Ndoa ya Muta’
- Makala hii inahusiana na wasifu kuhusu mafuhumu na maana ya kifikihi na hivyo haiwezi kuwa kigezo cha amali na matendo ya kidini. Kwa ajili ya amali za kidini, rejea katika vyanzo vingine.
Ndoa ya muta’ au Ndoa ya muda (Kiarabu: زواج المتعة أو الزواج المؤقت) ni ndoa ambayo ina muda maalumu na haipo katika sura ya ndoa ya daima. Waislamu wamekubaliana kwamba, ndoa ya aina hii ilikuweko katika zama za Mtume (s.a.w.w). Kwa mtazamo wa Waislamu wa Ahlu-Sunna, Zaydiyya, Ismailiya na Ibadhi ni kwamba, ndoa ya muta’ ilifutwa katika zama hizo hizo za Bwana Mtume na aina ya ndoa hii ni haramu; lakini Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaamini kwamba, katu Mtume hakuifuta ndoa hii bali ilikuweko katika zama zake na hata katika zama za ukhalifa wa Abubakar na ilikuwa ikitambulika kama ndoa halali na masahaba wakifanya muta’.
Kwa mujibu wa baadhi ya vyanzo vya hadithi vya Ahlu-Sunna (Masuni) imenukuliwa ya kwamba, kwa mara ya kwanza Omar ibn al-Khattab ndiye aliyeiharamisha ndoa hii. Wanazuoni wa sheria za Kiislamu (fiq’h) wakitegemea Aya ya muta’ na hadithi zilizonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) na Maimamu watoharifu (a.s) wametoa Fat’wa ya kuhalalisha ndoa ya muda (muta') kama ambavyo wamebainisha sheria na hukumu zake.
Kwa mujibu wa ijmaa (kauli moja) ya wanazuoni wa fikihi wa Kishia ni kwamba, katika kufunga ndoa ya muta’ muda wa ndoa na kiwango cha mahari ni mambo ambayo yanapaswa kubainishwa na kuwa wazi. Katika ndoa ya muta’ kinyume na ndoa ya daima, hakuna talaka; bali unapomalizika muda ulioainishwa au mwanaume kusamehe sehemu ya muda uliobakia, basi hali ya kutengana hutimia.
Baada ya kumalizika muda wa ndoa ya muta’ au mwanaume kusamehe muda uliobakia, kama wanandoa hao wawili waliingiliana kimwili (waifanya tendo la ndoa), ni wajibu kwa mwanamke kukaa eda kwa muda wa hedhi mbili.
Utambuzi wa Maana na Nafasi
Muta’ ni ndoa ya muda ambayo hufungwa baina ya mwanaume na mwanamke na ndani yake muda huainishwa. [1] Ndoa ya muta’ ni miongoni mwa mambo ambayo wanahitalifiana Waislamu wa madhehebu ya Shia na Suni. [2] Aina hii ya ndoa kwa mujibu wa mtazamo wa mafakihi wote wa Kishia ni halali. [3] Na wao wanazungumzia na kubainisha hukumu na sheria za ndoa hii katika mlango wa nikaha moja ya milango ya fikihi. [4]
Katika hadithi zilizonukuliwa kutoka kwa Maimamu wa Kishia kumebainishwa thawabu za kufunga ndoa ya muda. [5] Hata hivyo imekuja katika baadhi ya hadithi ya kwamba, msing’ang’anie na kutilia mkazo katika ndoa ya muta’. [6] Mafakihi wa Shia Imamiya kwa kuzingatia hadithi, sio tu kwamba, wametoa fat’wa ya kulalisha ndoa hii, bali wamekitambua kitendo hiki kuwa ni mustahabu. [7]
Kuhusiana na faida za ndoa ya muda imeelezwa kuwa, ni utatuzi wa matatizo mengi ya mahusiano kijinsia hususan kwa vijana na watu wote ambao kwa vyovyote vile hawawezi kufunga ndoa ya daima. [8] Kadhalika ndoa ya muta’ inaelezwa kuwa ni mbinu athirifu ya kupambana na ufuska na ufisadi mwingine mwingi wa kijamii. [9]
Katika sheria za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia ndoa ya muda imekubaliwa na maudhui yake inazungumziwa katika mlango wa sita wa katiba. [10]
Mitazamo ya Madhehebu za Kiislamu Kuhusiana na Ndoa ya Muda
Maulamaa wa Kiislamu wana mitazamo tofauti kuhusiana na uhalali wa ndoa ya muda: Madhehebu ya Shia Imamiya yanaitambua ndoa ya muda kuwa ni halali, ingawa madhehebu mengine ya Kislamu kama Ahlu-Sunna, [11] Zeydiyah, [12] Ismailiya [13] na Ibadhi [14] yenyewe hayaitambui ndoa hii kama ni halali.
Shahid Thani anasema: Mafakihi wote wa Imamiya wanaitambua ndoa ya muda kuwa ni halali. [15] Wakiwa na lengo la kuthibitisha uhalali wa ndoa ya muta’ wanategemea Aya za Qur’an ikiwemo Aya ya Muta’. [16] Kadhalika wanasema kuwa, kuna hadithi mutawatir zilizopokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) na Maimamu wa Shia Imamiya ambazo zinaeleza kuwa ndoa ya muda ni halali. [17] Madhehebu na makundi mengine ya Kiislamu yanaamini kwamba, ndoa ya muda ilikuwa halali katika zama za Mtume; lakini baadaye hukumu yake ikafutwa na kwa hivyo ni haramu. [18]
Je, Hukumu ya Ndoa ya Muda Imefutwa?
Wanachuoni wa Kiislamu wanakubali kwamba ndoa ya muda ilikuwa halali katika zama za Mtume (s.a.w.w) [19] Katika baadhi ya vyanzo vya hadithi vya Waislamu wa Kisunni, kuna riwaya kutoka kwa Omar ibn al-Khattab, khalifa wa pili, ambaye anakiri kwamba ndoa ya muta’ ilikuwa halali wakati wa Mtume, na yeye ndiye aliyeiharamisha. [20] Haya ni maneno yake ambapo anakiri kwamba, Muta’ mbili zilikuwa halali wakati wa Mtume wa Uislamu; lakini mimi ninaziharamisha na ninawaadhibu wale wanaozifanya: moja ni ndoa ya muta’ na nyingine muta’ ya Hija. [21]
Wakitegemea hadithi hizo, Shia Imamiyyah wanaamini kwamba ndoa ya muda iliharamishwa kwa mara ya kwanza na Omar bin Khattab [22] na kitendo chake hiki ni aina ya uzushi na bidaa katika dini na kinahesabiwa kuwa ni kufanya ijtihadi mbele ya andiko na kupingana na sheria ya Mtume (s.a.w.w). [23] Asqalani (773-852 AH), mmoja wa wanachuoni wa Kisunni, pia anasema kwamba ndoa ya muda ilikuwa halali wakati wa Mtume, na baada yake, ilikuwa halali katika zama za ukhalifa wa Abu Bakr na sehemu ya ukhalifa wa Omar bin al-Khattab. Lakini mwishoni mwa maisha yake Omar aliitangaza kuwa ni haramu. [24]
Hata hivyo akthari ya wanazuoni wa Kisuni wakitegemea baadhi ya hadithi zilizopo katika vyanzo vya hadithi [25] wanasema kuwa, ndoa ya muda ilikuweko katika zama za Bwana Mtume (s.a.w.w) na ilifutwa na mbora huyo wa viumbe. [26] Kundi miongoni mwao pia linaamini kwamba amri ya ndoa ya muda ilibatilishwa katika zama za Mtume (s.a.w.w) kwa kuteremshwa Aya kama vile ya 5 hadi ya 7 ya Surah al-Mu'minun.[27] Wanaamini kwamba kwa mujibu wa Aya hizi, waumini ni watu wasafi wa kimaadili ambapo ukiondoa wake zao au makanizi hawafanyi starehe na watu wengine na watu ambao watafuatilia starehe za kijinsia kupitai njia isiyokuwa hii watakuwa wamevuka mipaka ya Mwenyezi Mungu. [28]
Katika kujibu hilo wamesema Aya ya 5 hadi 7 ya Sura al-Muuminun iliteremka Makka, na Aya ya muta’ wanayoitumia kuihalalisha ndoa ya muda iliteremka baada ya Aya hizi zilizoshuka Madina na kinachofuta hakipasawi kuwa kabla ya kinachofutwa. [29] Aidha, katika ndoa ya muda, mwanamke anachukuliwa kuwa mke wa kisheria wa mwanamume kwa muda ulioainishwa na wahusika katika ndoa. Kwa hiyo, mahusiano yao ya ndoa si ya kuvuka mipaka ya Kimungu. [30]
Hukumu za Fikihi
Baadhi ya hukumu za fikihi za ndoa ya muda kwa mujibu wa fat’wa za mafakihi wa Kishia ni kama ifuatavyo:
- Katika ndoa ya muta’ muda na kiwango cha mahari vinapaswa kuwa wazi na kueleweka katika tamko la ndoa. [32] Kwa mujibu wa mtazamo mashuhuri wa mafakihi ni kuwa, kama katika tamko la ndoa ya muta’ muda hautatajwa, ndoa hiyo itabadilika na kuwa ya daima. [33]
- Kwa mujibu wa mtazamo wa mafakihi, kama pande mbili zitashindwa kutoa tamko la ndoa kwa lugha ya Kiarabu, hata kama wanaweza kumfanya mtu kuwa wakili wao kwa ajili ya hilo, inajuzu kusoma tamko la ndoa kwa lugha nyingine. [34] Baadhi wamesema kuwa, katika hali yoyote wanaweza kusoma tamko la ndoa kwa lugha yoyote. [35]
- Ndoa ya muda inajuzu baina ya mwanaume Mwislamu na mwanamke Ahlul-Kitab; [36] lakini haijuzu baina ya mwanamke Mwislamu na mwanaume Ahlul-Kitab. [37] Kadhalika ni haramu kwa mwanaume au mwanamke Mwislamu kufunga ndoa ya muda na asiyekuwa Mwislamu ambaye si Ahlul-Kitab. [38]
- Ni makuruhu kufunga ndoa ya muda na binti bikira na endapo itafungwa ndoa baina yao inachukiza kuondolewa ubikira wake. [39]
- Katika ndoa ya muta’ kama kitendo cha kuingiliana kimefanyika, baada ya kumalizika muda wa ndoa kama mwanamke sio yaisah (asiyepata hedhi kabisa) ni lazima akae eda. Eda ya mke wa Muta’ kama hapati hedhi (kama atakuwa katika umri wa kupata hedhi na siyo yaisah –asiyepata hedhi kabisa) ni siku 45 na kama anatapa hedhi kwa mujibu wa mtazamo wa baadhi ya mafakihi, eda yake ni hedhi mbili. [40]
- Kama muda wa ndoa ya mutaa utamalizika kabaa ya kuingiliana au mwanaume akasamehe muda wa ndoa hiyo, sio lazima kwa mwanamke kukaa eda. [41]
- Kama katika kipindi cha muda wa ndoa ya muta, mwanaume ataaga dunia, kama hawakuingiliana, mwanamke anapaswa kukaa eda ya kufiwa ambayo ni miezi minne na siku 10. [42]
- Katika ndoa ya muta’ hakuna talaka; bali muda wa ndoa hiyo utapofikia tamati au mwanaume kusamehe muda uliobakia, kutengana kunatimia.
Bibliografia
Wanachuoni wa Shia Imamiya wameandika vitabu na risala nyingi kuhusu ndoa ya muda. Najmuddin Tabasi, mmoja wa wahadhiri wa Chuo (Hawza) cha Qom, ameandika kitabu ambacho chenye anuani isemayo: “Izdevaj moaqat dar raftar va goftar sahabeh” "Ndoa ya muda katika matendo na semi za Maswahaba". Katika sehemu ya kitabu hiki, kazi 46 za wanavyuoni wa Imamiyyah zimetambulishwa, ambazo zimeandikwa kuhusu ndoa ya muda na uhalali wake. [44] Baadhi ya kazi hizi ni:
- Khulasat al-Ijaz fil mutaah: Kitabu hiki kinaundwa na milango minne na kinajihusisha na kubainisha na kuchambua mjadala wa uhalali, fadhila, namna na hukumu za ndoa ya mutaa na masuala tofauti kuhusiana nayo. [45] Baadhi ya athari hizi zimenasibishwa na Sheikh Mufid, [46] baadhi na Shahid al-Awwal [47] na zingine zikinasibishwa na Muhaqqiq Karaki. [48]
- Al-Ziwaj al-Mutaa: Mwandishi, Sayyid Ja’far Murtadha al-Amili. Ndani ya kitabu hiki, mwandishi sambamba na kujadili uhalali wa ndoa hii na hukumu zake anachambua na kukoasoa mitazamo ya wanazuoni wa Kisuni kuhusiana na kuharamisha muta’. [49]
- Al-Ziwaj al-Muaqat fil Islam: Mwandishi, Murtadha Askary. Katika kitabu hiki mwandishi amechambua uhalali wa ndoa ya muta’ katika Qur’an na hadithi kwa mtazamo wa wanazuoni wa Kishia na Ahlu-Sunna.