Adhabu ya kupiga mawe

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Adhabu ya Mzinifu)

Kupiga Mawe au Rajm (Kiarabu: الرجم) ni adhabu ambayo mhukumiwa hufukiwa ardhini mpaka kimo cha kiuno au kifua na kisha hupigwa mawe mpaka afe. Kupiga mawe ni katika hudud (adhabu zisizo za kimali) na ni adhabu kwa ajili ya mzinifu Muhsanah yaani mwanaume au mwanamke aliyezini ambaye ana mke au mume (yuko katika ndoa) na vilevile adhabu hii hutekelezwa dhidi aliyefanya liwati endapo mtawala wa kisheria atachukua uamuzi huo. Uthibitisho na utekelezaji wa kupiga mawe una masharti; ikiwa ni pamoja na kuwa na kuwa katika ndoa ya daima na wakati wa kufanya kwake zinaa kulikuwa na uwezekano wa yeye kufanya tendo la ndoa na mwebnza wake.

Baadhi ya Marajii Taqlid wametoa fat’wa ya kutekeleza adhabu mbadala badala ya upigaji mawe kutokana na kuuamini kwao kwamba, kutekeleza adhabu hii katika zama hizi sio kwa maslahi ya Uislamu.

Pia, katika Torati, adhabu za makosa kama vile kumchinja mtoto na kumtoa kafara kwa ajili ya sanamu, uchawi, kufuru, kuuvunjia heshima siku ya Jumamosi (Sabato) na uzinzi zimetajwa kuwa ni kupigwa mawe.

Utambuzi wa Maana na Namna ya Kuitekeleza

Kupiga mawe au rajm katika fikihi ya Kiislamu ni miongoni mwa adhabu au hudud (zisizo za kimali) na hutekelezwa katika makosa kama ya zinaa kwa kutumia masharti maalumu. [1] Kupiga mawe au rajm ni adhabu ambayo mhukumiwa hufukiwa ardhini mpaka kimo cha kiuno au kifua na kisha hupigwa mawe mpaka afe. [2]

Inaelezwa kuwa, Muhaqqiq Hilli anaamini kuwa, katika kutekeleza adhabu ya kupiga mawe, mwanaume anapaswa kufukiwa ardhi mpaka usawa wa kiuno na mwanamke afukiwe mpaka kifuani. Kama kosa limethibiti kupitia ushahidi wa mashuhuda, ni wajibu kwa mashahidi kuanza kumpiga mawe mhalifu na kama kosa limethibiti kwa mhusika kukiri mwenyewe basi Mtawala wa Kisheria ndiye anayepaswa kuanza kumpiga mawe mhalifu. [3]

Kama mzinifu atakimbia wakati wa kutekelezwa hukumu dhidi yake, kama adhabu yake ilikuwa ni kupigwa mawe na hilo lilithibiti kwa ikirari na ungamo lake, kwa mujibu wa mtazamo mashuhuri, hatoadhibiwa tena (kwa maana kwamba, hakuna haja ya kumtafuta na kumkamata na kisha kumuadhibi tena); lakini kama adhabu yake itakuwa ni kuchapwa mijeledi au kupigwa mawe kulikothibiti kupitia ushahidi wa mashuhuda, atakamatwa na kurejeshwa kwa ajili ya kuadhibiwa. [4]

Makosa ya Adhabu ya Kupigwa Mawe

Kwa mujibu wa fat’wa ya mafakihhi, kupigwa mawe ni adhabu ya mzinifu mwenye mke au kanizi na mwanamke mwenye mume. [5] Kunazungumziwa pia adhabu ya kupigwa mawe katika kesi ya liwati, lakini uamuzi wa kutekelezwa adhabu hii uko mikononi mwa mtawala wa kisheria. Kwa maana kwamba, anaweza kutekeleza adhabu hiyo au kuchagua aina nyingine ya kuua. [6]

Kwa mujibu wa agano la kale, adhabu ya baadhi ya makosa ni kupigwa mawe; adhabu za makosa kama vile kumchinja mtoto na kumtoa kafara kwa ajili ya masanamu [7], uchawi, [8] kukufuru, [9] kuvunjia heshima siku ya Jumamosi (Sabato), [10] kulingania kuabudu masanamu [11] na uzinzi. [12]

Hoja za Adhabu ya Kupigwa Mawe

Fat’wa mashuhuri ya Masuni na Mashia juu ya kuhalalisha kupigwa mawe na hata kutekelezwa kwake inategemea matukio kadhaa yaliyofanywa na Mtume (s.a.w.w) na Imam Ali (a.s) kuhusiana na hilo, lakini baadhi ya mafaqihi wengine kadhaa wamekataa na kuiona kuwa ni maalumu kwa Mayahudi, ambapo katika Sheria ya Kiislamu na hususan katika Qur'ani haijabainishwa au kutajwa. [13]

Baadhi ya hadithi na riwaya zilizopokewa na Waislamu wa Madhehhebu ya Shia zinasema kuwa, kuna adhabu ya kupiga mawe katika Uislamu, lakini utekelezaji wake unaruhusiwa kwa kuweko Maasumu. Rai ya baadhi ya mafaqihi wengine ni kuwa, adhabu ya uzinifu iko wazi katika Qur'an nayo ni kuchapwa viboko, na baadhi ya habari zinazohusiana na kupigwa mawe watu kama "Maiz" na "mke wa Ghamadiyah" zinakataliwa kwa mtazamo wa kitaalamu wa hadithi kutokana na utata na hitilafu nyingi zilizopo ndani yake. [14]

Kuna riwaya nyingi kuhusu adhabu ya kupigwa mawe au rajm. [15] Miongoni mwao ni riwaya ya Abu Basir kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s), ambayo kwa mujibu wake kupigwa mawe ni adhabu kubwa (isiyo ya kimali) ya Mwenyezi Mungu, na mtu mwenye mke au mume akizini atapigwa mawe. [16]. Pia kuna riwaya ambayo Imam Baqir (a.s) anasema kwamba Imam Ali (a.s) alikuwa akitoa hukumu ya kupigwa mawe mzinifu mwenye mke au mume. [17]

Hoja nyingine ya mafaqihi kuhusiana na adhabu ya kupiga mawe ni ijmaa yaani maafikiano na kauli moja ya wanazuoni. [18] Sheikh Tusi ameandika katika kitabu chake cha Kitab al-Khilaf: Mafakihi wote wa Kiislamu wanakubali na wana kauli moja kuhusiana na adhabu ya kupigwa mawe, na ni Makhawariji tu ndio wameikataa wakisema kuwa, haipatikani katika Qur'ani na hadithi zenye mapokezi mengi (Mutawatir). [19]

Kupigwa Mawe Katika Qur'ani

Wanazuoni wa Kishia wanaamini kwamba, katika Qur'ani hakuna Aya inayozungumzia adhabau ya kupigwa mawe; [20] na hukumu ya hili inapatikana katika hadithi na ijmaa (makubaliano) ya Wislamu; [21] lakini akthari ya mafakihi na wanazuoni wa elimu ya Usul wa Ahlu Sunna wanaamini kwamba, ndani ya Qur'ani kulikuweko na Aya inayozungumzia adhabu ya kupigwa mawe. [22] Hoja ya kundi hili la wanazuoni ni kuweko kwa hadithi zilizopokewa katika vyanzo kadhaa vya Ahlu-Sunna. [23]

Miongoni mwa hadithi hizo ni ile iliyoko katika Sahih Bukhari ambayo Omar bin al-Khatab amenukuliwa akisema kuwa, ninaogopa kupita zama kisha watu waseme kwamba, adhabu ya kupiga mawe haijaja ndani ya Qur’ani na watu wapotee kwa kuacha wajibu ambao umeshushwa na Mwenyezi Mungu. [24] Kadhalika Malik bin Anas amesema akinukuu kutoka kwa Omar kwamba: Isije mkaghafilika na Aya ya kupiga mawe kwa hoja kwamba, haipo ndani ya Qur’ani; kwani Mtume alikuwa akitekeleza adhabu ya kupiga mawe na sisi pia tulikuwa tukifanya. Aya hii ilikuweko katika Qur’ani na mimi sikuiandika kwa kuhofia kwamba, watu wasije wakasema nimeongeza kitu katika kitabu cha Mwenyezi Mungu. [25] Kwa mujibu wa Omar bin al-Khattab, Aya ya kupiga mawe ilikuwa hivi: «إذا زَنىٰ الشَيخ ُو الشَيخَة فَارْجُمُوهما اَلبَتَّة» [26] Atakapozini mwanaume mzee na mwanamke mzee, bila shaka wanapaswa kupigwa mawe. [27]

Baadhi ya Maulamaa wa Ahlu-Sunna akiwemo Abu Bakr Baqlani na zaidi kundi la Mu’tazilah akiwemo Abu Muslim Isfahani, hawakubaliani na nadharia hii. [28] Wao wanasema kwamba, kama ibara hii ingekuwa ni sehemu ya Qur’ani, bila shaka Omar bin al-Khattab angeiweka katika Qur’ani na asingeacha kufanya hilo kwa sababu ya maneno ya watu. Kadhalika fasihi ya ibara hii kwa upande wa balagha haifanani na muundo na fasihi ya Qur’ani. [29]

Ayatullah Khui mmoja wa mafakihi wa zama hizi wa Kishia ameandika katika al-Bayan: Kama hadithi hii itakuwa sahihi inapasa kusema kuwa, kuna Aya imefutwa ndani ya Qur’ani [30] na kwa muktadha huo, kukubali hilo inapaswa kukubali pia kwamba, Qur’ani imepotoshwa. [31]

Masharti ya Kutimia Adhabu

Kwa mtazamo wa mafakihi sharti la kutimia kupigwa mawe ni lazima mzinifu awe na mke au mume. Mtu ambaye anatekelezewa adhabu ya kupigwa mawe anapaswa kutimiza masharti yafuatayo:

  • Kuwa na mke wa ndoa ya daima na kuweko uwezekano wa kufanya naye tendo la ndoa.
  • Anayetekelezewa adhabu ya kupigwa mawe asiwe kanizi wala mtumwa.
  • Baleghe.
  • Akili. [32]

Kupigwa Mawe na Suala la Haki za Binadamu

Kumekuwa kukitolewa ukosoaji dhidi ya adhabu ya kupigwa mawe. Miongoni mwa ukosoaji huo ni kuwa, adhabu ya kupigwa mawe ni hukumu isiyo ya kiakili na inapingana na haki za binadamu. [33] Pia wakosoaji wa hili wanasema kuwa, hakuna uwiano kati ya uhalifu na adhabu; kwa sababu adhabu hii ni kali sana kwa mtu anayeteleza kwa muda kutokana na mashinikizo ya nguvu za ngono. Aidha wanadai kwamba, kitendo chake sio ufisadi hakiwadhuru wengine. [34]

Katika kutoa jibu la ukosoaji wa kwanza imeelezwa kuwa, Uislamu ni mkali sana katika hatua ya kuthibiti kosa na katika hatua ya utekelezaji adhabu ya kupiga mawe; kiasi kwamba, hukumu hii kwa namna fulani ni tishio zaidi na hutekelezwa kwa nadra sana. [35] Katika kujibu ukosoaji wa pili pia jibu lake ni kwamba, kuweko kwa adhabu kama hizi ni kutokana na athari nyingi haribifu za kidunia na akhera za zinaa kama vile kutoshikamana na dini, kutokuwa na staha na heshima, magonjwa ya zinaa, mgogoro wa watoto wasio na utambulisho, na ukosefu wa usalama wa kisaikolojia wa familia. Kwa msingi huo, katika hilo kosa na adhabu vinanasibiana na kuoana. [36]

Kubadilisha Hukumu ya Kupiga Mawe

Mwaka 1391 Hijria Shamsia, kulitolewa mtazamo wa kifat’wa wa baadhi ya Marajii Taqlidi kuhusiana na kubadilisha hukumu ya kisheria ya adhabu ya kupiga mawe mzinifu ambapo kulikuweko na majibu tofauti kutoka kwao. Ilikuja katika swali la kutaka mtazamo wa kisheria na kifat’wa ya kwamba: Kwa kuzingatia kwamba, hii leo kutekelezwa kwa adhabu ya kumpiga mawe mzinifu kunapelekea ukosoaji wa wapinzani wa Uislamu, je inawezekana kutoa adhabu mbadala wa kosa hili na hivyo kubadilisha hukumu hii? [37]

Picha yenye kuakisi kupigwa mawe kwa Mtakatifu Stephen iliyochorwa na Rembrandt.

Jibu la swali hili lilikuwa hivi: Ayatullah Noori Hamedani na Ayatullah Alavi Gorgani walitangaza kuwa: Hukumu ya kupiga mawe mzinifu si yenye kubadilika, lakini wakasema kuwa, kubadilisha namna ya utekelezaji wake ni jambo ambalo liko mikononi mwa Walii Faqih (Fakihi Mtawala). Kwa upande wao, Ayatullah Makarim Shirazi na Ayatullah Subhani wamesema kuwa, kutokana na mazingira ya sasa hukumu hiyo inaweza kubadilishwa na hivyo kupatiwa mbadala. Ayatullah Mousavi Ardebili ameandika: Adhabu ya kupiga mawe ni hukumu ambayo haiwezekani kuibadilisha, lakini kama itakuwa inaenda kinyume na maslahi ya Uislamu na Waislamu, Fakihi aliyetimiza masharti anaweza kutoa hukumu ya kutotekelezwa kwake. [38]

Adhabu ya Kupigwa Mawe Kabla ya Uislamu

Kupigwa mawe ilikuwa moja ya adhabu ya kawaida wakati wa kujitokeza Biblia. [39] Kadhalika wanasema kuwa, katika lauhu ya maandishi ya Wasumeria yaani Wasumerian (kaumu wanaoishi baina ya Nahrein), ambayo ni maandishi ya zamani zaidi ya kisheria, yanataja adhabu ya kupigwa mawe. [40] Kwa mujibu wa loho hizi zinazorejea nyuma miaka 2400 kabla ya kuzaliwa Masih Issa (a.s), makosa kama wizi na mwanamke kuingiliana na wanaume wawili adhabu yake ilikuwa ni kupigwa mawe. [41]

Rejea

Vyanzo