Sarah

Kutoka wikishia
Kaburi la Sarah lililopo katika Masjid Ibrahim, Hebron

Sarah ni mke wa kwanza wa Ibrahim (a.s) na ndiye mama wa Is'haq (a.s). Kwa mujibu wa kile kilichokuja katika sura mbili za Qur'an Tukufu, Malaika walimpa bishara Nabii Ibrahim ya kuzaliwa mtoto ambaye atakuwa na jina la Is'haq. Nabii Ibrahim alikuwa na umri wa miaka 90 wakati anapewa bishara hiyo. Kutokana na kuwa, Malaika walizungumza na Bi Sarah (mke wa Nabii Ibrahim) kama ilivyokuwa kwa Bibi Maryam na Bibi Fatma, anafahamika kwa jina la Muhaddatha.

Miaka kadhaa mingi kabla ya kuzaliwa Is'haq, Bi Sarah alimpatia Ibrahim kanizi wake aliyejulikana kwa jina la Hajar ili amzalie watoto. Sheikh Swaduq amenuukuu hadithi ambazo zinaashiria husuda ya Sarah baada ya kuzaliwa Ismail. Pamoja na hayo, baadhi ya wahakiki wa zama hizi wametilia shaka maana, madhumuni na sanadi (mlologo wa mapokezi) ya hadithi iliyotajwa.

Maisha

Amin al-Islam Tabarsi [1] na Abul-Futuh Razi [2], miongoni mwa wafasiri wa Qur'ani wa Kishia katika karne ya 6 Hijria wanaamini kwamba, Sarah ni binti ya Haran bin Yahur na ni binamu yake Nabii Ibrahim (a.s); hata hivyo katika baadhi vya vyanzo vya Kishia imeelezwa kuwa, Sarah ni binti ya Nabii Lahij na binamu yake Nabii Ibrahim. [3] Katika vyanzo vya historia kuna kauli zingine kama vile, Sarah ni binti ya Batuael bin Nahur, [4] binti ya Labin bin Birthweil bin Nahur [5] na binti ya mfalme Harran. [6]

Ibn Qutayba al-Dinawari, mwanahistoria wa Kisunni wa karne ya 3, amenukuu kutoka kwenye Torati kwamba Sarah ni mpwa wa Ibrahim. Kwa mujibu wa riwaya yake, Sarah na Lut (a.s) ni kaka na dada wa baba (wamechangia baba), na ni watoto wa Haran ndugu yake Ibrahim [7] Ibn Kathir, mwanahistoria wa Kisunni (aliyefariki 774 Hijiria), amekataa kauli na akazingatia kauli maarufu kwamba Sarah ni binamu yake Ibrahim. Abdul-Sahib Husseini Amili, mwandishi wa kitabu "al-Anbiya Hayatuhum, Qisasuhum" anaamini kwamba Lut ni kaka wa Sarah kwa kuchangia mama, na si kaka yake kwa upande wa baba; kwa hiyo, Sarah si mpwa wa Ibrahim. Kulingana naye, Sara alikuwa binamu wa Ibrahim. [9]

Sarah, pamoja na Lut, walimwamini Ibrahim na wakawa waumini wa Mungu mmoja. [10] Pia aliolewa na Nabii Ibrahim (a.s). [11] Sarah ametambulishwa kuwa mmoja wa wanawake wazuri sana wa zama zake. [12] Sara alikuwa akimiliki ardhi ya kilimo na mifugo mingi na alikabidhi milki zake zote Ibrahim. [13]

Kuhajiri kwake kwenda Misri

Baada ya da'awa na ulinganiaji wa Ibrahim juu ya kumuabudu Mungu mmoja huko Babylonia (Babeli), watu wachache tu ndio walimwamini, na kwa sababu hii, Ibrahim alihamia Sham pamoja na Sarah na Lut, lakini kutokana na kuenea kwa njaa, ukame na magonjwa, Sarah na mumewe Ibrahim (a.s) waliondoka na kwenda Misri. [14] Kulingana na vyanzo vya historia, mfalme wa Misri alipata habari kuhusu uzuri wa Sarah [15], na Ibrahim akijibu swali alipoulizwa kwamba, ana uhusiano gani na Sarah, akamtambulisha kama dada yake. [16] Kama alivyosema Ibn Athir ni kwamba, Ibrahim alikuwa akitambua kwamba, kama atasema Sarah ni mkewe, basi mfalme angetoa amri ya yeye kuuawa, ili amchukue Sarah. Ndio maana akaficha ukweli. [17] Mfalme wa Misri akamwita Sara na kujaribu kummiliki, lakini wakati huo huo mkono wake unakauka. [18] Mfalme akamtaka Sarah aombe dua ili mkono wake uwe na afya tena, ili amwachie aende zake, lakini baada ya Sarah kuomba dua na mkono wa mfalme kupona, mfalme yule akakiuka ahadi yake na akajaribu tena kumwendea Sarah na hili likatokea mara tatu. [19] Baada ya hapo, mfalme akajutia kitendo chake baada ya kufahamu kwamba, Sarah atakuwa sio mwanamke wa kawaida. Hivyo akampa na kumtunuku Sarah kanizi aliyejulikana kwa jina la Hajar na pamoja na zawadi nyingine na akamuachilia huru. [20]

Kwa mujibu wa Allamah Tabatabai ni kuwa, hii kwamba, Ibrahim alimtambulisha Sarah kama dada yake ni jambo ambalo haliendani na cheo cha Utume, na ni mojawapo ya mambo yanayokinzana na Torati ya sasa, ambayo yamekuja katika vyanzo vya kihistoria na hadithi za Sunni. [21] Pia, kwa mujibu wa hadithi iliyonukuuliwa na Allama Tabatabai kutoka katika kitabu cha al-Kafi ni kwamba, katika mkasa huu Ibrahim alimtambulisha Sarah kama mke wake, na kila wakati mkono wa mfalme ulipokauka, ilikuwa ni kwa sababu ya maombi ya Ibrahim ambapo mkono wake ulikuwa ukirejea katika hali yake ya awali. [22]

Bishara ya kupata mtoto katika umri wa miaka 90

Kama ilivyokuja katika vyanzo vya kihistoria, Sara alipokuwa na umri wa miaka 90, malaika wa Mwenyezi Mungu walimpa habari njema ya kuzaliwa kwa mtoto. [23] Alicheka kutokana na kutoamini na kusema mwanamke mzee angewezaje kupata mimba? [24] Alipata mimba baada ya muda. Is'haq ni mtoto wao yeye na Ibrahim. [25] Katika sura mbili za Qur'ani Tukufu, kumeashiriwa habari njema za Malaika na radiamali ya Sarah ya kupata mtoto. [26]

Kabla ya kupata bishara ya mimba yake, kwa kuwa alikuwa tasa, Sarah alimpa kijakazi wake, Hajar, kwa mume wake Ibrahim ili apate mtoto pamoja naye, na baada ya hapo, Ismail, mwana wa Ibaham na Hajar, akazaliwa. [27]

Kuaga dunia

Sarah, mke wa Nabii Ibrahim (a.s), aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 127 katika eneo la Hebron (al-Khalil). Baada ya Sarah kuaga dunia, Nabii Ibrahim alinunua mahali fulani katika eneo la Hebron kutoka kwa wakazi wake na kumzika Sarah huko. [29] Baadaye, Ibrahim, Is'haq na Yaqub walikuja kuzikwa mahali hapo. [30] Mahali palipotajwa hii leo panajulikana kama Haram ya Ibrahim na iko katika mji wa al-Khalil (zamani Hebron) kusini mwa Quds (Jerusalem) huko Palestina. [31]

Sifa maalumu

Kwa mujibu wa hadithi inayonasibishwa kwa Imamu Ali (a.s), Sarah anaitwa Muhaddatha kwa sababu Malaika walizungumza naye na wakampa habari njema ya kuzaliwa Is'haq (a.s). [32] Kwa mujibu wa riwaya iliyotajwa, Bibi Maryam, Bi Fatma Zahra na vilevile mama yake Nabii Musa (a.s) nao ni Muhaddatha. [33] Mashia wanaamini kwamba, malaika hawakuzungumza na Manabii na Mitume tu; bali wamezungumza na Maimamu, Bibi Fatima na wengineo.” [34] Aya za Qur’an Tukufu, zikiwemo Aya za 42 na 45 za Sura Al-Imran, kuhusu Malaika kuzungumza na Hadhrat Maryam, ni uthibitisho wa wazi wa imani na itikadi hii. [35]

Katika hadithi zilizonukuliwa na Sheikh Swaduq na Ali bin Ibrahim Qommi, kumeashiriwa husuda na muamala usio mzuri wa Sarah baada ya kuzaliwa Ismail, na subira ya Ibrahim kuhusiana na jambo hili. [36] Hata hivyo, baadhi ya watafiti wa zama hizi wanasema, hadithi hizi ni dhaifu kimaana na kimapokezi. [37] Kulingana na yale yaliyokuja katika Torati, Sarah alimtaka Ibrahim awafukuze Hajar na Ismail kutoka katika nyumba yake, lakini Ibrahim hakufurahishwa na ombi hili la Sarah. [38] Ingawa hatimaye, baada ya Mwenyezi Mungu kumtaka afanye hilo, alifanya kwa mujibu wa takwa la Sarah. [39]

Hata hivyo, katika baadhi ya hadithi zingine inaelezwa kuwa, usimamizi na ulezi wa watoto wa Mashia na watoto wa waumini katika ulimwengu wa barzakhi umekabidhiwa kwa Sarah na Ibrahim ili wawaleee na kisha kuwakabidhi kwa wazazi wao. [40]

Vyanzo

  • Daqas, Fuʾād Ḥamdū al-. Nisāʾ fī l-Qurʾān al-karīm. Tehran: Mashʿar, 1389 Sh.
  • Ḥasanī al-ʿĀmilī, ʿAbd al-Ṣāḥib al-. Al-Anbīyāʾ. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, 2002.
  • Ibn al-Athīr al-Jazarī, ʿAlī b. Abī l-Karam. Al-Kāmil fī l-tārīkh. Translated by Abū l-Qāsim Ḥālat & ʿAbbās Khalīlī. Tehran: Muʾassisa-yi Maṭbūʿātī-yi ʿIlmī, 1371 Sh.
  • Ibn Kathīr al-Dimashqī, Ismāʿīl b. ʿUmar. Al-Bidāya wa l-nihāya. Beirut: Dār al-Fikr, 1407AH .
  • Ibn Khaldūn, ʿAbd l-Raḥmān b. Muḥammad. Tārīkh Ibn Khaldūn. Tehran: Muʾassisa-yi Muṭāliʿāt wa Taḥqīqāt-i Farhangī, 1363 Sh.
  • Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407AH.
  • Maḥallātī, Dhabīḥ Allāh. Rayāḥīn al-sharīʿa. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1369 Sh.
  • Maqdisī, Muṭahhar b. Ṭāhir al-. Al-Badʾ wa l-tārīkh. Translated by Muḥammad Riḍā Shafīʿī. Tehran: Āgah, 1374 Sh.
  • Qummī, ʿAlī b. Ibrāhīm al-. Tafsīr al-Qummī. Edited by Ṭayyib Mūsawī Jazāʾrī. Qom: Dār al-Kitāb, 1363 Sh.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Al-Khiṣāl. Edited by ʿAlī Akbar Ghffārī. Qom: Jāmiʿa-yi Mudarrisīn-i Qom, 1403 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Maʿānī l-akhbār. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1361 Sh.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Man lā yaḥḍuruh al-faqīh. Edited by ʿAlī Akbar Ghffārī. Second edition. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1413 AH.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Tārīkh al-umam wa l-mulūk. Translated by Abū l-Qāsim Pāyandah. Fifth edition. Tehran: Asāṭīr, 1375 Sh.
  • Ṭabāṭabāyī, Mūhammad Ḥusayn. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1417 AH.