Nenda kwa yaliyomo

Wajibu wa Kumshukuru Mneemeshaji

Kutoka wikishia

Wajibu wa Kumshukuru Mneemeshaji: Wajibu wa kumshukuru Mneemeshaja (وجوب شکر مُنعِم) au mfadhili ni istilahi maalumu inayotumiwa na wataalamu wa taaluma ya wanatheolojia. Nayo ni ibara yenye maana ya kwamba; kuwepo kwa hisia ya wajibu ndani ya tabia ya mwanadamu, inayomlazimisha au kumpa msukumo wa kumshukru yule anayemneemesha mwanadamu. Wajibu huu wa kumshukuru mtoaji wa neema, umechukuliwa kama ni kanuni ya kiakili au hukumu ya kisharia ambayo imethibitishwa kupitia akili, Qur’ani, na Hadithi mbali mbali. Miongoni mwa Aya zinazounga mkono suala hili, ni ni ile Aya ya 7 ya Suratu Ibrahim, ambayo inatoa ufafanuzi wa kwamba; shukrani za neema huhakikisha kuendelea kwa neeme hizo, huku kuifuru neema huwa ndiyo msingi na sababu ya adhabu kali ya Mwenye Ezi Mungu. Wanazuoni wa Kiislamu wametofautiana kimaoni kuhusiana na asili ya kanuni ya wajibu wa kumshukuru Mneemeshaja . Wafuasi wa Adliyyah (ambao ni Mu‘tazila na Imamia), wanaamini kwamba; hii ni kanuni ya kiakili, ingawa pia imeungwamkono na kuhimiliwa na Qur’ani pamoja na Riwaya. Hivyo basi hukumu za kisharia zinazounga mkono kanuni hii, ni viimarishi na viashiria tu vya kanuni hii (hukmu irshadi). Wao wanasisitiza maoni yao wakisema; Ni jambo la wazi kabisa (lisilohitaji ithibati) kwamba; ni wajibu kwa mwanadamu kumshukuru Mneemeshaja . Pia wao hutegemea hoja za sira na nyenendo za wenye akili waliotangulia (siratu Al-uqalaa). Kinyume chake, Ash‘ari, walioko katika madhehebu ya kiitikadi ya upande wa Ahlus-Sunna, wao hutegemea Aya za Qur’ani na dalili nyengine maoni yao yasemayo kwamba; Kabla ya kushuka kwa sharia za mbinguni kutumwa kwa Manabii, hakukuwa na hukumu za kiakili inayomhukumu mwanadamu na kumlazimisha kumshukru Mneemeshaja . Wanazuoni wa Kishia huitumia kanuni hii katika nyanja mbalimbali za sayansi za Kiislamu, ikiwa ni pamoja na theolojia, usul al-fiqh, pamoja na fiqhi. Miongoni mwa maeneo inayotumika kanuni hii, pamoja na matumizi yake katika kuthibitisha wajibu wa mwanadamu kufanya uchunguzi wa masuala ya kiitikadi kabla ya kushikamana nayo. Pia kanunu hii hutumika katika kuthibitisha na umuhimu wa kuwepo kwa ijtihadi, taqlidi (kumfuata mwanazuoni katika utekelezaji wa amali), au ihtiyat (tahadhari), (kutomfuata mwanazuoni katika utekelezaji wa amali, katika hali ambayo wewe mwenyewe ni mwanazuoni mwenye daraja ya ijitihadi).

Utambulisho na Nafa Yake Kumshukuru Mneemeshaja ni hisia na jukumu la kiakili na kisharia, linalomwajibisha mwanadamu kumshuku yule aliye mneemesha [1]. Elimu hasa inayohusiana na nadharia hii, ni sayansi ya kikalamu (theolojia ya Kiislamu), ingawa wanazuoni wa fiqhi pia nao huchukua na kuitumia kama ni nyenzo maalumu ya kuainisha baadhi ya hukumu za kisheria. [2] Wafasiri wa Qur’ani wametaja Aya kadhaa kama ni ushahidi wa kuwepo kwa kanuni hii. Miongoni mwa Aya hizo ni pamoja na; Aya ya 11 hadi 15 za Suratu Az-Zukhruf [3], Aya ya 107 ya Suratu Al-A‘raf [4], Aya ya 109 ya Suratu Al-An‘am [5], Aya ya 164 ya Suratu Al-Baqarah [6], pamoja na Aya ya 7 ya Suratu Ibrahim. [7] Aya hizi ndizo zinazonabainisha kuwepo kwa wajibu wa mwanadamu katika kuthamini na kushukuru neema za Mwenye Ezi Mungu. Pia kuna masimulizi kadhaa ya Riwaya zinathibitisha uzito wa shukrani juu ya neema za Mwenye Ezi Mungu. Kwa mfano, katika moja ya Hadithi mashuhuri imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (A.S.) akisema kwamba: "Hata kama Mwenyezi Mungu hangetoa onyo lolote lile kuhusiana na adhabu ya dhambi, bado kwa ajili ya kushukuru neema zake, ingekuwa ni wajibu kujiepusha na kutenda dhambi." [8] Pia kanuni hii ya ulazima wa kumshukuru Mneemeshaja , imepewa sisitizo ndani ya mashairi ya washairi mbali mbali. Mathalan, Maulana Jalaluddin Rumi (aliyeaga dunia mwaka mwaka 672 Hijria) ameandika katika moja ya shairi yake akisema: Shukrani kwa Mneemeshaji ni amri ya hekima toka kwa Rabana, la si hivyo, lango la ghadhabu ya milele litafunguka bila huruma. [9]

Saadi Shirazi (aliaga dunia mwaka 691 Hijria) naye anaakisi kanuni kupitia shairi lake lisemalo: Sipinde wala sikiuke kumshukuru Mneemeshaji, Ama sivyo, siku ya malipo ni maskini mhamani. [10]

Msingi wa Akili au wa Kisharia? Mojawapo ya hitilafu baina ya madhehebu za kiitikadi za Uadiliah na Ash’ariyya, miongoni mwa Waislamu, juu ya msingi wa kumshukukuru Mneemeshaja , ni kwamba je, msingi huu ni wa kimantiki au wa kisheria? [11] Kwa mtazamo wa Adliyya, yaani Mu'tazila [12] na Imamiyya [13], ni kwamba; kanuni hii imejengeka juu ya misingi na hoja za kiakili, na zile amri na makatazo ya kisharia kuhusiana na kanuni hii, ni sharia au elekezi (amru au hukmu irshadi) tu. [14] Sheikh Ansari (aliyefariki 1281 Hijria), faqih na msomi wa Kishia wa fani ya usul al-fiqhi, anaamini kwamba; mzizi hasa wa suala hili unatokana na tafauti katika welewa wa dhana ya ya husnu na qubhu (asili ya uzuri na ubaya wa mambo mbali mbali) baina ya Adliyya na Ash’ariyya; kumaanisha kwamba iwapo mtu ataitambua akili kuwa ndio chanzo cha kutambua husnu na qubhu (wema na ubaya), huyo atakubaliana na kuwepo kwa ulazima wa kiakili juu ya kumshukuru Mneemeshaji. Lakini iwapo, ataamini wamba, husnu na qubhu ni sifa mbili zitokazo na vipimo vya kisheria tu (kama ilivyo kwa upande wa Ash’ariyya), huyo yeye ataamini kuwa wajibu wa kumshukuru Mneemeshaja unatokana na maamrisho ya kisharia. [15]

Pia soma: Husnu wa Qubhu

Hoja za Waodai Kuwa ni Kanuni ya Kiakili Wanazuoni wa elimu ya kalamu wameeleza kuwa msingi wa kiakili wa ulazima wa kumshukuru Mwenye Kuneemesha unatokana na dhati ya jambo lenyewe lilivyo, ambapo akili inahukumu kuwa; shukrani kwa Mneemeshaja ni wajibu usio na shaka ndani yake. [16] Al-Karajaki (aliyefariki 449 Hijria), ambaye mwanatheolojia mashuhuri wa Kishia, anaeleza kuwa; ulazima wa kumshukuru Mneemeshaja , ni kanuni iliyokubaliwa kwa makubaliano ya wenye akili timamu, bila mzozo wowote wa kimawazo kuhusu ukweli wake. [17] Kuna hoja mbalimbali za kimantiki zilizowasilishwa ili kuimarisha dhana hii. Mathalani, Allamah Hilli (aliyefariki 726 Hijria), mwanazuoni mashuhuri wa elimu ya kalamu na mwanafiqhi wa Kishia, anajenga hoja zake akisema kwamba; ikiwa kumshukuru Mneemeshaja si wajibu wa kiakili, basi hata utafutaji wa maarifa kwa ajili ya kumtambua Yeye hautakuwa na ulazima wowote ule ndani yake. Kutokuwepo kwa wajibu wa kutafuta maarifa hayo kunapelekea kubatilika kwa utumwaji wa mitume manabii kwa wanadamu, jambo ambalo ni lenye kukinzana na misingi ya mafundisho ya kiakili na ya kiwahyi. Kwa hivyo, kumshukuru Mneemeshaja ni wajibu wa kiakili unaojengeka juu ya misingi imara ya mantiki na falsafa. [18] Hoja za Waodai Kuwa ni Kanuni ya Kisharia Kwa mujibu wa madhehebu ya Ash’ariyya, kinyume na mtazamo wa Adliyya, ulazima wa kumshukuru Mneemeshaji hautokani na hukumu za kiakili bali unatokana na sharia. Ili kuimarisha mtazamo wao, wao wanaleta hoja zifuatazo: • Kwanza, Aya ya 15 ya Suratu al-Israa na Aya ya 165 ya Suratu an-Nisaa zinaashiria kuwa, kabla ya bi‘tha ya manabii (kutumwa kwa mitume) na kuwekwa au kushushwa kwa sharia, mwanadamu hawezi kustahili adhabu. Kwa mujibu wa mtazamo wa Ash’ariyya, hili linathibitisha kuwa akili kama akili, haina uwezo wa kuhukumu ulazima wa shukrani za kumshukuru Mwenye Ezi Mungu. [19] Hata hivyo, wapinzani wa hoja hii wanajibu kwamba; Aya hizo zinahusiana na adhabu ya kidunia, na si ya Akhera. Aidha wapainzani hawa wanaendelea wakisema kwamba; sababu halisi ya kuadhibiwa kwa mja fulani, ni uasi wa mtu dhidi ya Mola wake unaoambatana na ufahamu wa asili ya ubaya autendao, bila ya kujali namna yeye alivyouewa uasi huo. Hivyo basi ikiwa mtu, kwa kutumia akili, anatambua asili ya ulazima wa kumshukuru Mwenye Ezi Mungu kisha akalikaidi suala hilo, huyo atakuwa ni mwenye kustahili adhabu. [20] • Pili, Ash’ariyya wanadai kwamba dhana ya ulazima wa kumshukru Mneemeshaja , haiwezi kueleweka bila kuwepo kwa amri ya Mwenye Ezi Mungu, kwani kabla ya amri hiyo, hakutakuwa na maana ya kuwepo kwa ulazima huo. Kwa mtazamo wao, thawabu ni matokeo ya utiifu wa amri za Mungu, na adhabu hutokana na uasi dhidi ya amri hizo, hivyo basi dhana hizi hupata maana kamili baada ya kuwekwa kwa makatazo na amri za Mwenyezi Mungu. [21] Wapinzani wa hoja hii wanapinga mtazamo huo kwa kusema kuwa; kinachozungumziwa hapa ni wajib wa kiakili, yaani, ulazima unaotokana na mantiki na dhana ya haki na ya msingi, na si wajib wa kisheria, ambao unatokana na utekelezaji wa sharia za Mwenye Ezi Mungu. [22]

Mifano ya Utumiaji wa Kanuni Hii Katika Taaluma za Dini Katika taaluma mbalimbali za dini, dhana ya wajibu wa kumshukuru Mneemeshaji imekuwa mhimili wa hoja za kiakili, inayotumika katika fani tofauti za kidini. Miongoni mwa maeneo mnamotumika dhana hii ni kama ifuatavyo: Ulazima wa Uchunguzi wa Kina Katika Itikadi Katika jitihada za kuthibitisha wajibu wa kuchunguza uwepo wa Mungu sambamba na masuala mengine ya kiimani, wataalamu wa theolojia wamejenga hoja zao juu ya kanuni mbili kuu, wakitumia kanuni hizo kama ndiyo misingi ya mantiki na kiakili. Nazo ni; kanuni ya wujub daf‘i dharar muhtamal (wajibu wa kujihadhari na madhara yanayoweza kutokea) [23] na wujub shukr al-mun‘im (wajibu wa kumshukuru Mneemeshaji). [24] Mchakato wa hoja zao unafuata mpangilio ufuatao: 1. Kumshukuru Mwenye Kuneemesha ni wajibu wa kiakili. 2. Shukrani haziwezi kuwa timilifu bila kumtambua Mwenye Kuneemesha na wala haiwezekani kushukuru kikamilifu asiyefahamika. 3. Utambuzi wa Kumtambua Mwenye Kuneemesha unapatikana kupitia uchunguzi na uhakiki wa kina. 4. Kwa hivyo, kuchunguza Juu ya Uwepo Mwenye Kuneemesha ni wajibu wa kiakili na wa lazima kwa kila mtu mwenye busara. [25]

Misingi ya Kitheolojia ya Fani ya Usul al-Fiqh Baadhi ya wataalamu wa fani ya usul al-fiqhi (misingi ya ufahamu wa sharia za fiqhi), wamesema kwamba; wajibu wa kumshukuru Mneemeshaji, ni moja ya misingi ya kitheolojia ya sayansi ya usul al-fiqhi. Wao wanasema kwamba; Allama Hilli aliihisabu kanuni hii kama ni moja ya misingi ya kitheolojia ya usul al-fiqhi na akafungua mlango maalumu katika kujadili juu ya kanunu hiyo. [26] Sheikh Bahai ambaye ni mwanazuoni mwengine wa fani ya usul al-fiqhi, ambaye aliitaja na kuichunguza kanuni hii, kisha kuitambua kama ni moja ya misingi ya kitheolojia ya fani ya usul al-fiqhi. [27] Msingi wa Tatu: Ijtihad, Ihtiyat, na Taqlid Moja kati ya marejeo makuu yanayorejelewa katika kuthibitisha kanuni hii (wajibu wa kumshukuru Mneemeshaji), yanapatikana katika mjadala mitatu, ambayo ni; ulazima wa kufanya ijtihad (juhudi za kutambua hukumu za kisheria), ulazima wa ihtiyat (kutofuata mjitahidi kwa aliyefikia cheo cha ijitihadi), pamoja na ulazima wa taqlid (kumfuata mwanasheria mwenye sifa katika matendo ya kidini). [28] Kwa mujibu wa kanuni hii (wajibu wa kumshukuru Mneemeshaji), akili inaamini kuwa; ni wajibu wa mwanadamu kumshukuru Mneemeshaji. Na haiwezekani kwa mtu fulani kutimiza shukrani hizo bila ya kuwa na ufahamu wa sheria za Mneemeshaji. Hivyo basi, ni lazima kwa wanadamu kushikamana na mambo yafuatayo: 1. Kufanya ijtihad: Kujifunza kuchambua na kutoa hukumu za kidini kwa kujitegemea mwenyewe (na kuwa tegemeo la wengine). 2. Kuchukua ihtiyat: Tahadhari maalumu kwa aliyefikia daraja ya ijitihadi ila bado hajaruhusu watu kumfuata, ambaye hufanya matendo yake kwa uangalifu mkubwa ili kuhakikisha sheria za Mwenye Ezi Mungu zinatekelezwa. 3. Kufanya taqlid: Kumfuata mwanasheria mwenye sifa na ujuzi wa kutosha. [27]