injili?" Raasu al-Jalut akajibu: "Ndiyo, ninakubali." kisha Imamu akaendelea kusoma na kuonesha sehemu inayomhusu Muhammad, familia yake, na umma wake, na kumuuliza: "Unasemaje sasa? Je haya ni maneno ya kweli ya Yesu Kristo (a.s). Ikiwa utayakanusha maneno ya Injili, basi utakuwa unamkanusha Musa na Isa (a.s.), na iwapo utayakataa maneo yao, basi utastahili kifo, kwa sababu utakuwa umemkufuru Mungu, Mtume wake pamoja na kitabu chako." Jathaliq akasema: "Siwezi kupinga jambo lolote lile lililo wazi kutoka kwenye Injili; badala yake, nitalikubali." Imamu akasema kuwaambia wale waliokuwepo: "Shuhudieni makubaliano yake." Kisha Imamu akaendelea kumbambia: "Uliza utakacho." Jathaliq akauliza: "Hi wanafunzi wa Yesu na wanazuoni wa Injili walikuwa wangapi?" Imamu akajibu kwa kumwambia: "Swali lako ni la msingi. Wanafunzi wake walikuwa ni kumi na mbili, na miongoni mwao, Luka niye aliye kuwa mjuzi na bora zaidi kati yao. Wanazuoni wa Kikristo walikuwa ni watatu: Yohanna Mkuu huko Aaj, Yohanna wa Qarqisiyah, na Yohanna wa Dailam huko Rajjaz. Yeye (Yohanna wa Dailam) ndiye aliyetoa bishara kwa wafuasi wa Yesu na Wana wa Israeli, kuhusiana na Mtume Muhammad (s.a.w.w), Ahlul-Bait wake, pamoja na umma wake kwa jumla."

Imamu akaendelea kumwambia: "Ewe Mkiristo, naapa kwa jina la Mwenye Ezi Mungu kwamba; sisi tunamwamini Yesu aliyemwamini Muhammad (s.a.w.w), na hatuna shaka yoyote juu ya 'Yesu wenu,' isipokuwa tuna wasiwasi na mapungufu ya sala na saumu zake."

Jathaliq alisema: "Naapa kwa jina la Mungu, kwamba wewe umechanganya mambo na kujidhoofisha wewe mwenyewe. Nilidhani wewe ndiye mjuzi zaidi miongoni mwa Waislamu." Imamu akauliza: "Kuna tatizo gani?" Jathaliq akajibu: "Umesema kwamba Yesu alikuwa dhaifu na hakufunga wala kusali kwa kiwango kikubwa kinachostahiki, ilhali ukweli ni kwamba Yesu hakuna siku aliacha kufunga na wala usiku hakuna usiku uliompita bila kukesha. Alikuwa akifunga kila mchana na akisali usiku kucha." Imamu akamwuliza: "Alikuwa akifunga na kusali kwa ajili ya kumkaribia nani?!" Jathaliq alishindwa kujibu na akabaki kimya. Imamu akamwambia: "Nataka kukuuliza jambo fulani?" Jathaliq akasema: "Uliza, kama nitakuwa na jibu lake, nitakujibu." Imamu akamuuliza: "Kwa nini unakana kwamba Yesu aliweza kufufua wafu kwa idhini ya Mungu?" Jathaliq akajibu: "Kwa sababu yeyote anayefufua wafu na kuponya vipofu na wale wenye ukoma ni Mungu na anastahili kuabudiwa." Imamu akasema: "Lakini Yasai (Elisha) pia alifanya matendo kama yale ya Yesu: alitembea juu ya maji, aliwafufua wafu, aliwaponya vipofu na waliokuwa na ukoma, lakini umma wake hawakumchukulia yeye kuwa ni Mungu wala hawakumwabudu. Pia, nabii Hezekieli naye aliwafufua wafu kama Yesu mwana wa Mariamu, ambapo aliwafufua watu elfu thelathini na tano baada ya miaka sitini tangu kufariki kwao. Baada ya kusema hayo Imamu alimgeukia Raasu al-Jalut na kumuuliza: 'Je, umewahi kusikia hadithi kama hii kuhusiana na vijana wa Israeli katika Taurati?' Hao walikuwa ni vijana walio chaguliwa na Bukhonassor miongoni mwa wafungwa wa Israeli waliotekwa wakati wa uvamizi wa Yerusalemu na kuwapeleka Babeli (Mji ulioko Iraq ya sasa). Kisha Mungu alimpeleka Hezekieli kwao na kuwafufua. Hadithi hii ipo katika Taurati, na yeyote miongoni mwenu anayekataa, ni kafiri."

Raasu al-Jalut akasema: "Ndiyo, tumesikia hadithi hii na tunafahamu kuhusu hilo." Imamu akasema: "Ni kweli. Sasa sikiliza kwa makini na uone kama ninasoma kwa usahihi sehemu hii ya Taurati au la." Hapo Imamu alisoma Aya fulani kutoka Taurati mbele yetu.

Myahudi, baada ya kusikia usomaji na sauti ya Imamu, alipigwa na mshangao na akaanza kutingatinga kushoto na kulia. Kisha Imamu akamgeukia Jathaliq na kumuuliza: "Je, hawa watu walikuwepo kabla ya Yesu au Yesu alikuwepo kabla yao?" Jathaliq akajibu: "Wao walikuwepo kabla ya Yesu." Imamu akasema: "Makuraishi wote walimjia Mtume wa Mwenye Ezi Mungu (s.a.w.w.) na kumwomba awafufue wafu wao. Mtume akamtuma Ali bin Abi Talib (a.s) pamoja nao kwenda jangwani (au makaburini) na akawambia: 'Nenda jangwani (au makaburini) kisha waite kwa sauti kubwa, kwa kuwataja kwa majina wale ambao hawa wameomba kufufuliwa, uwaambie: Muhammad Mtume wa Mungu anasema: Simameni kwa idhini ya Mungu.'" "(Imamu Ali akawaita kwa majina yao) Wote walinuka na kuanza kufuta vumbi lililoko juu ya vichwa vyao." Watu wa kabila la Quraish wakawauliza kuhusu hali zao na pia wakasema: "Muhammad amekuwa ni Mtume." Wafu waliosimama kutoka kwenye vumbi wakasema: "Laiti tungeweza kumfikia na kumuamini." Mtume pia aliponya vipofu, wagonjwa wa ukoma, na wendawazimu, na alizungumza na wanyama, ndege, majini, na mashetani. Hata hivyo, hatumfanyi yeye kuwa Mungu, na pia hatukanushi wema na heshima za manabii hawa (Yesu, Yasai (Elisha), Hezekieli, na Muhammad (s.a.w.w))." Ila nyinyi mnaomfanya Yesu kuwa Mungu, mnapaswa pia kumfanya Yasai (Elisha) na Hezekieli kuwa Miungu, kwa sababu wao pia walifanya miujiza kama ya Yesu, ikiwa ni pamoja na kufufua wafu. Aidha, kundi la Wana wa Israeli, ambao idadi yao ilikuwa maelfu, waliokimbia kutoka mji wao kwa hofu ya tauni, na Mwenye Ezi Mungu akazichukua roho zao wote kwa moja. Watu wa mji huo walijenga ukuta kuzunguka sehemu waliyofia na kuwaacha hapo, hadi mifupa yao ilipoanza kuoza. Nabii mmoja wa Wana wa Israeli alipopita sehemu hiyo, alishangaa kwa wingi wa mifupa iliyooza. Mwenye Ezi Mungu Mtukufu akamshushia ufunuo na kumwambia: "Je, ungependa niwafufue ili uweze kuwaonya na kueneza dini Yangu?" Nabii akasema: "Ndio, bila shaka ningependa kufanya hivyo."

Mwenye Ezi Mungu akampa ufunua na kumwambia: "Inua sauti yako uwaite" Nabii huyo akawaita kwa kusema: "Enyi mifupa iliyooza, simameni kwa idhini ya Mwenye Ezi Mungu." Wote wakafufuka na kusimama huku wakiwa wanakumuta vumbi vichwani mwao. Vilevile, Nabii Ibrahimu (a.s) alipokamata ndege, akawakata vipande na kuweka vipande hivyo juu ya milima, kisha akawaita ndege hao, nao wakafufuka na kuja mbele yake. Pia, Nabii Musa (a.s) pamoja na watu sabini aliowachagua kutoka kwa Wana wa Israeli ili kwenda naye mlimani, waliposema: "Bilas haka wewe umemwona Mungu wako, basi sisi pia tunataka utuoneshe Mola wako."

Nabii Musa (a.s) alisema kuwambia: "Kwa kweli mimi sijawahi kumuona Mola wangu, lakini walikataa na kusema, 'Hatutakuamini mpaka tumuone Mungu kwa wazi wazi.'" (Suratu al-Baqarah, Aya 55). Matokeo yake, radi iliwateketeza na kuangamizwa, na Musa akabaki peke yake. Hpo Musa alimuomba Mwenye Ezi Mungu akisema: "Ewe Mungu, nilichagua watu sabini kutoka kwa Wana wa Israeli na kuwaleta pamoja nami, lakini sasa natarudi peke yangu. Vipi watu wangu watakubali maneno yangu kuhusiana na tukio hili? Kama ungelipenda, basi ungeweza kutuangamiza kabla ya hapo." (Muktadha wa Aya 155 ya Suratu al-A'raf). Mwenye Ezi Mungu Naye akafufua watu hao baada ya vifo vyao.

Imamu aliendelea akisema: “Hakuna chochote kati ya yale niliyokueleza unaweza kukataa; kwa sababu yote haya ni maudhui ya Aya za Taurati, Injili, Zaburi, na Qur’ani. Ikiwa kila anayefufua wafu na kuponya vipofu, wenye ulgonjwa wa ngozi, na wenda wazimu, hupaswa kuitwa Mungu, basi nayo watakuwa na haki kama hiyo. Sasa, unasemaje?” Jathaliq akajibu: “Ndiyo, ni sawa kama maneno yako yasemavyo, na hapana mungu isipokuwa Allah tu.” Hapo Imamu alimgeukia Raasu al-Jalut na kusema: “Nakuapia kwa Aya kumi zilizoteremshwa kwa Musa bin Imran, je, hakuna habari kuhusina na Muhammad na umma wake zinapatikana katika Taurati?” (Na habari hiyo ni kama ifuatavyo:) “Wakati umma wa mwisho, wafuasi wa mwanamume mwenye ngamia, watakapokuja na kumtukuza Mungu kwa wingi kabisa; sifa mpya katika majumba mapya ya ya ibada. Wakati huo, Wana wa Israeli watapaswa kuelekea kwao na kwa mfalme wao ili nyoyo zao zipate amani; kwa kuwa wana wafwasi wa mtume huyo watakuwa na mapanga mikononi mwao kwa ajili ya kulipiza kisasi dhidi ya wapagani (maadui) katika sehemu zote za duniani.” Je, maelezo haya hayako kama hivyo katika Taurati?”

Raasu al-Jalut alisema: "Ndiyo, tumeikuta habari kama hivyo katika Taurati." Hapo Imamu alimgeukia Jathaliq na kusema: "Unamaarifa kiasi gani kuhusiana na kitabu cha Isaya (Isaiah)?" Jathaliq akajibu kwa kusema: "Ninakijua kwa kina na nina ujuzi wa kutosha kuhusiana na kitabu chake." Imamu akawaambia: "Je, mnakubali kwamba ibara ifuatayo ni sehemu ya maneno yake: 'Enyi watu, bila shaka mimi nimeiona picha ya yule mtu aliyepanda mnyama mwenye masikio marefu, akiwa amevaa mavazi ya nuru, na nimemuona mpanda ngamia huyo ambaye nuru yaka ni kama mbaramwezi mwezi?' Wote walijibu: 'Ndiyo, Isaya alisema hivyo.'" Imamu akaendelea: "Je, mnafahamu kile alichosema Yesu (a.s) katika Injili: 'Nitaenda kwa Mungu wenu na Mungu wangu, kisha atakuja Faraklita (Paracletus).' Naye ndiye atakayetoa ushuhuda wa haki kwa manufaa yangu, kama mimi ninavyotoa ushuhuda kwa ajili yake."

Jathaliq alijibu akisema: "Tunakubaliana na kila kitu unachosoma kutoka katika Injili." Imamu akamwambia: "Je, una hakika kwamba hili linapatikana katika Injili?" Jathaliq akasema: "Ndiyo." Imamu akaendelea kusema: "Wakati Injili ya kwanza ilipopotea, mliipata wapi na nani aliye kuandikieni Injili hiyo kwa ajili yenu?" Jathaliq akajibu: "Kipindi fulani tulipoteza Injili, kisha tukaipata tena ikiwa katika hali nzuri kama mpya. Yohana na Matayo ndiwo walituonyesha Injili hiyo." Imamu akajibu: "Inaonekana hujui mengi kuhusiana na kisa cha Injili hii wala wanazuoni wake! Ikiwa mambo yangekuwa kama ulivyosema, basi ni kwa nini kulikuwa na migawanyiko kuhusiana na Injili? Migawanyiko hii ni juu ya Injili hii hii mlio nayo leo. Ikiwa pale mlipoiona Injili hiyo hali yake ilikuwa kama ilivyokuwa mwanzoni, mngelikuwa na makubaliano juu yake. Lakini mimi nitakueleza ukweli: Wakati Injili ya kwanza ilipopotea, Wakristo walikusanyika kwa walimu wao na kuwauliza: ‘Yesu mwana wa Maria ameuawa na Injili pia imepotea. Nyinyi walimu mna nini mikononi mwenu?’ Luka na Marko walijibu: ‘Sisi tunajua Injili kwa moyo na kila Jumapili tutawasilisha Sura moja kutoka katika injili hiyo. Msihuzunike na msiache kuhudhuria sinagogi tupu. Kila Jumapili, tutakusomeeni sura moja hadi Injili ikamilike.’ Kisha Luka, Marko, Yohana, na Matayo wakakusanyika na kuandika Injili hii baada ya kupotea kwa Injili ya kwanza, nao walikuwa ndiwo wafuasi wa wafuasi wa kwanza wa Nabi Isa. Je, ulikuwa na habari juu ya hili?"

Hapo Jathaliq alikiri akasema: "Sikuwahi kujua jambo hili hadi sasa, na leo limekuwa wazi kwangu kwa baraka za maarifa yako juu ya Injili. Nimeweza pia kusikia mengi unayoyajua uliyoyaeleza kikaoni humu. Moyo wangu unashuhudia kwamba; yote haya ni kweli. Nimejifunza mengi kutokana na maneno yako." Imamu akamuuliza: "Kwa maoni yako, hivi ushahidi wa watu hawa unakubalika?" Jathaliq akajibu: "Ushahidi wao unakubalika kabisa. Hawa ni wanazuoni wa Injili, na kila kitu wanachokithibitisha na kukishuhudia ni cha kweli." Imamu akawageukia Maamun, na familia yake, pamoja na wengine waliokuwepo, akasema: "Bilas haka nyinyi ni mashahidi juu ya hili." Wote walijibu kwa pamoja: "Ndio sisi ni mashahidi." Kisha Imamu akamgeukia Jathaliq na kusema: "Nakusihi kwa haki ya mwana (Yesu a.s) na mama yake (Maryam a.s), je, unajua kwamba Matayo amesema: Masihi ni mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu, mwana wa Isaka, mwana wa Yakobo, mwana wa Yuda, mwana wa Khizron? Na kuhusu asili na nasaba ya Isa bin Maryam (a.s), Marko amesema: Yeye ni 'Neno' la Mungu ambalo Mungu aliliweka katika mwili wa kibinadamu na akawa mwanadamu?"

Imamu akaendelea: "Na Luka amesema: Isa bin Maryam (a.s) na mama yake walikuwa wanadamu walioumbwa kwa damu na nyama, na Roho Mtakatifu aliingia ndani yao. Je, unakubali kwamba miongoni mwa maneno ya Isa kuhusiana na yeye mwenyewe, alisema: 'Enyi Mitume, kwa kweli nakuambieni kwamba, hakuna mtu atakayepanda mbinguni ila yule ambaye ameshuka kutoka mbinguni, isipokuwa yule mpandaji ngamia, Mjumbe wa mwisho wa Manabii, ambaye atapanda mbinguni na kushuka tena.' Unasemaje nini kuhusu maneno haya?" Jathaliq akasema: "Haya ni maneno ya Isa, na sisi hatuyakani." Kisha Imamu akamuuliza: "Unaonaje kuhusu ushahidi na uthibitisho wa Luka, Marko, na Matayo kuhusiana na Isa na nasaba yake?" Jathaliq akajibu: "Wamemzulia Isa." Imamu akawageukia wale waliokuwepo na kusema: "Je, huyu bwana hakuwathibitisha hawa mbele yenu kuwa ni watakatifu na wakweli? Na hakusema kuwa wao ni wanazuoni wa Injili na kwamba maneno yao ni haki na ukweli?"

Jathaliq akasema: "Ewe Mwanazuoni wa Waislamu, napenda unisamehe na tuachane na watu hawa wanne." Imamu akajibu: "Nimekukubalia, tumekusamehe na tumekubali udhuru wako." Kisha Imamu akaendelea kwa kumbwambia: "Sasa unaweza kuuliza chochote unachotaka." Jathaliq alijibu: "Ni bora mwingine aulize maswali yake. Naapa kwa haki ya Masihi, sikuwahi kufikiria kwamba miongoni mwa wanazuoni wa Waislamu, kuna mtu kama wewe." [27]

Mada Zinazo Husiana

Rejea

Vyanzo