Nenda kwa yaliyomo

Wajib Kifai

Kutoka wikishia

Wajib Kifai (Kiarabu: الواجب الكفائي) ni miongoni mwa wajibu za kidini ambao ni lazima kwa wakalafu (mukallafin) wote kutekeleza, lakini kama wakifanya na kutekeleza wajibu huo baadhi ya watu, baSi taklifu hiyo huondoka kwa wengine. Wajib Kifai ni mkabala wa Wajib Aini (wajibu ambao ni lazima kila mtu kufanya) au wajibu wa kila mtu. Kwa ibara nyingine ni kuwa, Wajib Aini ni aina za wajibu za kidini ambazo mukallafu anapaswa kuzitekeleza yeye mwenyewe. Kumuandaa maiti, kupigana jihadi, kuamrisha mema na kukataza maovu ni miongoni mwa wajibu Kifai. Kuswali Sala za kila siku (Sala Tano) na kufunga Saumu ya Ramadhani ni miongoni mwa Wajib Aini.

Wajib Kifai katika mambo mengi unahusiana na maslahi ya umma katika jamii; ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Wajib Kifai umetambulishwa kuwa ni mkakati na mbinu ya Uislamu ya kulinda maslahi ya jamii. Katika baadhi ya mambo yamkini Wajib Kifai ukabadilika na kuwa Wajib Aini; kama kwa mfano kutakuwa na kadhi mmoja tu hivyo katika hali hii kutoa kwake hukumu kutakuwa ni Wajib Aini. Wanazuoni na wasomi wa elimu ya Usul Fiqh wanasema kuwa, wakati itakapotokea mtu akashuku kwamba, huu ni Wajib Kifai au Aini, anapaswa kujengea katika Wajib Aini.

Maana ya Kifiq'h

Wajib Kifai ni moja ya sehemu za wajibu za kidini ambapo lengo la dini ni kutekeleza tu jambo hilo na kazi husika na hakuna tofauti ni nani anayetekeleza wajibu huo.[1] Katika wajibu huu, watu wote wanaohutubiwa na kulengwa jukumu na taklifu yao ni kwa sura sawa, lakini kama watajitokeza baadhi ya watu na kutekeleza wajibu huo, basi kwa wengine taklifu hiyo inaondoka.[2] Kwa maana kwamba, hawana jukumu na taklifu ya kutekeleza tena hilo. Miongoni mwa amali na matendo ambayo ni Wajib Kifai tunaweza kuashiria mambo ya wajibu kama kuondoa na kusafisha najisi msikitini, kuamrisha mema na kukataza maovu, kumuandaa maiti, jihadi, kujifunza na kufanya kazi na mambo ambayo yana mfungamano na maisha ya watu.[3] Wajib Kifai katika mambo mengi unahusiana na maslahi ya umma katika jamii; ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Wajib Kifai umetambulishwa kuwa ni mkakati na mbinu ya Uislamu ya kulinda maslahi ya jamii.[4]

Katika kubainisha kielimu jambo hili, kwamba, kimsingi Wajib Kifai ni wajibu wa nani, kuna kauli tofauti.[5] Kila mtu mmoja mmoja (mtazamo wa Akhund Khorasani,[6]) sio mtu maalumu (mtazamo wa Imamu Khomeini,[7]) mmoja kati ya watu ambaye ni mukallafu kwa sura mbadala (nadharia ya Sayyid Muhammad Baqir Sadr[8]), Wakalafu (wenye taklifu) kwa ujumla wake (nadharia inayonasibishwa na Qutb al-Din Shirazi[9] ni miongoni mwa mitazamo ambayo imetajawa kuhusiana na mas'ala haya.

Tofauti ya Wajib Kifai na Aini

Wajib Kifai uko mkabala wa Wajib Aini. Wajib Aini ni wajibu ambao ni wajibu kwa kila mukallaf kutekeleza; kwa maana kwamba, mukallaf hawezi kuacha kutekeleza taklifu yake kwa kisingizio kwamba, wengine washatekeleza. Kama vile Sala za kila siku na Saumu ya mwezi wa Ramadhani.[10] Katika Wajib Kifai, thawabu hutolewa kwa mtekelezaji wake tu, lakini kama hakuna mtu yeyote miongoni mwa wakallafu ambaye ametekeleza wajibu huo, wote watapata dhambi.[11] Kujifunza baadhi ya elimu ni Wajib Aini na kujifunza baadhi ya elimu ni Wajib Kifai. Elimu ambazo kujifunza kwake ni utangulizi wa kudhamini mahitaji ya kijamii (kama kujifunza elimu ya tiba) wajibu wake ni Kifai; kwa maana kwamba, wakijifunza baadhi waliobakia sio lazima na wajibu kujifunza elimu hiyo. Lakini kujifunza hukumu na itikadi ambazo kujifunza kwake ni utangulizi kwa ajili ya kumjenga mtu, ni Waajib Aini.[12]

Kubadilika Wajib Kifai na Kuwa Wajib Aini

Kama itakuwa kwamba, miongni mwa watu (wakallaf) kuna mtu mmoja tu ambaye anaweza kutekeleza Wajib Kifai, kuutekeleza wajibu huo ni mithili ya kutekeleza wajibu zingine ambazo ni Wajib Aini; kwa mfano, kutoa ushahidi mahakamani, licha ya kuwa kiasili ni Wajib Kifai, lakini kama itakuwa aliyeshuhudia tukio ni mtu mmoja tu, basi kutoa ushahidi katika hali hii kwa mtu yule kama ilivyo kwa wajibu zingine ambazo ni Aini kwake yeye wajibu huu pia utakuwa ni Wajib Aini.[13]

Wajib Kifai hauna maana kwamba, kila anayeweza kutekeleza wajibu huo atekeleze, bali ili kutekeleza wajibu huo awali kuna ulazima wa ustahiki; kwa mfano, kuwa kadhi ni Wajib Kifai, lakini ili mtu aweze kutoa hukumu awali anapaswa kuwa na vigezo na ustahiki wa kutoa hukumu.[14] Kwa msingi huo, katika matukio na kesi ambazo kuna mtu mmoja tu mwenye ustahiki wa kutenda Wajib Aini, katika hali hii Wajib Kifai wa mtu yule hubadilika na kwake yeye huwa ni Wajib Aini.[15]

Vigawanyo

Kuna aina kadhaa za Wajib Kifai:

  1. Wajibu ambazo haiwezekani kutekeleza kwa mara nyingine, kama vile kumuua aliyemtusi Nabii (kwani haiwezekani kuumuua mtu mara mbili).
  2. Wajibu ambazo licha ya kuwa inawezekana kutekeleza kwa mara nyingine, lakini kwa mujibu wa sheria ni marufuku kutekeleza tena wajibu huo, kama wajibu wa kumzika maiti (licha ya kuwa inawezekana kufukua kaburi na kumzika tena maiti, lakini kufukua kaburi ni haramu).
  3. Wajibu ambazo kutekeleza kwa mara nyingine haipendezi wala haikatazwi kama vile kumkafini maiti (kumkafini maiti mara kadhaa, sio mustahabu na wala sio haramu).
  4. Wajibu ambazo inafaa kutekeleza tena, kama vile kusali Sala ya maiti ambapo kusali tena ni mustahabu.[16]

Shaka Juu ya Wajib Aini au Kifai

Maulamaa wa elimu ya Usul-Fiq’h wanasema kuwa, katika maeneo ambayo hatuna uhakika na haifahamiki wazi na bayana kwamba, amri hii ya Mwenyezi Mungu ni Wajib Aini au Kifai, tunapaswa kujengea kwamba, ni Wajib Aini;[17] kwani akili inahukumu kwamba, wakati hatuna uhakika kwamba, kutekelezwa amri ya Mwenyezi Mungu na watu wengine hilo halitapelekea jukumu hilo kutuondokea au la, basi tunapaswa kulitekeleza hilo sisi wenyewe.[18]

Masuala Yanayo Husiana

Rejea

Vyanzo