Nenda kwa yaliyomo

Khawarij

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Makhawariji)

Khawarij (Kiarabu: الخوارج) Ni kundi la askari wa Imam Ali (a.s) waliomeguka katika vita vya Siffin ambao walimshutumu Ali bin Abi Talib kwa shutuma kumkufuru Mungu, na wakaasi dhidi yake. Kundi hili lilipewa jina la Khawarij kutokana na kumeguka kwao na kuwa dhidi ya Khalifa wa Waislamu. Kwa mtazamo wa Makhawarij; wale wote waliokubali wazo la Hakimiyaah lililo fanyika kupitia mazungumzo ya suluhu baina ya Ali bin Abi Talib na Muawiah kupitia Amru bin al-‘Aas na Abu Musa al-Ash’ari ni makafiri.

Miongoni mwa matendo mashuri yaliyo tendwa na Makharij, ni kupaza sauti dhidi ya Imam Ali (a.s) katika Msikiti wa Kufa pamoja na kutishia kumuua. Baada ya kupita suluhu baina ya Muawiah na Imamu Ali (a.s) iliyo andaliwa kwa njama za Amru bin al-‘Aas, Makhawarij walizidi kuwa wakaidi katika kumpinga Imam Ali (a.s). Hatimae Makahawarij waliachana na Imamu Ali (a.s), na kumpa kiapo cha utiifu Abdullah bin Wahab. Baada ya hapo waliondoka mjini Kufa na kwenda Nahrawan. Wakiwa njiani kuelekea Nahrawan, Makhawarij waliua watu kadhaa njiani humo. Mnamo mwaka 38 Hijiria, Imam Ali (a.s), baada ya kuwasimamishia hoja na kuwawekea wazi baina ya haki na batili, aliamua kupigana nao na wengi wao wakawa wameuawa katika vita hivyo. Hata hivyo, katika vita vyao na Imamu Ali (a.s), Makhawarij hawakumalizika bali kulikuwa na watu waliosalimika katika vita hivyo na kuendelea kubaki hai. Kihistoria Makhawarij waligawika katika madhehebu kadhaa, ila yote yalifutika isipokuwa madhehebu ya Kiibadhi, Maibadhi ni kundi pekee linalo nasibishwa na Makhawarij lenye misingi ya itikadi inayokaribiana na Waislamu wengine duniani. Madhehebu ya Kiibadhi yanapatikana katika maeneo kadhaa duniani, ikiwemo; Oman na Algeria, Zanzibar, Tunisia, Tanganyika, Kenya, Burundi na Rwanda.

Kuna sifa tofauti katika vyanzo vya Kiislamu walizopewa Makhawarij, na hata wakati mwingine sifa huonekana kuwa ukinzani baina yake, miongoni mwa sifa hizo ni; kusoma na kuhifadhi Qur'an bila kuitafakari Qur’an hiyo, ujinga na uelewa finyu, jeuri, uhasama na kuwa na dhidi ya imani za wengine. Wao wanachukuliwa kuwa ndio kundi la kwanza la upinzani na ndio madhehebu ya kwanza katika historia ya Uislamu. Kwa imani ya Makhawarij, mtu anayefanya dhambi kubwa ni kafiri. Makhawarij wengi ni wapinzani wa nadharia ya uteuzi wa Khalifa wa Kiislamu kupitia amri ya bwana Mtume (s.a.w.w), na waliamini ya kwamba; Khalifa anastahiki kuchaguliwa ya wanajamii wenyewe, pasina maoni ya Mtume Muhammad (s.a.w.w). Pia Makhawarij hawakubaliani na hukumu kumuadhibu mzinifu kwa kumpiga mawe, na pia wanapinga aina zote utendaji wa taqiya kimaneno na kivitendo.

Ingawa Makhawarij wa mwanzo hawakuonekana kuwa na hamu kubwa juu ya majadiliano ya kielimu, ila kuna mabaki kadhaa ya athari za kielimu zilizoachwa na Makhawarij wa mwanzo. Miongoni mwa mabaki hayo ni; vitabu katika fani ya elimu ya Qur'ani (ulumu al-Qur’ani), fani ya akida, fiqhi na usuli al-fiqhi pamoja na fani zinazohusiana na tauhidi (upweke wa Mwenye Ezi Mungu) na Uimamu. Kulingana na maelezo ya Ibnu Nadim, Makhawarij walificha maandiko na vitabu vyao, kutokana na upinzani watu dhidi yao. Kuna vitabu kadhaa makhususi na visivyo makhususi vilivyo andikwa katika kupinga fikra na matendo ya Makhawarij. Miongoni mwa maandiko yenye kupinga nyenendo za Makhawarij, ni Hadithi zinazo karipia nyenendo zao, miongoni mwa waandishi waliandika dhidi ya matendo ya Makhawarij, ni Ibn Abi al-Hadid ambaye maandiko yake yameonekana kupinga imani yao juu ya ukafiri wa mtenda dhambi kubwa.

Chimbuko lao na majina yao

Asili ya kundi la Khawarij inahusishwa na matukio yaliyotokea katika Vita vya Siffin wakati Imam Ali (a.s) alipopinga kwenda kinyume na maoni ya kutafuta suluhu baina ya na Muawiah yaliyo pendekezwa na Amru bin al-‘Aas. [1] Ingawa kundi hilo (la Makhawarij) ndilo lilipendekeza wazo hilo hapo mwanzoni, lakini baada ya kukubaliwa na Imam Ali (a.s) na kusitishwa kwa vita, waliacha matakwa yao na kumtaka Imam Ali (a.s) kutubu [2]. Makhawarij walilichukulia suala la kukubaliana wazo suluhu, kuwa ni kufuru na baada ya Imam Ali (a.s) kurudi mjini Kufa, wao walikwenda Haruraa karibu na mji huo wa Kufa [3].

Makhwariji, kinyume na maoni ya wanatheolojia na wanahistoria, walilichukulia suala la kumeguka kwao na kusimama dhidi ya Imam Ali (a.s), kuwa ni kukataa utawala muovu, hivyo basi walilinganisha kitendo chao hicho na hijra ya Mtume (ya kutoka Makka na kuelekea Madina) [4]. Mbali na jina maarufu la Khawarij ambalo lilitajwa katika maneno ya Imam Ali (a.s), 5] pia kuna majina mengine yanayo tumika kwa kwa ajili yao, ikiwa ni pamoja na; Muhakkimah (مُحَکِّمة) inayotokana na kauli yao mbiu isemayo "لا حکم الا لله" (hakuna hukumu yoyote ile halali sipokuwa ya Mwenye Ezi Mungu tu), kauli mbiu ambayo waliitumia  katika kupinga suluhu baina ya Imamu Ali (a.s) na Muawiah. [6] Jina jengine la Makhawarij ni Haruuriyyah (حَروریّة) jina walilopewa kulingana na sehemu walikimbilia Makhawaji ndani yake baada ya kuachana na Imamu Ali (a.s).[7] Pia wakati mwengine Makhawarij hutambulikana kwa jina la Maariqah (مارقة) kwa maana ya wapotofu. [8]

Makhawariji kwa sababu ya chuki zao dhidi ya Imamu Ali (a.s), wakati mwingine huitwa Nawasibu (نواصب)[9], Makhawarij wameita Mukaffira “مُکَفّره” kwa sababu wao ndio wa kwanza walio wapachika Waislamu watendao dhambi kubwa jina la ukafiri. [10] Jina jengine la Makhawariji ni Ahlu al-Nahri (اهل النهر) au Ahlu al-Nahrawan (اهل النهروان) ni jina lingine la Makhawarij. [11] Pia wanajulikana kwa jina la Shuratun (شُراة) kwa maana ya wale wanaouza maisha yao kwa ajili ya Pepo. [12]

Mwanzoni, Kufa na Basra zilikuwa ndio ngome kuu za Makhawarij. [13] Idadi ya Makhawarij mjini Basra, ilikuwa ni kubwa kuliko ndani ya mji wa Kufa, hii ni kwa sababu wengi wa Makhawaji waliachana na itikadi zao kupitia mazungumzo yaliofanyika baina yao na Imam Ali (a.s). [14] Baada ya hapo Makhawarij walitawanyika na kuelekea katika miji na maeneo tofauti; kuanzia Iran na Yemen hadi Afrika Kaskazini na maeneo ya Morocco. [15] Madhehebu mbalimbali ya Makhawariji yalidumaa na kutoweka katika uwanja wa historia. Madhehebu ya Kiibadhi ndio madhehebu pekee yaliobaki hadi miongoni mwa madhehebu mbali mbali ya Makhawarij. Itikadi za Kiibadhi zinawiana mno na imani za Waislamu wengine duniani, Maibadhi bado wanapatikana katika maeneo na nchi kadhaa duniani, ikiwemo; Oman, Hadramaut, Jurba, Zanzibar, Tripoli, Morocco, Congo na Algeria. [16]

Tuhuma za kufuru dhidi ya Imamu Ali (a.s)

Baada ya Imamu Ali (a.s) kukataa matakwa ya Makhawarij yaliosimama kwenye msingi majadiliano ya amani yaliofanyika baina ya Imamu Ali (a.s) na Muawiah, na baada ya wao kuasi na kutoka nje ya taa ya Ali bin Abi Talib (a.s), na baada ya kupita juhudi za Abdullahi bin Abbas na Imamu Ali (a.s) za kuwarudisha mjini Kufa, [17] kwa mara nyengine tena wakiwa mjini Kufa, Makhawarij walisimama tena dhidi ya wale walio wafikiana na maoni ya mazungumzo ya amani baina ya Imamu Ali (a.s) na Muawiah, na wakamhisabu Imamu Ali (a.s) kuwa ni kafiri. [18] Makhawarij hawakutosheka tu kuwakataa viongozi hao waliopambana katika vita vya Siffin (Imamu Ali na Muawiah), bali walipinga moja kwa moja suala la kuwepo kiongozi wa Kiislamu. [19] Wao walitangaza uasi wao hadharani, hasa katika msikiti wa Kufa, walitangaza kibaga unaga suala upinzani dhidi ya majadiliano yaliopita baina ya Imamu Ali (a.s) na Muawiah, walimkufurisha Imamu Ali (a.s) na kumtishia kumua na hata kunyanyua sauti zao dhidi yake pale alipokuwa akiwahutubia Waislamu msikitini humo. Walijaribu kutoa shinikizo la kumlazimisa Ali bi Abi Talib (a.s) kuanzisha vita dhidi ya Muawiah kutokana na majadiliano ya hadaa yaliotokea baina yake na Muawiah. Hata hivyo Imamu Ali (a.s), hakupambana na Makhawaji hadi pale wao waliposhika silaha ya Waislamu. [20]

Baada ya tukio la majadiliano ya amani yaliyo fanyika katika mwezi wa Shabani au Ramadhani ya mwaka wa 37 Hijiria kati ya Abu Musa Ashari na Amru bin Aas, na kumalizika kwa matokeo mabaya baada ya Abu Musa kudanganywa na Amr bin Aas, [21] Imamu Ali (a.s) aliyahukumu maamuzi ya mahakimu wawili hao (Abu Musa Ashari na Amru Aas) kuwa ni kinyume na hukumu ya Qur'ani na akajiandaa tena kwa vita dhidi ya Muawiyah. Katika barua kwa Abdullah bin Wahb al-Rasibi na Yazid bin Hisham, viongozi wawili wa Khawarij, ambao walikuwa wamekusanyika huko Nahrawan, aliwaomba waungane naye kwa ajili ya vita dhidi ya Muawiya na kuendeleza tena vita vya Siffin. Wao wakijibu barua walimtaka Imamu Ali (a.s) kukiri kuwa ni kafiri na kutubu, vinginevyo wataachana naye. Baada ya kutangazwa kwa uamuzi Abu Musa Ashari na Amru Aas, Khawarij walizidi kupingana na Imamu Ali (a.s) [22]

Khawarij waliapa kiapo cha utii kwa Abdullah bin Wahb kama Amir wao tarehe 10 Shawwal 37 Hijiria na walikubaliana kuondoka kutoka Kufa na kwenda Nahrawan. [23] Khawarij waliua watu wasio na hatia njiani. Imamu, baada ya kuwaita kwa haki na kukamilisha hoja, alilazimika kupigana nao. Katika Vita vya Nahrawan mwaka wa 38 Hijiria, aliwalaani wengi wao. Kundi lao lililoongozwa na Furaa bin Nufail lilijiondoa kwenye vita tangu mwanzo kwa sababu ya kusitasita kukabiliana na Imamu Ali (a.s). [24]

Licha ya ushindi wa Imamu Ali (a.s), Khawarij waliendelea kuwa kikundi cha kisiasa, kiitikadi na kijeshi. Imamu Ali (a.s) aliwakataza Waislamu kupigana na Khawarij baada yake. [25] Imamu Hassan (a.s) alikataa ombi la Muawiyah la kupigana na Khawarij baada ya makubaliano ya amani naye. [26]

Wasifu wa Makhawarj

Sifa tofauti na wakati mwingine zinazopingana katika kuzizungumzia wasifu wa Makhawarij zimeorodheshwa katika vitabu vya kihistoria na vile vile katika maandishi yanayo husiana na vikundi na madhehebu ya Kiislamu. Sifa hizi, ambazo kwa ujumla zimelaaniwa, zimeonyesha ni vipi Makhawarij walivyokuwa na welewa usio sahihi juu ya ufahamu wa Qur'an Tukufu, wajinga na wenye mtazamo finyu, wenye kiburi na majivuno, na pia ni wenye uhasama na wenye chuki. Orodha ya sifa hizi, ambazo zimeorodheshwa katika kazi tofauti za Kiislamu, ikiwa ni pamoja na Nahjul Balagha, ni kama ifuatavyo:

  • Ibada nyingi bila imani. [27]
  • Mwelekeo wa kiunyonge na kujifanya kuwa na unyenyekevu. [28]
  • Kutokujua Sunna za Mtume na sheria za kidini. [29]
  • Uelewa usio sahihi wa Qur'an Tukufu na kulinganisha Aya za Qur’ani isivyo sahihi, kwa ajili ya manufaa yao, pamoja na kuhadaika kirahisi na kuwa mtazamo wa kijuu juu. [30]
  • Kujivuna na kujiona bora na kuwaona Waislamu wote wasiokuwa wao kuwa ni makafiri na waliopotea. [31]
  • Kuwa na hamu ya kugombana na kubishana huku wakiwa na hoja dhaifu katika mijadala yao. [32]
  • Uchokozi, ukorofi, ubaguzi na msimamo mkali katika nadharia za imani ya dini. [33]
  • Kuwa na Maneno mazuri yanayo sindikizwa na tabia mbaya na ukatili. [34]
  • Kuto tumia hekima na mantiki katika kazi zao, hasa katika kuamrisha mema na kukataza mabaya. [35]
  • Kuyahisabu masuala ya Kudai haki, kuamrisha mema na kukataza mabaya na jihadi dhidi ya watawala waovu kama ni malengo ya juu ya kijamii, [36] kiasi kwamba kuto amrisha mema na kukaza na kuto pigana jihadi huhisabiwa kuwa ni ukafiri mbele ya itikadi ya Makhawarij. [37]
  • Kuhalalisha vita dhidi ya Waislamu na kuwachukua mateka au kuwaua watoto na wanawake wao, huku wakiamiliana vyema na Ahlul-Kitab pamoja na makafiri. [38]
  • Kuto kubaliana na nidhamu moja nakuendelea na migawanyiko ya mara kwa mara. [39]
  • Uadui na Imam Ali (a.s) na chuki dhidi yake hata baada ya kuuawa kwake. [40]
  • Ujasiri wa kivita na uvumilivu wa shida na kushikamana na nidhamu ya kijeshi, [41] jambo ambalo lilikuwa ndio sababu hasa ya wao kuwashida Bani Umayyah katika vita vilivyo pita baina yao, walikuwa na moyo huo hata pale walipokuwa na idadi ndogo ya askari. Hata hivyo, pia kuna taarifa zinazoelezea kukimbia kwao kutoka kwenye uwanja wa vita. [42]
  • Wakati mwingine Makhawarij walikuwa wakiwakata miguu farasi wao, na kuzivuta panga zao kwa ujasiri na kuwaandama maadui zao wote kwa pamoja na wakayakimbilia mauti kwa hamu ya kuelekea Peponi. [43] Sababu hii ndiyo iliyo pelekea mashambulizi ya kuwa ni kitu kipigiwacho mfano ndani ya jamii, ikisemwa kwamba; shambulio fulani ni kama shambulio la Kikhawarij. Walinyoa vichwa vyao kama ni ishara ya utumwa na utayari wa kifo na kujitolea kwao. Kwa hiyo, Waislamu wengine hawakuwa wakikata nywele zao, ili kuonesha upinzani wao dhidi ya Makhawarij. [44] Wakati mwingine pia walinyoa katikati ya vichwa vyao tu na wakaacha nywele nyengine za pembeni mwake. [45]
  • Ujinga, ukichwa mchungwa (ugumu wa kufahamu), kiburi, welewa finyu na utofauti wa maoni juu ya itikadi, ni miongoni mwa sifa za Makhawarij. [46]

Nafasi ya Makhawarij katika historia ya Uislamu

Khawarij wanachukuliwa kuwa na athari muhimu katika historia ya Uislamu, ikiwa ni pamoja na: Mmeguko wao na kuleta mgawanyiko katika jeshi la Imam Ali (a.s), [47] ambao ulisababisha kuanzishwa kwa kikundi cha kwanza cha upinzani na kidini katika historia ya Uislamu. [48] Khawarij mwanzoni walikuwa na mwelekeo wa kisiasa, lakini katika kipindi cha utawala wa Abdulmalik bin Marwan, waliyachanganya mafundisho yao pamoja na masuala mbali mbali ya kitheolojia. [49]

Kwa mujibu wa maoni ya wanahistoria kama vile Tabari na Ibn A'atham, mapambano baina ya Makhawarij na Imam Ali (a.s) na hatimae kumuua, yalimtengenezea fursa Muawiah ya kupora madaraka. [50] Hata hivyo, Makhawarij walijiunga na jeshi la Imam Hassan (a.s) [51] ili kupigana na Muawiya, na baada ya suluhu ya amani baina ya Muawiah na Imam Hassan (a.s), waliendelea kupigana dhidi ya Muawiya na Bani Umayyah. [52] Wao waliwahisabu Bani Umayyah na wafuasi wao kuwa makafiri na waliamini kwamba ili kuondoa dhuluma, ni lazima kupigana na makafiri. [53]

Makhawarij walishirikiana na uasi muhimu ulioibuka dhidi ya Bani Umayyah, na kwa sababu hiyo, waliwasaidia Abdullah bin Zubeir, Zayd bin Ali na Abu Muslim Khorasani katika mapambano yao. [54] Hata hivyo, katika baadhi ya matukio, walipatana na Makhalifa wa Bani Umayyah na wakachukua madaraka ya uendeshaji wa baadhi ya maeneo yaliyo kuwa chini ya utawala wa Bani Umayyah. [55] Wakati mwingine pia walichukua madaraka kwa kujitegemea katika miji fulani, ambapo viongozi wa waliitwa kwa majina kama vile Imam, Amirul Mu'minin na Khalifa. [56] Bani Umayyah, hasa nchini Iraq na Iran, walijitahidi sana kuwakandamiza Makhawarij. [57] Vita hivi vimeonekana kuwa ndio sababu muhimu zilizopelekea udhaifu na kuanguka kwa utawala wa Bani Umayyah. [58]

Maoni na Imani za Makhawarij

Moja ya imani muhimu zaidi ya Makhawarij; ni imani kwamba mtu anayefanya dhambi kubwa ni kafiri. Imani hii imeonekana kuwa na athari katika kuibuka na kupatikana mageuzi juu ya elimu ya akida. [59] Baadhi ya maoni na imani ya Makhawarij ni kama ifuatavyo:

  • Kuingia katika kufuru kwa mtendaji wa dhambi kubwa: Wazo la kwanza ambalo Makhawarij walikubaliana juu yake ni kumkufurisha mtu anayefanya dhambi kubwa. [60] Madhehebu ya Makhariji wanaoitwa Azaarqah yamekwenda mbali zaidi katika dhana hii, wao wanaamini kuwa mtenda dhambi kubwa hawezi kukubalika tena katika Usilimu, na ni lazima auawe yeye pamoja na watoto wake kutokana na kuritadi kwake, naye atadumu motoni milele bila ya kupata msamaha (shufaa).[61] Marejeo ya Makhawarij hao juu ya dhana hii, ni Aya ya 44 ya Surat Ma'idah. [62]
  • Ukhalifa: Maoni ya Khawarij kuhusu ukhalifa yalitokana na maoni yao kuhusu dhambi kubwa. Kwa msingi huo, mtu anayefanya dhambi kubwa hapaswi kuwa kiongozi wa jamii ya Waislamu na ikiwa yuko madarakani, ni wajibu wa Waislamu kumuasi na kusimama dhidi yake. [63] Wengi wa Makahawarij hawakubalianai ya imani ya kwamba; Khalifa wa Waislamu hupaswa kuteuliwa na Mtume wa Mwenye Ezi Mungu, na wanaamini ya kwamba, mtu yeyote yule anaweza kuwa Khalifa, ili mradi tu awe anatenda kulingana na kitabu cha Mwenye Ezi Mungu na Sunna za bwana Mtume (s.a.w.w). Makhawarij pia wanawafikiana na utezi wa Abu Bakar na Omar kama ni Makhalifa wa Waislamu. [64] Wao wanaamini kwamba; Uteuzi wa Imamu (Khalifa) uko kwenye mikono ya wanajamii wenyewe, [65] maoni ya ni kinyume na maoni ya wanajamii wa zama hizo, ya kwamba asiye kuwa Mquraishi hastahiki kushika nafasi ya Ukhalifa, bali kwa maoni yao wao; mtu yeyote yule anaweza kuwa Khalifa bila ya kujali nasaba yake. [66]
  • Makhalifa waongofu (Khulafa-u al-Rashiduna): Kwa kuzingatia matukio yaliyotokea wakati wa utawala wa Makhalifa Wanne, Makhawarij waliwakubali Omar na Abu Bakar kama Maimamu na Khalifa wa Mtume wa Mungu (s.a.w.w), lakini kuhusu Othman, walikubaliana naye katika kipindi cha miaka sita ya kwanza tu ya utawala wake, na kuhusu Imam Ali, walikubaliana naye hadi kabla ya kukubali mazungumzo yao yaliopita baina ya Abu Musa Ashari na Amru Aas katika kutafuta suluhu ya vita baina ya Ali (a.s) na Muawiah, na baada hapo walimtangaza kuwa ni kafiri na kuamini kwamba automatiki tayari yeye amesha uzulika kutoka madarakani. [67]
  • Maoni ya Kifiqhi: Baadhi ya maoni ya kifiqhi yaliyotolewa na baadhi ya madhehebu ya Makhawarij ni: kukataa kupigwa mawe kwa mwanamke mzinifu kwa kutegemea kwamba, hukumu hiyo haijatajwa katika Qur'ani Tukufu, kuruhusiwa kuua watoto na wake wa wapinzani wao, kuamini kwamba watoto wa washirikina pia watakuwa motoni, na kukataa taqiya katika maneno pamoja na vitendo. [68] Kwa maoni ya kundi la Makhawarij wa Madhehemu ya Azariqah ni kwamba; Ni lazima kuwauwa Waislamu wasio kuwa itikadi za Makhawarij, ila ni haramu kuwaua Wamajusi, Wakiristo na Mayahudi. [69]

Kazi andishi za Makhawarij

Makhawarij walianza kuandika vitabu vya kidini, vya kifiqhi, na vya kihistoria polepole katika nusu ya pili ya karne ya pili. Hatimae miongoni mwao mliibuka wanazuoni wa fani mbali mbali, wakiwemo waandishi pamoja na mafaqihi. [70] Makhawarij hawakuwa ni wenye kunukuu Hadithi, na waliamini kwamba Qur’ani ndiyo chanzo pekee cha sheria. [72]

Ibn Nadim Katika kitabu chake al-Fahrast, anaamini ya kwamba; Makhawariji walikuwa wakificha kazi zao andishi, kutokana na khofu ya wapinzani wao pamoja na shinikizo la watu dhidi yao. [73] Hata hivyo, Ibn Nadim alitaja wanavyuoni kadhaa wa Kikhariji walio andika kuhusiana na ulumu al-Qurani, theolojia, pamoja fiqhi na usulu al-fiqhi. [74] Pia kumenukuliwa vitabu kadhaa kutoka kwa Makhawarij kuhusiana na; Uimamu, Tawhidi pamoja na vitabu vinavyo kanusha madani ya wapinzani wao dhidi yao, vitabu ambavyo vilijibu madai wa wapinzani kadhaa wa Makhawarij, wakiwemo Mu'tazila, Murji'a, Shi'a, na Ghulati. [75]

Makhawarij pia walikuwa na wahubiri na washairi wengi ambao baadhi yao walikuwa ni mashuhuri katika jamii ya Waislamu. [76] Mengi ya mashairi ya Makhawarij yanajulikana kuwa na sifa ya mashairi ya hamasa, ambayo yalitungwa katika nyakati za vita. [77] Pia kuna baadhi ya khutba na barua zilizo nukuliwa kutoka kwa Makhawarij, ambazo zimenasibishwa kwa viongozi wao 18, zinazo sisitiza wito na silka za kidini na kisiasa za Makhawarij, pamoja na kuhimizwa kufanya Jihad na kuaamrisha mema. [78]

Sababu za Kuibuka kwa Makhawarij

Vyanzo vya Kiislamu vinaamini kwamba kuna mambo mbalimbali yalio changia katika kuibuka kwa Makhawarij, ikiwa ni pamoja na roho ya maisha waliokuwa nayo Waarabu wa zama hizo. Baadhi ya waandishi wanaamini kwamba viongozi wakuu wa Makhawarij walikuwa ni miongoni Mabedui na Waarabu wa zama za ujahilia kabla ya Uislamu ambao waliasi dhidi ya viongozi wa makabila yao, mila na maadili ya kikabila katika jamii zao. Waarabu ambao walikuwa wakipigana kwa kisingizo kisichokuwa na thamani, ambopo walikuwa wakifukuzwa kutoka katika makabila yao kutokana na tabia zao. [79] Wengi miongoni mwa watu mashuhuri ndani ya Makhawarij, walikuwa ni wa aina hiyo, amabo hawakuwa na mafungamano na kabila lolote lile mashuhuri la Waarabu. [80] Kwa msingi huo basi, hapakuwepo hata mmoja miongoni mwa Wahajirina na Maansari walio jiunga na Makhawarij. [81]

Wengine wanaamini kwamba kuanzishwa kwa Makhawarij kulitokana na uasi dhidi ya Othman. [82] Wao wanaamini kwamba; kuuliwa Othman na khitilafu za Masahaba juu ya suala la Ukhalifa, lilipepelekea kuzaliwa fikra ya kwamba; Iwapo Khalifa atakwenda kinyume na mawazo ya jamii pamoja na misingi ya dini, na akawa na uongozi mbovu kiasi ya kwamba akawa hana insafu wala hazingatii haki katika uongozi wake, basi iwapo hali itafikia hivyo, Waislamu watakuwa na haki ya kumuuzuli Khalifa huyo. [83] Baadhi ya vyanzo vya Kiislamu kama vile Taarikhu al-Tabari, vimeeleza wazi ya kwamba; Kulikuwa kiasi cha viongozi 30 walio ongoza uasi dhidi ya Othman, ambao baadae walikuja kuwa ni ndio watu mashuhuri walio kamata hatamu miongoni mwa Makhawarij. [84]

Sababu nyingine zilizotajwa katika kuibuka kwa Makhawarij, ni pamoja na kutoridhika na tabia ya Imamu Ali (a.s) katika kugawanya ngawira kwa usawa na kutokea kwa vita vya wenyewe vya Jamal na Siffin. Vita hivi vilikuwa ndio vita vya kwanza katika historia ya Uislamu ambapo Waislamu walipigana wenyewe kwa wenyewe. [85] Mwanafalsafa wa Kiislamu Murtadha Mutahhari (aliye fariki mwaka 1358 Shamsia) anaamini kwamba; kule Makhawarij kuto tumia mantiki katika mambo yao, hasa katika suala la kuamrisha mema na kukataza mabaya, ndiyo sababu kuu ya kutoweka kwao. [86]

Ukosoaji wa itikadi za Makahawarij

Tangu kuanzishwa kwa Khawarij katika historia ya Uislamu, Waislamu waliandika vitabu tofauti wakijibu hoja za kiitikadi za Makhawarij. Pia ndani ya Hadithi kuna kauli kadhaa zilizo kosoa imani na matendo ya Makhawarij. Miongoni mwa Hadithi hizo ni ile Hadithi ya bwana Mtume (s.a.w.w), iliyo bashiri kuzuka kwa Makhawarij na kutoka katika misingi ya dini, ambapo Hadithi hiyo imelaani na kupinga nyenendo zao, pia ndani yake mmesisitizwa suala la kupigana nao na kutolewa bishara ya thawabu katika kuwaua Makhawarij. [87] Wanazuoni wa Kishia wakitegemea moja ya Hadithi kutoka kwa Mtume (s.a.w.w), wamewahisabu wale wote walipigana na Ali (a.s), wakiwemo pia Makhawarij, kuwa ni Makafiri. Kulinga na Hadithi hiyo, yeyote yule atakaye pambana na Ali (a.s), atakuwa sawa na yule aliye pambana na bwana Mtume (s.a.w.w). [88]

Kuna vitabu kadhaa miongoni mwa vitabu vya tafsiri, vilivyo kosoa marejeo ya Makhariji kwenye Qur'ani Tukufu ili kuthibitisha imani zao, ikiwa ni pamoja na madai yao ya kuwakufurisha Waislamu watendao dhambi kubwa na kuwaita makafiri. Kwa kuzingatia Aya ya 97 ya Surat al-Imran, Makhariji wanaamini kwamba; yeyote asiye fanya ibada ya hija, atakuwa amefanya dhambi kubwa, na moja kwa moja atakuwa amekufuru, kwa sababu kutenda madhambi makubwa hupelekea mtu kuingia kwenye ukafiri. Kwa kujibu hoja hii, katika kujibu madai haya, wanazuoni wamesemwa kwamba; kufuru ina maana pana katika maandiko ya kidini, ambapo inajumuisha aina yoyote ila ya upinzani dhidi ya haki, iwe katika ngazi ya imani au katika ngazi ya chini ya amri za kisheria. Kwa hiyo, katika Aya ya 97 ya Surat al-Imran, ukafiri una maana ya mtu kuacha hija hali akiwa na uwezo wa kutenda ibada hiyo (uwezo wa kisheria), sio kwa maana ya mtu kutoka katika Uislamu kama walivyofikiria Makhawarij [89] Ibn Hazm amepina madai ya Makhawarij katika suala hili kwa kutaja Aya nyingine za Qur'ani Tukufu katika kufafanua suala hilo. [90]

Masuala yanayo fungamana

Rejea

Vyanzo