Kughushi Hadithi

Kutoka wikishia

Makala hii inahusiana na maana ya kughushi hadithi. Kama unataka kufahamu kuhusiana na hadithi za kughushi, angalia maudhui ya hadithi za kughushi.

Kughushi Hadithi (Kiarabu: وضع الحديث) au kupachika hadithi, ni kutunga na kubuni hadithi na kisha kuinasibisha na Mtume (saww) au Maimamu maasumu. Kughushi hadithii wakati mwingine kulikuwa kukifanyika kwa kutunga na kubuni hadithi na wakati mwingine kwa kuongezea maneno katika hadiithi au kubadilisha ibara miongoni mwa ibara za hadithi hiyo na kupindua asili ya hadithi yenyewe. Historia ya kuanza kughushi hadithi inarejea katika zama za uhai wa Bwana Mtume (saww) na kisha mwenendo huo ukaenea na kuchukkua wigo mpana zaidi katika zama za utawala wa Muawiya ibn Abi Sufyan. Kufifiza na kuhafifisha fadhila za Imamu Ali ibn Abi Twalib (as), kuhalalisha utawala wa Muawiya na kuwa na chuki na taasubi dhidi ya mirengo na makundi mbalimbali ni miongoni mwa malengo na msukumo wa kughushi hadithi. Kughushi na kuweka hadithi bandia ni jambo ambalo limekuwa na matokeo mabaya ambapo miongoni mwayo ni: Kunyimwa watu fursa ya kunufaika na Ahlul-Baiti (as), kupingwa baadhi ya hadithi ambazo kimsingi ni sahihi na kuwa gumu suala la kuzipata na kuzifikia hadithi sahihi. Kwa mujibu wa Maulamaa wa madhehebu ya Shia ni kwamba: Abu Hurayrah, Ka'b al-Ahbar, Ubayy ibn Ka'b na Ibn Abi al-Awjaa ni katika wapokezi wa hadithi bandia na za kughushi. Kuhusiana na hadithi bandia na za kughushi kumeandika vitabu vingi ambapo kitabu cha "al-Maudhuaat cha Ibn Jawzi (aliyeaga dunia 597 H) ni miongoni mwa vitabu vya awalii kabisa kuandikwa kuhusiana na maudhui hii. Al-Akhbar al-Dakhilah" kilichoandikwa na Sheikh Muhammad Taqi Shushtari (aliyeaga dunia 1374 Hijria Shamsia), al-Maudhuaat fi athaar wal-khabaar kilichoandikwa na Sayyid Hashim maaruf al-Hassani na "Yek Sado Panjah Sahabeh Sakhtegi" (Masahaba Bandia 150) kilichoandikwa na Sayyid Murtadha Askary (1293-1386 Hijria Shamsia) ni vitabu vingine vilivyoandikwa katika uwanja huu.

Utambuzi wa Maana

Vilevile angalia: Hadithi bandia Kughushii hadithi fasili na maana yake ni kutunga na kubuni hadithi. Katika vyanzo na vitabu mbalimbali kughushi hadithi kunaelezwa kuwa "kupachika hadithi" au kuweka hadithi bandia. [1] Na hadithi ya kubuni na kughushi inafahamika kama hadithi bandia. [2] Hadithii ya kughushi ni hadithii ambayo imebuniwa na kutengenezwa kwa makusudi au kwa kukosea na kisha kunasibishwa nayo Bwana Mtume (saww) au Imamu maasumu. [3] Kukiri aliyeghushi kuhusiana na hadithi hiyo kuwa bandia, kuweko mambo na ishara zinazoonyesha kuwa hadithi husika ni ya kutunga na ya bandia, [4] kukinzana muhtawa na maana ya hadithi husika na akili, Qur'ani au dharura miongoni mwa dharura za madhehebu [5] ni katika ishara za wazi na bayana za kuifanya hadithi ihesabiwe kuwa ni ya kughushi na bandia.

Mbinu na Aina ya Hadithi Bandia

Kughushi hadithi na kuja na hadithi bandia ni jambo ambalo lilikuwa likifanyika kwa mbinu na njia mbalimbali: Kuna wakati hadithii nzima ilikuwa ni ya kughushi na bandia na kisha kuelezwa kwamba, imenukuliwa kutoka kwa Mtume au Maimamu. Wakati mwingine kulikuwa kukiongezwa maneno katika hadithi fulani ambayo tayari ipo na hivyo kubadilishwa. [6] Inaelezwa kuwa, kughushi hadithi na kuweka hadithi bandia kumefanyika zaidi na kwa sura kamili katika maudhui za kiitikadi, kimaadili, kihistoria, kitiba, fadhila na dua. [7] Mfano wa kuongeza ibara na maneno katika hadithii, ni nyongeza iliyowekwa na Mansour Dawaniqi, Khalifa wa pili wa utawala wa Bani Abbas katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (saww) kuhusiana na Imamu wa Zama, Imamu Mahdi (atfs). Imekuja katika hadithi hiyo kwamba, Mwenyezi Mungu atamteua mtu kutoka katika kizazi changu (Ahlu-Baiti wangu), ambaye jina lake ni jina langu; [8] hata hivyo Mansour akiwa na lengo la kumtambulisha mwanawe kama misdaqi na mfano wa hadithi hiyo, aliongeza ibara hii: “ na jina la baba yake, ni (kama) jina la baba yangu"; hii ni kutokana na kuwa, jina la baba yake Mansur lilikuwa Abdallah kama jina la baba yake Mtume Muhammad (saww). [9] Mfano mwingine wa kubadilishwa maneno na ibara kuna hadithi pia iliyonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (saww) ambapo baadhi wamenukuu ikimsifia Muawiya. Imekuja katika hadithi hiyo kwamba: Kila mtakapomshuhudia Muawiyah anazungumza katika mimbari, basi mkubalini, kwani yeye ni mtu mwema na wa kuaminika. [10] Inaelezwa kuwa, kimsingi hadithi hii kiasili ilikuwa ikimlaumu Muawiya na kulikuweko na ibara isemayo: "Faqtuluuh" yaani muweni ikabadilishwa na kuwa "Faqbaluuh" yaani mkubalini. [11] Wizi na uporaji wa hadithi (kunukuu hadithi iliyonukuliwa na mpokezi mwingine na mtu kuweka jina lake na hivyo kuwa yeye ndiye mpokezi wa hadithi hiyo), kutia mkono (kuleta mabadiliko) katika vitabu vya wapokezi wa hadithi na kueneza nakala za uongo ni mbinu zingine zilizokuwa zikitumika katika suala la kughushi na kuweka hadithi za bandia. [12]

Historia Yake

Baadhi ya wahakiki na watafiti wanaamini kuwa, historia ya kughushi hadithii inarejea katika kipindi na zama za uhai wa Bwana Mtume (saww). Wahakiki hao wanatumia hadithi zinazobainisha nafasi ya watu ambao wanamnasibisha na mambo Mtume (ambao kimsingi hakuyasema) kwamba, kwamba mahali pao ni motoni, [13] na kulifanya hilo kama ushahidi wa kuthibitisha madai yao. [14] Kuna mifano pia ya kumsingizia uongo Bwana Mtume (saww) katika kipindi cha uhai wake. [15]. Kwa mujibu wa hadithi, Imamu Ali ibn Abi Twalib (as) ameashiria suala la kughushi hadithi katika zama za uhai wa mtukufu Mtume. [16] Hata hivyo kwa mujibu wa kauli ya Hashim Maaruf Hassani, baadhi ya wahakiki wa Ahlu Sunna wanaamini kwamba, suala la kughushi hadithi halikutokea katika zama za makhalifa wa mwanzo na kwamba, suala hili lilianza baada ya kuuawa shahidi Imamu Ali ibn Abi Twalib (as). Katika zama hizi kulidhihiri na kuibuka vyama na makundi mbalimbali ambayo yakiwa na lengo la kujiimarisha yalikuwa yakitumia Qur'ani na hadithi, na yalipokuwa yakikosa ushahidi wa Qur'ani na hadithi basi yalikuwa yakighushi na kupachika hadithi ya bandia ili kufikia malengo yao. [17] Inaelezwa kwamba, kughushi hadithi ni jambo lililopanuka na kuchukua wigo mpana zaidi katika zama za utawala wa Muawiya ibn Abi Sufyan. [18] Kwa mujibu wa kauli ya Ibn Abil-Hadid ambaye ni Mu’tazilah aliyetoa ufafanuni wa kitabu cha Nahaj al-Balagha katika karne ya 7 ni kuwa, Muawiya alikuwa akiwaunga mkono wapokezi wa hadithi ambao walikuwa wakighushi na kuweka hadithi bandia kuhusiana na fadhila za Othman na masahaba wengine na wakati huo huo kumtia dosari na mapungufu Imam Ali (as). [19] Kadhalika Bakriyyah (ambalo ni kundi linaloamini kwamba, Abu Bakr ibn Abi Quhafah alikuwa khalifa na kiongozi baada ya Mtume na kwamba, kuna ushahidi katika Uislamu wa kuthibitisha hilo), walikuwa wakighushi hadithi kwa maslahi ya Abu Bakr kwa ajili ya kukabilina na fadhila za Imamu Ali ibn Abi Twalib (as). [20]

Historia ya Kupambana na Kughushi Hadithi

Ahmad Paktechi anasema, mwishoni mwa karne ya tano kuliandikwa vitabu kuhusiana na hadithi bandia na za kughushi; hata hivyo kutumiwa suala la tuhuma za wazi kuhusu kughushi hadithi katika tathmini za wataalamu wa elimu ya hadithi wa Kishia linarejea mwanzoni mwa karne ya 4 Hijria na kuna mifano ya hilo katika matamshi ya ibn Uqdah [21] na ibn Walid [22] na katika karne ya 5 kunaonekana athari za ibn Adhair [23]. Kadhalika kwa mujibu wa msomi huyo ni kwamba, katika uga wa hadithi wa Ahlu Sunna, kwa mara ya kwanza wataalamu wa elimu ya hadithi wa maktaba ya Baghdad walinufaika na hadithi za kughushi katika tathmini zao. [24]

Msukumo na Sababu za Kughushi Hadithi

Kughushi hadithi na kupachika hadithi bandia kulifanyika kwa musukumo na malengo mbalimbali na baadhi ya hayo ni:

  • Kufifiza na kuhafifisha fadhila za Imamu Ali (as): Inaelezwa kuwa, mtu ambaye kulighushiwa hadithi nyingi dhidi yake ni Imamu Ali (as). [25] Ibn Abil-Hadid mfuasi wa Mu’tazila amenukuu katika sherhe na ufafanuzi wake wa Nahajul Balagha kutoka kwa Abu Ja'afar Iskafi mwanateolojia wa Kimu’tazilah wa karne ya tatu Hijria ya kwamba, Muawiya aliwapa jukumu kundi la masahaba na tabiina watunge na kughushi hadithi za kumlaumu Imamu Ali (as). [26] Anasema: Muawiya aliwaandikia barua wafanyakazi wake akiwaambiwa wawatake watu waghushi na kutunga hadithi za uongo ambazo zinaeleza sifa nzuri na fadhila za makhalifa watatu (Abu Bakr, Omar na Othman) ili kusiweko na hadithi inayoelezea fadhila na ubora wa Imamu Ali (as) isipokuwa kando yake pia kuna hadithi kama hiyo ambayo inatoa wasifu bora na fadhila kuhusu makhalifa wa mwanzo na masahaba au wabuni hadithi ambazo zitakuwa ziko dhidi au zinapingana na fadhila za Ali ibn Abi Twalib (as). [27]
  • Kuwalalalisha Watawala na Makhalifa: Hashim Maaruf Hassani mhakiki wa Kilebanoni wa karne ya 14 Hijria anasema: Tawala za Bani Umayya na Bani Abbas zikiwa na lengo la kuhalalisha tawala zao na kuzipa uhalali wa kisheria zilikuwa zikitunga na kughushi hadithi kuhusiana na fadhila za viongozi wao wakubwa au zilikuwa zikinasibisha tawala na ukhalifa wao na Mtume (saww). [28] Moja ya hadithi ambazo utawala wa Bani Abbas ulikuwa ukiinasibisha na kudai kwamba, imetoka kwa Mtume ni hii: Ukhalifa utakuwa mikononi mwa watoto wa Ami yangu (Abbas). [29]
  • Kuwa na Taasubi na kundi lao na kuyaweka kando makundi mengine: Wafuasi wa kila mrengo au kundi wakiwa na nia ya kuimarisha kundi na mrengo wao walikuwa wakitumia Qur’ani na hadithi na walipokuwa wakikosa walikuwa wakighushi hadithi. [30] Kusambaratisha dini, kuzusha hitilafu baina ya Waislamu kulikokuwa kukifanywa na wasiokuwa Waislamu [31], kujikurubisha kwa wafalme [32] na kutunga fadhila (kutengeneza na kubuni) na ubora kwa ajili ya watu [33] ni misukumo na sababu nyingine zilizopekea kughushi na kutunga hadithi. Kuna wakati pia kulikuwa na msukumo wa kidini kama vile kuleta mageuzi na marekebisho katika jamii, [34] kuwafanya watu katika jamii waizingatie Qur’ani [35] na kutaka ujira kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kulikuwa kukighushiwa hadithi. [36] Kadhalika hitilafu na mvutano kuhusiana na kiongozi baada ya Bwana Mtume (saww) na mielekeo ya kivikundi ni sababu zingine zilizotambuliwa na kutajwa kama zilipelekea kughushi hadithi. [37]

Athari na Matokeo

Baadhi ya matokeo ya kughushi hadithi ni:

  • Ugumu wa kufikia hadithi sahihi: Kughushi hadithi kumepelekea kuwa gumu suala la kupambanua baina ya hadithi sahihi na bandia. [38]
  • Kukataliwa baadhi ya hadithi sahihi: Baadhi ya hadithi sahihi zimekataliwa na kuwekwa kando kwa kisingizio cha kupambana na hadithi bandia. Kwa mfano Ibn Qayyim al-Jawziyya (aliyeaga dunia 751 Hijria), alimu na msomi wa Kisuni na ambaye pia ni mwanafunzi wa Ibn Taymiyyah anaamini kuwa, hadithi ya kutangazwa rasmi na kutawazwa Imamu Ali kuwa kiongozi wa Waislamu baada ya Mtume katika eneo la Ghadir Khum ni bandia na si sahihi; [39] licha ya kuwa kwa mujibu wa Allama Amini ni kwamba, hadithi ya Ghadir imenukuliwa kwa sura ya mutawatir (kwa mapokezi mengi) katika vitabu vya Kishia na Kisuni. [40] Vilevile Ibn al-Jawzi (aliyeaga dunia 597 Hijria) alimu na mwanazuoni wa Ahlu Sunna, ameorodhesha katika kitabu chake cha al-Maudhuuat baadhi ya hadithi kuhusiana na ubora na fadhila za Imamu Ali (as) ambazo amezitambua kama hadithi bandia na za kughushi. [41]
  • Kunyimwa watu fursa ya kunufaika na Ahlul-Beiti: Kulikuwa kukinukuliwa hadithi na kunasibishwa na Maimamu na kupelekea watu kuwachukia Maimamu hao kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume (saww). Aghalabu ya hadithi hizo zilikuwa zikighushiwa na makundi ya Kishia kama Zaydiyah, Fat’hiyah na Ghaliyan (makundi yenye misimamo ya kufurutu ada miongoni mwa Mashia). [42]
  • Kuandikwa vitabu vya elimu ya hadithi: Kughushi hadithi kulipelekea kuandikwa vitabu kuhusiana na wapokezi wa hadithi, aina ya hadithi na hadithi za kutunga. [43]. Na moja ya sababu za hitajio la Ilm Rijaal (elimu ya hadithi inayochunguza hali na sifa za wapokezi wa hadithi na kubainisha kanuni na misingi yake) imetajwa kuwa ni kutambua wapokezi wa hadithi pamoja na hadithi zao. [44]

Walioghushi Hadithi

Allama Amini ametaja majina 700 katika kitabu chake cha al-Ghadir kama watu waliohusika na kughushi hadithi sambamba na baadhi ya hadithi zao bandia na za kughushi. Baadhi yao wamehusishwa na hadithi za kughushi zaidi ya 100,000. [45] Sehemu hii ya kitabu cha al-Ghadir imechapishwa kama kitabu kinachojitegemea kwa anuani ya “al-Wadhauun Waahadithuhum al-Maudhuah”. [46]

Baadhi ya waliokuwa wakighushi hadithi ni:

  • Abu Hurayra: Katika vitabu vya hadithi kumenukuliwa hadithi 5,374 kupitia kwake; [47], hii ni katika hali ambayo, yeye aliishi miaka mitatu tu pamoja na Mtume. Kwa muktadha huo baadhi ya masahaba kama Ali (as), Omar, Othman na hususan Aisha wakalamikia wingi wa hadithi zake zinazodaiwa kwamba, amepokea kutoka kwa Mtume. Aisha alikuwa akisema: Abu Hurayra ananukuu hadithi kutoka kwa Mtume ambazo mimi sijawahi kuzisikia kabisa. [48]
  • Ka’b al-Ahbar: Kwa mujibu wa Sayyid Murtadha Askary ni kuwa, akthari ya habari za Mayahudi, kuwasifu Ahlul-Kitab na wasifu mwingi wa Baytul-Muqaddas zilinukuliwa na Bwana huyu na kutiwa katika vyanzo vya Kiislamu. [49]
  • Ubayy ibn Ka'b: Zimenukuliwa hadithi kutoka kwa Bwana huyu zinazohusiana na fadhila za sura za Qur’ani ambapo yeye mwenye amekiri kwamba, hadithi hizo ni za kughushi. [50]
  • Nuh ibn Abi Maryam al-Marwazi: Bwana huyu naye alighushi hadithi zinazohusiana na fadhila za sura za Qur’ani na anasema alifanya hivyo kwa sababu ya watu kuipa mgongo Qur’ani na kuzingatia fikihi ya Abu Hanifa na Maghazi ibn Is’haq. [51]
  • Ibn Abi al-Awjaa: Inaelezwa kuwa, Bwana huyu alighushi na kuweka hadithi bandia 4,000. [52]

Bibliografia

Kumeandika vitabu mbalimbali kuhusiana na madhui ya kughushi hadithi ambapo akthari ya vitabu hivyo vinahusiana na kukusanya hadithi bandia na kuwatambulisha waliofanya kazi ya kughushi hadithi. Kitabu cha al-Mawdhuat cha Ibn Jawzi (aliyeaga dunia 597), Dhayl Al-Lalai Al-Masnu'ah fi Al-Ahadith Al-Mawdhu'ah kilichoandikwa na Jamal al-Din Suyut (aliayeaga dunia 911 Hijria), al-Akhbar al-Dakhilah cha Muhammad Taqi Shushtari (aliaga dunia 1374 Hijria Shamsia), al-Mawdhuaat Fi Athaar wal-Akhbar cha Sayyid Hashim Maaruf al-Hassani na na "Yek Sado Panjah Sahabeh Sakhtegi" kilichoandikwa na Sayyid Murtadha Askary (1293-1386 Hijria Shamsia) ni miongoni mwa vitabu viliivyoandikwa katika uwanja huu. Kadhalika kuna vitabu vilivyoandikwa vikijadili tukio la kughushi hadithi na baadhi ya vitabu hivyo ni:

  • Al-Wadhau fil-Hadith, mwandishi: Omar in Hassan Falata kwa Lugha ya Kiarabu na kilichapishwa 1401 Hijria na Maktabat al-Ghazali Damascus Syria. [53].
  • Darsnameh Vaz’u Hadis, kwa lugha ya Kifarsi, mwandishi: Nassir Rafii Muhammadi. Katika kitabu hiki kumebainisha maana ya kughushi hadithi, historia yake, sababu ya hilo, mbinu zilizotumika pamoja na matokeo ya kuweka hadithi bandia. [54. Mwishoni mwa kitabu hiki pia, kumetambulishwa vitabu vinavyohusiana na maudhui ya kughushi hadithi. [55]

Rejea

Vyanzo