Kuondoa Najisi

Kutoka wikishia

Kuondoa najisi (Kiarabu: إزالة النجاسة) maana yake ni kufuta na kusafisha. Ni wajibu kuondoa najisi kutoka katika mwili, nguo ya mwenye kusali, mwenye kufanya tawafu, sehemu ya kusujudia, msikitini, katika Qur’an, kwenye Haram za Maimamu (a.s), mwili na sanda ya maiti, sehemu ya kutilia udhu na kuoga, hata hivyo sio sharti kufanya hivyo kuwe ni kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa mujibu wa mtazamo na nadhari mashuhuri ya mafaqihi wa Kishia, kuondoa najisi kutoka katika mwili wa mnyama ni miongoni mwa mambo yanayosafisha na pale sehemu ya mwili wa mnyama inaponajisika, mwili wa mnyama huo husafika kwa kutoa uchafu ma najisi hiyo.

Utambuzi wa maana na umuhimu

Kuondoa najisi maana yake ni kupangusa na kusafisha najisi kutoka katika kitu ambacho kimegusana na moja ya najisi kumi (damu, mkojo, kinyesi, manii, mzoga, mbwa, nguruwe, kafiri, pombe na fuqqa’) au kugusa kitu kilichonajisika (kitu ambacho kimenajisika kutokana na kugusana na najisi). [1]

Kuondoa na kusafisha najisi kumezungumziwa zaidi katika milango ya tohara na Sala, [2] na katika kufanya hivyo kwa nia ya kujikurubisha si sharti [3].

Kuondoa najisi kunafanyika kwa kutumia moja ya vitoharishi kama vile maji, ardhi, na jua. [4] Pia, kwa mujibu wa nadharia mashuhuri ya mafaqihi wa Kishia, mwili wa mnyama ambaye umekuwa na najisi kwa kugusana na najisi au umenajisika, husafika na kutoharika kwa kuondolewa najisi yenyewe. [5]

Hukumu

Inapendekezwa kuondoa uchafu kutoka kwa kila kitu ambacho kinaweza kutumika [6] na pia ni wajibu katika baadhi ya matukio kama vile:

  • Miskiti: Kutoharisha na kuondoa najisi kutoka msikitini ni wajibu mara moja [7] na haijuzu kuchelewesha kutekeleza wajibu huo. [8] Kwa hiyo, inapotokea mgongano wa faradhi nyinginezo kama vile Sala ambayo ina wakati (wakati wake upo wa kutosha), wajibu wa kuondoa najisi unatangulizwa mbele ya wajibu wa Sala hiyo. [9] Kwa mujibu wa fat’wa za mafakihi wa Shia, kusafisha na kutoharisha najisi kutoka msikitini ni wajibu Kifai (wajibu ambao wakifanya baadhi unawaondokea wengine), [10] na sio maalumu kwa mtu ambaye ameunajisi msikiti; bali ni wajibu kwa watu wote. [11] Hoja inayotumiwa na baadhi ya mafakihi katika hukumu ya wajibu wa kuondoa najisi katika misikiti ni Aya inayosema: Hakika washirikina ni najsi, kwa hivyo wasiukaribie Msikiti Mtakatifu. [12] Wamesema kuwa, katika hukumu hii hakuna tofauti baina ya msikiti mtakatifu (wa Makka) na misikiti mingine. [13]
  • Sehemu ya kusujudia: Kwa mujibu wa mtazamo na nadharia mashuhuri, kuondoa najisi sehemu ya kusujudia (ambayo mwenye kuswali anaweka paji la uso wake juu yake) ni mojawapo ya masharti ya kusihi Sala. [14] Abu Salah Halabi, mmoja wa mafaqihi wa Kishia, ametambua kuwa wajibu suala la kuondoa najisi katika viungo saba vya kusujudia. [15]
  • Sala: Kuondoa najisi kutoka katika mwili hata kucha na nywele na kutoka katika nguo ni wajibu kwa ajili ya Sala na ni sharti mojawapo la kusihi Sala. [16] Pia katika Sala ya ihtiyati (tahadhari), kulipa kadha ya tashahudi, sehemu ya kusujudia na vilevile katika sijida ya kusahahu ni wajibu kuondoa najisi kutoka katika mwili au nguo. [17]
  • Tawafu: Haijuzu kufanya tawafu (kuzunguka Kaaba) na nguo na mwili wenye najisi. Kwa muktadha huo, ni wajibu kwa Muhrim (aliyevaa vazi la Ihramu) kuondoa najisi kutoka katika mwili na nguo. [18] Kwa mujibu wa Yusuf Bahrani ni kwamba, Ibn Hamzah mmoja wa mafaqihi wa Kishia, yeye ametambua kuwa ni makuhuru kufanya tawafu na nguo na mwili wenye najisi. [19]
  • Qur’an na maeneo ya kufanya ziara ya Maimamu (a.s): Ni wajibu kusafisha na kuondoa najisi katika Qur'an, maeneo ya kufanya ziara ya Maimamu (a.s) na kila kitu ambacho kinaheshimiwa katika dini ya Kiislamu na imekatazwa kukivunjia heshima. [20]
  • Mwili na sanda ya maiti: Ni wajibu kuondoa na kusafisha najisi kutoka katika mwili wa maiti na sanda yake iliyonajisika hata kama atakuwa ameshawekwa kaburini. [21] Kwa mujibu wa Swahib al-Jawahir na Muhaqqiq Ardabil ni kwamba, ni wajibu kuondoa najisi kutoka katika mwili wa maiti kabla ya kuzikwa. [22]
  • Viungo vya udhu na ghulsi: Ni wajibu kuondoa najisi katika viungo vya udhu na ghusli. [23] Kwani tohara ya viungo vya udhu na ghusli (josho) ni katika masharti ya kusihi udhu na ghusli. [24]