Thiqah

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Mwaminifu)

Thiqah (Kiarabu: الثِقَة): Neno hili katika elimu ya rijali (elimu ya tafiti juu ya hali na wasifu wa wapokezi wa Hadithi) ni lenye kuashiri msimulizi wa Hadithi mwenye kuaminiwa. Ila neno hili kiasili humaanisha mpokezi au msimulizi msema kweli. Baadhi ya wataalamu wa ‘ilmu al-rijali wamefafanua zaidi kwa kusema ya kwamba; msimulizi thiqah ni mpokezi mwenye Imani ya madhehebu ya Shia Ithna Ashara, mwadilifu, na mwenye uhodari na umakini wa akili katika kuhifadhi Hadithi; yaani, mwenye uwezo wa kumbu kumbu imara katika kukumbuka Riwaya (Hadithi). Neno ‘thiqah’ linatumika katika uwanja wa kutambua na kutofautisha baina ya wasimilizi wachongezi na wazushi, na wasimulizi waaminifu wa Hadithi. Neno ‘thiqah’ limetumiwa na Masumina na pia linaonekana katika maneno ya wapokezi wa Hadithi wa zama za Maimamu waongofu.

Neno hili linapotumiwa na Maimamu au wanazuoni wa Hadithi, huwa na nia ya kuwaarifisha wapokezi waaminifu wa Hadithi wa katika zama hizo. Mingoni mwa vigezo na viashiria vya kuthibitisha ukweli wa mtu anayesimulia Hadithi ni; ashirio la wazi la kumsifu msimulizi fulani kwa sifa ya thiqah litokanalo kwa mmoja wa Maasumu, au mmoja wa wanazuoni na watafiti wa fani ya ‘Ilmu al-Rijali wa zama zililizo pita au hata wa zama za hivi sasa. Kigezo hichi hutumika kuthibitisha sifa ya ukweli aliyo nayo mpokezi fulani. Baadhi ya maneno yanayotumika katika Nyanja za Hadithi na fani ya Elimu ya Rijali (‘Ilmu al-Rijali), ambayo yamechukuliwa kama dalili na ashirio la sifa ya ukweli wa mpokezi wa Hadithi ni: "thiqah", "jaleel al-qadr", na wakati mwingine "thiqah 'ainun", na "saduuq".

Neno “thiqah” linaweza kutumika kwa njia tofauti, wakati mwingine huwa linamlenga mpokezi maalumu na kumpa sifa mpokezi mwaminifu na msema kweli katika kazi zake za upokezi wa Hadithi. Ashirio hilo ima huwa ni kutoka kwa Imamu au wanazuoni wa fani ya Hadithi, katika hali hii, mtu aliye sifiwa kwa sifa hiyo kiistilahi huitwa kuwa ni mtu aliye pata ithibati makhususi “tauthiqun khaassun”. Na mara nyingine neno hili hutumika kulenga kikundi cha wapokezi, ambao uwaminifu katika ukweli wao, unatokana ukubalikaji wao mbele ya wapokezi wa Hadithi, ambapo huonekana wanazuoni madhubuti kupokea Hadithi kutoka kwao. Kule wanazuoni waaminifu kupokea Hadithi kutoka kwao, huchukuliwa kama ni saini au ithibati ya kuthibitisha uaminifu wao. Kiistilahi hali hiyo haitwa ithibati ya kiujumla “tauthiqu aammun”. Katika “tauthiqu aammun” huwa hakuna kauli maalumu kutoka kwa Maasumu au mwanazuoni maarufu aliye thibitisha uaminifu na ukweli wa wapokezi hao kupitia akili, kama ilivyo katika “tauthiqu khaassun”, bali kupitia lugha ya matendo. Ithibati ya wapokezi wote katika tafsiri ya Qummi ni mfano wa ithibati ya kiujumla au “tauthiqu aammun”.

Utafiti na Welewa wa Dhana

Neno "thiqah" ni moja ya maneno yanayotumiwa sana katika vyanzo vya Hadithi na vitabu vinavyo tafiti hali halisi za wapokezi wa Hadithi na wasifu wao, ambapo hutumika kwa ajili ya kusisitiza uwaminifu wa mpokezi anaye sifiwa kwa sifa hiyo. [1] Wataalamu wa lugha wakielezea maana ya neno "thiqah", wamelifafanua neno hili kwa maana ya mtu mwenye kuaminika [2] au kwa maana ya mtegemewa na mwaminifu. [3]

Ibnu Ghadhairi, mmoja wa wanazuoni wa Kishia wa karne ya tano Hijria, haamini kuwa; sifa ya uwaminifu ni sifa pekee na tosha itakayo mpelekea mpokezi au msimulizi apewe hadhi ya msema kweli. Kwa matazamo wake; sifa ya uaminifu katika elimu ya rijali ya Shia, ni istilahi inayo husiana na sifa kadhaa ndani yake, ikiwemo sifa ya uwaminifu, uwezo wa kuhifadhi (kumbu kumbu) pamoja na sifa ya ufuasi wa madhehebu ya Shia Ithna Ashara. [4]

Kwa upande mwingine, Abu Ali Hairi (aliyezaliwa mwaka 1159 na kufariki 1215 Hijiria) na Mohammad Asif Mohsini, msomi wa kisasa wa Iran wa fani ya elimu ya rijali “’ilmu al-rijali”, wanaamini kwamba; madhumuni ya neno uaminifu au msema kweli “thiqah” katika maneno ya wanazuoni wa elimu ya rijali “’ilmu al-rijali” ni, sharti za kiujumla za mpokezi wa Hadithi, ikiwa ni pamoja na; Uislamu, ukomavu (kubaleghe), akili timamu, uadilifu, na Imani. Na watu thiqah ni wale watu waaminifu na wasema kweli ambao wana maarifa ya kutosha katika kutambua masimulizi ya ukweli ya Hadithi. [5] Wapo wengine walio lizingatia neno “thiqah” (uaminifu) kuwa ni zaidi ya kusema kweli, na wanamuona msimulizi wa kuaminika ni yule aliye kusanya sharti tofauiti za usimulizi; ikiwa ni pamoja na uaminifu (ukweli), kumbu kumbu imara, ujuzi wa kuelewa taqiyyah katika Hadithi, ujuzi wa siri za ndani ya makundi (makundi ya kiitikadi au makundi ya wapokezi), mafungamano ya kimadhehebu ya wapokezi na kadhalika. [6] Hata hivyo, baadhi ya watafiti wa kisasa, wakitegemea baadhi vielelezo, wanaamini kwamba; wengi wa wanahadithi (wasimulizi wa Hadithi au wahakiki wa Hadithi) na wanazuoni wa ‘ilmu al-rijali hutumia neno “thiqah” katika maana halisi ya kilugha, likimaanisha mtu anayeaminika, na neno hili katika fani ya ‘ilmu al-rijali halina maana zaidi ya maana ya kilugha. [7]

Uanzilishi wa Sifa ya Thiqah

Neno "thiqah" lilikuwa likitumiwa katika matamshi na maelezo ya Maimamu wa Kishia (a.s), likimaanisha hali na sifa maalumu kuhusiana na baadhi ya wasimulizi wa Hadithi. [8] Mara nyingi Maimamu (a.s), walikuwa wakiwaarifisha wapokezi wao wa Hadithi walio waaminifu kwa sifa hii mbele ya umma. [9] Baadhi ya wanazuoni kwa kuzingatia Hadithi za Maimamu, wamelifasiri neno “thiqah” kwa maana ya "mwaminifu" na "mwenye elimu" kutoka kwa Ahlul-Bayt (a.s). [10] Katika barua kutoka Imam Mahdi (a.t.f.s), pia watu wenye uaminifu (thiqah) wametajwa kuwa; ni wale wanaobeba siri za Maimamu ambao maneno yao yanalingana na maneno ya Imam wa Zama (a.t.f.s) na ni hoja kamili kwa watu. [11]

Neno hili pia linaonekana katika maneno ya wanahadithi wa zama za Maimamu pia katika zama zinazo karibiana na zama za Maimamu, likitumika katika kuwaarifisha wasimulizi waaminifu. Neno hili linaonekana kutumika mara 35 katika kitabu cha Rijal al-Kashi, mara 248 katika kitabu cha Rijal al-Tusi, na mara 533 katika kitabu cha Rijal al-Najashi, wakielezea kuhusiana na sifa za wasimulizi. [12] Vile vile ndani ya vitabu vya kale vya Hadithi, kunapatikana maneno kadhaa mengine yanayotokana na mzizi wa neno hili kama vile; "thuqaat" na "thiqatiy". [13]

Vigezo

Kwa kutokana tatizo la kuwepo kwa Hadithi bandia zilizosimuliwa kutoka kwa wazushi, wataalamu wa ‘ilmu al-rajali (fani ya uchambuzi wa hali za wapokezi) wameorodhesha njia maalumu za kuthibitisha uaminifu wa wasimulizi na kutambua Hadithi sahihi. [14] Wahid Bahbahani, faqihi wa Kishia na mwanachuoni wa juu wa fani ya usulu al-fiqhi, ameainisha njia 39 za kuthibitisha uaminifu wa msimulizi. [15] Baadhi ya njia hizo muhimu ni: kupatikana kauli ya uthibitosho juu ya uaminifu wa mpokezi (msimulizi wa Hadithi) kutoka kwa mmoja wa Maasumina, kuthibitishwa uaminifu wake kutoka kwa wataalamu wa zamani au wa sasa wa ‘ilmu al-rijali, kuwepo kwa madai ya makubaliano (ijmaa) juu ya uaminifu wa mpokezi, kuwa wakili wa mmoja wa Maimamu Maasum, kupatikana kwa mpokezi muaminifu aliye pokea Hadithi kutoka kwa kwake, (yaani iwapo mpokezi mwaminifu atapokea Hadithi kutoka kwa mtu Fulani, hiyo huchukuliwa kama ni kielelezo cha uwaminifu wake), awe ni mwanazuoni aliye pata ijaza (idhini) ya kunukuu Hadithi na ya mwisho ni kuwa na wingi wa Hadithi, yaani awe amenukuu Hadithi nyingi. [16]

Njia za Uthibitishaji Uaminifu

Uthibitishaji wa uaminifu kwa wapokezi wa Hadithi; Ni ushuhuda maalumu wa uaminifu kwa wapokezi, jambo ambalo linaweza kutimia kupitia njia mbili tofauti: mfumo wa kwanza ni thibitisho binafsi “tauthiqu khaassun”, ambapo mpokezi huwa ametajwa kwa jina na kusifiwa kwa sifa ya uaminifu. Njia ya pili ni thibitisho la ujumla “tauthiqu ‘aammun”, amapo sifa za wapokezi waaminifu huwa zinaanikwa ili kufahamisha watu na kuwapa vigezo maalumu vya kukubali Hadithi. Kwa msingi huu, ikiwa mpokezi wa Hadithi atahisabiwa kuwa ni mwaminifu na kuthibitishwa uaminifu wake kwa kauli, ambapo katika istilahi za ‘ilmu al-rijali husemwa kuwa Fulani amepewa tauthiq. [17] Kwa maneno mengine, ikiwa thibitisho linamrejelea mtu maalum miongoni mwa wapokezi, [18] katika ‘ilmu al-rijali thibitisho hilo, huitwa thibitisho maalum “tauthiqu khaassun”. Wengi wa wapokezi katika vyanzo vya ‘ilmu al-rijali wamethibitishwa kwa njia hii, ambapo wapokezi hao wamechukuliwa kuwa ni wapokezi wa waaminifu. [19] Baadhi ya wanazuoni wa fani ya ‘ilmu al-rijali, kama vile al-Najashi na Sheikh Tusi, wameandika vitabu vyao kwa kutegemea misingi ya uthibitishaji maalum. [20]

Allama Hilli ambaye ni mwanafani wa ‘ilmu al-rijali, ametumia njia tofauti katika kuhakiki uwepo wa uthibitisho juu ya uaminifu na udhaifu wa wapokezi wa Hadithi. Moja wapo ni kwamba; ikiwa kuna uthibitisho maalum wa uaminifu kuhusu mtu fulani, udhaifu wake unaotokana na kutokuwa mfuasi madhehebu ya Shia Ithna Ashari unaweza kufidiwa au kufunikwa. Yaani atahisabiwa kuwa ni mwaminifu hata kama atakuwa si Shia. [21]

Ikiwa kuna kikundi cha wasimulizi waliothibitishwa uaminifu wa kupitia sheria na kanuni maalum, na wakachukuliwa kuwa waaminifu, [22] uthibitisho huo huwa unaitwa uthibitisho wa jumla. [23] Walakini, wataalamu wa fani ya ‘ilmu al-rijali wamekuwa na tofauti juu ya mifano hai ya uthibitisho wa jumla. [24]

Baadhi ya mifano hai ya uthibitisho wa jumla ni pamoja na: uthibitisho wa wasimulizi wote waliotajwa katika kitabu cha Tafsiri ya Qummi, wasimulizi wa kitabu kamilu al-Ziyarat, masheikh (wanazuoni wa Hadithi) waliotajwa katika kitabu cha Rijalu al-Najashi, wasimulizi wote waliotajwa katika nukuu ya riwaya za Bani Fazal, [25] wapokezi maarufu (watu 22) wanao julikana kwa jina la As-habu al-Ijmaa, mawakili wa Maimamu (a.s) au Masahaba wote wa Imam Swadiq (a.s), [26] au kupatika ushuhuda maalumu unao onesha kwamba wapokezi fulani ni waaminifu kwa sababu wao huwa hawapokei Hadithi isipokuwa kwa watu wenye kuaminika, kama vile Ibn Abi Umair. [27] Kwa hiyo Hadithi za mtu kama huyu, zitakubalika bila pingamizi, hata kama Hadithi hiyo ni dhaifu au haijulikani msimulizi wake.

Ni muhimu kuelewa kwamba; ikiwa kuna ushuhuda wa thibitisho maalum kuhusu uaminifu wa mtu fulani, mtu huyo hatakuwa na haja ya kupata uthibitisho wa jumla. [28]

Maneno Yanayotumika katika Kuashiria Sifa ya Uaminifu

Katika vyanzo vya fani ya ‘ilmu al-Rajali, kumetumika maneno maalumu ili kudhamini uaminifu na kukuza imani juu wasimulizi. Baadhi ya maneno yametumika kwa ajili ya kudhibitisha uaminifu wa msimulizi maalumu na kuzipa thamani Hadithi za mtu huyo binafsi. Pia wakati wengine hutumika ibara za kumdhoofisha msimulizi fulani. [29] Kuna maneno fulani ambayo, licha ya kuwa si visawe vya neno “thiqah”, ila Maneno haya yanachukuliwa kuwa zaidi ya neno “thiqah” katika kuthibitisha uwaminifu wa wapokezi wa Hadithi. Kwa ujumla maneno hayo yametumika katika kuwasifu wanazuoni wakubwa wa Kishia. Maneno hayo ni pamoja na “Kabir al-Shaani” (mwenye shani au mwenye hadhi kubwa), “Jalil al-Qadr” (mwenye thamani adhimu), “Adhimu al-Manzilah” (mwenye daraja adhimu), “Authaqu al-Nas 'Inda al-Khaassah” (mwaminifu zaidi mbele ya watu maalumu), na “Fadhluhu Ash-haru Min an Yuusafa” (wasifu wake hauna kifani). [30] Pia kuna maneno mengine yanayo tumika kuonesha msisitiza wa hali ya juu wa uaminifu wa mpokezi fulani, nayo ni kama vile; “Thiqatun Thiqatun” (mwaminifu wa kweli), “Thiqatun ‘Ainun Saduqun”, “thiqatun Jaliilun”, na “thiqatun al-Mu'utamadu ‘Alaihi”. Kwa upande mwingine, kuna maneno fulani ambayo yana ashiria tu kuaminika kwa msimulizi, bila ya kudhamini ukweli na usahihi wa nukuu zake, kama vile “Thiqatun”, “Adlun”, “Saduuqun”, “Sahihu al-Hadithi”, na “Ma'amuunun”. [31]

Kundi jingine la maneno linalotumika katika istilahi za vyanzo vya ‘ilmu al-rijali, maneno ambayo ingawaje yana ashiria ubora wa mpokezi, ila huwa si ishara au ushuhuda wa kuthibitisha uaminifu wake. Ila maneno hayo yaneweza kusaidia katika kuinua hadhi ya Hadithi. Maneno hayo ni kama vile "خیر" (mwenye kheri), "صالح" (mwema), "صالح الحدیث" (mwenye hadithi njema), "حَسَن" (njema), "معتمد علیه" (mtegemewa), na "من خواص الامام" (mmoja wa watu wa karibu wa Imamu). [32] Katika muktadha huo huo, kuna baadhi ya maneno yanayo onyesha udhaifu wa wapokezi, na hufuta uaminifu na uhalali wa Hadithi zilizo pokewa kutoka kwa mpokezi maalum. Maneno yanayo tumika kuionesha udhaifu wa mwanahadithi Fulani ni; ubovu wa madhehebu yake (si Shia Ithana Ashari), udhaifu wa utu au sifa mbaya za tabia ya mpokezi. [33]

Kwa Utafiti Zaidi Soma Vitabu Vifuatavyo

  • Tauthiqu ‘Aam wa Khaas “توثیقات عام و خاص”; Katika kitabu hichi, kime kusanya mada kadhaa ndani yake, kama vile maana ya thibitisho la jumla na maalum (binafsi au makhususi) na njia za kuthibitisha kila moja kati yake. Mwandishi pia amechunguza mifano ya thibitisho la jumla na maalum (binafsi). Kitabu hichi kimeandikwa kwa lugha ya Kiajemi na Muhammad Kadhim Rahman-Setaayesh kwa kushirikiana na Sayyid Kadhim Tabatabai. [34]
  • Sheria za Kuthibitisha Wapokeaji “قواعد توثیق راویان”; Kitabu hichi kinajitolea kuelezea sheria kuu za uthibitishaji juu ya uwaminifu wa wapokezi, njia za kuthibitisha uwaminifu huo, uthibitisho wa wapokeaji wa vitabu, uthibitisho wa mashekhe wa wapokezi, uthibitisho wa wapokezi kabila maalumu (kama vile Banu Fadhaal) na uthibitisho kulingana na misingi maalum inayo tumika katika fani ya ‘ilmu al-rijali. Kitabu hichi kimeandikwa na Muhammad kadhim Setaayesh kwa ajili ya kusomeshea, kikiwa katika lugha ya Kiajemi na kuchapishwa na Darul Hadith mwaka wa 1396 Shamsia. 35

Masuala Yanayo Fungamana

Rejea

Vyanzo

  • Dihkhudā, ʿAlī Akbar. Lughatnāma. Tehran: Dānishgāh-i Tehran, 1377 Sh.
  • Fīrūzābādī. Al-Qāmūs al-muḥīṭ. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, [n.d].
  • Ghulāmʿalī, Mahdī. Sanad shināsī rijāl kārburdī bā shīwa-yi barrasī-yi asnād-i riwāyat. Qom: Dār al-Ḥadīth, 1395 Sh.
  • Ibn al-Ghaḍāʾirī, Aḥmad b. Ḥusayn. Al-Rijāl. Edited by Muḥammad Riḍā Ḥusaynī Jalālī. Qom: Dār al-Ḥadīth, 1422 AH.
  • Īrawānī, Muḥammad Bāqir. Durūs tamhīdīyya fī l-qawāʿid al-rijālīyya. Qom: Intishārāt Madyan, 1431 AH.
  • Kashshī, Muḥammad b. ʿUmar al-. Rijāl. Mashhad: Muʾassisa-yi Dānishgāh-i Mashhad, 1409 AH.
  • Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Qom: Dār al-Ḥadīth, 1429 AH.
  • Marʿī, Ḥusayn ʿAbd Allāh. Muntahā l-maqāl fī l-dirāyat wa l-rijāl. Beirut: al-ʿUrwa al-Wuthqā, 1417 AH.
  • Muḥsinī, Muḥammad ʿĀṣif. Buḥūth fī ʿilm al-rijāl. Qom: Jāmiʿat al-Muṣṭafā al-ʿĀlamī, 1432 AH.
  • Najāshī, Aḥmad b. ʿAlī. Rijāl al-Najāshī. Qom: Muʾassisat al-Nashr al-Islāmī, 1365 Sh.
  • Rabbānī, Muḥammad Ḥasan. Sabk shināsī-yi dānish-i rijāl-i ḥadīth. Qom: Markaz-i Fiqhī-yi Aʾimma-yi Aṭhār, 1385 Sh.
  • Raḥmān Sitāyish, Muḥammad Kāẓim. Āshnāyī bā kutub-i rijāl-i shīʿa. Tehran: Samt, 1385 Sh.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Kamāl al-dīn wa tamām al-niʿma. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī. Tehran: Islāmīyya, 1395 AH.
  • Ṣarāmī, Sayf Allāh. Mabānī-yi ḥujjīyat-i ārā-yi rijālī. Qom: Dār al-Ḥadīth, 1391 Sh.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Ghayba. Qom: Dār al-Maʿārif al-Islāmīyya, 1411 AH.