Nenda kwa yaliyomo

Khaybar

Kutoka wikishia
Ngome ya Khaybar

Khaybar (Kifarsi: خیبر) ni eneo ambalo kijiografia linapatikana nchini Saudi Arabia ambapo Vita vya Khaybar vilitokea na kupiganwa katika eneo hilo. Eneo la Khaybar lipo umbali wa kilomita 165 kutoka katika mji wa Madina na makao makuu yake ni mji wa al-Shurayf. Wakazi wa Khaybar mwanzoni mwa Uislamu walikuwa Mayahudi. Kwa mujibu wa wanahistoria wa Kiislamu, kwa sababu walikuwa wakiwachochea viongozi wa Makka kuwashambulia Waislamu, Mtume (s.a.w.w) alikata shauri kupigana nao.

Eneo la Khaybar lilikuwa na ngome kadhaa na wengine wamesema kwamba liliitwa Khaybar (ngome) kwa sababu hii. Katika Vita vya Khaybar, ambayo vilitokea katika mwaka wa saba Hijiria, Waislamu walishinda kwa kuziteka ngome za Khaybar. Baadhi ya ngome hizo zilitekwa na kukombolewa na Imamu Ali (a.s). Baada ya vita, Mayahudi hawakufukuzwa katika eneo hilo, lakini yalipita makubaliano baina ya pande mbili kwamba, watakuwa wakilipa nusu ya mazao yao ya kilimo kwa Waislamu.

Kulingana na vyanzo vya kihistoria, Mayahudi waliishi katika eneo hilo hadi wakati wa utawala wa Omar bin al-Khattab, Khalifa wa Pili, ndipo alipowalazimisha kuondoka katika eneo hilo.

Sababu ya kuitwa kwa jina hilo

Kuna riwaya na hadithi tofauti kuhusiana na sababu ya kwa nini eneo hilo liliitwa Khaybar. [1] Kulingana na Yaqut Hamawi, msomi na mwanajiografia, Khaybar ni neno la Kiebrania linalomaanisha ngome, na kwa sababu kulikuwa na ngome kadhaa katika eneo hilo, hivyo likaondokea na kujulikana kama "Khayabir". [2] Wengine pia wamesema kwamba sababu ilikuwa kwamba mtu wa kwanza kuishi hapo aliitwa Khaybar. [3]

Yaqut Hamavi alitaja ngome saba katika eneo hili, [4] Ya'qoubi alizingatia idadi ya ngome hizo kuwa ni sita [5] na katika kitabu cha historia ya Mtume wa Uislamu, imeripotiwa kwamba ngome kumi zilitekwa na kukombolewa na Waislamu katika ushindi wa Vita vya Khaybar. [6] Katika kitabu cha al-Sahih Min Sira al-Nabi cha Sayyid Ja’afar Murtadha al-Amili anasema, Mayahudi walikuwa na ngome nane huko Khaybar. [7]

Hali ya kijiografia

Muonekano wa eneo la Khaybar

Eneo la Khaybar liko Saudi Arabia na kaskazini mwa mji wa Madina. Eneo hili liko umbali wa kilomita 165 kutoka Madina. Makao makuu yake ni mji wa al-Shurayf. Wakazi wa Khaybar mwanzoni mwa Uislamu walikuwa Mayahudi. [8] Hapo awali, kulingana na Yaqut Hamavi, Khaybar ilikuwa na vituo (mafikio) nane [9] au umbali wa siku tano [10] kutoka Madina. Khaybar ilijulikana kama eneo lenye rutuba na ilikuwa na chemchemi nyingi na mashamba mengi na miti ya tende. [11]

Historia fupi

Wakati wa vita vya Waislamu na watu wa Khaybar, yaani, katika Vita vya Khaybar, wakazi wa eneo hili walikuwa Mayahudi. Ni vigumu kuainisha wakati na kipindi cha kuwasili kwa Wayahudi katika eneo hili. Baadhi ya ripoti zimetangaza kuwa, wakati wa shambulio la Warumi dhidi ya Palestina kulikwenda sambamba na kuingia Mayahudi katika eneo la Khaybar. Kundi fulani pia linasema kwamba Wayahudi walihajiri na kuhamia eneo hili kabla ya wakati wa utawala wa Wababiloni kwa Baytul-Muqaddas (Jerusalem). [12]

Baada ya ushindi wa Waislamu katika Vita vya Khaybar, mali za eneo hilo zilitolewa kwa Waislamu kama ngawira; lakini kwa ombi la Mayahudi waliokuwa wakiishi Khaybar, Mtume (saww) aliwaruhusu kukaa Khaybar, kwa sharti kwamba walipe nusu ya mazao yao ya kilimo kwa Waislamu. [13]

Kwa mujibu wa wanahistoria, Mayahudi waliishi Khaybar hadi kipindi cha Khalifa wa pili, Omar bin Khattab, alipowalazimisha kuhama kwa kutaja riwaya iliyonasibishwa kwa Mtume (s.a.w.w) kwamba dini mbili haziwezi kuwa pamoja katika Bara Arabu. [14]

Vita vya Khaybar

Makala asili: Vita vya Khaybar
Ufunguzi wa Khaybar,(picha inayoakisi namna mlango wa Kasri ya Khaybar ulivyong'olewa kwa mkono wa Imam Ali (a.s))

Katika mwaka wa saba Hijria, Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) aliishambulia Khaybar akiwa na jeshi. [15] Katika vita hivi Waislamu waliteka ngome za Khaybar na wakashinda. [16] Vita hivi viliitwa Vita vya Khaybar. [17] Wanahistoria wanasema kuwa, sababu ya kutokea vita hivi ni kwamba, Mayahudi wa Bani Nadhir, waliofukuzwa kutoka Madina na kwenda Khaybar baada ya njama ya kutaka kumuua Mtume, walikuwa wakiwachochea viongozi wa Makka kupigana dhidi ya Waislamu. [18]

Kwa mujibu wa riwaya ya Ibn Hisham, mwanahistoria wa karne ya tatu ya Hijria, Mtume (s.a.w.w) alimpa Abu Bakr bendera ya ukamanda wa jeshi na kisha Omar Ibn Khattab wakati wa kutekwa kwa ngome moja ya Khybar. Lakini wote wawili walirudi bila ushindi. Baada ya hayo, alikabidhi bendera kwa Imam Ali (a.s) na akaahidi kwamba ngome hiyo itatekwa na kukombolewa naye, na akaiteka ngome hiyo. [19]

Rejea

Vyanzo

  • ʿAlī, Jawād. Al-Mufaṣṣal fī tārīkh al-ʿarab qabl al-Islām. Beirut: Dār al-ʾIlm li-l-Malāyīn, 1391 AH.
  • Āyatī, Muḥammad Ibrāhīm. Tārīkh-i payāmbar-i Islām. Edited by Abu l-Qāsim Gurjī. Tehran: Intishārat-i Dānishgāh-i Tehran, 1378 Sh.
  • Ḥamawī, Yāqūt b. ʿAbd Allāh al-. Muʿjam al-buldān. Beirut: Dār al-Ṣādir, 1995.
  • Ibn Hishām, ʿAbd al-Malik. Al-Sīra al-nabawīyya. Edited by Muṣṭafā al-Saqā, Ibrāhīm Ābyārī and ʿAbd al-Ḥafīz Shalbī. Beirut: Dār al-Maʿrifa, [n.d].
  • Nahrawānī, Muḥammad b. Aḥmad. Tārīkh al-madina. Port Said (Egypt): Maktabat al-Thiqāfa al-Dīnīyya, [n.d].
  • Nājī, Muḥammad Riḍā. Khaybar, Ghazwa. In Dānishnāmah-yi Jahān Islām. Tehran: Bunyād-i Dāʾirat al-Maʿārif al-Islāmī, 1375 Sh.
  • Wāqidī, Muḥammad b. ʿUmar al-. Al-Maghāzī. Edited by Marsden Jones. Beirut: Muʾassisa al-Aʿlām, 1409 AH.
  • Yaʿqūbī, Aḥmad b. Abī Yaʿqūb al-. Tārīkh al-Yaʿqūbī. Beirut: Dār Ṣādir, [n.p].