Nenda kwa yaliyomo

Tafsiri au tarjumi ya Qur'an

Kutoka wikishia

Tarjumi ya Qur'an (ترجمة القرآن) ni kuitoa Qur'ani kutoka lugha yake asilia (Kiarabu) na kuipeleka kwenye lugha nyingine. Hili ni miongoni mwa masuala yanayo jadiliwa katika sayansi ya Qur'ani (ulumu al-Qur’ani), ambalo linagusa pia sheria za Kiislamu na itikadi zake. Wengine wameruhusu na kujuzisha tafsiri na tarjumi ya Qur'an. Uamuzi wa wanazuoni wa mrengo huu wamegemea au kuegemea kwenye matukio ya historia pamoja na hisia ya kuwepo ulazima au wajibu wa kuutangaza Uislamu na kufikisha ujumbe wa Qur'ani. Kinyume chake, kuna wengine wanaopinga dhana hiyo, ambao hawaruhusu ufasiri wa Qur’ani, nao pia wametowa hoja kadhaa juu ya msimamo wao huo. Miongoni mwa hoja zao ni kwamba; muktadha wa matini ya Qur'ani unashikamana aina maalumu za kimiujiza ndani yake, na kwamba lugha ya Qur'ani (Kiarabu) ina ubora iliopindukia lugha nyingine zote duniani.

Inasemekana kwamba historia ya tafsiri ya Qur'an ilinaanza tokea mwanzoni mwa Uislamu, miongoni mwa matukio ya yaliyo rikodiwa katika historia, ambayo hutumiwa kama ni hoja kwa waunga mkono wa ufasiri wa Qur’ani, ni barua za bwana Mtume (s.a.w.w) kwa viongozi wa baadhi ya nchi. Tafsiri ya kwanza ya Qur'ani iliyo fasiriwa kwa lugha za Ulaya, ilianzwa na makasisi wa Kikristo kwa nia ya kutafuta kasoro za kitabu hicho. Watafiti wanaamini kwamba; Tafsiri ya kwanza ya Qur'ani kwa lugha ya Kiajemi (Kifarsi) ilifanyika mnamo karne ya nne ya Hijiria. Baadhi ya wahakiki wameorodhesha tafsiri za Kifarsi katika makundi matatu: tafsiri (tarjumi) za zamani, tafsiri za kisasa, na tafsiri za kishairi.

Njia za kutafsiri (kutarjumi) Qur'ani ni pamoja na; tafsiri ya neno kwa neno, tafsiri huria au tafsiri ya kimuktadha (isiokwenda neno kwa neno), na tafsiri fafanuzi. Tafsiri za Qur'an ni zenye kutafautia baina yake, tafauti ambazo zasemekana kusababishwa na tafauti za kinadharia katika masuala kadhaa; kama vile tafauti za kifiqhi, kifasihi, na kikalamu.

Suala la Kutafsiri (Kutarjumi) Qur'ani

Kutafsiri (kutarjumi) Qur'ani: Ni kuitoa Qur’ani kutaka lugha yake asilia (Kiarabu) kuipeleka kwenye lugha nyengine. [1] Suala la tafsiri ya Qur'an limekuwa ni mojawapo ya masuala yenye mijadala mingi miongoni mwa Waislamu. Vitabu vingi vya sayansi ya Qur'ani (ulumu al-Qur’ani), huwa na kawaida ya kutenga sura maalumu inayo jadili mada hiyo. [2] Kwa imani ya Waislamu, si maneno au matini tu, bali hata maana na uchambuzi wa Qur'ani, yote kwa pamoja yaliteremshwa kwa lugha ya Kiarabu kutoka kwa Mwenye Ezi Mungu mwenyewe. Wengine wanaamini kwamba; Lugha ya Kiarabu ni lugha takatifu, na hilo ndilo lililo ifanya lugha hiyo kuwa na uwezo pekee wa kubeba maana ya Wahyi wa Mwenye Ezi Mungu. Kwa upande wa pili, wengine wanaona kwamba; matumizi ya tamathali (majazi) za lugha katika Qur'ani, kuanatokana na mipaka ya lugha hii. [4] Kujadili masuala kama vile; muujiza wa Qur'ani, au mijadala ya utangu wa Qur’ani yenye mabishano ya kwamb; Jee Qur’ani ni kitu kilicho umbwa baadae ua kitu cha utangu (cha dahari) kama Mungu mwenyewe alivyo? Pia ni miongoni mwa masuala yaliyo pelekea kuzuka kwa mjadala katika suala la tafsiri ya Qur'an. [5]

Aina za Tafsiri (Tarjumi)

  • Watafiti wa Qur'an wameainisha aina mbalimbali za tarjumi za Qur'an, ambazo ni pamoja na tafsiri au tarjumi linganishi (Tafsiru Tatbiiqi), tarjumi au tafsiri fafanuzi (Tarjamatu Tafsiiriyah), tarjumi au tafsiri ya neno kwa neno (Tarjamatu tahta allafdhiyyah), tafsiri au tarjumi huria au ya kimuktadha (Tarjamutu Madhmuuniyah), na tafsiri ya kishairi (Tarjamatu Sh’iriyyah). Ufafanuzi wa Tarjumi hizi ni kama ifuatavyo: [6]
  • Tafsiri Liganishi: Tafsiri hua Inalingana na maneno pamoja na muktadha, kiubora pamoja na kiwingi wa ujazo wa maneno. Yaani mtarjumi huwa hamimini kiwango cha maneno kupitiliza kiwango cha ibara ya Qur’ani yenyewe ilivyo, pia hujitahidi kuto engeza au kupunguza hadhi na thamani ya maneno yaliomo ndani ya Aya azifasirizo.
  • Tafsiri ya Neno kwa Neno: Katika aina hii ya kutarjumi, mtarjumi hutoa maana ya neno kutoka kwenye lugha asilia (Kiarabu) kwenda lugha kusudiwa. Kazi hii hufanyika kwa kuweka mbadala wa kila neno kulingana na muundo kwa kutumia neno jengine lenye maana na muundo unaofanana zaidi katika lugha lengwa. Kulingana na maelezo ya Muhammad Ali Kusha, ni kwamba; tafsiri hizi haziingii katika tafsiri kwa maana ya kiistilahi (kitaalamu), bali ziko katika mfumo wa kamusi za Qur'an. [7]
  • Tafsiri Huria au ya Kimuktadha: Katika tafsiri hii, mfasiri huweka tu muktadha wa Aya katika lugha lengwa na hafungiki na mfumo kulinganisha sentensi kwa sentensi kama zilivyo. Muhammad Hadi Ma'arifat anaamini kwamba; Kazi ya aina hii ya tafsiri ni sawa na ile tafsiri yenye kudhamini maana za maneno asilia (Tafsiri Fafanuzi), ambayo lengo lake kuu ni kuwasilisha maana kwa njia na muundo bora zaidi. [8]
  • Tafsiri Fafanuzi: Hii ni Tafsiri (tarjumi) iliyo changanywa na ufafanuzi pamoja na maelezo mafupi ndani yake.
  • Tafsiri ya Kishairi: Katika tafsiri hii, maana na maudhui ya Aya, huwasilishwa kwa mtindo wa kimashairi. [9]

Mawafanikio na Makhitilafiano ya Tafsiri ya Qur'ani

Tafsiri ya Qur'ani ina wafuasi waiungayo mkono na wapinzani wenye pingamizi nayo. Imeelezwa ya kwamba; upinzani dhidi ya tafsiri ya Qur'ani ulijitokeza zaidi kati ya miaka ya 1923 na 1938 Miladia, baada ya agizo la Mustafa Kamal Atatürk, Rais wa Uturuki, la kuibadili Qur'ani kuotka kwenye luhga asilia ya Kiarabu kwenda lugha ya Kituruki. [10] Rashid Rida, mfasiri wa Kimisri, ametoa sababu kumi na tano za kuthibitisha umarufuku wa tafsiri (utarjumi) wa Qur’ani. [11]

Baadhi ya Sababu za Wafuasi Waungao Mkono Tafsiri ya Qur'an:

Hoja za Wanaoafiki Tarjumi ya Qur'ani

  • Kutumwa barua kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) kwenda kwa baadhi viongozi wa nchi fulani. [12]
  • Kitendo cha Salman al-Farsi cha kutafsiri sehemu ya Qur'ani. [13]
  • Imani ya Abdullah bin Mas'ud juu ya uwezekano wa kubadilishwa kwa maneno ya Qur'ani. [14]
  • Tafsiri ya Qur'ani na Hasan al-Basri kwa watumiaj wa lugha ya Kifarsi. [15]
  • Ujumbe wa kimataifa wa Qur'ani na umuhimu wa au wajibu kuufikishwa kwake. [16]

Baadhi ya Sababu za Wapinzani wa Tafsiri ya Qur'ani:

Hoja za Wanaopinga Tarjumi ya Qur'ani

  1. Kutowepo uwezekano wa kuhamisha muujiza wa kilugha wa Qur'ani katika kuifasiri kwake. [17]
  2. Madhara ya kutafsiri Qur'ani kwa sababu ya ubora wa lugha ya Kiarabu juu ya lugha nyingine. [18]
  3. Kutoeleweka lugha ya Qur'ani nje ya tamaduni za Kiarabu. [19]
  4. Kutoeleweka lugha ya Qur'ani nje ya mipaka ya fikra na akili za Kiarabu. [20]
  5. Uwepo wa hakika na siri zilizojificha ndani ya lugha ya Kiarabu ya Qur'ani. [21]
  6. Kukosekana kwa maneno yenye maana sawa na yale ya Qur'ani kutoka katika lugha mbali mbali. [22]
  7. Hisia ya kuto kuwa na haja ya kujifunza lugha ya Kiarabu ambayo ni moja ya sababu za umoja na mshikamano wa Waislamu. [23]

Baadhi wanaamini kwamba tafsiri ya Qur'ani inakubalika ikiwa tu tafsiri hiyo takuwa itashikamana na kisawasawa na matini asili ya Qur’ani. Yaani pamoja na tafsiri hiyo kuenda sambamba na maana msingi ya sentensi za Qur’ani, pia inatakiwa kushikamana na kila mfumo au nyenzo za kilugha za ziada zilizomo nfani yake. Yaani, kama kuna msisitizo ndani yake, pia tafsiri hiyo inapaswa kuhamisha msisitizo huo na kuuwakilsha kwenye lugha lengwa, la si hivyo tafsiri hiyo haitaweza kukubalika. [24]

Historia ya Tafsiri ya Qur'an Tukufu

Historia ya tafsiri ya Qur'an inarudi nyuma hadi mwanzoni mwa Uislamu na inahusiana moja kwa moja na suala la umuhimu wa kufikisha ujumbe wa dini hii kwa wasiozungumza Kiarabu. [25] Imeelezwa kwamba; kazi hii ilidhihiri zaidi katika matukio matatu yafuatayo:

  • Kutumwa kwa barua kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.) kwenda kwa viongozi wa baadhi ya nchi, barua ambazo ndani yake zilikuwa zimeambatana na baadhi ya Aya za Qur'ani. [26]
  • Tafsiri ya sehemu ya Qur'an iliyofanywa na Salman al-Farsi. [27] Yasemekana kwamba yeye alitafsiri "Bismillah ar-Rahman ar-Rahim" kuwa ibara ya Kiajemi isemayo: “Be Name Yaazdan Bakh-shaayande” yaani: "kwa jina la Yazdan (Mungu) Mwenye rehema. [28]
  • Tafsiri ya sehemu ya Surat Mariam kwa lugha ya Kihabeshi iliyofanywa na Ja'far bin Abi Talib. [29]

Tafsiri ya Qur'ani kwa Lugha za Ulaya

Kazi ya tafsiri ya Qur'ani kwa lugha za Ulaya ilianza kufanywa na makasisi na wamonaki (makuhani) wa Kikristo. Walifanya hivyo ili kukosoa Uislamu katika mijadala ya kitheolojia, jambao liliwapa msukumo wa kutafsiri ibara kadhaa za Qur'ani.[30] Tafsiri kamili ya kwanza ya Qur'an kwa lugha ya Kilatini iliandikwa katika karne ya sita Hijiria (karne ya kumi na mbili Miladi).[31]

Pia Qur'ani imetafsiriwa kwa lugha nyingi duniani, ikiwa ni pamoja na tafsiri za lugha za Kiafrika (kama vile Kiswahili, Kihausa, na Kiyoruba), lugha za Bara Hindi (kama vile Kiurdu na Kibangali), lugha za Kituruki (kama Kiazari na Kiistanbuli) pamoja na lugha ya Kichina na lugha ya Kijapani. [32]

Tazama Pia: Orodha ya Tafsiri za Qur'an

Historia ya Tafsiri za Qur'an kwa Kifarsi

Adharnoosh, mwandishi wa makala “Tarjumehaye Qur’ani Farisi Qur’ani / Tafsiri za Qur'an kwa Kifarsi" katika kiitabu kiitwacho “Dairatu al-Maarif Bozorge Islami / Ensaiklopidia Kuu ya Kiislamu”,anaseam kwamba; Tafsiri rasmi ya kwanza ya Qur'ani kwa lugha ya Kifarsi ilifanyika mnamo karne ya nne Hijiria. Tafsiri hii ilifanywa kwa idhini ya Amir Nuh, mfalme wa nasaba ya Kisamaniy, aliye wataka wanazuoni wa wakati wake kufanya kazi hiyo, na baadae kimakosa ilijulikana kama ni Tafsir al-Tabari. [33]

Waajemi walibaki na tafsiri hiyo hadi karne ya nane, baada ya hapo kukapatikana tafsiri nyengine iitwayo Tafsir-i Ghazur. [34] Kwa maoni ya baadhi ya watafiti ni kwamba; Ukosefu huu wa tafsiri ulitokana na uvamizi wa Wamongolia. Iipoingia karne ya kumi na mbili, kulipatikana mabadiliko muhimu katika suala la tafsiri. Mabadiliko muhimu ni kupatikana kwa tafsiri ya “Fath al-Rahman” ya Shah Waliullah Dehlawi, [35] ambayo kwa mujibu wa baadhi watafiti, ilikuwa ni tafsiri ya kipekee kutokana na mtindo wake wa uandishi na utangulizi wake wa kuelezea mbinu za tafsiri, jambo ambalo limepelekea kuhisabiwa kuwa ni moja ya tafsiri bora za Qur'an za wakati huo. [36] Karne ya kumi na nne inajulikana kama ni kipindi cha wimbi la tafsiri za Qur'an. [37]

Orodha ya Tafsiri za Qur'an kwa Kifarsi

Makala Kuu: Orodha ya Tafsiri za Qur'an kwa Kifarsi
Tarjumi ya Muhammad Mehdi Foulavand

Tafsiri za Qur'an kwa Kifarsi zimegawanywa katika sehemu tatu: za sasa, za kale na za kishairi. Orodha ya tafsiri hizo ni kama ifuatavyo: [38]

  • Tafsiri za Kale:
  1. Tafsiri al-Tabari
  2. Tafsiri Ma'ani Kitab Allah Ta'ala
  3. Tafsiri al-Munir ya Abu-Nasr Ahmad bin Muhammad Haddadi
  4. Tafsiri ya Juzuu mbili za Qur'an kutoka kwa mfasiri asiyejulikana, iliyochapishwa mwaka 1353 Hijiria Shamsia, iitwayo "Puliy Miyane Shi’iri Hijaai wa ‘Urudhiy Farsi"
  • Tafsiri za Sasa zinazohusiana na karne ya kumi na nne na kumi na tano Hijiria:
  1. Tafsiri ya Taahiri Saffarzadeh
  2. Tafsiri ya Muhammad Mahdi Fuladvand
  3. Tafsiri ya Nasir Makarim Shirazi
  4. Tafsiri ya Ghulamali Haddad Adil
  5. Tafsiri ya Hussein Ostadwali
  6. Tafsiri ya Sayyid Ali Musawi Garmarudi
  7. Tafsiri ya Hussein Ansarian
  8. Tafsiri ya Ali-Asghar Barzi
  9. Tafsiri ya Abulfadhli Bahrampour
  10. Tafsiri ya Sayyid Kadhim Arif
  • Tafsiri za Kishairi:
  1. Tafsiri ya Mirza Hassan Esfahani (Safi Ali Shah)
  2. Tafsiri ya Omid Majdi
  3. Tafsiri ya Muhammad Shaeq
  4. Tafsiri ya Sayyid Muhammad Ali Muhammadi (Musawi Jazairi)

Sababu za Tofauti katika Tafsiri za Qur'an

Baadhi ya watafiti wa sayansi za Qur'an (ulumu al-Qur’ani) wameorodhesha sababu kadhaa zanazo pelekea kupatikana tofauti katika tafsiri za Qur'an. Sababu hizo ni kama ifuatavyo:

  • Fiqh: Kuwepo kwa tofauti katika misingi ya fiqhi kati ya Waislamu wa Shia na Sunni, hasa katika Aya za hukumu (Ayat al-Ahkam).
  • Lugha: Kuwepo kwa tofauti katika kuchagua neno sahihi kwa ajili ya tafsiri ya maneno.
  • Miundo: Kuwepo tofauti za kimiundo kati ya lugha mbalimbali, hasa katika miundo ya sifa-wasifu, na sifa-miliki, miundo ambayo kikawaida huwa haina mfanano wa moja kwa moja wa lugha asili (Kiarabu cha Qur’ani) na lengwa.
  • Sentensi na Miundo: Kuwepo kwa khitilafu za miundo ya ibara na sentensi, hasa katika sentensi zenye miundo changamani na tata.
  • Ijazi (Ufupisho): Kuondoa herufi, majina, maneno, na sentensi kwa ajili ya ufupisho wa kifasihi, uliofanyika katika Aya mbali mbali za Qur’ani.
  • Marejeo ya Viwakilishi: Kutokuwepo kwa uwazi wa marejeo ya viwakilishi katika baadhi ya Aya.
  • Mitazamo ya Kiimani: Tofauti katika ufahamu wa kiitikadi katika kufasiri Aya za kiimani, kama vile suala la kudura, kumuona Mungu, na isma (utakatifu wa kutokosea) kwa manabii. [39]

Tafsiri ya Kundi ya Qur'ani

Mwanzoni mwa karne ya kumi na nne Hijiria, suala la tafsiri ya Qur'ani lilizua mjadala mkubwa kutokana na tafsiri ya Kiingereza ya Muhammad Ali Lahori katika mabaraza ya kielimu ya Misri, hasa katika Chuo Kikuu cha Al-Azhar, mjadala ambao uliendelea kwa kiasi cha muda wa miaka mia moja. [40] Mnamo mwaka 1355 Hijiria, Muhammad Mustafa al-Maraghi, mkuu wa wakati huo wa chuo kikuu cha Al-Azhar, alitoa pendekezo kwa Waziri Mkuu wa Misri kuhusiana na kutafsiri Qur'ani kwa pamoja na rasmi kwa lugha ya Kiingereza. [41]

Huko Iran, baadhi ya watafiti wanaamini kuwa kuna muhimu wa kutengeneza tafsiri ya Kifarsi ya pamoja kupitia juhudi za watafiti wa sayansi za Qur'an (ulumu al-Qur’ani) na wanazuoni wa dini, watakaosaidiwa na serikali. [42]

Hukumu ya Kisheria (Fiqhi) Kuhusu Kusoma Tafsiri ya Qur'an Katika Sala

Wanazuoni wa fiqhi wa Kishia wamekubaliana kwa pamoja ya kwamba; Haifai kusoma tafsiri ya Qur'ani katika sala. [43] Wanazuoni wa madhehebu ya Shafi'i, Hanbali, na Maliki pia wamekubaliana kwamba; Haifai kufanya hivyo katika sala. [44] Hata hivyo, Abu Hanifa aliruhusu jambo hili. [45] Kwa mujibu wa mtazamo wake; Lugha ya Qur'ani haina utakatifu wa kiasilia, na kwa kuzingatia Aya ya 196 ya Suratu Al- Shu'ara, ni kwamba; yaliyomo kwenye Qur'an pia yapo katika lugha nyingine zilizomo katika vitabu vya awali. Kwa hiyo, kusoma tafsiri ya Qur'ani ni sawa na kusoma Qur'ani yenyewe. [46]

Masuala Yanayo Fungamana

Rejea

Vyanzo