Uandishi wa hadithi
Uandishi wa hadithi (Kiarabu: تدوين الحديث) au kuandika hadithi za Mtume (s.a.w.w) na Ahlul-Bayt (a.s) ni moja ya nyenzo na sababu muhimu za kuhifadhiwa hadithi na kuhamishiwa kwa vizazi vilivyokuja baadaye. Katika hadithi, umuhimu wa kuandika hadithi umesisitizwa na kutiliwa mkazo na katika hadithi ya Fatima (a.s), thamani ya hadithi iliyoandikwa inachukuliwa kuwa sawa na Hassan na Hussein (a.s). Shahid Thani (aliyefariki 955 au 965 AH) alikuwa akiutambua uandishi wa hadithi kuwa ni wajibu katika zama zake kutokana na ukosefu wa vitabu vya hadithi.
Wakati wa uhai wa Mtukufu Mtume s.a.w.w), maswahaba waliandika hadithi na wakati mwingine Mtume (s.a.w.w) alimsomea imla hadithi hizo Imam Ali (a.s) na kumtaka aandike. Hata hivyo, baada ya kifo cha Mtume na wakati wa ukhalifa wa Abu Bakr na Omar Ibn Khattab, uandishi wa hadith ulipigwa marufuku. Masunni wanaona kuwa kuzuia kuenea kwa hadith batili na hofu ya kutokea kitabu kingine kando ya kitabu cha Qur’an ni miongoni mwa sababu za kupigwa marufuku uandishi wa hadithi. Kwa upande mwingine, kwa mujibu wa Mashia, moja ya sababu za kupiga marufuku uandishi wa hadithi ilikuwa ni kuzuia kuenea sifa na fadhila za Imamu Ali (a.s). Baada ya kuondolewa marufuku ya kuandika hadithi na Omar bin Abdul-Aziz (63-101 Hijiria) kuliandikwa vitabu vingi kuhusiana na hadithi.
Katika karne ya kwanza Hijiria, wakati sera ya utawala wa jamii ilikuwa ni marufuku ya kuandika hadithi, uandishi wa hadithi za Ahlul-Bayt pia ulikuwa na mipaka, na hadithi nyingi za Maimamu wanne wa kwanza wa Shia zilipotea. Lakini katika karne ya pili ya Hijiria, kuondolewa kwa marufuku ya kuandika hadithi, kulikwenda sambamba na Mashia kuaandika vitabu vingi vya hadithi. Vitabu vya hadithi vya Shia katika zama hizo viliitwa Rasail, Asl na Musannaf. Katika kipindi cha muda mfupi kuliandikwa mamia ya vitabu vya hadithi vilivyojulikana kwa jina la Asl, ambapo muhimu zaidi miongoni mwavyo vilikuwa Usul al-Ar’ba’a Mia.
Nafasi na Umuhimu wa Kuandika Hadithi
Kuandika hadith au kuandika riwaya za Mtukufu Mtume (s.a.w.w) na Ahlul-Bayt (a.s) kumekuwa na nafasi muhimu katika kuhifadhi hadithi za Kiislamu.[1] Noor al-Din Itr, mwanachuoni wa hadithi wa Ahl al-Sunni, anasema kuwa, uandishi wa hadithi ni njia kuu ya kuhifadhi hadith na kuzifikisha kwa vizazi vijavyo. [2] Kwa mujibu wa Sayyid Mohsen Amin, mwandishi wa kitabu cha A’yan al-Shiah, Mashia waliandika vitabu vya hadithi 6,600 kuanzia zama za Imam Ali (a.s) hadi kipindi cha Imam Askari (a.s). [3]
Kwa kuwa hadithi za Maasumin (a.s) zinazingatiwa kuwa ni chanzo cha pili cha kujua elimu ya dini, kuandika hadithi ilikuwa muhimu katika zama za Mtume na Maimamu. [4] Katika hadithi mbalimbali Maasumina (a.s) walihimiza uandishi wa hadithi. [5] Mwanachuoni wa hadithi Ali Akbar Ghaffari mtambuzi wa hadithi wa Kishia, amenukuu hadithi kutoka katika kitabu Dalail al-Imamah juu ya umuhimu wa kuandika hadithi [6], ambapo kwa mujibu wake, Fatima (a.s) alipenda hadithi iliyoandikwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) kwa kiwango cha Hassan na Hussein. [7]
Kazi ya ukusanyaji hadithi katika vipindi tofauti ilikuwa na sifa tofauti; kwa hiyo, wanachuoni wa hadithi wamezungumzia kuhusu vipindi vya hadithi na wametaja sifa bainifu kwa kila kipindi. [8] Kwa mujibu wa Shahid Thani, mmoja wa wanachuoni na mafakihi wa Kishia katika karne ya 10 Hijiria, kuandika hadithi kunaweza kuwa ni wajibu au mustahab kutegemea mada na umuhimu wake. [9] Wakati wa uhai wa Shahidi Thani, kutokana na kutokuweko vitabu vya kidini kwa kiwango cha kutosha, alizingatia uandishi wa hadithi kuwa ni Wajib Aini (wajibu wa kila mtu). [10]
Uandishi wa Hadithi za Mtume (s.a.w.w)
Kwa mujibu wa hadithi nyingi zilizopokewa kutoka kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni, Mtume (s.a.w.w) alikuwa akiusia kuandikwa hadithi zake. [11] Noor al-Din Itr anaamini kwamba, hadithi zinazothibitisha uandishi wa hadithi wakati wa uhai wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) ni mutawatir. [12] Licha ya kuwa, katika vyanzo vya Ahlu-Sunna kumenukuliwa pia hadithi zinazokataza uandishi wa hadithi, lakini Muhammad Mustafa Al-A’dhami, mmoja wa wanavyuoni wa Kisunni, hatambui hata hadithi moja kati ya hizo kuwa ni sahihi. [13] Wakati wa uhai wa Mtume, baadhi ya masahaba walikusanya majimui ya hadithi chini ya jina la Sahifa, ambayo sio tu kwamba hilo halikukatazwa na Mtume, bali baadhi yao yalifanyika kwa idhini yake; [14] miongoni mwazo tunaweza kuashiria sahifa ya Abu Rafi’. [15]
Kwa kuzingatia riwaya kutoka katika kitabu cha Rijal Nijashi, Mtume (s.a.w.w) yeye mwenyewe alikuwa akimsomea imla hadithi Imamu Ali (a.s) naye akiziandika. [16] Ali Akbar Ghaffari, mtambuzi wa nakala wa kishia anakitambua kitabu cha kwanza kilichoandikwa katika Uislamu kuwa ni kitabu cha Ali (a.s). [17] Kitabu hiki kimetambuliwa kuwa ndio kikongwe zaidi miongoni mwa vitabu vya hadithi katika ulimwengu wa Kiislamu. [18] Sayyid Hassan Sadr anasema, miongoni mwa maswahaba wa Mtume (s.a.w.w) na Maimamu (a.s), Abu Rafi (mtumwa wa Mtume) ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kuandika hadithi. [19] Pia Salman Farsi, Abu Dhar al-Ghiffari na Asbagh bin Nabatah wametajwa kuwa waandishi wa kwanza wa hadith za Shia. [20] Mahdavi Rad, mmoja wa wahakiki wa Chuo cha Kidini (Hawza), alitaja majina ya masahaba 48 wa Mtume katika makala ya yake ya Sahaba wa Kitabat Hadith (Sahaba ya Uandishi wa Hadithi) ambao walikuwa amilifu na wenye harakati kubwa katika uandishi wa hadithi. [21] Kwa mujibu wa Mahdavirad, katika vitabu vya zamani, maandishi ya Maswahaba yametajwa chini ya jina la Sahifah au Nushkha. [22]
Marufuku ya Kuandika Hadithi
- Makala Asili: Marufuku ya Kuandika Hadithi
Uandishi wa hadithi za Mtume (s.a.w.w) ulipigwa marufuku katika zama za Ukhalifa wa Abu bakr na kuendelea mpaka katika zama za Khalifa wa pili Omar bin al-Khattab. Aidha marufuku hiyo iliendelea mpaka katika zama za Ukhalifa wa Omar bin Abdul-Aziz yaani kwa takriba miaka 100. [23] Mbali na Omar kupiga marufu uanzishi wa hadithi alizuia pia kunakili hadithi za Mtume (s.a.w.w). Si hivyo tu bali alichukua hatua ya kuwafunga jela masahaba kama Abu Darda na Ibn Mas’oud kwa kosa la kunakili hadithi za Mtume. [24] Kwa mtazamo wa Waislamu wa Kisunni ni kuwa, katazo na zuia la kuandika hadithi lilikuwa na lengo la kuzuia kuchanganyika hadithi na Qur’an, kuzuia kuibuka hitilafu baina ya Waislamu, [25] kuepusha kueneza hadithi zisizo na itibari [26] na wasiwasi wa kuibuka kitabu kingine kando ya kitabu cha Qur’an. [27] Hata hivyo, kwa mujibu wa mwandishi wa kitabu cha “Maan’i Tadwin al-Hadith” (Marufuku ya Kuandika Hadithi), waandishi wengi wa Kishia wanaamini kwamba moja ya sababu za kukataza na kuzuia kuandika hadithi ilikuwa ni kuzuia kuenea kwa fadhila za Imam Ali (a.s). [28] Ili kuzuia kuandika hadithi kuna matukio ambayo yametajwa kuhusiana na hilo ambapo miongoni mwayo ni kuangamizwa maandiko ya kwanza ya hadithi, kupachika hadithi za bandia, kubadilisha Sunna za Mtume (s.a.w.w) na kujitokeza madhehebu mbalimbali. [29] Pamoja na hayo, baadhi ya waandishi wanaamini kwamba, marufuku ya kuandika hadithi kwa Masuni haikutoa pigo kwa uga wa hadithi wa Shia. [30]
Kuondolewa Marufuku
Marufuku ya kuandika hadithi iliendelea mpaka katika kipindi cha ukhalfa wa Omar ibn Abdul-Aziz (63-101 H), Khalifa wa Nane kutoka katika ukoo wa Bani Umayyah ambapo alitoa marufuku hiyo. [31]. Kwa mujibu wa Ibn Hajar Asqalani, mmoja wa wanavyuoni wa hadithi wa Kisunni, Ibn Shahab Zuhri ndiye mtu wa kwanza miongoni mwa Masunni aliyeanza kukusanya hadithi kwa amri ya Omar Ibn Abdul Aziz mwaka 100 AH. [32] Kadhalika Suyuti mmoja wa waandishi wa wa Ahlu-Sunna amewataja watu kama Malik bin Anas (93-179), Sufyan Thauri (97-161 AH) na Ibn Juraij (80-150) kuwa, ni miongoni mwa waandishi wa kwanza wa hadithi wa Kisunni ambao walikusanya hadithi katika katika milango tofauti (maudhui mbalimbali) [33]. Kwa mujibu wa Rasul Jafarian, mwanahistoria wa Kishia, ingawa baadhi ya hadithi za Sunni ziliandikwa katika karne ya pili ya Hijiria, lakini hadi mwanzoni mwa karne ya tatu suala la kuandika hadithi halikuwa jambo la kawaida na lililokuwa limeenea na baadhi ya wanazuoni wa Sunni waliziandika hadithi hizo kwa kulazimika na kwa ajili tu ya hifadhi ya kumbukumbu zao. [34]
Uandishi wa Hadithi za Ahlul-Bayt (a.s)
Kwa mujibu wa Sayyid Hassan Sadr, mwanachuoni wa hadithi wa karne ya 14, Mashia ambao wanazichukulia hadithi za Maimam (a.s) kuwa ni hoja sawa na hadithi za Mtume (s.a.w.w), tangu awali wakiwafuata Maimamu wao walizingatia na kulipa umuhimu suala la kuandika hadithi, [ 35] kwa vile kabla ya zama Sadiqayn (a.s) yaani Maimamu Baqir na Sadiq, sera iliyokuwa inatawala katika jamii ilikuwa ni marufuku ya uandishi wa hadithi, uandishi wa hadithi na Mashia naopia ulikuwa na mipaka; kwa muktadha huo, Majid Ma'arif, mmoja wa watafiti wa Kishia, anaamini kwamba, hadithi nyingi za Maimamu wanne wa kwanza wa Kishia zimepotea. [36] Pamoja na hayo, wakati wa ukhalifa wake, Imam Ali (a.s) alikuwa na waandishi ambao walikuwa wakiandika barua na amri zake, ambazo baadhi yake zimekusanywa katika Nahj al-Balagha. [37]
Baada ya kuondolewa marufuku ya kuandika hadithi miongoni mwa Masunni, Maimamu wa Kishia waliwahimiza masahaba wao kuandika hadithi, na wakati mwingine walikuwa wakiwasomea imla wanafunzi darsa zao na wakati mwingine walikuwa wakitoa majibu ya maandishi kwa maswali ya Shia. [38] Kwa mujibu wa Rasul Jafarian kuanzia zama za Imamu Swadiq (a.s) na kuendelea, kuliandikwa vitabu vingi vya hadithi. [39] Baadhi ya hadithi za Shia zilizokusanywa katika kipindi hiki ziliandikwa chini ya anuani za: Rasail, [40] Asl na Musannaf. [41] Vitabu vilivyojulika kwa jina la Asl ni vile ambavyo waandishi wake walisikia hadithi moja kwa moja kutoka kwa Imamu au kwa kuweko mtu mmoja tu katikati. [42] Baada ya muda vitabu hivyo viliondokea kuwa vyanzo vya vitabu vingine. [43] Kwa maagizo ya Maimamu masahaba zao walifanya hima ya kuandika na katika kipindi cha muda mfupi tu kukajitokea mamia ya vitabu vilivyojulikana kwa jina la Asl [44] ambapo muhimu zaidi miongoni mwavyo vilikuwa mashuhuri kwa jina la Usul al-Ar’baa Mia. [45] Kulikuwa na vitabu vingine vilivyojulikana kwa jina la Musannaf ambavyo navyo vilikuwa vyua hadithi ambapo mwandishi wake hakutosheka tu na kunukuu hadithi bila ya kupitia kwa mtu, bali mbali na kunakili hadithi, alibainisha mtazamo wake kuhusiana na mapokezi ya hadithi husika. [46]
Vyanzo
- Abū l-Faraj al-Iṣfahānī, ʿAlī b. al-Ḥusayn. Maqātil al-ṭālibīyyīn. Najaf: 1385 AH.
- Abū Rayya, Maḥmūd. Aḍwāʾ ʿala al-sunnat al-muḥammadiyya. Beirut: Muʾassisa al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, [n.d].
- Abū Zahū, Muḥammad. Al-Ḥadīth wa al-muḥaddithūn. Riyadh: 1404 AH.
- Abū Zahū, Muḥammad. Al-Ḥadīth wa al-muḥaddithūn. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿArabī, 1404 AH.
- Aʿzamī, Muḥammad Muṣṭafā. Dirāsāt fī al-ḥadīth al-nabawī wa tārīkh tadwīnih. Beirut: al-Maktab al-Islāmī, 1413 AH.
- ʿAskarī, Sayyid Murtaḍā. Naqsh-i aʾimma dar Iḥyāʾ dīn. [n.p]. Nashr-i Majmaʿ ʿIlmī, 1357 Sh.
- ʿAjjāj Khaṭīb, Muḥammad. Al-Sunna qabl al-tadwīn. Beirut: Dār al-Fikr, 1401 AH.
- Bukhārī, Muḥammad b. Ismāʿīl al-. Ṣaḥīḥ al-Bukhārī. Beirut: Dār al-Qalam, 1405 AH.
- Dārmī, ʿAbd Allāh b. ʿAbd al-Raḥmān. Sunan Dārmī. [n.p]. Nashr-i Istanbul, 1401 AH.
- Dhahabī, Shams al-Dīn Muḥammad. Tadhkirat al-ḥuffāz. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1374 AH.
- Ḥusaynī Jalālī, Muḥammad Riḍā. Tadwīn al-sunna al-sharīfa. [n.p]. Daftar-i Tablīghāt-i Islāmī, 1413 AH.
- Ibn al-Athīr al-Jazarī, ʿAlī b. Muḥammad. Usd al-ghāba fī maʿrifat al-ṣaḥāba. Beirut: Dār al-Fikr, 1409 AH.
- Ibn Abī l-Ḥadīd, ʿIzz al-Dīn. Sharḥ Nahj al-balagha. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1378 AH.
- Ibn Saʿd, Muḥammad. Al-Ṭabaqāt al-kubrā. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1410 AH/1990.
- Ibn Ṣalāḥ, ʿUthmān b. ʿAbd al-Raḥmān. Maʿrifat anwāʿ ʿilm al-ḥadīth. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, 2002.
- Ibn ʿAbd al-Barr, Yūsuf b. ʿAbd Allāh. Jāmiʿ bayān al-ʿilm wa faḍlih. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, [n.d].
- Ibn Māja, Muḥammad ibn Yazīd . Sunan Ibn Māja. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1407 AH.
- Ibn Ghaḍāʾirī, Aḥmad b. Ḥusayn. Rijāl Ibn Ghaḍāʾirī. Edited by Muḥammad Riḍā Jalālī. Qom: 1422 AH.
- Ibn Qutayba al-Dīnawarī, ʿAbd Allāh b. Muslim . Taʾwīl mukhtalaf al-ḥadīth. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, [n.d].
- Ibn Ḥajar al-ʿAsqalānī, Aḥmad b. ʿAlī. Tahdhīb al-tahdhīb. Beirut: Dār al-Fikr, 1404 AH.
- Ibn Ḥajar al-ʿAsqalānī, Aḥmad b. ʿAlī. Fatḥ al-bārī bi sharḥ ṣaḥīḥ al-Bukhārī. Beirut: Dār al-Maʿrifa, [n.d].
- Ibn Ḥajar al-ʿAsqalānī, Aḥmad b. ʿAlī. Hady al-sārī. Beirut: Dār al-Maʿrifa, [n.d].
- Khaṭīb Baghdādī, Aḥmad b. ʿAlī. Taqyīd al-ʿilm. [n.p]. Dār Iḥyāʾ al-Sunna al-Nabawī, 1974.
- Khoeī, Abū l-Qāsim. Al-Bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Beirut: Dār al-Zahrāʾ, [n.d].
- Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmiyya, 1363 Sh.
- Katānī, Muḥammad Jaʿfar. Al-Risāla al-mustaṭrifa. Beirut: Dār al-Bashāʾir, 1414 AH.
- Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār al-jāmiʿa li-durar akhbār al-aʾimmat al-aṭhār. Beirut: Muʾassisat al-Wafāʾ, 1402 AH.
- Maʿārif, Majīd. Pazhūhishī dar tārīkh-i ḥadīth-i Shīʿa. [n.p]. Intishārāt-i Ḍarīḥ, 1374 Sh.
- Maʿārif, Majīd. Tārīkh-i ʿumūmī-yi ḥadīth. [n.p]. Intishārāt-i Kawīr, 1377 Sh.
- Maʿārif, Majīd. Tadwīn-i ḥadīth dar miyān-i Ahl-i Sunnat. Dānishnāmah-yi Jahān Islām, vol. 6. 1380 Sh.
- Maʿrūf al-Ḥasanī, Hāshim. Dirāsāt fī al-ḥadīth wa al-muḥaddithūn. Beirut: Dār al-Taʿāruf, [n.d].
- Najāshī, Aḥmad b. ʿAlī al-. Rijāl al-Najāshī. Edited by Mūsā Shubayrī Zanjānī. Qom: 1407 AH.
- Nayshābūrī, Muslim b. Ḥajjāj. Al-Ṣaḥīḥ. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1972.
- Qāsimī, Jamāl al-Dīn. Qawa'id al-taḥdīth. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1399 AH.
- Rāmyār, Maḥmūd. Tārīkh-i Qurʾān. 2nd edition. Tehran: Intishārāt-i Amīr Kabīr, 1362 Sh.
- Suyūṭī, Jalāl al-Dīn. Tadrīb al-rāwī. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿArabī, 1405 AH.
- Sharaf al-Dīn, ʿAbd al-Ḥusayn. Al-Murājiʿāt. Egypt: Muʾassisa al-Najāḥ, 1399 AH.
- Shahristānī, ʿAlī. Manʿ tadwīn al-ḥadīth. Beirut: Muʾassisa al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, [n.d].
- Ṣubḥī Ṣāliḥ. ʿUlūm al-ḥadīth wa muṣṭaliḥihi. Qom: Manshūrāt al-Raḍī, 1363 Sh.
- Ṣadr, Sayyid Ḥasan al-. Taʾsīs al-Shīʿa li-ʿulūm al-Islām. [n.p]. Manshūrāt al-Aʿlamī, [n.d].
- Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Maʿānī al-akhbār. Beirut: Dār al-Maʿrifa, 1399 AH.
- Ṣaffār, Muḥammad b. Ḥasan. Baṣāʾir al-darajāt. Tehran: Muʾassisa al-Aʿlamī, 1362 Sh.
- Tirmidhī, Muḥammad ibn ʿĪsā al-. Al-Jāmiʿ al-ṣaḥīḥ. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1408 AH.
- Ṭabāṭabāʾī, Sayyid Muḥammad Ḥusayn al-. Qurʾān dar Islām. Tehran: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1353 AH.
- Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-.Tārīkh al-umam wa l-mulūk. Beirut: Dār al-Maʿrifa, [n.d].