Nenda kwa yaliyomo

Ahlul-Kitab

Kutoka wikishia

Ahlul-Kitab (Watu wa Kitabu): ni istilahi maalumu iliyotumiwa na Uislamu ikirejelea watu watu maalumu wasio Waislamu, ambao hutambuliwa kama ni wafuasi wa dini zenye maandiko ya ufunuo kutoka mbinguni. Maulamaa wa dini ya Kiislamu (wa upande wa madhehebu ya Shia) huwaainisha; Wayahudi, Wakristo, na Wazoroasta katika kategoria ya Ahlul-Kitab. Utafiti wa kihistoria unaonyesha kuwepo kwa majadiliano na mazungumzo kati ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Watu wa Kitabu. Utafiti huo umeweza kutufikishia baadhi ya majadiano hayo, ambapo bwana Mtume (s.a.w.w) ameonekana kusimama na kujibu hoja za Ahlul-Kitab. Miopngoni mwa mahojiano hayo, ni pamoja na midahalo ya kitaaluma kati yake na wanazuoni wa wafwasi wa dini za watu wa Ahlul-Kitab. Pia miongoni matukio kati ya Waislamu na watu wa Ahlul-Kitab, ni kutiwa saini kwa baadhi ya mikataba ya amani ili kuhakikisha maisha ya pamoja yenye utulivu kati yao na Waislamu. Katika Fik'hi ya Kiislamu, kuna hukumu kadhaa zililzobainishwa kuhusiana na namna ya kuamiliana na watu wa Ahlul-Kitab. Miongoni mwa hukumu hizo ni zile zisemazo kwamba: iwapo watu wa upande wa Ahlul-Kitab watataka kuishi katika ardhi ya Kiislamu, basi watalazimika kuukubali Uislamu au watalazimika kulipa jizya (fidia maalumu), kinyume na hivyo, Waislamu watawajibika kusimamisha jihadi dhidi yao. Pia ni haramu kwa Waislamu kuwaozesha binti zo kwa wasiokuwa Waislamu, si ndoa ya daima wala si ndoa ya muda. Pia fatwa za mafaqihi wengi, zinasema kwamba; Ahlul-Kitab ni najisi, aidha si halali kula kichinjwa kilichochinjwa na watu wa Ahlul-Kitab.

Ufafanuzi wa Dhana ya Ahlul-Kitab "Ahlul-Kitab" ni istilahi ya kifiqhi na kishari'a inayowarejelea makafiri (wasiokuwa Waislamu) wenye kumiliki kitabu cha ufunuo wa mbinguni. [1] Mafuqaha wa Kishia huwaainisha Wayahudi, Wakristo na Wamajusi (Wazoroasta) kama vielelezo hai vya istilahi hii. [2] Kwa mujibu wa maelezo ya Sheikh Tusi, ni kwamba; kuna msingi thabiti wa ijmai, ya kwamba, hukumu za kifiqhi zinazohusiana na Ahlul-Kitab, hazihusiani kabisa wala haziwajumuishi Wasabai ndani yake. Hivyo basi uhusishwaji wao na kategoria hii unahitaji dalili madhubuti za kisheria. [3] Hata hivyo, wanazuoni mashuhuri kama Sayyid Abulqasim Khui [4] na Sayyid Ali Khamenei [5] wanawatambua Wasabai kama ni moja kati ya watu wa Ahlul-Kitab. Istilahi ya Ahlul-Kitab imekuja kinyume na istilahi ya Ahlul-Qibla, ambayo ni istilahi inayohusiana na Umma wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), ambao ni wafuasi wa Qur'ani Tukufu. [6] Sheikh Ahmad Pakatchi, mtafiti wa Kishia, akitoa mawazo yake kuhusiana na Ahlul-Kitab, anabainisha akisema; tukizingazia Aya za Qur'ani, tutakuta kwamba, wakati wa kudhihiri Uislamu kundi hili dogo la watu Ahlul-Kitab lilikuwa upande mmoja, huku upande wa pili kukikuwa moja kundi kubwa la Ummiyyuna. Kwa aghalabu, Ummiyyuna Hawa walikuwa ni washirikina wa Bara Arabu ambao hawakupata neema ya kujua kusoma na kuandika, wala hawakuwa na Kitabu cha mbinguni. [7]

Taswira na Sifa za Ahlul-Kitāb Katika Qur'ani Tukufu Miongoni mwa jumla ya majina yaliyotumiwa na Qur'ani kuhusiana na Ahlul-Kitāb (Watu wa Kitabu) ni pamoja na: «Ahlal-Kitab» (Watu wa KItabu), «Alladhina Kafaru» (Waliokufuru), «Alladhina Ataynahumul- Kitab» (Wale Tuliowapa Kitabu) na «Alladhina Utul- Kitab» (Wale Wliopewa Kitabu). [8] Wanazuoni wanasema kuwa; Qur'ani imetoa ufafanuzi wa kutosha kabisa kuhusiana na suala la Ahlal-Kitab, ufafanuzi ambao unapatikana katika Aya kadhaa za Qur’ani tukufu. Qur’ani inawasifu baadhi yao kwa sifa kadhaa njema ikiwemo; imani, uaminifu na ukweli, huku ikiwakemea wengine vikali na kuwasifu kwa sifa mbali mbali zisizopendeza, kama vile; chuki na uadui. Zifa hizi mbaya ni kwa wale waliopotoka miongoni mwao ambao husimama kidete dhidi ya Waislamu. [9] Aidha, miongoni mwa sababu za upotofu wa kundi hili zilizoashiriwa na Qur’ani ni pamoja na; kuifahamu dini isivyo sawa, kughushi maandiko ya kidini (tahrif), husuda pamoja na kuvunja ahadi. [10]

Namna Bwana Mtume (s.a.w.w) Alivyoamiliana na Watu wa Kitabu Moja ya kundi la wafasiri wa Qur’ani wa madhehebu ya Shia wamesema kwamba; wakati bwana Mtume (s.a.w.w) alipokuwa Makkah, hakuwa na majadiliano ya kidini wala mizozo ya kijeshi kati ya Waislamu na Watu wa Kitabu, kwani wakati huo hapakuwepo na watu wa Ahlal-Kitab waliokuwa wakiishi katika mji huo. [11] Watafiti wamejaribu kuchambua jinsi bwana Mtume (s.a.w.w) alivyokuwa akiamiliana na Watu wa Kitabu, hatua kwa hatua, huku lengo kuu likiwa ni kuwakaribisha watu hao katika Uislamu. [12] Katika wito huu, awali bwana Mtume (s.a.w.w) alionekana kutumia mbinu kadhaa zenye mvuto wa kitamaduni, pamoja na kujadiliana na kwa njia bora kabisa, kwa ajili ya kuwavutia na kuwaita katika dini ya Uislamu. [13] Alijibu maswali ya wanazuoni wao na kuhoji itikadi zao potofu. Aidha, alithibitisha ujumbe halisi wa mitume wao, huku wito wake ulijikita kwenye misingi ya imani wanayoshirikiana nayo pamoja. [14] Ili kudumisha amani kati ya Waislamu na watu wa Ahlal-Kitab, bwana Mtume (s.a.w.w) aliamua kuingia katika mikataba ya suluhu na Ahlul-Kitab [15] mikataba amabayo ilisimama kama ni kizuizi dhidi ya maadui mbali mbali. [16] Kwa mujibu wa maelezo ya Sayyid Abu al-Qasim Khui, ni kwamba; vita dhidi ya Ahlul-Kitab vilijiri tu chini ya mazingira matatu maalumu: pale wao walipoanzisha uhasama wa kijeshi, wao kujihusisha na fitina, na pale wao waliposimama na kususia ulipaji wa Jizya (fidia maalumu). [17] Kwa mujibu wa moja ya Riwaya, ni kwamba; bwana Mtume (s.a.w.w) aliwaelekeza makamanda wa kijeshi kuwalingania watu wa Ahlul-Kitab ili kuukubali Uislamu kabla kuanzisha vita dhidi yao, na endapo watakataa, basi aliamuru wapewe fursa nyengine ambayo ni kulipa Jizya na kutii masharti yaliyowekwa na bwana Mtume (s.a.w.w). [18] Watafiti wa historia wamehitimisha wakisema kuwa; chanzo cha baadhi ya vita kama vile; Khandaq na Khaybar vilitokana na hujuma na ufadhili wa kifedha wa Wayahudi dhidi ya Waislamu. [19]

Hukumu za Kifiqhi Mafiqihi wa Kishia, wamebainisha wazi hukumu zinazowahusu Ahlul-Kitab katika milango mbalimbali iliyomo katika vitabu vya fiqhi. Baadhi ya hukumu hizo ni kama ifuatavyo: • Maisha yao katika Darul-Islam: Ahlul-Kitab wanaoishi katika Dola ya Kiislamu, hupewa hiari na kiongozi wa Kiislamu baina ya mambo mawili: kuukubali Uislamu, au kuishi chini ya masharti ya Kafir Dhimmi (Kafiri aliyeko chini ya himaya ya Dola ya Kiislamu) na kulipa Jizya. Wakikataa yote mawili, pamoja na masharti kutimia, hapo basi inapasa kupigana nao Jihad. [20] • Tohara na Unajisi Wao: Kwa mujibu wa kauli ya Sayyid Abul-Qasim Khui (faqīhi wa Kishia), ni kwamba; Hukumu ya unajisi wa Ahlul-Kitāb ndiyo kauli mashuhuri zaidi miongoni mwa Mafiqihi wa Kishia. Hata hivyo, baadhi ya Mafiqihi wa kale (Mutaqaddimuna) pamoja na kundi fulani la wanazuoni wa zama za mwisho (Muta'akhkhiruna) wametoa fatwa ya utohara kwa Kafir aliye upande wa Ahlul-Kitab. [21] • Jizya na Ulinzi: Kuna makubaliano katika fatwa za Mashia Imamiyya na Ahlus-Sunna ya kwamba; ni wajibu kwa Dola ya Kiislamu kupokea Jizya kutoka kwa Ahlul-Kitab ili kuwaruhusu waishi katika miji ya Kiislamu, na wajibu wa dola ya Kiislamu kulinda dhidi ya madhara mbali mbali. [22] Kwa kukubali masharti ya Kafir Dhimmi na kulipa Jizya, hii itapelekea kutambulika rasmi kama raia wa Dola ya Kiislamu, na serikali itabidi kuchukua jukumu la kuwalinda na kuwapa usalama, na hivyo watapata haki za kisheria kama ilivyo kwa raia wengine. [23] • Ndoa: Mafiqihi wa Kishia hutofautisha baina ya ndoa ya kudumu na ndoa ya muda (Mut'a), hii ni kwa mwanamme Mwislamu anayetaka kufunga ndoa na mwanamke wa kutokea upande wa Ahlul-Kitabu. Wao wanaihalalisha ndoa ya muda na kuiharamisha ndoa ya kudumu katika sekta hii. [24] Baadhi ya wanazuoni kama vile Muhaqqiq al-Hilli na Faidhu Kashani wamesema kwamba; hii ndiyo kauli mashuhuri zaidi miongoni mwa wanazuoni wa madhehebu ya Shia Maimamiyya. [25] Hata hivyo, kuna ripoti isemayo kuwa; kauli mashuhuri miongoni mwa wanazuoni wa kale ilikuwa ni uharamu wa kufunga ndoa ya aina yoyote ile na watu wa Ahlul-Kitab. [26] Pia, kuna Ijmaa (makubaliano) kutoka Fiqhi za pande zote mbili, Shia pamoja na Sunni ya kwamba; haijuzu kwa mwanamke Mwislamu kuolewa na mwanamume asiye Mwislamu, hata atakuwa wa kutokea upande wa Ahlul-Kitab. [27] • Dhabihu (Vichinjwa): Sheikh Baha'i akielezea suala hili ameripoti akisema kuwa; Mafiqihi wengi wa Kishia, kama vile Sheikh Tusi, Sheikh Mufid, Sayyid Murtadha na Shahid al-Awwal, wanaharamisha kula nyama ya mnyama aliyechinjwa na Ahlul-Kitab, nyama hiyo itendelea kuwa haramu hata kama watakuwa wametaja jina la Allah wakati wa kumchinja myama huyo. [28] Pia Imamu Khomeini (r.a) anashikilia msimamo huu huu kuhusiana na hukumu hii. [29] Kwa mujibu wa maelezo ya Sheikh Baha'i, ni kwamba; kuna Mafiqihi wachache tu wanaohalalisha kichinjwa cha watu wa Ahlul-Kitab. [30] • Kuingia Msikitini: Kwa Mtazamo wa baadhi ya Mafiqihi ni haramisha kwa Ahlul-Kitab kuingia msikitini. Miongoni mwa wale waliotoa hukumu hii ni pamoja na; Allamah al-Hilli na Sahibu ar-Riyadh. Na kwa mujibu wa mtazamo wa Allamah al-Hilli, hakuna Mwislamu anayeruhusiwa kuwapa idhini watu hawa kuingia msikitini. [31] • Uharamu wa Kumzika Kafiri Kwenye Mava ya Waislamu: Haijuzu kwa Muislamu kumzika kafiri kwenye mava ya Waislamu, awe wa upane wa Ahlul-Kitab au asiye wa upande huo. [32] Watu wa Kitabu katika Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Kifungu cha kumi na tatu cha Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kinawatambua Wazoroasta, Wayahudi na Wakristo wa Iran kama ni makundi pekee ya wachache wa kidini, ambao wanaruhusiwa kwa mujibu wa sheria kutekeleza mambo yao binafsi na ibada zao za kidini kulingana na mila zao nchini Iran. [33] Monografia • Moja kati ya vitabu muhimu vilivyoandikwa katika uwanja huu, ni kitabu kiitwacho “Ahkamu Ahl al-Kitab fi al-Islam” kilichoandikwa na Ali Saidi Shahrudi mnamo mwaka 1384 Shamsia (sawa na mwaka 2005 Miloadia), na kuchapishwa na Majma’a Dhakha’ire Islami. Hichi ni kitabu kinachambua masuala ya Ahl al-Kitab na hukumu zao katika sura tatu. • Makala yenye jina la Irtibate Ahlul-Kitabe wa Shiweye Barkhord ba Aanaan az Diidgaahe Qura’ne wa Hadiith (Uhusiano na Ahl al-Kitab na Namna ya Kuamiliana Nao kwa mtazamo wa Qur’ani na Hadithi), nayo ni makala iliyoandikwa na bwana Mansur Qasimi. katika makala yake hii Qasimi akitumia Aya pamoja na riwaya mbali mbali, anajadili vya kutosha mipaka ya uhusiano na baadhi ya hukumu za Ahl al-Kitab. [34] Mada Zinazohusiana: Kafiri Dhimmi Jizya Haki za wachache wa kidini