Muharaba

Kutoka wikishia
Makala hii inahusiana na maana ya Muharaba. Ili kujua kuhusiana na ufisadi katika ardhi, angalia makala ya Mufsid fil Ardh.

Muharaba (Kiarabu: المُحارَبَة) ni kutoa silaha kwa ajili ya kuzusha hofu na wasiwasi baina ya watu. Mafakihi wanamtambua mtu ambaye anafanya uporaji na kuleta ukosefu wa amani katika jamii ya Kiislamu kuwa ni Muharib (anayepigana vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake) na wakitegemea Aya ya 33 ya Surat al-Maidah wanaamini kwamba, adhabu ya Muharib ni kuuawa, kusubiwa, kukatwa mikono na miguu kwa mabadilisho (makusudio ya hilo ni mkono wa kulia na mguu wa kushoto) na kubaidishwa (kupelekwa uhamishoni).

Sheikh Saduq, Sheikh Mufid na kundi jingine la wanazuoni wanasema kuwa, Kadhi anaweza kutekeleza adhabu moja kati ya hizi dhidi ya aliyepatikana na hatia hiyo, huku kundi jingine akiwemo Sheikh Tusi na Sahib al-Jawahir wakisema kuwa, hilo linategemea na aina ya uhalifu aliyoufanya Muharib (anayepigana vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake), na hivyo inawezekana kumpatia adhabu moja au adhabu kadhaa kati ya hizo nne.

Katika kubainisha maana ya Muharaba, kumebainishwa tofauti kadhaa baina ya hilo na mafahimu zingine kama vile kufanya ufisadi katika ardhi, uasi dhidi ya Imamu halali na mtawala wa kisheria na uasi wa kiraia; miongoni mwazo ni, Muharib yeye anapigana vita na watu, lakini anayemuasi Imamu na mtawala wa Kiislamu anapigana vita na mtawala. Mafakihi wa Kishia wanaamini kuwa, kama Muharib atatubu kabla ya kukamatwa, toba yake itakubaliwa na hatoadhibiwa, lakini kama kuna haki ya watu kwake, haki hiyo inapaswa kushughulikiwa.

Nafasi na umuhimu

Muharaba katika fikihi ina maana ya kutoa silaha na kuwaelekezea watu kwa nia ya kuwatisha. [1] Kwa mujibu wa fat’wa za mafakihi, kila mtu ambaye anatumia silaha na kuiba waziwazi mali za watu au anawachukua mateka, anatambulika kama Muharib (anayepigana vita na Mwenyezi Mungu na Mtume). [2] Makusudio ya silaha ni kila suhula na wenzo ambao unatumiwa katika mapigano baina ya wanadamu; kama vile upanga, upinde na mshale na silaha za leo. [3]

Adhabu za muharaba, na adhabu kama za kuritadi, zinaa na kunywa pombe ni miongoni mwa adhabu zisizo za kimali; yaani kuna adhabu maalumu ambazo zimeainishwa katika sheria za Kiislamu. [4] Pamoja na hayo, Muharaba ina tofauti na adhabu nyingine kwa kuwa Muharaba imeainishiwa adhabu nne ambapo inawezekana kutekeleza adhabu moja au kadhaa. [5]

Muharaba ni nini?

Katika vitabu vya fikihi kuna maudhui zilizojadiliwa kuhusiana na mazingira ya kuthibiti Muharaba (kupigana vita na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake). [6] Mafakihi wa Kishia na Kisuni wanaamini kwamba, Muharaba haithibiti bila ya kutoa silaha. [7] Akthari ya mafakihi wa Kishia wanaamini kwamba, kuwa na lengo la kutisha ni miongoni mwa masharti ya kuthibiti Muharaba. [8] Sayyid Abdul-Karim Musawi Ardabili, Marjaa Taqlidi wa karne ya 15 Hijiria amenukuu maneno kutoka kwa Shahidi Thani tu na kusema, inaonekana na kufahamika ya kwamba, sharti hili hakukubaliana nalo. [9] Pamoja na hayo, kwa mujibu wa Ardabili, Shahidi Thani katika kitabu chake kingine, ametambua kama ilivyo kwa mafakihi wengine ametambua “nia na kusudio la kutisha” kuwa sharti la kuthibiti Muharaba. [10]

Kuwa fisadi mtu ambaye ametoa silaha, yaani kuwa na historia ya hilo na kuwatisha watu ni miongoni mwa masharti ya hitilafu. [11] Katika uga wa sharti la mwisho mjadala na ni kwamba, ili kuthibiti Muharaba je ni lazima watu waogope au hii hii hatua ya mtu kuwa na ni ya kuogopesha watu inatosha?; hata kama kitendo hicho hakitaisha watu. [12] Shahid al-Awwal, Shahid Thani na Sahib Riyadh wanaamini kwamba, nia na kusudio la kutisha watu inatosha. [13] Kwa upande mwingine, Muhaqqiq Ardabili, Fadhil Isfahani na Imamu Khomeini wanamaini kuwa, kama mtu atatoa silaha kwa nia na kusudio la kutisha watu lakini watu wakawa hawajaogopa, hahesabiwi kuwa ni Muharib. [14]

Kadhalika kama mtu kutokana na uadui aliokuwa nao na mtu au kwa watu akamtolea au akawatolea silaha hahesabiwi kuwa ni Muharib. [15] Imekuja pia katika sheria za adhabu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kwamba, kosa la Muharib linathibiti pale kitendo hiki kinapokuwa na upande jumuishi na mtu awe na uwezo wa kuondoa usalama. [16]

Mifano

Mafakihi wa Kiislamu wamezungumzia mitazamo tofauti kuhusiana na mifano na vielelezo vya Muharib katika Aya ya Muharaba; baadhi wamesema kuwa, makusudio ya Muharib ni kafiri dhimmi (kafiri anayeishi katika nchi ya Kiiislamu na analipa kodi) endapo atavunja ahadi na kukiuka makubaliano na akaingia vitani na Waislamu. Kundi jingine la wanazuoni linasema kuwa, kwa kuzingatia sababu ya kushuka Aya, makusudio yake ni wartadi, (walioritadi) majambazi. [18] Kwa mujibu wa Sheikh Tusi, raia na mtazamo wa mafakihi wa Kishia ni huu: Kila ambaye atatoa silaha ili awatishe watu anahesabiwa kuwa ni Muharib. [19]

Tofauti ya Muharib na Mufsid fil Ardh

Kundi la mafakihi likitumia Aya ya Muharaba linaamini kuwa, Mufsid fil-ardh ni tofauti na Muharib na kundi jingine limetambua anuani mbili hizi (Muharib na mufsid fil ardh) kwamba, ni moja. Imam Khomeini (1902-1989), fakihi wa Kishia na muasisi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran, yeye ametambua kuwa, mufsid fil ardh na Muharib ni kitu kimoja. Kwa mtazamo wake ni kuwa, Muharib ni mtu ambaye anatoa na kujiandalia silaha kwa ajili ya yake ili kutisha watu na kusababisha ufisadi katika ardhi. [20] Muhammad Mu’min Qomi (1938-2019), mmoja wa mafakihi wa Kishia anaamini kuwa, Mufsid fil ardh katika Aya ina maudhui, na kwamba, Muharaba inahesabiwa kuwa moja ya vielelezo na mifano ya kufanya ufisadi katika ardhi. [21] Muhammad Fadhil Lankarani (1931-2007), Marjaa Taqlidi anasema kuwa, kuhusiana na Mufsid fil ardh na Muharib kuna suala la umuum (hali jumla) na khusus mutlaq (maalumu mutlaki); kwa maana kwamba, kila Muharib ni Mufsid fil al-rdh (mwenye kufanya ufisadi katika ardhi), lakini si kila mfanya ufisadi katika ardhi ni Muharib. [22] Nassir Makarem Shirazi (aliyezaliwa 1927), mmoja wa Marajii Taqlid anaamini kwamba, Mufsid fil-ardh na Muharib ni maneno na mafuhumu mbili tofauti. [23]

Tofauti ya Muharaba na Baghy (uasi)

Katika fikihi, Muharaba na Baghy ni masuala mawili tofauti na yana fasilihi na maana tofauti na hukumu za kisheria zinazotofautiana; [25] Muharib anapambana na kupigana vita na watu na Baghi (muasi) anatoa silaha kwa nia ya kupigana na mtawala. [26] Mafakihi wamewjadili hukumu ya Baghy katika mlango wa jihadi ilihali hukumu ya Muharaba imejadiliwa katika mlango wa adhabu (hudud). [27] Nyaraka na hoja za kila moja pia zinatofautiana na kadhalika pia, kuwatisha watu, ufisadi na kuvuruga usalama pia havijatajwa kuwa ni sharti katika Baghy (uasi). [28]

Tofauti ya Muharaba na uasi wa kiraia

Sayyid Javad Warai’ mtafiti wa fikihi ya kisiasa, anaamini kwamba muqawama wa kiraia na uasi wa kiraia unafanywa kwa lengo la kubadilisha sheria au sera au msimamizi na kadhalika, na madhumuni yake sio kupindua mfumo wa kisiasa au kuleta wahka na wasiwasi baina ya ya watu. Kwa hiyo, uasi wa kiraia hauwezi kuchukuliwa kuwa Muharab au Baghy (kuanzisha uasi wa kupigana na mtawala) na haipaswi kumtetea Muharib kwa jina la uasi wa kiraia. [29]

Adhabu ya Muharib

Mafakihi wakitegemea Aya ya 33 ya Surat al-Maidah wamefikia kauli moja , adhabu ya Muharaba ni kuuawa, kusulubiwa, [30], kukatwa mikono na miguu kwa mabadilisho (makusudio ya hilo ni mkono wa kulia na mguu wa kushoto) na kubaidishwa (kupelekwa uhamishoni), [31], hata hivyo wametofautiana kuhusiana na namna ya kutekelezwa adhabu. [32] Sayyid Abdul-Karim Musawi Ardabili ameandika kuwa, baina ya mafakihi wa Ahlu-Sunna pia kuna tofauti hii ya kimtazamo. [33]

Nadharia ya hiari

Sheikh Saduq, Sheikh Mufid, Allama Hilli, Shahid al-Awwal, Shahid Thani na Imam Khomeini, wanaamini kwamba, ni hiari kutekeleza adhabu dhidi ya muharib na wanaamini kwamba, Kadhi anaweza kuchagua moja kati ya adhabu hizo nne kwa ajili ya kumuadhibu muharib. [34]

Nadharia ya utaratibu

Kwa mujibu wa Musawi Ardabili, fat’wa ya kundi jingine la Maulamaa kama Sheikh Tusi, Ibn Zuhra, Ibn Barraj, Abu Salah al-Halabi, Sahib Riyadh, Sahib Jawahir na Sayyid Abul-Qassim Khui, ni kwamba, kuamuadhibu muharib ni kwa mtindo wa utaratibu, mfuatanisho na kulingana na kosa alilofanya. Kwa maana kwamba, inategemea aina ya kosa ambapo huenda akaadhibiwa kwa adhabu moja miongoni mwa adhabu hizo au adhabu kadhaa zilizotajwa katika Aya. [35] Khui anafafanua adhabu kwa nadharia ya utaratibu kwa kusema: Mtu ambaye anatoa silaha na kuwatisha tu watu, adhabu yake ni kubaidisha (kupelekwa uhamishoni); mtu ambaye mbali na kutoa silaha atamdhuru mtu au watu, kwanza ataadhibiwa kwa adhabu ya kisasi na kisha atapelekwa uhamishoni. Yule ambaye anatoa silaha na kuiba mali za watu, atakatwa mkono na mguu; mtu ambaye anatoa silaha na kisha kumuua mtu au watu kadhaa lakini haibi na kuchukua mali zao, adhabu yake ni kuuawa. Mtu ambaye mbali na kuuawa, anaiba pia mali, awali anakatwa mkono wake wa kulia na kisha anakabidhiwa kwa familia ya muuliwa ili wachukue mali zao na kisha wamuue. Kama familia ya muuliwa watamsamehe, mtawala anapaswa kuchukua jukumu la kumuua. [36]

Katika sheria za adhabu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, adhabu ya Muharib ni moja kati ya adhabu nne yaani kunyongwa, kusubiwa, kukatwa mkono wa kulia na mguu wa kushoto na kubaidishwa. [37]

Toba ya Muharib

Kwa mujibu wa fat’wa ya mafakihi wa Kishia ni kuwa, kama Muharib atatubu kabla ya kukamatwa, toba yake itakubaliwa na hatoadhibiwa, lakini kama katika mabega yake kuna haki ya watu, haki hiyo inapaswa kushughulikiwa; yaani kwa mfano kama ameua mtu au amemdhuru na kumjeruhi mtu au ameiba mali, endapo wahusika hawatomsamehe atafanyiwa kisasi, kulipa dia au kufidia hasara, lakini kama mtu atatubu baada ya kukamatwa hatafutiwa adhabu. [38] Mafakihi wa Kishia wana kauli moja katika mas’ala hii. [39]

Mtazamo huu umechukuliwa kutoka katika Aya inayofuata baada ya Aya ya Muharaba ambayo inasema: ((إِلَّا الَّذِینَ تٰابُوا مِنْ قَبْلِ أَنْ تَقْدِرُوا عَلَیهِمْ ; Isipokuwa wale walio tubu kabla hamjawatia nguvuni)). [40]Kwa mujibu wa Aya hiyo, mtu ambaye ametubu kabla ya kutiwa mbaroni, ameondolewa katika adhabu. [41] Kuna hadithi pia ambazo zinaunga mkono nadharia na mtazamo huu. Miongoni mwazo ni hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s): Ikiwa Muharib atatubu kabla ya kukamatwa na mtawala, hatoadhibiwa. [42]

Aya ya Muharaba

Mkala asili: Aya ya Muharaba

Hoja kuu ya mafakihi kuhusiana na hukumu ya Muharaba ni Aya ya 33 katika Surat al-Maidah. Aya hiyo inasema:

إِنَّمَا جَزَاءُ الَّذِینَ یحَارِبُونَ اللهَ وَرَسُولَهُ وَیسْعَوْنَ فِی الْأَرْضِ فَسَادًا أَن یُقَتَّلُوا أَوْ یُصَلَّبُوا أَوْ تُقَطَّعَ أَیدِیهِمْ وَأَرْجُلُهُم مِّنْ خِلَافٍ أَوْ یُنفَوْا مِنَ الْأَرْضِ

Basi malipo ya wale wanao mpiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakawania kufanya uchafuzi katika nchi, ni kuuawa, au kusalibiwa, au kukatwa mikono yao na miguu yao kwa mabadilisho, au kutolewa nchi.
(Quran: 5: 33)[44]

Kwa mujibu wa kile kilichokuja katika Tafsiri ya Nemooneh ni kwamba: Sababu ya kushuka Aya hii ni kisa cha kusilimu kundi la washirikina ambao kutokana na kuwa hali ya hewa ya Madina haikuwa mwafaka na nzuri kwao kwa amri ya Mtume (s.a.w.w) wakahamia katika eneo lenye hali ya hewa nzuri. Kwa kuzingatia kuwa, eneo hilo lilikuwa sehemu ya malisho ya ngamia. Siku moja watu hawa, waliwaua Waislamu na kuiba ngamia zao. Aya hii ilishuka ikizungumzia na kubainisha adhabu zao. [45]

Katika vitabu vya Fiqhi, Aya hii inazungumziwa na kujadiliwa katika uga wa aina ya adhabu za Muharib na vilevile na vielelezo vyake. [46]

Masuala yanayo fungamana