Mukhtar ibnu Abi Ubaid al-Thaqafi
- Makala hii inamzungumzia Al-Mukhtar ibn Abi Ubayd al-Thaqafi. Ili kujua kuhusu mapinduzi yake angalia makala ya harakati na mapinduzi ya Mukhtar.
Mukhtar ibn Abi Ubayd Thaqafi (1-67 Hijiria) ni miongoni mwa tabiina (waliokutana na masahaba wa Mtume) ambaye alianzisha harakati na mapinduzi kwa ajili ya kulipiza kisasi cha damu ya Imamu Hussein (a.s). Katika tukio la Karbala, Mukhtari alikuwa na jukumu la kuwa mwenyeji wa Muslim bin Aqil, mjumbe wa Imamu Hussein (a.s) katika mji wa Kufa na alishirikiana naye mpaka alipouawa shahidi, kisha Ubaydullah bin Ziyad akamtia jela. Kwa msingi huo, hakuweko katika tukio la siku ya Ashura huko Karbala.
Mwaka 66 Hijiria, Mukhtar alianzisha uasi dhidi ya mtawala wa Kufa. Katika mapinduzi haya, akthari ya waliohusika katika tukio la Karbala waliuawa. Mukhtar aliuawa na Mus’ab bin Zubeir baada ya kutawala Kufa kwa muda wa miezi 18. Kando ya msikiti wa Kufa kuna kaburi linalonasibishwa na yeye na ambalo liko jirani na kaburi la Muslim bin Aqil.
Kuhusiana na shakhsia ya Mukhtar, mapinduzi yake na utendaji wake kuna nadharia na maoni tofauti na kumeandikwa vitabu mbalimbali kuhusiana na hilo. Baadhi wanaamini kwamba Mukhtar alianzisha mapinduzi kwa idhini ya Imamu Zainul Abidin (a.s) kwa ajili ya kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein (a.s), lakini wengine wanamwona kuwa ni shakhsia aliyekuwa akisaka madaraka ambaye alianzisha harakati hiyo kwa lengo la kutaka kutawala. Wengine pia wanaamini kwamba, Mukhtar alikuwa Shia, lakini utendaji wake hauungwi mkono, hata hivyo, sio mtu wa motoni. Chanzo cha rai hizi ni aina mbili za hadithi ambazo ndani yake Mukhtar anasifiwa na kukosolewa. Baadhi ya wasomi wa elimu ya hadithi wa Kishia kama Abdallah Ma'maqani na Ayatullah Khui wamefadhilisha hadithi zinazomsifu.
Nasaba na lakabu
Mukhtar bin Abi Ubayd bin Masoud al-Thaqafi anatokana na kabila la Thaqif. [1] Baba yake Abu Ubayd aliyekuwa mmoja wa masahaba wa Mtume (s.a.w.w) [2] aliuawa katika vita vya Qadisiyah wakati wa Khalifa wa pili. [3] Masoud Thaqafi alikuwa mmoja wa wazee wa Hijaz na alipewa lakabu ya Adhim al-Qariyatayn (mzee wa Makkah na Taif). [4] Mama yake ni Dawmah binti Amr bin Wahab, ambaye ametajwa na Ibn Tayfur katika orodha ya wanawake waliokuwa na balagha na fasaha katika kitabu chake cha Balaghat al-Nisa [5] Kwa mujibu wa Ibn Athir, mwanahistoria wa karne ya 7 Hijiria, Mukhtar hakuwa miongoni mwa masahaba. [6] Hata hivyo, wasifu wake umejumuishwa katika vyanzo vya kuelezea wasifu wa masahaba. [7]
Kuniya ya Mukhtar ni Abu Is’haq [8] na lakabu yake ni Kayyisan (mjanja mwenye akili). [9] Imenukuliwa kutoka kwa Asbagh Nubatah kwamba, wakati Mukhtari alipokuwa mdogo, Imam Ali (a.s) alimpakata na kumuita kwa lakabu ya Kayyis. [10]
Kushiriki vita vya Qadisiyya
Mukhtar alizaliwa katika mwaka wa kwanza wa Hijiria. [11] Inaelezwa kwamba akiwa na umri wa miaka 13, alishiriki katika Vita vya al-Jisr, mojawapo ya vita vya Qadisiyya, na alikuwa akijaribu kuingia kwenye medani ya vita. Lakini ami yake Sa’d bin Mas’ud alimzuia. [12] Baba na kaka yake Mukhtar waliuawa katika vita hivi. [13]
Sa’d bin Mas’ud Thaqafi, ami yake Mukhtar, alikuwa gavana wa Mada'in kwa niaba ya Imam Ali (a.s). [14] Alimteua Mukhtar kuwa mrithi wake huko Mada'in wakati alipoondoka kwa ajili ya kupigana na Makhawarij. [15]
Bega kwa bega na Muslim bin Aqil
Kwa mujibu wa Shamsuddin Dhahabi, Mukhtar alikwenda Basra katika zama za utawala wa Muawiya na akawaita na kuwalingania watu kwa Imamu Hussein (a.s). Wakati huo, Ubaydullah bin Ziyad, ambaye alikuwa ameteuliwa na Muawiya kuwa gavana wa Basra, alimkamata na kumpeleka uhamishoni Taif. [16]
Mukhtar alishirikiana na Muslim bin Aqil, mjumbe wa Imamu Hussein (a.s) huko Kufa. Muslim alipoingia Kufa, alikwenda nyumbani kwa Mukhtar. [17] Baada ya Ubaydullah bin Ziyad kujua mahali alipo Muslim, mjumbe huyo wa Imamu Hussein alihamia nyumbani kwa Hani bin Urwa. [18] Pia, kwa mujibu wa ripoti za kihistoria, Mukhtar alitoa kiapo cha utii kwa Muslim bin Aqil, [19] alikuwa nje ya Kufa siku ya kuuawa kishahidi Muslim na alisikia habari za kuanza mapema zaidi kabla ya wakati wake harakati ya Muslim; lakini alipofika Kufa, Muslim na Hani walikuwa wameshauawa shahidi. [20]
Kutokuweko Karbala
Katika siku ya Ashura Mukhtar alikuwa gerezani. Kwa hiyo, hakuwepo katika tukio la Karbala. Baada ya kuuawa shahidi Muslim, Ibn Ziyad alikusudia kumuua Mukhtar, lakini kwa upatanishi na uombezi wa Amr bin Hurayth, alijizuia kumuua. Lakini alimtia gerezani. Mukhtar alikuwa gerezani hadi baada ya tukio la Karbala. [21] Baada ya tukio la Karbala, Mukhtar aliachiliwa huru kwa upatanishi wa Abdullah ibn Umar, ambaye alikuwa mume wa Safiyya, dada yake Mukhtar. [22] Aliachiliwa huru mbele ya Yazid bin Muawiyah. [23] Kwa mujibu wa ripoti ya Abd al-Razzaq Maqram, wakati mateka wa Karbala walipoletwa kwenye baraza la Ibn Ziyad, mtawala huyo aliamrisha kuletwa pia Mukhtar ambaye alikuwa mfungwa wakati huo. Katika kikao hiki kulitokokea majibizano makali ya maneno kati ya Mukhtar na Ibn Ziyad. [24] Kwa mujibu wa ripoti hii, Mukhtar aliachiliwa kutoka gerezani baada ya kuuawa shahidi Abdullah bin Afif; lakini Ubaydullah bin Ziyad aliweka sharti kwamba naye asikae Kufa kwa zaidi ya siku tatu. Baada ya kuuawa shahidi Abdullah bin Afif, Ubaydullah alisoma khutba ambayo ndani yake aliwatukana Ahlul-Bayt (a.s). Mukhtar akampinga na Ibn Ziyad akamfunga tena; lakini aliachiliwa kwa uombezi wa Abdullah bin Omar. [25]
Kutoa baia kwa Abdullah bin Zubeir
Mukhtar alitoa baina na kiapo cha utii kwa Abdullah bin Zubeir, kwa sharti kwamba ashauriane naye katika masuala mbalimbali. [26] Katika shambulio la jeshi la Yazid huko Makka na kuzingirwa kwa Abdullah bin Zubeir, Mukhtar alipigana pamoja na Abdullah, dhidi ya jeshi la Yazid [27]. Baada ya kifo cha Yazid Ibn Muawiya, Ibn Zubeir alidai ukhalifa. Mukhtar pia alikwenda Kufa na akafanya maandalizi ya uasi na harakati yake. [28] Ibn Zubeir alimteua Abdullah bin Mut’i kuwa gavana wa Kufa. Mukhtar alipigana naye na akamshinda. [29]
Kwa nini Mukhtar hakushiriki harakati ya Tawwabina
- Makala asili: Harakati ya Tawwabina
Mukhtar hakushiriki katika uasi na harakati ya Tawwabina; kwa sababu aliuona uasi na harakati hiyo kwamba, haina maana na isiyokuwa na faida na alimuona Suleiman bin Surad al-Khaza'i kuwa mtu asiye na ujuzi na mbinu za vita. [30] Kufuatia kutoshiriki kwa Mukhtar, watu 4,000 kati ya 16,000 waliotoa kiapo cha utii kwa Suleiman hawakushiriki katika vita. [31] Mukhtar alifungwa gerezani sambamba na kutokea harakati ya tawwabina. [32] Baada ya kushindwa kwa harakati ya tawwabina, Mukhtar, aliwandika barua manusura wa harakati hiyo na kuwafariji. [33] Viongozi wa Tawwabina walitaka kumuachilia huru kutoka gerezani; lakini Mukhtar aliwaonya, na akaachiliwa kupitia upatanishi wa Abdullah bin Omar. [34]
Kisasi dhidi ya wahusika wa mauaji ya Karbala
- Makala asili: Harakati ya Mukhtar
Katika mwaka wa 66 Hijiria, Mukhtar alianzisha harakati kwa ajili ya kulipiza kisasi damu ya Imamu Hussein (a.s) na Mashia wa Kufa walijiunga naye. [35] Katika harakati yake hii, Mukhtar alitumia kauli mbiu mbili, "Ya Latharat al-Hussein" na " ya Mansour Amit". [36] Katika harakati hii, Mukhtar aliua idadi kadhaa ya wahusika wa mauaji ya Karbala kama Shimr bin Dhil al-Jawshan, Khawli bin Yazid, Umar bin Sa’d na Ubaydullah bin Ziyad. [37] Alipeleka vichwa vya Ubaydullah bin Ziyad na Umar bin Sa’d kwa Imam Sajjad (a.s.) huko Madina. [38]
Uhusiano wake na Imamu Sajjad (a.s)
Kumenukuliwa ripoti mbalimbali kuhusianan na uhusiano wa Imamu Sajjad (a.s) na Mukhtar. Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa katika Rijal Kashi, Mukhtar alituma dinari 20,000 kwa Imamu wa nne na akazitumia kuikarabati nyumba ya Aqil bin Abi Talib na Bani Hashim wengine zilizokuwa zimeharibiwa. Mukhtar kwa mara nyingine tena alituma dinari 40,000 kwa Imam Sajjad, lakini Imamu hakukubali kuzipokea. [39] Na pia alimpa Imamu Sajjad kijakazi (mama yake Zayd bin Ali) ambaye alimnunua kwa dirham 30,000 kama zawadi. [40] Mukhtar baada ya kumuua Ubaydullah, alikipeleka kichwa chake kwa Imam Zainul al-Abidin (a.s). Imamu alisujudu kwa kushukuru, na ilikuwa wakati huu ambapo wanawake wa familia ya Bani Hashim walitoa nguo za maombolezo walizokuwa wamezivaa kwa ajili ya Imamu Hussein (a.s). [41]
Kwa mujibu wa hadithi nyingine, kundi la viongozi wa Kufa lilikwenda kwa Imamu Sajjad (a.s) na kumuuliza kuhusu jukumu Mukhtar, na Imamu wa nne akawatuma kwa Muhammad bin Hanafiyya na kusema: “Ewe ami, ikiwa mtumwa mweusi ataonyesha taasubi ya kutupenda sisi Ahlul-Bayt ni wajibu kwa watu kumuunga mkono na kumsaidia. Fanya lolote utakalo kuhusiana na hili, mimi nimekufanya mwakilishi katika jambo hili. [42] Ayatullah Khui [43] na Ma'maqani [44] wanaamini kuwa, mapinduzi na harakati ya Mukhtar ilifanyika kwa idhini ya Imamu Zainul-Abidin (a.s).
Uhusiano wake na Muhammad Hanafiyya
Kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, Mukhtar alikuwa akiwalingania watu kwenye Uimamu wa Muhammad bin Hanafiyya. [45] Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana wengine wanamwita na kuumtaja kama mwanzilishi wa Kaisaniya na wafuasi wake wanajulikana kama Kaisaniya. [46] Kwa mujibu wa Ayatullah Khui, hii si kweli kwa sababu Muhammad Ibn Hanafiyya hakudai Uimamu, hata Mukhtar awaite na kuwalingania watu kwake. [47] Pia, kundi la Kaisaniya liliundwa baada ya kuuawa kwa Mukhtar na baada ya kuaga dunia Muhammad bin Hanafiyya. [48] Kwa mujibu wa Ma'maqani, kwamba; hii lakabu ya Mukhtar kuitwa Kaisani haithibitishi kwamba yeye ni mfuasi wa kundi Kisaniyah. [49]
Kuokolewa Muhammad ibn Hanafiyya
Baada ya Abdullah bin Zubeir kupata habari ya kuanza harakati ya Mukhtar, alimshinikiza Muhammad bin Hanafiyya na jamaa zake wa karibu ili wampe kiapo cha utii na akatishia kuwachoma moto. Ibn Hanafiyya alimuandikia barua Mukhtar na kumwomba msaada. Mukhtar alituma kundi la watu huko Makka na kuwaokoa. [50]
Hadithi tofauti kuhusu Mukhtar
Kuna aina mbili za hadithi zilizonukuliwa kuhusiana na Mukhtar ambapo baadhi yazo zinamlaumu na kumkosoa na zingine zinamsifu.
Hadithi za kumsifu
- Imenukuliwa kutoka kwa Imamu Sajjad (a.s) akisema: Mwenyezi Mungu ampe Mukhtar malipo ya kheri. [51]
- Imamu Swadiq (a.s) alipokutana na Abul-Hakam mtoto wa Mukhtar baada ya kumkirimu alimsifu na kumtaja kwa wema Mukhtar na akamwambia mtoto wa Mukhtar: Mwenyezi Mungu amrehemu baba yako. [52] Abdallah Ma'maqani, msomi na mwanazuoni wa Kishia wa elimu ya kutathmini wapokezi wa hadithi anasema kuwa, hatua ya Imam Swadiq ya kumuombea rehma Mukhtar ni hoja ya kuwa sahihi itikadi yake; kwa sababu katika madhehebu ya Imamiya ridhaa ya Maimamu inafuata ridhaa ya Mwenyezi Mungu. Kwa msingi huu, si jambo linaloingilika akilini kwa Imamu Swadiq kumuombea rehma mtu ambaye itikadi yake ni potofu na kuanzisha harakati tu ya kulipiza kisasi cha damu ya Imamu Hussein (a.s) si kitu cha kuhalalisha hilo. [53]
Hadithi za kumlaumu na kumkosoa
- Imepokewa kutoka kwa Imamu Muhammad Baqir (a.s) kwamba, Imam Sajjad (a.s) alikataa kuwaruhusu wajumbe wa Mukhtar wakutane naye na akarudisha zawadi zake na kumwita mwongo. Ma'maqani ameitambua hatua na radiamali hiyo ya Imamu Sajjad kwamba, ilitokana na kumuogopa Abdul-Malik bin Marwan na kufanya taqiyyah. [54]
- Imam Sadiq (a.s): Mukhtar alikuwa akisema uongo dhidi ya Imamu Sajjad (a.s). [55] Kwa mujibu wa Ayatullah Khui, hadithi hii ni dhaifu kwa upande wa sanadi na mapokezi. [56]
- Akiwa Sabat, Mukhtar alimpa pendekezo ami yake Sa'd bin Masoud amkabidhi Imam Hassan (a.s) kwa Muawiyah ili nafasi yake isitetereke .[57] Kwa mujibu wa Ayatullah Khui, hadithi hii si ya kutegemewa kutokana na ukweli kwamba, ni mursal (hakujatajwa jina la mpokezi katika sanadi na mapokezi ya hadithi). Kadhalika kama tutajaalia usahihi wake, inawezekana kusema kuwa, Mukhtar hakuwa na nia ya dhati katika kauli yake; badala yake, alitaka kugundua maoni ya ami yake. [58]
- Kulingana na hadithi, Mukhtar ni mtu wa motoni, lakini Imamu Hussein (a.s) atamuombea. [59] Hadithi hii ni dhaifu kwa mujibu wa wanazuoni wa Elimu ya al-Rijal. [60]
- Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, Mukhtar alidai Utume [61] Kulingana na Abdallah Ma'maqani, hakuna athari ya madai haya katika vyanzo vya Shia, na Waislamu wa Kisuni ndio waliompachika na kumpa sifa hii; kwa sababu aliwaua baadhi ya shakhsia kubwa waliohusika katika tukio la Karbala. [62]
Ayatullah Khui, baada ya kutaja hadith za kusifu na kulaumu, alifadhilisha zaidi hadithi za kumsifu Mukhtar mbele ya hadithi za kumkosoa na kumlaumu.[63]
Mitazamo mbalimbali kuhusu Mukhtar
Kuna mitazamo na nadharia mbalimbali kuhusiana na shakhsia ya Mukhtar.
Mukhtar mlipiza kisasi cha damu ya Ahlul-Bayt (a.s)
Baqir Sharif Qurashi anaamini kwamba, harakati na mapinduzi ya Mukhtar lengo lake halikuwa ni kutaka jaha na uongozi bali alianzisha harakati hiyo kwa ajili ya kulipiza kisasi cha damu ya Ahlul-Bayt (a.s) na kulipiza kisasi dhidi ya wauaji wao. [64] Najmuddin Tabasi pia anasema kuwa, hatua ya Imamu Baqir ya kumuombea rehma Mukhtar kwa namna fulani ni kuunga mkono matendo yake na mauaji aliyofanya dhidi ya wauaji wa Imamu Hussein (a.s) [65] Ibn Nama Hilli anaamini kwamba, dua ya kheri ambayo Imamu Sajjad (a.s) alimuombea Mukhtar ni uthibitisho kwamba alichukuliwa na Imam Sajjad (a.s) kuwa mmoja wa watu wasafi na wema. [66]
Abdallah Ma'maqani amemtambua Mukhtar kwamba, ni Shia Imamiya lakini akasema mithaki na kuwa kwake thiqa na mtu wa kuaminika hakujathibiti. [67] Kwa mujibu wake, Allama Hilli pia alimtaja Mukhtar katika sehemu ya kwanza ya kitabu chake, na hakumjumuisha kama mtu asiyekuwa Shia Imamiya.
Mukhtar alipigania madaraka
Baadhi wanaamini kwamba inaweza kwa kuangalia majimui ya ushahidi ikafahamika kwamba, harakati ya Mukhtar ilikuwa kwa ajili ya kupata mamlaka, uongozi na madaraka. [69] Kwa mujibu wa maoni haya, Mukhtar aliwatumia Ahlul-Bayt kama chombo na alikusudia kufikia malengo yake kupitia kwao.[70] Kulingana na Rasul Jafarian, mwandishi wa historia ni kwamba, maneno haya si sahihi na ni matokeo ya propaganda na mazingira dhidi ya Mukhtar yaliyoandaliwa na Bani Umayya na Zubayriyan.[71]
Kujizuia kutoa hukumu kuhusu Mukhtar
Kundi la wanazuoni wa Kishia wamekataa kutoa maoni ya moja kwa moja kuhusu Mukhtar; katika kitabu Jam'i Al-Ruwat, imenasibishwa kwa Mirza Muhammad Astrabadi kwamba, haipasi kumtaja kwa ubaya Mukhtar; hata hivyo, hazitambui hadithi zake kuwa ni za kutegemewa na amejizuia kumzungumzia Mukhtar.[72] Allama Majlisi hajaitambua imani ya Mukhtar kuwa ni kamilifu na amezitambua hatua zake kuwa alizifanya bila ya idhini na ruhusa ya Imamu Maasumu. Pamoja na hayo, anaamini kwamba kwa sababu Mukhtar amefanya mema mengi, amekuwa mwisho mwema. Hata hivyo yeye pia, amesimamia hapo na hajamzungumzia kwa undani Mukhtar. [73] Sha'rani katika Dam'i al-Sujum anaamini kuwa, Mukhtar ni mmoja wa watu waliokuwa na akili na mashujaa miongoni mwa Waarabu na anapinga madai ya kuweko habari zinazogongana kuhusiana na Mukhtar na anasema kwamba, hesabu ya waja siku ya Kiyama ipo mikononi mwa Mwenyezi Mungu na Mukhtar pia kama walivyo walio wengi miongoni mwa watu amefanya mambo mazuri na mabaya. [74]
Mtazamo wa Maulamaa wa Kisuni
Katika baadhi ya vyanzo vya Sunni, Mukhtar amepewa sifa kama vile nasibi (mtu mwenye chuki na Imamu Ali na Ahlul-Bayt) na mwongo. Kuna hadithi inayohusishwa na Mtume (s.a.w.w) ya kwamba, amesema, mwongo na mtenda jinai atatoka Thaqif. Riwaya hii imepokewa na Asma binti Abu Bakr, mama yake Abdullah bin Zubeir. [75] Inasemekana kwamba maana ya Kadhaabu (mwongo) katika riwaya hii ni Mukhtar. [76] Wasomi wanaokosoa kauli hii wanasema kwamba, jina la Mukhtar halikutajwa katika riwaya hii bali jina lake liliongezwa na mpokezi. Pia hadithi hii inakinzana na riwaya nyinginezo ambamo wametambulishwa watu wengine kwamba, ndio kigezo cha uongo na uhalifu. [77] Kwa mujibu wa ripoti, Hajjaj bin Yusuf alikuwa akiamuru watu wamlaani Imamu Ali (a.s) na Mukhtar. [78] Moqrizi pia anamtambua Mukhtar kuwa ni katika Makhawariji [79].
Mke na watoto
Mukhtar Thaqafi alikuwa na wake wanne:
Mke wa Kwanza: Umm Thabit, binti ya Samura bin Jundab. [80]
Mke wa Pili: Umra binti Nu'man bin Bashir (mwanamke wa kwanza aliyekatwa kichwa katika Uislamu). [81]
Mke wa Tatu: Umm Zayd al-Sughra, binti ya Said bin Zayd bin Amr.[82]
Mke wa nne: Umm Walid, binti ya Umair Bin Ribah. [83] Umm Thabit alimzalia Mukhtar watoto wawili ambao ni Muhammad na Is'haq, [84] na Ummu Walid akamzaa Umm Salama [85]. Ummu Salamah alikuja kuolewa na Abdullah bin Abdullah bin Omar bin al-Khattab.[86]
Watoto wengine wa Mukhtar ni Abul-Hakam, [87], Jibr [88], Umayya, [89] Bilal, [90] na Omar. [91]
Kuaga dunia na lilipo kaburi lake
Baada ya miezi 18 ya utawala, Mukhtar aliuawa na Mus'ab bin Zubeir akiwa na umri wa miaka 67 mnamo tarehe 14 Ramadhani [92] mwaka wa 67 Hijiria. [93] Kaburi la Mukhtar liko karibu na msikiti wa Kufa, na katika Kitabu Al-Mazar Shahidi Awwal ziara yake imetajwa. [95]
Athari kuhusiana na Mukhtar
- Makala asili: Orodha ya vitabu kuhusiana na Mukhtar Thaqafi
Kumeandikwa athari mbalimbali kuhusiana na Mukhtar. Katika vitabu hivi kumefanyiwa uchunguzi na kutolewa ufafanuzi kuhusiana na shakhsia ya Mukhtar pamoja na malengo ya thaura na mapinduzi yake. Agha Bozorg Tehrani ametaja katika kitabu chake cha al-Dharia zaidi ya vitabu 37 kuhusiana na Mukhtar. [96]
Baadhi ya vitabu hivyo ni:
- Sharh al-Thar fi ahwal al-Mukhtar, kimeandikwa na Ibn Nama Hilli: [97] Allama Majlisi amekitaja kitabu hiki katika juzuu ya 45 ya kitabu chake cha Bihar al-Anwar. [98]
- Rawdhat al-Mujahidin, kwa lugha ya Kifarsi: Kitabu hiki kinajumuisha ripoti za vita na miongozo ya Mukhtar ambacho kimetoka katika hali ya simulizi na kuwa katika hali ya nathari na hamasa. Kitabu hiki kimeandikwa na Waidh Harawi, (karne ya 10 Hijiria) ambapo alikuwa akisimulia watu katika mimbari katika masiku ya Muharram. Usomaji wa kitabu hiki katika vikao vya maombolezo ulienea na kuzoeleka kwa muda mrefu.
Filamu ya mfululizo ya Muktarnameh
- Makala asili: Mukhtarnameh (filamu ya mfululizo)
Mukhtarnameh ni mjumuiko wa filamu ya mfulizo kuhusiana na maisha na harakati ya Mukhtar Thaqafi. Muongozaji wa filamu hii ya mfululizo ni Mir Davood Mir Bagheri. Filamu hii ya mfululizo ina sehemu 40 na kila sehemu ina dakika 60. Sehemu ya kwanza ilionyeshwa katika Shirika la Utangazaji la Radio la Televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran 11 Oktoba 2010 na sehemu ya mwisho ilirushwa hewani 29 Julai 2011. [99] Fariborz Arabnia ameigiza nafasi ya Mukhtar katika filamu hii ya mfululizo.
Vyanzo
- Abū l-Faraj al-Iṣfahānī, ʿAlī b. al-Ḥusayn. Maqātil al-ṭālibīyyīn. Edited by Sayyid Aḥmad al-Ṣaqar. Beirut: Dār al-Maʿrifa, [n.d].
- Amīn, Sayyid Muḥsin al-. Aʿyān al-Shīʿa. Beirut: Dār al-Taʿāruf, 1406 AH.
- Basawī, Yaʿqūbī b. Sufyān. Kitāb al-maʿrifa wa al-tārīkh. Edited by Akram Ḍīyāʾ al-ʿAmrī. 2nd edition. Beirut: Muʾassisat al-Risāla, 1401 AH.
- Bīnish, ʿAbd al-Ḥusayn. Ba kārawān-i Ḥusaynī. Qom: Zamzam-i Hidāyat, 1386 AH.
- Balādhurī, Aḥmad b. Yaḥyā al-. Kitāb jumal min ansāb al-ashrāf. Edited by Suhayl Zakār & Riyāḍ al-Ziriklī. Beirut: Dār al-Fikr, 1417 AH.
- Dīnawarī, Aḥmad b. Dāwūd al-. al-Akhbār al-ṭiwāl. Edited by ʿAbd al-Munʿim ʿĀmir. Qom: Manshūrāt al-Sharīf al-Raḍī, 1368 Sh.
- Dīnawarī, Aḥmad b. Dāwūd al-. al-Akhbār al-ṭiwāl. Edited by Maḥmūd Mahdawī Dāmghānī. 4th edition. Tehran: Nashr-i Ney, 1371 Sh.
- Maḥallātī, Ḍhabīḥ Allah. Rayāḥīn al-sharī'a. [n.p]. [n.d].
- Dhahabī, Muḥammad b. al-Aḥmad al-. Siyar aʿlām al-nubalāʾ. Beirut: Muʾassisat al-Risāla, 1410 AH.
- Dhahabī, Muḥammad b. al-Aḥmad al-. Tārīkh al-Islām wa wafayāt al-mashāhīr wa l-aʿlām. Edited by ʿUmar ʿAbd al-Salām al-Tadmurī. Second edition. Beirut: Dār al-Kitāb al-ʿArabī, 1413 AH.
- Gulām Alī, Mahdī. Mujtabā Gharīb. Mukhtār Thaqafī dar gustara-yi athār-i rijālīyān. Ḥadīth-i Andīsha, No 10 and 11.
- Ibn al-Athīr al-Jazarī, ʿAlī b. Muḥammad. Usd al-ghāba fī maʿrifat al-ṣaḥāba. Beirut: Dār al-Fikr, 1409 AH.
- Ibn al-Athīr al-Jazarī, ʿAlī b. Abī l-Karam. Al-Kāmil fī l-tārīkh. Beirut: Dār Ṣādir, 1385 AH-1965.
- Ibn Aʿtham al-Kūfī, Aḥmad b. Aʿtham. Kitāb al-Futūḥ. Edited by ʿAlī Shīrī. Beirut: Dār al-Aḍwaʾ, 1411 AH-1991.
- Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. ʿIlal al-sharāʾiʿ. Qom: Intishārāt-i Dāwarī, 1385 Sh.
- Ibn al-Jawzī, ʿAbd al-Raḥmān b. ʿAlī. Al-Muntaẓam fī tārīkh al-umam wa l-mulūk. Edited by Muḥammad ʿAbd al-Qādir ʿAṭāʾ and Musṭafā ʿAbd al-Qādir ʿAṭā. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1412 AH.
- Ibn Ḥabīb, Muḥammad b. Ḥabīb b. Umayya. Kitāb al-muḥabbar. Edited by Ilza Likhtin Shititr. Beirut: Dār al-Āfāq al-Jadīda, [n.d].
- Ibn Ḥajar al-ʿAsqalānī, Aḥmad b. ʿAlī. Al-Iṣāba fī tamyīz al-ṣaḥāba. Edited by ʿĀdil Aḥmad ʿAbd al-Mawjūd and ʿAlī Muḥammad Muʿawwaḍ. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1415 AH.
- Ibn Ḥazm, ʿAlī b. Aḥmad. Jumhurat ansāb al-ʿarab. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1403 AH.
- Ibn Khaldūn, ʿAbd al-Raḥmān b. Muḥammad. Muqaddima Ibn Khaldūn. Translated by Muḥammad Parvīn Gunabadī. 8th edition. Tehran: Intishārāt-i Ilmī wa Farhangī, 1375 Sh.
- Ibn Qutayba al-Dīnawarī, ʿAbd Allah b. Muslim . Al-Maʿārif. Edited by Tharwat ʿAkkāsha. Cairo: Al-hayʾa al-Misrīyya al-'āmma li l-kitāb. 1992 CE.
- Ibn Saʿd, Muḥammad b. Manīʿ al-Hāshimī al-Baṣrī. Al-Ṭabaqāt al-kubrā. Edited by Muḥammad ʿAbd al-Qādir ʿAṭā. Beirut: Dar al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1410 AH-1990.
- Ibn Shahrāshūb, Muḥammad b. ʿAlī. Maʿālim al-ʿulamā. Mashhad: Muʾassisat Āl al-Bayt, 1390 Sh.
- Ibn Ṭaqṭaqī, Muḥammad b. ʿAlī b. Ṭabāṭabā. Al-Fakhrī fī ādāb al-sulṭānīya wa al-duwal al-islāmīya. Edited by ʿAbd al-Qādir Muḥammad Māyu. 1st edition. Beirut: Dār al-ʿIlm al-ʿArabī, 1418 AH.
- Jazāʾirī, Niʿmat Allāh b. ʿAbd Allāh. Rīyāḍ al-abrār fī manāqib al-aʾimma al-aṭhār. Beirut: Muʾassisat al-Tārīkh al-ʿArabī, 1427 AH.
- Khoei, Sayyid Abū l-Qāsim al-. Muʿjam rijāl al-ḥadīth wa tafṣīl ṭabaqāt al-ruwāt. Qom: Markaz Nashr al-Thiqāfīyya al-Islāmīyya, [n.d].
- Kashshī, Muḥammad b. ʿUmar al-. Ikhtīyār maʿrifat al-rijāl known as Rijāl al-Kashshī. Mashhad: Intishārat-i Dānishgāh-i Mashhad, 1409 AH.
- Karyutilī, Alī Ḥasan. Āʾīena-yi asr-i umawī yā Mukhtār Thaqafī. Translated by Abu l-faḍl Ṭabāṭabāʾī. Tehran: Padīda, [n.d].
- Mamaqānī, ʿAbd Allāh b. Ḥasan. Tanqīḥ al-maqāl fī ʿilm al-rijāl. Najaf: Maṭbaʿat al-Murtaḍawīyya, 1349 AH.
- Masʿūdī, ʿAlī b. al-Ḥusayn al-. Murūj al-dhahab wa maʿadin al-jawhar. Edited by Asʿad Dāghir. Qom: Dār al-Hijra, 1409 AH.
- Maqrizī, Aḥmad b. ʿAlī. Imtāʿ al-asmāʾ. Edited by Muḥammad ʿAbd al-Ḥamīd al-Namīsī. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1420 AH.
- Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Edited by Muḥammad Bāqir Maḥmūdī. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1403 AH.
- Maqdisī, Muṭahhar b. Ṭāhir. Āfarīnish wa tārīkh. Translated by Muḥammad Riḍā Shafīʿī Kadkanī. 1st edition. Tehran: Āgah, 1374 Sh.
- Samʿānī, ʿAbd al-Karīm b. Muḥammad. al-. Al-Ansāb. Edited by ʿAbd al-Raḥmān b. Yaḥyā al-Muʿallimī al-Yamānī. 1st edition. Hyderabad: Majlis Dāʾirat al-Maʿārif al-ʿUthmānīyya, 1382 AH/1962.
- Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-.Tārīkh al-umam wa l-mulūk. Edited by Muḥammad Abu l-faḍl Ibrāhīm. 2nd edition. Beirut: Dar al-Turāth, 1387 AH.
- Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Tahdhīb al-aḥkām. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
- Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥaasn al-. Al-Rijāl. Qom: Muʾassisa Nashr-i Islāmī, 1373 Sh.
- Tihrānī, Aqā Buzurg al-. Al-Dharīʿa ilā taṣānīf al-Shīʿa. Beirut: Dār al-Aḍwāʾ, 1403 AH.
- Yaʿqūbī, Aḥmad b. Abī Yaʿqūb al-. Tārīkh al-Yaʿqūbī. Beirut: Dār Ṣādir, [n.p].
- Ziriklī, Khayr al-Dīn al-. Al-Aʿlām qāmus tarājum li ashhur al-rijāl wa al-nisāʾ min al-ʿarab wa al-mustaʿribīn wa al-mustashriqīn. 8th edition. Beirut: Dār al-ʿIlm li-l-Malāyyīn, 1989.