Nenda kwa yaliyomo

Ulumu al-Qur’ani

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Elimu juu ya Qur'ani)

Ulumu al-Qur’ani (Kiarabu: علوم القرآن) ni mkusanyo wa elimu zinazohusiana na Qur'ani zinazotumiwa ili kuelewa mambo kadhaa, yakiwemo; asili na kiini cha mafunzo ya Qur’ani, mabadiliko ya kihistoria, misingi ya Tafsiri na tafiti mbali mbali zilizofanywa kuhusiana na Qur’ani. Kuthibitisha kuwa Qur’ani ni ufunuo, asili ya maandishi yake na pia kuitetea Qur’ani dhidi ya pingamizi mbali mbali, ni miongoni mwa sababu za kuu zinazoipa umuhimu na hadhi maalumu elimu hii. Sayansi za Qur’ani (ulumu al-Qur’ani) zinachukuliwa kuwa ni tofauti na maarifa ya Qur’ani (elimu ya tafsiri), na hupewa kipaumbele kabla ya kuingia katika elimu ya tafsiri.

Baadhi ya Aya za Qur’ani Hadithi za bwana Mtume (s.a.w.w) pamoja na Maimamu (a.s), ndio jiwe la msingi katika kuanzishwa kwa fani hii ya sayansi za Qur’ani, na Msahafu wa tafsiri wa Imamu Ali (a.s) unahisabiwa kuwa ndiyo kazi ya mwanzo kabisa kufanyika kuhusiana na sayansi za Qur’ani. Mchakato wa maendeleo ya Sayansi za Qur’ani umeelezewa kufanyika kupitia hatua kadhaa, ambazo ni; Uandishi wa makala maalumu kuhusiana na Qur’ani, uliyo fanyika mnamo katika karne ya kwanza na ya pili, kuundwa na kuzaliwa rasmi kwa fani hii mnamo karne ya tatu na ya nne, kuakisiwa katika tangulizi za tafsiri mbali mbali za Qur’ani hadi karne ya nane, na kutambulishwa rasmi kama ni elimu kamili kuanzia karne ya nane na kuendelea.

Kuongezeka kwa fikra za Kishia katika Sayansi za Qur’ani kulianza na tafiti zilizo fanywa na wanazuoni wa Kishia akiwemo; Sayyid Murtadha, Sheikh Saduq, Sheikh Mufidu, na Fadhil bin Hassan Tabrasi kuanzia karne ya tano hadi ya saba Hijiria. Mada kuu na masuala ya msingi katika Sayansi za Qur’ani ni: Wahyi, Kuteremshwa kwa Qur’ani, Sababu za Kushuka kwa Aya au Sura, Qiraa-aat a-Sab-a, Fadhila (Faida) za Sura, Tajwidi, Muhkumu (Aya za Wazi) na Mutashabihu (Aya Tatanishi), Nasikh (Aya Zilizofutwa Hukumu Zake) na Mansukh (Aya Mbadala), Miujiza ya Qur’ani, Mpangilio wa Kuteremka kwa Sura, Ukusanyaji wa Qur’ani, Makkiyya (za Makka) na Madaniyya (za Madina), Historia ya Qur’ani, Kutoharibiwa kwa Qur’ani, na Hurufu Mukatta'a (Herufi Zisizo Unda Neno Kamili).

Umuhimu na Nafasi Yake

Muhammad Hadi Ma'arifat, mfasiri wa Kishia na mwana nadharia wa Sayansi za Qur’ani, anaona kwamba; Elimu hii ni muhimu zaidi kuliko tafiti za kuelewa yaliomo ndani ya Aya za Qur’ani, yaani ni muhimu zaidi kuliko elimu ya tafsiri ya Qur’ani; [1] kwa sababu, kwa mujibu wa maoni yake yeye, Sayansi za Qur’ani ni mkusanyo wa elimu za msingi zinazo muezesha mtu kuelewa maudhui za Qur’ani na pia kuthibitisha kuwa ni ufunuo utokao kwa Mungu. [2] Kwa mujibu wa Muhammad Ali Kusha, mfasiri na mtafiti wa kisasa wa Qur’ani, ni kwamba; Tafiti kuhusiana na Qur’ani pamoja na welewa wa masuala yake, ulianza tangu enzi za mwanzo za Uislamu, na wanazuoni wengi walikaa kitako kujadiliana kuhusiana na mada hii. [3]

Sababu zilizotajwa juu ya umuhimu wa Sayansi za Qur’ani ni pamoja na: kuthibitisha kuwa Qur’ani ni ufunuo, kuthibitisha asili ya maandishi ya Qur’ani na kutoharibiwa kwake katika muda wote, jukumu la msingi la kufasiri na kutafuta welewa wa Qur’ani, pamoja na kujenga uwezo wa kuilinda Qur’ani dhidi ya pingamizi tofauti kutoka kwa wapinzani mbali mbali. [4]

Sababu muhimu za mtu kujifunza kuelewa sayansi za Qur’ani, ni ule mwingiliano na uhisiano uliopo kati ya sehemu mbalimbali za sayansi za Qur'ani na sayansi nyingine za Kiislamu kama vile; historia na sira, hadithi, elimu ya lugha na fasihi ya Kiarabu, akida, tafsiri, fiqhi pamoja na usul-ul-fiqhi. [5] Hivyo basi, kutokana na wenevu mkubwa wa mada za Qur'ani ulioko katika sekta za elimu mbali mbali, umepelekea watafiti kutumia njia na nyenzo mbali mbali katika tafiti zao, kama vile; Elimu za lugha, historia na hadithi, fasihi na chambuzi zake, elimu ya hadithi na elimu ya rijali (tafiti juu ya wapokezi wa Hadithi). [6] Hata hivyo, imeelezwa kwamba njia zote hizi mwishowe ima huhushwa na nukuu fulani, akili, au uchambuzi wa lugha. [7]

Kwa mujibu wa Ahmad Paaketchi, mtafiti wa sayansi za Qur'ani, ni kwamba; elimu hii ilizaliwa kwenye kutoka kwenye mieleka ya tafsiri za Qur’ani kutoka kwa wanazuoni wa sayansi mbali mbali za Kiislamu. Kikawaida kila mtaalamu wa fani fulani, huwa ameathiriwa na fani hiyo katika welewe wake, hii ilipelekea kila mfasiri kutoa tafsiri yake kulingana na mtazamo wake wa kielemu, jambo ambalo liliweza kuzalisha tafsiri zenye mirengo tofauti, kama vile tafsiri yenye rangi ya kiakida, kifiqhi na kifalsafa. Kila moja kati ya tafsiri hizo, zilikuwa zikilenga wanafunzi au washabiki wenye mitazamo yenye rangi za mirengo sayansi hizo. Jambo lilipelekea wanazuoni wa sayansi za Qur'ani kujaribu kutafuta kivukio kitachowavusha watu kutoka kweye bahari za wataalamu wenye mirengo mbali mbali ya kielimu na kuwakaribisha katika welewe mmoja katika kuifahamu Qur'ani hii. [8] Wataalamu wa sayansi za Qur’ani, kwa kutumia istilahi maalumu kama vile; nasikh na mansuukh, muhkam na mutashabih, na asbabun nuzul, waliweza kujenga lugha ya pamoja kati ya tafsiri zenye mirengo mbalimbali. [9]

Welewa wa Dhana (Conceptology)

Kulingana na maelezo ya Muhammad Hadi Ma'arifat, ni kwamba; Sayansi za Qur’ani ni jina au ibara inayohusisha ndani yake masuala yanayohusiana na uelewa wa Qur’ani, [10] ambao ndani yake inajumuisha tafiti kadhaa kama vile; Wahyi, Kuteremshwa kwa Qur’ani, Mpangilio wa Sura na Aya Zake, Sababu za kushuka Kwake, Waandishi wa Wahyi, Kusawazisha kwa Misahafu, Ukusanyaji, Uandishi, Kuzaliwa kwa Viraa (Visomo) na Chanzo cha Tofauti za Viraa Hivyo, Uthibitisho wa Usahihi wa Qur’ani na Kutoharibiwa Kwake, Miujiza, Tafsiri, Nasikh na Mansukh, Muhkamu na Mutashabihu pamoja na pia kuitetea Qur’ani dhidi ya pingamizi mbali mbali. [11] Hata hivyo, baadhi ya watafiti wanaamini kuwa fani ya Sayansi za Qur’ani haijajifunga kwenye mada hizo maalum, bali hupanuka kulingana na sababu mbalimbali ikiwemo uibukaji wa maswali mapya yanayojitokeza katika zama na nyakati mbali mbali. [12] Ayatullah Jawadi Amuli, mmoja wa wanazuoni na mwandishi wa Tafsir Tasnim, anaamini kuwa; Sayansi za Qur’ani ina sehemu tatu kuu: Sehemu inayohusiana na tafsiri, ambayo kwa kweli ni kuelewa maana ya Aya za Qur’ani; Sehemu inayohusiana na ufahamu wa Qur’ani kama vile: kuteremshwa kwake, miujiza ya Qur’ani, idadi ya Sura, ukusanyaji, qira'a, n.k.; na sehemu ya tatu inayohusiana na aina fulani ya elimu na hekima za siri, ambazo lau kama kusingekuwepo Qur’ani, basi kusingekuwepo mwenye kuzielewa na kuzitambua elimu hizo katika jamii ya wanadamu, na hata bwana Mtume (s.a.w.w) asingekuwa na ujuzi nazo. Qur’ani ikitupa mafunzo kuhusiana na jambo hili inasema: (وَ يُعَلِّمُكُمْ مَا لَمْ تَكُونُوا تَعْلَمُونَ ; Na anakufunzeni (Mola wenu) yale ambayo hamkuwa mkiyajua), na katika Aya nyengine Mwenye Ezi Mungu anamwambia Mtume wake ya kwamba: (وَعَلَّمَكَ مَا لَمْ تَكُن تَعْلَمُ ; Na amekufunza (Mola wako) yale ambayo hukuwa ukiyajua). [13] Fani ya Sayansi za Qur’ani, ambayo katika fasihi ya Kifarsi pia inayojulikana kwa jina la «Ulume Qur’aniy» / Elimu au Sayansi za KiQur’ani, [14] humaanisha mkusanyiko wa elimu zinazohusiana na ufahamu mzima wa Qur’ani tukufu, [15] elimu ambazo hutumika katika harakati za kuelewa asili ya Qur’ani, mabadiliko yake ya kihistoria, misingi mingine yote ya welewa Qur’ani na tafsiri ya yake, pamoja na shughuli na tafiti mbali mbali zilizofanywa kuhusiana na Qur’ani. [16] Watafiti wengine wanasema kwamba; Ibara ya «Elimu au Sayansi za Qur’anii» inaweza kuwa na maana tofauti kama vile: «Sayansi za ndani ya Qur’ani» ambazo ni elimu za Qur’anii au elimu ambazo zipo katika Aya za Mwenyezi Mungu na zinapatikana kutoka katika Qur’ani, au «Sayansi kwa Ajili ya Qur’ani» ambazo ni sayansi zote zinazohudumia Qur’ani au zinazotegemea au kuwa na mafungamano fulani na Qur’ani, kama vile: Hadithi, Theolojia, Lugha, Kanuni za Fiqhi, Hadithi, Historia na Sira.

Tofauti Kati ya Sayansi za Qur’ani na Sayansi Nyingine Zinazohusiana na Qur’ani

Elimu zinazohusiana na Qur’ani zimegawanywa katika makundi matatu:

  1. Elimu za ndani ya Qur’ani, kama vile; imani, maadili na hukumu za kisheria, [17] ambapo moja ya matunda yake ni tafsiri ya kimaudhui. [18]
  2. Elimu funguzi ambazo ni msingi wa kufahamu Qur’ani, kama vile sarufi, nahau, mantiki na balagha zinazotumika kuelewa maneno na maana ya Qur’ani. [19]
  3. Sayansi zilizo nje ya Qur’ani ambazo zinazohusiana na Qur’ani. Kama vile; historia ya Qur’ani na pamoja historia ya bwana Mtume (s.a.w.w), miujiza ya Qur’ani na njia za kuthibitisha kuwa Qur’ani ni ufunuo wa Mungu. [20]

Chimbuko na Historia Yake

Mpini wa tafiti kuhusianana na Qur'ani umeshikama na mwanzo wa kuteremshwa kwa Qur’ani yenyewe. Kwa mujibu wa maelezo ya Muhammad Ali Mahdawi-Rad, ambaye ni mtafiti wa Qur’ani, ni kwamba; Aya zinazohusiana na kutochafuliwa kwa Qur’ani, Aya zinazo husiana na kuteremshwa kwa Qur’ani, Aya zinazohusu Wahyi, muhkumu na mutashabihu, pamoja na nasikh na Mansukh, ni miongoni mwa tafiti ambazo Qur’ani yenyewe imejishughulisha nazo. [21] Pia imeelezwa kuwa; Sayansi za Qur’ani, ni sawa na sayansi nyingine za Kiislamu, zilianzishwa kwa kutumia Qur’ani pamoja na Hadithi. [22] Katika muktadha huu imeelezwa kwamba; Msingi mkuu na wa mwanzo uliotunika katika uanzilishi wa sayansi za Qur’ani ni: Hadithi za bwana Mtume (s.a.w.w) na Ahlu-Bayt (a.s), kuhusiana na fadhila (faida) za Qur’ani, Hadithi kuhusiana na visomo saba vya Qur’ani isemayo: (اُنزل القرآن علی سَبعة الاحرف ; Qur’ani imeteremshwa kwa lugha (lahaja) saba), pamoja na ripoti za Al-qurraa (Wasomaji maarufu wa Qur’ani kama vile Hafsi), zilizo tajwa katika vyanzo ya Hadithi. [23]

Mushafu wa Tafsiri wa Imamu Ali (a.s) unachukuliwa kuwa ndiyo kazi ya kwanza kabisa iliyoandikwa kuhusiana na baadhi ya tafiti za Sayansi za Qur’ani. [24] Kwa mujibu wa watafiti, kazi hii iliandikwa aidha wakati wa Mtume (s.a.w.w) au mara tu baada ya kufariki kwake, Msahafu ambayo ulikusanywa na Imamu Ali (a.s) kwa mpangilio wa historia ya kushuka kwa Qur’ani, ikijumuisha masuala kadhaa kama vile; nasikh na mansukh, mahkumu na mutashabihu, na sababu za kushuka kwa Aya na Sura za Qur’ani. [25]

Kwa mujibu wa maelezo ya Subhi Saleh, kazi za kwanza kuhusiana na Sayansi za Qur’ani, kwa maana ya kiistilahi (kitaalamu) ya “Ulumu Al-Qur’ani/ Sayansi za Qur’ani”, zilianza mnamo karne ya tatu Hijria kupitia kitabu kilichoitwa “Al-Hawi fi Ulum al-Qur’ani” kilichoandikwa na Muhammad bin Khalaf bin al-Marzban, [26] kikituatiwa na kitabu “Aja’ib Ulum al-Qur’ani”, kilichoandikwa mnamo karne ya nne Hijria na Abu Bakar Muhammad bin Qasim bin Bashar al-Anbari (aliyefariki mwaka 328 Hijria). [27] Kwa mujibu wa watafiti, kitabu “Aja’ibu Ulumi al-Qur’ani” ilikuwa ndia kazi ya kwanza kushughulikia baadhi ya mada kwa maana halisi ya jina hili la “Sayansi za Qur’ani” ambapo ilijishughulisha na fadhila (faida) za Qur’ani, namna ya kushuka kwake kwa lugha (lahaja) saba, uandishi wa misahafu, na idadi ya Sura, Aya pamoja na maneno yaliyomo ndani yake. [28]

Mchakato wa Ukuaji Wake

Kulingana na mtazamo wa Mohamed Hadi Ma'arifati; Elimu ya Qur'ani imepitia hatua mbalimbali za ukuaji katika karne tofauti. [29] Karne ya kwanza na ya pili Hijria zinajulikana kama ni karne za uandishi wa vitabu maalum katika maudhui hii. [30] Baadhi ya maandiko muhimu kuhusiana na kipindi hicho ni pamoja na: "Kitabu fi al-Qiraa" cha Yahya bin Yamar, mwanafunzi wa Abu al-Aswad al-Du-ali, "Kitabu Adad Aayi al-Quran" cha Abu al-Hassan al-Basri, Kitabu Gharib al-Quran cha Aban bin Taghlib, mwanafunzi wa Imam Sajjad (a.s), na Kitabu al-Ayat al-Mutashabihat cha Muqatil bin Suleiman. [31]

Imeelezwa kwamba mwanzo wa kuundwa au kuanzishwa rasmi kwa elimu ya Qur'ani kulifanyika mnamo karne ya tatu na ya nne Hijiria, ambayo iliendana sambamba na ukuaji wa masuala ya lugha na kilele cha mijadala na tafiti za kikalamu (elimu ya akida) kuhusiana na Qur'ani. [32] Miongoni mwa watu maarufu karne hizi mbili katika nyanja za elimu za Qur'ani ni; Yahya bin Ziyad al-Farra', Ibn Qutaybah al-Dinawari, Hassan bin Ali bin Faddhaal, ambaye ni miongoni mwa wafuasi wa Imam Ridha (a.s), Umar bin Bahr maarufu kama al-Jahidh, na Ahmad bin Musa bin Mujahid (Sheikh al-Qurraa wa Baghdad). [33] Katika kipindi hichi, kuliibuka mijadala maalumu kuhusiana na asili au uhalisia wa Qur’ani, pamoja na maswali kadhaa yatokanayo na shaka za kiitikadi, ambacho pia kiliambatana na kuenea kwa mawazo ya Mu'utazila na kuenea kwa visomo saba maarufu vya Qur'ani. [34]

Kuongezeka Kwa Fikra za Shia Ndani ya Fani ya Sayansi za Qur’ani Kuongezeka kwa tafiti za kifasihi na fikra za Shia katika uwanja wa tafiti za Qur'ani, kunarjea kwenye karne ya tano hadi ya saba Hijiria. Wanazuoni maarufu wa Shia kama vile; Sayyid Murtadha, Sheikh Saduq, Sheikh Mufidu, Sayyid Razi, Qutb al-Diin Rawandi, Fadhlu bin Hassan Tabarsi, na Sayyid bin Tawus ndio walio jihusisha rasmi na tafiti za Qur'ani katika kipindi hichi. [35] Katika kipindi hichi, vitabu kadhaa vya tafsiri vilianza kuakisi Tafiti za ulumu al-Qur'ani ndani ya tangulizi zake. Miongoni mwa vitabu vilivyo akisi fani hiyo katika utangulizi wake ni; Tafsir Majma'u al-Bayan, Al-Tibyan, Tafsir al-Safi, Alaa al-Rahmani na Al-Bayanu fi Tafsiri al-Qur’an. [36]

Karne ya nane hadi ya kumi inajulikana kama ni kipindi cha kuimarishwa, kukamilishwa na kutangazwa kwa fani hii ya ulumu al-Qur'ani kama ni taaluma yenye hadhi na muundo wa fani kamili. [37] Miongoni mwa matunda ya kazi andishi muhimu zilizo fanyawa katika kipindi hichi ni; “Al-Burhan fi Ulumi al-Qur'an” cha Muhammad bin Abdullah al-Zarkashi na kitabu “Al-Itqanu fi Ulumi al-Qur'an” cha Jalal al-Din al-Suyuti [38]. Karne ya kumi na moja hadi kumi na tatu zinajulikana kama ni kipindi cha kudorora kwa fani ya sayansi za Qur'ani (ulumu al-Qur’ani), hii ni kutokana na ushawishi mkubwa wa kazi andishi maridadi ya kitabu (“Al-Itqanu fi Ulumi al-Qur'an”) iliyo fanywa na Al-Suyuti. Kazi hiyo ilitia pingu kalamu zote za wanazuoni wa kipindi hicho. Badala yake, kipindi hichi, kiligeuka kuwa ni kipindi cha kazi za kuandika vitabu maalumu vyenye kutoa orodha ya vitabu vihusianavyo na fani ya Ulumu al-Qur’ani pamoja na kamusi zinazo tafiti maneno ya Qur'ani. Kutoka na kuongezeka kwa harakati za Akhbariyyina, baadhi ya kazi muhimu kuhusiana na fani ya sayansi za Qur'ani (ulumu al-Qur’ani), ziliandikwa katika vyanzo vya vya Hadithi, hii ni kwa kuwa wao walikuwa na mrengo wa Kihadithi uliofurutu ada. Miongoni mwa kazi andishi muhimu za wakati huo ni ile orodha kamili zaidi kuhuisana na maudhui za Aya za Qur'ani ilioko katika kitabu kiitwacho Biharu al-Anwari kilicho andikwa na Allama Majlisi. [39]

Karne ya kumi na nne na kumi na tano zinajulikana kama ni karne za upanuzi na kuendeleza upya fani ya sayansi za Qur'ani. Kipindi hichi kilianza na uandishi wa kitabu Fasl al-Khitab fi Tahrif Kitab Rabb al-Arbab kilichoandikwa na Muhaddith Nuri kuhusiana na mabadiliko na upotoshwaji uliopita ndani ya Qur'ani, jambao ambalo liliambatana na upinzani dhidi yake. Katika enzi hii, kulikuwa na maendeleo ya kiasi cha chini katika fani ya sayansi za Qur'ani. Kazi andishi muhimu ya wakati huo kuhusiana na fani ya sayansi za Qur'ani, ilikuwa ni kitabu cha Muhammad Hadi Ma'rifat kilichoitwa Al-Tamhid fi Ulum al-Qur'ani. Sifa kuu za kipindi hichi ni pamoja na; Kujibu pingamizi dhidi ya Qur'ani na kuingia kwa wasomi kadhaa wa Kimagharibi katika nyanja za fani ya Sayansi za Qur’ani, ambao miongoni mwano ni; Ignaz Goldziher, Theodor Nöldeke, Arthur Jeffery, Toshihiko Izutsu. Kipindi ambacho pia kiliambatana na kuibuka kwa wimbi la wasomi na wanafikra wapya wa kidini waliojishughulisha na fani hii, wakiwemo; Muhammed Arkoun, Nasr Hamid Abu-Zaid na wengineo. [40]

Maudhui za Fani ya Sayansi za Qur’ani

Madhui kuu zinazo jadiliwa katika fani ya sayansi za Qur'an, huku kila moja ikiwa na jina na hadhi kama ni elimu binafsi, ni pamoja na: wahyi, kushushwa kwa Qur'ani, sababu za kushushwa kwake, usomaji kupitia visomo au lahaja saba, fadhila (faida) za Qur'ani, tajwid, Aya za wazi na Aya kanganyifu, Aya zifutazo na Aya zifutwazo, miujiza ya Qur'ani, mpangilio wa kushushwa kwa Sura, ukusanyaji wa Qur'ani, Makkiyya na Madaniyya, historia ya Qur'ani, kutokuwepo kwa mabadiliko na upotoshwaji katika Qur'ani, pamoja na herufi ziundazo Aya bila ya kuunda neno lenye maana ifahamikayo, kama vile Haa Miim na Alif Laam Miim.

Wahyi

Makala kuu: Wahyi

Wahyi ni mawasiliano ya manabii na ulimwengu wa ghaibu kwa ajili ya kupokea ujumbe wa Mwenye Ezi Mungu. [41] Neno "Wahyi" katika Qur'ani limetumika likimaanisha maana tofauti kama vile; ishara ya siri (kama ilivyo kuja katika kisa cha Nabii Zakaria), [42] mwongozo wa kimaumbila kwa wanyama kama nyuki, [43] ufunuo wa kwa vitu visivyo na uhai, [44] ufunuo kwa wasio manabii kama mama wa Musa, [45] na Wahyi kwa manabii wa Mungu. [46] Kulingana na wafasiri wa Qur’ani ni kwamba, wahyi kwa manabii hufanyika kwa njia tatu: mazungumzo ya moja kwa moja bila ya kuwepo pazia fulani kati ya Mungu na nabii wake, kupitia mwakilishi (mjumbe maalumu) asiye mwanadamu kama vile Jibril, na kwa njia ya nyuma ya pazia. [47]

Muujiza wa Qur'ani

Makala kuu: Muujiza wa Qur'ani na Aya za Changamoto

Muujiza wa Qur'ani unarejelea sifa za kipekee za Qur'ani ambazo ni za; kimuundo, kimaneno na kimatini, zilizopo nje ya uwezo wa kibinadamu. Kwa mweye katika kuelewa Qur’ani atafahamu kwamba; katu sifa kama hizo za ajabu haziwezi kuletwa na mwengine yeyote yule isipokuwa Mwenye Ezi Mungu. [48] Qur'an, ili kuthibitisha muujiza wake, inatoa changamoto kwa wapinzani wake [49] kwa kuwataka walete maandiko yanayofanana na Qur'ani hii. [50] Wakati Qur’ani ikitoa changamoto zake, imewata wapinzani wake ima waje na Sura chache zifananazo na Qu’ani, [51] au angalau sura moja tu. [52]

Sababu za Kushuka kwa Aya na Sura za Qur’ani

Makala kuu: Sababu za Kushuka kwa Aya na Sura za Qur’ani

Sababu za kushuka au kwa lugha ya Kiarabu “Shān Nuzūl” zinarejelea watu, matukio, na mahali ziliposhuka Aya au Sura za Qur'ani tukufu. [53] Sababu za kushuka kwa Qur’ani zina umuhimu mkubwa katika kutafsiri Aya za Qur'ani. [54] Wanazuoni wa Kiislamu wameandika vitabu maalum kuhusiana na sababu za kushuka kwa Aya na Sura za Qur’ani tukufu. Ni muhimu kuelewa kwamba, sio Aya zote za Qur'ani zina sababu maalumu kuhusiana na kushuka kwake. Baadhi ya watafiti wa Qur'ani wamekadiria idadi ya matukio 460 kuhusiana na sababu za kushuka kwa Qur’ani. [55] Wafasiri wa Kishia na baadhi ya wafasiri wa Kisunni wamerekodi idadi ya sababu kadhaa za kushuka kwa Aya zinazohusiana na hadhi na sifa za Imam Ali (a.s.) pamoja na Sifa na wasifu wa Ahlul-Bait (a.s). [56]

Kushuka kwa Qur'ani

Makala kuu: Kushuka kwa Qur'ani

Kushuka kwa Qur'ani ni kule bwana Mtume (s.a.w.w) kushushiwa Aya za Qur'ani kupitia ufunuo maalumu. [57] Si sawa kutumia neno "kushuka" katika maana inayofahamika kupitia hisia za kimwili, katika welewa wa dhana ya kuhusiana kwa Qur'ani tukufu; hivyo basi, wanafikra wa Kiislamu wametumia ibara maalumu kuhusiana na maudhui hii, ili kuzikingiusha akili kutoka kwenye maana ya kihisia kwenda kwenye maana za kiroho. Maneno yaliyotumiwa na wanatafakuri hawa katika kuwakilisha maana kusudiwa ya dhani ya ni pamoja na; kushuka kiroho (نزول روحانی) , [58] kushuka kwa mfumo halisia (نزول حقیقی) , [59] na kushuka kidaraja (ونزول مقامی) . [60]Kuna ibara na maneno kadhaa katika Qur’ani yanayo ashiria suala la kushuka kwa Qur’ani, miongoni mwayo ni kama vile; «anzalna", «nazzalna», «awhayna», «sanulqi», «sanuqri-uka», «nat-luha», na «rattalnahu». [61]

Miongoni mwa tafiti zenye khitilafu katika mada za fani ya sayansi za Qur'ani, ni suala la kushuka kwa Qur'ani kwa hatua mbili; hatua ya kushuka kwake yote kwa pamoja, na hatua ya polepole au kipengele kwa kipengele. Watafiti kama vile Muhammad Hadi Ma'rifat wanaamini juu ya kushuka kwa Qur’ani kwa mfumo wa polepole peke yake, [62] ila kwa upande mwingine, watu kama vile Allama Tabatabai wanaamini juu ya kushuka kwa Qur'ani kwa njia zote mbili za mfumo mmoja na polepole. [63]

Fadhila (Sifa au Faida) za Qur'ani

Makala kuu: Fadhila za Sura

Fadhila za Sura (فضائل سُوَر) ni mkusanyiko wa Hadithi zinazobainisha nafasi na hadhi ya Sura za Qur'ani pamoja na athari za kidunia na za kiakhera zinazopatikana katika kusomwa kwake. [64] Lengo kuu la Hadithi hizi za fadhila za Sura za Qur’ani, ni kuwatia moyo Waislamu kusoma Qur'an na kutafakari juu yake. [65] Kuna Hadithi nyingi kuhusu fadhila za Sura na Aya za Qur'ani zinazo patikana katika vyanzo vya Hadithi za Kishia na pamoja Kisunni. [66] Hadithi hizi zimegawanya sifa za Sura katika makundi mawili: [67] fadhila (faida) na sifa (athari) maalumu, huku sifa maalumu za Sura zikiwa zimegawanywa katika makundi mawili; sifa (faida) za kidunia [68] na sifa (faida) za kiakhera. [69] Qur'an pia nayo imeashiria baadhi ya fadhila (sifa) za baadhi ya Sura za Qur’ani. [70]

Kutunga kwa Hadithi bandia ni mojawapo ya madhara makubwa kwenye nyanja za fadhila (sifa) za Sura za Qur’ani. Miongoni mwa Hadithi bandia zilizo maarufu zaidi kuhusiana na nyanja hii, ni zile Hadithi zinazohusishwa na Abayya bin Ka'ab na Ibn Maryam Marwazi. [71] Kuna khitilafu za kimitazamo kati ya wanazuoni kuhusiana na matumizi ya Hadithi dhaifu zinazo husiana na fadhila (sifa) za Sura za Qur’ani. Ingawa baadhi ya wanazuoni wanaojuzisha kutumia Hadithi hizo. Waliojuzisha matumizi ya Hadithi hizo dhaifu wametegemea hoja mbili muhimu zilizopo kwenye sharia za kifiqi; moja ni kanunu (qaida) ya kifiqi, isemayo kuwa; ni vyema kusahilisha mambo juu ya Hadithi zinazohusiana na mambo ya Sunna, na ya pili ni Hadithi ya Man balagh, ambayo kwa mujibu wake watu walipwa kulingana na dhana zao njema katika kuamiliana na Riwaya zilizo wafikia. Hoja mbili hizi ndizo zilizo jenga dhana na kisingizio cha kuamiliana vyema na Hadithi hizo dhaifu. [72]

Visomo Saba

Makala kuu: Wanaosomaji Saba

Wanaosoma saba, au Maquraa saba, walikuwa ni wasomaji saba Qur'ani Tukufu walio ishi katika karne ya pili ya Hijria. Wasomaji hawa walikuwa na tofauti katika njia ya kusoma baadhi ya maneno ya Qur'ani. Wao walijifunza njia zao hizo za kusoma kutoka kwa baadhi ya Matabiina, ambao nao walikuwa wanafunzi wa Masahaba. [73]

Waislamu wa Kisunni wengi wanaamini kuwa visomo saba vimepokewa kwa njia ya mutawatir, na hata miongoni mwa Waislamu wa Kishia, kuna baadhi wanazuoni ya wanazuoni kama vile Allama Hilli na Shahid Thani wanao amini kuwa viomo hivi zimepokewa kwa njia ya mutawatir na pia inajuzu kwa mwenye kusali kutumia moja ya visomo hivyo katika sala yake. [74]

Muhkam na Mutashabih

Makala kuu: Muhkam na Mutashabih

Muhkam na Mutashabih ni maneno mawili yanayorejelea sifa za makundi mawili ya Aya za Qur'ani. Aya zenye sifa ya Muhkam ni zile Aya ambazo maana yake huwa iko wazi kabisa, kiasi kwamba haiwezi kuwa na maana nyingine zaidi hiyo, Aya ambazo huwa ni wazi na zisizo na shaka katika kueleweka kwake. Kwa upande mwingine, Mutashabih ni zile Aya zenye sifa pembuzi, ambazo zina uwezekano wa kuwa maana kadhaa, kwa hiyo huwa ni gumu kuweza kupata maana halisi na ya moja kwa moja kutoka katika Aya hizo, kiufupi Aya hizi twaweza kuzipa jina la “Aya Kanganyifu” amabazo kikawaida huwa ni zenye kuzipembua akili. [75] Baadhi ya Waislamu wa Kisunni wanaamini kuwa Mwenye Ezi pee ndiye mwenye elimu ya Aya hizo za Mutashabih; [76] lakini kwa mujibu wa watafiti kama vile Muhammad Hadi Ma'rifat, kulingana na Aya ya saba ya Surat Aal-Imran, wanaamini kwamba; Elime hiyo inawezekana kufikiwa na wanazuoni walio watoharifu pamoja na wafuasi wao walioshikamana nao kwa yakinifu. [77]

Naskh na Mansukh

Makala kuu: Naskh na Mansukh

Naskh na Mansukh ni makundi mawili ya Aya za Qur'an ambapo Aya ya Naskh huwa inabadilisha hukumu ya Aya ya Mansukh na kwa kuteremka kwa Aya ya Naskh, muda wa kutekelezwa kwa mafunzo au amri za Aya ya Mansukh huwa unakomea hapo. [78] Kwa mujibu wa watafiti wa Qur'an na wanazuoni wa fiqhi, ni kwamba; suala Naskh na Mansukh ni la kaida kuanzia kwenye Qur’ni hadi kwenye Hadithi. Kwa hiyo kuna Naskh ya Qur'an kwa Qur'ani, Qur'an kwa Sunna, Sunna kwa Sunna, na Sunna kwa Qur'ani inakubalika na ina historia yake. [79]

Rejea

Vyanzo