Mjadala kati ya Imamu Ridha na Ra’asu al-Jaaluut
Mjadala kati ya Imamu Ridha na Ra’asu al-Jaaluut (Kiarabu: مناظرة الإمام الرضا (ع) مع رأس الجالوت) ni mazungumzo ya kidini yaliyolenga kuthibitisha utume wa Mtume Muhammad (s.a.w.w). Katika mjadala huu, Imamu Ridha (a.s) alirejelea maandiko kutoka Taurati, Injili na Zaburi kama ushahidi wa kuthibitihsha utume wa Mtume Muhammad (s.a.w.w). Mazungumzo haya yamenukuliwa katika Hadithi zilizokusanywa na Sheikh Saduq, ambapo inasemekana kuwa, Khalifa Maamun ambaye ni Khalifa wa ukoo wa Abbasiyya, aliwaalika wanazuoni wa dini za; Kiyahudi, Kikristo, Zoroastria (Kimajusi) na Sabaa’iyya, ili walishiriki katika mdahalo huu kati yao na Imamu Ridha (a.s).
Sheikh Saduq ameripoti maandishi (matini) ya mjadala huu katika vitabu vyake vyake viwili maarufu viitwavyo Tawhidi na Uyuni Akhbar al-Ridha. Kulingana na ripoti za Hadithi hii, Raasu al-Jalut alishindwa kujibu hoja za Imamu Ridha (a.s) wakati wa mjadala huo.
Muktadha wa Kuanzishwa kwa Mjadala
Mjadala wa Imamu Ridha (a.s) na Ra’asu al-Jaaluut ulijiri kupitia amri ya Maamun, Khalifa wa Abbasiyya. Kwa mujibu wa ripoti ya Sheikh Saduq, wakati Imamu Ridha (a.s) alipokuwa akisafiri kutoka Madina kuelekea ikulu ya Maamun huko Marw, Maamun aliwaalika wanazuoni wa dini mbalimbali -Kikristo, Kiyahudi, Zoroastrian na Saabi'i- kushiriki katika mjadala na Imamu Ridha (a.s) baada ya yeye wasili mjini humo. Mdahalo huo ulilenga kuthibitisha utume wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) kwa kutumia maandiko ya kidini kama Taurati, Injili, na Zaburi. [1]
Ra’asu al-Jaaluut alikuwa mwanazuoni wa Kiyahudi, mbali na yeye kikao hichi pia kilihudhuriwa na Jathaliq (kiongozi wa Wakristo), viongozi wa Wakisabi'i, Hirbidh (kiongozi wa Wazoroastria), na Imran al-Sabi’i, ambao wote walishiriki katika mjadala huo. [2] Hassan bin Muhammad Naufali, mpokezi wa mjadala huu, alieleza kuwa lengo la Maamun kuandaa mjadala huu, lilikuwa kumjaribu Imamu Ridha (a.s). [3] Kulingana na ripoti hiyo, wakati Imamu Ridha (a.s) alipoona wasiwasi wa Naufali juu ya mjadala huu, alimgeukia na kumwambia, "Je, unaogopa wanaojadiliana nami kunishinda? ... Unajua ni wakati gani Maamun atakujja kujuta kutokana na kuandaa mjadala huu? Ni pale atakapoona na kusikia kwamba ninajadiliana na Wayahudi kwa kutumia Taurati, Wakristo kwa kutumia Injili, wafwasi wa Zaburi kwa kutumia Zaburi yao wenyewe. Pia, Wasabi'i, Warumi na Wafarsi kwa kutumia yale wanayokubaliana nayo wenyewe." [4]
Mada ya Mjadala na Matokeo Yake
Mjadala kati ya Imamu Ridha (a.s) na Ra’asu al-Jaaluut ulilenga kuthibitishiwa Utume wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) kupitia maandiko ya vitabu vya dini vya Taurati, Injili na Zaburi. Ra’asu al-Jaaluut alimuomba Imamu Ridha kutoa ushahidi wa Utume wa Muhammad (s.a.w.w) kutoka kwenye maandiko haya matakatifu, akisema kwamba; yeye hatakubaliana na ithibati zozote zile zitakazo tolewa kutoka nje ya maandiko ya vitabu hivyo. Imamu Ridha alikubali ombi hili na akaweka mbele ushahidi uliopatikana kutoka kwenye vitabu hivi vitakatifu kimoja baada ya chengine, kama ifuatavyo:
- Taurati: Musa ambaye ni mtume wa Bani Israeli aliwaambia Wana wa Israeli, «Nabii atatokea kutoka kwa ndugu zenu. Basi msadikini na mtiini mtume huyo». Imamu Ridha alifafanua kuwa; Kwa kuzingatia kuwa ndugu wa Wana wa Israeli ni watoto wa Ismaili, na kati ya watoto wa Ismaili, ni Muhammad bin Abdullah ndiye mtu pekee aliyejulikana kama ni Mtume wa Mweye Ezi Mungu. Hii inathibitisha kuwa yeye ndiye Nabii aliyetajwa na ni Mtume wa Mungu. [5]
- Taurati: Imamu Ridha alitoa ushahidi mwingine kutoka Taurati unaosema, «Nawaona wapanda farasi wawili; ambao ardhi inawang'aria: mmoja wao amepanda punda na mwingine ngamia». Alieleza kuwa yule aliyepanda punda ni Yesu, na aliyepanda ngamia ni Muhammad, akithibitisha Utume wake. [6]
- Zaburi: Kutoka Zaburi ya Daudi, Imamu Ridha alimnukuu Daudi aliyesema, «Ee Mola, mtume (mlete) mfufuaye Sunna baada ya kipindi cha ukimya (kipindi cha kutokuwepo kwa Nabi Isa)». Bila shaka hakuna alifafanua Sunna (sheria mpya za Mungu) baada ya kipindi kirefu cha ukimya isipokuwa Muhammad (s.a.w.ww), na sio Yesu, kwa kuwa Yesu hakupinga Sunna ya Taurati. [7]
- Injili: Imamu Ridha alinukuu kutoka Injili maneno yasemayo; "Mwana wa mwanamke mwema ataondoka, na baada yake atakuja Faraklita (Paracletus au mfariji). Yeye ndiye atakayefanya mambo kuwa mepesi na kufafanulieni kila kitu. Kama nilivyotoa ushuhudia kwa ajili yake, yeye pia atatoa ushuhuda kwa ajili yangu. Mimi nimekuleeni mifano, na yeye atakuleteeni tafsiri yake (Taawili yake)". Akithibitisha utume wake alisema; jina Faraklita hapa ni Mtume Muhammad (s.a.w.w). [8]
Vyanzo vya Hadithi
Matini ya Mjadala huu inapatikana katika vitabu vya Tawhidi[9] na Uyun Akhbar al-Ridha, [10] vilivyoandikwa na Sheikh Saduq (305-381 Hijria). Ahmad bin Ali Tabarsi, aliyeishi katika karne ya sita Hijria, pia naye amenukuu muhtasari wa mjadala huu katika kitabu chake kiitwacho Al-Ihtijaj. [11] Aidha, Allama Majlisi ameinukuu Riwaya hii kutoka katika vitabu vya Sheikh Saduq, na kuiorodhesha katika kitabu chake maarufu Bihar al-Anwar. [12]
Tathmini ya Hadithi
Wanazuoni wa elimu ya rijali, ambao ni wataalamu wa kuchunguza thamani ya wapokezi wa hadithi, wamekuwa na maoni tofauti kuhusiana na mnyororo wa wapokezi wa Hadithi hii. Baadhi yao wamewakubali na kuwakosha kwa uaminifu wapokezi wote wa Hadithi hii, huku wengine wakiwahesabu baadhi yao kuwa ni madhaifu na wasio aminika. [13] Tukiachana na ya hayo, pia Hadihti hii ni mursal, kwa maana ya kwamba; kuna baadi ya wapokezi wa Hadithi hii ambao hwakutajwa ndani ya mlolongo wa wapokezi wake, jambo linaloifanya Riwaya hii kuwa ni dhaifu. [14] Hata hivyo, kuna wanazuoni wanaoamini kuwa; hata kama Hadithi hii ni dhaifu ila ni miongoni mwa Hadithi zinazokubalika. Hii ina maana kwamba, licha ya udhaifu wa mnyororo wa wapokezi wake, ila bado Hadithi hii ni yenye kuaminika. Hii ni kwa sababu ya heshima na hadhi ya Sheikh Saduq, ambaye ni mwanazuoni mashuhuri wa Kishia, na kwa kuwa Sheikh Saduq alikuwa ni maarufu kwa kupokea na kuripoti Hadithi alizokuwa na uhakika tu. Kwa lugha nyengine ni kwamba yeye alikuwa hanukuu Hadithi isipokuwa baada ya kuwa uhakika kwamba Hadithi hizo zinatoka kwa Maasumina. Kwa msingi huo basi, wanazuoni hawa huihisabu Riwaya hii kuwa ni sahihi na kutojali mapungufu yaliomo ndani yake. [15]
Matini na Tafsiri ya Mjadala
Imamu al-Ridha alimwelekea kwa Ra’asu al-Jaaluut na kusema: "Sasa, ni nani atakayekuwa na jukumu la kuuliza maswali? Je, ni wewe au mimi?" Ra’asu al-Jaaluut alijibu: "Mimi nitakuuliza maswali, na nitakubali majibu yako iwapo tu yatakuwa ni kutoka katika Taurati, Injili, Zaburi ya Daudi, au Maandiko Risala (Suhuf) za Ibrahim na Musa." Imamu akakubaliana naya akimwambia: "Usikubali majibu yangu isipokuwa yale yatakayotokana na Taurati ya Musa, Injili ya Yesu, au Zaburi ya Daudi."
Hapo Ra’asu al-Jaaluut akauliza: "Ni jinsi gani utauthibitisha unabii wa Muhammad?" Imamu alijibu: "Ewe Myahudi elewa ya kwamba, Musa bin Imran, Isa bin Maryam, na Daudi, ambao walikuwa ni wawakilishi (makhalifa) wa Mungu duniani, walikiri juu ya unabii wa Muhammad."
Kusikia hayo Ra’asu al-Jaaluut akataka uthibitisho wa kauli ya Musa bin Imran. Imamu akamwambia: "Je, unakubali kwamba Musa aliwausia Wana wa Israeli kwa kusema: ‘Mtume atatokea kutoka kwa ndugu zenu; basi muaminini na mutii mtume huyo?’ Ikiwa unakubali kuwa; kama kuna undugu kati ya Wana wa Israeli (Yaakobo) na Ismaili basi utakuwa unatokana na Ibrahim (a.s), je, unakubali kuwa Wana wa Israeli hawakuwa na ndugu wengine isipokuwa watoto wa Ismail?"
Ra’asu al-Jaaluut akasema: "Ndiyo, haya ni maneno ya Musa na hatuyakatai." Imamu Ridha akamwuliza: "Je, kati ya ndugu wa Wana wa Israeli, je, kuna mtume mwingine isipokuwa Muhammad (s.a.w.w) ambaye amedai Utume?" Ra’asu al-Jaaluut akajibu: "Hapana." Imamu Ridha akaendelea: "Je, mnasema hivi hili si sahihi?" Ra’asu al-Jaaluut akakubali kwa kusema: "Ndiyo, ni sahihi, lakini ningependa unithibitishie ukweli huo kutoka katika maandiko ya Taurati." Imamu Ridha akamjibu: "Je, unakata kudai kwamba Taurati haikunadi ikisema kwamba: 'Mwangaza ulitoka kutoka Mlima Sinai, ikatuangaza kutokea Mlima Seiri, na kutudhihirikia kutoka Mlima Parani?'"
Ra’asu al-Jaaluut akakubali na kusema: "Ninafahamu maneno haya, ila sifahamu tafsiri yake."
Imamu Ridha akamjibu akimwambia: "Nitakueleza tafsiri yake. Ama kauli ya 'Mwanga uliotoka kutoka Mlima Sinai' inaashiria wahyi wa Mungu uliofunuliwa kwa Musa (a.s) kwenye Mlima Sinai. Na kauli isemayo; Ikatuangaza kutokea Mlima Seiri inaashiria mlima huo ambapo Mungu alizungumza na Isa bin Maryam (a.s). Na kauli ismayo 'Ikutudhihirikia kutoka Mlima Parani ' inaashiria mlima mmoja wa milima ya Makkah, ambao umbali wake hadi Makkah ni masafa ya mwendo wa siku moja."
Imamuu Aliongeza kuwa kusema: "Kulingana na maneno ya nabii Isaya, kama ulivyosema wewe na marafiki zako, Taurati inasema: 'Ninaona wapanda wanyama wawili: mmoja amepanda mnyama mwenye masikio marefu (punda), na mwingine amepanda ngamia.' Je, unajua ni nani anayepanda punda na ni nani anayepanda ngamia?" Ra’asu al-Jaaluut alijibu: "Sijui, tafadhali tueleze."
Imamu Ridha akasema: "Yule anayepanda punda ni Isa (a.s), na yule anayepanda ngamia ni Muhammad (s.a.w.w). Je, unakataa ukweli huu uliomo ndani ya Taurati?"
Ra’asu al-Jaaluut alijibu: "Hapana, siwakatai wala kupinga ukweli huo." Imamu Ridha akamuuliza: "Je, hivi unamjua Nabii Habakuki?" Ra’asu al-Jaaluut akajibu: "Ndio, namjua." Imamu Ridha akaendelea: "Habakuki amesema yafuatayo ambayo hata kitabu chako pia kinaeleza hivyo hivyo, nayo ni kama ifuatavyo: Mungu alileta 'ufafanuzi' kutoka Mlima Paran, na mbingu zikajaa tasbihi (za utajo wa Mwenye Ezi Mungu) zitokazo kwa Muhammad na umma wake. Wapanda farasi wake (jeshi lake) linaweza kupita baharini na nchi kavu, sentensi ambayo inaashiria mamlaka ya umma wake majini na nchi kavu. Baada ya kuanguka kwa Yerusalemu, Mungu atatuletea kitabu kipya, ambacho ni Furqan. Je, unaamini juu haya?" Ra’asu al-Jaaluut akajibu: "Haya ni maneno ya Habakuki na hatuwezi kuyakataa."Imamu Ridha akaendelea: "Daudi katika Zaburi yake, ambayo wewe pia unaisoma, amesema: 'Ewe Mungu, mtume (mteuwe) mtume atakaye simamisha Sunna (atakaye kuja na sheria) baada ya kipindi cha ukimya (baada ya kuondoka Nabi Isa).' Je, unamjua nabii mwingine zaidi ya Muhammad (s.a.w.w) ambaye ameanzisha na kudumisha sheria (za Mungu) baada ya kipindi cha ukimya?"
Ra’asu al-Jaaluut alisema: "Haya ni maneno ya Daudi, nami nakubaliana nayo na wala sikatai maneno yake, lakini yeye alikuwa akimkusudia Yesu, na wakati wa Yesu ndio kipindi hicho cha ukimya." Imamu Ridha akamjibu: "Kwali hapo umefeli na umekosea. Yesu hakupingana na sheria ya Torati (hakuja na sheria mpya); badala yake, aliendelea kuzingatia sheria hiyo hadi Mungu alipomchukua. Injili, inasema: 'Mwana wa mwanamke mwema atakwenda, na baada yake atakuja Faraklita (Paracletus' au mfariji), naye ndiye atakayesahili yalio mazito na kusahilisha yaliyo magumu, naye ndiye atakaye kufafanulieni kila kitu, na kama mimi nilivyo shahidi kwa ajili yake, naye pia atakuwa ni shahidi kwa ajili yangu. Mimi nimekuleteeni mifano, naye akuleteeni tafsiri (ta’awili).' Je, unaamini juu ya haya yaliyomo ndani ya Injili?" Ra’asu al-Jaaluut akasema: "Ndiyo, sikatai maneno hayo." Imamu Ridha akaendelea kumwambi: "Ewe Ra’asu al-Jaaluut, ninataka kukuuliza kuhusiana na nabii wako Musa bin Imran." Ra’asu al-Jaaluut akajibu akimwambia: "Uliza, tafadhali." Imamu akauliza: "Kuna uthibitisho gani unaothibitisha unabii wa Musa?"
Myahudi akasema: "Musa alileta miujiza ambayo manabii waliomtangulia hawakuweza kuleta. Kwa mfano, aliipasua bahari, alibadilisha fimbo kuwa nyoka, aligonga jiwe na kupelekea jiwe hilo kutirirka maji, aliweka mkono wake hadharini ukiwa mweupe na wenye kung’ara, na akaja na miujiza mingine ambayo wengine hawakuweza na wala hawatawezi kuwa nayo."
Imamu Ridha alimjibu akisema: "Ni kweli Musa alithibitisha unabii wake kwa kuleta miujiza ambayo wengine hawakuweza kuifanya. Sasa, kutakuja mtu mwengine atakayekuwa na madai ya utume, kisha akaja na miujiza ambayo wengine watashinda kuifanya, je katika hali kama hiyo, hivi itakuwa ni wajibu kwako kumwamini mtu huyo?
Myahudi akasema: "Hapana, kwa sababu Musa alikuwa na hali ya kipekee na alikuwa karibu sana na Mungu. Hivyo basi, kila nabii atakayekuja na madai ya unabii, ni lazima atupe miujiza kama ile aliyokuja nayo Musa. Na si wajubu kwetu kumwamini mtu yeyote yule anayedai kuwa ni nabii isipokuwa kama atakuwa na miujiza kama ya Musa." Imamu akamjibu: "Sasa, kwa nini mnawaamini manabii waliomtangulia Musa, licha ya kwamba hawakuchana bahari, hawatoa chemuchemu kumi na mbili za vyanzo vya maji kutoka kwenye jiwe, hawakuwa na 'mkono mweupe' kama Musa, na hawakubadilisha fimbo zao kuwa nyoka?" Myahudi akajibu: "Nilisema kwamba, iwapo watatoa miujiza inazothibitisha unabii wao, hata ikiwa ni tofauti na miujiza ya Musa, basi itakuwa ni wajibu kwetu kuwaamini." Imamu akaendelea: "Kwa hivyo, kwa nini huamini utume wa Yesu bin Maryam, licha ya kuwa yeye alifufua wafu, alitibu vipofu na wenye mabalanga, aliumba ndege kupitia udongo na kwa kuupuliza tu udongo huo, na udongo huo ukawa ndege hai kwa idhini ya Mwenye Ezi Mungu?"
Ra’asu al-Jaaluut akasema: "Wanasema kwamba ni kweli Yesu alifanya mambo hayo, ila sisis hatukushuhudia matendo hayo kwa macho yetu." Imamu akasema: "Je, kwani wewe umeshuhudia miujiza ya Musa? Je, taarifa kuhusu miujiza hii haijakufikia kupitia watu wa kuaminika?" Ra’asu al-Jaaluut akajibu: "Ndiyo, hivyo ndivyo ilivyo." Imamu akaendelea: "Basi mijuza ya Isa bin Maryam pia imekufikia kwa mtindo huo huo, miujiza ambayo imekufikia kupitia taarifa nyingi (mutawatir) na sahihi zisizoweza kadhibika. Kwa nini basi mnakubaliana na miujiza ya Muasa na mnamwamini yeye, ila hamwamini Yesu?" Hapo Ra’asu al-Jaaluut alikosa majibu. Imamu akaendelea: "Kadhalika, hali ndivyo ilivyo kwa unabii wa Nabii Muhammad (s.a.w.w) pamoja na manabii wote waliotumwa na Mwenye Ezi Mungu. Moja ya miujiza ya Mtume wetu ni kwamba; Yeye alikuwa yatima na maskini, akichunga kondoo kwa malipo. Hakuwa na elimu rasmi na hakuwahi kwenda kujuifunza kwa mwalimu yeyote. Licha ya hayo yote, Yeye amekuja na Qur’ani ambayo inasimulia kwa ufasaha kabisa matukio na habari za manabii na maisha yao, Qur’ani ambayo inatoa habari za watu wa waliopita, wajao na mwishowe habari za Siku ya Kiyama. Si tu imenukuu habari zao peke yake, bali pia imezungumzia siri zao pamoja na matendo yao waliyokuwa wakiyatenda majumbani mwao, na ndani mna miujiza isiyohesabika."
Raasu al-Jaluut akajibu kwa kusema, "Kwa mtazamo wetu, uthibitisho wa suala la Yesu na Muhammad bado haujapatikana, na hivyo hatuna ruhusa ya kuamini jambo ambalo halijathibitishwa." Imamu Ridha akajibu, "Ikiwa ni hivyo, je, shahidi aliyetoa ushahidi kwa ajili ya Yesu na Muhammad (s.a.w.w) alitoa ushahidi wa uongo?" Hapo Myahudi akabaki kimya bila kutoa jibu lolote. [17]
Sherehe Za Kisa cha Raasu Al-Jaalut
Kuna takriban sherehe tisa zilizo andikwa juu ya Hadithi ya Raasu al-Jaaluut. Miongoni mwa sherehe hizo ni: [18]
- Al-Fawaidu al-Radhawiyya: kilichoandikwa na Qadhi Said Qummi.[19] Imamu Khomeini alikidherehesha kitabu hiki kwa kutoa maelezo kuhusiana na matini yake.[20]
- Sherhe Hadith Raasu al-Jaaluut: kilichoandikwa na Mulla Abdul Sahib Muhammad Ibn Ahmad Naraqi, aliyefariki mwaka wa 1297 Hijria.[21]
- Mirza Qumi, aliyefariki mwaka wa 1231 Hijria.
- Ahmad Ahsaei, aliyefariki mwaka wa 1243 Hijria.
- Muhammad Ibn Muhammad Hassan Mash’hadiy Tusi, aliyefariki mwaka wa 1257 Hijria.
- Muhammad Ismail Ibn Muhammad Jafar Isfahani, aliyefariki mwaka wa 1280 Hijria.
- Mulla Abdul Rahim Ibn Muhammad Yunus Damawandiy.[22]