Kubomolewa Haram ya Askariyein

Kutoka wikishia
Makala hii inahusiana na kubomolewa haram ya Askariyein. Ili kujua kuhusiana na Haramu ya Imam Hadi (a.s) na Imamu Askary (a.s) angalia makala ya Haram ya Askariyein.
haram ya Askariyein kufuatia mashambulio ya kigaidi

kubomolewa haram ya Askariyein (Kiarabu: هدم حرم العسكريين عليهما السلام): Haram ya Maimamu wawili, Imamu Hadi (a.s) na Imamu Askary (a.s) zililipuliwa kufuatia mashambulio ya kigaidi ya makundi ya kitakfiri katika miaka ya 2006 na 2008 na kupelekea kubomolewa. Hatua hiyo ya kigaidi ilikabiliwa na radiamali kali ya Marajii Taqlidi na Waislamu wa madhehebu ya Kishia katika maeneo mbalimbali ya dunia. Kamati ya Ukarakati ya Maeneo Matakatifu ya Iran iliikarabati haram hiyo baina ya mwaka 1389 mpaka 1394 Hijiria Shamsia.

Haram ya Askariyein

Makala asili: Haram ya Askariyein

Haram ya Askariyein, ni mahali alipozikwa Imamu Hadi (as) –aliyeuawa shahidi 254 Hijria – ni Imamu wa 10 na mwanawe Imamu Hassan Askary (as) – aliyeuawa shahidi 260 Hijria – Imamu wa 11 wa Waislamu wa madhehebu ya Shia. Mahali hapo panapopatikana katika mji wa Samarra, Iraq pamekuwa ni mahali pa kufanya ziara. [1]

Kubomolewa mara ya kwanza

Tarehe 23 Muharram mwaka 1427 Hijria magaidi wenye mfungamano na kundi la kigaidi la al-Qaeda waliweka mada za milipuko na kulipua haram hiyo. [2] Katika shambuio hilo la bomu, sehemu ya kuba ya haram hiyo ambayo ilikuwa imejengwa kwa matofali na kurembeshwa kwa dhahabu ya kuchovya na kuta zake ziliporomoka na kubomoka, lakini nguzo za kuba na jengo lake la asili pamoja na kuta zake zilibakia salama. [3]

Radiamali

Kufuatia tukio hilo, Marajii Taqlidi, Maulamaa wa Hawza (vyuo vya kidini) nchini Iraq na Iraq walisimamisha darsa zao. [4] Kadhalika nchini Iran na Iraq masoko yalifungwa na kukatangazwa maombolezo ya umma. [5] Nchini Iran kulifanyika mikusanyiko ya malalamiko kwa kuhudhuriwa na Marajii Taqlidi na Maulamaa wa Hawza katika mji wa Qom katika msikiti wa A’dham. [6] Kadhalika Ayatullah Khamenei na shakhsia wengine wa kisiasa wa Iran na Iraq walitoa taarifa ya kulaani shambulio hilo la kigaidi. [7] Baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa nchi za Kiislamu, madola ya Ulaya na vilevile Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo alilaani shambulio hilo la kigaidi.

Kubomolewa mara ya pili

Tarehe 27 Jamadil Awwal 1428 Hijria kulitokea milipuko miwili katika Haram ya Askariyein. Katika mlipuko huo minara miwili ya haram hiyo ilibomolewa kikamilifu. [8]

Kabla ya hapo pia kulitokea matukio ya mawili ya hujuma na wizi katika haram hiyo katika miaka ya 1355 na 1356 Hijria na mali na vitu vya thamani vilikuwako humo vikaibiwa. [9]

Msukumo wa watekelezaji wa mashambulio

Kamiyar Sedaqatsamar Husseini, mjumbe wa Kamati ya Kielimu ya Kituo cha Utafiti cha Sayansi na Utafiti wa Masuala ya Kiutamaduni anasema kuwa, msukumo wa matakfiri wa kubomoa Haram ya Askariyein ni wa kisiasa na kimadhehebu. Kwa mujibu wake ni kwamba, kitendo hiki kilifanyika kwa lengo la kuzusha mifarakano baina ya Mashia na Masuni na ni katika fremu ya malengo ya madola ya Marekani, Uingereza na utawala wa Israel; na upande wake wa kimadhehebu unarejea katika itikadi ya Mawahabi kuhusiana na ziyara na kujengewa makaburi. [10] Ibn Taymiyah anasema kuwa, ni haramu kujengea makaburi na kwamba, ni wajibu kubomoa makaburi yaliyojengewa. [11] Mawahabi wakitumia msukumo huu na wakitegemea fat’wa za mamufti wao mwaka 1344 Hijria walibomoa turathi zote za kihistoria za makaburi ya Baqi’i. [12] Hata hivyo itikadi ya Mawahabi kuhusiana na hili ni kinyume na mtazamo wa Waislamu. [13]

Angalia pia: Kujenga juu ya makaburi

Ukarabati

Baada ya kubomolewa, kutokana na kuwa kuba la haram hiyo lilikuwa katika orodha ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu la Utamaduni (UNESCO), ikaafikiwa kuwa, ukarabati wake uwe chini ya usimamizi wa UNESCO; hata hivyo serikali ya Iraq ikalikabidhi jukumu hilo Kamati ya Ukarabati wa Maeneo Matakatifu ya Iran. [14] Kazi hiyo ya ukarabati ilifikia tamati 1394 Hijria Shamsia. Kwa mujibu wa Mkuu wa Kamati ya Ukaratabati wa Maeneo Matakatifu ya Iran, katika ukarabati huu zaidi ya matofali 23,000 yalichovewa dhahabu. [15]

Dharih mpya

Kadhalika ili kuharakisha ukarabati huo ofisi ya Ayatullah Ali Sistani nchini Iran, mmoja wa Marajii Taqlidi wa Kishia, ilichukua jukumu la kutengeneza dharih (eneo la ndani) ya haramu hiyo. [16] Kituo cha kutengeneza dharih (eneo la ndani linalozunguka kaburi) ya Haram ya Askariyein kilikuwa kikifanya kazi zake katika mji wa Qum. Lajurdi, afisa msimamizi wa mradi huo anasema, Katika kujenga dharih kulitumika kilo 4,500 za fedha na kilo 70 za dhahabu. [17] Ujenzi wa dharih (eneo la ndani linalozunguka kaburi) ya haram ya Askariyein ulifikia tamati 1393 Hijria Shamsia. [18] na mwaka 1395 dharih hiyo ikahamishiwa Samarra na mwaka 1396 ikazinduliwa. [19]