Nenda kwa yaliyomo

Dua ya Arubaini na Nne ya kitabu cha Sahifa Sajjadiyya

Kutoka wikishia

Dua ya Arubaini na Nne ya kitabu cha Sahifa Sajjadiyya: ni miongoni mwa dua adhimu yaliyotufikia kutoka kwa Imamu Sajjad (a.s), aliyekuwa akiisoma dua hiyo wakati wa kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Katika dua hii, Imamu Sajjad (a.s) anaainisha majukumu ya Mu'min wa kweli katika Ramadhani na anabainisha masharti ya saumu iliyo sahihi. Jenginge lililomo katika dua hii, ni yale maombi yake ya kumuomba Mwenye Ezi, Mungu kinga dhidi ya fitna na shari za Shetani. Mwanzoni mwa dua hii tukufu, Imamu Zain al-Abidin (a.s) ameanza kwa kumshukuru Mwenye Ezi Mungu kwa kuwajalia waja wake neema ya shukrani. Kisha anamwomba Mwenye Ezi Mungu amtakase kutokana na uchafu wa dhambi, na ampe taufiki ya kufikia daraja tukufu za watu wema na wachamungu. Dua tukufu ya arubaini na nne iliyoko katika kitabu cha *Sahifa Sajjadiya* imepata fursa ya kushereheshwa (kupewa tafsiri chambuzi) na maulamaa walioifasiri dua hiyo kwa lugha mbali mbali sambamba na dua nyengine zilizomo katika kitabu hicho. Miongoni mwa tafsiri chambuzi zilizoandikwa kwa lugha ya Kiajemi, ni pamoja na ile ya Sheikh Hussein Ansariyan iliyoko katika kitabu chake kiitwacho ‘Diare Asheqan’, tafsiri ya Sheikh Hassan Mamduhi Kermanshahi, iitwayo ‘Shuhud va Shenakht’, pamoja na kazi ya Ayatullahi Mohammad-Taqi Mesbah-Yazdi katika kitabu chake kiitwacho ‘Sahbaye Huzur’. Na kwa upande wa lugha ya Kiarabu, tafsiri chambuzi ya dua hii adhimu inapatikana katika kitabu kiitwacho ‘Riyad as-Salikin’, kilichoandikwa na al-Allamah Sayyid Ali Khan Madani.

Mafunzo Yanayopatikana Ndani ya Dua ya Arubaini na Nne Dua ya arubaini na nne ya Sahifa Sajjadiyya ni dua maalumu iliyokuwa ikisomwa na Imamu Sajjad (a.s) katika mapokezi ya kuupokea mwezi wa Ramadhani. Maudhui ya dua hii yanajikita katika kubainisha fadhila za mwezi huu mtukufu, na sambamba na hilo, pia dua hii inaelezea kwa kina nyadhifa na majukumu ya muumini katika kipindi hicho cha mwezi wa Ramadhani. [1] Maudhi zilizomo ndani ya dua ya arubaini na nne zimekuja katika vipengele vifuatavyo: • Kumshukuru Mwenye Ezi Mungu kwa kuwapa waja wake fursa ya kuwa na shukrani kwa Mola wao. • Uhusiano wa moja kwa moja kati ya kushukurani na kupata ongezeko la neema za Mwenye Ezi Mungu. • Malipo mema ya Mwenye Ezi Mungu kwa wale wanaomshukuru. • Kumsifu na kumshukuru Mwenye Ezi Mungu kwa kutunukiwa neema ya dini. • Ramadhani ni mwezi wa kuufikia wema na kupata radhi za Mwenye Ezi Mungu. • Ramadhani ni mwezi wa kusimama imara katika ibada. • Majina ya mwezi wa Ramadhani: (Mwezi wa Mwenye Ezi Mungu, Mwezi wa kusalimu amri na kuwa na unyenyekevu mbele ya Mwenye Ezi Mungu, Mwezi wa utakaso, Mwezi wa majaribio (mwa kutakaswa kupitia mtihani wa saumu), Mwezi wa kusimama kwa katika ibada, Mwezi wa kuteremshwa Qur'an). • Ubora wa mwezi wa Ramadhani kuliko miezi mingine. • Ubora wa Laylatul-Qadr (Usiku Wenye Cheo) kuliko masiku mengine. • Waja kunufaika na baraka za kudumu za usiku wa Laylatul-Qadr. • Maombi ya kuomba kuujua utukufu wa mwezi wa Ramadhani. • Kuomba taufiki ya kuutukuza mwezi wa Ramadhani. • Kuomba kuepuka na usikilizaji wa maneno ya upuuzi na kutazama mambo yasiyofaa ndani ya mwezi wa Ramadhani. • Kuomba taufiki ya kujiepusha na kugusa vilivyoharamishwa pamoja na kuepukana na katika njia za haramu. • Kuomba kuepushwa na kula chakula cha haramu. • Kuomba taufiki ya kuzungumza kulingana na matakwa na maagizo ya Mungu. • Kuomba taufiki ya kufanya matendo bila mema kujionyesha au kutafuta sifa za walimwengu. • Umuhimu wa kuzingatia nyakati za sala tanondani ya mwezi wa Ramadhani. • Hadhi ya juu ya wale wanajali hadhi na umuhimu wa sala za lazima. • Kanuni za kufunga na mambo yanayoharibu saumu: kudhibiti uchu wa viungo vya nje pamoja na vya ndani, kuwa na nia safi, n.k. • Kuomba taufiki ya kufikia daraja za juu kuliko Malaika kupitia matendo mema na usafi wa kujitenga na dhambi. • Uislamu unakidhi mahitaji yote ya asili ya mwanadamu. • N yenendo bora za kimaadili na kijamii ndani ya mwezi wa Ramadhani: kuunga undugu, kuwa na uhusiano mzuri na majirani, kusafisha mali kwa kutoa Khumsi na Zaka, kuwapenda marafiki na kuwachukia maadui kwa ajili ya Mwenye Ezi Mungu, kushika njia ya wastani kwa ajili ya maadui, n.k. • Kujikinga mbele ya Mungu dhidi ya kupotoka na kutengana na imani ya Mungu Mmoja. • Kuomba taufiki ya kunufaika na heshima ya marafiki wa Mwenye Ezi Mungu. • Kuomba kuwa miongoni mwa waja bora katika mwezi wa Ramadhani. • Kuomba ulinzi wa Mwenye Ezi Mungu dhidi ya udanganyifu wa Shetani. • Kuomba kupata msamaha wa Mungu. • Kuomba taufiki ya kufanya ibada na kuwa na utiifu mbele ya Mwenye Ezi Mungu ndani ya mwezi mzima wa Ramadhani. • Ombi la kuomba dhambi zifutwe kama vile unavyopotea mwezi mwandamo wa Ramadhani. • Idadi kubwa ya watu wa motoni kusamehewa katika Ramadhani. • Kutafuta kinga ya Mwenye Ezi Mungu dhidi ya kutawaliwa na Shetani ndani ya mwezi wa Ramadhani. • Umuhimu wa masiku na nyakati za mwisho za mwezi wa Ramadhani. • Mchana na usiku wa Ramadhani kushuhudia matendo ya mwanadamu. • Kuomba hali ya ibada na utumwa iendelevu baada ya Ramadhani na mwaka mzima. • Kuomba kurithi wa Pepo. • Ombi la kumuombea Baraka na amani Mtume Muhammad (s.a.w.w) kila wakati na katika hali zote. Tafsiri Chambuzi za Dua ya Arubaini na Nne Kuna kazi kadhaa zilizoandikwa kwa lugha mbali mbali kwa ajili ya kutoa tafsiri chambuzi kwa ajili ya Dua ya arobaini na nne, sambamba na dua nyengine za kitabu cha Sahifa Sajjadiyya. Miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa kwa lugha ya Kifarsi kuhusiana na kazi hizo ni pamoja na; kitabu cha Hussein Ansarian kiitwacho ‘Diare Asheqan’, [3] kazi ya Mohammad Hassan Mamdouhi Kermanshahi, iitwayo ‘Shuhud wa Shenakht’, [4] pamoja na cha Sayyid Ahmad Fahri chenye jina la ‘Sharh va Tarjomeh-ye Sahifa Sajjadiya’. [5] Kitabu kiitwacho 'Sahbaye Huzur' kilichoandikwa na mwanazuoni aitwaye Muhammad-Taqi Misbah-Yazdi, ni miongoni mwa vitabu muhimu zaidi vilivkuja kutoa ufafanuzi wa dua hii. Umuhimu wa Kitabu hichi, unatokana na umahiri wake wa kuifafanua dua hii kulingana na nadharia mbali mbali, zikiwemo ndharia za kiirfani (kisufi), kiuchamungu (kiibada), pamoja na kimaadili (kiakhlaqi). Aidha, miongoni mwa tafiti muhimu zilizofanyiwa kazi ndani ya kitabu hicho ni zile sifa pekee za mwezi wa Ramadhani, ikiwa ni pamoja na; uongofu, ibada, rehema, baraka, msamaha, toba, fanaka, maarifa, utakaso, ikhlasi, kuteremshwa kwa Qur'ani, kuwepo kwa Usiku wa Cheo (Laylat al-Qadr), pamoja na sala na saumu. Yote hayo yametafitiwa na kujadiliwa kitabuni humo kulingana na mtazamo wa Imam Sajjad (a.s). [6] Miongoni mwa vitabu vyengine muhimu vilivyotoa tafafsiri chambuzi ya dua ya arobaini na nne ni kile kitabu kiitwacho ‘Simaye Ramadhan’ kilichofasiri dua hiyo sambamba na dua ya kuaga na mwezi wa Ramadhan, kazi ya Ali Karimi Jahromi. [7] Kitabu chengine kilichofanya kazi hiyo kwa lugha ya Kiajemi, ni kitabu kiitwacho ‘Suruush Ramadhan’ (maelezo juu ya maombi ya Imamu Sajjad katika mwanzo na mwisho wa mwezi wa Ramadhan), kazi ya Sayyid Ridha Baqirian-Muwahhid na Ali Baqirifar. Katika hivi vitabu viwili kumepita uchunguzi wa nyanja tofauti kuhusiana na mwezi wa Ramadhan pamoja na kujadili baadhi ya fadhila za Eid el-Fitr na adabu za kuagana na mwezi. [8] Pia ufafanuzi wa dua ya arubaini na nne ya kitabu cha Sahifa Sajjadiya unapatikana katika vitabu kadhaa vilivyoandikwa kwa Kiarabu kwa nia ya kufasiri dua hiyo sambamba na dua nyengine zilizomo ndani ya kitabu cha Sahifa Sajjadiyya. Baadhi ya vitabu vya lugha ya Kiarabu vilivyofanya kazi hiyo, ni pamoja na; Riadhu al-Salikin, (kazi ya Sayyid Ali Khan Madani) [9], Fi Dhilali al-Sahifa al-Sajjadiyya (kazi ya Muhammad Jawad Mughniyya), [10] Riadhu al-Arifina (kazi ya Muhammad bin Muhammad Darabi), [11] na Afaqi al-Ruh (kazi ya Sayyid Muhammad Hussein Fadlallah). [12] Vilevile, maelezo ya kina kuhusu msamiati na maneno yaliyotumika katika dua hii, sambamba na msamiati wa dua nyengine za Sahifa Sajjadiyya, yamekusanywa kwenye vitabu maalumu vilivyofanya kazi ya kufasiri msamiati huo kwa mfumo wa fasihi ya kilugha. Miongi mwa mifano ya vitabu hivyo ni kama vile; Ta'liqat 'ala al-Sahifa al-Sajjadiyya (kazi ya Fayd Kashani), [13] na Sharhu al-Sahifa al-Sajjadiyya (kazi ya Izz al-Din Jazairi) [14].

Matini ya Dua ya Arubaini na Nne kwa Kiarabu Pamoja na Maelezo yake Kwa Kiswahili

وَ كَانَ مِنْ دُعَائِهِ عَلَيْهِ السَّلَامُ إِذَا دَخَلَ شَهْرُ رَمَضَانَ Na (ifuatayo) ilikuwa ni miongoni mwa dua zake (amani iwe juu yake), aliyoizoea kuiomba pindi uingiapo mwezi wa Ramadhani. الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي هَدَانَا لِحَمْدِهِ، وَ جَعَلَنَا مِنْ أَهْلِهِ لِنَكُونَ لِإِحْسَانِهِ مِنَ الشَّاكِرِينَ، وَ لِيَجْزِيَنَا عَلَى ذَلِكَ جَزَاءَ الْمُحْسِنِينَ

Himdi zote anastahikia Mwenye Ezi Mungu (sifa njema zote ni za Mwenye Ezi Mungu), ambaye ametuongoza kwenye njia ya kumhimidi. Na akatujaalia kuwa miongoni mwa watu wenye kumshukuru, ili tuwe katika kundi la wenye kushukuru kutokana na hisani Zake, na ili atulipe juu ya jambo hilo jazaa ya wafanyao wema. وَ الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي حَبَانَا بِدِينِهِ، وَ اخْتَصَّنَا بِمِلَّتِهِ، وَ سَبَّلَنَا فِي سُبُلِ إِحْسَانِهِ لِنَسْلُكَهَا بِمَنِّهِ إِلَى رِضْوَانِهِ، حَمْداً يَتَقَبَّلُهُ مِنَّا، وَ يَرْضَى بِهِ عَنَّا

Na himdi kamilifu zote ni ya Mwenye Ezi Mungu, Ambaye ametukirimu kwa Dini Yake, na akatuhusisha (akatuchagua) kwa ajili ya mila (dini) Yake, na akatusahilishia mapito (njia) ya hisani Zake, ili tuyapite kwa fadhila Zake, hadi kwenye ridhaa Yake. Twamhimidi kwa himdi yenye matarajio ya Yeye kuitakabali (himidi hiyo) kutoka kwetu, na yenye matarajio ya Yeye kuridhika nasi kupitia himidi hiyo.


وَ الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي جَعَلَ مِنْ تِلْكَ السُّبُلِ شَهْرَهُ شَهْرَ رَمَضَانَ، شَهْرَ الصِّيَامِ، وَ شَهْرَ الْإِسْلَامِ، وَ شَهْرَ الطَّهُورِ، وَ شَهْرَ التَّمْحِيصِ، وَ شَهْرَ الْقِيَامِ «الَّذِي أُنْزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ، هُدىً لِلنَّاسِ، وَ بَيِّناتٍ مِنَ الْهُدى‏ وَ الْفُرْقانِ« Na sifa kamilifu zote zamstahikia Mwenye Ezi Mungu, Ambaye ameuteua mwezi Wake wa Ramadhani, miongoni mwa njia Zake mbali mbali za (kufikia) fadhila Zake, kisha akufanya kuwa ndiyo mwezi ni mwezi wa saumu (kujizuia na kula na kunywa n.k), mwezi wa Uislamu (unyenyekevu na kusalimu amri), mwezi wa tohara (utakaso wa kiroho na kimwili), mwezi wa uchujaji na usafishaji wa madhambi, na mwezi wa visimamo vya ibada. Ni mwezi ambao, kama ilivyoelezwa katika Qur'ani (2:185), 'ndani yake iliteremshwa Qur'ani, ikiwa ni mwongozo (Huda) kwa jamii ya wanadamu, na ni dalili bayana za uongofu huo, na pambanuo (Al-Furqan) baina ya haki na batili'. فَأَبَانَ فَضِيلَتَهُ عَلَى سَائِرِ الشُّهُورِ بِمَا جَعَلَ لَهُ مِنَ الْحُرُمَاتِ الْمَوْفُورَةِ، وَ الْفَضَائِلِ الْمَشْهُورَةِ، فَحَرَّمَ فِيهِ مَا أَحَلَّ فِي غَيْرِهِ إِعْظَاماً، وَ حَجَرَ فِيهِ الْمَطَاعِمَ وَ الْمَشَارِبَ إِكْرَاماً، وَ جَعَلَ لَهُ وَقْتاً بَيِّناً لَا يُجِيزُ- جَلَّ وَ عَزَّ- أَنْ يُقَدَّمَ قَبْلَهُ، وَ لَا يَقْبَلُ أَنْ يُؤَخَّرَ عَنْهُ. Hivyo basi, Mwenye Ezi Mungu akabainisha ubora wa mwezi huu juu ya miezi mingine yote kwa kuujaza hadhi tukufu zilizo tele, pamoja na kuupa sifa bora zilizo mashuhuri (zilizoenea). (Kwa mantiki hiyo, na kwa kigezo cha taadhima ya mwenzi huo), aliyaharamisha ndani yake yale yaliyokuwa halali katika nyakati za miezi mingine. Aidha, kwa kigezo cha takrima (ya mwezi huu), alizuia matumizi ya vyakula na vinywaji ndani ya mchana wake. Halikadhalika, aliupangia muda mahsusi na dhahiri (kwa kila mmoja wetu), ambao Yeye – Jalla wa ‘Azza – haidhinishi uwasilishwe kabla ya wakati wake, na wala haridhii uakhirishwe baada ya kuingia wakati wake.

ثُمَّ فَضَّلَ لَيْلَةً وَاحِدَةً مِنْ لَيَالِيهِ عَلَى لَيَالِي أَلْفِ شَهْرٍ، وَ سَمَّاهَا لَيْلَةَ الْقَدْرِ، «تَنَزَّلُ الْمَلائِكَةُ وَ الرُّوحُ فِيها بِإِذْنِ رَبِّهِمْ مِنْ كُلِّ أَمْرٍ» سَلامٌ دَائِمُ الْبَرَكَةِ إِلَى طُلُوعِ الْفَجْرِ عَلَى مَنْ يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ بِمَا أَحْكَمَ مِنْ قَضَائِهِ.

Kisha, (Mwenye Ezi Mungu) akaufanya usiku mmoja miongoni mwa nyusiku zake kuwa bora kuliko miezi elfu moja, na akaupa jina la Lailatul Qadr (Usiku wa Cheo). Katika usiku huo, 'Malaika Hushuka pamoja na Roho kwa idhini ya Mola wao, hukuwa wakiwa (wamekuja na) kila jambo.' (Usiku huo) ni (usiku wenye) amani yenye baraka za kudumu hadi kuchomoza kwa alfajiri, (ambazo) humshukia yeyote anayemtaka miongoni mwa waja wake, kulingana na yale aliyoyahukumu katika majaaliwa yake.

اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ، وَ أَلْهِمْنَا مَعْرِفَةَ فَضْلِهِ وَ إِجْلَالَ حُرْمَتِهِ، وَ التَّحَفُّظَ مِمَّا حَظَرْتَ فِيهِ، وَ أَعِنَّا عَلَى صِيَامِهِ بِكَفِّ الْجَوَارِحِ عَنْ مَعَاصِيكَ، وَ اسْتِعْمَالِهَا فِيهِ بِمَا يُرْضِيكَ حَتَّى لَا نُصْغِيَ بِأَسْمَاعِنَا إِلَى لَغْوٍ، وَ لَا نُسْرِعَ بِأَبْصَارِنَا إِلَى لَهْوٍ

Ewe Mwenye Ezi Mungu, (twakuomba) umshushie amani na rehema zako Muhammad pamoja na Aali zake. (twakuomba) utujalie kuutambua ubora wake (ubora wa mwezi huu), utupe taufiki ya kuiheshimu hadhi yake, na utupe taufiki ya kujiepusha na yale uliyoyakataza ndani yake. Tusaidie kuitekeleza saumu yake kwa kuvizuia viungo vyetu visifanye matendo ya kukuasi, na badala yake vitumike kwa ajili ya yale yanayokupendeza. (Twakuomba utupe taufiki hiyo) ili tusiweze kuyatumia masikio yetu kwa ajili ya kusikiliza maneno ya upuuzi, na (ili tuyazuie) macho yetu yasikimbilie kwenye mambo ya anasa yasiyo na maana.

وَ حَتَّى لَا نَبْسُطَ أَيْدِيَنَا إِلَى مَحْظُورٍ، وَ لَا نَخْطُوَ بِأَقْدَامِنَا إِلَى مَحْجُورٍ، وَ حَتَّى لَا تَعِيَ بُطُونُنَا إِلَّا مَا أَحْلَلْتَ، وَ لَا تَنْطِقَ أَلْسِنَتُنَا إِلَّا بِمَا مَثَّلْتَ، وَ لَا نَتَكَلَّفَ إِلَّا مَا يُدْنِي مِنْ ثَوَابِكَ، وَ لَا نَتَعَاطَى إِلَّا الَّذِي يَقِي مِنْ عِقَابِكَ، ثُمَّ خَلِّصْ ذَلِكَ كُلَّهُ مِنْ رِئَاءِ الْمُرَاءِينَ، وَ سُمْعَةِ الْمُسْمِعِينَ، لَا نُشْرِكُ فِيهِ أَحَداً دُونَكَ، وَ لَا نَبْتَغِي فِيهِ مُرَاداً سِوَاكَ.

Na (twakuomba utupe tauffiki hiyo) ili tusinyooshe mikono yetu kuelekea mambo yaliyokatazwa, wala tusipige hatua kwa miguu yetu, kwa ajili ya kwenda kwenye maeneo yaliyozuiliwa. Na ili matumbo yetu yasije kupokea chochote kile isipokuwa kile ulichokiruhusu (ulichokihalalisha), na ili ndimi zetu zisizungumze isipokuwa yale uliyoyaweka kuwa kigezo (kwa ajili ya uzungumzaji wetu). Na wala tusije kujikalifisha isipokuwa yale yanayotukaribisha (yanayotusogeza) kwenye malipo Yako, na wala tusijihusishe (na chochote kile), isipokuwa na kile kinachotuepusha na adhabu Yako. Baada ya hayo, (twakuomba) uzifisha amali zetu zote hizo kutokana na unafiki wa wenye kujionyesha, na (utusafishe na tabia ya wale wenye) kutafuta sifa na wanaopenda kusikika. (Tujaalie kutenda matendo hayo bila ya) kumshirikisha yeyote yule isipokuwa Wewe, wala tusiwe wenye kutatafuta ndani yake lengo jengine zaidi Yako.

اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ، وَ قِفْنَا فِيهِ عَلَى مَوَاقِيتِ الصَّلَوَاتِ الْخَمْسِ بِحُدُودِهَا الَّتِي حَدَّدْتَ، وَ فُرُوضِهَا الَّتِي فَرَضْتَ، وَ وَظَائِفِهَا الَّتِي وَظَّفْتَ، وَ أَوْقَاتِهَا الَّتِي وَقَّتَّ

Ewe Mwenye Ezi Mungu, msalie Muhammad na Aali zake. Na utujalie katika mwezi huu, tuwe ni wenye kuzingatia kikamilifu nyakati za Sala tano; (tupe taufiki ya kufanya hivyo) kulingana na mipaka yake kama ulivyo iweka (Wewe mwenyewe), na kwa mujibua wa faradhi zake ulizozifaradhisha, na kwa majukumu yake uliyoainisha, na kulingana na nyakati zake maalum ulizozipanga. وَ أَنْزِلْنَا فِيهَا مَنْزِلَةَ الْمُصِيبِينَ لِمَنَازِلِهَا، الْحَافِظِينَ لِأَرْكَانِهَا، الْمُؤَدِّينَ لَهَا فِي أَوْقَاتِهَا عَلَى مَا سَنَّهُ عَبْدُكَ وَ رَسُولُكَ- صَلَوَاتُكَ عَلَيْهِ وَ آلِهِ- فِي رُكُوعِهَا وَ سُجُودِهَا وَ جَمِيعِ فَوَاضِلِهَا عَلَى أَتَمِّ الطَّهُورِ وَ أَسْبَغِهِ، وَ أَبْيَنِ الْخُشُوعِ وَ أَبْلَغِهِ.

Na utujaalie, katika ibada hii (katika utekelezaji wa sala hizo), daraja la wale wanaoitekeleza kwa usahihi katika kila hatua yake; wale wanaohifadhi nguzo zake, na wanaoitekeleza katika nyakati zake maalum, sawasawa na alivyoielekeza mtumishi Wako na Mtume Wako—rehema Zako ziwe juu yake pamoja na Aali zake. Tujaalie kuitekeleza (kikamilifu) katika rakaa zake, sijda zake, pamoja na fadhila (sifa) zake nyengine zote, kwa twahara iliyotimia na yenye kamilifu zaidi, na kwa unyenyekevu ulio dhahiri na wenye athari kubwa zaidi. وَ وَفِّقْنَا فِيهِ لِأَنْ نَصِلَ أَرْحَامَنَا بِالْبِرِّ وَ الصِّلَةِ، وَ أَنْ نَتَعَاهَدَ جِيرَانَنَا بِالْإِفْضَالِ وَ الْعَطِيَّةِ، وَ أَنْ نُخَلِّصَ أَمْوَالَنَا مِنَ التَّبِعَاتِ، وَ أَنْ نُطَهِّرَهَا بِإِخْرَاجِ الزَّكَوَاتِ، وَ أَنْ نُرَاجِعَ مَنْ هَاجَرَنَا، وَ أَنْ نُنْصِفَ مَنْ ظَلَمَنَا، وَ أَنْ نُسَالِمَ مَنْ عَادَانَا حَاشَى مَنْ عُودِيَ فِيكَ وَ لَكَ، فَإِنَّهُ الْعَدُوُّ الَّذِي لَا نُوَالِيهِ، وَ الْحِزْبُ الَّذِي لَا نُصَافِيهِ.

(Ewe Mola wetu tunakuomba), tujaalie taufiki katika kipindi hichi, ili tuweze kuwaunga ndugu zetu kwa wema na ukarimu, na kuwatunza majirani zetu kwa fadhila na zawadi. Tuwezeshe kuzisafisha mali zetu kutokana na dhima (madeni na haki za watu), na kuzitakasa (mali zetu hizo) kwa kutoa Zaka. Tujaalie turejeane na wale waliotutenga, tuwatendee haki wale waliotudhulumu, na tufanye amani na wale waliotufanyia uadui. Hata hivyo, twakuomba uijaalie amani hii isimuhusishe yule anayefanywa adui kwa ajili Yako na katika njia Yako (na kwa malengo ya kushikamana na njia Yako). Kwa hakika, huyo ndiye adui ambaye hatupaswi kumfanya mwandani wetu, na ni kundi ambalo hatuwezi kulisafia nalo nyoyo zetu. وَ أَنْ نَتَقَرَّبَ إِلَيْكَ فِيهِ مِنَ الْأَعْمَالِ الزَّاكِيَةِ بِمَا تُطَهِّرُنَا بِهِ مِنَ الذُّنُوبِ، وَ تَعْصِمُنَا فِيهِ مِمَّا نَسْتَأْنِفُ‏ مِنَ الْعُيُوبِ، حَتَّى لَا يُورِدَ عَلَيْكَ أَحَدٌ مِنْ مَلَائِكَتِكَ إِلَّا دُونَ مَا نُورِدُ مِنْ أَبْوَابِ الطَّاعَةِ لَكَ، وَ أَنْوَاعِ الْقُرْبَةِ إِلَيْكَ.

Na (twakuomba) utupate fursa na taufiki ya kujikurubisha Kwako katika kipindi hiki kupitia amali takasifu; ambazo kwazo utatutakasa dhidi ya maasi, na utatukinga dhidi kurejea kwenye kasoro zetu za awali. (Tupe taufiki hiyo), ili kuwe hakuna malaika Wako yeyote atakayewasilisha mbele Yako taarifa yoyote ile, isipokuwa ile (yenye thamani) duni kuliko yale tuliyoyawasilisha sisi kutoka katika nyanja za utiifu na aina mbalimbali za ukuruba wa kujikaribisha Kwako. اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ بِحَقِّ هَذَا الشَّهْرِ، وَ بِحَقِّ مَنْ تَعَبَّدَ لَكَ فِيهِ مِنِ ابْتِدَائِهِ إِلَى وَقْتِ فَنَائِهِ: مِنْ مَلَكٍ قَرَّبْتَهُ، أَوْ نَبِيٍّ أَرْسَلْتَهُ، أَوْ عَبْدٍ صَالِحٍ اخْتَصَصْتَهُ، أَنْ تُصَلِّيَ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ، وَ أَهِّلْنَا فِيهِ لِمَا وَعَدْتَ أَوْلِيَاءَكَ مِنْ كَرَامَتِكَ، وَ أَوْجِبْ لَنَا فِيهِ مَا أَوْجَبْتَ لِأَهْلِ الْمُبَالَغَةِ فِي طَاعَتِكَ، وَ اجْعَلْنَا فِي نَظْمِ مَنِ اسْتَحَقَّ الرَّفِيعَ الْأَعْلَى بِرَحْمَتِكَ. Ewe Mwenye Ezi Mungu, hakika mimi ninakuomba kupitia hadhi ya mwezi huu, na kupitia hadhi ya kila mmoja aliyekuabudu ndani yake, tangu mwanzo wa kuingia mwezi huu hadi mwisho wake. (Ninakuomba kwa hadhi ya) Kuanzia yule Malaika uliyemweka karibu Nawe, au (kwa hadhi ya) Nabii uliyemtuma, au mja mwema uliyemchagua. (Ninakuomba) umrehemu Mtume Muhammad na familia yake (Aali zake). Na Katika mwezi huu, (Ninakuomba) utufanye tuwe ni wenye kustahili ule ukarimu uliowaahidi watu wako wa karibu. Tuwajibishie kupata yale uliyoyaweka kwa ajili ya wale wanaojitolea kikamilifu katika kukutii. Na (Ninakuomba) kwa Rehema zako, utuweke katika safu ya wale waliopata cheo cha juu kabisa.

اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ، وَ جَنِّبْنَا الْإِلْحَادَ فِي تَوْحِيدِكَ، وَ الْتَّقْصِيرَ فِي تَمْجِيدِكَ، وَ الشَّكَّ فِي دِينِكَ، وَ الْعَمَى عَنْ سَبِيلِكَ، وَ الْإِغْفَالَ لِحُرْمَتِكَ، وَ الِانْخِدَاعَ لِعَدُوِّكَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ

Ewe Mwenye Ezi Mungu, mshushie rehma na amani Muhammad na Aali zake, na (twakuomba) utuepushe na upotofu wa kiimani katika Tauhidi Yako (katika Upweke Wako), utuepushe na uzembe katika mchakato wetu wa kukuadhimisha, na (twakuomba utuepeshe na) shaka katika dini Yako, pia utuepeshe na upofu juu ya njia Yako, pia utuepeshe na kupuuza matukufu Yako, na kudanganywa na adui Yako, (ambaye ni) Shetani aliyelaaniwa. اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ، وَ إِذَا كَانَ لَكَ فِي كُلِّ لَيْلَةٍ مِنْ لَيَالِي شَهْرِنَا هَذَا رِقَابٌ يُعْتِقُهَا عَفْوُكَ، أَوْ يَهَبُهَا صَفْحُكَ فَاجْعَلْ رِقَابَنَا مِنْ تِلْكَ الرِّقَابِ، وَ اجْعَلْنَا لِشَهْرِنَا مِنْ خَيْرِ أَهْلٍ وَ أَصْحَابٍ.

Ewe Mwenye Ezi Mungu, (twakuomba) uziteremshe rehema Zako juu ya Muhammad na Aali zake. Na iwapo, katika kila usiku wa mwezi wetu huu, kutakuwa na nafsi fulani zenye bahati ya kukombolewa na msamaha Wako, au zilizotunukiwa uhuru kupitia fadhila ya msamaha Wako, basi zijaalie nafsi zetu kuwa ni miongoni mwa nafsi hizo. Na tujaalie katika uhusiano wetu na mwezi huu, tuwe ni watu wa kheri na wenye usuhuba mwema na mwezi huu. اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ، وَ امْحَقْ ذُنُوبَنَا مَعَ امِّحَاقِ هِلَالِهِ، وَ اسْلَخْ عَنَّا تَبِعَاتِنَا مَعَ انْسِلَاخِ أَيَّامِهِ حَتَّى يَنْقَضِيَ عَنَّا وَ قَدْ صَفَّيْتَنَا فِيهِ مِنَ الْخَطِيئَاتِ، وَ أَخْلَصْتَنَا فِيهِ مِنَ السَّيِّئَاتِ.

Ewe Mwenyezi Mungu, mswalie Muhammad na Aali zake. Na uzifutilie mbali dhambi zetu sawia na kufifia kwa mwezi wake mwandamo (kadri ya mwezi huu unavyoelekea mwisho mwake). Na utuvue (ututue) mizigo wa maovu yetu sambamba na kumalizika kwa siku zake. Hadi utakapokwisha, uwe tayari umeshatutakasa na makosa yote, na umeshatuepusha (umeshatukomboa) na maovu yote.

اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ، وَ إِنْ مِلْنَا فِيهِ فَعَدِّلْنَا، وَ إِنْ زُغْنَا فِيهِ فَقَوِّمْنَا، وَ إِنِ اشْتَمَلَ عَلَيْنَا عَدُوُّكَ الشَّيْطَانُ فَاسْتَنْقِذْنَا مِنْهُ. Ewe Mwenyezi Mungu, mswalie Muhammad na Aali zake. Na endapo tutapinda naku utaelemea kwenye upotofu, basi twakuomba tunyooshe. Na pia endapo tutapotoka, (twakuomba) uturekebishe. Na endapo adui wako Shetani atatutawala, basi (twakuomba) tuokoe dhidi yake.


اللَّهُمَّ اشْحَنْهُ بِعِبَادَتِنَا إِيَّاكَ، وَ زَيِّنْ أَوْقَاتَهُ بِطَاعَتِنَا لَكَ، وَ أَعِنَّا فِي نَهَارِهِ عَلَى صِيَامِهِ، وَ فِي لَيْلِهِ عَلَى الصَّلَاةِ وَ التَّضَرُّعِ إِلَيْكَ، وَ الْخُشُوعِ لَكَ، وَ الذِّلَّةِ بَيْنَ يَدَيْكَ حَتَّى لَا يَشْهَدَ نَهَارُهُ عَلَيْنَا بِغَفْلَةٍ، وَ لَا لَيْلُهُ بِتَفْرِيطٍ.

Ewe Mwe Ezi Mungu, (twakuomba) uushibishe (ushehenishe) mwezi huu kwa shehena ya ibada zetu juu Yako, na uvirembe (uzipambenyakazi zake kwa matendo yetu ya kukutii Wewe. Utuwezeshe mchanani mwake kwa uwezo kutekelezawa saumu yake, na (utuwezeshe) usikuni mwake kwa uwezo wa kutekeleza ibada ya sala, pamoja na maombi unyenyekevu Kwako, na utupe taufiki ya kuwa na khushui (heshima adhimu/uso wa kutahayari) mbele Yako, na utupe taufiki ya kuwa na unyenyekevu kamili mbele ya hadhi Yako. Ili mchana wake usitoe ushahidi dhidi yetu kutokana na hali ya kughafilika kwetu, na wala usiku wake, kutokana na hali ya mapungufu yaliyopo katika utekelezaji wetu. اللَّهُمَّ وَ اجْعَلْنَا فِي سَائِرِ الشُّهُورِ وَ الْأَيَّامِ كَذَلِكَ مَا عَمَّرْتَنَا، وَ اجْعَلْنَا مِنْ عِبَادِكَ الصَّالِحِينَ الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيها خالِدُونَ، وَ الَّذِينَ يُؤْتُونَ ما آتَوْا وَ قُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ، أَنَّهُمْ إِلى‏ رَبِّهِمْ راجِعُونَ، وَ مِنَ الَّذِينَ يُسارِعُونَ فِي الْخَيْراتِ وَ هُمْ لَها سابِقُونَ. Ewe Mwe Ezi Mungu, na (twakuomba) utujaalie tuwe katika hali hii njema (ya utiifu) katika miezi na masiku mengine yote utakaotujaalia kuishi ndani yake. Na utujaalie tuwe miongoni mwa waja wako wema; wale ambao watairithi Pepo ya Firdausi na watadumu humo milele. Na (twakuomba utujaalie tuwe miongoni mwa) wale wanoutoa wanachokitoa (katika sadaka na matendo yao mema), huku nyoyo zao zikiwa zimejawa na khofu, wakijua kuwa bila shaka wao watarejea kwa Mola wao. Na utujaalie tuwe miongoni mwa wale wanaokimbilia kutenda mema, huku wakiwa ni wenye kuyatangulia (kuyakimbilia).

اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ، فِي كُلِّ وَقْتٍ وَ كُلِّ أَوَانٍ وَ عَلَى كُلِّ حَالٍ عَدَدَ مَا صَلَّيْتَ عَلَى مَنْ صَلَّيْتَ عَلَيْهِ، وَ أَضْعَافَ ذَلِكَ كُلِّهِ بِالْأَضْعَافِ الَّتِي لَا يُحْصِيهَا غَيْرُكَ، إِنَّكَ فَعَّالٌ لِمَا تُرِيدُ. Ewe Mwenye Ezi Mungu, (twakuomba) umbariki Muhammad na Aali zake, kila wakati, kila kipindi na katika hali zote. Mbariki kwa idadi ya baraka za yule uliyembariki, na (umzidishie) mara dufu zaidi ya hizo zote (ulizombariki yule uliyembariki), kwa wingi ambao hakuna yeyote yule atakayeweza kuzihesabu isipokuwa Wewe. Hakika, Wewe mfanyaji wa lolote lile ulitakalo.