Nenda kwa yaliyomo

Umarufuku wa Kuandika Hadithi

Kutoka wikishia

Umarufuku wa Kuandika Hadithi (Kiarabu: منع تدوين الحديث) ni kuzuia kunukuu na kuandika hadithi za Bwana Mtume (s.a.w.w) tukio ambalo lilitokea katika karne ya kwanza Hijiria. Marufuku ya kuandika na kunukuu hadithi ilianza katika zama za Khalifa wa kwanza na Khalifa wa pili na iliendelea mpaka katika zama za Ukhalifa wa Omar ibn Abdul-Aziz yaani tukio hili lilidumu kwa takribani miaka 100.

Maulamaa wa Ahlu-Sunna wanasema kuwa: Sababu ya Khalifa wa Kwanza na wa Pili ya kutekeleza sera na siasa hii ilikuwa ni kuzuia kuchanganyika Qur’ani na hadithi, kuzuia kuibuka hitilafu baina ya Waislamu, hofu ya kujishughulisha watu na kitu kisichokuwa Qur’an na wapokezi wa hadithi kutojua kuandika.

Wanazuoni wa Kishia wao wanaamini kuwa: Sababu na msukumo wa kuzuia kuandikwa hadithi ilikuwa ni kuzuia kuenea fadhila za Imamu Ali (a.s) na kufanyika juhudi za kuimarisha utawala wa Makhalifa. Kwa mujibu wa Mashia ni kwamba: Marufuku ya kuandika hadithi ilipelekea kuweko hadithi za bandia, kusambaratika maandiko (matini) ya awali ya hadithi, kuibuka madhehebu mbalimbali na kubadilika Sunna za Bwana Mtume (s.a.w.w).

Historia Yake kwa Mukhtasari

Marufuku ya hadithi ni istilahi inayotumika kubainisha zuio la kuandika na kunukuu hadithi za Bwana Mtume (s.a.w.w). Historia ya kutambuliwa rasmi hilo inarejea katika zama za Masheikh wawili (Abu Bakr na Omar). [1] Kabla ya hapo, kuandika na kunukuu hadithi ni jambo lililokuwa limeenea baina ya Waislamu [2] na Mtume (s.a.w.w) alikuwa akiwashajiisha masahaba zake kuandika na kunukuu hadithi. [3]

Katika kipindi cha uongozi wa Ukhalifa wake, Abu Bakr alipiga marufuku kuandikwa hadithi na alichoma na kuangamiza hadithi nyingi. [4] Kadhalika imekuja katika vitabu vya hadithi ya kwamba, Khalifa wa Pili alikuwa akiwatahadharisha magavana wake na suala la kunakili hadithi za Mtume na akiwatolea mwito na kuwataka wazingatie Qur’ani. [5] Kwa mujibu wa vyanzo vya Ahlu-Sunna ni kwamba, Omar ibn al-Khattab awali alikuwa na uamuzi wa kukusanya hadithi na kuziandika; lakini baada ya muda akaachana na kazi hii na sababu ya hilo alitangaza kuwa ni uwezekano wa kuchanganyika hadithi na Qur’ani Tukufu. [6]

Marukufu ya Kunukuu Hadithi

Baada ya kutangazwa marukufu ya kuandika hadithi, baadhi ya masahaba wa Mtume wakawa wakiwanukulia watu hadithi za Mtume. Kwa msingi huo, Khalifa wa Pili akatangaza marufuku ya kutotoka Madina [6] masahaba wa Mtume bila idhini na kunukuu hadithi. [8] Si hivyo tu bali alichukua hatua ya kuwafunga jela masahaba kama Abu Darda na Ibn Mas’oud kwa kosa la kunakili hadithi za Mtume. [9] Baadhi ya wahakiki wanasema, kuna uwezekano kwamba, marufuku na zuio la kuandika hadithi lilichukuliwa baada ya marufuku ya kunakili hadithi. [10]

Kuondolewa Marufuku

Marufuku ya kunakili na kuandika hadithi iliendelea mpaka katika kipindi cha ukhalfa wa Omar ibn Abdul-Aziz (63-101 H), Khalifa wa Nane kutoka katika ukoo wa Bani Umayyah. Alimuandikia barua Abu Bakr ibn Hazm gavana na mtawala wa Madina na kumtaka aandike hadithi za Mtume; kwani kuna wasiwasi na hofu ya kupotea elimu na watu wake. [11]

Waungaji Mkono na Wapinzani

Inaelezwa kuwa, baadhi ya Masahaba na Tabiina akiwemo Zayd ibn Thabit, Abu Mussa, Abu Saeed Khudri, Abu Hurayrah na Ibn Abbas walikuwa wakiona kuwa kuandika hadithi ni makuruhu na huku watu kama Imamu Ali (a.s), Imamu Hassan, Abdullah ibn Omar, Anas bin Malik, Ata ibn Yasar na Saeed ibn Jubayr walikuwa wakiamini kwamba, jambo hilo linajuzu.

Sababu na Misukumo

Ahlu-Sunna na Mashia wana mitazamo tofauti kuhusiana na sababu ya marufuku na zuio la kuandika hadithi. Wanazuoni wa Kisuni wanasema: Sababu ya marukufu ya kunukuu na kuandika hadithi ilitokana na kuweko hofu ya kuchanganyika hadithi na Qur’an, [13] na kuzuia kuibuka hitilafu baina ya Waislamu, [14] wasiwasi wa kupungua kuzingatiwa na kupewa umuhimu suala la kuhifadhi hadithi na hivyo kutosheka tu na maandiko yake, [15], hofu ya watu kujishughulisha na kitu kingine kisichokuwa Qur’ani, [16], kuzuia kuenea hadithi zisizo na itibari, [17] wasiwasi wa kuibuka kitabu ambacho kitakuwa kando ya Qur’an [18] na wapokezi wa hadithi kutokujua kuandika. [19]

Hata hivyo kwa mujibu wa Sayyid Ali Shahristani katika kitabu chake cha Man’u Tadqin al-hadith ni kwamba, akthari ya waandishi wa Kishia wanaamini kuwa, moja ya sababu za kupiga marufuku uandishi wa hadithi ilikuwa ni kuzuia kuenea sifa na fadhila za Imamu Ali (a.s). [20] Miongoni mwa ushahidi wao ni kwamba, Ahmad Nasai mmoja wa waandishi wa Sihah Sittah, amenukuu kutoka kwa Ibn Abbas ya kwamba, wahusika waliamua kuacha Sunna za Mtume kwa sababu ya chuki waliokuwa nayo dhidi ya Imamu Ali. [21] Miongoni wa sababu na misukumo yao mingine ya kupiga marufuku hadithi ni Makhalifa hao kutokuwa na hali ya ufahamu wa kila nyanja wa hukumu za dini na kufanya kwao juhudi kwa ajili ya kuimarisha utawala na mamlaka yao ya kisheria pamoja na mamlaka yao ya kisiasa. [22]

Bidaa au Sunna?

Wanaoafiki na kuunga mkono marufuku ya kunukuu na kuandika hadithi wakiwa na lengo la kuthibitisha nadharia yao wanatumia hadithi kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) ambayo inasema: “Kila ambaye ameandika kitu kutoka kwangu isipokuwa Qur’ani, basi na akitokomeze (akiangamize)”. [23] Kwa upande wao wanaopinga marukufu ya hadithi wananukuu hadithi kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) ambazo zinaagiza kuandika hadithi zake; miongoni mwazo ni hadithi ambayo ndani yake Abdullah ibn Omar ametakiwa aandike hadithi. Kwa mujibu wa hadithi hii, Makureshi walikuwa wakimlaumu Abdallah ibn Omar kutokana na kuandika na kutunza maneno ya Bwana Mtume (s.a.w.w), lakini Mtume alimshajiisha aandike hadithi. [24] Kadhalika kuna hadithi inayosema: Kila ambaye atanukuu elimu au hadithi kutoka kwangu, basi ataendelea kupata ujira na thawabu madhali hadithi hiyo ingali katika maandishi. [25]

Baadhi ya wanasema, katika zama za uhai wa Bwana Mtume (s.a.w.w) baadhi ya masahaba waikuwa wakikusanya majimui ya hadithi kwa anuani ya Sahifa; ikiwemo Sahifa ya Imamu Ali (a.s) na Sahifa ya Ubayy ibn Rafi ambapo sio tu kwamba, hilo halikukatazwa na Mtume, [26] bali baadhi ya kazi hizo zilifanyika kwa ruhusa na idhini yake. [27]

Nadharia ya Ignac Goldziher

Ignac Goldziher, msomi na mtaalamu wa mambo ya nchi za mashariki (orientalist) wa Kiyahudi anaamini kuhusiana na kuibuka majimui ya hadithi za Kiislamu katika nusu ya pili ya karne ya pili. Anaamini kuwa, hadithi za kupiga marufuku na kukataza kuandika hadithi na hadithi za ruhusa ya kuandika, zote mbili ni bandia na kimsingi zinaakisi hitilafu za kimitazamo mwanzoni mwa Uislamu. [28]

Matokeo

Kwa itikadi ya Maulamaa wa Kishia ni kuwa, zuio na katazo la kuandika hadithi, lilikuwa na matokeo hasi muhimu ambapo kuangamia matini za awali za hadithi, kupachikwa hadithi za bandia, kubadilika Sunna za Mtume na kuibuka madhehebu mbalimbali ni miongoni mwa matukio hayo:

  • Kuangamia matini (maandiko) za awali za hadithi: Maneno yaliyoandikwa na masahaba wa karibu kutoka kwa Mtume (s.a.w.w), yaliangamizwa na kutokomezwa katika kipindi hiki na kutopatikana tena. [29] Kwa mujibu wa kile kilichonukuliwa na Bibi Aisha ni kuwa, Abu Bakr alichoma hadithi 500 za Mtume (s.a.w.w). [30] Kadhalika baadhi ya hadithi ambazo zilikuwa zimehifadhiwa katika vifua na kumbukumbu za masahaba kutokana na kupigwa marufuku uandikaji wa hadithi, zilipotea na kutopatikana tena baada ya kifo cha masahaba hao waliokuwa wamehifadhi hadithi hizo. [31]
  • Hadithi za bandia: Kutekelezwa sera na siasa ya kupiga marufuku kunukuu na kuandika hadithi na kufuatia kufariki dunia wapokezi wa hadithi, suala la kunukuu hadithi bandia na za kutunga na kuzinasibisha na Bwana Mtume (s.a.w.w) likawa limeenea katika zama hizo. [32] Kwa mfano kukiwa na lengo la kuandaa mazingira ya fadhila kwa ajili ya shakhsia wa kisiasa na kidini, kulinukuliwa hadithi ambazo zilinasibishwa na Mtume ambapo zilikuwa zikijumuisha hata watu ambao walizaliwa baada yake. [33] Kukithiri upachikaji wa hadithi za uongo na za bandia kulikuwa kukubwa kiasi kwamba, kitabu cha Sahihi Bukhari kinajumuisha hadithi 2,761 ambazo hazijajikariri ambazo zimechaguliwa kutoka miongoni mwa hadithi 600,000 [34] na katika Sahih Muslim kuna hadithi 4,000 ambazo si za kujikariri ambapo mwandishi wa kitabu hiki anasema amezichagua kutoka karika hadithi 300,000. [35]
  • Kubadilika Sunna za Mtume (s.a.w.w): Baadhi wamesema kuwa, marufuku ya kuandika hadithi ilipelekea kubadilika Sunna za Mtume katika jamii. [36] Ili kuthibitisha madai haya kumetumiwa baadhi ya nukuu za kihistoiria; ikiwemo hadithi iliyonukuliwa na Imamu Shafi, kiongozi wa madhehebu ya Shafi ambapo amenukuu kutoka kwa Wahab ibn Keisan ambapo kwa mujibu wake Sunna zote za Mtume zimebadilika hata Swala. [37]
  • Kuibuka madhehebu: Kupotea na kutokomea Sunna za Mtume na kubadilika, kuongezeka idadi ya hadithi bandia na zenye malengo na utashi, kulipelekea kuibuka madhehebu mbalimbali na matawi tofauti ya kitheolojia na kifikihi; [38] hii ni kutokana na kuwa, tofauti za utashi zilikwenda sambamba na uwekwaji wa hadithi za bandia na hivyo kulikuwa kukipelekea kujitenga kundi miongoni mwa makundi na kundi fulani katika jamii ya Kiislamu na kuanzisha madhehebu mpya. [39]

Monografia

Kitabu cha Man’u al-hadith, asbab wanataij kilichoandikwa na Sayyid Ali Shahristani, kinahusiana na sababu na matokeo ya kuzuia kuandikwa hadithi za Mtume. Mtarjumi wa kitabu hiki anasema: Mwandishi wa kitabu hiki anathibitisha kwamba: Kujitokeza “Maktaba ya Ijtihadi na Nadharia” yalikuwa matokeo ya marufuku ya hadithi. [40] Kitabu hiki kimeandikwa kwa lugha ya Kiarabu ambapo taasisi ya Al-Alami Lil-mat’buat ilikichapisha na kukisambaza mwaka 1418 Hijria. Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Baiti pia imechapisha tajruma ya kitabu hiki kwa lugha za Kifarsi na Kiingereza. [41].