Nenda kwa yaliyomo

Mjadala kati ya Imamu Ridha (a.s) na Abu Qurra

Kutoka wikishia

Mjadala kati ya Imamu Ridha (a.s) na Abu Qurra (Kiarabu: مناظرة الإمام الرضا عليه السلام مع أبي قرّة) ni mazungumzo ya kina ya kielimu yanayohusu suala la uwepo wa Mungu katika mfumo wa kiwiliwili. Katika mjadala huu, Abu Qurra anashikilia imani ya kwamba; Mungu ana mwili, anaweza kuonekana, yuko katika mahali maalum, na ana ulimi kama wanadamu autumiao katika kuzungumza na kuwasiliana na viumbe mbali mbali.

Abu Qurra amejitahidi kuthibitisha imani yake kwa kutumia Aya za Qur'ani na Hadithi, akilenga kuthibitisha na kuhalalisha mawazo yake. Kwa upande mwingine, Imamu Ridha (a.s) amekosoa vikali maoni haya, akitegemea Aya za Qur'ani na hoja za kimantiki ili kupinga dhana ya kumfananisha Mungu na viumbe wake. Kulingana na ripoti ya Ahmad Tabarsi, Abu Qurra alishindwa kujibu hoja za Imamu Ridha (a.s) katika mjadala huu, na hatimae hoja na imani yake ikawa ni duni mbele ya mantiki ya Imamu.

Hadithi hii muhimu inapatikana katika vitabu vya Al-Kafi kilichoandikwa, Ya'qub Kulayni, Al-Tawhidi kilichoandikwa na Sheikh Saduq na Ihtijaj kilichoandikwa na Ahmad Tabarsi. Vitabu hivi vinatoa mwanga tosha juu ya mjadala huu wa kihistoria na jinsi ulivyodhihirisha umuhimu wa tafakuri ya kina katika masuala ya imani juu ya uungu wa Mwenye Ezi Mungu.

Mukhtasari wa Ripoti ya Mjadala

Kwa mujibu wa maelezo ya Safwan bin Yahya, msimulizi wa mjadala huu, ni kwamba; mazungumzo ya mjadala huu yalifanyika kupitia ombi la Abu Qurra , mwanazuoni na kiongozi wa wafuasi wa Mujassima (wale wanaoamini kwamba Mungu ana mwili). [1] Abu Qurra alimuomba Safwan aombe ruhusa kwa Imamu Ridha (a.s) ili apate fursa ya kukutana naye. [2] Baadhi ya vyanzo vinamuhisabu Abu Qurra  kama ni mmoja wa waandishi wa ripoti za habari na ni waandishi wa zama za Imamu Ridha (a.s). [3]

Katika mazungumzo ya mjadala huo, Abu Qurra alianza kwa kuuliza maswali yanayo husiana na sheria za kifiq-hi, ingawa maswali hayo hayakuandikwa na wala hayamo ndani matini ya Hadithi ya tukio hili. [4] Alipomaliza maswali yake ya kifiq-hi, alileta mjadala unaohusiana na sifa za Mungu. Aliendeleza hoja zake kwa kutumia Aya za Qur'ani na Hadithi ili kuthibitisha kwamba Mwenye Ezi Mungu huzungumza kama azungumzavyo wanadamu, anaweza kuonekana, na yuko ndani ya mahali maalumu. [5]

Imamu Ridha (a.s) alijibu maswali hayo kwa kutumia Aya za Qur'ani na kubainisha udhaifu wa maoni ya Abu Qurra. [6] Kulingana na Hadithi hii, Abu Qurra alishindwa kutoa majibu ya kuridhisha katika kujibu maswali ya Imamu Ridha (a.s) na hakufanikiwa kujibu hoja hata moja miongoni mwa zilizowekwa mbele yake. [7]

Sehemu ya Mjadala

  • Abu Qurra: Imepokewa kwamba: "Mungu ameugawa uwezo wake wa kuzungumza na kuona kati ya manabii wawili, ambapo amempa Musa uwezo wa kuzungumza na Muhammad (s.a.w.w) uwezo wa kuona."
  • Imamu Ridha: Je, hivi Mwenye Ezi Mungu hakuseme: لا تُدْرِكُهُ الْأَبْصارُ (macho hayawezi kumuona), [8] "Wa la وَ لا يُحِيطُونَ بِهِ عِلْماً (viumbe haviwezi kumjua kwa undani), [9] لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْ‏ءٌ (hakuna kitu kinacho fanana na Yeye). [10] Je hivi kuna mwengine aliyemwona Mungu isipokuwa Muhammad (s.a.w.w)?
  • Abuqurah: Hapana.
  • Imamu Ridha: Je, Iweje atokee mtu anayedai kuwa ametumwa kwa na la Mwenye Ezi Mungu na kuwalingania watu kwa amri ya Mungu, akiwapa habari ya kwamba: "Macho hayawezi kumuona Mungu" na "viumbe haviwezi kumjua kwa undani" na "hakuna kitu kama Yeye", kisha kusema: "Nimeona Mungu kwa macho yangu na nimeweza kumjua kwa undani, na wala hakuna kitu kinacho fanana Naye, kisha yeye mwenyewe awambie watu kwamba; mimi nimemuona Mungu kwa macho yangu, ninamtambua juu chini, Naye ana umbile lifananalo na wanadamu"?!
  • Abu Qurra: Mungu amesema: لَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرى (na kwa hakika, alimuona kwa mara nyengine tena katika mteremko mwengine (katika daraja nyengine)). [11]
  • Imamu Ridha: Aya inayofuata inaeleza kile alichokiona Mtume: ما كَذَبَ الْفُؤادُ ما رَأى (moyo haukukihisabu kuwa ni cha uwongo kile kilicho onya na macho (ya Muhammad)); [12] hii ina maana kwamba moyo wa Muhammad haukukidhibisha kile kilicho onwa na macho. Kisha baada ya hapo Mungu akapasha habari kuhusiana na kile alichokiona Muhammad na kusema: لَقَدْ رَأى‏ مِنْ آياتِ رَبِّهِ الْكُبْرى (Mtume aliona baadhi ya ishara kuu za Mola wake), [13] na bila shaka "ishara za Mungu" si "Mungu Mwenyewe". Aidha, Mungu amesema: وَ لا يُحِيطُونَ بِهِ عِلْماً (watu hawawezi kumjua Mungu kwa undani). [14] Ingekuwa kuna uwezekano wa kumuona Mungu kwa macho, basi tungemjua kiundani kabisa.
  • Abu Qurra: Basi,  unaikataa hiyo Hadithi niliyokutajia?
  • Imamu Ridha: Ikiwa Hadithi zinapingana na Qur’ani, mimi sitakuwa na jisi isipokuwa kuzikaa tu; zaidi ya hayo, Waislamu wanaafikiana kwamba haiwezekani mtu kuweza kumjua Mungu kwa undani. [15]

Vyanzo

Mazungumzo ya Imamu Ridha (a.s) na Abu Qurra yaliripotiwa kwa mara ya kwanza katika kitabu cha Al-Kafi, kilichoandikwa na Ya'qub al-Kulaini. [16] Kitabu hichi kimeigawa Hadithi ya majadiliano haya katika sehemu mbili tofauti, zenye mwonekano wa Hadithi mbili: Hadithi ya kwanza imepewa jina la Abṭāl al-Ruʾya (Utenguzi wa Nadharia ya Kuonekana kwa Mungu) [17], wakati Hadithi ya pili ikichukua jina la «Arshun wa Kursiyyun» [18]. Ila Hadithi zote mbili zinarejea kwenye kwenye nukuu moja.

Sheikh Saduq ameinukuu Hadithi ya kwanza katika kitabu chake Tawhidi, akirejelea kutoka kwa Ya'qub al-Kulaini; [19] huku Ahmed bin Ali Tabarsi, mwanahadithi na mtaalamu theoliojia kutoka madhehebu ya Shia aliyeishi karne ya sita Hijria, amenukuu mjadala wote kiukamilifu katika kitabu chake kiitwacho Al-Ihtijaj. Kitabu hichi kinajumuisha mazungumzo yote ya mjadala huo, kwa kina zaidi kuliko hata ilivyo ripotiwa na Kulaini katika Hadithi zake mbili alizohadithia ndani ya kitabu chake. [20]

Pia, Hadihti hii imeripotiwa katika Bihar al-Anwar, kilichoandikwa na Allama Majlisi, ambapo mjadala huu umetajwa kwa kunukuliwa kutoka kwa; Ya'qub al-Kulaini, [21] Sheikh Saduq [22] na Ahmad Tabarsi. [23]

Matini na Tafsiri Yake

Safwan bin Yahya anasema kwamba Abu Qurra, mtaalamu fani ya Hadithi na rafiki wa Shubruma, alimuomba kupanga mipango ya kukutana na Imamu Ridha (a.s). Safwan akakubaliana na ombi hilo na akamwomba ruhusa Imamu Ridha (a.s) ili amkaribishe nyumabi kwake. Abu Qurra akatumia fursa hiyo na akafika mbele ya Imamu Ridha (a.s). Abu Qurra alipofika alianza kumuuliza Imamu Ridha (a.s) maswali kuhusiana na masuala ya halali na haramu, hukumu za faradhi mbali mbali, na hukumu za kifiq-hi. Baada ya kumaliza maswali hayo, alielekeza maswali yake kwenye uwanja wa masuala ya Tawhid. Alimuuliza Imamu akimwambia: "Ewe bwana wangu roho yangu iwe ni fidia kwako, tafadhali nieleze jinsi Mungu alivyomzungumza na Musa."

Imamu Ridha (a.s) akajibu akisema: "Mungu na Mtume wake wanajua zaidi kuhusiana na lugha aliyotuka katika mazungumzo hayo, iwe Kisiria (Syriac) au Kiebrania." Abu Qurra akauashiria ulimi wake akisema; swali likusudia ulimi huu kama ulimi na sikusudii lugha, Imamu Ridha (a.s) akajibu akisema: "Subhanallah! Mawazo haya ni ya kushangaza! Mungu hafanani na viumbe wala hajazungumzi kama wazungumzavyo wanadamu. Kwani hakuna kitu kinachofanana Naye; Yeye si msemaji wala mtendaji kama watendavyo viumbe." Abu Qurra akauliza: "Hivyo basi, mazungumzo hayo yalikuwaje?" Imamu Ridha (a.s) akajibu: "Maneno ya Muumba si kama maneno ya viumbe; hayategemei matendo ya midomo wala lugha. Mungu hutamka kwa kutumia amri isemayo: Kuwa bila shaka mazungumzo ya Mungu na Musa yalijiri kulingana na matakwa Yake." Abu Qurra akaendelea kuuliza: "Una maoni gani juu ya vitabu vya mbinguni?"

Imamu Ridha (a.s) akajibu akisema: "Torati, Injili, Zaburi, Furqani, na kila kitabu kilichoteremshwa ni maneno ya Mungu, yaliyoletwa kama na mwongozo kwa wanadamu. Hata hivyo, vitabu hivi ni muhdath (vilivyo umbwa ambayo hapo mwanzo havikuwepo) na haviwezi kuwa Mungu, bali ni maneno ayasemayo ukumbusho aupelekao kwao; kama Qur’ani inavyosema: (ما يَأْتِيهِمْ مِنْ ذِكْرٍ مِنْ رَبِّهِمْ مُحْدَثٍ إِلَّا اسْتَمَعُوهُ وَ هُمْ يَلْعَبُونَ  ; Watu walipokumbushwa kwa kuletewa ukumbusho kutoka kwa Mola wao, ila huusikiliza huku wakiufanyia mchezo). (Taha, 113). Mungu ndiye chanzo cha vitabu vyote vilivyoteremshwa."

Abu Qurra akauliza: "Je, vitabu hivi vitachakaa na kutoweka?"

Imamu Ridha (a.s) akamjibu: "Waislamu wanakubaliana kwamba kila kitu kisichokuwa Mungu kitachakaa na kutoweka. Kila kitu kingine kisichokuwa Yeye ni kitendo Mungu. Hivyo; Torati, Injili, Zaburi, na Furqani ni vitendo vyake. Je, hujasikia watu wakisema: 'Mola wa Qur’ani', hata Qur’ain yenyewe siku ya Kiyama itatamka ikiwaashiria watu hali ya kwamba Mungu ni  mjuzi zaid wa watu hao, siku hiyi Qur’ani itasema: 'Ewe Mola, huyu ni mtu fulani, ambaye amebaki na kiu mchana kutwa (amefunga) na kusImamua usiku (amekesha akisali), basi kubali maombezi (shufaa) yangu kwa ajili yake -hivyo basi elewa kwamba hakuna tofauti kati ya Qur’ani, Torati, Injili, na Zaburi,  vyote havyo ni muhdath (vilivyo kuja baadae) na ni makhluq (vilivyo umbwa), na muumba wao ni yule ambaye hakuna kitu chochote kile kinachofanana Naye. Vitabu hivyo ni mwangaza kwa wenye busara. Hivyo, anayefikiria kwamba vitabu hivi vilikuwepo milele na milele, huyo atakuwa anamaanisha kwamba Mungu si Mtangu wa kale wa pekee, na kwamba neno lake ni la tangu na tangu na linaendelea bila kuwa na mwanzo, hali likiwa halistahiki kuabudiwa."

Abu Qurra akasema: "Kuna simulizi zisemazo kwamba; vitabu vyote vya mbinguni vitafika siku ya Kiyama, ambapo watu wote watakuwa wamesImamua safu moja, kwenye uwanja wenye muinuko mbele ya Mola wa Walimwengu, wakitazama vitabu hivyo vikirejea kwa Mwenye Ezi Mungu, kwa sababu vitabu hivyo vinachukuliwa kuwa ni sehemu ya Uungu wa Mwenye Ezi Mungu na vinatokana naye." Imamu Ridha (a.s) akamjibu: "Hii inafanana na imani ya Wakristo juu ya Yesu, wakisema kuwa yeye ni roho ya Mungu na ni sehemu yake, na hivyo yeye (Isa) atarudi kwake. Vile vile, Wamajusi wanaamini moto na jua kuwa sehemu ya Mungu na vitarejea kwake. Lakini Mola wetu ni mtukufu mno, ametakasika na sifa za kuwa na sehemu au kugawika kwa vigao mbali mbali. Utofauti na kuwa na miundo ni sifa za viumbe vinavyogawika kupitia vigao mbali mbali, kwani kila kilichogawika kinaweza kufikiriwa, na wingi au uchache ni viashiria kuwepo kwa Muumba wa viumbe."

Abu Qurra akasema: "Imesimuliwa kwamba: 'Mwenye Ezi Mungu aligawa mazungumzo na uwezo wa kuona kati ya manabii wawili: Mazungumzo akapewa Musa (a.s), na uwezo wa kuona akapewa Muhammad (s.a.w.w).'" Imamu Ridha (a.s) alijibu: "Je, si Muhammad (s.a.w.w) ndiye aliye wafikishia wanadamu na majini ujumbe kutoka kwa Mwenye Ezi Mungu, na kusema kwamba; macho hayawezi kumwona Mungu, elimu ya viumbe haiwezi kumzunguka, na hakuna kitu kinachofanana Naye?"

Abu Qurra akakubali akisema: "Ndiyo, ni yeye."

Imamu Ridha (a.s) akaendelea: "Basi inawezekanaje mtu huyohuyo ambaye amekuja na ujumbe wa Mungu kwa ajili ya viumbe wote, akisema kwamba ametumwa na Mungu, akiwalingani kwa amri Yake, na kuwambia kuwa macho hayawezi kumwona Mungu, elimu haiwezi kumzunguka, na hakuna kitu kinachofanana naye, kisha huyo huyo aseme: Nilimwona Mungu kwa macho yangu, na ninamfahamu kwa undani kabisa, na kwamba Yeye (Mungu) ana sura ya kibinadamu? Je, huu si upotoshaji? Hata wazandiki (mitume bandia) hawakuthubutu kumzulia Mungu jambo jama hilo, kiasi ya kwamba adai kuwa ameleta ujumbe kutoka kwa Mungu kisha akaseme kinyume cha ujumbe aliokuja nao."

Abu Qurra alisema: "Mwenyezi Mungu amesema: لَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرى (na kwa hakika, alimuona kwa mara nyengine tena katika mteremko mwengine (katika daraja nyengine)). (Najm, 13)." Imamu Ridha (a.s) akajibu: "Aya inayofuata inafafanua kile alichokiona Mtume: ما كَذَبَ الْفُؤادُ ما رَأى (moyo haukukihisabu kuwa ni cha uwongo kile yalicho kiona macho (ya Muhammad)). Mwenyezi Mungu anaendelea kufafanua zaidi kwa kusema: لَقَدْ رَأى‏ مِنْ آياتِ رَبِّهِ الْكُبْرى (Mtume aliona baadhi ya ishara kuu za Mola wake), [13] na bila shaka "ishara za Mungu" si "Mungu Mwenyewe". Pia, Mwenyezi Mungu amesema: 'Watu hawawezi kumzunguka kielimu.' Ikiwa macho yangemwona Mungu, basi elimu ingemzunguka, na kumfahamu kwa undani kungelipatikana."

Abu Qurra akauliza: "Kwa hiyo, unakataa hadithi hizi?"

Imamu Ridha (a.s) akajibu: "Hadithi yoyote inayopingana na Qur'ani inapaswa kukataliwa. Waislamu wamekubaliana kuwa elimu ya waja haiwezi kumzunguka Mwenye Ezi Mungu, macho hayawezi kumuona, na hakuna kitu kinachofanana Naye. Hapo Abu Qurra akauliza kuhusiana na Aya inayosema: سُبْحانَ الَّذِي أَسْرى‏ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِنَ الْمَسْجِدِ الْحَرامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى‏ ; Ametakasika Yule aliyemchukua mja Wake wakati wa usiku, kutoka Msikiti Mtakatifu hadi Msikiti wa Al-Aqsa' (Isra, 1).

Imamu Ridha (a.s) akamjibu: "Mwenyezi Mungu alimchukua Mtume usiku huo ili kumuonesha baadhi ya ishara Zake, kama inavyo elezwa katika Aya hiyo. Ishara hizi ni tofauti na Mungu Mwenyewe. Mwenyezi Mungu ametaja wazi sababu ya tendo hilo na kuonesha ishara hizo, na Mwenye Ezi Mungu katika Qur’ani amesema: فَبِأَيِّ حَدِيثٍ بَعْدَ اللَّهِ وَ آياتِهِ يُؤْمِنُونَ‏ ; Basi ni kipi (ni maneno gani) baada ya maneno ya Mungu na ishara Zake watakachoamini?' (Jaathia, 6). Hii inaonyesha kwamba ishara hizo ni tofauti na Mungu Mwenyewe, Aya na ishara zake ni tofauti na Yeye mwenyewe."

Hapo Abu Qurra aliuliza: "Basi, Mungu yuko wapi?" Imamu Ridha (a.s) akajibu: "'Wapi' ni swali linaloashiri mahali fulani, na ni swali la muulizaji aliepo anaye muulizia mwngine ambaye hayupo, likimaanisha uwepo wa kiumbe mahali pamoja na kutokuwepo mahali pengine. Mwenye Ezi Mungu yupo kila mahala na hakuna mahala asipo kuwepo; hakuna anayeweza kumzunguka au kumhudhuria. Yeye yupo kila mahali, ndiye MsImamuizi, Muumba, na Mlinzi wa mbingu na ardhi."

Abu Qurra akauliza: "Je, kwani Yeye hayuko juu ya mbingu, akiwa mbali na viumbe vyote?" Imamu Ridha (a.s) akajibu: "Mwenyezi Mungu ni Mola wa mbingu na ardhi. Yeye ndiye anayeabudiwa mbinguni na ardhini, na ndiye anayeumba katika matumbo ya mama zenu kwa kadiri Atakavyo. Yeye yupo pamoja nanyi popote mlipo. Ni Yeye aliyeshughulikia mbingu wakati zilikuwa katika hali ya moshi, na Yeye ndiye aliyefuma mbingu saba. Yeye ndiye Mwenye Ezi Mungu aliye juu ya Arshi, akiwa na mamlaka na usImamuizi kamili wa ulimwengu. Alikuwapo kabla ya viumbe, na atabaki kuwa hivyo daima, bila kubadilika wala kusafiri au kuhama kama viumbe walivyo."

Abu Qurra akauliza: "Kwa nini wakati wa kuomba dua huwa mnainua mikono yenu juu kuelekea mbinguni?" Imamu Ridha (a.s) akajibu: "Mwenye Ezi Mungu amewafundisha waja wake namna ya kumwabudu kupitia njia tofauti, na Ameweka sehemu maalum za ibada ambazo waja wake huzitumia kwa nia ya kumkaribia Mola wao. Waja wake hulazimika kufuata kanuni za ibada, matendo, na maombi. Amewafundisha unyenyekevu na heshima katika maombi yao. Amewaamrish kuelekea au kuhudhuria kwenye Kaaba katika baadhi ya ibada zao ikiwemo; Sala Hija na Umra. Amewata kuwa na unyeyekevu katika dua na maombi yao na akawataka kufungua mikono yao, kuiinua na kuielekeza mbinguni wakati wa dua zao. Amewataka kufanya hivyo ili kuonyesha hali ya unyenyekevu, udhaifu,uduni wao, na kujenga utambuzi wa kutambua mamlaka ya Mola wao."

Abu Qurra akauliza: "Je, watu wa duniani wako karibu zaidi na Mwenye Ezi Mungu au malaika?"

Imamu Ridha (a.s) alijibu: "Ikiwa unazungumzia ukaribu kwa muktadha wa umbali wa kijiografia au kiumbo, ni muhimu kuelewa kwamba kila kitu kilichomo ulimwengu ni matokeo ya matendo ya Mungu. Na wala hakuna kizuizi cha kijiografia kinachoweza kumzuia Mungu kutekeleza matakwa Yake. Mungu anasImamuia mambo yote ya viumbe wa juu na wa chini kwa usawa kabisa, bila hitaji la juhudi, muda, au msaada wowote. Hata hivyo, kama swali lako linahusiana na ukuruba wa mja kwa Mola wake kupitia nyenzo ya ibada, basi elewa kwamba; kimsingi ukurubu wa kuwa karibu zaidi na Mungu, huwa unahusiana na kiwango cha utiifu na unyenyekevu wa mja mbele Yake. Mtume Muhammad (s.a.w.w) alieleza kwamba hali inayo pmelekea mja kuwa karibu zaidi ya na Mola wake, ni pale mja anapokuwa katika hali ya kusujudu. Pia, kuna Hadithi inayosimulia kisa malaika wanne walioko katika pande nne za ulimwengu -juu, chini, mashariki, na magharibi- ambao walikutana pamoja na kila mmoja akawa anamuuliza mwengie juu jukumu lake, na wote walijibu kwa pamoja: "Tumetumwa na Mungu kwa lengo utumwa maalum." Hii inaonyesha kuwa ukaribu huu ni wa hadhi na heshima, na si wa kipimo cha kijiografia au kupita vipimo kulinganisha masafa.

Hapo Abu Qurra aliuliza: "Je, hivi unakubali kwamba; Mungu ni 'mhamiliwa' (mbebwa)?" Imamu Ridha (a.s) akamjibu: "Kila kibebwacho kinahitaji msaada au usaidizi kupitia kitu chengine. Hivyo, neno 'kubeba' linaashiria hali ya upungufu na hali maana ya ukamilifu. Na mbebaji ni mtendaji na sifa ya mtendaji ni na sifa nzuri kulingana na matumizi ya neno hili kwenye muktadha huu. Pia kama kuna asemaye kuwa Mungu yupo juu au chini, au kudai kuwa yupo juu kitu au chini ya kitu, huyo atakuwa amemsifu Mwenye Ezi Mungu kwa sifa asizostahiki nazo. Bila shak, Mungu ametukuka na majina bora zaidi, kama Mungu asevyosema katika Qur'ani: وَ لِلَّهِ الْأَسْماءُ الْحُسْنى‏ فَادْعُوهُ بِها ; Na Mwenye Ezi Mungu ni mwenye majina bora kabisa, basi mwombe kupitia majina hayo (Al-A'raf, 180). Wala Mwenyezi Mungu hajawahi kusema katika vitabu vyake kuwa Yeye ni 'Mbembwa au Mhimiliwa.' Badala yake, Yeye ndiye Mhimili wa mbingu na ardhi, na kila kitu kisichokuwa Mungu huhimiliwa na Mwenye Ezi Mungu. Hatujasikia mtu yeyote anayemheshimu Mungu akitumia neno 'Mhamiliwa au Mbebwa' katika dua zake. Je uliwahi kumsikia mcha-Mungu fulani akimwomba Mola wake kwa kusema “Ewe Mbebwa au Mhimiliwa”?

Abu Qurra akasema: "Basi, je, hivi unakataa Hadithi isemayo kwamba: 'Pale Mungu anapo kasirika, Malaika wanaobeba kiti chake cha enzi huengezekewa na uzito mabegani mwo kutokana na hasira hizo, nao papo hapo huanguka wakimsijudia Mola wao. Na pale hasira zinapompunguka, uzito huo hupungua, kisha Malaika hao hurejea kwenye nafasi zao?"

Abu al-Hassan (a.s) akamwambia: "Hebu nieleza kuhusiana na hasira za Mwenyezi Mungu, Mtukufu na Mjuzi, kuanzia pale alipomlaani na kummkasirikia Iblisi hadi sasa na mpaka Siku ya Kiyama. Je, hivi Mwenye Ezi Mungu ataendelea kuwa na hasira dhidi ya Iblisi na wafuasi wake, au kuna kipindi fulani aliridhika nao, au labda katika kipindi kijacho atakuja kuridhika nao?"

Abu Qurra akajibu: "Bila shaka, Mwenyezi Mungu bado ana hasira dhidi yao wote, na ataendelea kuwa hivyo." Imamu Ridha akasema: “Ni lini basi aliridhika nao ili uzito wa Arshi yake upunguke na usiwaelemee Malaika wake, hali ya kwamba wewe unaelewa wazi kuwa Yeye bado yumo katika hasira zake hizo dhidi ya Ibilisi na wafwasi wake”? Kisha akamwambia: “Ole wako, wawezaje kuwa na jeuri ya kumsifu Mwenye Ezi Mungu kwa sifa za mabadiliko kutoka hali moja kwenda hali nyengine, na kwamba Yeye hupitiwa na mabadiliko yafananayo na yale ya viumbe wake? Mwenye Ezi Mungu ametakasika na sifa hizo, Yeye yukama alivyo huku viumbe wakiondokewa na sifa mbali mbali, Naye habadiliki pale viumbe wapitiwapo na mabadiliko mbali mbali.

Safwani ananukuu hitimisho la mjadala huu akisema: “Hapo Abu Qurra alipigwa na butwaa, wala hakupata jibu la kumjibu Imamu (a.s), hatiamae akainuka na kuondoka. [24]

Mada Zinazo Husiana

Rejea

Vyanzo