Al-I’jaz al-Qur’an

Kutoka wikishia

Al-I’jaz al-Qur’an (Kiarabu: الإعجاز القرآني) maana yake ni kwamba, hakuna mwanadamu mwenye uwezo wa kuandika kitabu mfano wa Qur’an au kushindwa mwanadamu kuleta mfano wa Qur’an hii, na lenyewe hili ni ishara ya wazi kwamba, Qur’an aliyoshushiwa Bwana Mtume (s.a.w.w) ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Maulamaa wa Kiislamu wanaitambua Qur’ani kuwa ndio muujiza mkubwa zaidi wa Mtume (s.a.w.w) na dalili na hoja ya Utume wake. Suala la muujiza wa Qur’an ni katika maudhui za Ulum-Qur’an na teolojia ya Kiislamu.

Waislamu wanaichukulia Qur'an kuwa ni kitu ambacho hakuna mtu anayeweza kuleta mfano wake na ni muujiza katika masuala kama ya ufasaha, sayansi (elimu) maarifa, kutoa habari za ghaibu na kutokuwepo migongano ndani yake. Qur’an yenyewe imeashiria muujiza wa kitabu hiki na ikatoa changamoto katika Aya sita; Yaani imewaalika wapinzani waje na kitu kama hicho wakiweza.

Wanazuoni wa Kiislamu wameandika vitabu vingi kuhusu al-’Ijaz al-Qur’an (kushindwa mwanadamu kuleta mfano wa Qur'an), baadhi yake ni kama ifuatavyo: Al-I’jaz al-Qur’an kilichoandikwa na Abu Bakr Baghilani (aliyefariki 403 Hijiria), Al-I’jaz al-Qur’an Wal-kalam fi Wujuhih, cha Sheikh Mufid (aliyefariki 413 Hijiria), al-Sarf fi A’jaz al-Qur’an, kilichoandikwa na Seyyed Murtadha (aliyefariki 436 Hijria), Dalai al-I’jaz, kilichoandikwa na Abdul Qahir ali-Jurjani (aliyefariki dunia 471 Hijiria).

Maana ya al-I’jaz al-Qur’an na umuhimu wake

Waislamu wanaitambua Qur’ani kuwa ni muujiza wa Mtume s.a.w.w). [1] Kuwa kwake muujiza ni kwa maana hii kwamba, hakuna mwanadamu anayeweza kuleta kitabu mfano wake, kinatoka kwa Mwenyezi na katu hakuna mtu anayeweza kuleta mfano wake. [2] Shekhe Tusi katika tafsiri yake ya al-Tibyan ameitambua Qur’an kuwa, ni muujiza mkubwa zaidi na mashuhuri zaidi katika miujiza ya Mtume (s.a.w.w). [3]

Abu Bakr Baghilani (aliyefariki 403 Hijiria), mmoja wa wanazuoni wa Kisunni ameandika kuhusiana na umuhimu wa kuzingatia muujiza wa Qur’an licha ya kwamba, Mtume alikuwa na miujiza mingine, Utume wa Mtume wa Uislamu umesimama juu ya Qur’an kuwa ni muujiza; hii ni kutokana na kuwa, miujiza yake mingine ilitokea katika zama na mazingira maalumu na kwa watu kadhaa wachache; lakini Qur’an ilikuwa kwa wote na hakuna mtu aliyekana uwepo wake. [4]

Changamoto ya Qur’an

Changamoto katika Ulumul-Qur'ani [5] na teolojia ya Kiislamu, [6] maana yake ni Mitume kuwaita wale wanaokanusha utume wao kuleta mfano wa miujiza yao. [7] Qur'ani imetoa changamoto katika Aya sita; Yaani inawataka wanaokanusha kuwa ni muujiza waje na mfano kwa ajili yake. [8] Aya hizi zinaitwa Aya za changamoto. [9]

Mitazamo tofauti kuhusiana na al-I’jaz

Wanazuoni wa Kiislamu wametoa maoni tofauti juu ya kile kinachoifanya Quran kuwa muujiza. Maoni mengi ambayo Suyuti (aliyefariki mwaka wa 911 Hijria), mwanazuoni mashuhuri wa Kisunni wa Qur'ani, alitoa katika al-Itqan, ni kuhusu muujiza wa kifasihi wa Qur'ani. Bila shaka, kila moja ya maoni haya yameelezea muujiza wa kifasihi kwa mtazamo fulani. [10]

Lakini wasomi wa Kiislamu wanaamini kwamba Quran ina miujiza (hakuna mtu anayweza kuleta mfano wake) katika nyanja nyingine. Kwa mfano, Allama Tabatabai (aliyefariki dunia mwaka 1360 Hijiria Shamsia) mfasiri wa Qur’ani alisema kwamba muujiza wa Qur’ani mbali na balagha na ufasaha, unajumuisha pia elimu na maarifa, kutokujua kusoma na kuandika Mtume (s.a.w.w), habari za ghaibu. na kutokuwepo tofauti na migongano katika Qur'an. [11] Abu Bakr Baghilani, mbali na kusisitiza muujiza wa kifasihi wa Qur'ani, pia alizungumzia habari za ghaibu na Mtume kutojua kusoma na kuandika. Muhammad Hadi Marafet (aliyeaga dunia 1385 Hijria Shamsia), mtafiti wa Qur’an pamoja na miujiza ya kifasihi, pia amezungumzia miujiza ya kielimu na kisheria. [12]


Nadharia ya al-Sarfah

Nadharia nyingine inayozungumziwa kuhusu al-I’jaz al-Qur’an ni nadharia ya Sarfa. Kwa mujibu wa nadharia hii, Qur’an kuwa muujiza inamaanisha kwamba ikiwa mtu fulani alikusudia kupingana nayo, Mungu angemzuia asilete kitabu kama hicho. Kauli hii ina maana kwamba wanadamu wanaweza kuandika kitabu kama Qur'an; lakini Mungu amewanyima uwezo huo. [13] Kwa mujibu wa Suyuti, katika Al-Itqan, Ibrahim Nazam (aliishi katika karne ya 2 na 3 ya Hijria), mmoja wa wanazuoni wa Kisunni, amezungumzia hili. [14] Sayyid Murtadha na Shekhe Mufid pia wamekubali mtazamo huu. [15] Kulingana na Muhammad Hadi Marafet, wanazuoni wa Kiislamu wa zamani na leo, wameikataa nadharia hii. [16]

Pande za al-I’jaz al-Qur’an

Baadhi ya pande za al-I’jaz al-Qur’an kwa mujibu wa itikadi ya Maulamaa wa Kiislamu:

Muujiza wa kifasihi

Muujiza wa kifasihi una maana kwamba, andiko la Qur’an lina sifa maalumu ambazo hakuna mwanadamu ambaye anaweza kufanya hilo. [17] Baadhi ya sifa hizi ni kama zifuatazo: Kutumia maneno sahihi na mahala pake, kuwa na mtindo mpya na wa ajabu na wa kipekee ambao si kama mashairi ya kawaida, wala kama nathari ya kawaida, maneno matamu na muziki wa kupendeza. [18]

Kutoa habari za ghaibu

Kwa mujibu wa wanazuoni wa Kiislamu ni kuwa, Qur’ani inatoa na mambo ya zamani na yajayo ambayo hakuna mtu aliyeyajua. [19] Kwa mfano, hakuna mtu aliyekuwa akijua kuhusiana na habari na ufafanuzi wa kisa cha Maryam, Nuhu na tufani yake, Yusuf na ndugu zake na kkadhalika. [20] Pia, baada ya kushindwa kwa Roma na Iran mwaka 615 Miladia, Qur'n ilitangaza kwa uthabiti kabisa kwamba Roma ingeishinda Iran katika muda usiozidi miaka kumi, na jambo hilo hilo likatokea. [21] Utabiri kuhusiana na hatima na mambo yaliyowakumba watu kama Abu Lahab na utabiri wa kukombolewa Makka ni habari nyingine za ghaibu ambazo zote Qur’an imezitabiri na zilitokea. [22]

Muujiza wa kielimu

Makala asili: Muujiza wa kielimu wa Qur’an

Maana ya muujiza wa kielimu wa Qur’ani ni kwamba kitabu hiki kimeeleza mambo kuhusu sayansi (elimu) za majaribio ambazo yalikuwa bado hayajagunduliwa wakati ule na hakuna wakati ambao yalikwenda kinyume. [23]

Pande zingine

Muujiza wa kisheria [27] na muujiza wa kiadadi wa Qur’an [28] ni pande zingine za al-I’jaz al-Qur’n ambazo zimebainishwa na baadhi ya wasomi wa Kiislamu. Kwa mujibu wa nadharia hii hukumu na sheria ambazo Uislamu umemuwekea mwanadamu, kinyume na kanuni na sheria zilizotungwa na kuwekwa na mwanadamu, zimezingatia engo na pande zote za uwepo wa mwanadamu kama ambavyo upande wa kimaada una uratibu na upande wa kimaanawi. Sheria hizo zinadhamini saada na utulivu wa duniani wa mwanadamu kama ambavyo zinaendana na fitra na maumbile ya mwanadamu. Kutokana na kuwa hakuna mtu mwenye uwezo wa kufanya hili, ni lazima Qur’an ishuke na iwe imetoka kwa Mwenyezi Mungu. [29] Nadharia ya muujiza wa kiadadi wa Qur’an inasema kuwa, idadi ya herufi na maneno ya Qur’an yamepangika kwa namna ambayo hakuna mwandishi ambaye anaweza kuja na mpangilio kama huu na nidhamu na mpangilio huu ni ishara ya kuwa kwake muujiza. [30] Kwa mfano, katika Qur’an neno “saa” limetumika kwa maana ya idadi ya saa za usiku na mchana yaani masaa 24. Neno “shahar” (mwezi) linaanshiria idadi ya miezi wa mwaka, yaani miezi 12. Neno “Sijdah” limetumika mara 34 katika Qur’an idadi ambayo inalingana na idadi ya sijida za Sala za wajibu za kila siku. [31] Hata hivyo nadharia hii ina wapinzani wengi. [32]

Bibliografia

Kumeandikwa vitabu vingi na wasomi wa Kiislamu kuhusiana na maudhui hii. [33] Miongoni mwa vitabu hivyo ni vile vya maudhui ya teolojia ambavyo vinathibitisha Utume wa Nabii Muhammad (saww). [34] Kadhalika maudhui hii imezungumziwa katika vitabu vya Ululm-Qur’an. [35]. Baadhi ya vitabu vilivyoandikwa kuzungumzia maudhui hii pekee ni:

  1. al-Qur'an fi nazmeh va taalifeh, Abu Abdullah Muhammad bin Zayd Wasiti (aliaga dunia 306 au 307 Hijria), mmoja wa wana teolojia mashuhuri wa Baghdad. [36]
  2. E’jaz al-Qur'an Ali ibn Isa Rumani (aliaga dunia 384 Hijria), ni katika wafuasi wa Mu’tazilah wa Baghdad. [37]
  3. Bayan I’jaz al-Qur'an Abu Suleiman Hamad bin Muhammad Al-Khattabi (aliaga dunia 388 Hijria), mmoja wa Maulamaa wa hadithi wa Khorasan. [38]
  4. I’jaz al-Qur'an Qadhi Abu Bakr Baghilani (alifariki dunia 403 Hijria). [39]
  5. I’jaz al-Qur'an wa Al-Kalam fi Al-Wajah- Sheikh Mufid (alifariki dunia 413 Hijria), fakihi, mwanateolojia na mtambuzi mkubwa wa hadithi wa Kishia; [40]
  6. Al-Sarfah fi I’jaz al-Qur'an", Sayyid Murtadha (aliaga dunia 436). [41]
  7. Dalail al-Ijaz, Abdul Qahir Jarjani (aliaga dunia 471 Hijria). [42]
  8. Al-Risalah al-Shafiyyah fi I’jaz Al-Quran» Abdul Qahir al-Jurjani. [43]
  9. Nihayat al-I’jaz fi Dirayat eIi’jaz, Fakhr al-Din Razi. (aliaga dunia 606 Hijria). [44]
  10. I’jaz Quran Sayyid Muhammad Hussein Tabatabai. [45]

Pia, vitabu, makala na nadharia nyingi zimeandikwa kuhusu miujiza ya Quran. Katika makala, kumetambulishwa kazi 348 kuhusiana na maudhui hii. [46]


Rejea

Vyanzo