Suratu al-Qadri

Kutoka wikishia

Suratu al-Qadri (Kiarabu: سورة القدر أو إنا أنزلناه ): Ni Sura ya tisini na saba ya Qur’ani tukufu ilioko katika juzuu ya 30 ya Qur’ani tukufu, na mojawapo ya Sura zilizo shuka katika mji wa Makka. Jina Qadri limetokana na Aya zake za mwanzo ambazo zinazungumzia kushuka kwa Qur'an katika usiku wa Qadri (Usiku Wenye Cheo) na umuhimu wa usiku huo. Suratu al-Qadri inazungumzia juu ya ukuu, fadhila na baraka za usiku wa Qadri na kushuka kwa Malaika wa rehema katika usiku huo. Mashia wanatumia maudhui ya Sura hii kuthibitisha umuhimu wa uwepo uwendelevu wa Imam Maasum (a.s) duniani humu hadi siku ya Kiyama. Miongoni mwa amali muhimu zinazosisitizwa kuhusiana na Suratu al-Qadri, ni kukithirisha kuisoma Sura hii katika sala za kawaida, sala zisizo za faradhi, pamoja na kuisoma mara elfu katika usiku wa Lailatu al-Qadri katika mwezi wa Ramadhani. Inasemekana kuwa Sura bora zaidi baada ya Suratu al-Fatiha kusomwa katika sala za faradhi ni Suratu al-Qadri na Suratu al-Tawhid.

Utambulisho

Uhusiano wa jina

Sura hii imepewa jina la "Qadri" kwa sababu ya kule Mwenye Ezi Mungu kuuarifisha usiku wa Lailatu al-Qadri kuwa ndio usiku ambao Mwenye Ezi Mungu alishusha ndani yake, na kuuelezea umuhimu wake katika Aya za mwanzo za Sura hiyo. Jina nyingine la Sura hii ni "Inna Anzalnaa", jina ambalo linatokana na kule Sura hii kuanza kwa ibara hiyo. [1]

Namba ya sura na mahali ilipoteremka

Sura ya Qadr ni moja ya Sura za Makkah na ni Sura ya ishirini na tano aliyo teremshiwa bwana Mtume (s.a.w.w). Hii Sura ni Sura ya tisini na saba kulingana na mpangilio wa sasa wa Msahafu, nayo iko katika Juzuu ya thelathini ya Qurani. [2] Kutokana Riwaya fulani, baadhi ya wafasiri wanaona kuwa Sura hii iliteremka Madina. Sababu ya kushuka Sura kunatokana na ndoto ya bwana Mtume (s.a.w.w), ambapo yeye akiwa usingizini aliwamuona watu wa Bani Umayya wakipanda juu ya mimbari yake, jambo ambalo lilipelekea yeye kuhuzunika sana na kusikitika; hapo ndipo Suratu al-Qadri iliteremka ili kumtuliza bwana Mtume (s.a.w.w). [3]

Idadi ya Aya na sifa zake nyingine

Suratu al-Qadri ina Aya tano, maneno thelathini na nne, na herufi mia moja na kumi na nne. Sura hii ni moja ya Sura fupi ukilinganisha urefu wake na Sura ziitwazo “Mufassalaatu” “Sura refu”, na ni Sura ya kundi la kati na kati “Awsaat” za Qurani na ni miongoni mwa Sura ndogo. [4]

Maudhui

Kiujumla maudhui kuu za Suratu al-Qadri zilizotajwa ndani yake ni; kushuka kwa Qur'ani katika usiku wa Qadri (usiku wenye cheo), utambulisho juu ya ukuu na utukufu wa usiku huo (ambao ni bora kuliko miezi elfu), kushuka kwa Malaika wa rehema na Roho (Jibrilu), kuainisha hatma za watu na baraka za usiku huo. [5] Kulingana na maoni ya wafasiri, kwa upande wa ibada, ustawi wa kheri za usiku wa Qadri ni bora kuliko miezi elfu. Hii ni kwa kuwa lengo la Qur'ani ni kule mwanadamu kuwa na mazingatio maalum na kukaribiana zaidi mbele ya Mwenye Ezi Mungu. Kwa msingi huu, kudumisha usiku wa Qadr kwa kufanya ibada ni bora kuliko ibada katika miezi elfu ya kawaida. [6]

Sababu za kushuka kwake

Kuhusiana na sababu ya kushuka kwa Suratu al-Qardi imeelezwa kwamba; Siku moja bwana Mtume (s.a.w.w) aliwaelezea wafuasi wake kisa cha mtu fulani kutoka ukoo wa Bani Israil ambaye alivaa vazi la kivita kwa miezi elfu moja katika njia ya Mwenyezi Mungu. Wafuasi wake walishangazwa na kisa hicho, baada ya hapo Mwenye Ezi Mungu akaiteremsha Suratu al-Qadri ambayo inaonyesha kuwa; kufanya ibada katika Usiku wa Qadri ni bora kuliko hata kuvaa vazi la kivita kwa muda wa miezi elfu moja katika njia ya Mwenyezi Mungu. [8]

Fungamano kati ya usiku wa Qadri na Bibi Fatima Zahraa (a.s)

Katika baadhi ya Hadithi Usiku wa Qadri unahusishwa na bibi Fatima Zahra (a.s). Katika Hadithi hizo, usiku wa "Layla" ni bibi Fatima (a.s) na “Qadri” ni Mwenye Ezi Mungu, kwa hiyo "Laylatu al-Qadri" katika Hadithi hizo ni bibi Fatima (a.s). Imamu Sadiq (a.s) katika moja ya Hadithi alisema kwamba; mtu yeyote anayemtambua Fatima (a.s) kama anavyostahili na kuelewa nafsi yake, bila shaka yeye ataudiriki Usiku wa Qadri. Na Fatima kaitwa Fatima kutokana na kule watu kuto kuwa na uweza wa kuelewa upeo wa uhakika wake. [9]

Hoja kupitia Surat al-Qadri katika kuthibitisha uwepo wa Imamu Mahdi (a.s)

Kuna hoja zitolewazao ya kwamba Suratu al-Qadri ni uthibitisho wa uwepo wa Imamu wa Zama (Mahdi) (a.s). Katika vyanzo vya Hadithi vya madhehebu ya Kishia, kuna Hadithi fulani zinukuliwazo kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w), Imam Ali (a.s), na Imam Baqir (a.s) zisemazo kwamba; malaika wa Mwenye Ezi Mungu huja duniani katika Usiku wa Qadri na kuwashukia viongozi wa Uislamu baada ya Mtume (s.a.w.w), amabo ni Ali (a.s) na watu kumi na mmoja watokao katika kizazi chake. Kwa hivyo, Waislamu wa Kishia hutumia Suratul Qadri kama ni hoja na ushahidi wa ulazima wa kuwepo kwa Imamu katika nyakati zote hadi siku ya mwisho, kwa hiyo wao hutumia hoja hii katika kuthibitisha uwepo wa Imamu aliye hai katika zama za hivi sasa, naye ni Imamu Mahdi (a.s). Hoja yao ni kwamba; Suala la kushuka kwa Malika na kushusha makadirio na hatima za mwaka unao fuata katika Usiku wa Qadri, si tu kwa ajili ya zama za bwana Mtume (s.a.w.w) peke yake, bali suala hili ni tukio la kila mwaka na kila zama. Kwa hiyo ni wazi kwamba baada ya bwana Mtume (s.a.w.w), Malaika watakuwa wanamshukia mshika nafasi yake baada yake naye ni Imamu Maasumu ambaye ni mwenye kushabihiana naye zaidi kinyenendo na kihadhi. [10] Mashia wakishikamana na kigezo cha kwamba Lailatu al-Qadri ni tukio la kuendelea miaka nenda na miaka rudi, na kwamba usiku huo ni usiku washukao Malaika ndani yake, hilo limepelekea wao kuamaini kwamba; Malaika hao hawawezi kushuka bila ya kuwepo mashukio yenye hadhi kamili, ambapo natija yake ni kukubali ulazima wa kuwepo kwa Imamu katika zama zote hadi kufikia siku ya Kiama. [11]

Maana ya neno “Amri” katika Suratu al-Qadri

Allameh Tabatabai ametoa uwezekano wa aina mbili kuhusiana na maana ya neno amri (امر) katika Suratu al-Qadri. Uwezekano wa kwanza ni kwamba; neno amri linahusiana na ulimwengu wa amri (ulimwengu wa ghaibu), ambapo kulingana kauli hii, maana ya Aya itakuwa ni kwamba; Malaika na Roho hushuka kwa idhini ya Mola wao katika Usiku wa Lailatu al-Qadri na kufikisha kila amri ya kiungu walioamrishwa kuifikisa. Uwezekano wa pili ni kwamba neno “amri امر" litakuwa linahusiana na matukio ambayo yanatarajiwa kutokea, hivyo kwa kauli hii, maana ya Aya itakuwa ni kwamba; Malaika na Roho hushuka Usiku wa Lailatu al-Qadri kwa ajili ya kuchukua jukumu la kupanga na kuendesha mambo na matukio yote yanatarajiwa kutokea katika mwaka unao fuata. [12] Ibn Arabi, katika tafsiri yake, amefasiri akisema kwamba ibara ya "مِنْ كُلِّ أَمْرٍ" inashiria maarifa ya welewa dhana ya uwepo wa kila kitu katika ulimwengu wa viumbwa na viliomo ndani yake, dhati ya Allah, sifa zake, mambo makhususi yanayohusiana naye, sheria, hali mbali mbali, uendeshaji na ushikaji wa hatamu na shemere za kila kitu. [13]

Maana ya neno ruhu katika Surat al-Qadri

Maana ya neno Ruhu (روح) katika aya ya nne ya Surat Al-Qadr ina angalau tafsiri tatu:

  • Baadhi ya wanazuoni wanaamini kuwa neno Ruhu linamaanisha Malaika Jibril.
  • Wanazuoni wengine wanadai kuwa kulingana na muktadha wa Aya isemayo: ((و كَذلِكَ أَوْحَيْنا إِلَيْكَ رُوحاً مِنْ أَمْرِن ; Na hivi ndivyo tulivyokushushia Roho kupitia amri yetu)) [14], neno Ruhu katika Suratu al- Qadri litakuwa na namana ya ufunuo (wahyi).
  • Mtazamo wa tatu kuhusiana na neno Ruhu unasema kwamb; neno hili limaanisha kiumbe mkubwa zaidi ya Malaika. Maana hii inatokana na Hadithi kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s). [15]

Vipengele vya kifiqhi kuhusiana na Surat al-Qadri

Kuwa na mwandamo mmoja dunia nzima

Baadhi ya wanazuoni wakitegemea Aya isemayo: ((انا انزلناه فی لیله القدر)), wanaamini kwamba; Kuonekana au kuandama kwa mwezi katika eneo moja, ni sawa na kuandama mwezi huo ulimwenguni kote. Madai hayo yansema kwamba: kwa kuwa Usiku wa Qadri ni mmoja tu, ambao ndani yake huamuliwa hatima za watu wote duniania nzima ndani ya usiku huo. Ni wazi kwamba haiwezekani kusema kuwa Usiku wa Qadri upo katika sehemu moja tu, na haupo sehemu nyingine duniani. Hivyo basi, Usiku wa Qadri unatokea mara moja ulimwengu mzima, na katika usiku mmoja tu. Hata hivyo, katika kujibu dai hili, imesemwa ya kwaba; Aya hii inahusiana tu na tukio la kushushwa kwa Quran ndani ya Usiku wa Qadri, na wala hakuna ushahidi unaopatikana katika Aya hii, linalounga mkono wazo la Usiku wa Qadri kuwa ni tukio linalotokea mara moja au katika mara tofauti ulimwenguni. [16]

Kusoma Suratu al-Qadri kwenye Sala za Faradhi

Katika moja Hadithi Imamu Swadiq (a.s) amesema: “Mtu anayesoma Suratu al-Qadri katika moja ya sala zake za faradhi, hutajwa huko mbinguni na kuambiwa: Ewe mja wa Mungu! Mwenye Ezi Mungu amekusamehe dhambi zote zilizotangulia hadi kufikia hivi sasa, chukua hatua mpya katika utendaji wa amali zako”. [17] Katika Hadithi nyingine, Imamu (a.s) amesema: Ninamshangaa mtu asiye soma Suratu al-Qadri katika sala zake, ni jinsi gani sala zake zitakubaliwa”. [18] Katika baadhi ya vitabu vya fiqhi, imesisitizwa na kupendekezwa kusoma Surat al-Qadri katika rakaa ya kwanza, na Surat al-Tawhid katika rakaa ya pili ya kila sala, hata kama mwenye kusali atakuwa ameanza kusoma Sura zisizokuwa hizo, mtu anaweza kuachana na Sura hizo na badala yake kusoma Sura mbili hizi zilizopendekezwa. [19]

Kusoma Surat al-Qadri katika Sala za Sunna

Katika baadhi ya Sala za Sunna hunapendekezwa kusoma Surat al-Qadri; nao ni kama vile:

  1. Sala ya Mtume (s.a.w.w): Nayo ni sala yenye rakaa mbili, ambapo katika kila rakaa, husomwa Surat al-Hamd mara moja na Inna anzalnahu mara kumi na tano. [20]
  2. Sala ya bibi Fatima: Nayo ni sala yenye rakaa mbili, ambapo katika rakaa ya kwanza, husomwa Surat al-Hamd mara moja na Inna anzalnahu mara mia moja, na katika rakaa ya pili, husomwa Surat al-Hamd mara moja na Suratu al-Tawhid mara mia moja. [21]
  3. Sala ya Wahsha (Hofu): Nayo ni sala yenye rakaa mbili, ambapo katika rakaa ya kwanza, husomwa Surat al-Hamd mara moja na Ayatu al-Kursi mara moja, na katika rakaa ya pili, baada ya kumaliza kusoma Suratu al-Hamd, husomwa Inna anzalnahu mara kumi. [22]
  4. Sala ya Mwanzo wa Mwezi: Nayo ni sala yenye rakaa mbili, ambapo katika rakaa ya kwanza, baada ya kumaliza kusoma Surat al-Hamd, husomwa Surat al-Tawhid mara thelathini, na katika rakaa ya pili, baada ya kumaliza kusoma Suratu al-Hamd, husomwa Inna anzalnahu mara thelathini. [23]

Kusoma Surat al-Qadri katika nyakati na maeneo mbalimbali

Imepokewa kutoka kwa Imamu Jawadi (a.s), kwamba; mtu yeyote anayesoma Surat al-Qadri na kutimiza mara 76 katika nyakati katika na masaa tofauti ya siku hiyo, Mwenye Ezi Mungu atamuumbia Malaika elfu kwa ajili yake watakao mwandikia thawabu zake kwa muda wa miaka 360, na maombi yao ya kuwombea yeye msamaha yataongezeka mara elfu kwa kipindi cha miaka 2000. Namna ya kusoma Suratu al-Qadri mara 76 katika nyakati tofauti ni kama ifuatavyo:

  1. Mara saba wakati wa kuchomoza alfajiri na kabla ya Sala ya Subuhi, ili malaika wamtumie sala na salamu kwa muda wa siku sita.
  2. Mara kumi baada ya Sala ya Asubuhi, ili awe katika ulinzi wa Mwenye Ezi Mungu hadi usiku.
  3. Mara kumi wakati wa adhuhuri na kabla ya Sala za Nafilah ya adhuhuri, ili Mwenye Ezi Mungu amwangalie kwa jicho la rehema, na afungue milango ya rehema za mbinguni kwa ajili yake.
  4. Mara ishirini na moja baada ya Sala ya Nafilah za adhuhuri, ili Mwenye Ezi Mungu ampe nyumba yenye urefu na upana wa dhiraa themanini Peponi, na awaambie Malaika wamuombee maghufira mpaka Siku ya kusimama Kiyama.
  5. Mara kumi baada ya Sala ya Alasiri, ili apate malipo kwa idadi ya matendo ya viumbe vyote.
  6. Saba baada ya Sala ya Isha, ili awe katika ulinzi wa Mwenye Ezi Mungu hadi asubuhi.
  7. Mara kumi na moja wakati wa kwenda kulala, ili Mwenye Ezi Mungu amteulie Malaika adhimu wa kumtakia maghufira kulingana na idadi ya nywele zake, hadi Siku ya kusimama Kiyama. [24]

Pia Kusoma Surat al-Qadri ndani ya nyusiku za Qadri ni miongoni ya amali muhimu ndani ya nyusiku hizo. Jengine linalo pendekezwa ni kusoma Sura hiyo mara elfu moja ndani ya usiku wa 23 wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambapo faida zake zimeelezwa ndani ya Riwaya mbali mbali. [25] Katika riwaya imeelezwa kwamba; yeyote yule atakayesoma Surat al-Qadri mara saba karibu na kaburi la muumini, Mwenye Ezi Mungu atamtuma Malaika mahali hapo ili amwabudu Mwenyezi Mungu akiwa katika eneo hilo, na thawabu za ibada ya Malaika huyo itakuwa thawabu kwa ajili ya maiti alioko kaburini humo, na pale Mwenye Ezi Mungu atakapomtoa maiti huyo kutoka kaburini huymo, atamuepushia hofu na wasiwasi kupitia Malaika huyo, ili aingie Peponi yake salama usalimini. [26] Marehemu Saduq amenukuu katika kitabu chake Man La Yahduruhu al-Faqih ya kwamba Imamu Ridha (a.s) alisema: "Hakuna mja muumini anayezuru kaburi la nduguye muumini kisha akasoma Surat al-Qadri mara saba akiwa kaburini hapo, isipokuwa Mwenye Ezi Mungu atamsamehe yeye pamoja na mwenye kaburi hilo." 27

Kazi kuhusiana na Suratu Qadri

Kazi za Sanaa

Wengi wa wasomaji wameisoma Sura hii kwa sauti zao zivutiazo. Unaweza kusikiliza visomo hivyo kupitia kiungo kilichopo hapa. Katika sekta ya sanaa ya uchoraji pia kuna kazi kadhaa zinazohusiana na sura hii. Kuna Maonyesho [28] na warsha [29] kadhaa kaitka nyanja ya uandishi na kazi za kaligrafia zinazohusiana na Suratu Qadri yaliomefanyika nchini Iran.

Kazi makhususi za kiuandishi kuhusiana na Surat al-Qadri

Mbali na Surat al-Qadri kutafsiriwa katika muktadha wa tafsiri kamili ya Qur’ani, mara nyingine inaonekana kutafsiriwa kama ni Sura pekee au mara nyingine pamoja na sura nyengine kadhaa. Baadhi ya kazi za kipekee ni pamoja na:

Ubora na sifa makhususi za Surat al-Qadri

Kuna thawabu nyingi zilizoelezwa katika Hadithi, kuhusiana na malipo ya kusoma Suratu al-Qadri. Imenukuliwa katika Hadithi ya kwamba; Sura hii ndio bora zaidi kuliko Sura yoyote ile isomwayo baada ya Suratu al-Fatiha katika sala za faradhi. [35] Imepokewa kutoka kwa Imamu Muhammad al-Baqir (a.s) ya kwamba: "Ubora wa imani ya mtu mwenye kuamini sententensi isemayo: "Inna anzalnahu" pamoja na tafsiri yake, ni kubwa zaidi kuliko yule asiye na imani kama hiyo, kwa kiasi cha ubora wa mwanadamu juu ya wanyama." [36] Katika Hadithi nyingine kutoka kwa Imamu Sadiq (a.s.), imesemwa kwamba: mtu ambaye atasoma Sura ya "Inna anzalnahu" katika moja ya sala zake za faradhi, atanadiwa katika ulimwengu wa ghaibu na kuambiwa ya kwamba: Ewe mja wa Mwenyezi Mungu! Mwenye Ezi Mungu amekusamehe dhambi zote zilizotangulia, hivyo basi anza upya amali zako. [37] Katika moja ya Hadithi nyingine kutoka kwa Imamu Sadiq (a.s), ni kwamba; Sura hii ni moja ya Sura ambazo ndani yake kumetajwa jina kuu la Mwenyezi Mungu (Ismu Llahi al-A’adhamu). [38]"