Vikundi vya Madhehebu ya Kishia

Kutoka wikishia

Vikundi vya Madhehebu ya Kishia (Kiarabu: فرق الشيعة): Ni matawi mbalimbali ya Waislamu wa Kishia ambayo, licha ya kuamini kwao juu ya uongozi wa moja kwa moja wa Ali bin Abi Talib (a.s), ila yanatofautiana katika imani nyingine kadhaa kama vile; Idadi ya Maimamu Maasumina (wasiokosea). Madhehebu makuu ya Kishia yaliyo hai hadi sasa ni: Imamiyyah, Zaidiyya na Ismailiyya. Baadhi ya vyanzo vinahusisha madhehebu mengine kadhaa yaliyotoweka miongoni mwa madhehebu ya Kishia kama vile; Kiisaniyya, Fat-hiyyah, Waaqifiyyah, Naausiyyah na vikundi vya Maghulati.

Tofauti juu ya urithi wa uongozi na uteuzi wa Imamu baada ya kifo cha kila mmoja kati ya Maimamu (a.s), pamoja na kupenyezwa kwa itikadi za kupindukia mipaka (za Kighulati) na mwelekeo usio sahihi katika kumtambua Mahdi al-Muntadhar (a.s), zinachukuliwa kama ndio sababu kuu za kuibuka kwa madhehebu tofauti katika madhehebu ya Shia.

Kwa mujibu wa idadi ya wafuasi, kikundi cha Mashia Imamiyya kinachukuliwa kuwa na wafuasi wengi zaidi kati ya vikundi mbali mbali vya Mashia, hasa katika nchi kama Iran, Iraq, Pakistan na Lebanon. Vitabu vingi vimeandikwa kuhusiana na madhehebu ya Kishia. Kitabu cha Firaq al-Shi'a kilichoandikwa na Hassan ibn Musa al-Nawbakhti ni mojawapo ya vitabu vya zamani zaidi kuhusiana na mada hii.

Umuhimu wa Madhehebu ya Shia

Kwa ujumla Madhehebu ya Kishia yanaashiri matawi na makundi yote yalioko chini ya kivuli cha madhehebu Shia (ambayo ni moja ya madhehebu makubwa mawili ya Uislamu). Vikundi vyote Kishia vinaamini juu ya haki uongozi wa Imamu Ali (a.s) baada ya kufariki kwa bwana Mtume (s.a.w.w). [1] Mijadala kuhusiana na madhehebu ya Kishia ilianza tangu karne za mwanzo za Hijria. Kitabu kiitwacho Firaq al-Shi'a kilichoandikwa na Hassan bin Musa al-Nawbakhti katika karne ya tatu na ya nne Hijria kiliandikwa maalumu kuhusiana na mada hii. Mnamo zama zetu hizi (karne ya 15 Hijria), kuna baadhi ya vyuo vikuu vilivyo anzisha taaluma (fani) makhususi kuhusiana na madhehebu ya Kishia. [2]

Mgawanyiko wa Kwanza Kabisa

Sayyid Muhammad Hussein Tabataba'i katika kitabu chake Shie Dar Islam (Shia katika Uislamu) anasema kuwa; Mgawanyiko wa kwanza kabisa ndani ya madhehebu ya Shia ulitokea baada ya kuuawa kwa Imamu Hussein (a.s) mnamo mwaka 61 Hijria. Wengi baada ya kuuwawa kwa Imamu Hussein (a.s), walimkubali Imamu Sajjad (a.s) kama ndiye mshika hatamu wa nafasi ya Uimamu, ila kikundi kidogo kinachojulikana kama Kiisaniyyah kilimkubali na kumtambua Muhammad ibnu al-Hanafiyya, mtoto mwingine wa Imamu Ali, kama ndiye Imamu wao. [3] Pia Hussein Tabataba'i anaamini kwamba; baada ya kipindi cha Imamu Ridha (a.s) hadi kipindi cha Imam Mahdi (a.s), hakukuwa na mabadiliko makubwa ya kugawanyika, na kama kuliwahi kulitokea tukio lolote lile la mgawanyiko, tukio hilo halikudumu kwa muda mrefu, na lilionekana kutawanyika wenyewe kwa yenyewe baada ya siku chache tu. [4] Hata hivyo, kwa maoni ya baadhi ya watafiti ni kwamba; Kikundi cha kwanza katika Ushia kilianzishwa mwishoni mwa utawala wa Othman na mwanzoni mwa utawala wa Imamu Ali (a.s) ambacho kilijulikana kama Sabaa'iyyah, kilichoanzishwa na Abdullah bin Saba. [5]

Idadi ya Vikundi vya Madhehebu ya Shia

Kuna maoni tofauti kuhusiana na idadi ya vikundi vya madhehebu ya Kishia. Kitabu kiitwacho Farhang Shi'a kinataja ndani yake vikundi miamoja vinavyohusiana na madhehebu ya Kishia, maarufu zaidi miongoni mwavyo vikiwa vikundi vya; Imamiyyah, Kiisaniyyah, Zaidiyyah, Ismailiyyah, Fat-hiyyah na Maghulati. [6] Abu al-Hussein al-Malti, mwanachuoni wa kifiqhi wa karne ya nne Hijri, ametaja makundi 18 kuhusiana na madhehebu ya Kishia katika kitabu chake Al-Tanbih wal-Radd ala Ahli al-Ahawa wal-Bid’a. [7] Abdul al-Qahir al-Baghdadi (alifariki mwaka 429 Hijria), ametaja madhehebu (makundi) makuu matatu ya Kishia katika kitabu chake «Al-Farq bayn al-Firaq», nayo ni: Imamiyyah, Kaysaniyyah na Zaidiyyah. [8] Shahrastani (alifariki mwaka 548 Hijria) ameyataja madhehebu makuu matano katika chake Al-Milal wa al-Nihal, na kusema kwa hayo ndiyo madhehebu makuu ya Kishia, nayo ni: Imamiyyah, Zaidiyyah, Kiisaniyyah, Ismailiyyah na Maghulat. [9] Tabataba'i (alifariki mwaka 1402 Hijria) ametaja madhehebu makuu matatu ya Kishia katika kitabu chake Shia Dar Islam (Shia katika Uislamu) ambayo ni: Imamiyyah, Ismailiyyah na Zaidiyyah. [10]

Sababu za Kuibuka kwa Vikundi Kadhaa vya Kishia

Sababu kuu za kuibuka kwa makundi mbalimbali ndani ya madhehebu Shia ni:

  • Kadhia ya Uimamu: Tofauti juu ya suala la uongozi na uteuzi wa Imamu, kama ilivyotajwa na Rasul Jafarian, ilikiwa ndio chanzo cha mwazo kabisa katika kuibuka makundi mbalimbali ndani ya madhehebu ya Shia. [11] Kwa mfano, Kiisaniyyah waliamini kuwa Imamu aliye kuwa akistahiki kushika nafasi ya Uimamu baada ya kuuawa kwa Imamu Ali (a.s), alikuwa ni Muhammad bin al-Hanafiyyah, na sio Imamu Hassan Mujtaba (a.s). [12]
  • Kupenyeza kwa Itikadi za Kupindukia Mipaka: Katika zama za maisha ya Imamu Ali na hata Maimamu wengine (a.s), kulikuwa na baadhi ya wafuasi waliokuwa na mtazamo wa kuwatukuza Maimamu (a.s) kupita kiasi na kuwapa sifa za Kimungu. Hii ilisababisha kuibuka kwa madhehebu mbalimbali ya yaliopindukia mipaka (Maghulat), ambayo yaliandikwa na kurikodiwa na watafiti na wanahistoria mbali mbali, wakiyahisabu makundi hayo kuwa ni miongoni mwa madhehebu ya Shia. [13] Kwa mfano, kundi la Sabaa-iyyah, moja ya makundi ya Maghulati na wafuasi wa Abdullah bin Saba, walikuwa na imani kwamba Imam Ali (a.s) hajafariki na wala hatafariki, bali siku moja atarudi tena na kueneza haki na uadilifu duniani baada ya kujazwa dhuluma na ukandamizaji. [14]
  • Kutoelewana katika Uteuzi wa Mahdi al-Muntadhar: Hii ni sababu nyingine iliyosababisha kuibuka kwa makundi au madhehebu tofauti katika Kishia katika karne tatu za mwanzo. [15]

Madhehebu Yanayoendelea Kuishi

Madhehebu makuu ya Kishia yanayo tambuliwa kuwa ndiyo Madhehebu ya Kishia yanayoendelea kuishi hadi leo ni: Imamiyyah, Zaidiyyah na Ismailiyyah: [16]

Imamiyyah

Makala Asili: Imamiyyah

Wanaamini kuwa baada ya kifo cha bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w), Imam Ali (a.s) ndiye aliye teuliwa na Mwenye Ezi Mungu kushika nafasi ya Uimam. Kwa ya Madhehebu haya ni kwamba; Wanaostahiki kushika nafasi hiyo ya Imamu Ali (a.s), ni: Imamu Hassan (a.s) na Imamu Hussein (a.s). Na walifuata kushika nafsi hiyo baada yao kwa amri ya Alla, ni Mimamu tisa kutoka katika kizazi cha Imamu Hussein (a.s) ambao ni; Imamu Sajjad (a.s), Imamu Baqir (a.s), Imamu Swadiq (a.s), Imamu Kadhim (a.s), Imamu Ridha (a.s), Imamu Jawadi (a.s), Imamu Hadi (a.s), Imamu Hassan Askari (a.s) na Imamu Mahdi (a.s).  [17]

Kwa mujibu wa mtazamo wa Imamiyyah, Imamu wa kumi na mbili, yaani Imam Mahdi (a.s), ndiye Qaim (atakaye simama dhidi ya dhulma) na Mwokozi ambaye yuko katika ghaiba (mafichoni), ambaye atakuja kudhihiri katika zama za mwisho wa dunia. [18] Imamiyyah wanaamini kuwa ‘isma (kutokukosea) kwa Imamu kuwa ni jambo lazima, na wanaamini kuwa Maimamu wote ni maasumu (hawakosei). [19] Kwa imani yao, Maimamu ni wafasiri wa kweli wa Kitabu cha Qur'ani na Sunna za bwana Mtume (s.w.w.w). [20]

Ismailiyyah

Makala Asili: Ismailiyyah

Kwa mujibu wa maelezo ya Muhammad Jawad Mashkoor (aliyefariki mwaka wa 1374 H), mwanahistoria na profesa wa Chuo Kikuu cha Tehran, katika kitabu «Farhange Firaqe Islami», ni kwamba; Ismailiyyah ndio jina la jumla kwa makundi yote ambayo baada ya Imamu Swadiq (a.s), waliamini kuwa nafasi ya uongozi ilimstahikia mwanawe mkubwa aitwaye Ismail bin Jafar au mjukuu wake, ambaye ni Muhammad bin Ismail. [21] Mwanzoni, Ismailiyyah waligawanyika makundi mawili: [22] Ismailiyyah Khaassa (kundi makhususi) na Ismailiyya ‘Aamma (kundi la kijumla jamala). Ismailiyyah Khaassa waliku wakiamini kuwa; Ismail alikuwa Imamu wakati wa uhai wa baba yake kisha akatoweka, naye ndiye Imamu wa saba wa Mashia. Ismailiyyah Aamma walikuwa wakiamini kuwa; Ismail alifariki dunia wakati wa uhai wa baba yake, na kabla ya kifo chake alimteua mwanawe ambaye ni Muhammad kuwa ndiye mrithi wake. [23] Tabatabai katika kitabu Shia Dar Islami anaeleza ya kwamba; baada ya muda mfupi tu makundi mawili haya yalipotea na kuweka, kisha kuliibuka kundi jingine ambalo liliamini kuwa; Ismail alikuwa Imamu wakati wa uhai wa baba yake, na baada ya yeye, uongozi ulihamia kwa mwanawe aitwaye Muhammad bin Ismail na kisha kwa kizazi chake. Kundi hili ndilo kundi ambalo bado limebaki hai na kufuatwa na wafuasi kadhaa hadi sasa. [24]

Inasemekana kuwa; Baada ya kundi la Imamiyyah, Ismailiyyah ndilo kule lenye idadi kubwa zaidi ya wafuasi, ila nao hawa pia wamegawanyika katika makundi mbalimbali katika historia yao, na wameenea katika nchi zaidi ya 25 barani Asia, Afrika, Ulaya, na Amerika ya Kaskazini. [25]

Zaidiyyah

Makala Asili: Zaidiyyah

Wafuasi wa Zaid bin Ali nao ni wale wanaoamini juu ya Uimamu wake. [26] Yasemekana kuwa; wao wanamhisabu Zaid bin Ali kama ni Imamu wao wa tano. [27] Sheikh Mufidu (aliyefariki mwaka 413 Hijiria) katika kitabu Awail al-Maqalat ameandika akisema kuwa; Wao wanaamini juu ya uongozi wa Imam Ali, Imamu Hassan na Imamu Hussein (a.s) na kisha wanaamini juu ya Uimamu wa Zaid bin Ali. [28] Pia kundi la Zaidiyyah linaamini kuwa; Ni lazima Imamu atoke katika kizazi cha Fatima (a.s), hivyo basi yeyote yule atakayetokea kutoka katika kizazi cha bibi Fatima ambaye atakuwa ni mjuzi, jasiri na mkarimu ambaya ameinuka kwa ajili ya kusimamisha haki, huyo ndiye Imamu wa haki. [29]

Zaidiyya hawashikamani na imani ya ‘isma ya Maimamu (kutokosea kwa Maimamu), wala hawana imani juu ya kurudi kwa wafu duniani kwa mara ya pili (raj'a), na wanatofautiana na Imamiyyah ambao wanaamini kuwa kuna maandiko ya wazi kabisa (nassun jaliyyun) juu ya umrithi wa Imam Ali (a.s) wa kurithi nafasi ya uongozi baada ya Mtume (s.a.w.w). Wao wanaamini kuwa maandiko yaliopo kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w), yanayolielezea suala hili la urithi wa Imam Ali, ni maandiko yaliyofichika au yasio wazi (nassun khafiyyun), na kutokana na maslahi fulani Imam Ali ilibidi kuyaeleza maandiko hayo kwa baadhi ya masahaba wake maalum tu. [30]

Ingawa Zaidiyya wanamwona Imam Ali (a.s), kama ni mrithi wa moja kwa moja wa kushika nafasi ya bwana Mtume (s.a.w.w), ila wanakubali uhalali wa ukhalifa wa Makhalifa watatu waliomtangulia Imamu Ali (a.s). [31] Mohammad Jawad Mashkoor katika kitabu Farhange Firaqe Islami, ametaja makundi 16 yaliyotokana na madhehebu ya Zaidiyyah. [32] Makundi matatu muhimu kati ya hayo ni; Jarudiyyah, Sulaimaniyah (wafuasi wa Sulaiman bin Jarir) na Butriyyah (wafuasi wa Hassan bin Saleh bin Hayyi). [33]

Makundi Yaliyotoweka

Baadhi ya madhehebu muhimu ya Kishia ambayo yalikuwepo zamani na baadaye yakatoweka ni pamoja na:

  • Kiisaniyyah: Hili ni lililomkubali Muhammad ibnu al-Hanafiyya kama Imamu baada ya kifo cha Imam Ali (a.s). [34] Shahrastani katika kitabu chake Al-Milal wa al-Nihalu aliandika akisema kuwa; Baada ya Muhammad bin Hanafiyyah kufariki dunia, kulitokea mgawanyiko miongoni mwa wafuasi wake. [35] Baadhi yao waliamini kuwa Muhammad bin Hanafiyyah hakufairiki dunia, na kwamba atarudi tena na kueneza haki na uadilifu duniania humu. [36] Wengine wakaamini kuwa amefariki na nafasi ya uongozi wake mehamishiwa kwa mwanawe aitwaye Abu Hashim. [37] Kulingana na ripoti ya Mohammad Jawad Mashkoor, ni kwamba; Baada ya kifo cha Muhammad bin Hanafiyyah, Madhehebu ya Kiisaniyyah yaligawanyika katika makundi kumi na mbili, [38] ambapo wote walikuwa na imani ya pamoja juu ya uongozi wa Muhammad bin Hanafiyyah. [39] Baadhi ya makundi ya Kiisaniyyah ambayo yalijulikana kama ni madhehebu yenye msimamo mkali ni pamoja na: Hashimiyyah, [40] Karubiyyah, [41] Hamziyyah, [42] Bayaniyyah [43] na Harbiyyah. [44]
  • Fathiyyah: Hili ni kundi la Waislamu wa Kishia ambao baada ya kifo cha Imamu Jafar al-Sadiq (a.s) walikuwa na imani juu Uimamu wa mwanawe, aitwaye Abdullah al-Aftah. [45] Kulingana na ripoti ya Shahrastani, ni kwamba; Abdullahi alifariki siku sabini baada ya kuuawa kwa Imamu Ja’afar al-Sadiq (a.s) na hakuacha watoto yoyote yule baada yake. [46] Hivyo, imani ya uongozi wa Abdullah al-Aftah ilifikia kikomo baada tu ya kufariki kwake, na wafuasi wake wengi walimkubali Imamu Musa al-Kadhim (a.s) kama ni kiongozi wao mpya. [47]
  • Nawusiyyah: Hili ni kundi la Waislamu wa Kishia ambalo lilikuwa na imani ya kwamba Imamu Jafar al-Sadiq (a.s) bado hajafa na wakaamini kuwa yeye ndiye Mahdi mtarajiwa (al-Muntadhar), ambaye atadhihiri na kuonenkanana tena mwishoni mwa dunia. [48] Inasemekana kuwa Nawusiyyah walikuwa ni wafuasi wa mtu aitwaye Ajlan bin Nawus kutoka mji wa Basra nchini Iraq. [49]
  • Waqifiyyah: Hili nalo ni kundi la Waislamu wa Kishia lililo amini juu ya uongozi wa Imamu Musa al-Kadhim (a.s) lakini wakataa kukuubali uongozi (Uimamu) wa mwanawe, aitwaye Imamu Ali al-Ridha (a.s). [50] Kwa mujibu wa nukuu za kitabu kiitwacho Rijal al-Kashi, ni kwamba; Wakati Imam Musa al-Kadhim (a.s) akiwa gerezani, baadhi ya wafuasi wake walikuwa na mali ambazo zilikuwa ni sehemu ya haki ya Imamu. Pale wafuasi hawa walipata habari za kifo cha Imamu Musa al-Kadhim (a.s) na waliamua kutoamini kifo chake pamoja na kupinga uongozi (Uimamu) wa mwanawe, ambaye ni Imam Ali al-Ridha, (a.s) na hivyo washikilia imani yao juu Imam Musa al-Kadhim (a.s) peke yake, na hakuendelea kuamini Maimamu waliofuata baada yake, kwa hiyo wafuasi wao wakajulikana kwa jina la Waaqifiyyah. [51]

Makundi ya Maghulati

Makala Asili: Maghulati

Maghulati ni watu waliompa Imamu Ali (a.s) na watoto wake sifa za Uungu au unabii, na walikuwa na kawaida ya kupindukia mipaka katika kuwasifu Maimamu wao. [52] Vitabu vinavyotafiti madhehebu mbali mbali vimekhitilafiana juu ya idadi hasa ya makundi ya Maghulati, ambapo baadhi yake vimetoa ripoti yenye rikodi ya idadi ndogo kabisa. Kiuhalisia; idadi ndogo kabisa kuhusiana na makundi ya Maghulati, ni tisa na idadi kubwa zaidi ni idadi ya makundi mia moja. [53] Baadhi ya makundi maarufu ya Maghulati yaliyohusishwa na Mashia ambayo kwa hivi sasa yamekwisha potea ni pamoja na: Sabaa-iyyah (wafuasi wa Abdullah bin Saba), Bayaniyyah, Khattabiyyah, Bashiiriyyah, Mufawwidha na Mughiriyyah. [54]

Aliyyu-Ilahi au Ahlu Haqqi: Ni miongoni mwa makundi mengine ya Maghulati yanayo husishwa na Mashia, ambalo baadhi ya wafuasi wake bado wanaishi katika maeneo fulani ya Iran. [55] Inasemekana kuwa; wao wanaamini kuwa Mungu alifichua siri yake na kuwapa manabii, ambayo ilikuwa ni siri ya unabii, na siri hiyo iliendelea kutoka kwa Nabii Adam hadi kwa Nabii Muhammad (s.a.w.w), na baada ya kifo cha Nabii Muhammad (s.a.w.w), siri hiyo ilimfikia Imam Ali na kisha ikaendelea kwa Maimamu waliofuatia hadi kumfikia Imamu wa kumi na mbili. [56] Baada ya ghaiba (kuingia mafichoni) ya Imamu wa kumi na mbili, siri hiyo (siri ya Uimamu) imeendelea kufunuliwa kwa wafuasi na viongozi wao ambao wanakuja mmoja baada ya mwingine hadi adhihiri tena Imamu Mahdi (a.s). [57]

Makundi Yalopotoka Katika Kipindi cha Ghaiba Ndogo

Nawbakhti katika kitabu chake kiitwacho Firaq al-Shi'a ametaja ndani yake makundi kadhaa ya Kishia yaliyozuka baada tu ya kifo cha Imamu Hassan al-Askari (a.s), ambayo yalipotoka na kukengeuka kutoka njia iliyo sahihi, jambo ambalo lilitokana suala la kumchagua Imamu anayestahiki kukamata nafsi ya Imamu Hassan al-Askari (a.s), na katika kuainisha ni nani hasa Mahdi al-Maw'ud (Mahdi Mtarajiwa). Nawbakhti ametaja idani ya makundi 14 yaliopotoka katika kitabu chake hicho. [58] Kwa mfano, miongoni mwao kundi moja lilidau kuwa Imamu Hassan al-Askari (a.s) hakufariki dunia, bali yeye ndiye Mahdi al-Qa'im (Mahdi Mtarajiwa). [59] Kundi jingine likadai kuwa; Imamu Hasan al-Askari (a.s) alifariki, lakini kwa kuwa hakuwa na mtoto wa kiume, ilibidi aishi tena baada ya kifo hicho, na yeye ndiye Mahdi al-Qa'im. [60] Kundi jingine lilikanusha Uimamu wa mtoto wa Imam Hasan al-Askari (a.s), ambaye ni Imamu Mahdi (a.s), nao wakasema kwamba; Baada ya Imamu Hasan al-Askari, kaka yake ambaye ni Ja’afar, ndiye Imamu halisi. [61] Sheikh Mufidu katika kitabu chake kiitwacho Al-Fusul al-Mukhtaara akinukuu kutoka kwa Nawbakhti, anasema kuwa; Ukiachana na kundi la Imamiyya, kati ya makundi haya 14, makundi mengine yote yaliobakia yametoweka. [62]

Aidha, watu kama vile Hassan Shari'i, Muhammad bin Nusair Numairiy, Ahmad bin Hilal Abartaiy na wengineo, walikuwa ni miongoni mwa Waislamu wa Shia ambao walidai kuwa Wawakilishi wa Maimamu na walidai kuwa walikuwa ni manaibu kutoka kwa Imam Mahdi (a.s), na wakaunda makundi kahdaa ambayo yote yalipotea na kutoweka. [63]

Idadi ya Mashia na Usambazikaji Wao Kijiografia

Kwa mujibu wa ripoti iliyotajwa katika kitabu "Naqshe Jami’iyyate Musalmaanane Jihaan/Ramani ya Idadi ya Waislamu Duniani" (kilichotungwa mwaka 1393 Shamsia), yaonesha kamba; Kuna Idadi ya zaidi ya watu milioni 300 ya Waislamu wa Kishia duniani, ambao ni Ithna Ashariyyah, Ismailiyyah, na Zaydiyyah, ambayo ni moja ya tano ya jumla ya idadi ya Waislamu wote duniani. [64] Kwa mujibu wa Shirika la Habari la BBC Farsi ya mwaka 1394 Shamsia, ni kwamba; Mashia wa kundi la Ismailiyyah inakadiriwa kuwa ni milioni 15, ambayo ni chini ya asilimia kumi ya Waislamu wa Kishia duniani, ambapo wengi wao wanaishi katika nchi za: India, Pakistan, Afghanistan, Tajikistan. Pia takriban watu 30,000 miongoni mwa Mashia hao wanaishi ndani ya mikoa mbali mbali nchini Iran, kama vile; Khorasan, Kerman na vitongoji vya kati kati ya Iran “Markazi”. [65] Katika Ensaiklopidia ya Britannica, chini ya kichwa cha neno «Shia», imeelezwa kwamba kundi la Nizariyyah, moja ya matawi yenye idadi kubwa zaidi ya Ismailiyyah, lina idadi ya kati watu milioni tano hadi milioni 15. [66]

Yasemekana kwamba Zaydiyyah ni tawi lenye idadi ndogo zaidi ya watu kati ya makundi ya Shia yaliopo hivi sasa, na wengi wao kwa hivi sasa (katika karne ya kumi na tano Hijria), wanaishi nchini Yemen. Idadi ya kundi hili nchini Yemen, linaunda nusu nzima ya idadi ya watu wa nchi hiyo. [67] Pia kuna baadhi yao wanaishi Najran, eneo la kusini mwa nchi ya Saudi Arabia. [68] Kati ya makundi ya Mashia yaliyopo hivi sasa duniani, Ithna Ashariyyah ndio kundi lenye idadi kubwa zaidi ya wafuasi duniani, [69] na wengi wao wanaishi katika nchi kama vile; Iran, Iraq, Pakistan na Lebanon. [70]

Vitabu Makhususi Vilivyo Andikwa Juu ya Maudhui hii

Baadhi ya kazi zinazo jitegemea zilizo andikwa katika kutayambulisha makundi ya madhehebu ya Shia ni pamoja na:

  • Kitabu kiitwacho Firaq al-Shia (Makundi ya Shia): ambacho ni kitabu cha Hassan bin Musa al-Nawbakhti. Kazi hii ni mojawapo ya vyanzo vya utambuzi wa madhehebu ya Shia hadi mwishoni mwa karne ya tatu Hijria. Katika kitabu hiki, mbali na kutayambulisha madhehebu ya Shia, pia kuna mijadala ya kina ndani yake kuhusiana na baadhi ya madhehebu mengine ya Kiislamu. Inasemekana kwamba; kwa kuzingatia kuwa mwandishi huyu alikuwa akiishi katika enzi za Ghaibah Sughra na kushuhudia migawanyiko ya Shia katika kipindi hicho, kazi hii inahesabika kama ni chanzo cha kwanza kabisa katika uwanja huu. [71]
  • Kitabu kiitwacho Aashenai Baa Firaqe Tashayyu «Utambuzi wa Makundi ya Shia»: kilichoandikwa na Mahdi Farmanian. Kitabu hiki kinajumuisha utangulizi mmoja na masomo ishirini katika kutayambulisha makundi ya madhehebu ya Shia, ambacho kimekusudiwa kuwa ni matini maalumu ya kutoa mafunzo juu ya suala hilo. Pia kuna mijadala miwili ndani yake yenye vichwa visemavyo; Firqehaye Inhirafiy wa Inshi’abiy az Tashayyu «Makundi Potofu na Migawanyiko Kutoka Katika Madhehebu ya Shia» na Firqehaye Shi’iy Bar Asase Kutube Mash-huur Milale wa Nihal «Madhehebu ya Shia kulingana na vitabu maarufu vya Milal na Nihal», ambavyo vimeambatanishwa mwishoni mwa kitabu hichi. [72]

Rejea

Vyanzo