Aya ya Udhu
- Makala hii inazungumzia na kujadili Aya ya Udhu. Ili kujua kuhusiana na hukumu za fikihi za Udhu rejea kiungo cha makala ya Udhu.
Aya ya Udhu (Kiarabu: آية الوضوء) ni Aya ya 6 katika Surat al-Maidah na ni katika Aya za hukumu za Qur’ani ambayo kupitia kwayo, wanazuoni na mafakihi wanabainisha na kuthibitisha namna ya kutia udhu na wajibu wa udhu kwa ajili ya Sala. Katika Aya hii Waislamu wameamrishwa kutia udhu kwanza kila wanapotaka kutekeleza ibada ya Sala ambapo kwanza wanatakiwa kuosha nyuso zao, na kisha mikono yao mpaka vifundoni na kisha wapake vichwa vyao na miguu yao mpaka vifundoni.
Kuna tofauti za kimitazamo baina ya mafakihi wa Kishia na Kisuni kuhusiana na namna ya kutia udhu ambapo sehemu ya tofauti hizo chimbuko lake ni ufahamu tofauti baina yao kuhusiana na Aya hii na sehemu nyingine ya tofauti hizo inatokana na hadithi ambazo kila kundi miongoni mwa makundi hayo mawili limeshikamana nazo.
Kwa mfano, mafaqihi wa Kishia, wakirejea na kutegemea Aya na Sunna za Mtume (s.a.w.w) na Maimamu Maasumu (a.s), wanaona kuwa kuosha mikono katika udhu kunatakiwa kuanzie kwenye kiwiko (kifundo) cha mkono hadi kwenye ncha za vidole; lakini mafakihi wengi wa Kisunni, wakirejea na kutegemea Aya na Sunna za Mtume na maswahaba wanasema kwamba, kuosha mikono kunapaswa kufanywa kuanzia kwenye ncha za vidole hadi kwenye viwiko.
Kadhalika Shia Imamiyyah wanasema kwamba, kwa mujibu wa Aya ya Udhu ni wajibu kupangusa miguu, na kuiosha badala ya kuipangusa ndio hatua ambayo inabatilisha udhu. Hii ni katika hali ambayo, Sunni wanaona kuwa ni wajibu kuosha miguu.
Aya ya Udhu na Tarjumi yake
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ فَاغْسِلُوا وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ وَامْسَحُوا بِرُءُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى الْكَعْبَيْنِ
Enyi mlio amini! Mnapo simama kwa ajili ya Sala basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu na miguu yenu mpaka vifundoni.
(Qur'an: Surat al-Maidah: 6)
Umuhimu na Nafasi yake
Aya ya Udhu ni Aya ya 6 katika Surat al-Maidah ambayo kupitia kwayo, wanazuoni na mafakihi wanabainisha wajibu wa Udhu kwa ajili ya Sala [1] na wanaitumia kueleza namna ya kutia udhu. [2] Vile vile Aya hii inatumiwa ili kuthibitisha suala kwamba maji yanapelekea kusafika hadathi ndogo. [3] Aya hii ni moja ya Ayaatul Ahkaam (Aya za hukumu na sheria) ambayo mbali na wafasiri, [4] wanachuoni pia wanaijadili katika vitabu vinavyohusiana na Ayat al-Ahkam. [5]
Wajibu wa Udhu kwa Ajili ya Sala kwa Mujibu wa Aya
Katika Aya ya Udhu kuna ibara hii: (...إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ، فَاغْسِلُوا ; Mnapo simama kwa ajili ya Sala basi osheni…) Hapa kuna amrisho la kutia udhu ambapo kwa mujibu wa mafakihi ibara hii ni ithbati tosha juu ya kuwa wajibu Udhu. [6]
Pia, kwa mtazamo wa mafakihi, Aya hii inabainisha kwa uwazi kwamba utohara ni sharti la kusihi Sala, [7] na inafahamika kwamba wajibu wa tohara au udhu, sio wajibu unaojitegemea, bali ni faradhi na wajibu unaofuata; [8] kwa maana kwamba, kutia udhu sio wajibu kwa mtu ambaye hataki kuswali na hivyo kuliacha hilo hakuna adhabu. [9] Kwa maneno mengine mepesi zaidi ni kwamba, udhu huwa wajibu pale mtu anapotaka kutekeleza ibada ya Sala ghairi ya hivyo sio wajibu bali nii suna na jambo lililopendekezwa kulifanya
Kuosha Nyuso na Mikono
Kwa mujibu wa fat’wa za mafakihi wa Shia na Sunni na kwa mujibu wa Aya hiyo, uso ni sehemu ya kwanza ambayo lazima ioshwe katika udhu. Kwa sababu imetajwa kwanza: «فَاغْسِلُوا وُجوهَکُم» yaani: Osheni nyuso zenu. [10] Neno Wujuh yaani “nyuso” ni wingi wa Wajih yaani “uso” . [11] Pia, kwa mujibu wa ijmaa (kauli moja) ya mafakihi wa Kiislamu ni kwamba, kwa kuzingatia kile kilichokuja katika Aya yaani: (فَاغْسِلُوا وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ ; basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni) Kuosha mikono katika udhu ni wajibu. [12] Hata hivyo kuna hitilafu za kimitazamo baina ya mafakihi ya Shia Imamiyah na Ahlu-Sunna kuhusiana na kwamba, ni kiwango gani cha mkono ambacho ni wajibu kuoshwa wakati wa kutia udhu na namna ya kuosha mikono hiyo ikoje. [13]
- Mafakuhi wa Shia Imamiya wameafikiana kwa kauli moja kwamba, katika kutia udhu kuosha pia kiwiko, na ni wajibu pia wakati wa kuosha mikono kuanzia katika kiwiko na kuielekea katika nchi za vidole yaani kuanzia juu kwenda chini; [14] hii ni kwa sababu: Kwanza kwa mujibu wa mtazamo wa baadhi neno «الی» lililokuja katika Aya ya udhu kwenye ibara ya «الی المرافق» yaani mpaka vifundoni ina maana ya «مع» yaani pamoja na. Hivyo basi kwa maana hiyo, ni wajibu kuosha kiwiko pia wakati wa kutia udhu. Yaani kuosha mkono pamoja na kiwiko. [15] Pili, iwe ni katika udhui au ghairi ya udhu, kikawaida kuosha mkono huanzia juu kwenda chini. [16] Tatu, kupitia sunna za Bwana Mtume (s.a.w.w) na Maimamu Maasumu (a.s) inafahamika juu ya wajibu wa kuosha mikono kuanzia katika viwiko hadi katika ncha za vidole na vilevile kuosha kiwiko chenyewe. [17]
- Kwa mtazamo wa akthari ya mafakihi wa Ahlul-Sunna ni kwamba, ni wajibu kuosha kiwiko katika udhu. [18] Baadhi ya mafakihi wa Ahlu-Sunna wamesema, kupitia Aya hii inafahamika kwamba, namna ya kuosha mikono inapaswa kuanzia katika ncha za vidole kuelekea upande wa kiwiko cha mkono. [19] Kwa mujibu wa Fakhrurazi ni kwamba, kwa mujibu wa mtazamo wa mafakihi wengi wa Ahlu-Sunna ni kwamba, kuosha mikono kuanzia katika kiwiko kuelekea katika nchi za vidole hakutii dosari katika usahihi wa udhu; lakini ni bora mtu anapotia udhu na anapoosha mikono aanzie katika ncha za vidole na kuelekea katika kiwiko. [20]
Kupaka
Kwa mujibu wa mtazamo wa mafakihi Waislamu ni wajibu [21] kupaka kichwa na miguu katika udhu. Wenye mtazamo huu wanategemea sehemu ya Aya ya udhu isemayo: (وَامْسَحُوا بِرُءُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى الْكَعْبَيْنِ ; na mpake vichwa vyenu na miguu yenu mpaka vifundoni). Hata hivyo kuna tofauti za kimitazamo baina ya mafakihi wa Shia Imamiya na Ahlu-Sunna pia kuhusiana na namna ya kupaka na mwanzo na mwisho wake. [22]
Kupaka Kichwa
Mashia Imamiyyah na Mashafi wanaamini kuwa, inatosha kupaka sehemu tu ya kichwa kwa kiwango ambacho inateswa kuwa amepaka maji. [23] Kwa mtazamo wa madhehebu haya mawili ni kwamba, herufi ya «باء» iliyokuja katika ibara ya «بِرُءُوسِكُمْ» yaani vichwa vyenu, ina maana ya "baadhi" na makusudio yake ni kupaka sehemu ya kichwa na sio kichwa kizima. [24] Hata hivyo Shia Imamiyah wakitegemea baadhi ya hadithi [25] na ijmaa (maafikianio ya wanazuoni) [26] wanaamini kwamba, upakaji huo unapaswa kuwa ni sehemu ya mbele ya kichwa. [27] Dhehebu la Shafii lenyewe linaamini kwamba, katika Aya hakujaainishwa sehemu ya kupaka kichwa, na kwa muktadha huo inajuzu kupaka sehemu yoyote katika kichwa wakati wa kutia udhu. [28] Kadhalika kwa mtazamo wa madhehebu ya Shafii ni kwamba, inajuzu pia kuosha au kumwagia maji kichwa wakati wa kutia udhu badala ya kupaka; lakini Shia Imamiya wanaona kuwa, haijuzu kufanya hivyo. [29]
Madhehebu ya Hanbal inaamini kwamba, ni wajibu kuosha kichwa chote na hata masikio. [30] Madhehebu ya Malik kwa upande wake inaamini kuwa, ni wajibu kuosha kichwa chote bila kuhusisha masikio. Madhehebnu ya Hanafi yenyewe inaamini kwamba, ni wajibu kupaka robo ya kichwa (moja ya nne) na inatosha pia kuingiza kichwa ndani ya maji au kumwagia maji juu yake. [31]
Kupaka Miguu
Kuna tofauti kubwa za kimitazamo baina ya mafakihi wa Shia Imamiya na Ahlu-Sunna kuhusiana na kupaka juu ya miguu au kuosha wakati wa kutia udhu. [32] Shia Imamiyah wakitegemea Sunna za Bwana Mtume (s.a.w.w) na Maimamu watoharifu (a.s) [33] na hoja ya ijmaa [34] wanaamini kwamba, ni wajibu kupaka miguu kuanzia katika ncha za vidole mpaka katika vifundo na kuosha badala ya kupaka kunabatisha udhu; hii ni katika hali ambayo, akthari ya mafakihi wa Ahlu-Sunna wakitegemea Sunna za Bwana Mtume (s.a.w.w) [35] na ijmaa ya masahaba [36] wanaamini kwamba, ni wajibu kuiosha mpaka katika vifundo na sio ku paka.
Hitilafu katika Usomaji wa Aya
Kuna usomaji au visomo vya aina mbili katika Aya ya Udhu:
- Katika visomo au usomaji wa Ibn Kathir, Hamza bin Habib, Abu Amr na vilevile usomaji wa Abu Bakr Ayyash kutoka kwa Asim ni kwamba, neno «أَرْجُلِكُمْ» limeunganishwa na «بِرُءُوسِكُمْ» na limekuja kwa sura ya Majrur (kwa kasr). [38]
- Katika visomo au usomaji wa Nafi’, Abu Amir na Kisomo cha Hafs kutoka kwa Asim neno «أَرْجُلَكُمْ» limekuja kwa sura ya Mansub (kwa fat’h). [39] Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana baadhi ya mafakihi wa Kisuni wamesema, neno «أَرْجُلَكُمْ» linaunanganishwa na «وُجُوهَكُمْ» ambalo ni mansub. Kwa msingi huo inapatikana natija kwamba, kama ambavyo kuosha uso katika udhu ni wajibu, vivyo hivyo ni wajibu pia kuosha miguu na haitoshi kupangusa miguu; [40 hata hivyo wanazuoni wa Kishia wana mtazamo tofauti kabisa na huo. Wao wanasema: Neno «أَرْجُلَكُمْ» hapa pia limeunganishwa na «بِرُءُوسِكُمْ» na licha ya kuwa kidhahiri «بِرُءُوسِكُمْ»، ni majrur (kwa kasr ya herugi ya baa), lakini kwa kuwa ni maf'uul; kwa mujibu wa kanuni za lugha ya Kiarabu lipo katika nafasi ya nasb na ni katika sehemu ya mansub. [41]