Al-Sayyida Nafisa

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Bibi Nafisah)
Kaburi la Sayyida Nafisa katika mji wa Misri

Sayyida Nafisa au Nafisa Khatun (Kiarabu: السيدة نفيسة)(145-208 Hijiria) ni mmoja wa wajukuu wa Imamu Hassan Mujtaba (a.s) na binti ya Hassan bin Zayd bin Hassan. Vyanzo vya historia vimemchukulia kama mmoja wa wanawake wacha Mungu, msomi na mtaalamu wa hadithi, mtenda wema na hisani na Qur'an. Alikuwa mke wa Is'haq Mu'tamin, mtoto wa Imam Swadiq (a.s). Sayyida Nafisa, ambaye alisafiri kwenda Misri kuzuru kaburi la Nabii Ibrahim (a.s), aliamua kubakia huko Misri kutokana na msisitizo wa watu na akaishi huko hadi mwisho wa maisha yake. Katika baadhi ya vyanzo, kumenukuliwa baadhi ya karama zinazonasibishwa kwa Sayyida Nafisa kama vile kuponya wagonjwa na kuiokoa Misri na Mto Nile kunako ukame.

Sayyida Nafisa alikuwa mjuzi wa tafsiri na hadithi, ndiyo maana baadhi ya wanazuoni wa hadithi, akiwemo Muhammad bin Idris Shafi'i na Ahmad bin Hanbal, walishiriki katika vikao vyake vya vya kunukuu hadithi na wakanukuu kutoka kwake. Nafisa Khatun alifariki mwezi wa Ramadhani mwaka 208 Hijiria. Is'haq Mu'tamin alikuwa na nia ya kupeleka mwili wa marehemu mkewe Madina; lakini kwa ombi la watu wa Misri, akamzika huko. Kaburi lake huko Cairo ni mahali pa Waislamu kufanya ziara.

Maisha yake

Nafisa Khatun alizaliwa katika mji mtakatifu wa Makka na kukulia mjini Madina. [1] Inasemekana kwamba nyumba aliyokuwa akiishi Nafisa huko Madina ilikuwa magharibi mwa Madina na ilikuwa ikitazamana na nyumba ya Imam Swadiq (a.s). [2] Katika kitabu cha al-Durr al-Manthur fi Tabaqat Rabbat al-Khudur imekunuliwa kutoka katika kitabu cha As'af al-Raghbin kwamba, Nafisa alizaliwa mwaka wa 145 Hijiria [3] Azizullah Attaridi alitaja kuzaliwa kwake kwamba, kulikuwa tarehe 11 Rabi al-Awwal mwaka huo huo. [4]

Nasaba yake kwa upande wa baba yake inafika kwa Imamu Hassan Mujtaba (a.s) [5] Baba yake Hassan bin Zayd alichaguliwa na Mansur Abbasi kuwa mtawala wa Madina na alihudunmu wadhifa huo kwa muda wa miaka 5. Lakini baadaye alimuondoa madarakani na kumtia jela. [6] al-Maqrizi ananukuu kutoka katika kitabu cha "Rawdhat al-Anisah Bifadhl Mash'had al-Sayidah Nafisah" kwamba, mama yake alikuwa Ummu Walad. [7]

Ndoa

Nafisa Khatun aliolewa na Is'haq bin Jafar, anayejulikana kama Is'haq Al-Mu'tamin, mtoto wa Imam Swadiq (a.s). [8] Baadhi ya vyanzo vilivyokuja baadaye vinaeleza kuwa, wakati anaolewa alikuwa na miaka 15. [9]Is'haq al-Mu’tamin alifahamika kuwa mtu mwaminifu katika kunukuu hadithi [10] na alikuwa mmoja wa mashahidi wa wasia wa Imam wa 7 (Imamu Kadhim) kuhusu mwanawe Imam Ridha (a.s). [11] Nafisa alimzalia Is'haq bin Ja'afar watoto wawili waliojulikana kwa majina ya Qasim na Ummu Kulthum. [12]

Kuhajiri kuelekea Misri

Katika kitabu cha al-Durr al-Manthur fi Tabaqat Rabbat al-Khudur imenukuliwa kutoka katika kitabu cha al-Mazarat Sakhawi kwamba, mwaka 193 Hijiria baada ya kukamilisha ibada ya Hija, Bi Nafisa akiwa na mumewe walifunga safari na kuelekea Baytul-Muqaddas kwa ajili ya kuzuru kaburi la Nabii Ibrahim (a.s) na kisha baadaye akaenda Misri. Wananchi wa Misri walimpokea na mwanzoni alikaa katika nyumba ya mfanyabiashara mkubwa wa Misri aliiyejulikana kwa jina la Abdallah bin Jassas. Inaelezwa kuwa, watu wengi wa Misri na kando kando yake walikuwa wakimjia kwa nia ya kutabaruku naye kutokana na hatua yake ya kumponya binti wa Kiyahudi. Bi Nafisa Khatun alikusudia kuondoka Misri na kwenda Hijaz. Hata hivyo wananchi wa Misri walimuomba mtawala wa wakati huo wa Misri azungumze naye ili abadilishe wazo na uamuzi wake wa kuondoka Misri na kuelekea Hijaz. Bi Nafisa Khatun alimwambia mtawala wa Misri: "Mimi ni mwanamke dhaifu na nimeshindwa kutekeleza ibada na kumuabudu Allah kama inavyostahiki na sehemu yangu ya kuishi ni ndogo na haina uwezo wa kuingia watu wote hawa wanaonijia. Mtawala wa Misri ambaye alikuwa na nyumba huko Darb Sib'ah alimpa zawadi nyumba hiyo na akamtaka akaweke siku mbili kwa wiki kwa ajili ya watu na siku zilizobakia ajishughulishe na ibada. Nafisa alitenga siku mbili za Jumamosi na Jumatano kwa ajili ya watu na akaamua kuishi milele huko Misri.[13]

Nafasi yake ya kimaanawi na kielimu

Zirikli amemtaja Sayyida Nafisah kwa sifa kama vile mcha Mungu, mwema, msomi wa tafsiri na hadithi. [14] Nafisah al-Darain, Nafisah al-Tahirah, Nafisah al-'Abidah, Nafisah al-Misriyyah, na Nafisatul Misriyyin [15] ni miongoni mwa lakabu zingine alizosifika nazo.

Nafasi yake ya kimaanawi

Baadhi ya ripoti zimezungumza kuhusu ibada za Sayyida Nafisa, zuhdi (kujinyima na kuipa mgongo dunia) na ukarimu na kueleza kwamba, alikuwa na mali nyingi na alisaidia watu, hasa maskini na wagonjwa. [16] Nafisa alihiji mara 30. [17] Kwa mujibu wa ripoti za vyanzo mbalimbali Bi Sayyida Nafisa alikuwa mtu wa tahajudu na kufanya ibada za usiku na alikuwa akifunga sana Saumu.[18] Imetajwa pia kuwa alikuwa amejichimbia kaburi ambalo kila siku alikuwa akiingia, kusali na kuhitimisha Qur’an humo. [19]Inaelezwa kuwa, alifanikiwa kuhitimisha kusoma Qur’ani katika kaburi hilo mara 190. Baadhi wamesema, alihitimisha Qur’ani humo mara 2000 huku wengine wakisema ni mara 1900. [20] Kwa mujibu wa ripoti ya kitabu cha Nasikh al-Tawarikh, Sayyida Nafisa alikuwa na daraja na nafasi ya juu kwa wananchi wa Misri. [21] Abu Nasr Bukhari amesema, wananchi wa Misri wakiwa na lengo la kuthibitisha madai yao walikuwa wakila kiapo kwa jina la Nafisa Khatun. [22] Baadhi ya watafiti wa Misri wanaamini kwamba, mapenzi ya Wamisri kwake yalitokana na maisha yake ya kujinyima na ya zuhdi.[23]

Sayyida Nafisa alikuwa ameinisika na kushikamana mno na Qur'an na alikuwa ameihifadhi. [24] Aliaga dunia [25] wakati anasoma Aya hii: قُل لِّمَن مَّا فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ قُل لِلَّهِ كَتَبَ عَلَى نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ ; Sema: Ni vya nani viliomo katika mbingu na katika ardhi? Sema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Yeye amejilazimisha nafsi yake kurehemu. [26] Au Aya isemayo: لَهُمْ دَارُ السَّلامِ عِندَ رَبِّهِمْ وَهُوَ وَلِيُّهُمْ بِمَا كَانُواْ يَعْمَلُونَ ; Hao watapata nyumba ya salama kwa Mola Mlezi wao. Naye ndiye Rafiki Mlinzi wao kwa sababu ya waliyo kuwa wakiyatenda. [27] [28] Zaynab (binti ya Yahya Mutwwaj, mtoto wa kaka yake nafisa anasema: Mama yangu mdogo alianza kuugua siku ya kwanza ya mwezi Rajab na maradhi yake yaliendelea mpaka mwezi kumi Ramadhani na yakashadidi na akawa katika hali ya kukata roho. Akiwa katika hali hii akaanza kusoma Surat al-An’am. Aliendelea kusoma mpaka akafika katika Aya hii: قُل لِلَّهِ كَتَبَ عَلَى نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ ; Ni vya Mwenyezi Mungu. Yeye amejilazimisha nafsi yake kurehemu.” Roho yake ikapaa. [29] Imekuja katika kitabu cha Durar al-Asdaf ya kwamba Zaynab amesema: Alipofika katika Aya hii: “Hao watapata nyumba ya salama kwa Mola Mlezi wao. Naye ndiye Rafiki Mlinzi wao kwa sababu ya waliyo kuwa wakiyatenda” alikumbwa na hali ya kuzimia na kupoteza fahamu. Nikamsogeza kifuani kwangu, hapo akatamka shahada na kuaga dunia. [30]

Daraja yake ya kielimu

Sayyida Nafisa alikuwa mjuzi wa tafsiri na hadithi. [31] Baadhi ya wanachuoni walinukuu hadithi kutoka kwake. [32] Muhammad bin Idris Shafi'i (mmoja wa mafaqihi wa madhehebu manne ya Sunni) alikuwa akichukua hadithi kutoka kwake, [33] na Ahmad bin Hambal (kiongozi wa madhehebu ya Hambal) alikuwa akishiriki katika vikao vya Sayyida Nafisa vya kunukuu hadithi. [34] Wakati Muhammad bin Idris Shafi'i alipofariki, mwili wake ulipelekwa nyumbani kwa Sayyida Nafisa na yeye akashiriki katika Sala ya maiti. [35]

Karama

Katika baadhi ya vyanzo, kumenukuliwa karama zake kama vile kuponya wagonjwa [36] na kuiokoa Misri na Mto Nile kutokana na ukame [37] na matukio haya yamhusishwa na Seyyeda Nafisa. Jamal al-Din bin Taghri Bordi amesema kwamba, fadhila na karama zake zinajulikana kila mahali.[38] Ahmad Abu Kaf anaamini kwamba, kupewa Nafisa lakabu ya Karima al-Darain ni kwa sababu watu wa Misri waliona karama kutoka kwake wakati wa uhai wake na baada ya kifo chake. [39] Katika baadhi ya vyanzo, kumenukuliwa karama za baada ya kifo chake. [40]

Kifo na kaburi lake

Nafisa Khatun alifariki dunia mwezi wa Ramadhani mwaka wa 208 Hijiria. [41] Is’haq al-Mu’tamin alitaka kuupeleka mwili wa mkewe Madina, lakini kwa ombi la watu wa Misri alimzika huko. [42] al-Maqrizi anasema kwamba, watu wa Misri walimtaka Is’haq aruhusu Nafisa azikwe Misri kutokana na baraka alizokuwa nazo. [43] Lakini kulingana na vyanzo vingine, Is’haq hakukubali. Watu wa Misri walikwenda kwa mtawala wa Misri na kumtaka amzuie Is’haq asiuchukue mwili wa mkewe hadi Madina. Kumhusisha mtawala wa Misri katika kadhia hii hakukuwa na ufanisi, walitoa mali na kumpa Is’haq na kumtaka akubaliane na ombi lao, lakini Is’haq alikataa kata kata. Lakini hatimaye alikubali kumzika mke wake huko Misri. Inasemekana Is’haq alikubali matakwa ya watu wa Misri kwa sababu ya ndoto aliyoota. Kulingana na ndoto hii, Mtukufu Mtume alimwambia "mzike mkeo hapa hapa." [44]

Sayyida Nafisa alizikwa katika nyumba yake katika sehemu inayojulikana kama Darb al-Saba' na Darb Yazrab.[45] Maqrizi alilichukulia eneo alilozikwa Nafisa kuwa mojawapo ya sehemu nne nchini Misri zinazojulikana kwa kujibiwa dua. [46]Vile vile amenukuu ya kwamba, mtu wa kwanza aliyejenga mnara juu ya kaburi lake ni Ubaidullah bin Siri bin Hakam, Amir wa Misri, na tarehe yake imeandikwa katika maandishi yaliyowekwa kwenye mlango wa kaburi lake ambayo ni Rabi al-Thani mwaka wa 482 Hijiria. [47] Na katika mwaka wa 532 Hijiria, Hafidh Khalifa aliijenga upya na akalijengea kaburi na Kuba juu yake [48]. Yaqut Hamawi (mwanajiografia wa karne ya 7 Hijiria) aliripoti kuhusu kuba kwenye kaburi lake wakati huo. [49] Ibn Kathir, ambaye aliona kuwa, kuzuru makaburi kuwa ni shirki, anasema: Wamisri wanasema maneno kumhusu Nafisa ambayo yanapelekea ukafiri na shirki. Kupitia kauli yake hii, inaweza kufahamika ya kwamba, watu wa Misri katika zama hizo Mashia kwa Masuni walikuwa na heshima maalumu kwa Nafisa Khatun na walikuwa wakitembelea na kulizuru kaburi lake. [50] Pia, kutokana na ripoti ya Dhahabi, ambayo anaihusisha na Wamisri wanaomwomba Mwenyezi Mungu msamaha kupitia kwake. Hivyo inafahamika kwamba, watu wa Misri walikuwa wakifanya tawasuli kwake. [51]

Watu wa Misri wamekuwa wakisherehekea siku ya kuzaliwa kwa Sayyida Nafisa tangu 889 Hijiria wakati wa enzi ya Malik Ashraf Qaitbay (aliyetawala 872-901 Hijria). Katika usiku wa kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwake, umati mkubwa wa Mashia na Masunni husoma Maulidi na sherehe kwenye kaburi lake hadi usiku sana. Watu wa Misri humuelekea Sayyida Nafisa na kupitia kwake wanamuomba Mwenyezi Mungu awakubalie haja zao na wakiwa na lengo la kutabaruku hulibusu kaburi lake. Pia ni ada mazoea kufanya sherehe za harusi kando kando ya kaburi lake hilo takatifu na ni ada pia kwa Bwana na bibi harusi kuzunguka haram ya Bibi nafisa. [52]

Wakati wa zama za Qajar, baadhi ya Mashia wa Iran waliokwenda Damascus na Misri wakati wa ibada ya Hija walikuwa pia wakienda kutembelea haram ya Sayyida Nafisa. Safari hizi za kufanya ziara zimeakisiwa katika baadhi ya maandiko ya kumbukumbu za wasafiri wafanyaziara wa Kiirani na hutoa habari kuhusu haram yake na imani za Wamisri kumhusu bibi mwema huyu. [53]

Andiko la ziara

Kuna vitabu aambavyo vimetaja na kubainisha matini na maandiko ya ziara kwa ajili ya Sayyida Naafisa. Katika maandiko hayo ya ziara, kunatolewa wasifu wa kimaanawi, daraja yake na anatumiwa salamu kama ni mwanamke kutoka katika familia ya Bwana Mtume (s.a.w.w). [54] Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, Waislamu wakati wanapomzuru Nafisa Khatun kuna ziara maalumu ambayo husoma wakiwa katika haram yake. [55] Maandiko ya ziara hiyo yametajwa katika kitabu cha al-Durr al-Manthur. Baadhi ya maandiko ya ziara yake ni:

السلام و التحیة و الاکرام و الرضا من العلی الاعلی الرحمن علی سیدة نفیسة سلالة نبی الرحمة و هادی الامة... و اقض حوائجنا فی الدنیا و الاخرة یا رب العالمین.[56]

Wananchi wa Misri wanaitambua siku ya Jumatano kuwa siku ya kumzuru Sayyida Nafisa. [57]

Monografia

Kumeandikwa vitabu kadhaa kwa lugha ya Kiarabu na kifarsi kuhusana na Nasifa Khatun au Sayyid Nafisa. Kitabu cha al-Tuhfat al-Insiyah min Maathar al-Nafsiyah, kitabu hiki kinahusiana na karama zake. Kuna kitabu kingine kiitwacho al-Sayidah al-Nafisah mwandishi: Tawfiq Abu Ali kwa lugha ya Kiarabu. Kadhalika Azizullah Attardi ameandika kitabu cha Gohar Khandan Imamat au Zendegi Nameh Sayyid Nafiseh huku Ghulam Golizavareh akiandika kitabu cha Banui Ba Karamat kuhusiana na Bibi Nafisa. [58]


Rejea

  1. Zarkali, Al-Alam, 1989, juzuu ya 8, uk.44.
  2. Golizavareh, Banui Karamet, 2002, uk.38.
  3. Fawaz Al-Amili, Al-Dur Al-Manthur, 1312 AH,uk. 521.
  4. Atardi, Gem of Imamat family, 1373, uk. 7.
  5. Ibn Kathir, al-Badaiya wa al-Nahiya, 1407 AH, juz.10, uk.262.
  6. Ibn Kathir, al-Badaiya wa al-Nahiya, 1407 AH, juz.10, uk.262.
  7. Maqrizi, Al-Shaqt al-Maqriziyah, 1998, juzuu ya 3, uk.637.
  8. Maqrizi, Al-Shaqt al-Maqriziyah, 1998, juzuu ya 3, uk.638.
  9. Ataridi, Gem of Imamate, 1373, p. Abu Kaf, Al Bait al-Nabi fi Misr, 1975, uk. 101-102.
  10. Maqrizi, Al-Shaqt al-Maqriziyah, 1998, juzuu ya 3, uk.637.
  11. Kilini, Al-Kafi, Juz. 1, uk. 316.
  12. Moqrizi, Al-Shaqtar al-Maqriziyya, 1998, juzuu ya 3, uk. 637.
  13. Fawaz Al-Amili, Al-Dur Al-Manthur, 1312 AH, 522.
  14. Zarkali, Al-Alam, 1989, juzuu ya 8, uk.44
  15. Abu Kaf, Al Bait al-Nabi fi Misr, 1975, uk 111.
  16. Ibn Kathir, al-Badaiyah na al-Nahiyah, 1407 AH, juzuu ya 10, uk. 262; Muhammad al-Hasoon, Tangazo la Wanawake wa Imani, 1411 AH, uk. 626-628.
  17. Zarkali, Al-Alam, 1989, juzuu ya 8, uk. 44; Moghrizi, Al-Shaqt al-Mughrizieh, 1998, juzuu ya 3, uk. 639.
  18. Maqrizi, Al-Shaqt al-Maqriziyah, 1998, juzuu ya 3, uk.639.
  19. Sephehr, Naskh al-Tawarikh, 1352, juzuu ya 3, uk.126
  20. Shablanji, Noor al-Absar fi Manaqib al-Bait al-Nabi al-Mukhtar, alinukuliwa na: Tehrani, Noor Malkoot Qur'an, juzuu ya4 uk. 489.
  21. Sepehr, Naskh al-Tawarikh, 1352, juzuu ya 3, uk. 120.
  22. Abu Nasr Bukhari, Sir al-Silsal al-Alawiyya, 1381 AH, uk. 29.
  23. Sheikh Mohammad Saban, Isaaf al-Raghbin, muswada, uk. 81.
  24. Maqrizi, Al-Shaqt al-Maqriziyah, 1998, juzuu ya 3, uk.637.
  25. Maqrizi, Al-Shaqtar Al-Maqriziyya, 1998, juzuu ya 3, uk.640.
  26. Surah An'am, aya ya 12.
  27. Surah An'am, aya ya 127.
  28. Fawaz Al-Amili, Al-Dur al-Manthur, 1312 AH, uk. 521; Muhadith Qomi, Mentehi al-Amal, 1379, juzuu ya 2, uk.1418.
  29. https://maktabevahy.org/document/Book/details/39/نور-ملکوت-قران-ج4?page=487
  30. https://maktabevahy.org/document/Book/details/39/نور-ملکوت-قران-ج4?page=492
  31. Alvardani, Al-Shia fi Misr, 1414 AH, uk. 109.
  32. Ibn Khalqan, The Deaths of Alaian, Dar Sader, Vol.5, pp. 423-424.
  33. Shablanji, Nur al-Absar, Cairo, uk. 256; Fawaz al-Amili, Al-Dar al-Manthur, 1312 AH, uk. 521.
  34. Attardi, Gem of Imamate, 1373, uk. 12, 29; Abu Kaf, Al Bait al-Nabi fi Misr, 1975, uk. 107
  35. Ibn Emad Hanbali, Shazerat al-Dhahab, 1406 AH, juzuu ya 3, uk.43; Ibn Khalqan, Vifo vya Al-Ayyan, Juz 5.uk. 424; Fawaz al-Amili, Al-Dar al-Manthur, 1312 AH, uk. 521.
  36. Abu Kaf, Al Bait al-Nabi fi Misr, 1975, uk. 107; Mahalati, Riyahin al-Sharia, Dar al-Katb al-Islamiya, juzuu ya 5, ukurasa wa 87-88; Moghrizi, Al-Shaqt al-Mughrizieh, 1998, juzuu ya 3, uk. 641.
  37. Shablanji, Nur al-Absar, Cairo, uk. 256; Mahalati, Riyahin al-Sharia, Dar al-Katb al-Islamiya, juzuu ya 5, uk. 85; Moghrizi, Al-Shaqt al-Mughrizieh, 1998, juzuu ya 3, uk. 641.
  38. Ibn Taghri Berdi, Al-Nujum al-Zahera, Wizara ya Utamaduni na Al-Arshad al-Quumi, Juz. 2, uk. 186.
  39. Abu Kaf, Al Bait al-Nabi fi Misr, 1975, uk. 107.
  40. Kwa mfano, rejea: Fawaz al-Amili, Al-Dur al-Manthor, 1312 AH, uk. 522.
  41. Ibn Kathir, al-Badaiyah na al-Nahiyah, 1407 AH, juzuu ya 10, uk. 262; Ibn Khalqan, Vifo vya Al-Ayyan, Dar al-Thaqafa, juzuu ya 5, uk. 424; Moqrizi, Al-Shaqtar al-Maqriziyya, 1998, juzuu ya 3, uk.640.
  42. Ibn Kathir, al-Badaiyah na al-Nahiyah, 1407 AH, juzuu ya 10, uk.262; Fawaz al-Amili, Al-Dar al-Manthur, 1312 AH, uk. 521.
  43. Maqrizi, Al-Shaqtar Al-Maqriziyya, 1998, juzuu ya 3, uk.640.
  44. Shablanji, Nur al-Absar, Cairo, uk. 258; Abu Kaf, Al Bait al-Nabi fi Misr, 1975, uk. 104; Sheikh Mohammad Saban, Isaaf al-Raghbin, muswada, uk. 81; Qomi, Mentehi al-Amal, 1379, juzuu ya 2, uk.1418; Mohammad al-Hasoon, Tamko la Wanawake, uk. 189.
  45. Maqrizi, Al-Shaqtar Al-Maqriziyya, 1998, juzuu ya 3, uk.640.
  46. Maqrizi, Al-Shaqtar Al-Maqriziyya, 1998, juzuu ya 3, uk.640.
  47. Maqrizi, Al-Shata Al-Maqriziyah, 1998, juzuu ya 3, uk. 641-642.
  48. Maqrizi, Al-Shata Al-Maqriziyya, 1998, juzuu ya 3, uk.642.
  49. Hamvi, Majam Al-Baldan, 1995, juzuu ya 5, uk. 142.
  50. Rejea kwa: Ibn Kathir, al-Badaiya wa al-Nahiya, 1407 AH, juz.10, uk.262.
  51. Ibn Imad Hanbali, Shazerat al-Dhahab, 1406 AH, juzuu ya 3, uk.43.
  52. Alvardani, Al-Shia fi Misr, 1414 AH, uk. 110, 113.
  53. Kwa mfano: Jafarian, "Safari ya Hajj ya Iraqi", 1389, uk. 271.
  54. Shablanji, Nur al-Absar, Cairo, uk. 259.
  55. Fawaz Al-Amili, Al-Dur Al-Manthur, 1312 AH, 522.
  56. Fawaz al-Amili, Al-Dur al-Manthor, 1312 AH, uk. 522.
  57. Atardi, Gem of Imamate family, 1373, uk. 62.
  58. بانوی با کرامت، شرح حال و ذکر کرامات سیده نفیسه نواده امام حسن مجتبی(ع) سایت آدینه بوک

Vyanzo

  • Ibn Taghri Bardi, Jamal al-Din, Al-Nujum Al-Zahira Fi Maluk Misr na Cairo, Cairo, Wizara ya Utamaduni na Al-Arshad Al-Quumi, Beta.
  • Ibn Khalqan, Ahmed bin Muhammad, kifo cha al-Ayyan, utafiti wa Ehsan Abbas, Beirut, Dar al-Thaqafa, Bita.
  • Ibn Emad Hanbali, Abd al-Hay bin Ahmad, Shazarat al-Dhahab, Utafiti: Arnawut, Damascus-Beirut, 1406/1406/1986.
  • Ibn Kathir Damaschi, Ismail Ibn Umar, Al-Badayah na Al-Nahayah, Beirut, Dar al-Fikr, 1407 AH/1986 AD.
  • Abukaf, Ahmad, Al Bait al-Nabi fi Misr, Cairo, Darma'arf, 1975.
  • Abu Nasr Bukhari, Sahl bin Abdullah, Sir Al-Silsilah Al-Alawiyyah, imetafitiwa na Sayyid Muhammad Baqir Bahrul Uloom, Najaf, Al-Maktab Al-Haydariyyah, 1381 AH.
  • Tawfiq Abu Alam, Al-Siedah Nafiseh, Utafiti: Mohammad Shoghi, Tehran, Al-Majjam Al-Alami kwa Kukaribiana kati ya Dini za Kiislamu, 1428 AH/2008 AD.
  • Jafarian, Rasul, "kitabu cha usafiri cha Iraqi Algerian Hajj", vitabu hamsini vya kusafiri vya Qajari Hajj, Tehran, uchapishaji wa Alam, 1389.
  • Hamvi, Yaqut bin Abdullah, Al-Baldan Museum, Beirut, Dar Sader, 1995.
  • Zarkali, Khair al-Din, Kamusi ya tafsiri ya Al-Alam ya wanaume na wanawake wa Waarabu na Waarabu na watu wa Mashariki, Beirut, Dar al-Alam kwa Waislamu, 1989.
  • Sepehr, Abbas Qalikhan, Naskh al-Tawarikh (zama za Imam Kazem), Tehran, Islamia, 1352.
  • Shablanji, Momin bin Hasan, Noor al-Absar fi Manaqib bint al-Nabi al-Mukhtar, kilichochapishwa katika ukingo wa kitabu Asaf al-Raghbeen, Cairo, lithography, beta.
  • Sheikh Mohammad Saban, Asaaf al-Raghbeen katika wasifu wa Mustafa na fadhila za Ahl al-Baytah.
  • Attardi, Azizullah, Gem of Imamat Family au Wasifu wa Seyyedah Al-Nafisa, Tehran, Attard Publications, 1373.
  • Fawaz Ameli, Zainab bint Youssef Nawaz, Al-Dar Al-Manthor fi Tabaqat Rabat al-Khodor, Misri, Al-Kubari Al-Amiriyah Press, 1312 AH, Beirut Offset, Dar al-Marafa, Beta.
  • Kahaleh, Omar Reza, Tamko la Wanawake katika Ulimwengu wa Waarabu na Uislamu, Beirut, Taasisi ya Al-Rasalah, 1412 AH/1991 AD.
  • Kilini, Muhammad bin Yaqub, Al-Kafi, Tehran, Dar al-Kitab al-Islamiyya, 1407 AH.
  • Gholizavareh, Gholamreza, Bakhramat Lady, Qom, Hassanin Publications, 2002.
  • Mahalati, Zabihullah, Riyahin al-Sharia, Tehran, Dar al-Katb al-Islamiya, Beta.
  • Muhammad al-Hasoun Umm Ali Mashkoor, Tangazo la Wanawake Waumini, Machapisho ya Eswa, 1411 AH.
  • Maqrizi, Ahmed bin Ali, Al-Mawa'az na al-Lagha na al-Aqtior al-Maqriziyyah, utafiti: Mohammad Zainham na Madina al-Sharqawi, Cairo, Madbouli School, 1998.
  • Wardani, Saleh, Al-Shia fi Misr Man al-Imam Ali hata al-Imam Khomeini, Cairo, shule ya Madbouli al-Saghir, chapa ya kwanza, 1414 AH.
  • Muhaddith Qomi, Sheikh Abbas, Mantehi al-Maqal fi Tawarikh al-Nabiy wa al-Al, Qom, Dilil Ma, 1379.
  • https://maktabevahy.org/document/Book/details/39/%D9%86%D9%88%D8%B1-%D9%85%D9%84%DA%A9%D9%88%D8%AA-%D9%82%D8%B1%D8%A7%D9%86-%D8%AC4?page=490