Mutahhirat
- Makala hii inahusiana na wasifu kuhusu mafuhumu na maana ya kifikihi na hivyo haiwezi kuwa kigezo cha amali na matendo ya kidini. Kwa ajili ya amali za kidini, rejea katika vyanzo vingine.
Mutahhirat (Kiarabu: المطهرات) ina maana ya vitu vinavyotoharisha. Hii ni istilahi ya kifikihi ambayo hutumiwa kwa vitu vinavyoondoa najisi kama vile maji. Vitu vinayotoharisha vimegawanyika katika makundi kadhaa na kila moja kati ya vitoharishi hivi husafisha na kuondoa kiini cha najisi kwa masharti ambayo yameelezwa katika vitabu vya fikihi.
Baadhi ya vitu vinavyotoharisha ni maji, ardhi, jua, istihala (kubadilika utambulisho wa najisi na kisha kuwa chenye kutoharisha kama mbwa akifa na kisha akabadilika na kuwa udongo), kupinduka hali (kubadilika pombe na kuwa siki), kuhama, kusilimu, kufuata, na kuondoa kiini cha najisi.
Maana ya kifikihi ya Mutahhir (kinachotoharisha)
Mutahhirat ni vitu ambavyo kupitia kwavyo najisi huondolewa. [1] Vitu hivi ambavyo vinajulikana kwa jina la vitoharishi au vitu vinavyotoharisha vimegawanyika katika mafungu kadhaa na wanazuoni wa fikihi wamebainisha idadi yake ambayo inafikia mpaka 21.
Katika vitabu vya ufafanuzi wa sheria za sheria (Tawdhih al-Masail) vitoharishi vifuatavyo vimetajwa: Maji, ardhi, jua, istihala (kubadilika utambulisho wa najisi na kisha kuwa chenye kutoharisha kama mbwa akifa na kisha akabadilika na kuwa udongo), kupinduka hali ya kitu (kwa mfano kubadilika pombe na kuwa siki), kuhama, kusilimu, kufuata, kuondoa kiini cha najisi, kutoweka Mwislamu, kupungua theluthi mbili za juisi ya zabibu mbivu, kutoka damu kiwango kinachojulikana kwa mnyama aliyechinjwa na kumtoharisha mnyama aliyezoea kula kinyesi. [3]
Kila moja kati ya vitu vinavyotoharisha kina hukumu zake na kwa kutimia masharti hupelekea kutoharika vitu vilivyonajisika. Zifuatazo ni baadhi ya hukumu za vitu vinavyotoharisha:
Maji
- Makala Asili: Maji
Maji yanasafisha na kuondoa najisi (yanatoharisha) [4] kwa sharti kwamba, yawe halisi, yawe tohara, baada ya kuosha kiini cha najisi kiondoke, yasiwe mudhafu (yawe maji halisi). [5] Kuna aina kadhaa za maji kama: Maji yanayotiririka (yanayotembea), maji ya kuru na maji machache ambapo baadhi ya hukumu zake zinatofautiana. [6]
Ardhi
Ardhi kama yenyewe itakuwa tohara na vilevile kavu inatoharisha vitu kama nyayo na viatu; kwa sharti kwamba, kiini cha najisi kiondoke kama vile damu, mkojo au kilichonajisika kama vile udongo ulionajisika ambao umegandamana katika sehemu za nyayo au viatu kwa kutembea juu ya ardhi au kusugua juu yake. [7]
Jua
Jua linatoharisha ardhi, majengo na mfano wake kama vile milango, madirisha ya majengo yakinajisika vivyo hivyo hutoharisha misumari iliyopigiliwa ukutani na hiyo ni kwa masharti sita. [8]
Kubadilika na Kupinduka
Istihala maana yake ni kubadilika utambulisho wa najisi na kuwa kitu kingine kama mbao kuwa majivu au moshi (baada ya kuungua). [9] Mabadiliko au kupinduka katika Fiqhi kunajulikana pia kama mchakato wa kubadilika pombe na kuwa siki. [10] Baadhi ya mafakihi wameitambua hali hii kwamba, ni istihala. [11]
Kupungua Theluthi Mbili za Juisi ya Zabibu Mbivu
Mafaqihi wanasema kuwa, ni haramu kunywa maji ya zabibu yaliyochemeshwa. Baadhi yao wanasema ni najisi pia. [12] Vyovyote itakavyokuwa, kama maji ya zabibu yatachemshwa na theluthi zake mbili zikapungua, yanatoharika na ni halali kunywa kwa sharti kwamba, yasiwe yanalewesha. [13]
Kuhama
Kuhama maana yake ni damu ya binadamu au mnyama anayetoka damu kwa kasi wakati wa kuchinjwa ikihama kwenda katika mwili wa mnyama asiyetoka damu kwa kasi na ikahesabika kuwa ni katika damu yake na hii inaitwa intiqal “kuhama”. Katika hali hii damu hii ni safi kama damu ya mbu anayonyonya kutoka katika mwili wa mwanadamu na hivyo kuwa sehemu ya damu yake. [14]
Uislamu
Kafiri akisilimu (akitamka shahada yaani akisema “Ash hadu an laa ilaaha ila llah wa ash hadu anna Muhammadan Rasulullah) anakuwa Mwislamu na hivyo anatoharika. [15]
Kufuata
Kufuata maana yake ni kutoharika najisi kwa njia ya kutoharika kitu kilichonajisi kama vile kafiri akisilimu na kuingia katika Uislamu, watoto wake ambao hawajabaleghe nao wanatoharika kwa kumfuata baba. Kadhalika kama pombe itabadilika na kuwa siki chombo nacho kitatoharika. [16]
Kumtoharisha Mnyama Anayekula Vinyesi
Mkojo na kinyesi cha mnyama ambaye nyama yake ni halali kuliwa aliyezoea kula vinyesi vya binadamu ni najisi na ili kumtoharisha ni lazima kumzuia mnyama huyo kwa muda kutokana na kula vinyesi kiasi ambapo hatoitwa mnyama anayekula vinyesi, na alishwe malisho tohara kwa muda huo. Hata hivyo muda unatofautiana kulingana na aina ya mnyama. [18]
Kutoweka Mwislamu
Mwili wa mwislamu ukinajisika au nguo yake na kitu chake kingine kama vile vyombo, godoro n.k. ambavyo viko katika milki yake kisha akatoweka pamoja na vitu hivyo, vitu hivi vinahukumiwa kuwa ni tohara. [19]
Kutoka Damu Kiwango Kinachojulikana kwa Mnyama Aliyechinjwa
Mnyama aliyehalali kuliwa akichinjwa kwa njia ya kisheria na ikatoka kwake damu kwa kiwango cha kawaida kinachojulikana, damu iliyobaki katika mwili wake itakuwa tohara. [20]