Nenda kwa yaliyomo

Jamhuri ya Kiislamu

Kutoka wikishia

Jamhuri ya Kiislamu (Kiarabu: الجمهورية الإسلامية) ni mfumo wa utawala unaosimama au kujengeka kupitia nguzo mbili kuu, nazo ni: umma na Uislamu. Wafuasi wa mfumo huu wa kisiasa wanaufasiri muundo na aina ya serikali hii, kama ni mfumo wa kijamhuri wenye nyenzo na taratibu za Kiislamu. Kwao, Jamhuri ya Kiislamu ina maana ya ushirikishwaji wa matakwa na ridhaa ya umma katika uendeshaji wa dola, chini ya wigo wa sheria za Kiislamu. Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Mkuu wa pili wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika kutathmini kwake dhana ya Jamhuri ya Kiislamu, ameoneka kutumia istilahi pacha ya demokrasia inayozingatia theocracy kwa maana ya utawala wa umma unaozingatia kidini. Hii inamaanisha ushiriki wa umma pamoja na athari zake katika nyanja na sekta zote za mamlaka ya uendeshaji, ndani ya mfumo wa vigezo vya Kiislamu.

Kulingana na mitazamo ya wengine, dhana ya Jamhuri ya Kiislamu haioani na haki ya umma ya kushiriki katika mamlaka ya uendeshaji wa nchi yao. Sababu inayotolewa kuhusiana na madai haya ni kwamba; ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, huwa kuna ulazima wa kuzingatia na kufuata sheria za Kiislamu, hata pale zinapokinzana na matakwa ya umma. Mwanatafakuri wa kidini, Murtadha Mutahhari, alikabiliana na pingamizi hili na kujibu hoja za madai haya akisema kwamba; demokrasia haifungamani kabisa na masuala ya itikadi. Hivyo basi; kuwa na itikadi, kutokuwa na itikadi, kukubaliana na mfumo au kuto kubaliana na mfumo fulani si miongoni mwa masuala yanayofasiri maana ya demokrasi. Bali demokrasia ni kule kukubaliana na chaguo la waliowengi, kwani haiwezekani kila mmoja kuanzisha mfumo wake kulingana na itikadi yake binafsi. Hiyo basi, endapo jamii itakukubali kuendeshwa kulingana na itikadi fulani, hapo ridhaa yao itakuwa ni ithibati tosha ya kuthibitisha demokrasia ya serikali yao.

Kuna nchi kadhaa duniani zenye kuendesha nchi zao kulingana na mfumo wa kisiasa wa Jamhuri ya Kiislamu, baadhi ya mataifa hayo ni kama vile; Iran, Pakistan na Mauritania.

Dhana na Hadhi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu

Jamhuri ya Kiislamu ni mfumo wa kisiasa wa utekelezaji wa mamlaka ya utawala uliojengwa juu ya nguzo mbili: dhana ya ujumhuri na itikadi ya Kiislamu. [1] Serikali ya jamhuri ni serikali ambayo mkuu wa nchi yake huchaguliwa moja kwa moja na umma wa nchi hiyo. Uchaguzi wao huo huwa ni ruhusa maalumu inayomwezesha raisi huyo kushika mamlaka ya wananchi wake kwa muhula maalum. [2] Kwa mujibu wa maoni ya Imam Khomeini (Aliyezaliwa mnamo 1902 na kufariki mwaka 1989), ambaye ni muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, pamoja na Murtadha Mutahhari (alifariki 1979), mwanatafakuri wa Kishia, ni kwamba; Jamhuri ya Kiislamu ni mfumo maalumu ambao sura na umbile lake ni la kijamhuri, ilhali nyezo na chimbuko la kiini chake chake ni Uislamu. [3]

Sayyid Muhammad Beheshti (aliyefariki 1360 H.Sh./1981 M.) akifafanua mifumo mbali mbali ya kijamhuri, aliiainisha mifumo hiyo katika kategoria mbili kuu: Kategoria ya kwanza ni mfumo unayojikita katika mhimili mmoja pekee, ambao ni ridhaa ya wananchi (umma). Nao ni ule mfumo wa kidemokrasia unaoyofungamana na itikadi (ideology) maalum. Kategoria ya pili ni mfumo uliojengwa juu ya msingi wa itikadi (ideology) maalum. Katika mfumo wa aina hii, matakwa na mitazamo ya umma hupata uhalali wake ndani ya wigo wa itikadi husika, iliyokubaliwa na umma (wananchi) wenyewe. Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu upo katika kategoria hii ya kundi la pili. [4]

Uwiano kati ya Serikali kuwa ni ya Kiislamu na Haki ya Wananchi ya Kujitawala

Makala asili: Demokrasia ya Kidini

Baadhi ya watu wamehoji wakisema kwamba; dhana ya Jamhuri ya Kiislamu inapingana na haki ya wananchi ya kujitawala; hii ni kwa sababu ya kwamba; katika Jamhuri ya Kiislamu, kuna ulazima wa kufuata sheria na kanuni za Kiislamu, wakati katika demokrasia, watu wanapaswa kuwa na haki ya kuchagua hatima yao wenyewe. Murteza Motahhari, mwanafikra wa kidini, anajibu hoja hii akisema kuwa; maana ya neno demokrasia haifungamani itikadi ya mtu fulani. Hivyo basi, ikiwa wananchi wa jamii fulani watakubaliana na mfumo fulani wenye itikadi fulani, basi matakwa ya umma yatalazimiana na utekelezwaji wa sheria za mfumo huo, uamuzi ambao hutambulikana kama ni moja ya aina za demokrasia. [5] Pia Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi wa pili wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika uchambuzi wake wa kuelezea muundo huu wa kisiasa, ameufasiri muundo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kama ni utimizwaji wa matakwa ya watu katika masuala ya kisiasa, sambamba na utekelezwaji wa sheria za Kiislamu, na ameutaja mfumo huu kwa jina la Demokrasia ya Kidini. [6]

Mataifa Yenye Mfumo wa Utawala wa Jamhuri ya Kiislamu

Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, kama moja ya aina za serikali za kijamhuri katika siasa za dunia, ulijitokeza mnamo karne ya 20, kama ni mmo wa mifumo uliotawala katika nchi kadhaa duniani. Jamhuri ya Kiislamu ya Turkestan Mashariki inatajwa kuwa ndiyo serikali ya kwanza kabisa iliyoanza kubeba jina la Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ulimwenguni. Serikali hii iliundwa katika miaka ya 1930 kwenye mji wa Kashgar, eneo la magharibi mwa China, kupitia Harakati za Kiislamu za Turkestan ya Mashariki, ila serikali hii haikuweza kudumu kwa muda mrefu. [7] Pia mnamo tarehe 28 Novemba mwaka 1960, baada ya Mauritania kupata uhuru kutoka kwa Ufaransa, mfumo rasmi wa nchi hiyo ulitangazwa kuwa ni mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. [8]

Mnamo mwaka 1973, katiba ya Pakistan iliutambua mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kama ni utawala rasmi wa nchi hiyo. Na ili kuhakikisha kwamba; sheria za nchi hiyo zinaendana moja kwa moja na dini ya Kiislamu, katika ya nchi hii iliamua kujenga «Baraza la Itikadi za Kiislamu» na kuliingizwa katika katiba ya nchi hiyo. [9] Mnamo tarehe 1 Aprili 1979, baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kushika hatamu za nchi, kufuatia pendekezo la Imam Khomeini na kupitia kura ya maoni, Jamhuri ya Kiislamu ilichaguliwa kuwa ndio mfumo rasmi wa kisiasa nchini Iran. [10] Nchi ya Afghanistan ilioko barani Asia, [11] pamoja na Gambia [12] barani Afrika, pia ziliwahi kuwa na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ulioendesha nchi hizo.

Rejea

Vyanzo