Nenda kwa yaliyomo

Vazi la Mwenye Kusali

Kutoka wikishia

Vazi la Mwenye Kusali (Kiarabu: لباس المصلي) ni nguo ambayo anaivaa mtu anayesali. Mafakihi wamebainisha hukumu na masharti mbalimbali ya vazi la mwenye kusali pamoja na kiwango kinachomfunika. Mafakihi wana kauli moja (ijmaa) ya kwamba, ni wajibu kwa wanawake kujisitiri katika Sala bila kujali kuna asiyekuwa maharimu wake au la. Mwanamke wakati wa kusali anapasa kufunika mwili wake wote; hata hivyo sio lazima kwa mwanamke wakati wa kusali kufunika mduara wa uso wake, mikono na miguu mpaka kwenye viganja. Nguo ya mwanaume mwenye kusali inapasa kusitiri tupu mbili (ya mbele na ya nyuma).

Miongoni mwa masharti mengine ni vazi hilo kuwa tohara, lisiwe na najisi, liwe la halali, lisiwe la kughusubu (kunyang’anya), lisiwe linatokana na sehemu ya mzoga, lisiwe linatokana na mnyama ambaye nyama yake ni haramu kuliwa na vilevile lisiwe linatokana na mnyama ambaye nyama yake ni halali kuliwa (lakini hakuchinjwa kwa njia ya kisheria yaani kwa kutajwa jina la Allah).

Kwa mujibu wa mafakihi ni haramu kwa mwanaume kuvaa vazi ambalo linatokana na dhahabu au limechongwa dhahabu humo kama ambavyo vazi la mwanaume halipaswi kuwa linatokana na hariri halisi na kufanya hivyo kunabatilisha Sala. Mafakihi kadhalika wamebainisha hukumu na sheria mbalimbali za mustahabu na makuruhu kuhusiana na vazi la mwenye kusali.

Nafasi

Vazi la anayesali lina hukumu na masharti maalumu ambayo yanapaswa kutimia. Mafakihi hubainisha hukumu na sheria za hili katika baadhi ya milango ya fikihi kama vile katika milango ya tohara na Sala. [1] Hurr al-Amili ametenga mlango maalumu katika kitabu chake cha Wasail al-Shiah kwa anuani ya “Milango ya Vazi la Mwenye Kusali” na ameleta hadithi mbalimbali zinazobainisha hukumu za vazi la mwenye kusali. [2]

Kiwango cha Vazi katika Sala

Kiwango cha vazi la mwanaume na mwanamke katika Sala kinatofautiana kwa mujibu wa mitazamo ya mafakihi.

Vazi la Mwanamke

Mafakihi wana kauli moja (ijmaa) [3] ya kwamba, ni wajibu kwa wanawake kujisitiri katika Sala bila kujali kuna asiyekuwa maharimu wake au la. [4] Mwanamke wakati wa kusali anapasa kufunika mwili wake wote; hata hivyo sio lazima kwa mwanamke wakati wa kusali kufunika mduara wa uso wake, (kiwango ambacho anakiosha wakati wa kutia udhu) mikono na miguu mpaka kwenye viganja na vifundo. Ukiacha sehemu hizo ni wajibu kwa mwanamke kufunika sehemu nyingine zote zikiwemo nywele za kichwa. [5] Hata hivyo baadhi ya mafakihi wa Kishia wametilia shaka wajibu wa kufunika nywele za kichwa katika Sala. [6] Kwa mujibu wa fat’wa ya Ibn Junayd, mmoja wa mafakihi wa karne ya nne Hijria, hakuna tatizo kwa mwanamke kusali hali ya kuwa hajafunika nywele zake ikiwa hakuna asiyekuwa maharimu anayemuona. [7]

Baadhi ya mafaqihi wanaamini kwamba, mbali na uso, mikono hakuna tatizo kutofunika pia juu ya miguu (kuanzia katika kifundo cha chini). [8] Tabatabai Yazdi (Sahib-Urwa) amesema kuwa, hakuna shida kutofunikwa chini ya miguu wakati wa kusali. [9]

Vazi la Mwanaume

Kwa mujibu wa ijmaa (kauli na maafikiano) ya mafakihi [10] ni kwamba, nguo ya mwanaume mwenye kusali inapasa kusitiri tupu mbili (ya mbele na ya nyuma) na sio wajibu kwake kufunika sehemu zingine za mwili wakati wa kusali. [11] Tabatabai Yazdi anasema, kwa tahadhari ya mustahabu (ihtiyat mustahab) ni vyema mwanaume akajifunika na kujistiri wakati wa kusali kuanzia kitovuni mpaka mpagotini. [12] Kwa mujibu wa mtazamo wa Sahib al-Jawahir ni kwamba, kusali uchi mwanaume endapo atajistiri tupu zake tu licha ya kuwa inajuzu lakini inachukiza (makuruhu). [13]

Hukumu Zingine

Baadhi ya hukumu zingine za vazi la mwenye kusali ni kama ifuatavyo:

Usafi na Tohara

Kwa mujibu wa kauli moja (ijmaa) ya mafakihi wa Kishia, vazi la mwenye kusali linapaswa kuwa safi na lenye tohara [14] na kama litakuwa najisi ni wajibu kuondoa na kusafisha najisi hiyo. [15] Hata hivyo mafakihi wamezitoa katika hukumu hiyo baadhi ya mambo kama vazi ambalo lina damu ya jeraha, jipu na kadhalika damu ambayo ni chache kiwango cha mduara wa kidole gumba (ghairi ya damu ya hedhi, nifasi na istihadha). [16] Kwa maana kwamba, damu hizo zisiwe ni katika damu hizi tatu za hedhi, nifasi na istihadha.

Kadhalika wamesema, nguo ndogo ambazo kwazo Sala haitimii (yaani haiwezekani kufunika tupu kwa kutumia hizo) kama soksi, kofia, glovu, kofia aina ya baraghashia na kadhalika... kama zitakuwa na najisi, hakuna tatizo kusali na vitu hivi. [17] Kwa mujibu wa baadhi ya mafakihi vitu vidogo ambavyo mwenye kusali navyo wakati wa kusali kama pete, funguo, saa na sarafu kama zinakuwa na najisi hakuna tatizo kusali navyo. [18]

Kwa mujibu wa mtazamo mashuhuri wa mafakihi na wanazuoni wa Kishia [18] ni kwamba, mwanamke ambaye ni mlezi wa mtoto (awe ni mama wa mtoto au siyo mwanaye kama yaya kwa mfano) na ambaye ana nguo moja tu (hana nguo nyingine ya kubadilisha), endapo vazi hilo litanajisika kwa mkojo wa mtoto huyo, alifue mara moja tu katika kipindi cha mchana kutwa na hakuna ulazima wa kulitoharisha katika kila Sala. [20]

Nguo Iwe ya Halali

Kwa mujibu wa kauli moja (ijmaa) ya mafakihi, nguo ya mwenye kuswali ni lazima iwe ya halali (isiwe ya kughusubu yaani kunyang’anya). [21] Kwa muktadha huo mwenye kusali kama atakuwa na ufahamu kamili juu ya uharamu wa kutimia knguo ya kughusubu (kunyang’anya) kisha akaswali nayo kwa makusudi, Sala yake itabatilika. [22] Hata hivyo mwenye kusali kama hajui au amesahau kwamba, nguo yake ni ya kughusubi na kisha akaswali nayo, Sala yake itakuwa sahihi; [23] lakini kama wakati akiwa katika hali ya kusali akakumbuka na kuna uwezekano wa kuendelea na Sala kwa kufunika tupu zake na kuna nguo isiyo ya kughusubu anapaswa kuvua mara moja nguo ya kughusubu na hata kama ataweza kusali japo rakaa moja ndani ya wakati anapaswa kuvua vazi la kughusubu. Hata hivyo kama amelazimika kusali na vazi hilo la kughusubu (unyang’anyi) kwa ajili ya kuhifadhi roho na mali yake, Sala yake itakuwa sahihi. [24] Kama mwenye kusali amenunua nguo kwa pesa ambayo haijatolewa Khumsi na Zaka ma kisha akatumia kuisalia, Sala yake itabatilika. [25] Fat’wa nyingine ni hii kwamba, kutumia vitu vingine vilivyopatikana kwa njia isiyo halali kama pete, simu ya mkononi (rununu) na mkanda ni haramu na kuwa na vitu hivyo wakati wa kusali kunapelekea Sala kubatilika. [26]

Asili ya Vazi

Kwa mujibu wa fat’wa ya mafakihi. Vazi la mtu anayeswali halipaswi kuwa limetokana na mnyama ambaye nyama yake ni haramu. Kwa msingi huo, kama asili ya nguo yake imetokana na ngozi, nywele, manyoya na kadhalika ya mnyama ambaye nyama yake ni haramu au vitu mfano vya hivyo na kisha akawa ameambatana navyo katika Sala au moja ya hivyo kikawa kimeganda katika nguo yake, Sala yake itabatilika. [27] Fauka ya hayo imeelezwa kuwa, endapo vitu kama mate na kinyesi cha mnyama na ndege ambaye nyama yake ni haramu kitakuwa katika nguo, Sala itakayosaliwa kwa nguo hiyo itabatilika. [28] Kadhalika vazi la mtu anayeswali lisiwe linatokana na mnyama ambaye nyama yake ni haramu kuliwa na lisiwe linatokana na mnyama ambaye nyama yake ni halali (lakini hakuchinjwa kwa njia ya kisheria yaani kwa kutajwa jina la Allah). [29]

Ni haramu kwa mwanaume kuvaa nguo iliyoshonwa kutokana na dhahabu au imechongwa dhahabu humo na akisali nayo Sala yake inabatilika. [30] Kadhalika ni haramu kwa wanaume kuvaa cheni ya dhahabu, pete ya dhahabu na saa ya dhahabu na kwa mujibu wa fat’wa za makafihi ni wajibu wakati wa kusali kujiepusha na vitu hivyo. [31]

Kwa mujibu wa fat’wa za mafakihi, ni haramu kwa mwanaume kuvaa vazi ambalo linatokana na hariri na kufanya hivyo kunabatilisha Sala. [32] Vitu kama soksi, kofia, glovu, kofia aina ya baraghashia na kadhalika... kama zitakuwa zinatokana na hariri halisi kwa mtazamo wa baadhi ya mafakihi hilo linabatilisha Sala. [33]

Mambo Yaliyo Mustahabu na Makuruhu

Mafakihi wakizingatia hadithi za Maimamu Maasumu (a.s) mbali na masharti ambayo vazi la mwenye kusali linapaswa kuwa nayo, wamebainisha pia hukumu ambazo ni mustahabu na makuruhu katika uwanja huu: [34]

Mambo ya Mustahabu

Baadhi ya mambo ambayo yametajwa kuwa ni mustahabu katika kuhusiana na vazi la mwenye kusali ni:

  • Kuvaa nguo nyeupe.
  • Mwanaume avae joho na mwanamke chador (aina ya baibui).
  • Mwenye kusali avae vazi safi zaidi.
  • Atumie uturi na manukato.
  • Avae pete ya aqiq. [35]

Mambo Ambayo ni Makuruhu

Sahib Ur’wah ametaja mambo 33 ambayo ni makuruhu kwa vazi la mwenye kusali.

Baadhi ya hayo ni:

  • Kuvaa nguo nyeusi.
  • Kuvaa nguo chafu.
  • Kuvaa nguo ambayo ina picha ya mtu au mnyama.
  • Kuvaa niqabu kwa wanawake.
  • Kuvaa nguo inayobana.
  • Kuvaa nguo ya umashuhuri (nguo ambayo mtu akivaa hupelekea kuonyeshwa vidole). [36]

Rejea

Vyanzo