Aya ya Muharaba

Kutoka wikishia
Makala hii inahusiana na Aya ya Muharaba. Ili kujua kuhusiana na mafuhumu ya Muharaba angalia makala ya Muharaba.
Aya ya Muharaba

Aya ya Muharaba (Kiarabu: آية المحاربة) (al-Maida: 33) inazungumzia malipo ya wale wanaompiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake (.a.w.w). Akthari ya wafasiri wa Qur'ani wanaamini kuwa, Aya hii ilishuka kuhusiana na kundi la Waislamu wapya ambalo liliwaua Waislamu na kuiba ngamia zao na Mtume akwaadhibu kwa mujibu wa Aya hii.

Aya hii inatumiwa kama msingi wa kunyambua hukumu za Muharaba (vita) katika fikihi. Mafakihi wanasema, mtu ambaye anatumia silaha na kuiba waziwazi mali za watu au anawachukua mateka, anatambulika kama Muharib (anayepigana vita na Mwenyezi Mungu na Mtume) na wakitegemea Aya hii wanaamiini kwamba, adhabu dhidi ya Muharib ni: Kuuawa, kusulubiwa (kufungwa katika kitu kinachoshabihiana na msalaba), kukatwa mikono na miguu mbalimbali (kukatwa mkono wa kulia na mguu wa kushoto) na kubaidishwa. Hata hivyo, kundi miongoni mwa linaamiini kwamba, Kadhi anaweza kutekeleza adhabu moja kati ya hizi dhidi ya aliyepatikana na hatia hiyo, huku kundi jingine likisema kuwa, hilo linategemea na aina ya uhalifu aliyoufanya Muharib (anayepigana vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake), na hivyo inawezekana kumpatia adhabu moja au adhabu kadhaa kati ya hizo nne.

Andiko na tarjumi ya Aya

إِنَّمَا جَزَاء الَّذِينَ يُحَارِبُونَ الله وَرَسُولَهُ وَيَسْعَوْنَ فِي الأَرْضِ فَسَادًا أَن يُقَتَّلُواْ أَوْ يُصَلَّبُواْ أَوْ تُقَطَّعَ أَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُم مِّنْ خِلافٍ أَوْ يُنفَوْاْ مِنَ الأَرْضِ ذَلِكَ لَهُمْ خِزْيٌ فِي الدُّنْيَا وَلَهُمْ فِي الآخِرَةِ عَذَابٌ عَظِيمٌ

Basi malipo ya wale wanao mpiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakawania kufanya uchafuzi katika nchi, ni kuuwawa, au kusalibiwa, au kukatwa mikono yao na miguu yao kwa mabadilisho, au kutolewa nchi. Hii ndiyo hizaya yao katika dunia; na katika Akhera watapata adhabu kubwa.
(Quran: 5: 33)

Sababu ya kushuka

Akthari ya wafasiri wa Qur'an tukufu wanaamini kwamba, Aya ya Muharaba ilishuka kuhusiana na kaumu ya Uraynah; [1] washirikina ambao walikwenda Madina na kisha wakasilimu, [2] lakini kutokana na kuwa hali ya hewa ya Madina haikuendana nao wakaugua na kwa agizo la Mtume wakatumia maziwa ya ngamia na wakapona. Lakini baada ya kupona wakaritadi na baada ya kuua idadi kadhaa ya Waislamu, waliiba ngamia na kukimbia kutoka Madina. [3] Kwa mujibu wa Allama Tabatabai, Imam Ali (a.s) aliwatia mbaroni kwa amri ya Mtume na kuwaleta mbele yake [4] na ni wakati huo ambapo Aya ya Muharaba iliposhuka na Mtume akwaadhibu kwa mujibu wa Aya hii. [5] Baadhi wanaamini kuwa, watu wa kabila la Uraynah waliiba tu na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Mtume aliwakata mikono na miguu kwa mujibu wa Aya hii. [6] Kisa cha watu wa Uraynah kimekuja pia katika kitabu cha Kafi ambapo kinasimuliwa kwa kunukuliwa Imam Swadiq (a.s). [7]

Kuhusiana na Aya ya Muharaba kumebainishwa sababu nyingine ya kushuka kwake; [8] kwa mujibu wa Fakhrurazi ni kwamba, Aya hii ilishuka kuhusiana na kaumu ya Bani Israil kwa sababu walichupa mipaka katika kuwaua mafisadi. [9] Wafasiri wengine wameelezea uwezekano wa sababu nyingine ya kushuka Aya hii kwa kundi fulani la watu ambao: Majambazi, wezi wa misafara ya Hijja na wafanyaziara, washirikina na wavunja makubaliano (mikataba) [10] Kwa mujibu wa nukuu ya Allama Tabatabai ni kwamba, hadithii zinazozungumzia sababu ya kushuka Aya hii zinapatikana katika vitabu sita sahihi vya Sunni venye itibari ingawa kwa tofauti ndogo. [11]

Tafsiri

Aya ya 33 ya Surat al-Maidah imeondokea kuwa mashuhuri kwa Aya ya Muharaba [12] na wafasiri wanaamini kwamba, mtu ambaye anafanya uporaji na kuleta ukosefu wa amani katika jamii ya Kiiislamu anahesabiwa kuwa ni Muharib (anayepigana vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake); [13] hii ni kutokana na kuwa, mtu wa namna hiyo kimsingi ametangaza vita na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. [14] Katika Aya hii, Muharib anaadhibiwa kwa moja kati ya adhabu nne: [15]

  1. Kuuawa, ni adhabu ya Muharib ambaye ameua mtu. [16] Fadhil Miqdad, fakihi na mfasiri wa Qur'ani wa Kishia wa karne ya 9 Hijiria anaamini kwamba, kwa kutoa msamaha walii wa damu (mwenye haki ya kisheria ya ndugu yake aliyeuawa ya kutaka kisasi au kusamehe na kuchukua dia), hukumu ya kuuawa kwake haindoki, kwani mtu ambaye ni Muharib na aliyetenda kosa hili la mauaji lazima auawe. [17]
  2. Kusulubiwa, hii ni hukumu ya Muharib ambaye mbali na kuua ameibiwa pia. [18] Fadhl bin Hassan Tabarsi, fakihi na mfasiri wa Kishia wa karne ya 6 Hijiria anaamini kwamba, ambaye ni wajibu kusulubiwa, anauawa kabla ya kusulubiwa na kisha anatundikwa katika kitu kama msalaba kwa muda wa siku tatu. [19] Kwa mujibu wa ripoti ya kitabu cha Kashf al-Asrar, Muharib atatundikwa katika kitu kama msalaba siku tatu kabla ya kuuawa kwake au siku tatu baada ya kuuawa kwake, na mwenye kuamua hilo ni Imam. [20]
  3. Kukatwa mikono na miguu: Hii ni adhabu na malipo ya Muhariub ambaye amefanya kosa la kuiba tu. [21] Imam Swadiq (a.s) anasema kuwa, makusudio ya hilo ni mkono wa kulia na mguu wa kushoto. [22] Fauka ya hayo, baadhi ya wengine wamesema, makusudio ya kukatwa mkono na mguu ni kukatwa vidole vinne vya mkono au mguu. [23] Adhabu ya kukatwa mkono na mguu, hutekelezwa pale mali iliyoibiwa inapofikia kiwango hitajika (kiwango cha kisheria). [24]
  4. Kubaidishwa au Kufungwa jela: Hii ni adhabu ya mtu ambaye ameleta hofu na ukosefu wa amani baina ya watu. [25] Kundi miongoni ma wafasiri linaaminii kuwa, makusudio ya: أَوْ يُنفَوْا مِنَ الأَرْضِ (au kuhamishwa katika nchi yake), ni kumhamisha na kumpeleka uhamishoni Muharib katika mji mwingine huku wengine wakisema kuwa, makusudio hapo ni kumfunga gerezani. [26] Kadhalika imeelezwa kwamba, kuna ulazima wa kuzuia Muharib kwenda katika miji ambayo ndani yake wanaishi washirikina. [27]

Katika kitabu cha Kanzul-Irfan, kilichoancdikwa na Fadhil Miqdad, amenukuliwa Imam Shafi, muasisi wa moja ya madhehebu nne za Waislamu wa Kisuni akisema: Haipaswi kuwa na uhusiano wa aina yoyote na Muharib aliyebaidishwa na kupelekwa uhamishoni kama vile kuuza na kununua, kumsaidia na kuwa na maingiliano naye. Haipaswi kabisa kuamiliana na mtu huyo. [28]

Wafasiri wa Kiislamu wanaamini kuwa, adhabu zilizotajwa zimeanishwa kulingana na uzito wa kosa la Muharib; [29] kama ilivyonukuliiwa kutoka kwa Imam Baqir (a.s) na Imam Swadiq (a.s). [30] Baadhi pia wameliacha mikononi mwa mtawala [31] au Imam [32] suala la kuainisha namna ya kumuadhibu Muharib. Kwa mujibu wa Aya ya Muharaba, adhabu hizi ni za hapa duniani na hazijumuishi adhabu dhidi ya Muharib huko akhera. [33]

Toba

Wafasiri wa Qur'an wanaamini kwamba, kama Muharib atatubu kabla ya kukamatwa, toba yake itakubaliwa na hatoadhibiwa. [34] Kwa mujibu wa ripoti ya al-Suyuti, mpokezi wa hadithi wa karne ya 10 Hijiria ni kwamba, Harith bin Badr alitoa upanga mbele ya watu huko Misri, lakini akatubu na baadhi ya watu wakamchukua na kumpeleka kwa Imam Ali (a.s). Baada ya Imam Ali (a.s) kupata uhakika juu ya majuto yake kwa kitendo alichofanya, Imam alikubali toba yake na akampa barua ya amani. [35] Hata hivyo endapo Muharib atatubu, kosa lake la kuvuruga tu amani ya umma ndilo litakalofumbiwa macho, lakini kama aliiba au aliua, ataadhibiwa adhabu inayolingana na kosa lake hilo. [36] Kadhalika kama atatubu baada ya kukamatwa, hatafutiwa adhabu yake. [37]

Matumizi ya Kifiq'h

Makala asili: Muharaba

Katika vitabu vya fikihi, kumebainiisha hukumu za kisheria kwa kuzingatia Aya ya Muharaba. Kwa mujibu wa Fat’wa za mafaqihi, kila ambaye atatumia nguvu waziwazi na akachukua na kupora mali ya mwingine au akachukua mateka watu, anasabiwa kuwa ni Muharib (anayepigana vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake). [38] Ili kuthibitika kitendo cha Muharaba kumebainishwa masharti mbalimbali kama vile kutoa silaha, kuzusha hofu na woga miongoni mwa watu na kuwa fisadi mtu ambaye ni muharib. [39]

Kundi miongoni mwa mafakihi limeainiisha mifano na vielelezo vya mtu kuwa muharib. Miongoni mwayo ni: Kafiri dhimmi (kafiri anayeishi katika nchi ya Kiiislamu na analipa kodi), wartadi (walioritadi) majambazi na kila ambaye atazusha wasiwasi na woga baina ya Waislamu. [40] Kadhalika baadhi ya mafakihi wanasema, makusudio ya muharaba ni kupigana vita na Waislamu. [41]

Hiari au kwa utaratibu

Kwa mujibu wa Aya ya Muharaba, kumeainishwa adhabu nne kwa ajili ya muharib; [42] lakini mafakihi wana mitazamo tofauti kuhusiana na namna ya kumuadhibu Muharib; [43] Sheikh Swaduq, [44] Sheikh Mufid, [45] Allama Hilli, [46] na Imam Khomeini, wanaamini kwamba, ni hiari kutekeleza adhabu dhidi ya muharib na wanaamini kwamba, Kadhi anaweza kuchagua moja kati ya adhabu hizo nne kwa ajili ya kumuadhibu muharib. Mkabala na wao kuna Sheikh Tusi, Muhammad Hassan Najafi, Swahib Riyadh na Sayyid Abul-Qassim Khui wao wanaamini kwamba, kuamuadhibu muharib ni kwa mtindo wa utaratibu, mfuatanisho na kulingana na kosa alilofanya. [48]

Vyanzo

  • Abū l-Futūḥ al-Rāzī, Ḥusayn b. ʿAlī. Rawḍ al-Jinān wa Rawḥ al-Janān fī Tafsīr al-Qurʾān. Edited by Yāḥiqī wa Naṣiḥ . Mashhad: Āstān-i Quds-i Raḍawī, 1375 Sh.
  • Fāḍil Miqdād, Miqdād b. ʿAbd Allāh al-. Kanz al-ʿirfān fī fiqh al-Qurʾān. Tehran: Nashr-i Murtaḍawī, 1373 SH.
  • Fakhr al-Rāzī, Muḥammad b. al-ʿUmar al-. Mafātīḥ al-ghayb (al-Tafsīr al-Kabīr). Third edition. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1420 AH.
  • Ḥillī, Jaʿfar b. al-Ḥasan al-. Mukhtalaf al-Shīʿa fī aḥkām al-sharīʿa. Qom: Jāmiʿat al-Mudarrisīn, 1413 AH.
  • Ḥillī, Jaʿfar b. al-Ḥasan al-. Sharāʾiʿ al-Islām fī masāʾil al-ḥalāl wa l-ḥarām. Edited by Muḥammad ʿAlī Baqqāl. Second edition. Qom: Muʾassisa-yi Ismāʿīlīyān, 1408 AH.
  • Khomeini, Sayyid Rūḥ Allāh. Taḥrīr al-wasīla. Qom: Muʾassisat Maṭbūʿāt Dar al-ʿIlm, [n.d].
  • Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī & Muḥammad Ākhūndī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Tafsīr-i nimūna. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmiyya, 1371 Sh.
  • Maybudī, Aḥmad b. Muḥammad. Kashf al-asrār wa 'uddat al-abrār. Tehran: Amīr Kabīr, 1371 Sh.
  • Mishkinī, ʿAlī. Muṣṭalaḥāt al-fiqh. First edition. Beirut: Manshūrāt al-Riḍā, 1431 AH.
  • Mufīd, Muḥammad b. Muḥammad al-. Al-Muqniʿa. Qom: Kungira-yi Jahānī-yi Hizāra-yi Shaykh Mufīd, 1413 AH.
  • Mūsawī Ardabīlī, ʿAbd al-Karīm. fiqh al-ḥudūd wa l-taʿzīrāt. Scond edition. Qom: Muʾassisat al-Nashr li Jāmiʿa l-Mufīd raḥimah-u Allah, 1427 AH.
  • Shahīd al-Thānī, Zayn al-Dīn b. ʿAlī. Al-Rawḍa al-bahiyya fī sharḥ al-lumʿat al-Dimashqiyya. Edited by Muḥammad Kalāntar. Qom: Maktabat al-Dāwarī, 1410 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Al-Muqniʿ fī al-fiqh. Qom: Muʾassisa al-Imām al-Hādī, 1415 AH.
  • Ṣāliḥī Najafābādī, Niʿmat Allāh. "Tafsīr-i āya-yi muḥāraba wa aḥkām-i fiqhī-yi ān." majalla nāma-yi mufīd 9 (1376 sh).
  • Sayyid Quṭb, Muḥammad. Fī ẓilāl al-Qurʾān. Beirut: Dār al-Shurūq, 1408 AH.
  • Suyūṭī, ʿAbd al-Raḥmān b. Abī Bakr al-. Al-Durr al-manthūr fī tafsīr al-maʾthūr. Qom: Kitābkhāna-yi Āyatollāh Marʿashī al-Najafī, 1404 AH.
  • Ṭabāṭabāʾī, Mūhammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, 1390 AH.
  • Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Majmaʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Edited by Muḥammad Jawād Balāghī. 3rd edition. Tehran: Intishārāt-i Nāṣir Khusraw, 1372 Sh.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Mabsūṭ fī fiqh al-imāmīyya. Qom: al-Maktabat al-Raḍawīyya li Iḥyāʾ al-Āthār al-Jaʿfarīyya, 1387 AH.