Nenda kwa yaliyomo

Mauaji ya kukusudia

Kutoka wikishia

Mauaji ya kukusudia: Ni tendo la makusudi la kuhitimisha uhai wa binadamu fulani bila idhini ya sheria, jambo ambalo limeorodheshwa miongoni mwa madhambi makubwa zaidi katika sheria za Kiislamu. Uhalifu huu wa kuua nafsi kinyume na sheria, ni miongoni mwa dhambi zinazoshutumiwa vikali na dini zote za mbinguni, pamoja na sheria za kibinadamu ulimwenguni. Kwa mujibu wa Aya za Qur'ani, damu ya binadamu inapaswa kuheshimiwa, na kitendo cha kumuua binadamu kinyume na sheria, ni haramu isiyo na pingamizi ndani yake.

Qur'ani Tukufu nayo imeonya vikali na kutoa ahadi ya adhabu kali za Akhera kwa watendao amali hii, huku ikisema kuwa; Watendao dhambi hii watakabiliwa na adhabu ya kubaki milele katika moto wa Jahannamu Siku ya Kiama. Aidha, Qur'ani imesema kwamba; Kuua mtu mmoja kinyume na sheria (kinyume na haki), ni sawa na kuwaangamiza wanadamu wote ulimwenguni. Imenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) kwamba; kesi ya kwanza itakayohukumiwa na Mwenyezi Mungu Siku ya Kiama, ni ile inayohusiana na umwagaji wa damu.

Kwa mujibu wa sheria za Kiislamu, ni haramu kwa mtu yeyote yule kutenda au kushiriki tendo la mauaji ya mtu anayeheshimika mbele ya sheria za Kiislamu, awe ni Muislamu au kafiri asiye mpiganaji anayejaribu kupambana na Uislamu. Fat'wa mashuhuri miongoni mwa mafaqihi wa Kishia kuhusiana na kitendo cha mauaji ya binadamu, inasema kwamba; Mauaji ya kukusudia hutegemea masharti mawili: kwanza, nia ya kukusudia kuua, na pili, matumizi ya chombo fulani kinachosababisha hatari ya mauti, dhidi ya mtu fulani. Katika sheria za Kiislamu, adhabu ya mauaji ya makusudi ni kisasi (yaani ni kuuawa kama vile yeye alivyoua). Vilevile, vitendo kama kujiua na utoaji mimba pia navyo huchukuliwa kama ni mifano hai matendo ya mauaji kwa makusudia.


Uzito wa Dhambi za Mauaji

Tendo la mauaji ya makusudi ni miongoni mwa dhuluma kubwa mno, na kulingana na sheria za Uislamu, dhambi hii ni miongoni mwa dhambi kuu zilizoorodheshwa katika vyanzo mbali mbali vya kidini. [1] Kuhusiana na dhambi hii hatari, Uislamu umeahidi adhabu ya milele kwa wale wote wanaotenda mauaji ya makusudi. [2] Vilevile, dini zote za mbinguni zimeharamisha kitendo cha mauaji ya makusudi kinyume na sheria, na kukitambua kuwa ni miongoni mwa makosa makubwa zaidi ya kimaadili yatendekayo ulimwenguni. [3] Kanuni inayoharamisha mauaji ya nafsi, ni kanuni inayokubalika na kuungwa mkono na sheria zote za kibinadamu ulimwenguni. [4] Haki ya kuishi, ikiwa ni moja ya haki msingi za kibinadamu, ndiyo msingi mkuu wa haki zonte nyingine zote za kibinadamu. [5] Msingi ambao umetambuliwa na kuwekwa wazi katika vyanzo na nyaraka mbalimbali za kimataifa za ulinzi wa haki za binadamu. [6] Umuhimu wa suala hili pia unaweza kuupata katika vyanzo vya maudhui kadhaa za kidini, ikiwa ni pamoja na maudhui inayohusiana na uharamu wa kuua nafsi, kujiua, na kitendo cha kuua fetasi (kutoa mimba). [7]

Uharamu wa kuua nafsi umepewa uzito mkubwa katika fiqhi (sheria) ya Kiislamu, [8] huku hukumu zinazohusiana na mauaji zikijadiliwa katika nyanja mbalimbali za kifiqhi kama vile jihadi, amri ya kufanya mema na kukataza maovu, mirathi, huduud (adhabu za kifiqhi), qisas (kisasi), na diya (malipo faini). [9]

Suala la kuheshima damu ya mwanadamu -kama tunavyoona katika dini ya Kiislamu- halijazingatiwa kwa Waislamu peke yao; bali pia linahusisha na wale wote wasio Waislamu, ambao hawapo hali ya katika vita dhidi ya Waislamu, pamoja na wale wote wanaoishi kwa amani pamoja na Waislamu. [10]

Ujumbe wa Imam Ali (A.S.) kwa Malik al-Ashtar:


"Kwa hiyo, usithibitishe uwezo wa mamlaka yako kwa njia ya kumwaga damu kinyume na sheria; kwani kitendo hichi ni miongoni mwa yale yanadhoofisha na kudunisha mamlaka yako, na pengine hata kuyaangamiza kabisa kabisa. Na hakuna udhuru wowote utakaokubaliwa mbele ya Mungu kuhusiana na kosa la mauaji ya makusudi." [11]


Ufafanuzi, Masharti, na Sheria

Kiuhalisia mauaji yamegawanywa katika aina tatu kuu; Mauaji ya makusudi, Mauaji ya nusu makusudi, na mauaji ya bahati mbaya. [12] Mauaji ya makusudi kinyume na sheria, ni yale mauaji ya kumuua mtu bila ya mtu huyo kufanya kosa la mauaji au ufisadi maalumu duniani. [13] Katika fiqhi (shria) ya Kiislamu, kuthibiti kosa la mauaji ya makusudi huwa kinazingatia vigezo maalumu, navyo ni kwamba; muuaji awe mtu mzima na mwenye akili timamu, na awe na nia ya kutenda kitendo kinachosababisha mauaji pale atimizapo mauaji hayo, au atende kitendo ambacho kwa kawaida husababisha mauaji, huku akiwa na nia ya kuua ndani ya utendaji wake. [14]

Baadhi ya sheria nyingine zinazojadiliwa katika hukumu za mauaji ya makusudi ni kama zifuatazo:

1.     Katika sheria za Kiislamu Mauaji ya makusudi yanayofanywa na mtoto au mwendawazimu, huhisabiwa kama ni mauaji ya bahati mbaya. [15]

2.     Kwa mujibu wa fatwa mashuhuri miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu, mauaji ya makusudi yanahitaji kuthibitishwa kupitia ushahidi wa wanaume wawili tu waadilifu. [16]

3.     Kulingana na sheria za Kiislamu, kujitoa uhai (kujiua) [17] na kutoa mimba pia ni miongoni mwa aina za mauaji ya makusudi. [18]

4.     Ikiwa aliyeuawa ni miongoni mwa jamaa wa muuaji, tendo hili la mauaji ya makusudi huspelekea mtendaji wa mauaji hayo kunyimwa urithi. [19]

5.     Kwa mujibu wa sheria za Kiislamu, ni haramu mtu fulani kumuua mtu anayeheshimika mbele ya sheria za Kiislamu, kama vile kumuua Mwislamu au kafiri asiyekuwa na uadui dhidi ya Uislamu, isipokuwa kama kumuua kwake kutakuwa kumeidhinishwa na kitengo cha kisheria za Kiislamu; kama vile kuuawa kwa mvamizi kwa nia na lengo la kujilinda dhidi ya madhara yake, au kumuua mtu fula katika hali ya vita, au katika kisasi, au kutekeleza hukumu hiyo dhidi ya mhalifu afanyaye ufisadi nchini. [20]

6.     Kwa mujibu wa fatwa maarufu zaidi miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu ni kwamba; Ni haramu mtu fulani kumuua mtu mwengine, hata kama atakuwa katika hali ya takiyya (kuficha itikadi yake) au atakuwa amepewa shinikizo la lazima linalomtaka kutenda tendo hilo. Na hata ikiwa maisha ya mtu fulani yako hatarini, bado tendo hilo litahisabiwa kuwa nit endo la haramu. Na iwapo ataamua kutenda tendo hilo, mtu huyo kisheria atakabiliwa na hukumu ya kufanyiwa kisasi dhidi yake. [21]

Mauaji ni Miongoni mwa Dhambi Kubwa Katika Qurani

Kwa mujibu wa maelezo na mafundisho ya Qur’ani; kuheshimu damu za wanadamu ni wajibu wa kimaadili na kisheria wa kila mwanadamu, na haramu kabisa kabisa kuua nafsi kinyuma na sheria za Mungu.[22] Tendo la mauaji, la kumuua mtu asiye na hatia, huchukuliwa kuwa ni miongoni mwa dhambi kubwa mno katika mafundisho ya Qurani. [23] Nasir Makarim Shirazi, mfasiri mashuhuri wa Qur’ani tukufu, anabainisha akisema kwamba; adhabu za Kiakhera zilizotajwa katika Qurani juu ya kosa la wauaji kinyume na sheria, ndiyo adhabu kali zaidi miongoni mwa zinazoweza kufikiriwa dhidi ya watendaji wa makosa mbali mbali. [24]

Aya za Qurani zinasisitiza adhabu kali kwa watendaji wa kosa hili kwa kusema kwamba; "Na yeyote atakayemuua mtu mwenye imani kwa makusudi, basi huyo adhabu yake itakuwa ni moto wa Jahannam; na atadumu humo milele, na Mungu atamkasirikia, atamlaani, na atamwandalia adhabu kubwa dhidi yake".[25]

Adhabu Nne Kali Kwa Wauaji Kinyume na Sheria Kulingana na Qurani:

1.    Kudumu milele katika Jahannam: Wauaji wa makusudi kinyume na sheria wanahukumiwa kutokomea milele katika adhabu ya moto wa Jahannam.

2.    Kukumbwa na ghadhabu za Mungu: Ghadhabu za Mwenye Ezi Mungu ni adhabu kubwa ya kiroho inayokumba wauaji watendao mauaji kinyume na sheria, hii ni kwa sababu ya kitendo chao cha kuvunja heshima ya uhai wa mwanadamu.

3.    Kuangukiwa na laana za Mungu: Mwenye Ezi Mungu huwalaani wauaji kinyume na sheria, ikiwa ni alama ya kutengwa na rehema za Mungu milele.

4.    Kupata adhabu kubwa: Adhabu kubwa ya Kiakhera inawasubiri wale waliokiuka amri za Mwenye Ezi Mungu kwa makusudi, na kuua nafsi ni miongoni mwa makosa hayo makubwa. [26]

Mauaji ya Mtu Mmoja ni Sawa na Kuua Wanadamu Wote

Qur’ani Tukufu ili kutahadharisha juu utendaji wa dhambi hii, inatoa msisitizo mkubwa juu ya thamani ya maisha ya mwanadamu. Ili kufikisha ujumbe huo, Qur’ani inasema kwamba; mauaji yasiyo ya haki ya mtu mmoja asiye na hatia, ni sawa na kuua wanadamu wote waliomo arhini humu. Kuhusiana na hili Aya ya 32 ya Suratu Al-Ma'idah inasema:

"Na kwa sababu hiyo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba yeyote atakayemuua mtu fulani, bila ya yeye kutenda kosa la kuua mtu fulani au kufanya uharibifu katika ardhi, (dhambi zake) huwa ni kama kwamba amewaua wanadamu wote; na yeyote yule atakayemwokoa mtu fulani, ni kama kwamba amewaokoa wanadamu wote."

Allama Muhammad Husayn Tabataba'i, mfasiri maarufu wa Qurani, katika tafsiri yake Al-Mizan, ameeleza kwa kina maana ya aya hii. Anabainisha kuwa kuua mtu asiye na hatia ni tendo linalochukuliwa kuwa sawa na kuharibu mpango wa uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Mungu ameumba mwanadamu ili kuendeleza kizazi chake kwa misingi ya maadili na ustawi wa jamii. Kitendo cha mauaji yasiyo ya haki kinaharibu kusudi hili na kubatilisha thamani ya maisha kama zawadi takatifu kutoka kwa Muumba.

Tabataba'i pia anaeleza kuwa uzito wa dhambi hii unatokana na athari zake za kijamii na kiroho, kwani kuua mtu mmoja huathiri familia, jamii, na maadili ya kiulimwengu. Kwa upande mwingine, kuokoa maisha ya mtu mmoja kunathaminiwa sawa na kuokoa wanadamu wote kwa sababu kinacholindwa si tu uhai wa mtu binafsi, bali pia msingi wa maisha ya jamii kwa ujumla.


Hadithi Kuhusu Mauaji ya Makusudi

Kuna Hadithi nyingi zinazosisitiza ukubwa wa dhambi za kosa la mauaji ya makusudi. [30] Katika moja ya Hadithi bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w), anasema kwamba; Jambo la kwanza ambalo Mwenyezi Mungu atalishughulikia Siku ya Kiyama ni kosa la kumwaga damu. [31] Pia katika Hadithi nyingine kutoka kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), imeelezwa ya kwamba; Uharibifu wa dunia nzima, ni rahisi zaidi mbele ya Mungu kuliko kumwaga damu kinyume na sheria. [32] Katika barua ya Imamu Ali (a.s) kwa Malik al-Ashtar, amemwandikia akimwambia: "Jiepushe na kumwaga damu kinyume na sheria; kwani hakuna kitu kinachoweza kuleta maharibifu zaidi juu ya majaaliwa kuliko kitendo hiki, na hakuna kitu chenye athari mbaya zaidi kuliko hicho, na hakuna kitu kinachoweza kuondoa neema kama kitendo hicho". [33]

Adhabu ya Mauaji Katika Sheria za Nchi Mbalimbali

Kuna adhabu kali zilizowekwa katika sheria za jinai za nchi mbalimbali dhidi ya kkosa la mauaji ya makusudi. Miongoni mwazo ni; adhabu ya kifo, kifungo cha maisha, au vifungo vya muda mrefu. [34] Katika sheria za Kiislamu, adhabu dhidi ya kosa la mauaji ya makusudi ni adhabu ya kisasi (kuuawa). [35] Katika sheria za Kiislamu, walii wa marehemu wana haki ya kutekeleza moja ya hukumu zilizowekwa na sheria za Kiislamu tatu dhidi ya kosa la muuaji. Huku tatu hizo ni; kisasi, kusamehe bila kudai fidia (faini ya kifedha) ya damu, au kusamehe kwa kudai fidia ya damu. [36]

Adhabu dhidi ya kosa la mauaji ya makusudi katika baadhi ya nchi kama vile Kanada na Uingereza, huwa ni adhabu ya kifungo cha maisha. [37] Nchini Iraq, adhabu kuu kwa mhalifu aliyeua kwa makusudi kinyume na sheria, ni kifungo cha muda meru au kifungo cha maisha, na katika hali maalum, katika nchi hiyo adhabu ya mauaji ya makusudi huwa ni hukumu ya kifo. [38]

Kulingana na kifungu cha 381 cha Sheria ya Adhabu za Kiislamu ya Iran, iliyopitishwa mwaka 2013, adhabu ya mauaji ya makusudi ni hukumu ya kisasi. Kulingana na sheria hii, ikiwa walii wa marehemu ataridhia, kupokea malipo ya fidia ya damu, mhusika wa kosa hilo atawajibika kulipa fidia hiyo badala ya kukabiliwa na adhabu ya kifo (kisasi). [39]

Kulingana na kifungu cha 295 cha Sheria ya Adhabu za Kiislamu, kukosa kutekeleza kitendo kitachoweza kusababisha kifo kwa mtu fulani, chini ya masharti fulani, mauaji hayo yanaweza kuchukuliwa kuwa ni moja ya aina za mauaji ya makusudi. Miongoni mwa mifano inayoweza kuingia katika kosa la mauaji ya makusudi ni; kama vile mama au yaya fulani aliyekabidhiwa kunyonyesha mtoto fulani, ataacha kumnyonyesha mtoto huyo hadi afe, au kama daktari au muuguzi ataacha kutekeleza wajibu wake wa kisheria na kusababisha mtu fulani kupoteza maisha kutokana na uzembe wa daktari huyo. [40]