Nenda kwa yaliyomo

Mnafiki

Kutoka wikishia

Mnafiki (Kiarabu: المنافق) ni mtu ambaye hajaukubali Uislamu moyoni mwake, lakini kidhahiri anajionyesha kuwa ni muumini. Suala la unafiki lilizungumziwa baada ya Mtume (s.a.w.w) kuhama kutoka Makka kwenda Madina na kuchukua hatamu za uongozi mjini Madina. Katika kipindi hiki, kulikuweko na watu ambao walikuwa dhidi ya Uislamu, lakini hawakuwa na uwezo wa kupinga waziwazi, na ndiyo maana kidhahiri walikuwa wakijiita kuwa ni Waislamu. Unafiki ni miongoni mwa mambo ambayo yamezungumziwa sana ndani ya Qur'ani tukufu na kuna sura haswa inayojulikana kwa jina la Surat al-Munafiqun ambayo inazungumzia sifa maalumu za wanafiki na kuwatambulisha wanafiki kwamba, ni watu wa aina gani. Kusema uongo, dhana mbaya, kujikweza, kufanyia masihara haki, kutenda dhambi na ufuska ni sifa ambazo zimetajwa na Qur'an kuwa sifa za wanafiki.

Abadallah bin Ubayy (Ibn Salul), Abdallah bin Uyaynah na wafuasi wa Aqaba wametajwa kuwa katika orodha ya wanafiki mashuhuri. Kwa mujibu wa ripoti za kihistoria, Mtume (s.a.w.w) alikuwa akiwalegezea kamba wanafiki na alikuwa akizifanya hatua zao kutokuwa na athari lakini kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Masjid al-Dhirar uliokuwa kituo cha baadhi ya wanafiki katika mji wa Madina, ulibomolewa kwa amri ya Bwana Mtume (s.a.w.w).

Kwa mujibu wa Aya ya 145 ya Surat al-Nisaa, wanafiki watakuwa katika tabaka ya chini kabisa motoni. Wafasiri wa Qur'an wakitegemea Aya hii kama ushahidi wao, wameutambua unafiki kuwa ni mbaya zaidi ya ukafiri. Swala ya maiti ambaye alikuwa mnafiki ina tofauti na Swala ya maiti kwa muumini na badala ya kumtakia msamaha na maghufira, hulaaniwa.

Vitabu vya "Sifat al-Nifaq na Sifat al-Munafiqin mina al-Sunan al-Maathura an Rasulillah vilivyoandikwa na Abu Nuʿaym al-Isfahani, na Sifat al-Muunafiqin kilichoandikwa na Ibn Qayyim al-Jawziyya na al-Nifaq wal-Munafiqun Fil Qur'an al-Karim kilichoandikwa Sheikh Ja'afar Sub'hani ni miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa kuhusiana na wanafiki.

Dhana ya Unafiki

Mnafiki ni mtu ambaye anaficha ukafiri wake na kudhihiirisha kisichokuwa hicho na anauficha ukafikiri wake kwa kudhihirisha na kuonyesha kwamba, ni Muislamu.[1] Mnafiiki ni neno linalotumika mkabala na maneno mawili ya muumini na kafiri.[2] Shahidi Murtadha Mutahhari anasema: Muumini ni mtu ambaye ana imani na Uislamu katika moyo, ulimi na katika vitendo, ilihali kafiri ni mtu ambaye hajaukubali Uislamu kidhahiri na kibatini na mnafiki huitwa mtu ambaye anaupinga Uislamu katika moyo wake, lakini kidhahiri ana imani na itikadi na Uislamu.[3]

Tofauti ya Unafiki na Ufisadi

Imani ni itikadi ya kimoyo na kukiri kwa ulimi na kutekeleza kwa mujibu wa wadhifa na majukumu. Kwa msingi huo mwenye kuwa na vitu hivi vitatu ni muumini, na kila ambaye hana vitatu hivi ni kafiri, na kila ambaye atakiri kwa ulimi (kwa uongo) lakini akawa hana itikadi ndani ya moyo wake kwa kile alilokiri basi ni mnafiki, na kila ambaye ana itikadi ya moyoni na amekiri wa ulimi, lakini anazembea na kutofanyia kazi hayo ni fisadi na fasiki.[4]

Allama Tabatabai ameitambua unafiki na udhaifu wa imani kwamba, ni mambo mawili tofauti ambapo la kwanza yaani unafiki ni mtu kusema jambo ambalo hana itikadi nalo na halifanyi kazi na jambo la pili ni mtu kusema kitu ambacho ana itikadi nacho lakini hakifanyi kazi kutokana na udhaifu wa matakwa na kutokuwa na hima.[5]

Umuhimu wa Wanafiki katika Historia ya Uislamu

Kwa mujibu wa tafsiri ya Qur’an ya Nemooneh, suala la unafiki na wanafiki katika Uislamu lilizungumziwa baada ya Mtume kuhamia katika mji wa Madina. Katika mji wa Makka, wapinzani wa Uislamu walikuwa wakiendesha propaganda zao waziwazi dhidi ya Uislamu; lakini baada ya Waislamu kupata nguvu na kujiimarisha mno katika mji wa Madina, maadui wakawa katika hali ya udhaifu na kutoweza kukabiliana waziwazi na Waislamu. Hivyo ili kuendeleza mipango yao michafu dhidi ya Mtume (s.a.w.w) na Waislamu, kidhahiri walijiunga na safu za Waislamu katika hali ambayo, hiakuwa na imani ya sawa sawa, kwa maana kwamba, walikuwa wakificha itikadi yao iliyo dhidi ya Uislamu.[6]

Surat al-Munafiqun imeshuka ikizungumzia maudhui hii. Ndani ya sura hii, Mwenyezi Mungu amebainisha sifa na wasifu wa wanafiki na imeelezewa uadui wao dhidi ya Waislamu. Kadhaklika katika sura hii Mtume (s.a.w.w) amepewa amri kwamba, awe na tahadhari juu ya hatari ya wanafiki.[7] Katika Surat al-Tawba pia, kuna Aya kadhaa zinazozungumzia wanafiki.[8] Allama Tabatabai, anaamini kwamba, tathmini na uchambuzi wa kihistoria unapaswa kufanywa kwa mujibu wa Aya za Qur’an Tukufu ili kuweka wazi ufisadi, uharibifu na matatizo yaliyoikumba jamii ya Kiislamu.[9]

Shakhsia za Kinafiki Mwanzoni mwa Uislamu

Katika vyanzo vya historia na hadithi, baadhi ya wanafiki waliokuwako mwanzoni mwa Uislamu wametambulishwa na kutajwa. Maqrizi amewataja katika kitabu chake cha “Imtina’a al-Isma’a” wanafiki wa kabila la Aws na Khazraj pamoja na hatua zao za kiuadui walizochukua dhidi ya Uislamu na Mtume (s.a.w.w). Miongoni mwao ni: Abdallah bin Ubayy ambaye alitishia kuwafukuza Muhajirina kutoka Madina na Abdallah bin Uyayna ambaye alikuwa akiwahamasisha masahaba zake wamuue Mtume (s.a.w.w).[10]

Watu wa Aqaba nao wamo katika orodha ya wanafiki. Hili ni kundi la masahaba ambao wakati Mtume akiwa njiani anarejea kutoka katika vita vya Tabuk walipanga njama za kumuua, lakini hawakufanikiwa katika hilo.[11] Wanahistoria na waandishi wa sira, wamesema kuwa, watu wa Aqaba walikuwa 12 mpaka 15. [12] Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Baqir (a.s) ni kwamba, watu hao walikuwa 12 ambapo wanane kati yao walikuwa wanatokana na kabila la Qureshi.[13] Sheikh Swaduq akitegenea hadithi amewataja 12 kati yao kuwa ni kutoka Bani Umayya na watano kati yao kutoka katika makabila mengine.[14] Suyuti mmoja wa Maulamaa wa Ahlu-Sunna amenukuu majina ya watu wa Aqaba wakiwemo: Saʿd bin Abi Sarḥ, Abu Ḥaḍhir al-Aʿrabī, Julas bin Suwayd, Maj’maa bin Jariyah, Mulayh al-Taymi, Huswayn bin Numayr, Tuʿayma bin Ubayriq, na Murra bin Rabi.[15]

Muamala wa Mtume na Wanafiki

Kwa mujibu wa watafiti, kutokana na matokeo yote ya kihistoria kuhusu namna Mtume (s.a.w.w) alivyowashughulikia wanafiki, inawezekana kufikia natija hii kwamba, kila mara alikuwa akiamialiana na wanafiki kwa uvumilivu na msamaha kadiri ilivyowezekana.[16] Mtume (s.a.w.w) alikuwa akifahamu vyema unafiki uliofichikana wa wanafiki na katika hali nyingi, Aya za Qur’an zilikuwa zikiwatambulisha watu hao.[17] Mtume alikataa mara chungu nzima pendekezo lililokuwa likitolewa la kuwaua wanafiki na alikuwa akikataza kufanyika jambo kama hilo. Pamoja na hayo, inaelezwa kuwa, msamaha na hatua ya Mtume ya kuwavumilia na kufumbia macho vitendo vya wanafiki hao haikuwa ikipelekea aipuuze jamii ya Kiislamu. Mtume (s.a.w.w) alikuwa akifuatilia kwa karibu nyendo za wanafiki, akivuruga mipango yao na wakati wa kutokea uvumi na uzushi alikuwa akiwabainisha na kuwajuza Waislamu ukweli halisi wa mambo. Hata hivyo, katika baadhi ya matukio nadra, Mtume aliwashughulika wanafiki kwa nguvu zote na bila kuwafumbia macho au kuwaonea huruma hata kidogo. Miongoni mwa matukio hayo ni kubomoa msikiti wa Dhirar.[18]

Sifa Maalumu za Wanafiki kwa Mujibu wa Qur’an

Katika Qur'an na hadithi, sifa maalumu za wanafiki zimeelezwa. Kwa mujibu wa waandishi wa tafsiri ya Nemooneh, katika Surat al-Munafiqun kumetajwa sifa zao kumi: Kusema uongo, kuapa kiapo cha uongo, kutokuwa na udiriki na ufahamu sahihi wa ukweli, kujionyesha kidhahiri na kuwa na lugha nzuri na laini ambazo zimeficha ukweli nyuma yake, kutokuwa tayari kubadilika na kusalimu amri mbele ya maneno ya haki, dhana mbaya, kuogopa kila tukio, kuifanyia masihara haki, ufuska, dhambi, kuwa na taswira ya kumiliki kila kitu, kuwaona watu wengine kuwa wahitaji wake, kujikweza na kuwadogosha wengine.[19] Kwa mujibu wa Tafsir al-Mizan ni kwamba, kutumika neno “Hushubun Musannadah” yaani magogo yaliyoegemezwa, na kushabihishwa nalo wanafiki katika Surat al-Munafiqun ni jambo linalobainisha kulaumiwa kwao. Hii ina maana kwamba, licha ya wao kuwa na miili mizuri, ya kusifiwa, kuwa wazungumzaji wazuri na wenye maneno matamu, lakini wao ni mithili ya magogo yaliyoegemezwa katika ukuta ambayo hayana faida.[20]

Muhammad Taqi Yazdi ameashiria hotuba ya 194 ya Nahaj al-Balagha na kuzibainisha sifa hizi kwa wanafiki: Kutumia mbinu za siri, kujipamba kidhahiri na kuwa wachafu kwa ndani, kuwatakia mabaya waumini na kutafuta maslahi katika mahusiano na maingiliano yao na watu wengine.[21]

Tathmini ya Kusema Uongo Wanafiki

Qur’an tukufu inanukuu maneno ya wanafiki ambao walikuwa wakitoa ushuhuda juu ya Utume na risala ya Mtume wa Mwenyezi Mungu na wakieleza wazi kwamba, wanashuhudia kwamba, yeye ni Mtume wa Allah, lakini kimsingi walikuwa wakisema uongo. ((Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu anashuhudia ya kuwa hakika wanaafiki ni waongo)).[22]

Hivyo basi, kukadhibishwa maneno ya wanafiki hapa kunatokana na kuwa, walikuwa wakitoa habari ya kitu ambacho kimsingi hawana imani wala itikadi nacho. Kwani hawakuwa wakiamini kikweli kweli risala ya Mtume.[23] Mwandishi wa Tafsir Nour ana anasema kuwa, kimsingi unafiki ni uongo wa kivitendo ambao ni kuficha ukafiri na kuonyesha imani kwa uongo.[24]

Kushabihisha Hali ya Kiroho ya Mnafiki

Kwa mujibu wa Aya ya 17 hadi 19 za Surat al-Baqarah wanafiki wanashabihishwa na watu ambao wako katika giza totoro na ambao hawawezi kuainisha njia iko wapi. Wanatafuta mwanga ili wawze kuona sehemu zinazowazunguka. ((Mfano wao ni kama mfano wa aliyekoka moto, na ulipo tanda mwangaza wake kote kote Mwenyezi Mungu aliiondoa nuru yao na akawawacha katika giza, hawaoni. Viziwi, mabubu, vipofu; kwa hivyo hawatarejea, au ni kama mvua kubwa itokayo mbinguni, ina giza na radi na umeme; wakawa wakitia vidole vyao masikioni mwao kwa ajili ya mingurumo, kwa kuogopa kufa. Na Mwenyezi Mungu amewazunguka makafiri.

Ufananishaji huu unaonyesha kuwa, mnafiki hapendi imani, lakini anadhihirisha kuwa na imani kutokana na kutokuwa na budi, lakini kwa kuwa moyo wake na ulimi wake haviko katika hali moja, kwa maana kwamba, anachokisema, sio anachokiamini, hawezi kuona njia. Mtu wa namna hii daima huwa katika kuteleza na kukosea. Hutembea hatua moja na Waislamu, lakini husimama tena na kutoendelea pamoja nao.[25]

Nafasi ya Wanafiki Motoni

Kwa mujibu wa Aya ya 145 ya Surat al-Nisaa ni kuwa, wanafiki watakuwa katika tabaka ya chini kabisa motoni: ((Hakika wanaafiki watakuwa katika t'abaka ya chini kabisa Motoni, wala hutompata yeyote wa kuwanusuru)). Hatimaye Aya hii inawabainisha wanafiki.[26] Ayatullah Nassir Makarem Shirazi mmoja wa wafasiri wa Qur’an wa Kishia anasema, kwa mujibu wa Aya za Qur’an tukufu, unafiki ni mbaya zaidi ya ukafiri, na wanafiki ni viumbe wa mbali kabisa wa Mwenyezi Mungu.[27]

Monografia

Mbali na maudhui na mijadala iliyopo katika vitabu vya fikihi na tafsiri kuhusiana na wanafiki, kuna vitabu vya kujitegemea vilivyoandikwa kuhusiana na maudhui hii ambapo baadhi ya vitabu hivyo ni vikongwe kama vile:

  • Sifat al-nifaq wa dhamm al-Munafiqin, mwandishi: Ja’afar bin Muhammad al-Faryani 9207-301 Hijria).
  • Sifat al-nifaq wa naʿt al-munafiqin min al-sunan al-maʾthura ʿan Rasul Allah mwandishi: Abu Nuʿaym al-Isfahani (234-430 Hijria).
  • Sifat al-munafiqin kilichoandikwa na Ibn Qayyim al-Jawziyya (691-751 Hijria).

Baadhi ya vitabu vingine kuhusiana na maudhui hii ni:

  • Al-Munafiqun fil Qur’an, mwandishi Sayyid Hussein Sadr.
  • Al-Nifaq Wal-Munafiquun fil Qur’an al-Karim, mwandishi: Ja’afar Subhani.
  • Dhahirat al-nifaq wa khaba'ith al-munafiqin fi al-tarikh, mwandishi Abd al-Rahman Hasan Habanka al-Maydani.
  • Al-Muwajiha bayn al-Nabi (s) wa bayn al-munafiqin, mwandishi: Abd al-Karim Nayyiri.
  • Suwar al-munafiqin fi al-Quran al-Karim, mwandishi: Bukhari Saba'ie.
  • Nifaq wa munafiq az didgah-i shahid Mutahhari, mwandishi: Zahra Ashiyan and Firishta Salami.
  • Chehre munafiqan dar Qur'an, mwandishi: Farazmand.

Rejea

  1. Ṭurayḥī, Majmaʿ al-baḥrayn, juz. 5, uk. 241.
  2. Muṭahharī, Majmūʿa-yi āthār, juz. 25, uk. 201-202.
  3. Muṭahharī, Majmūʿa-yi āthār, juz. 25, uk. 206.
  4. Hosseini Shah Abdul Azimi, Tafsir Ithina-ashar, 1363 S, juz. 13, uk. 177; Qaraati, Tafsir Noor, 1363 S, juz. 10, uk. 50.
  5. Ṭabāṭabāʾī, al-Mīzān, juz. 19, uk. 249.
  6. Makarem Shirazi, Tafsir al-Nashon, 1374 S, juz. 24, uk. 146.
  7. Tabatabai, Al-Mizan, 1417 H, juz. 19, uk. 278.
  8. Rak: Quydel, Munafiqin dar Quran.
  9. Tabatabai, Al-Mizan, 1391 H, juz. 9, uk. 414.
  10. Moghrizi, Imtaa al-Isma, 1420 H, juz. 14, uk. 343-364.
  11. Maqrizi, Imtaa al-Isma, 1420 H, juz. 2, uk. 74.
  12. Waqidi, al-Maghazi, 1409 H, juz. 3, uk. 1045-1044; Ibn Kathir, Al-Badiyah na Al-Nahiyah, 1398 H, juz. 5, uk. 200.
  13. Tabarsi, Majmam al-Bayan, 1372 S, juz. 5, uk. 79.
  14. Sheikh Swadouq, Al-Khiswal, 1362 S, juz. 2, uk. 398.
  15. Suyuti, Al-Dar al-Manthur, Dar al-Fikr, juz. 4, uk. 243.
  16. Dānish, Rasūl-i Khudā wa istirātizhī-yi īshān dar barābar-i khaṭṭ-i nifāq, uk. 23.
  17. Dānish, Rasūl-i Khudā wa istirātizhī-yi īshān dar barābar-i khaṭṭ-i nifāq, uk. 23.
  18. Jaʿfarīyān, Tārīkh sīyāsī-yi Islām, uk. 650; Dānish, Rasūl-i Khudā wa istirātizhī-yi īshān dar barābar-i khaṭṭ-i nifāq, uk. 21-22.
  19. Makārim Shīrāzī, al-Amthal fī tafsīr kitāb Allāh al-munzal, juz. 3, uk. 504.
  20. Tabatabai, Al-Mizan, 1394 H, juz. 19, uk. 281.
  21. Misbah Yazdi, "Akhlaq islami", uk. 4.
  22. Surat al-Manafiqun aya ya 1
  23. Tabatabai, al-Mizan fi Tafsir al-Qur'an, juz. 9, uk. 315, juz. 19, uk. 279.
  24. Qiraati, Tafsir Noor, 1383 S, juz. 10, uk. 49.
  25. Tabatabai, tafsiri ya Tafsir al-Mizan, 1374 S, juz. 1, uk. 89.
  26. Makarem, Al-Amthal, 1421 H, juz. 3, uk. 505.
  27. Makarem, Al-Amthal, 1421 H, juz. 3, uk. 504.

Vyanzo

  • Dānish, Muḥammad Qādir. Rasūl-i Khudā wa istirātizhī-yi īshān dar barābar-i khaṭṭ-i nifāq, Ma'rifat Magazine, no. 129, 1387 Sh.
  • Ḥillī, al-Ḥasan b. Yūsuf al-. Taḥrīr aḥkām al-sharʿīyya ʿalā madhhab al-imāmīyya. Edited by Ibrahim Bahaduri. Qom: Muʾassisa-yi Imām Ṣādiq (a), 1420 AH.
  • Ibn Kathīr al-Dimashqī, Ismāʿīl b. ʿUmar. Al-Bidāya wa l-nihāya. Beirut: Dār al-Fikr, 1398 AH.
  • Jaʿfarīyān, Rasūl. Tārīkh sīyāsī-yi Islām; sīra-yi Rasūl-i Khudā. Qom: Intishārāt-i Dalīl-i Mā, 1380 Sh.
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Al-Amthal fī tafsīr kitāb Allāh al-munzal. First edition. [n.p.], 1421 AH.
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Tafsīr-i nimūna. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmiyya, 1374 Sh.
  • Maqrizī, Aḥmad b. ʿAlī. Imtāʿ al-asmāʾ. Edited by Muḥammad ʿAbd al-Ḥamīd al-Namīsī. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1420 AH.
  • Misbāḥ Yazdī, Muḥammad Taqī. Akhlāq-i islāmī. Maʿrifat Magazine, no. 4, 1372 Sh.
  • Muṭahharī, Murtaḍā. Majmūʿa-yi āthār. Tehran: Intishārāt-i Ṣadrā, 1390 Sh.
  • Najafī, Muḥammad al-Ḥasan al-. Jawāhir al-kalām fī sharḥ sharāʾiʿ al-Islām. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, [n.d.].
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Al-Khiṣāl. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī. Qom: Jāmiʿat al-Mudarrisīn-i Ḥawza-yi ʿIlmiyya, 1362 Sh.
  • Suyūṭī, ʿAbd al-Raḥmān b. Abī Bakr al-. Al-Durr al-manthūr fī tafsīr al-maʾthūr. Beirut: Dar al-Fikr, [n.d.].
  • Ṭabāṭabāʾī, Sayyid Muḥammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Qom: Intishārāt-i Islāmī (Jāmiʿat al-Mudarrisīn), 1417 AH.
  • Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Majmaʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Tehran: Nāṣir Khusruw, 1372 Sh.
  • Ṭurayḥī, Fakhr al-Dīn b. Muḥammad al-. Majmaʿ al-baḥrayn. Edited by Sayyid Aḥmad Ḥusaynī. Tehran: al-Maktaba al-Murtaḍawīyya, 1416 AH.
  • Wāqidī, Muḥammad b. ʿUmar al-. Al-Maghāzī. Edited by Marsden Jones. Beirut: Muʾassisat al-A'lami, 1409 AH.