Vazi Jeusi
Wakati wa Kufanyika | Mwezi Muharram, Safar na kwenye Maombolezo ya Ahlul-bayt (a.s) |
---|---|
Mahali pa Kufanyika | Maeneo Yote Wanapopatikana Shia |
Asili Kihistoria | Kabla ya Uislamu |
Aina | Maombolezo |
Vazi Jeusi (Kiarabu: لَبسُ السّواد) ni kuvaa nguo nyeusi na kupamba maeneo fulani kwa vitambaa vya rangi nyeusi, ni tendo lenye nia ya kutoa ishara ya kuwepo kwa hali ya maombolezo. Miongoni mwa Waislamu wa Shia, tamaduni hii imekuwa ya kawaida tokea mwanzo mwa Uislamu. Kuna ushahidi mbalimbali kutoka katika Hadithi za Maasumina (Maimamu 12 pamoja na Mtume na bibi Fatima) zinazothibitisha kuwepo kwa desturi hii.
Mafakihi wa Kishia wanalihisabu suala la kuvaa nguo nyeusi kwa ajili ya kuomboleza viongozi wakuu wa dini kuwa ni moja ya mifano hai ya kuheshimu na kutukuza nembo za Mwenye Ezi Mungu, na wanaliona jambo hilo kuwa ni miongoni mwa mambo yaliopendezwa (Sunna). Mafaqihi na wanazuoni wa Kishia wanakataa chukizo la kuvaa nguo nyeusi lililotajwa katika baadhi ya Hadithi, huku wakizihusisha Hadithi hizo na hali ya kuvaa nguo nyeusi katika hali ya kutowepo maombolezo. Badhi ya mafakihi kama vile Sayyid Ja’afar Tabatabai Hairi, Sayyid Hassan Sadri na Mirza Jawad Tabrizi wameandika tasnifu maalumu katika kuthibitisha pendezo (Sunna) ya kuvaa nyeusi katika kuomboleza viongozi wakuu wa kidini.
Nguo nyeusi pia inachukuliwa kama ni alama ya Bani Abbas. Kundi la wanahistoria linaamini kwamba; mwelekeo wa Bani Abbas wa kutumia bendera na nguo nyeusi, ilikuwa ni ishara maalumu ya kuonesha mrengo wao hamu ya kulipiza kisasi dhidi ya mateso waliofanyiwa Ahlul-Bayt (a.s) katika enzi za Bani Umayyah. Pia ilikuwa ni nyenzo au nembo yenye lengo la kujiunga na wapenzi na wafuasi wa Maimamu (a.s). Baadhi wanaamini kuwa sababu ya Maimamu kutoa Hadithi zinazokataza kuvaa nyeusi kulikuwa na lengo la kuwazuia Bani Abbas kuto tumia vibaya nyenzo hizo kwa manufaa yao binafsi.
Imekuwa ni mila ndani ya jamii, kwamba mwanzoni mwa masiku ya kuomboleza yanapowadia, watu huanza kuingia katika huzuni zao kuvaa na kupamba maeneo ya ibada kwa nguo nyeusi, ambapo wafanyao hivyo kwa lugha ya Kifarsi huotwa Siah-Poushan. Waombolezaji huvaa mavazi ya huzuni ya rangi nyeusi kwa taratibu maalum, na huchukua juhudi za kupamba kuta za maeneo ya ibada kama misikiti, makaburi ya Maimamu na Huseiniyya kwa nguo nyeusi. Katika baadhi ya miji ya Azerbaijan, pia kuna desturi inayoitwa Yaqe-Bandan inayofanyika tarehe 12 ya mwezi wa Muharram. Katika sherehe hii, wazee na waandishi wakongwe wa mashairi ya maombolezo, hufunga vifungo vya nguo za waombolezaji vilivyo wazi, kama ni ishara ya kimila na kimaadili inayo ashiria huzuni.
Rangi Nyeusi Ima ni Ishara ya Huzuni au Usharifu
Kuvaa mavazi meusi imekuwa ni desturi mashuhuri miongoni mwa watu wa mataifa mbali mbali inayo ashiria kuwepo kwa hali huzuni na majonzi. Kwa sababu hiyo, Waislamu wa madhehebe ya Shia na wapenzi wa Ahlul-Bayt (a.s) huvaa mavazi meusi katika siku za maombolezo ya viongozi wakuu wa kidini, hususan wakati wa kuomboleza kifo cha Imam Hussein (a.s), nao hupamba kuta na maeneo ya ibada kwa nguo nyeusi. [1] Ali Abu al-Hassani (aliyefariki mwaka 1390 Hijiria Shamsia), ambaye ni mwanahistoria wa upande wa madhehebu ya Shia, amenukuu ushauri wa Imamu Sadiq (a.s) unaomshauri mwanamke kuvaa mavazi meusi katika kuomboleza kifo cha mumewa, [2] na akaelezea kuwa siku ya Eid Ghadeer kuwa ni siku ya kuvua mavazi meusi, [3] akaonesha kuwa; Maimamu pia walithibitisha sifa hii ya asili ya rangi nyeusi kuwa ishara inayoashiria huzuni na majonzi. [4]
Sifa nyingine ya rangi nyeusi ni haiba, usharifu (usayyid), na kuwa na ubora fulani. Kwa mujibu wa imamani ya Abu al-Hasani, ni kwamba; sifa hizi ndizo zilizo pelekea bwana Mtume (s.a.w.w) pamoja na Ahlul-Bayt (a.s) kuvaa vilemba vyeusi katika matukio maalum kama vile tukio la Ghadeer, na hata masayyid (masharifu) pia nao huvaa vilemba vyeusi kufuatia tendo hilo la bwana Mtume na Ahlul-Bayt (a.s). [5]
Mila ya Mavazi Meusi Katika Maombolezo
Kwa mujibu wa ripoti ya Mohsin-Hisam Madhaahiri katika kitabu cha Farhang-e Soug-e Shia, ni kwamba; Waombolezaji katika siku za maombolezo huvaa mavazi meusi kwa taratibu na sherehe maalum, na hupamba kuta za maeneo ya ibada na kadhalika kwa vitambaa ambavyo kawaida huwa na mashairi ya maombolezo, ibada za kidini, majina ya Maimamu na mashahidi wa Karbala. Sherehe hii huitwa Siah-Poushan. [6]
Sherehe nyingine inayojulikana kama Yaqe-Bandan (kwa Kituruki: Yakha Baghlama), hufanyika katika baadhi ya miji ya Azerbaijan kama vile mji wa Tabriz na Khalkhal mnamo siku ya tatu ya kuuawa kwa Imamu Hussein (a.s) (12 Muharram). Katika sherehe hii, wazee wa maombolezo hufunga vifungo vya shingoni mwa mashati meusi ya waombolezaji, ambavyo vilikuwa wazi kwa ajili ya kuonyesha hali ya maombolezo, ikiwa ni ishara ya kumaliza maombolezo ya siku kumi za kwanzo za mwezi wa Muharram. [7]
Sunna ya Kuvaa Nyeusi Katika Maombolezo ya Viongozi wa Dini
Kuvaa nguo nyeusi kwa ajili ya kuomboleza vifo vya viongozi wakuu wa dini ni moja ya Sunna za kidini katika madhehebu ya Shia, na mafakihi wengi wametoa fatwa juu ya hilo kwa lengo la kuheshimu na kutukuza nembo za kidini (Sha’airu Llahi). [8] Baadhi ya wanazuoni wa kidini wa madhehebu ya Shia kama vile; Ayatullah Ali Khamenei, Ayatullah Sistani, Nasir Makarim Shirazi, Lutfullah Safi Golpaygani na Hussein Wahid Khorasani, wamelihisabu suala la kuvaa nguo nyeusi katika kuomboleza vifo vya Ahlul-Bayt (a.s) kuwa ni miongoni mwa matendo mustahabu. [9] [10] Kivitendo, wengi miongoni mwa wanazuoni walikuwa wakivaa nguo nyeusi ndani ya siku za maombolezo. [11] Katika wasia wake Ayatullah Marashi Najafi ameusia kuzikwa na nguo nguo zake nyeusi alizokuwa akivaa katika masiku ya Muharram na Safar, ambapo alitaka ziambatanishe nguo zake hizo pamoja na sanda yake.[12]
Licha ya Riwaya zilizotajwa kuhusu machukizo ya kuvaa nguo nyeusi,[13] pamoja na kauli za mafakihi zinazo kemea kuvaa nguo nyeusi katika sala au katika hali nyengine za kiujumla, [14] lakini imeelezwa kwamba; licha ya usahihi wa Riwaya zinazokataza kuvaa nguo nyeusi, ila kulingana na nyenendo na kauli za ya Ahlul-Bayt (a.s), yaonekana kwamba kuvaa mavazi meusi wakati wa maombolezo, na kwa nia ya heshima nembo za kidini, ni suala lilipo nje ya makatazo ya kuvaa nyeusi katika hali ya kawaida.[15]
Tasnifu za Mafakihi Kuhusu Mavazi Meusi
Maulamaa wa Shia wametunga tasnifu kadhaa katika kufafanua suala la kuvaa mavazi meusi katika kuomboleza vifo vya viongozi wa kidini, miongoni mwake ni:
- Irshad al-'Ibad ilaa Istihab Labsu as-Sawadi 'ala Sayyid ash-Shuhada' wa al-A'immah al-Amjad: Ni kitabu kilichoandikwa na Sayyid Ja'afar Tabatabai Hairi (aliyefariki mwaka 1321 Hijiria), ambaye ni mjukuu wa Sahibul-Riyadh. [16]
- Agha Bozorge Tehrani amekitaja kitabu fulani kiitwacho Tabyinu al-Rashdi fi Istihabi Labsu as-Sawad 'ala al-A'immah al-Amjad, ambacho baadae kilikuja kufasiriwa kwa lugha ya Kifari na Sayyid Hasan Sadri (aliyefariki 1354 Hijiria). [17]
- Risalatu Mukhtasara fii Labsi as-Sawadi: Nacho ni kitabu kiliandikwa kulingana na mihadhara ya masomo ya Ayatullah Mirza Jawad Tabrizi, kuhussiana na sheria ya kuvaa mavazi meusi. [18] Mbali na kueleza ubora wa kisheria wa kuvaa mavazi meusi wakati wa maombolezo ya Ahlul-Bayt (a.s), pia kitabu hichi kinashughulikia maswali yalioulizwa kuhusiana na mada hii. [19]
Historia ya Kuvaa Mavazi Meusi
Historia ya kuvaa nguo nyeusi inahusiana na utamaduni wa kuvaa mavazi hayo wakati wa maombolezo ndani ya nchi mbali mbali duniani. [20] Hata katika tamaduni za Iran ya zamani, rangi hii ilikuwa ni ishara ya maombolezo, na ilikuwa ni sehemu muhimu ya mila na desturi za maombolezo ndani ya tamaduni za Kiajemi. [21] Kwa mfano, Hamdallah Mustawfi, mwanahistoria kutoka kipindi cha Ilkhani, katika kitabu chake Tarikhe Gozide akizungumzia matokeo ya kuuawa kwa Siawash, anasema kwamba; Suala la kuvaa mavazi meusi na kuwenywele refu, ni miongoni mwa mila na desturi zilizoigwa baada ya kifo cha Siawash. [22] Katika tamaduni ya Kiarabu pia, rangi nyeusi ilikuwa ishara ya maombolezo tangu karne za mwanzo za Hijria. [22] Pia katika maeneo mengi kama vile Iraq na sehemu nyingine, kuvaa nguo nyeusi kulikuwa ni ishara ya huzuni na maombolezo tangu karne za mwanzoni mwa Hijria. [24]
Nyenendo za Bwana Mtume (s.a.w.w) Pamoja na Maimamu (a.s)
Kulingana na maoni ya Ali Abu al-Hasani katika kitabu chake Siya-Poushi dar Soug-e A'immeye Noor (Kuvaa Mavazi Meusi katika Maombolezo ya Maimamu wa Nuru), ni kwamba; mkusanyiko wa ripoti ulioripotiwa katika suala hili, bila kujali kiwango cha uaminifu na tofauti ya thamani ya kila moja kati ya ripoti hizo, ila yaonekana kuwa; bwana Mtume (s.a.w.w) na Maimamu (a.s) walivaa mavazi ya maombolezo ya rangi nyeusi katika maombolezo ya wapendwa wao, na kwamba desturi hii ilikuwa ni ya kawaida baina yao na wafuasi wao. [25]
Kuna ripoti nyingi zinazo onyesha kwamba bwana Mtume na Maimamu (a.s) walivaa nguo nyeusi kama ni ishara ya maombolezo kwa wapendwa wao. Kwa mfano, Zainab binti Umm Salama alivaa nguo nyeusi kwa siku tatu baada ya kifo cha Hamza bin Abdul Muttalib, na Mtume (s.a.w.w) alimpa faraja.[26] Vivyo hivyo, kwa Asmaa binti Umays, Mtume (s.a.w.w) aliagiza avae nguo nyeusi kwa siku tatu kufuatia kifo cha mumewe, Ja'far bin Abi Talib.[27] Na kwa mujibu wa sharh ya Nahjul Balagha na Ibn Abil Hadid, Imamu Hassan Mujtaba (a.s) alihudhuria mkutano wa watu akiwa amevaa nguo nyeusi baada ya kifo cha Imam Ali (a.s). [28] Sheikh Saduq pia, katika Uyun Akhbar al-Ridha, ameandika kuwa Mashia wa Imamu Musa Kadhim (a.s) walivaa nguo nyeusi.[29]
Kwa mujibu wa maelezo ya Allama Majlisi katika kitabu chake Bihar al-Anwar, ni kwamba; Baada ya Yazid kuwaachilia huru mateka wa Karbala, wanawake wote wa Bani Hashim walivaa mavazi meusi na walilia na kuomboleza kifo cha Imamu Hussein (a.s) kwa muda wa siku saba huko Sham (Syria). [30] Kulaini naye katika kitabu cha Al-Kafi amenukuu ripoti inayosema kuwa; mavazi ya Imamu Sajjad (a.s) yalikuwa ni mavazi ya rangi nyeusi. [31] Kulingana na ripoti ya kitabu cha Mahasinu Barqi, ni kwamba; Baada ya kuuawa kwa Imamu Hussein (a.s), wanawake wa Bani Hashim walivaa mavazi meusi na katika harakati za maombolezo ya matokeo ya Karbala, na Imamu Sajjad (a.s) alichukua jukumu la kuwatayarishia chakula. [32] Hadithi hizi zinachukuliwa kuwa ndio Hadithi zenye nguvu zaidi kiushahidi na kimaana katika suala hili. [33]
Utamaduni wa Kawaida wa Kishia Katika Kipindi cha Ghaiba
Kwa mujibu wa ripoti za kihistoria, utamaduni wa kuvaa mavazi meusi ulikuwa ni utamaduni maarufu miongoni mwa Waislamu wa Shia baada ya kumazika kipindi cha uongozi wa Maimamu, na katika Kipindi cha Ghaibatu al-Kubra. Katika kipindi cha utawala wa Alu-Buwaihi, ilikuwa ni kawaida kwa Mashia kuvaa mavazi meusi wakati wa maombolezo ya Ahlul Bayt (a.s). [34] Katika kitabu cha Al-Kamil fi al-Tarikh imeripotiwa kuwa maombolezo ya kwanza rasmi ya Waislamu wa Shia kwa ajili ya Imamu Hussein (a.s) yalifanyika kwa amri ya Mu'izzu al-Dawla Dailami mnamo mwaka wa 352 Hijria, na katika maombolezo haya iliamriwa kuwa wanawake wazitimue nywele zao na wapake rangi nyeusi nyusoni mwao. [35] Katika kitabu kiitwacho Adab al-Taf kuna shairi litokalo kwa mshairi wa karne ya tano Hijria ambalo linaelezea kuvaa mavazi meusi wakati wa maombolezo ya Imam Hussein (a.s). [36]
Inasemekana kuwa Khaaje Ali Siyahpoush (aliyefariki mnamo mwaka wa 830 Hijria), ambaye alikuwa ni miongoni mwa wazawa (mjukuu) wa Sheikh Safiu al-Din Ardabili na ni mmoja wa mababu wa wafalme wa Kisafawi, ambaye alipata umaarufu wa jina hili kutokana na tabia yake ya kuvaa mavazi meusi mara kwa mara katika harakati za maombolezo ya Imamu Hussein (a.s). [37] Pietro Della Valle, mtalii wa Kiitaliano, alielezea maombolezo ya watu wa Isfahan katika kipindi cha utawala wa Kisafawid mnamo mwaka 1027 Hijria, akisema kuwa watu hao walikuwa wakivaa mavazi meusi wakati wa siku za maombolezo ya Muharram. [38]
Count de Gobineau, mwandishi wa Kifaransa, alielezea kuwa; mavazi ya wafalme, mawaziri, na wafanyakazi wakati wa kipindi cha maombolezo wa enzi za utawala Qajar, yalikuwa mavazi meusi na yaliokolea weusi ndani. [39] Wisale Shirazi (aliyefariki mnamo mwaka wa 1262 Hijria), ambaye ni mshairi wa Kishia wa zama hizo, alianza ushairi wake wa maombolezo ya Ashura kwa maneno yasemayo, «Nguo hii nyeusi ya mbingu ni kwa ajili ya maombolezo ya nani?» [40] Charles James Wills, daktari wa Kiingereza wa kipindi cha Qajar nchini Iran, pia aliripoti kuwa vazi rasmi la maombolezo wakati wa Muharram na Safar lilikuwa jeusi, na watu wengi walivaa nguo nyeusi tangu mwanzoni mwa mwezi huo wa Muharram. [41]
Mavazi Meusi ya Bani Abbas
Kulingana na maelezo ya Muhsin Husam Madhahri, mtafiti wa masomo ya kijamii ya Mashia, ni kwamba; watu mashuhuri zaidi wa kuvaa mavazi meusi katika historia ni Abu Muslim Khurasani na wafuasi wake. Kutokana na ripoti hii yaonekana kwamba; baada ya Uslamu, watu hawa walikuwa ndio watu wa kwanza kuinuka na kusimama dhidi ya dhulma huku wakiwa na bendera nyeusi, ambao walijiita kwa jina la "al-Musawwadah" lenye maana ya (wenye kuvaa mavazi meusi). [42] Bani Abbas walisimama wakiwa na bendera na mavazi meusi kama ni alama na ishara ya kutaka kulipiza kisasi cha mauaji ya mashahidi wa Ahlul Bayt (a.s). [43] Baadhi ya wanahistoria wanaamini kwamba uchaguzi wa mavazi meusi kama alama ya Bani Abbas, haukuwa kitu kingine zaidi ya kuonyesha huzuni na majonzi kutokana na misiba iliyo wakumba Ahlul Bayt (a.s) ili kuungana na Mashia. [44] Kulingana na George Ziidan (aliyefariki mnamo mwaka 1332 Hijiria), ni kwamba; Kuvaa mavazi meusi miongoni mwao kulikuwa ndio desturi yao, kiasi ya kwamba mtu yeyote yule aliyetaka kumtembelea Khalifa alilazimika kuvaa joho jeusi linalofunika mavazi yote ya ndani. [45] Baadhi ya watu wanaamini kwamba sababu ya Maimamu kukataza kuvaa mavazi meusi katika baadhi ya Hadithi [46] ilikuwa ni kuzuia watu wasifanane na Bani Abbas na kuzuia matumizi mabaya ya vazi hili. [47]
Ali Abu a-l Hassan akielezea tofauti kati ya vazi la maombolezo la Bani Abbas na lile la Mashia anasema:
- Mashia walikuwa wakivaa mavazi meusi siku maalum kama ni ishara ya maombolezo, lakini Bani Abbas walichagua mavazi meusi kama ni mavazi yao ya kawaida na rasmi. [47]
- Kuvaa mavazi meusi kwa Washia kulikuwa ni jambo la hiari kabisa na lililofanywa ili kuonyesha upendo na huzuni ilioko ndani ya nasfi zao, jambo amablo ni tofauti kwa wafuasi wa Bani Abbas ambao walilazimishwa kuvaa mavazi meusi na hata adhabu zilitolewa kwa wale waliokataa kufanya hivyo. [48]
- Bani Abbas walikuwa na sheria maalum, mtindo na sherehe maalumu za kuvaa mavazi meusi, tofauti na jambo ambalo ni tofauti na Mashia ambao hawakuwa na mambo kama hayo katika suala hili. [49]