Nenda kwa yaliyomo

Tahajjud

Kutoka wikishia

Tahajjud (Kiarabu: التَهَجُّد) ni msamiati na neno la Ki-Qur’ani ambalo lina maana ya kuamka usiku kwa ajili ya kusali Sala za usiku, kusoma Qur’ani, kumtaja Mwenyezi Mungu na kuomba maghufira au kuamka na kukesha kwa ajili ya kufanya ibada.[1]

Neno Tahajjud limekuja katika Qur’an katika Aya isemayo: ((وَ مِنَ اللَّيْلِ فَتَهَجَّدْ بِهِ ; Na amka usiku kwa ibada)).[2]Sheikh Swaduq (aliaga dunia: 381 Hijiria) akitegemea ibara au neno la: «فَتَهَجَّدْ» yenye maana ya “Na amka usiku kwa ibada” kama hoja anasema kuwa, Sala ya usiku ni wajibu kwa Mtume (s.a.w.w) na kwa Waislamu ni sunna (mustahabu).[3] Kadhalika katika Aya isemayo:((قُمِ اللَّيْلَ إِلَّا قَلِيلًا ; Simama usiku, ila kidogo tu)). Mtume (s.a.w.w) anaamrishwa akeshe usiku isipokuwa kidogo tu, yaani abakie macho na kufanya ibada sehemu kubwa ya usiku isipokuwa muda mchache tu ndio alale na kupumzika.[4] Ayatullah Makarim Shirazi anasema katika tafsiri yake ya Nemooneh: Mtume alifikia daraja ya Maqam Mahmoud (daraja ya kuombea shifaa siku ya Kiyama) kutokana na Tahajjud na kukesha usiku akifanya ibada.[5]

Katika hadithi kumenukuliwa fadhila za Tahajjud. Miongoni mwa hadithi hizo ni ile iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) ambaye anasema, kukesha usiku (kwa ajili ya ibada) ni sababu ya afya na uzima wa mwili, kunamfurahisha Mwenyezi Mungu, kunamfanya mhusika awe katika rehema na mapenzi ya Allah na kushikamana na akhlaq na maadili ya Mitume (a.s).[6] Kadhalika katika Qur’an imeelezwa kuwa, kuomba msamaha na maghufira wakati wa usiku ni katika sifa maalumu na wachamungu.[7]

Allamah Tabatabai ameandika katika kitabu chake cha Tafsir ya al-Mizan kwamba: Tahajjud katika lugha ina maana ya kuamka baada ya kulala.[8] Kwa mujibu wa Allamah Majlisi ni kwamba, wakati mwingine Sala ya usiku inajulikana pia kwa jina la Tahajjud.[9]

Rejea

  1. Musalai Pur, ((Tahajjud)), uk. 689.
  2. Surat al-Israa, Aya ya 79.
  3. Saduq, Man la yahdhuhuruhu al-faqih, 1413 H, juz. 1, uk. 484.
  4. Surat Zumar, Aya ya 2.
  5. Makarim Shirazi, Tafsiri namune, 1374 S, juz. 12, uk. 225.
  6. Majlisi, Bihar al-anuar, 1403 H, juz. 87. uk. 144.
  7. Tazama: Surat al-Imran, Aya 17; Surat Dhariyat, Aya 17-18.
  8. Tazama: Tabatabai, Al-Mizan, 1390 H, juz. 13, uk. 175.
  9. Majlisi, Biharu al-anuar, 1403 H, juz. 1, uk. 222.

Vyanzo

  • Sadouq, Muhammad Bin Ali, Man La yahdhuruhu Al-faqih, Qom, Daftar Intishar Islami, chapa ya pili, 1413 H.
  • Tabatabai, Sayyid Muhammad Hussein, Al-Mizan fi Tafsir al-Qur'an, Beirut, Muasasatu al-'alamu lil-matubuat, 1390 H.
  • Majlisi, Muhammad Baqir, Bihar al-Anwar, Beirut, Daru Ehiya al-Turrath-e Arabi, chapa ya pili, 1403 H.
  • Masalaipour, Abbas, Danishnameh Jahan Islam, juz. 8, Tehran, Buniyad Deirat Al-Ma’arif Bozorg Islami, 1383 S.
  • Makarim Shirazi, Nasser, Tafsir Namouneh, Tehran, Dar Al-Kutub Al-Islamiyyah, Chapa ya 32, 1374 S.