Nenda kwa yaliyomo

Kisomo cha Hafs kutoka kwa Asim

Kutoka wikishia
Kitabu kitukufu, Al-Qur'an Al-Kariim

Kisomo cha Hafs kutoka kwa Asim (Kiarabu: قرائت حفص از عاصم) ni riwaya na hadithi mashuhuri ya kisomo cha Asim bin Abi al-Najud Kufi mmoja wa wasomaji wa visomo saba mashuhuri vya Qur’ani ambayo imenukuliwa na mwanafunzi wake Hafs bin Sulayman Asadi. Abu Bakr bin Ayyash pia amenukuu qiraa na kisomo cha Asim; lakini hadithi na riwaya ya Hafs imeondokea kuwa mashuhuri zaidi. Riwaya ya Hafs imekubaliwa zaidi kutokana na itifaki na ufasaha wake na kutokana na kuwa ina tofauti ndogo sana kulinganisha na qiraa cha Asim. Hii leo kisomo hiki kinatumika na kimeenea kwa asilimia 95 katika nchi za Kiislamu.

Watambuzi wa visomo wanaamini kuwa, riwaya ya Hafs kuhusu kisomo kutoka kwa Asim na kuunganishwa sanadi na mapokezi yake kwa Mtume (s.a.w.w) ni sahihi na wanasema kuwa, Asim amechukua kisomo chake kutoka kwa Imamu Ali (a.s) kukiwa na pengo la mtu mmoja tu katikati yaani kupitia kwa Abu Abdul-Rahman Sullami. Asim ametambuliwa kuwa mtu thiqah (muaminifu) na mtu aliyekuwa mcha Mungu na kisomo chake kimetambuliwa kuwa fasaha zaidi miongoni mwa visomo. Kadhalika Hafs ametambuliwa kuwa, mwanafunzi msomi na mweledi zaidi miongoni mwa wanafunzi wa Asim kuhusiana na qiraa yake na kisomo chake kimetambuliwa kuwa cha kuaminika na makini. Abu Abdul-Rahman Sullami naye ametambulishwa kuwa mtu mwaminifu na mwenye adhama.

Kuhusiana na kwamba, ni wakati gani qiraa na kisomo cha Asim kwa riwaya ya Hafs kiliondokea kuwa mashuhuri katika nchi za Kiislamu kuna nadharia na mitazamo tofauti:Muhammad-Hadi Maarifat anasema kuwa, tangu mwanzo kisomo hiki kilikuwa kimeenea na kilikuwa kikikubaliwa na wote. Baadhi pia wana mtazamo huu kwamba, kuenea na kukubaliwa na wote kisomo cha Asim kwa riwaya ya Hafs, kulianzia karne ya 10 Hijiria na hilo lilitokana na juhudi za serikali ya Utawala wa Othmania.

Nafasi na umuhimu wake

Kisomo cha Hafs kutoka kwa Asim, ni riwaya ya Hafs bin Sulayman Asadi Kufi kuhusu kisomo cha mwalimu wake yaani Asim bin Abi al-Najud Kufi moja ya visomo saba mashuhuri vya Qur’ani. [1] Inasemekana kisomo hiki ni miongoni mwa visomo ambavyo ni mutawatir na vilivyokubaliwa na Waislamu wote. [2] Muhammad Ismail Muhammad al-Mash’hadani, mtafiti na mwalimu wa Nahw na visomo vya Qur’ani katika Chuo Kikuu cha Mosul Iraq anasema kuwa, hii leo takribani kisomo cha Asim kwa riwaya ya Hafs kimeenea kwa asilimia 95 ya nchi za Kiislamu na asilimia 5 nyingine iliyobakia ya nchi zingine zinatumia visomo vingiine kati ya visomo saba mashuhuri. [3]

Hata hivyo kuna kundi kubwa ambalo limepokea kisomo cha Asim kupitia kwa watu wengine au bila kupitia kwa watu wengine. [4] Hata hivyo riwaya ya Hafs na vilevile riwaya ya Abu Bakr bin Ayyash zimeondokea kuwa mashuhuri zaidi. [5]

Itibari ya kisomo cha Asim

Watambuzi wa visomo wanaamini kuwa, riwaya ya Hafs kuhusu kisomo kutoka kwa Asim na kuunganishwa sanadi na mapokezi yake kwa Mtume (s.a.w.w) ni sahihi; [6] kwani Asim amechukua kisomo chake kutoka Abu Abdul-Rahman Sullami na yeye amechukua kama kilivyo kutoka kwa Imamu Ali (a.s). Kadhalika Asim amechukua riwaya hii kutoka kwa Zar bin Habish ambapo yeye amejifunza kutoka kwa Abdallah bin Mas’oud na Abdallah bin Mas’oud amechukua kutoka kwa Mtume (s.a.w.w). [7] Kwa upande mwingine kisomo hiki amekinukuu Hafs ambaye ni mtu makini zaidi miongoni mwa wapokezi wa Asim na mwanafunzi wake msomi na mweledi zaidi ya wanafunzi wake wengine. [8]

Muhammad-Hadi Maarifat mtafaiti wa masuala ya Qur’an na Fiqhi wa Kishia (aliaga dunia 1385 Hijiria Shamsia) anaamini kwamba, kisomo cha Hafs kutoka kwa Asim, ni kisomo pekee ambacho kina sanadi na mapokezi sahihi na kuanzia mwanzo kilipata nguvu kutokana na himaya na uungaji mkono wa Waislamu wote na katika kipindi cha karne zote, kimeenea kutoka kizazi hadi kizazi kingine na mpaka leo kimeenea na kuzoeleka miongoni mwa Waislamu. [9]

Ibn Nadim anasema, Asim alichukua kisomo chake kutoka kwa Abu Abdul-Rahman Sullami na Zar bin Habish; [10] lakini Abu Bakr bin Ayyash mpokezi mwingine wa kisomo cha Asim anasema: Asim aliniambia, hakuna mtu yeyote aliyenifundisha Qur’ani ghairi ya Abu Abdul-Rahman Sullami na mimi nilipokuwa nikirejea kutoka kwake nilikuwa nikimpatia Zar bin Habish yale niliyojifunza. [11]

Kuna hitilafu kuhusiana na suala kwamba, Sullami mwenyewe alijifunza Qur’ani kutoka kwa sahaba gani miongoni mwa masahaba wa Mtume (s.a.w.w): [12] Baadhi wamesema, alijifunza Qur’ani kutoka kwa Imamu Ali (a.s), Othman na Abdallah bin Mas’oud. [13] Imenukuliwa kutoka kwa baadhi ya kwamba, alijifunza Qur’ani kutoka kwa Imamu Ali (a.s). [14] Imeelezwa pia kwamba, alijifunza Qur’ani kutoka kwa Othman. [15].

Kuenea kisomo cha riwaya ya Hafs kutoka kwa Asim

Inaelezwa kuwa, kuchaguliwa kisomo cha Hafs kwa riwaya ya Asim na serikali ya utawala wa Othman na kuenezwa misahafu kwa mujibu wake takribani katika karne ya 10 Hijiria, ilikuwa sababu ya kuenea kwa kisomo hiki na kujikitika kwake katika jamii ya Kiislamu.

Tofauti ya kisomo cha Hafs na Asim

Inaelezwa kuwa, kisomo cha Hafs kinatofauti moja tu na kisomo cha Asim nayo ni usomaji wa neno Dhu’f katika Aya ya 54 ya Surat al-Rum ambapo Asim amesoma kwa fataha na Hafs amesoma kwa Dhumma. [33] Hii ni katika hali ambayo, baina ya kisomo cha Hafs na kisomo cha Abu Bakr bin Ayyash ambaye pia amechukua kisomo chake kutoka kwa Asim kumeripotiwa hitilafu zaidi ya 500. [34] Kuhusiana na sababu ya hitilafu za kisomo cha Hafs na Abu Bakr bin Ayyash imeelezwa kwamba, ni kuwa, kisomo alichojifunza Asim kutoka kwa Zar bin Habish na ambapo yeye (Zar bin Habish) alijifunza kutoka kwa Abdallah bin Mas’oud alimfundisha Ayyash. [35].

Monografia

Baadhi ya athari na vitabu vilivyoandikwa kuhusiana na kisomo cha Hafs kutoka kwa Asim ni:

  • Ahamiyat Qeraat Asim be revayat Hafs, mwandishi Akram Khodaei Esfahani. Katika faslu ya kumi anailinganisha riwaya ya Hafs na Abu Bakr bin Ayyash. [45] Katika faslu ya 11 ameitenga maalumu kwa ajili ya tofauti baina ya kisomo cha Asim na visomo vingine. [46]
  • Mabahith fi elm al-Qeraat maa bayan usul riwayat Hafs, Mwandishi Muhammad bin Abbasbaz. Awali mwandishi anawatambulisha Hafs na Asim na kisha anabainisha sanadi na mapokezi ya hadithi ya Hafs kwa kisomo cha Asim. Kisha baadaye anachunguza na sifa maalumu na misingi yake. [47]
  • Al-Qimat al-Dalaliyah Liqeraat Asim bi riwayat Hafs, mwandishi, Muhammad Ismail al-Mash'hadani. Katika kitabu hiki mwandishi mbali na kujadili jinsi muuundo wa neno na maana unavyoweza kubadilika kutokana na usomaji anafadhilisha Qeraa na kisomo cha Asim kwa riwaya ya Hafs mbele ya visomo vingine. [48] Kitabu hiki kinaundwa na utangulizi mmoja na faslu tatu na faslu moja ya hitimisho. [49]

Rejea

Vyanzo