Kuritadi

Kutoka wikishia
Hitilafu kutengeneza picha ndogo:

Kuritadi (Kiarabu: الارتداد) ni kutoka katika dini ya Kiislamu kwa mtu aliyekuwa Muislamu. Waislamu wanamuita murtadi mtu ambaye ametoka katika Uislamu. Kuritadi kunatimia kwa mtu kukana uwepo wa Mwenyezi Mungu, haki ya Mtume wa Uislamu, dini ya Uislamu na mambo ya dharura katika dini kama vile Swala na Swaumu na vilevile kuvunjia heshima matukufu ya dini kama al-Kaaba, Qur'an na kadhalika. Murtadi amegawanywa katika vigawanyo viwili, na kila kigawanyo kina hukumu zake maalum:

  • Al-Murtadd al-Milli: Mtu aliyekuwa mkristo kisha baada ya kubaleghe akasilimu na kuingia katika Uislamu lakini baadaye akaritadi na kuwa kafiri.
  • Al-Murtadd al-Fitri: Ni mtu ambaye amezaliwa katika Uislamu yaani baba na mama yake au mmoja kati ya wazazi wake ni Waislamu kisha yeye baada ya kubaleghe akaritadi na kutoka katika Uislamu.

Kila mmoja kati ya wawili hawa ana hukumu zake maalumu za kisheria. Kwa mujibu wa mtazamo mashuhuri baina ya mafakihi, adhabu ya Murtadd Fitri ni kuuawa; lakini adhabu ya Murtadd wa Milli hupatiwa fursa ya kutubu na kurejea katika dini na endapo hatatubu basi atauawa. Mwanamke aliyeritadi (awe muritadi milli au fitri) adhabu yake siyo kuuawa lakini madhali hajatubia ataendelea kufungwa jela.

Kuwa najisi murtadi na kutojuzu kuoana naye ni hukumu nyingine zinazohusiana na kuritadi. Baadhi wanaamini kwamba, sababu ya kuweko adhabu kama hizi kwa kuritadi ni kuzuia Waislamu kuwa na upuuzaji na suala la kushikamana na dini na kutodhoofishwa itikadi za kidini na wapinzani wa Uislamu.

Utambuzi wa maana na aina zake

Kuritadi ni istilahi ya kifikihi na mafakihi wametaja maana yake ni mtu kutoka katika Uislamu. [1] Inaelezwa kuwa, Muislamu ambaye anatoka katika Uislamu na kuachana na dini hii ni murtadi. [2] Katika vitabu vya fikihi kuritadi kunajadiliwa katika milango mbalimbali ya tohara, Swala, Zaka, Swaumu, Hija, biashara, ndoa na urithi. [3] Katika baadhi ya vitabu vya fikihi kuna mlango maalumu na wa kujitegemea unajulikana kama "Mlango wa kuritadi" ambao unajadili maudhui hii. [4]

Aina za kuritadi

Makala asili: Al-Murtadd al-Milli na Al-Murtadd al-Fitri

Kuna aina mbili ya wenye kuritadi na kila mmoja ana hukumu maalumu zinazomhusu: [5] Murtadi wa kwanza ni mtu aliyetoka kwenye Uislamu ambaye kiasili amezaliwa muislamu ]6]; yaani wazazi wake baba na mama au mmoja kati yao ni waislamu. [7] Kisha akatoka katika Uislamu. [8] Aina ya pili, ni murtadi ambaye kiasili siyo muislamu kwa maana kwamba, alikuwa mkristo kisha akasilimu na kuingia katika Uislamu halafu baadaye akaritadi. [9] Murtadi wa kwanza anajulikana kwa jina la al-Murtadd al-Fitri na wa pili al-Murtadd al-Milli.

Masharti na njia za kuthibiti kuritadi

Kuritadi kunathibiti kwa kauli na kwa vitendo pia:

Kuthibiti kuritadi kwa kauli ni kwa sura hii kwamba, mtu aseme maneno na kutoa matamshi ambayo yanaonyesha kuwa ametoka katika dini ya Uislamu. Kwa mfano aseme: Hakuna Mungu, au mtukufu Muhammad sio Mtume au Uislamu sio dini ya haki. [10] Kukana dharura za kidini na mambo ya lazima katika Uislamu nako ni katika aina hii. [11] Makusudio ya dharura ya dini ni kitu ambacho uwepo wake katika Uislamu uko wazi kwa namna ambayo hakuna haja ya kutafuta hoja za kuthibitisha hilo na Waislamu wote wanalikubali hilo; kama vile wajibu wa Swala, Swaumu na Hija. [12]

Kuritadi kwa vitendo ni mtu kufanya jambo la kukufurisha kwa makusudi na kwa kufahamu kwamba, ni la kukuukufurisha. Kwa mfano, asujudie sanamu, au aabudu mwezi au jua au "avunjie heshima kwa wazi na dhahiri" matukufu ya kidini kama al-Kaaba, Qur'an na kadhalika. [13]

Ayatullah Fadhil Lankarani anaamini kuwa, kutilia shaka na kuleta utata kuhusiana na tawhidi (kumpwekesha Mwenyezi Mungu) na Utume, hakupelekei mtu kuritadi madhali mtu hajakana na kukanusha wazi mambo hayo. [14] Allama Sha'arani anasema kuwa, mtafiti ambaye anatafuta hoja, endapo atakumbwa na shaka na akawa ni mwenye kutafuta dini ya haki, shaka yake haimfanyi akufuru na kuritadi katika kipindi cha kufanya kwake uhakiki na utafiti; kwa sharti kwamba, asitamke na kukana hilo kwa ulimi. [15]

Mafakihi wanasema kuwa, masharti ya kuthibiti kuritadi ni akili, kubaleghe, kusudio na hiari (kufanya hilo kwa hiari na bila ya kulazimishwa). [16] Kwa mujibu wa masharti haya, endapo kichaa atatamka neno la kukukufurisha au mtu ambaye hajabaleghe hilo haliwezi kumfanya ahesabike kuwa ameritadi na kutoka katika Uislamu. [17] Kadhalika mtu ambaye atatamka maneno ya kukufurisha bila ya kukusudia au amelazimishwa kufanya hivyo, hahesabiwi kama amekufuru. [18] Kwa mujibu wa fat’wa ya mafakihi ni kwamba, kuritadi kunathibitika kwa njia mbili:

Njia ya Kwanza: Kukiri murtadi mwenyewe juu ya kuritadi kwake.

Njia ya Pili: Ushahidi bayana nao ni watu wawili waadilifu kutoa ushuhuda juu ya kuritadi mtu fulani. [19]

Shahidi Thani anasema, kama watu wawili walitoa ushahidi wa kuritadi mtu fulani, kisha mtu mhusika mwenyewe akajitokeza na kusema, walikosea, maneno yake yanakubalika. Kadhalika kama mtu atasema kuwa, alilazimishwa kufanya hivyo (kutoa maneno au kufanya jambo la kumfanya aritadi) na kuweko ishara katika maneno yake. [20]

Mifano ya kuritadi katika ulimwengu wa kiislamu

Katika vitabu vya tafsiri na vya historia kumeripotiwa mifano ya kuritadi watu katika zama za Bwana Mtume(s.a.w.w). [21] Miongoni mwao wapo watoto wawili wa kiume wa Abu-Hasin aliyekuwa muansari. Wawili hawa waliritadi baada ya kulinganiwa Ukristo na kundi moja na hivyo wakajiunga na Ukristo. [22] Mtume aliwalaani na wakatambulika kuwa watu wa kwanza kuritadi. [23] Uqbah bin Abi Mu'it ambaye alikuwa mmoja wa shakhsia wakubwa wa Quraish, alitamka shahada mbili ili Mtume ale chakula chake; lakini baada ya muda akijibu takwa na ombi la rafiki yake alimtemea mate Mtume na akaritadi. Bwana Mtume (saww) alitoa amri ya kuuawa kwake baada ya Bwana huyo kukamatwa katika vita vya Badr. [24]

Ummu Hakam binti wa Abu Sufiyan na Fatma dada wa Ummu Salama mke wa Mtume ni miongoni mwa wanawake ambao waliritadi na kutoka katika Uislamu katika zama za Bwana Mtume. Baada ya Fat’h Makka (kukombolewa Makka) Ummu Hakam alisilimu tena na kuingia katika Uislamu. [25]

Sayyied Abdul Karim Musawi Ardabili, ametoa mifano katika kitabu chake cha fikihi cha Fiq’h al-Hudud wal-Taazirat kuhusiana na watu walioritadi katika zama za Bwana Mtume(s.a.w.w) na Maimamu. [26] Katika miaka ya hivi karibuni kuna watu waliuawa kwa tuhuma za kuritadi au walihukumiwa kuritadi ambao ni:

  • Ahmad Kasrawi kutokana na kutusi na kuvunjia heshima Uislamu na Ushia katika jarida la “Shiegera” mwaka 1324 Hijria Shamsia aliuawa na wafuasi wawili wa kundi la Fedaiyan Eslam kwa tuhuma za kuritadi. [27]
  • Salman Rudshie: Mwaka 1989, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Ruhullah Khomeini alitoa fat’wa ya kuuawa murtadi Salman Rushdie baada ya kuandika na kuchapisha kitabu chenye anuani ya Aya za Shetani "Satanic Verses" kinachomvunjia heshima Mtume (s.a.w.w). [28]. Sababu ya kutolewa hukumu hiyo ni kuritadi Salman Rushdie. [29]

Hukumu za kuritadi

Baadhi ya hukumu za kuritadi ni:

Adhabu ya murtadi

Adhabu ya Murtadi Milli (mkristo aliyesilimu kisha akaritadi) kama hatofanya toba na vilevile Murtadi Fitri (aliyezaliwa katika Uislamu kwa baba na mama au mmoja ya wazazi wake kisha akaritadi) ni kifo; [30] lakini kwa upande wa mwanamke anatiwa jela mpaka atubu au afe. [31] Hata hivyo murtadi fitri ambaye ni mwanamke na murtadi milli awe ni mwanamke au mwanaume akitubia toba yao inakubaliwa. [32]

Baadhi ya mafakihi wametoa mitazamo mingine mkabala wa fat'wa mashuhuri kuhusiana na hukumu za kuritadi; miongoni mwao ni Abdul-Karim Musawi Ardabili [33] na Muhammad Is'haq Fayadh miongoni mwa Marajii Taqlidi ambao wametambua hukumu ya murtadi fitri mwanaume kuwa ni sawa na hukumu za aina nyiingine ya kuritadi. Kwa maana kwamba, wametoa fat'wa ya kwamba, murtadi fitri mwanaume kama atatubu, basi hatoadhibiwa. [34] Abdallah Jawad Amoli naye amesema, mtu ambaye atakumbwa na utata kutokana na kufanya uhakiki na akatoka katika dini (akaritadi), adhabu ya kuuawa haitekelezwi dhidi yake; kwa sababu kwa mujibu wa hadithi, adhabu za kisheria (kama kupigwa mijeledi, kukatwa mkono, kuuawa na kadhalika) kwa kuweko utata (shubha) haipaswi kutekelezwa. [35]

Falsafa ya adhabu ya kuritadi

Katika kubainisha na kutoa ufafanuzi kuhusiana na falsafa ya adhabu ya kuritadi kumeashiriwa hekima mbalimbali:

  • Kwa kuwa Uislamu ni msingi wa mfumo na nidhamu ya kisiasa, kuritadi na kuonyesha dhahirii hilo, ni sababu ya kudhoofika Uislamu na kusambaratika nidhamu na mfumo wa kisiasa ambao unasimama kwa msingi wake. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana utawala wa Kiislamu una wadhifa wa kukabiliana na suala ya kuonyesha dhahiri kuritadi na kuainisha adhabu kwa kitendo hicho. [36]
  • Kwa kuwa Uislamu ni sababu ya mfungamano katika jami, kuritadi na kuonyesha dhahiri hilo, hupelekea kutokea hali ya kutetereka na msambaratiko katika jamii. Mahdi Bazargan ananukuu kauli ya Profesa Marcel Boisard, mhadhiri wa kitivo cha sheria katika Chuo Kikuu cha Geneva: "Sababu ya Uislamu kuwa mkali katika suala la adhabu kwa murtadi huenda inatokana na kuwa, katika mfumo wa kiutawala na kiidara wa jamii za Kiislamu, kumuamini Mwenyezi Mungu ni kitu ambacho hakina upande wa kiitikadi na kibinafsi tu, bali ni katika vipengee vya mfungamano wa umma na misingi ya utawala, kiasi kwamba, kukosekana kwake, uimara wa jamiii husambaratika na jamii kutodumu na ni kama vile kuua nafsi, fitina na ufisadi ambavyo haiwezekani kuvivumilia."[37]
  • Mtu kuwa Muislamu maana yake ni kufungamana na kushikamana na nidhamu na mfumo maalumu na kuukubali utambulisho maalumu; kwa msingi huo kuritadi ni aina fulani ya kukengeuka na kuwa dhidi ya utambulisho jumla wa jamii ambao unapelekea kuvurugika amani na utulivu katika jamii. [38]
  • Sababu ya Uislamu kuwa mkali kuhusiana na adhabu ya kuritadi ni kwamba, tusiione na kuihesabu dini kwamba, ni jambo dogo na hivyo tuwe na umakini katika kuichagua. [39]
  • Kuadhibiwa murtadi kunazuia wapinzani wa Uislamu kuingia katika Uislamu kwa ajili ya kuidhoofisha dini hii na kisha baadaye watoke katika Uislamu; kama ambavyo huu ulikuwa mpango wa maadui wa Uislamu wakati wa kudhihiri Uislamu na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana kukawekwa adhabu dhidi ya murtadi. [40]

Hukumu zingine

Kwa mujibu wa vyanzo vya fikihi, baadhi ya hukumu za kuritadi ni kama ifuatavyo:

  • Najisi: Kuritadi kutamfanya mhusika kuwa najisi. [41] Murtadi Fitrid mwanamke na Murtaddi Milli, awe mwanamke au mwanaume, kama atatubu hutoharika. [42]
  • Kuvunjwa ndoa: Kama baada ya ndoa na kabla ya kufanya tendo la ndoa, mmoja kati yao mwanamke na mwanaume akaritadi, ndoa hiyo inabatilika. [43] Ikiwa baada ya ndoa na baada ya kufanya tendo la ndoa mwanaume akaritadi na akawa ni Murtadd Fitri, ndoa inabatilika; lakini kama mwanamke ataritadi na akawa ni Murtadd Fitri au Murtaddi Milii, kama mpaka kumalizika eda (eda ya talaka) akawa hajatubia, ndoa inabatilika; kinyume na hivyo (kama atatubia) ndoa itakuwa sahihi na vilevile kama mwanaume atakuwa ni Murtadd Milli (ambaye asili yake sio Mwislamu). [44] Kuritadi kunazuia ndoa ya muislamu na murtadi. [45]
  • Urithi: Kuritadi kunamfanya mhusika asimrithi muislamu. [46]

Kuritadi katika kanuni na sheria za Iran

Katika sheria ya adhabu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kuritadi hakujatajwa kama ni kosa na uhalifu na kwa msingi huo, hakujaanishwa adhabu dhidi yake, [47] hata hivyo baadhi wakitumia kifungu cha 167 cha katiba, wanalitambua hilo kuwa ni kosa. [48]