Nenda kwa yaliyomo

Kubomolewa Makaburi ya Baqi'i

Kutoka wikishia

Makala hii inahusiana na tukio la kubomolewa makaburi ya Baqi'i. Ili kuipata taarifa za hauli (kumbukumbu) ya kubomolewa makaburi ya Baqi’i tazama makala ya Yaum al-Hadm (siku ya ubomoaji).

Kubomolewa makaburi ya Baqi'i (Kiarabu: هدم قبور أئمة البقيع) kunaashiria tukio ambalo lilijiri baada ya mji wa Madina kuzingirwa 1344 Hijria. Historia inaonyesha kuwa, katika tukio hilo la kusikitisha, lililotokea tarehe 8 Mfunguo Mosi Shawwal 1345 Hijria (1925 Miladia) Mawahabi wa Saudi Arabia walibomoa makaburi ya Ahlul-Beiti wa Mtume (s.a.w.w) ambayo yanapatikana Baqi’i, katika mji mtakatifu wa Madina. Baada ya Muhammad Ibn Saud kutawala tena maeneo ya Hijaz, likiwemo eneo la Madina, Sheikh Abdullah bin Bulaihad mmoja wa makadhi wa Mawahabi, alitoa fatuwa ya kuhalalisha kuharibiwa kwa makaburi matukufu na ya kihistoria ya mjini Madina. Mawahabi walikusanya watu kwa nguvu na kuwalazimisha kwenda katika makaburi hayo ya Baqi’i na kuanza kubomoa na kuharibu kila kitu kilichokuwa juu ya makaburi ya mji wa Madina na nje ya mji huo. Miongoni mwa makaburi yaliyobomolewa na kuharibiwa vibaya ni makaburi manne ya Maimamu na wajukuu wa mtukufu Mtume (s.a.w.w) ambao ni Imam Hassan, Imam Sajjad, Imam Baqir na Imam Swadiq (as). Makaburi ya Abdullah na Amina, wazazi wa mtukufu wa Mtume (s.a.w.w), kaburi la Ibrahim mtoto wa kiume wa Mtume (s.a.w.w) na kaburi la Ummul Banin mama wa Abul Fadhlil-Abbas nayo yalibomolewa. Kaburi pekee lililobakishwa na Mawahabi hao ni la mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w), kwani walijua kuwa kubomoa kaburi la mtukufu huyo kungezua hasira kali za Waislamu duniani. Mawahabi mara mbili, awali ilikuwa 1220 Hijria na 1344 Hijria wakitegemea fatuwa za Mamufti 15 wa Madina zinazosisitiza kwa kauli moja juu ya marufuku ya kujenga jengo juu ya makaburi na ulazima wa kulibomoa, walibomoa maeneo na majengo yaliyokuwa yamejengwa katika makaburi ya Baqi'i. Kubomolewa makaburi hayo kulikabiliwa na radiamali ya watu na Maulamaa wengi nchini Iran, Iraq, Pakistan, Muungano wa Kisovieti na kadhalika. Serikali ya wakati huo ya Iran katika radiamali yake dhidi ya kubomolewa maeneo matakatifu ya Waislamu ilitangaza siku moja ya maombolezo ya kitaifa na kufuatilia tukio hilo, ikaakhirisha kwa miaka mitatu kuitambua rasmi nchi ya Saudi Arabia iliyokuwa ndio kwanza imeasisiwa. Baada ya makaburi ya Baqi'i kubomolewa eneo hilo likawa ni ardhi ya tambarare. Hata hivyo, sehemu yalipo makaburi ya Maimamu wanne imewekewa alama ya mawe na hivyo yanatambulika. Juhudi za Maulamaa wa Kishia na vilevile serikali ya Iran za kuhakikikisha juu ya makaburi ya Maimamu hao wanne kunawekwa kivuli na vilevile kujengewa ukuta kuzunguka makaburi hayo hazijazaa matunda licha ya serikali ya Saudia kuafiki hilo katika hatua ya awali. Maulamaa wa Kishia mbali na kulalamikia kubomolewa makaburi ya Baqi’i na kusawazishwa na ardhi, wametunga na kuandika vitabu kuhusiana na misingi ya Uwahabi na kubomoa kwao maeneo matakatifuu. Miongoni mwa vitabu hivyo ni Kashf al-Irtiyab kiilichoandikwa na Sayyid Muhsin Amin na Da'wat al-Huda kilichoandaikwa na Muhammad Jawad Balaghi. Inaelezwa kuwa, Mawahabi lilikuwa kundi la kwanza kubomoa maeneo ya kidini likitegemea mitazamo na nadharia ya kidini.


Nafasi na Umuhimu wa Makaburi ya Baqi'i

Eneo la Jannat al-Baqi'i au Baqi'i al-Gharqad (jina la Baqi'i kabla ya kudhihiri Mtume wa Uislamu) [1], yalikuwa makaburi muhimu kabisa ya Waislamu katika Madina [2] na kwa mujiibu wa hadithi, eneo hili lilikuwa likipewa umuhimu na kuzingatiwa mno na mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w). [3] Baqi'i ni eneo ambalo wamezikwa Maimamu maasumu wanne na masahaba wengi pamoja na tabiina. [4] Kabla ya kubomolewa eneo hilo mwaka 1220 na kisha mwaka 1344 na Mawahabi, kulikuweko na majengo juu ya Maimamu wanne (Hassan, Zainul-Abidina, Baqir na Swadiq) na makaburi ya shakhsia wengine. [5] Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, jengo ambalo ndani yake kulikuwa na makaburi ya Maimamu hao wa Kishia, Beit al-Ahzan na majengo mengine kadhaa, hadi mwaka 1297 Hijria yalikuweko katika makaburi ya Baqi'i. [6] Majengo haya kabla ya kubomolewa mara ya kwanza na kufuatia kudhibitiwa tena mji wa Madina na Mawahabi, yalikuwa yamejengwa mwaka 1234 kwa amri ya Mahmoud wa Pili, mfalme wa utawala wa Othmania. [7] Kama alivyoandika Murad Mirza, mtoto wa Abbas Mirza (1212-1168) na mashuhuri kwa Hissam al-Saltana katika kitabu chake ni kuwa, kwa akali hadi kufikia 1297 Hijria kulikuweko na haram ya Imam Hassan (as), Imam Sajjad (as), Imam Baqir (as) na Imam Swadiq (as) katika makaburi ya Baqi’i ambapo mbali na mihrabu na dharih iliyojengwa kwa mbao na rangi ya kijani kulikuweko pia na Bayt al-Ahzan (Nyumba ya Huzuni) inayonasibishwa na Bibi Fatma Zahra (as) ambayo ilikuwa nyuma ya jengo na haram ya Maimamu wanne wa Mashia. [8]. Kwa mujibu wa kumbukumbu za safari za Ayaz Khan Qashqai ambazo aliziandika miaka miwili kabla ya kubomolewa kikamilifu haram ya Baqi’i, eneo la maziara ya Maimamu hao mwanne lilikuwa katika haram moja, ingawa kila moja lilikuwa likifahamika na kueleweka wazi. [9] Ayaz Khan Qashqai alizungumzia pia uwepo wa makaburi yaliyokuwa yamejengewa ya Ibrahim mtoto wa Mtume (saww) na Abdallah ibn Ja’far Tayyar na katika kichochoro cha karibu kulikuweko na makaburi yaliyokuwa yamejengewa yaliyokuwa yakinasibishwa na Saffiyah shangazi ya Mtume, Atika bint Abdul-Muttalib, Ummul-Banin mama wa Abul-Fadhl al-Abbas na watu wengine kutoka ukoo wa Bani Hashim.


Baada ya Kubomolewa Kikamilifu

Kwa mujibu wa Muzaffar A’lam mjumbe wa serikali ya Iran katika mji wa Jeddah wakati huo katika barua yake aliyoandika akiihutubu Kamisheni ya Kudumu ya Hija 13 Disemba 1951 ni kwamba, baada ya Baqi’i kubomolewa na Mawahabi 1344 Hijria, [11] eneo hilo limekuwa ni makaburi ambayo, majengo yote yaliyokuwa yamejengewa makaburi ya Maimamu yalibomolewa na makaburi ya shakhsia wakubwa hayafahamiki. [12] Katika barua yake hiyo, alisisitiza juu ya udharura wa serikali ya Saudi Arabia kuafiki suala la kujengwa ukuta na madirisha ya chuma kando kando ya makaburi manne ya Maimamu wa Kishia. [13] Pamoja na hayo, Rasul Ja’fariyan anaamini kuwa, kukutana Sheikh Abdul Rahim Sahib Fusul Hairi (1294-1367 Hijria) mmoja wa Maulamaa wa Tehran na Mfalme Abdul Aziz Saud kulipelekea sehemu ya makaburi ya Baqi’i ambayo kuna makaburi ya Maimamu wanne wa Kishia, isisawazishwe na ardhi kama ilivyokuwa kwa maeneo mengine, na kwa akali mahali yalipo makaburi hayo ikawa inafahamika vyema na kwa uwazi. [14] Baada ya kubomolewa makaburi ya Baqi’ na maeneo mengine matakatifu ya Kiislamu, kulifanya juhudi mbalimbali kutoka kwa serikali ya wakati huo ya Iran [15] na Afghanistan [16] na vilevile Maulamaa wa Kishia wa Najaf Iraq, [17], Qom Iran, India [18} na Pakistan [19] kwa minajili ya kutaka kufanyike ukarakati na kujengengewa tena makaburi hayo. Lakini juhudi zote hizo hazikuzaa matunda. Hata juhudi za za kuhakikikisha juu ya makaburi ya Maimamu hao wanne kunawekwa kivuli na vilevile kujengwe ukuta kuzunguka makaburi hayo hazijazaa matunda licha ya serikali ya Saudia kuafiki hilo katika hatua ya awali. [20] Pamoja na hayo, katika zama za Mfalmed Fahad bin Abdul-Aziz ukuta wa makaburi ya Baqi’i ulikarabatiwa na kisha katika miaka ya 1418 hadi 1419 Hijria njia za kwenda na kurejea katika makaburi hayo zinazotumiwa na mazuwari (wafanyaziara) zilitengenezwa kwa kutumiwa mawe. [21] Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali ni kwamba, watu ambao wananasibishwa na idara inayojulikana kama ya “Kuamrisha Mema na Kukataza Maovu” katika serikali ya Saudi Arabia husimama karibu na mlango mkuu wa kuingilia katika makaburi ya Baqi’i na huwazuia mazuwari kukaribia makaburi hayo kwa ajili ya kufanya tabaruku. [22] Hii leo sehemu walipozikwa Maimamu wa Kishia huko Baqi’i na makaburi ya shakhsia wakubwa wa mwanzoni mwa Uislamu hayana ishara na alama ya kufahamika isipokuwa vipande vya mawe. [23] Pamoja na hayo, hii leo hali ya makaburi ya Baqi’ ni bora kidogo ikilinganishwa na miaka ya awali baada ya kubomolewa kikamilifu. [24]


Matukio Yaliyopelekea Ubomoaji

Mwaka 1220 Hijria baada ya mwaka mmoja na nusu wa kuzingirwa mji wa Madina na Mawahabi na kufuatia kuibuka ukame katika mji huo wafuasi wa kundi hilo walifanikiwa kuudhibiti mji huo kikamilifu. [25] Kwa mujibu wa vyanzo vilivyopo baada ya mji wa Madina kujisalimisha, Saud bin Abdul Aziz alidhibiti na kushikilia fedha na mali zote zilizokuweko katika haram ya Mtume na vilevile akatoa amri ya kuharibiwa na kubomolewa majengo na minara yote ikiwemo ya makaburi ya Baqi’i. [26] Ni kwa msingi huo ndio maana haram za Maimamu wanne wa Mashia na vilevile kuba linalonasibishwa na Bibi Fatma (as) ambalo lilikuwa likifahamika kama Bayt al-Ahzan ziliangamia au ziliharibiwa vibaya katika shambulio la kwanza la Mawahabi mwaka 1220 Hijria. [27] Baada ya tukio hili, utawala wa Ufalme wa Othmania ulituma jeshi kwa ajili ya kuudhibiti mji wa Madina na kuukomboa kutoka katika mikono na udhibiti wa Mawahabi, na hatimaye Dhul-Hija mwaka 1227 ulifanikiwa kufikia lengo hilo. Ni kwa muktadha huo, Mahmoud wa Pili, mfalme wa 30 wa utawala wa Kiothmania, mwaka 1234 akatoa amri ya kukarabatiwa haram na majengo yaliyokuwa yamebomolewa. [28] Mawahabi kwa mara nyingine tena yaani Mfunguo Tano Safar mwaka 1344 wakaushambulia tena mji wa Madina. [29] Haram ya Mtume na maeneo ya kidini, yaliathiriwa na kudhurika. [30] Miezi saba baadaye, mwezi wa Ramadhani 1344 Hijria Sheikh Abdallah bin Bulaihad (1284-1359 H) ambaye alikuwa kadhi mkuu wa Makka kuanzia 1243 hadi 1345, [31] aliwasili Madina na akitumia fatuwa na Mamufti alipata hukumu ya kubomoa makaburi. [32] Tarehe 8 Mfunguo Mosi Shawwal 1344 Hijria athari zote za kihistoria yakiwemo makaburi ya Baqi’ yalibomolewa kwa fatuwa ya Sheikh Abdallah Bulaihad Kadhi Mkuu wa Saudia akitegemea fatuwa za Mamufti wa Madina [33]. Mamufti 15 wa Madina [34] katika fatuwa yao tajwa kwa kauli moja ya walipiga marufuku kujenga juu ya makaburi na kutoa hukumu ya kubomolewa makaburi yaliyojengewa. [35] Pamoja na hayo, kinyume na itikadi ya Mawahabi, kujengea makaburi kwa itikadi mashuhuri ya Waislamu wa Kisuni na Kishia ni jambo ambalo halipingani na imani na itikadi ya Kiislamu na hata kuzuru makaburi ya shakhsia wakubwa wa kidini na waumini kwa ujumla, linatambuliwa kuwa jambo la sunna. [36] Kwa mujibu wa nyaraka zilizopo, baada ya ubomojia huo, mfalme Abdul-Aziz wa Saudia aliandika barua 12 Shawwal 1344 Hijria ambapo akimhutubu Abdallah bin Bulaihad alimsifu kwa hatua yake hiyo. [37]

Radiamali na Matukio

Radiamali ya Maulamaa na Athari za Vitabu

Kubomolewa makaburi ya Baqi’i na maeneo mengine matakatifu ya Waislamu katika miji ya Makka na Madina na hususan kubomolewa makaburi ya Baqi’i kulikabiliwa na radiamali na upinzani tofauti wa wasomi na wanazuoni wa Kiislamu akiwemo Sayyid Abul-Hassan Isfahani, Sheikh Abdul-Karim Hairi, shakhsia wakubwa wa vyuo vikuu vya kidini (Hawza) Najaf na Qom na kupelekea kusimamishwa masomo na kufungwa soko kuu. [38] Hili lilifanyika kuonyesha kuchukizwa na kitendo hicho. Sheikh Muhammad Khalisi na Sayyid Hassan Modarres nao walionyesha radimalai yao kwa kubomolewa makaburi ya Baqi’i na wakatoa mwito wa kuchukuliwa hatua kali dhidi ya wahusika waliobomoa makaburi na maeneo matakatifu. [39] Sayyid Hassan Tabatabai Qomi, ambaye ni mashuhuri kwa jina la Ayatullah Qomi alikuwa miongoni mwa Marajii Taqlidi wa Kishia ambao kwa miaka mingi tangu kubomolewa makaburi ya Baqi’i alikuwa akifuatilia kuhakikisha kuwa kunafanyika ukarabati. Ili kujibu takwa lake hilo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ikaingia katika mazungumzo na utawala wa Saudi Arabia. [40] Muhammad Hussein Kashif al-Ghitaa aliandika barua akimhutubu Abdallah bin Bulaihad Kadhi Mkuu wa Mawahabi ambapo sambamba na kubainisha itikadi za Mashia kwa tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, alimuita na kumtaka wafanye mjadala na mazungumzo ya kielimu, na kutoitikia na kujibu hilo kulikuwa na maana ya udhaifu wa hoja. [41] Kufuatia kubomolewa maeneo matakatifu ya Kiislamu Sayyid Muhsin Amin alifanya safari Hijaz (Saudia) na kuanza kujishughulisha na kuandika kitabu cha Kashf al-Irtiyab ili abainishe Uwahabi ni nini, historia yake pamoja na hatua na mambo yaliyofanywa na Mawahabi. [42] Kitabu hicho kimejumuisha ubainishaji wa itikadi na imani ya Mawahabi na majibu dhidi ya itikadi zao. Kitabu hiki kimetarajuumiwa kwa lugha ya Kifarsi. [43] Muhammad Javad Balaghi ameandika kitabu chenye anuani ya: "Rad al-Fatwa Bihadm Qubur al Aimah fil Baqi'i" ambapo ndani yake amekosoa misingi ya kifikra ya Mawahabi kuhusiana na kubomoa maeneo matakatifu. [44] Katika kitabu kingine kinachoitwa: Da'wat al-Huda ilal Wara'a fil af'ali wal-Fatwa, kumeonyeshwa radiamali kuhusiana na fatuwa ya kubomoleea maeneo matakatifu yaliyojengewa. [45] Kadhalika kuna washairi wengi ambao wametunga beti za mashairi na kuonyesha kuchukizwa kwao na kitendo cha Mawahabi cha kubomoa makaburi ya Baqi'i. [46] Katika kitabu chake cha al-Radd ala al-Wahabiyah, Muhammad Javad Balaghi akitegemea hadithi za Bwana Mtume (s.a.w.w), Imam Ali ibn Abi Twalib (as), Imam Swadiq (as) na Maimamu wengine na vilevile akitegemea ada zilizozoeleka baina ya Waislamu mwanzoni mwa Uislamu ametoa majibu ya kupinga itikadi za Mawahabi kuhusiana na suala la kubomoa kwao makaburi na kupinga makaburi kujengewa. Aidha anasema, hadithi zinazotumiwa na Mawahabi kulalalisha kitendo chao hicho hazihusiani na jambo hilo; kwani kwa mujibu wake ni kwamba, katika hadithi zinazotumiwa na Mawahabi kama hoja, kujenga majengo kama kuta juu ya makaburi kumepigwa marufuku, na sio jengo ambalo linafunika makaburi. [47] Inaelezwa kwamba, Mawahabi lilikuwa kundi la kwanza kutumia nadharia na mitazamo ya kidini kubomoa haramu na makaburi ya shakhsia wakubwa wa kidini yaliyokuwa yamejengewa. Pamoja na hayo kuna matukio ya watu wengine kutaka kuharibu majengo katika makaburi ya Baqii' lakini hawakufanikiwa katikak hilo. [48] Idadi kadhaa ya mafakihi wa Kishia wametoa fatuwa zinazoeleza ulazima wa kujengewa tena makaburi ya Baqi'i; [49] ambapo miongoni mwao ni Muhammad Fadhil Lankarani, Nasser Makarem Shirazi na Lotfollah Safi Golpaygani ambao wametambua suala la kufanya juhudi kwa ajili ya kukarabati makaburi ya Maimamu huko Baqi’i kuwa ni wajibu au ni wajibu Kifai (wajibu ambao wakifanya baadhi unawaondokea wengine) huku Sayyid Ali Sistani akilitaja hilo kuwa ni jambo linalojuzu. [50]

Hatua za Kiraia za Kiserikali

Baada ya tukio la kubomolewa makaburi ya Baqi’i Waislamu wa maeneo mbalimbali ya Umoja wa Kisovieti (Urusi ya Zamani) na vilevile Waislamu wa mataifa ya Uturuki, Afghanistan, China na Mongolia walitoa risala na kutuma jumbe wakitaka kuhifadhiwa na kuchungwa maeneo matakatifu ya Makka na Madina. [51] Katika mwaka 1925, serikali ya Iran ilitoa taarifa na kutangaza tarehe Tarehe 5 Septemba 1925 kuwa siku ya maombolezo ya kitaifa [52] na kwa utaratibu huo wakazi wa mji wa Tehran wakajishughulisha na kufanya maombolezo. [53] Baadhi ya vyanzo vimesema kuwa, kulifanyika mikusanyiko ya maombolezo ya maelefu ya wananchi kando kando ya eneo la Darvaze Dowlat mjini Tehran. Mikusanyiko hiyo ilifanyika kwa lengo la kulalamikia hatua ya Mawahabi ya kuyavunjia heshima maeneo matakatifu. [54] Serikali ya Iran katika hatua yake nyingine ilitangaza mwaka huo huo kwamba, kutokana na hofu ya usalama wa mahujaji ni marufuku kwenda Hijaz (Saudi Arabia kwa ajili ya ibada ya Hija. [55] Katika taarifa nyingine rasmi ambayo ilitolewa 23/06/1926 serikali ya Iran sambamba na kueleza kwamba, hatua ya kuvunjia heshima maeneo matakatifu ya shakhsia wakubwa wa kidini katika makaburi ya Baqi’i imewaumiza sana na kuwazunisha waumini ilikumbusha kutozuia serikali ya Saudi Arabia suala la kuvunjiwa heshima itikadi za Waislamu. Si hayo tu baali serikali ya Iran ilikataa mwaliko wa Ibn Saud wa kushiriki katika Baraza Kuu la Hijaz [56], na kwa msingi huo Iran ikawa imekataa kuitambua rasmi serikali ya Saudia. [57] Pamoja na hayo baada ya serikali ya Saudia kuzitumia barua nchi za Kiislamu mwaka 1307 Hijria Shamsia ikiwemo serikali ya Iran, ilitangaza kuchukua dhima na jukumu la kusimamia usalama wa Mahujaji, [58] na mwaka mmoja baadaye uhusiano wa Iran na Saudia ukaanza [59] ambapo matokeo yake yakawa ni kuondolewa marufuku rasmi ya Hija baada ya kupita miaka minne. [60].

Rejea

Vyanzo