Kuto Potosheka kwa Qur’ani Tukufu
Kuto Potosheka kwa Qur’ani Tukufu (Kiarabu: سلامة القرآن من التحريف) ndio imani inayo shikiliwa na Waislamu walio wengi wa madhehebu mbali mbali ya Kiislamu ulimwenguni. Waislamu wanaamini kwamba; Qur’ani ilioko mikononi mwao ndio Qur’ani ile ile aliyo teremshiwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), ambayo haina kasoro ndani yake.
Waislamu wote wanakubaliana kwamba hakuna kitu kilicho ongezwa wala kupunguza kutoka kwenye Qurani iliyopo mikononi mwao. Hata hivyo, kuna tofauti za maoni kuhusiana na uwepo wa mapungufu ndani yake. Baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu wachache wanaamini kwamba Qurani ina mapungufu ndani yake. Ushahidi wa wanazuoni hao umeegemea kwenye baadhi ya Riwaya zilizomo ndani vyanzo vya Hadithi za Sunni pamoja na Shia. Hata hivyo, baadhi ya Mawahabi wamewashutumu Mashia juu ya kushikamana na imani ya upotoshwaji wa Qurani.
Mtazamo maarufu kati ya wanazuoni wa Kishia ni kwamba; hakuna upotoshaji wowote unaohusiana na ziada au upungufu katika Qur’ani, na kwamba Qur’ani iliyopo mikononi mwa Waislamu ndio ile ile aliyo teremshiwa Mtume Muhammad (s.a.w.w). Ili kuthibitisha imani zao juu ya suala hili, wanauoni hawa wamekuwa wakitumia Aya za Qur’ani pamoja na Hadithi za bwana Mtume (s.a.w.w), ikiwemo Hadithi ya Thaqalaini pamoja na Riwaya nyingine zilizosimuliwa na Maimamu wa Kishia (a.s). Pia wao wametumia hoja kadhaa za kiakili (kimantiki) katika kuthibitisha kwamba; Qur’ani haikutiwa mkono wala hakuna kilicho badilishwa ndani yake. Wanazuoni wa Kishia wamechunguza Riwaya zote kutoka vyanzo vya Sunni na Shia zinazo onesha au kuashiria kuwepo kwa mapungufu ndani ya Qur’ani. Wao wamefanya uchunguzi kamili juu uhalali wa nyaraka za mapokezi ya Hadithi hizo pamoja na aina za ushahidi wake. Uchunguzi huu wa wanazuoni wa Kisha umehitimika na kuifikia imani isemayo kwamba; Haiwezekani kabisa kutegemea Riwaya hizo katika kuthibitisha uwepo wa aina yoyote ile ya mapungufu ndani ya Qur’ani Tukufu.
Kuna kazi kadhaa za kimaandishi kutoka kwa wafasiri, mafaqihi na wahakiki wa Qur’ani wa Kishia, zilizo andikwa juu ya kukataa uwezekano wa kupotosheka kwa Qur’an Tukufu. Miongoni mwa vitabu vilivyo andikwa kupingana na nadharia ya uwezekano wa kupotosheka kwa Qur’ani ni; Burhan Rashin, Al-Burhan ‘Ala Adami Tahrifi Al-Qurani, kilichoandikwa na Mirza Mahdi Burujurdi, pamoja na kitabu kiitwacho Siyaanatu Al-Qur’ani Mina Al-Tahrifi, kilichoandikwa na Muhammad Hadi Ma’arifat.
Maana ya Kupotosha na Aina Zake
Neno kupotosha linamaanisha ya kitendo cha kubadilisha na kugeuza maneno kutoka hali yake ya awali na kuyaweka katika hali nyengine. [1] Kuna aina mbalimbali za upotoshaji zilizo elezwa na watafiti mbali mbali, [2] ikiwa ni pamoja na:
Upotoshaji wa Kimaneno
Kuna aina tofauti za upotoshaji wa kimaneno, muhimu zaidi ya aina za upotoshaji huu ni kama ifwatavyo: [3]
- Upotoshaji wa kuongeza au kuzidisha kitu ndani yake: Ikiwa tutakubalina na itikadi hii kuhusiana na Qur'an, hii itamaanisha kwamba; kuna sehemu fulani ya ziada ndani ya Qur'an ilioko mikononi mwa Waislamu, na kwamba Qur’ani hii sio ile aliyo eremshiwa bwana Mtume (s.a.w.w). [4]
- Upotoshaji wa kupunguza na kuleta mapungufu: Itikati hii ina maana kwamba Qur'an ilioko mikononi mwa Waislamu haijumuishi yale yote yaliyoteremshwa kwa Mtume (s.a.w.w). [5]
Upotoshaji wa Maana
Kusudio la upotoshaji wa maana au maudhui ni kwamba; mpotoshaji anageuza maana ya maneno kuelekea kwenye kile anachokipendelea yeye mwenyewe na kuachana na maana lengwa iliokusudiwa na msemaji wa maneno husika. [6] Kwa lugha nyengine ni kwamba; aina ya upotoshaji huwa ni mwelekeo wa kufasiri na kuabiri kwa kutumia tafsiri ya maneno kinyume na maana inayojitokeza kwenye asili ya maneno husika. [7]
Maana Mengine za Upotoshaji
Kutokuweka sura za Qur'ani kwa mpangilio asili kama ilivyo shuka hapo awali, kubadilisha neno na kuweka neno mbadala lenye maana sawa (upotoshaji wa kubadilisha neno na kutumia visawe), na kusoma maneno ya Qur'an kinyume na usomaji unaokubalika (upotoshaji wa kiusomaji), ni aina nyingine za upotoshaji zilizotajwa na watafiti mbali mbali. [8]
Mtazamo wa Waislamu kuhusu Upotoshwaji wa Qur'ani
Sayyid Abul-Qasim Khui (aliyefariki mwaka 1371 Shamsia), ameeleza akisema; kulingana na misingi mikuu ya dini ya Kiislamu, na kulingana na makubaliano ya Waislamu wote ulimwenguni, ni kwamba; hakuna upotoshaji uliotokea katika kuongeza kitu ndani ya Qur’ani. Yaani kwa mujibu wa maelezo yake, hakukutokea mtu aliyeweka nyongeza ya maneno katika Qur'an. [9] Ila kuna tofauti ya maoni miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu kuhusiana na upotoshaji wa kupunguza, yaani kuondoa baadhi ya maneno na Aya fulani kutoka katika Qur'an. Wanazuoni wengi wa Kiislamu wanaamini kuwa aina hii ya upotoshaji pia haikutokea ndani ya kitabu cha Qur'an. Kwa upande mwingine, wachache wanaamini kuwa kuna aina hii ya upotoshaji uliotokea ndani ya Qur’ani. [10]
Kuhusu upotoshaji wa maana ya Qur'an, Sayyid Abul-Qasim Khui ameandika katika kitabu cha Al-Bayan fi Tafsir al-Qur'an ya kwamba; hakuna khitilafu miongoni mwa Waislamu kwamba aina hii ya upotoshaji ilitokea katika zama tofauti, na kwamba baadhi ya madhehebu potovu yalibadilisha maana ya Aya za Qur'an kwa mujibu wa mitazamo na mawazo yao wenyewe. [11] Katika lugha ya kisharia, aina hii ya upotoshaji inajulikana kama ni tafsiri kwa maoni binafsi, tafsiri ambayo imekemewa na kukatazwa. [12]
Kwa mujibu wa baadhi ya watafiti wa Qur'ani, hata aina nyingine mbili tuizozitaja hapo mwanzo, nazo haijawahi kutokea. Yaani upotoshaji wa kubadilisha neno na kuweka kisawe cha neno lenye maana sawa, au usomaji wa maneno ya Qur'an kinyume na usomaji unaokubalika pia hazikuwahi kutokea ndani ya Qur'an. [13]
Imani ya Shia kuhusu Upotoshwaji wa Qur'ani
Mtazamo maarufu miongoni mwa wanazuoni wa Shia ni kwamba sio tu upotoshaji wa kuongeza; bali hata upotoshaji kwa kupunguza na kuleta kasoro haukuwahi kutokea ndani ya Qur'an, na Qur'ani inayotumiwa na Waislamu wa hivi sasa ndio ile ile iliyoteremshwa na Mwenye Ezi Mungu kwa Mtume (s.a.w.w). Sheikh Saduq katika kitabu Al-I'tiqadaat ameandika akisema kuwa: Imani ya Shia ni kwamba Qur'an iliyoteremshwa kwa bwana Mtume (s.a.w.w) ndio Qur'ani ile ile iliyoko mikononi mwa waislamu, na hakuna Qur’ani nyengine zaidi ya hiyo, na wale wasemao kwamba; Mashia wanaamini kuwa Qur'ani iliyoteremshwa ni kubwa zaidi ya hii Qur'ani iliyopo hivi sasa, ni wenye kuwadanganya watu tu. [15]
Sheikh Tusi katika utangulizi wa Tafsiri ya Al-Tibyan amesema kwamba; Habari sahihi zitokazo kwenye madhehebu sahihi ya Shia Imamiyyah, ni kwamba; hakuna upungufu uliopatikana kutokea ndani ya Qur'ani hii tukufu, na zile Hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mashia na Masunni kuhusiana na upungufu wa Qur'ani, ni hadithi ahadi (zenye mapokezi dhaifu) ambazo hazifidishi elimu tosha kuhusiana na suala hili, na ni bora zaidi kuzipuuza na kuto zijali. [16]
Pia, Muhammad Jawad Balaghi (aliyefariki mwaka 1352 Hijiria) katika kitabu Ala' al-Rahman amemnukuu Muhaqqiq Karaki akisema: Kwa kuwa Hadithi zirejelewazo na wale wanaodai kuwepo kwa mapungufu ndani ya Qur'an, ni Hadithi ziendazo kinyume na hoja za Qur'an, Sunna Mutawatir pamoja na Ijmaa, yabidi kufasiriwa kwa maana nyengine kabisa, na kama hauitowezekana kuzifasiri, basi zinapaswa kuachwa na kuto zijali. [17]
Kashif al-Ghita (aliyefariki mwaka 1228 Hijiria) ni miongoni mwa wanazuoni na mafaqihi wa Kishia aliye kuwa, akipinga na nadharia ya upotoshwaji kwa njia ya kupunguzwa kitu fulani kutoka katika Qur'ani. Akielezea mtazamo wake amesema: Kuna Aya za wazi ndani ya Qur'ani, na makubaliano ya wanazuoni wa kila zama yanashuhudia kuwa hakuna upungufu uliotokea katika Qur'ani, na yale maoni ya wachache wenye madai kama hayo hayana uzito wowote katika jamii ya waislamu. Na dalili hizi wazi na dhahiri wake, unapingana na nadharia ya kuwepo kwa upotoshwaji ndani ya Qur'ani, jambo ambalo ni lenye kuzipiku Hadithi hizo ziashiriazo kuwepo kwa upotoshwaji wa Qur’ani. [18]
Kuhusishwa kwa Shia Juu ya Imani ya Upotoshwaji wa Qur'ani
Tabarsi katika kitabu Majma'u al-Bayan (aliyefariki mwaka 548 Hijiria) anaesema kwamba; Baadhi ya Mashia na kundi la Hashawiyya (madhehebu ya Ahlu-Sunna wanaoshikilia tafsiri dhahiri ya Hadithi) wamekunuu baadhi ya Hadithi ambazo kwa mujibu wake, yaonesha kwamba Qur’ani ina mapungufu ndani yake. [19] Kiuhalisia wale wanaodai kuwepo kwa upotoshwaji na mapungufu ndani Aya za Qur'ani, wanarejelea Hadithi zilizopo katika vyanzo vya Hadithi za Shia [20] na Sunni. [21] Kwa hiyo siyo kuwa upande mmoja tu ndiwo wenye aina kama hiyo ya Hadithi ndani ya vyanzo vyao vya Hadithi. Inasemekana kwamba; kuna wachache miongoni mwa Akhbaariyyuun, [23] wakitegemea Hadithi hizo, wanadai kuwa kuna mapungufu a katika Qur'an, na Qur'an iliyoko mikononi mwa Waislamu wa hivi sasa si yenye kujumuisha idadi nzima ya ile Qur’ani yaliyoteremshwa katika zama za bwana Mtume (s.a.w.w). [24] Jambo hili limefanya baadhi ya Mawahabi kudai kwamba Mashia wote wanaamini kuwepo kwa aina fulani ya upotoshwaji ndani ya Qur'ani. [25]
Tuhuma hizi ziliongezeka hasa baada ya kuchapishwa kwa kitabu kiitwacho Faslu al-Khitabi kilichoandikwa na Mirza Hussein Nuri mnamo mwaka 1292 Hijiria, [26] na hadi leo (karne ya kumi na tano Hijria) kitabu hicho kimekuwa ni miongoni mwa vyanzo vinavyotumiwa katika kuwahusisha Mashia na imani ya upotoshwaji wa Qur'ani. [27] Kwa mfano, Ehsan Elahi Dhahir, mwandishi wa Kiwahabi kutoka Pakistan, katika kitabu chake kiitwacho Al-Shia wa al-Qur'ani, baada ya kurejelea kitabu Faslu al-Khitabi, ameuhusisha mtazamo wa mwandishi huyo na Mashia wote. Ehsan Elahi Dhahir pia amewahusisha Mashia na imani ya kuwepo ongezeko ndani ya Qur’ani, katika tuhuma hizi ameandiaka a akisema kwamba; Mirza Hussein Nuri hayuko peke yake katika imani ya upotoshwaji wa Qur'an, bali yeye ameifunua imani ambayo wanazuoni wengine wa Kishia wanajaribu kuificha kwa sababu ya taqiyya (kuto dhihirisha imani ilioko nyoyoni). [28]
Majibu Kutoka kwa Wanazuoni wa Shia
Kulingana na maelezo ya Mirza Mahdi Borujerdi (aliyefariki mwaka 1347 Samsia), mwanachuoni wa Shia na mmoja wa wanafunzi wa Sheikh Abdul Karim Ha'iri Yazdi katika kitabu Burhane Roushan; ambacho kwa Kiarabu chajulikana kwa jina la Al-Burhan 'ala Adam Tahrif al-Qur'an, ameandika akisema kwamba; Hadithi nyingi za upotoshwaji wa Qur'ani, ikiwa ni pamoja na Hadithi 188 ambazo zimetajwa katika kitabu cha Faslu al-Khitab cha Mirza Husayn Nuri, zimenukuliwa kutoka kwenye kitabu cha Ahmad bin Muhammad Siyari. [29] Abu al-Qasim Khui amesema kuwa wanazuoni wa elimu ya utafiti wa wapokezi wa (ilmu al-rijal), wamemtambulisha Siyari kama ni mwongo na wote wanakubaliana kuhusu upotovu wa imani yake. [30]
Kulingana na maelezo ya Allamah Tehrani (aliyefariki mwaka 1389 Hijiria) katika kitabu chake al-Dhari'ah, ni kwamba; kitabu cha Faslu al-Khitabi kilipingwa na wanazuoni wa Kishia tokea mwanzoni mwa uandishi wake, [31] kiasi ya kwamba inasemekana kuwa; Muhammad Hussein Kashif al-Ghita, aliyeishi zama moja na mwandishi wa kitabu hicho, baada ya kusoma kitabu hicho, alitoa fat’wa ya kulaani uchapishaji wa kitabu hicho. [32] Pia kazi nyingi za uandishi amabzo ziliandikwa maalumu kwa ajili ya kupinga nadharia ya mwandishi huyo. [33] Wengine waliandika vitabu vyao kuhusiana na mada hiyo tu, huku wengine kama vile; wanatafsiri wa Qur'an, mafaqihi na wahakiki wa mbali mbali wa Kishia wakitenga milango maalumu ndani ya vitabu vyao katika kupingana na mwandishi huyo. [34]
Sayyid Kamal al-Haidari, ametaja majina ya wanazuoni 32, wakiwemo mafaqihi, na wahakiki mashuhuri wa Kishia ndani ya kitabu chake kiitwacho Qur'ani wa Musuuniyyat az Tahrif, ambao wamekataa na kupinga aina yoyote ile ya upotoshwaji au mapungufu ndani ya Qur'an. [35] Pia ndani ya moja ya makala iliyoitwa Ghaliyan wa Fikra al-Tahrif al-Qur'an, kunapatikana aina ya madai kama hayo, ambapo ndani yake kuna idada ya Hadithi zinazohusiana na imani ya upotoshwaji wa Qur'an, huku karibu ya theluthi mbili ya Hadithi hizo zikiwa zimepokewa kupitia Maghulati. [36]
Dalili ya Kutowepo Uwezekano wa Kuipotosha Qur'an
Wale wanaoamini kutokuwepo uwezekano wa kuipotosha Qur'an, ili kuthibitisha hoja zao, wametegemea hoja zifuatazo:
Aya ya Dhikr
Kulingana na nadharia za wafasiri wa Qur’ani, neno Dhikr «ذکر» lililoko katika Aya isemayo: «نَحنُ نَزَّلنا الذِّکْرَ و اِنّا لَهُ لَحافِظونَ ; Kwa hakika Sisi ndio tulio iteremsha Qur’ani na hakika Sisi ndio tutakao ihifadhi». lina maana ya Qur'ani, ambayo Mwenye Ezi Mungu aliiteremsha kwa Mtume (s.a.w.w), na yeye mwenyewe amejitolea kwa ajili ya kuilinda dhidi ya upotoshwaji wa kuongeza au kupunguza kitu ndani yake. [37]
Hadithi
Katika baadhi ya hadithi, kuna maelezo ya wazi kuhusiana na kutowepo upotoshwaji ndani ya Qur'ani. [38] Kwa mfano: Hadithi ya Thaqalaini ni mojawapo ya Hadithi zinazo tumiwa juu ya kuthibitisha usalama wa Qur’ani na kuto pita upotoshwaji ndani yake. [39] Kulingana na Hadithi hii ambayo imenukuliwa kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w), ni kwamba; [40] kuna uwezekano wa wanajamii kushikamana na Qur'an katika kila zama; hali ya kwamba imani ya upotoshwaji wa Qur'an inamaanisha kuto wepo uwezekano wa kushikamana nayo, kwa hiyo ingelikuwa Qur'an imebadilishwa, basi kusingekuwa na haja ya bwana Mtume (s.a.w.w) kuamuru kushikamana na Qur’ani hii. [41] Pia, katika baadhi ya Hadithi, imeelezwa kuwa; moja ya njia za kutofautisha Hadithi za kuaminika na zisizoaminika ni kuzilinganisha na Qur'ani, [42] sasa ikiwa Qur'an imebadilishwa, hakutokuwa na haja ya kuwata watu kuzilinganisha Hadithi hizo na Qur'ani. [43]
Kulingana na maelezo ya Sheikh Saduq katika kitabu Al-I'itiqadat, ni kwamba; Hadithi zilizopokewa kutoka kwa Maimamu Maasumu (a.s.) kuhusiana na fadhila za sura fulani, thawabu za kusoma Qur'an, na thawabu za kusoma kila sura, zinaashiria kutokuwepo kwa upotoshwaji wa Qur'ani tukufu. [44] Pia Hadithi zinazohusiana na thawabu za kukhitimisha Qur'ani, [45] zinaashiria kutowepo kwa upotoshwaji wa Qur'ani. [46]
Hoja za Kiakili (Kimantiki)
Kulingana na maelezo ya Mirza Mahdi Borujerdi, ni kwamba; Mtume (s.a.w.w) alitoa madai matatu baada ya kukabidhiwa utume wake: Dai la kwanza, ni kwamba yeye ametumwa kwa ajili ya watu wa wilimwengu mzima. Dai la pili, ni kwamba kuja kwake kunamaanisha kufutwa kwa sheria zote za awali, na inapaswa kufuata sheria yake yeye tu peke yake. Dai la tatu, ni kwamba; yeye ndiye Mtume wa mwisho, na hakuna mtume au nabii atakayekuja baada yake. [47] Kwa kuzingatia madai hayo, akili inahukumu kwamba Qur'ani ambayo Mwenye Ezi Mungu alimteremshia mjumbe wake wa mwisho kwa ajili ya kuongoza wanadamu hadi Siku ya Kiyama, inapaswa kuwa mbali na aina yoyote ile ya upotoshwaji iwe ya kuongeza au kupunguzwa kndani yake. [48]
Wengine pia wametumia kanuni ya hisani ya Mungu (lutfun Ilaahiyyun), wakisema kwamba kutuma mitume na kuteremsha vitabu kutoka kwa Mwenye Ezi Mungu ni neema kwa ajili ya kufaulu na kupata mafanikio ya kidunia na ya kiroho kwa ajili ya wanadamu. Kwa mujibu wa kanuni hii, kitabu cha Qur'ani ambacho ni kitabu cha mwisho kilichoteremshwa kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu, kinapaswa kuwa mbali na aina yoyote ile ya maongezo au mapungufu, na ikiwa upotoshwaji wa kuongezwa au kupunguzwa utatokea ndani yake, hiyo itakuwa ni kinyume na matakwa ya mWenye Ezi Mungu. [49]
Ushahidi wa Uaminifu wa Shia Kuhusuiana na kuto husika kwao na Imani ya Kupotoshwa kwa Qur’ani Kutoka kwa Wanazuoni wa Kisunni
Baadhi ya wanazuoni wa Kisunni wameeleza wazi kwamba; Mashia hawaamini juu ya kuwepo kwa upotoshwaji wa Quran. [50] Kwa mfano, Abul Hassan al-Ash'ari (aliyefariki mwaka wa 324 Hijria) katika kitabu chake Maqalatu al-Islamiyyin, anasema kwamba: Imani ya kupungua kwa Qurani inahusishwa tu na kikundi kimoja cha Shia, katika maelezo yake amesema kwaba, baadhi ya Mashia wengine wano amini juu ya uongozi wa Maimamu 12 (Imamiyyah) wao wanaamini kwamba Qurani haijaongezwa wala kupunguzwa kitu ndani yake. [51]
Rahmatullah Dehlawi (aliyefariki mwaka wa 1308 Hijria), ambaye ni mwanazuoni wa Kisunni kutoka India, ameandika katika kitabu chake kiitwacho "Idh’haru al-Haqqi», akisema: Kwa mujibu wa maoni ya wanazuoni wengi wa Shia Imamiyyah ni kwamba, Qur’ani imehifadhiwa kutokana na aina yote ya mabadiliko, na ni wachache tu ambao waliozungumzia suala la kuwepo kwa mapungufu ndani yake, na maoni yao yamekataliwa mbele ya makundi mengine ya Mashia. [52]
Muhammad Abdullah Daraaz (aliyefariki mwaka wa 1337 Hijria), ambaye ni mwanazuoni na mfasiri wa kutoka nchi ya Misri, katika kitabu chake kiitwacho «Madhkhal ila al-Quran al-Karim» akielezea maoni ya Sheikh Saduq kuhusiana na kupotoshwa kwa Qur’ani amesema: Imamiyyah wanaamini kuwa Qur’ani iliyoko mikononi mwa Waislamu haijawahi kupata aina yoyote ile ya mabadiliko ndani yake, si mabadiliko ya nyongeza wala mapungufu. [53] Muhammad Muhammad al-Madani (aliyefariki mwaka wa 1388 Hijria), ambaye ni mwanazuoni wa Misri na mwalimu wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar, katika makala iliyochapishwa kwenye jarida la «Risalatu al-Islami», ameandika akisema kuwa; hakuna mtafiti yeyote wa Kishia Imamiyyah au Msunni anayekubali kuwepo kwa upotoshwaji wa Quran. [54]
Bibliografia
«Kitabushenasi Adame Tahrifu Qur’ani»: Ni jina la kitabu chenye kurasa 275 kinachojumuisha ndani yake zaidi ya kazi 500, kuhusiana na mada ya kukanusha imani kuwepo uposhwaji ndani ya Quran. Kitabu hichi kimeandaliwa na Kadhim Ustadi na kikachapishwa mwaka 1392 Hijria Shamsia na Shirika la Hija na Ziara la Iran (Sazimane Hajj wa Ziarat). [55] Baadhi ya kazi muhimu zaidi zilizoandikwa na wanazuoni wa Kishia kuhusiana kuto wepo uwezekano wa kupotoshwa kwa Qur’ani ni kama ifuatavyo:
- Kashfu al-Irtiyaabi ‘an Taharifi al-Kitabi, kilichoandikwa na Sheikh Mahmoud Tehrani: Inasemekana kuwa kazi hii ndio ya kwanza kuandikwa baada ya kuchapishwa kwa kitabu Faslu al-Khitabi, na ndicho kitabu cha kwanzo kukanusha maudhui ya kupotoshwa kwa Qur’ani. [56] Aqa Bozorge Tehrani amesema kuwa; mwandishi wa Faslu al-Khitabi (Mirza Hussein Nuri) alisoma kazi hii kisha akaandika risala kwa lugha ya Kiajemi akikanusha maudhui yake mwanzo (ya kupotoshwa kwa Qur’ani), na akapendekeza ichapishwe pamoja na kitabu chake kiitwacho Faslu al-Khitabi. [57] Katika risala hiyo, aliandika akisema kuwa; Makusudio yake juu ya neno "taharif" alilolitumia kitabuni mwake, halikuwa na maana ya kwamba kuna kitu kilicho ongezwa au kupunguzwa kutoka katika Qur’ani iliyokusanywa wakati wa zama za Ukhalifa wa Othmani, amabayo ndio Qur’ani ilioko mikononi mwa Waislamu, bali anachokusuni ni kwamba, kuna sehemu fulani ya ufunuo wa Mwenye Ezi Mungu ulioteremshwa kwa bwana Mtume (s.a.w.w) haikuandikwa kwenye Quran hii iliyopo hivi sasa mikononi mwetu. [58]
- Burhane Rooshan; ambacho kwa Kiarabu kinajulikana kwa jina la al-Burhan ala Adami Taharifi al-Qur’ani, kilichoandikwa na Mirza Mehdi Boroujerdi: Mwandishi katika kitabu hichi ametoa hoja za wazi katika kukanusha uwezekano wa kupotoshwa kwa Qur’ani. [59] Pia, amepitia na kukosoa Hadithi zilizotumika katika Faslu al-Khitabi katika kuthibitisha kuwepo mapungufu ndani ya Qur’ani. Yeye amekosoa mapungufu yote ya kimapokezi na kiufahamu yaliomo kwenye Hadithi hizo. [60] Mwandishi ameainisha maoni ya zaidi ya wanazuoni 40 wa tafsiri, mafiqhi, na watafiti wa Qur’ani wa madhehebu ya Shia katika kukanusha upotoshwaji wa Qur’ani wa kuongeza au kupunguza kitu ndani yake. [61]
- Siānatu al-Qur'ani min al-Taharifi, kilichoandikwa na Muhammad Hadi Ma'arifati: Kitabu hichi kina sura nane na kimejadili mada zifuatazo: Maana ya kilugha na kiistilahi ya neno la Kiarabu «taharif» (upotoshwaji), sababu za kuto wezekana kuwepo kwa taharifu (upotoshwaji) katika Qur’ani, maoni ya baadhi ya wanazuoni wa Shia kuhusiana na kuto wepo kwa upotoshwaji wa Qur’ani, ushahidi kutoka kwa wataalamu wa Sunni kuhusu usafi wa Shia kutokana na madai ya taharif, taharif na uchafuzi uliotokea katika vitabu vya Agano la Kale na Agano Jipya, taharifu (upotoshwaji na maharibifu) yaliopo miongoni mwa kikundi cha Hashwiyyah, taharifu (upotoshwaji na maharibifu) yaliopo miongoni mwa Akhbariyyah, pamoja na ukosoaji wa maoni ya mwandishi wa Faslu al-Khitabi. [62] Kitabu hichi kimefasiriwa kwa lugha ya Kiajemi na Ali Nasiri Gilani na kuchapishwa na Taasisi ya Samte Publishers mwaka 1379 Hijria Shamsia kwa jina «Tahrif naa Paziiriye Qur’ani». [63]
Mada Zinazo Husiana
Rejea
Vyanzo