Kutendea Wema Wazazi Wawili

Kutoka wikishia
Usichanganye na Haki ya Wazazi Wawili

Kutendea Wema Wazazi Wawili (Kiarabu: برّ الوالدين أو الإحسان إلى الوالدين): Humaanisha kuwaheshimu baba na mama, kuwatukuza na kutenda aina yeyote ile ya matendo ambayo kimantiki huhesabiwa kuwa ni kwao. Katika Qur'an, suala la Kutendea Wema Wazazi Wawili linawekwa sambamba na amri ya kumwabudu Mwenye Ezi Mungu. Wafasiri wa Qur'an wamefasiri amri hii kwa kuhusisha na aina zote za wazazi, iwe ni makafiri au Waislamu, na iwe ni watenda mema au watenda maovu.

Katika vyanzo vya Hadithi za Kishia na Kisunni, suala hili la kutendea wema wazazi wawili, linachukuliwa kuwa ni moja ya matendo bora yanayopendaza zaidi mbele ya Mwenye Ezi Mungu, na faida mbalimbali zimeelezwa kuhusiana na silka hii ya kuwatendea mema wazazi wawili, miongoni mwazo ni oamoja na; kuongezeka kwa riziki, kuongezeka kwa umri, kupungukiwa na taabu za sakarati al-maut wakati wa kifo, msamaha wa dhambi, na kupata hatima njema ya kuingia Peponi Siku ya Kiyama.

Kuwa na tabia njema na kuto wafanyia wazazi wawili hata uchokozi mdogo, kuwa na mtazamo wa upendo na kutopandisha sauti mbele yao ni mifano ya kutendea wema wazazi.

Dhana na Hadhi yake

وَقَضَیٰ رَ‌بُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِیَّاهُ وَبِالْوَالِدَیْنِ إِحْسَانًا إِمَّا یَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْکِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ کِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْ‌هُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا کَرِ‌یمًا وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّ‌حْمَةِ وَقُل رَّ‌بِّ ارْ‌حَمْهُمَا کَمَا رَ‌بَّیَانِی صَغِیرً‌ا

Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye, na kuwafanyia wema wazazi wawili, ikiwa mmoja wao au wote wawili wamefikia uzee pamoja nawe, basi usiseme kuwaambia walau neno dogo baya mfano wa (uff), lakini usiwakemee na sema nao kwa kauli njema, na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa rehema, na useme: Mola wangu Mlezi, warehemu kama walivyo nilea kipindi nikiwa mdogo.



Kuwatendea wema wazazi wawili ni mojawapo ya amri muhimu zaidi katika Qur'ani. [1] Suala hili katika Qur’ani, limewekwa sambamba na amri ya kumwabudu Mwenye Ezi Mungu. [2] Wafasiri wa Qur'an wanachukulia hii kuwa ni ishara ya umuhimu wa kuwatendea wema baba na mama, [3] na kwamba tendo hili ni miongoni mwa matendo yenye hadhi kikubwa mbele ya Mwenye Ezi Mungu. [4] Wanazuoni wa kifiqhi pia wanalichukulia na kulihisabu suala hili kuwa ni miongoni mwa mwa wajibu wa watoto mbele ya wazazi wao. [5] Pia, katika baadhi ya vitabu vya maadili, imeelezwa kwamba; kutendea wema wazazi ni jambo bora zaidi linalosababisha kufuzu na kuwa karibu na Mwenye Ezi Mungu. [6]

Katika kitabu cha Tafsiri Nemune, chini ya Aya ya 23 Surat Al-Isra, imeelezwa kuwa; kule suala la Tawhid (imani ya kuamini Mungu mmoja), kuwekwa sambamba na suala la kutendea wema wazazi, ni dalili ya msisitizo wa Qur'an juu ya tabia njema kwa baba na mama. [7]

Suala la kutendea wema wazazi, lina maana ya kuwaheshimu baba na mama na kuwathamini kwa hali ya juu kabisa, [8] jambao ambalo linajumuisha kila aina ya wema ambao unastahili hadhi yao. [9] Pia, inaelezwa kuwa neno "wazazi", linajumuisha aina zote zile za wazazi, iwe ni watenda mema au watenda mabaya. [10] Au pia iwe ni makafiri au Waislamu. [11]

Sababu Amri ya Kuwatendea Mema Wazazi Wawili na Uhusiano Wake na Tawhidi

Makala: Aya ya Ihsani kwa Wazazi Wawili

Baadhi ya wafasiri katika kuelezea uhusiano kati ya tawhid (umonotheism) na ihsan (wema) kwa wazazi wawili, uliotajwa katika Qur'an, kusema kwamba: Mungu ndiye sababu halisi ya kuwepo kwa binadamu, na wazazi wawili ni sababu ya pili kuwepo kwa binadamu hoyo, ambapo matunzo yatokayo kwa baba na mama ni sababu kuu ya kuendelea kwa maisha ya mwanadamu. [12] Vilevile wamesema kwamba; kama ilivyokuwa ni muhimu na wajibu kushukuru neema za Mwenye Ezi Mungu, kwa kuwa yeye ndiye Mneemaji halisi, basi pia ni wajibu kushukuru neema za waja wake, na hakuna mtu wema zaidi kuliko wazazi wawili, hivyo basi hakuna anayestahili kushukuriwa zaidi kwa mema zake miongoni mwa wanadamu kuliko wazazi wawili, kwani wao ndio walio beba mzigo mkubwa zaidi wa kumtunza mwanadamu duniani humu. [13]

Mwanazuoni na mfasiri wa Qur’ani ajulikanaye kwa jina la Tabatabai, ameelezea akisema kwamba; sababu ya Qur'an kutilia mkazo juu ya wema kwa wazazi ni kwamba: Uhusiano wa kihisia na kimapenzi uliopo kati ya wazazi na watoto husaidia kuunganisha au kuweka fungamano kati ya kizazi kipya na kizazi kilichopita na kusababisha mshikamano uimara wa kifamilia. Uimara wa kifamilia pia ni moja ya mambo muhimu yanayojenga mahusiano ya kijamii na kusaidia kuimarisha jamii ya wanadamu. [14]

Mtazamo wa Hadithi Juu ya Kuwatendea Hisani Wazazi Wawili

Wazazi wawili wamepewa hadhi maalumu katika Hadithi za Maimamu watukufu (a.s), na limetiliwa mkazo mno suala la kuwaheshimu na kuwathamini wazazi wawili. [15] Katika vyanzo vya Shia na Sunni, kuna milango maalumu na makhususi inayojadili na kuzungumzia suala hilo. [16] Kulingana na riwaya hizo, ukarimu wa hisani katika tabia zetu mbele ya baba na mama, ni miongoni mwa vitendo vyenye daraja la juu kabisa za kiroho [17], na ni miongoni mwa matendo yapendwayo zaidi mbele ya Mwenye Ezi Mungu [18], na sifa hii ni moja wapo ya muhimu itakiwayo Waislamu wa madhehebu ya Shia kujipamba nayo. [19]

Zaidi ya hayo, imekuja katika vyanzo mbali mbali ya kwamba; kuwatazama kwa upendo wazazi wawili ni ibada [20] na ridhaa na hasira ya Mwenyezi Mungu hupimwa kupitia ridhaa na makasiriko ya wazazi juu ya watoto wao. [21] Pia imeelezwa ya kwamba; hakuna udhuru unaokubalika katika kuto watimizia hisani wazazi wawili. [22]

Kuhusiana na mwenendo wa bwana Mtume (s.a.w.w), imeelezwa kwamba; alimheshimu sana mama yake wa kumnyonyesha (mama wa kambo) [23] na aliwaheshimu wale walikuwa na tabia njema kwa wazazi wao. [24] Pia katika Hadithi katika mbali mbali, utakutia kwamba; Waislamu wameamriwa kuwatendea wema wazazi wao na kuvumilia ugumu katika kuwatunza wazazi wawili, [25] hata kama wazazi wao ni washirikina [26] au ni miongoni mwa watu waovu. [27] Pia imependekezwa kwamba ikiwa hawapo hai, basi vyema kwa mwanadamu kuwafanyia wema kwa kuwaombea msamaha kwa Mwenye Ezi Mungu, kulipa madeni yao na kukamilisha ibada zao ambazo hawakuweza kuzikamilisha walipokuwa hai. [28]

Masisitizo ya Nyongeza Katika Kuwathamini Wazazi Wawili

Katika Aya ya 15 Surat al-Ahqaf, baada ya kutoa amri ya kuwatendea wema wazazi na kueleza mantiki yake, Mwenye Ezi Mungu ametukumbusha tu juu ya dhiki walizobeba mama zetu. Suala hili, kwa maoni ya wanazuoni wa Kiislamu, lina nia ya kutoa msisitizo zaidi wa haki alizonazo mama mbele ya wanawe. [29] Imamu Sajjad (a.s) katika Hadithi maarufu ijulikanayo kwa jina la Risatu al-Huquuq, anaeleza ndani yake namna ya shida ambazo mama huzipata katika kipindi chake cha ujauzito na baada ya hapo katika zama za utoto wa wanawe, na kwa njia maalum, anamshauri mtoto kuthamini dhiki hizo za mama alizokubali kuzibeba kwa ajili yake. [30] Pia, Kulayni naye amenukuu Hadithi katika kitabu cha al-Kafi ya kwamba; Mtu mmoja alimwuliza bwana Mtume (s.a.w.w), akesema; Ni nani nimfanyie wema kati ya wazazi wawili? Mtume akajibu: Mama yako. Mtu huyo akauliza tena swali hilo mara mbili zaidi na Mtume akamjibu tena: Mama yako. Na alipo endelea kuuliza kwa mara ya nne, bwana Mtume alimjibu kwa kasema: Baba yako. [31] Katika Hadithi nyingine itokayo kwa bwana Mtume (s.a.w.w) imenukuliwa ya kwamba; Kumfanyia wema mama ni kaffarah inayo epusha adhabu ya dhambi zilizo pita. [32]

Mifano ya Wema

Katika Aya ya 23 na 24 ya Suratu al-Isra, baada ya Mwenye Ezi Mungu kutoa amri ya kuwatendea wema wazazi wawili, pia yeye ameendelea kutoa baadhi ya mifano ambayo ni kinyuma na kuwathamini wazazi hao. Miongono mwa mifano hiyo; ni kusema "uf", lugha ambayo kwa Kiswahili tunaweza kusema ni kuwaguti wazazi wawili. Lapili lililokatazwa katika Aya hiyo, ni kuwakaripia au kutumia lugha ya ukali dhidi yao. [33] Katika vyanzo vya Hadithi, kuna Riwaya isemayo kwamba kwamba; Wakati Imamu Swadiq (a.s) alipoulizwa kuhusu maana ya hisani katika Aya hii, alijibu kwamba: Maana ya hisani kwa wazazi wawili ni kuwatendea wema na kuwapa kabla ya wao kukuomba kitu, hata kama wao wenyewe wana uwezo wa kukipata kitu hicho. [34]

Katika mwendelezo wa Hadithi hii, imeelezwa ya kwamba; pale Aya isemapo: Wala usiwaambie uff, hii ina maana ya kwamba: iwapo utakerwa na wazazi wako wawili, basi usiwafanyie ukali hata kama ni ni mdogo kiasi gani. Na pale iliposemwa kwamba: uzungumze nao kwa maneno ya heshima, ina maana ya kwamba; Hata kama wao watakupiga, basi jawabu yako kwao iwe ni kuwaambia; Mungu akusameheni. Na pale isemwapo kwamba; na ujishushe mbele yao kwa unyenyekevu, ina maana ya kwamba: usiwaangalie kwa dharau na jeuri, bali uwaangalie kwa huruma na unyenyekevu, na wala usinyanyue sauti yako kuipindukia sauti yao. Pia, wakati wa kuwapa kitu, usiweke mkono wako juu ya mkono wao na wala usiwatangulie wakati wa kutembea na wakati wa kukaa kitako. [35]

Faida za Kuwafanyia Hisani Wazazi Wawili

Kulingana na vyanzo vya hadithi, ni kwamba; kuna faida mbali mbali za kiduni na Kiakhera (kiroho) zinazo patikana katika kuwatendea wema wazazi wawili. Miongoni mwazo ni pamoja na: kuondokewa na umaskini, [36] kuongezeka kwa riziki, [37] kuongezeka kwa umri, [38] kupata ahueni katika kifo (katika sakarati al-maut), [39]kupata ridhaa ya Mungu na kusamehewa dhambi, [40] urahisi wa kuhesabiwa kwa matendo yake siku ya Kiama [41] na kupata cheo cha kuingia Peponi siku ya Kiama. [42]

Pia imekuja katika Hadithi ya kwamba; jicho na mtazamo wenye huruma wa mtoto kwa wazazi wao, husababisha kufunguliwa kwa milango ya rehema za Mungu [43] na kuata ujira wa thawabu ya hija inayokubalika mbele ya Allah. [44] Katika kitabu cha Kafi, imenukuliwa kutoka Imamu Swadiq (a.s) ya kwamba; Mtu atakaye watendea wema wazazi wake wawili, na kufanyia ibada, kama vile sala na sadaka baada ya kufariki kwao, naye pia atapata thawabu za matendo hayo, na hata kupindukia zaidi ya thawabu za kawaida za matendo hayo. [45]

Kulingana na Hadithi nyingine ni kwamba; Kutozingatia wema kwa wazazi wawili, kunasababisha kupatika kwa matokeo mbali mbali kama vile; kupotoka na kukaa nje ya utiifu wa Mungu, kutokuwa na shukurani juu ya neema za Allah, kuzikufuru neema za Mwenye Ezi Mungu, kubatilika kwa amali, kukatika kwa kizazi [46] na kutengwa na Peponi ya Mwenye Ezi Mungu. [47]

Maudhui Yanayo Fungamana