Al-Khatamiyya

Kutoka wikishia

Al-Khatamiyya (Kiarabu: الخاتمية) ina maana kwamba, Muhammad (s.a.w.w) ndiye Nabii wa mwisho na Uislamu dini ya mwisho ya mbinguni, na hakuna Nabii mwingine au dini ya Mwenyezi Mungu itakayokuja baada yake. Kwa maneno mengine ni kwamba, Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni hitimisho la Mitume. Suala la Al-Khatamiyya (hitimisho la Mitume) limetajwa katika Qur’an na hadithi mbalimbali katika vyanzo tofauti vya hadithi vya Kiislamu, na wanazuoni wa Kiislamu wanaona kuwa ni miongoni mwa mambo muhimu na ya dharura ya dini ya Kiislamu.

Katika Aya ya 40 ya Surat Al-Ahzab, Mtume wa Uislamu ametambulishwa kama mwisho wa Manabii (hitimisho la Manabii), jambo ambalo wanazuoni wa Kiislamu wamefasiri kuwa yeye ndiye Nabii wa mwisho wa Mwenyezi Mungu. Upana wa dini ya Kiislamu au kuwa jumuishi dini hii na kutowezekana kupotosha Qur'an vimezingatiwa kuwa ni sababu za hitimisho la Mitume na kutokuweko haja ya kuwa na dini mpya.

Tangu mwisho wa karne ya 20, kutokana na kuzuka kwa madhehebu kama vile Babiyya na Bahaiyya, ambayo yalidai sheria mpya, na pia kutokana na kuibuka kwa maoni mapya juu ya ufunuo na unabii, suala la Al-Khatamiyya (hitimisho la Mitume) lilipata uzingatiaji maalumu katika mijadala ya kitheolojia( Aqaid).

Miongoni mwa vitabu na athari ambazo zimeandikwa kuhusu maudhui ya hitimisho la Manabi ni kitabu cha al-Al-Khatamiyyah fi al-Kitab wa Sunnah wa al-Aql al-Sarih, kilichoandikwa na Jafar Sobhani, mmoja wa wanazuoni, wasomi na Marajii wa Kishia, na kitabu cha Khatmu al-Nubuwwah fi Dhau'i al-Quran wa al-Sunnah kilichoandikwa na Abul A’la Maududi (1282-1358 Hijria Shamsia), mwanzilishi wa Jamaat-e-Islami Pakistan.

Fasili (maana)

Neno al-Khatamiya katika asili linatokana na Khatama ambayo ina maana ya kufikia tamati kitu. [1] Khatama al-Nabiyin maana yake ni mtu ambaye kupitia kwake Unabii umefikia mwisho yaani mwisho wa Manabii. [2] Al-Khatamiyya pia katika istilahi ina maana ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) ndiye Nabii wa mwisho wa Mwenyezi Mungu kwa maana kwamba, baada yake hakuna Mtume mwingine atakayekuja yaani hakuna Nabii baada yake. [3] Kupitia Muhammad kuwa hitimisho la Unabii inapatikana natija hii kwamba, dini aliyokuja nayo (Uislamu) ndiyo dini ya mwisho ya Mwenyezi Mungu. [4]

Nafasi na umuhimu wa Al-Khatamiyya

Al-Khatamiyya ina maana ya kufikia tamati Unabii, risala na kuwa ya mwisho dini ya Uislamu na hii ni moja ya dharura miongoni mwa dharura za dini ya Uislamu na katika Qur’an Tukufu na hadithi jambo hili limezungumziwa na kujadiliwa. [5]

Kulingana na baadhi watafiti na wahakiki, kabla ya mwisho wa karne ya 20, suala la Al-Khatamiyya (hitimisho la Mitume) halikuwa likijadiliwa kwa upana na kwa sura ya kujitegemea katika vyanzo vya Kiislamu. Wamezingatia kuibuka kwa madhehebu kama vile Babiyya na Bahaiyya na madai yao ya kuunda sheria mpya na vilevile na kuunda utendaji tofauti kwa kuitazama dini kwa mtazamo wa sunna ambao ulileta tafsiri maalum ya Unabii, Wahyi na hitimisho la Mitume kama sababu za kupata umuhimu suala la hitimisho la Unabii katika kipindi hiki. [6]

Wengine wamesema kwamba mtazamo mpya juu ya Al-Khatamiyya ulianza na maneno ya Iqbal Lahori na kuendelea na ukosoaji dhidi ya matamshi yake hayo. [7] Vitabu na risala zimeandikwa kuhusu mawazo yake. Murtadha Mutahhari alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kukosoa maoni na mitazamo ya Iqbal Lahori. [8]

Katika mafundisho ya Ukristo, maudhui ya Al-Khatamiyya (hitimisho la Unabii) halikuwa likijadiliwa; lakini baadhi ya wanazuoni na wasomi wa Kikristo, katika mijadala ya kitheolojia na Waislamu, hasa katika karne ya pili ya Hijiria, walikuwa wakisema kwamba, Yesu ndiye hitimisho la Mitume. [9]

Hoja za hitimisho la Mitume

Mafundisho ya Al-Khatamiyya (hitimisho la Mitume) limezungumziwa katika Qur’an na vilevile katika hadithi. [10]

Hoja za Qur’an

Makala asili: Aya ya Al-Khatamiyya

Moja ya hoja za Qur’an za mafundisho haya ambayo inatumiwa na wanatteolojia ni Aya ya 40 ya Surah Ahzab: ((مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَكِن رَّسُولَ اللَّهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ وَكَانَ اللَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا ; Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu)). [11]

Katika Aya hii neno Khatam limesomwa kwa sura mbili ya Khatam na Khatim: Katika kisomo cha Asim neno hili limesomwa Khatam kwa maana ya kuhitimisha au kwa maana muhuri na Mtume wa mwisho. [12] Katika usomaji mwingine imesomwa Khatim kwa maana ya mhitimishaji wa Utume. [13]

Kwa mujibu wa Murtadha Mutahhari, katika usomaji wa aina zote mbili mafuhumu na maana ya Aya ni hii kwamba, Mtume Muhammad (s.a.w.w) atakuwa Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu. [14]

Ili kuthibitisha hitimisho la Mitume kuna Aya nyingine zilizotumika; kwa mfano imeelezwa kwamba, Aya ambazo zinaarifisha na kutambulisha risala ya Mtume wa Uislamu kwa sura jumuishi na pana, zinabainisha hitimisho la Utume na kwamba, baada yake hakuna Mtume mwingine atakayekuja. [15] Aya zifuatazo ni katijka kundi la Aya hizo. [16]

  • ((وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلاَّ كَافَّةً لِّلنَّاسِ بَشِيرًا وَنَذِيرًا ; Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe mbashiri, na mwonyaji)). [17]
  • ((تَبَارَكَ الَّذِي نَزَّلَ الْفُرْقَانَ عَلَى عَبْدِهِ لِيَكُونَ لِلْعَالَمِينَ نَذِيرًا ; Ametukuka aliye teremsha Furqani kwa mja wake, ili awe mwonyaji kwa walimwengu wote)). [18]
  • ((وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلاَّ رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ ; Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote)). [19]

Hoja za hadithi

Hadithi kuhusu Al-Khatamiyya (hitimisho la Utume) zimenukuliwa katika vitabu vya Hadith vya Shia na Sunni. Kwa mfano, Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) katika hadithi ya Manzila, aliuchukulia uhusiano wa Ali (a.s) kwake kuwa mithili alivyokuwa Harun kwa Mussa, kwa tofauti kwamba, hakuna Mtume atakayekuja baada yake. [20] Pia imepokewa kutoka kwake kwamba, ikiwa mtu atakuja kudai Utume baada yangu, basi huyo ni mwongo. [21]

Katika baadhi ya dua zilizonukuliwa kutoka kwa Maimamu (a.s), kumezungumziwa pia suala la kwamba, Mtume wa Uislamu ndiye Mtume wa mwisho. [22]

Kwa nini hitimisho la Utume?

Wanafikra wa Kiislamu, hasa katika zama hizi, wametoa hoja kuhusu sababu ya hitimisho la Utume kuwa mojawapo ni kutowezekana kupotosha Qur'an, Uislamu kuwa dini jumuishi na kutokuweko haja ya Mitume wa kimahubiri ni miongoni mwa sababu hizo:

Kutowezekana kupotosha Qur'an

Kadhalika angalia: Kutopotoshwa Qur'an

Kuja kwa dini mpya ya Mwenyezi Mungu kulitokana na ukweli kwamba, dini za Mitume waliotangulia zilipotoshwa; lakini suala hili haliuhusu Uislamu; kwa sababu Mwenyezi Mungu ametoa dhamana na hakikisho kwamba, Qur’an haitapotoshwa. Kwa hiyo, baada ya Uislamu, hakuna haja ya dini nyingine. [23]

Kuwa jumuishi dini ya Uislamu

Makala asili: Kuwa jumuishi na kamili Uislamu

Kwa mujibu wa Aya ya Ikmal al-Dini (Kukamilika dini) ni kuwa: Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini. Aya hii inaonyesha bayana kwamba, Uislamu ni dini jumuishi ambayo inakidhi mahitaji hata ya vizazi vijavyo. Kwa muktadha huo tunapata natija hii kwamba, hakuna ulazima wa kuweko dini nyingine. [24]

Kutokuweko haja ya Mitume wa kimahubiri

Moja ya sababu za kudhihiri Mtume mpya ni kueleza undani wa Sharia na kuendelea kwa mawasiliano kati ya Mungu na watu. Katika Uislamu, suala hili limedhaminiwa na Mtume (s.a.w.w) na Maimamu maasumu (a.s), na wakati wa kutokuwepo (ghaiba) Imamu wa kumi na mbili, jukumu la kubainisha dini yamekabidhiwa kwa mujtahid wenye sifa. Kwa hiyo, hakuna ulazima wa kuwepo kwa Manabii wanaohubiri. [25] Murtadha Mutahhari, mwanafalsafa na mwanafikra wa zama hizi, anaamini kwamba kipindi cha Al-Khatamiyya ni kama kipindi cha mwisho na cha kitaalamu ikilinganishwa na vipindi vilivyotangulia vya masomo ya msingi na awali yaani kipindi cha mwanadamu kuwa na nadharia. Kama vile ngazi ya masomo ya chuo kikuu, ambayo ni kozi maalumu ambayo inamaanisha mwanadamu kuwa na nadharia na maoni, Ni kipindi cha ijtihadi katika uwanja husika. Kipindi cha dini ya mwisho kwa wanadamu kwa ujumla, si kwa kuzingatia mtu mmoja hasa kwa mtu mwingine, ni kipindi cha kuwa na maoni. Ni katika kipindi cha mwanadamu kuwa na maoni ambapo masuala ya ijtihadi na mujtahidi katika dini hupata hadhi na maana. Vile vile anaamini kwamba jambo kama hilo halikuwepo katika dini za Ibrahim, Mussa na Issa, na kile ambacho Qur’an inakifasiri kuwa “kutambua sheria"” na “kubobea katika dini” hakionekani katika dini hizo kwa njia yoyote ile. [26]

Dosari zilizotiwa kuhusiana na hitimisho la Utume

Kumetiwa dosari na kuhojiwa kuhusiana na suala la Al-Khatamiyya (hitimisho la Utume) ambapo Maualamaa wametoa majibu yake. [27]

Khatam ina maana ya pambo

Miongoni mwayo yaliyosemwa kukosoa hitimisho la Utume ni: Katika Aya ya 40 ya Surat al-Ahzab, Khatam ina maana ya pete na makusudio yake ni kwamba, Mtume wa Uislamu ni pambo la Mitume na sio wa mwisho wao. [28]

Katika kujibu imeelezwa kuwa, katika asili maana yake ni kitu cha kupigia muhuri na pete pia imeitwa jina hilo (Khatam) kutokana na kuwa, pete ilikuwa ikitumika sana kupigia muhuri barua baada ya pete hiyo kuchongwa muhuri. Kwa msingi huo, kutumia lafudhi au neno la Khatam kwa maana ya pambo ni kinyume na maana inayofahamiwa na akili katika Aya hiii. [29]

Hitimiisho la risala au Utume?

Baadhi ya watu wamepinga na kutia dosari ya kwamba, Qur'an inamtaja Mtume Muhammad kuwa ni hitishimisho la Manabii (Khatam al-Nabiyin), sio Khatam al-Mursalin (hitimisho la Mitume, wajumbe). Kwa hiyo, Mtume ndiye Nabii wa mwisho, si mjumbe wa mwisho, na anaweza kutumwa Mtume mwingine baada yake. [30]

Kama ilivyotajwa katika tafsir Nemooneh, baadhi wamejibu kwamba: Daraja ya risala iko juu zaidi ya unabii na mtu ambaye anafikia daraja ya ujumbe alikuwa tayari ni Nabii. Matokeo yake ni kuwa, wakati Unabii unapofikia mwisho, katika hatua ya kwanza ya Utume na ujumbe nao unakuwa umeshafikia tamati. [31]

Al-Khatamiyya na kurejea Nabii Issa (a.s)

Chini ya tafsiri ya Aya ya Al-Khatamiyya (hitimisho la Unabii) kumezungumziwa pia maudhui ya kurejea Nabii Issa (a.s), ingawa hilo halitambuliwi kuwa linakinzana na kwamba, Muhammad ndiye Mtume wa mwisho. Hii ni kutokana na kuwa, wakati Nabii Issa atakaporejea atakuwa katika dini ya Mtume Muhammad (s.a.w.w). [55] Kama ambavyo, Unabii wake katika asili ulikuwa kabla ya kuja na kupewa Utume Mtume Muhammad. [56] Kwa kuzingatia kuwa, sheria zote zilifutwa baada ya kuja Mtume Muhammad [57] na madai ya wafuasi wa dini zingine hayakubaliwi, [58] Nabii Issa atarejea akiwa ni sehemu ya umma wa Muhammad. [59]

Vitabu vilivyoandikwa katika maudhui hii

Kumeandikwa vitabu vingi kuhusiana na maudhui ya hitimisho la Utume. Baadhi yavyo ni:

  • Khatamiyat, kimeandikwa na Shahidi Murtadha Mutahhari.
  • Khatmu al-Nubuwwah fi Dhau'i al-Quran wa al-Sunnah kilichoandikwa na Abul A’la Maududi (1282-1358 Hijiria Shamsia), mwanzilishi wa Jamaat-e-Islami Pakistan. Kitabu hiki kimeandikwa kwa lugha ya Kiurdu.
  • Al-Al-Khatamiyyah fi al-Kitab wa Sunnah wa al-Aql al-Sarih, kilichoandikwa na Jafar Sobhani, mmoja wa wanazuoni, wasomi na Marajii wa Kishia. Kitabu hiki kimeandikwa kwa lugha ya Kiarabu. Kitabu hiki kimetarjumiwa kwa lugha ya kifarsi na Reza Ostadi. [60]

Vyanzo

  • Abū l-Futūḥ al-Rāzī, Ḥusayn b. ʿAlī. Rawḍ al-jinān wa rawḥ al-janān. Edited by Muḥammad Jaʿfar Yaḥaqī & Muḥammad Mahdi Nāṣiḥ. Mashhad: Bunyād-i Pazhūhishhā-yi Islāmī, 1377 Sh.
  • Ālūsī, Maḥmūd b. ʿAbd Allāh. Rawḥ al-maʿānī. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, [n.d].
  • Ḥurr al-ʿĀmilī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Wasāʾil al-Shiʿa. Qom: [n.p], 1416 AH.
  • Ibn ʿArabī. Fuṣūṣ al-ḥikam. Edited by ʿAbū l-ʿAlāʾ ʿAfīfī. Tehran: al-Zahrāʾ, 1370 Sh.
  • Aḥmad b. Fāris. Muʿjam maqāyīs al-lugha. Edited by Muḥammad Hārūn. Qom: Maktab al-Aʿlām al-Islāmī, 1404 AH.
  • Aḥmad b. Ḥanbal. Musnad b. Ḥanbal. Beirut: Dār al-Ṣādir, [n.d].
  • Ibn Saʿd, Muḥammad b. Manīʿ al-Baṣrī. Al-Ṭabaqāt al-kubrā. Edited by Iḥsān ʿAbbās. Beirut: [n.p], 1405 AH.
  • Ibn Ṭāwūs, ʿAlī b. Musā. Iqbāl al-aʿmāl. Edited by Jawād al-Qayyūmī al-Iṣfahānī. Qom: Maktab al-Aʿlām al-Islāmī, 1414 AH.
  • Iqbāl Lāhūrī, Muḥammad. Iḥyāʾ-i fikr-i dīnī dar Islām. Translated to Farsi Aḥmad Ārām. Tehran: Risālat-i Qalam, 1362 Sh.
  • Makkī, Muḥammad b. ʿAlī. Quwwat al-qulūb fī muʿāmilat al-maḥbūb. Cairo: [n.p], 1961.
  • Miṣbāḥ, Muḥammad Taqī. Maʿārif-i Qurʾān. Qom: Muʾassisa-yi Āmūzishī wa Pazhūhishī Imām Khomieni, 1379 Sh.
  • Motahhari, Muḥammad Taqī. Islam wa nīyāzhāy-i zamān,. Tehran: Intishārāt-i Ṣadrā
  • Motahhari, Muḥammad Taqī. Majmūʿa-yi āthār. Tehran: Intishārāt-i Ṣadrā, 1381 Sh.
  • Mufīd, Muḥammad b. Muḥammad al-. Al-Amālī. Edited by Ustād Walī wa ʿAlī Akbar Ghaffārī. Beirut: Dār al-Mufīd, 1993.
  • Mullā Ṣadrā, Muḥammad b. Ibrāhīm. Al-Shawāhid al-rabawīyya fī l-manāhij al-sulūkīyya. Edited by Mullā Hādī Sabziwārī. Tehran: [n.p], 1360 Sh.
  • Muslim b. Ḥajāj al-Nīyshābūrī. Ṣaḥīḥ Muslim. Beirut: Dār al-Fikr, [n.d].
  • Rabbānī Gulpāyigānī, ʿAlī. Kalām-i taṭbīqī.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī. Man lā yaḥḍuruh al-faqīh. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī. Qom: al-Nashr al-Islāmī, 1414.
  • Ṣaffār al-Qummī, Muḥammad b. al-Ḥasan. Baṣāʾir al-darajāt al-kubrā. Edited by Muḥsin Kūcha Bāghī Tabrīzī. Tehran: Aʿlamī, 1381 Sh.
  • Subḥānī, Jaʿfar. Al-Ilāhīyāt ʿalā huda al-kitāb wa al-sunnat wa al-ʿaql. Edited bu Muḥammad Makkī al-ʿĀmilī. Qom: [n.p], 1412 AH.
  • Subḥānī, Jaʿfar. Khātimīyyat az naẓar-i Qurʾān wa ḥadīrh wa ʿaql. Translated to Farsi by Riḍā Ustādī. Qom: Muʾassisat Sayyid al-Shuhadāʾ,1369 Sh.
  • Ṭabāṭabāyī, Sayyid Muḥammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Beirut: [n.p], 1394 AH.
  • Ṭūsī, Muḥamamd b. al-Ḥasan al-. Miṣbāḥ al-mutahajjid. Beirut: Muʾassisat Fiqh al-Shīʿa, 1411 AH.
  • Zamakhsharī, Maḥmūd al-. Al-Kashshāf ʿan ḥaqāʾiq ghawāmiḍ al-tanzīl. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1407 AH.