Mkopo:Dua ya arubaini na nane kutoka katika kitabu cha Sahifa Sajjadiya
Nakala ya Sahifa al-Sajjadiyah, katika hati ya Naskh ya Abdullah Yazdi, iliyoandikwa mnamo Sha'ban 1102 AH. | |
| Mada | Dua iliyokuwa ikisomwa na Imamu Sajjad (a.s) wakati wa maadhimisho ya Idi al-Adha na siku za Ijumaa. |
|---|---|
| Ina Mapokezi au Haina Mapokezi | Ina Mapokezi |
| Imenukuliwa Kutoka kwa | Imamu Sajjad (a.s) |
| Mpokezi | Mutawakkil ibn Harun |
| Vyanzo vya Kishia | Sahifa Sajjadiyah |
| Dua ya Tawassuli • Dua ya Kumaili • Dua ya Nudba • Dua ya Samati • Dua ya Faraji • Dua ya Abu Hamza Thumali • Ziara ya Ashura • Ziara ya Jamiat Kabira • Ziara ya Warith • Ziara ya Aminu-Llah • Ziara ya Arobaini | |
Dua ya Arubaini na Nane ya Sahifa Sajjadiya (Kiarabu: الدعاء الثامن والأربعون من الصحيفة السجادية) ni miongoni mwa dua zilizopokewa kutoka kwa Imamu Sajjad (a.s), aliyekuwa akiisoma dua hiyo katika siku ya Idi al-Adha (Idi ya kuadhimisha ibada ya Hija) pamoja na siku ya Ijumaa. Katika dua hii, Imamu Sajjad (a.s.) anaichukulia (anaihisabu) mikusanyiko ya Waislamu katika siku za Idi, kama ni dhihirisho (akisiko) la ukuu wa Uislamu (taadhima ya Uislamu), na anamuomba Mwenye Ezi Mungu kumpa rehema na msamaha ndani yake. Ndani ya dua hii, kuna marejeo mengi ya kumswalia Mtume wa Muhammad (s.a.w.w) pamoja na Aali zake (a.s).
Kadhalika, katika dua hii, mamlaka ya kiuongozi ya umma wa Kiislamu yanatambulika kuwa ni milki au haki ya kipekee ya Maimamu Maasumu (a.s), mamlaka ambayo yameporwa na watawala wa kidhalimu. Imamu wa Nne (Imamu Sajjad) (a.s), kupitia dua hii, anaiomba mambo kadhaa kutoka kwa Mwenye Ezi Mungu, ikiwa ni pamoja na kupatikana ukombozi wa, kinga dhidi ya balaa, kupata wasaa wa rizki (upanuzi wa riziki), na kughufuriwa kwa madhambi mbali mbali.
Dua ya arubaini na nane, ilioko katika ndani ya kitabu cha Sahifa Sajjadiyya, imefasiriwa na kushereheshwa kwa lugha mbali mbali, sambamba na dua nyengine za kitabu cha Sahifa Sajjadiyya. Miongoni mwa vitabu vya Kifarsi vyenye tafsiri chambuzi ya dua za Sahifa Sajjadiya ikiwemo dua ya arubaini na nane, ni pamoja na; Diare Asheghan, kilichoandikwa na mwanazuoni Hussein Ansarian, na Shuhud wa Shenakht, ilichoandikwa na Hassan Mamdouhi Kermanshahi. Aidha, tafsiri na ufafanuzi wa kina wa dua hii sambamba na dua nyengine za kitabu hichi, iliyoandikwa kwa lugha ya Kiarabu unapatikana katika kitabu kiitwacho Riyad al-Salikin, kilichoandikwa na Sayyid Ali Khan Madani.
Mafundisho Yaliomo Ndani ya Dua ya Arubaini na Nane
Dua ya arubaini na nane ni moja ya sehemu za mkusanyiko wa dua zinazopatikana katika kitabu cha Sahifa Sajjadiyya, iliyokuwa ikisomwa na Imamu Sajjad (a.s) wakati wa maadhimisho ya Idi al-Adha na siku za Ijumaa. Maudhui kuu zilizomo katika dua hii zinajumuisha uchambuzi wa sifa bainifu za siku ya Idi al-Adha pamo na siku ya Ijumaa, pamoja na kuteremka kwa rehma mahususi za Mwenye Ezi Mungu ndani ya nyakati mbili hizi adhimu. Aidha, Imamu Zainu al-Abidin (a.s) anatumia dua hii kuelezea masikitiko yake juu ya suala la utawala wa kisiasa kuwa chini ya mamlaka ya watu wasio na sifa stahiki, akisisitiza kuwa kigezo na sifa msingi ya kiongozi wa jamii ya Kiislamu ni kuwa maasumu (aliyekingiwa dhidi ya makosa).[1] Ndani ya dua hii kuna ibara nyingi zilizotumika kwa ajili ya kumtakia rehema Mtume Muhammad (s.a.w.w) pamoja na Aali zake. Kuwepo kwa wingi wa ibara hizo ndani ya dua hii, kunatafsiriwa kama ni njia maalumu iliyotuka kwa ajili ya kuienzi nafasi Yake pamoja na Aali zake, pamoja na kuwashukuru watukufu hao kutokana na juhudi zao zilizopelekea kupatikana kwa mafanikio ya milele ya mwanadamu yalioegemea kwenye mgongo wa mwongozo wao.[2]
mafunzo ya dua ya arubaini na nane yameorodheshwa kama ifuatavyo:
- Baraka za siku ya Ijumaa na Idi al-Adha: Siku mbili hizi ni siku tukufu mno na ibada zake ni zenye malipo makubwa ndani ya Uislamu.
- Utawala na sifa stahiki ni za Mwenye Ezi Mungu peke yake: Mwenye Ezi Mungu ndiye mtawala mkuu anayestahiki sifa zote kamilifu, dhana inayojulikana kwa jina la Tawhidi.
- Mikusanyiko ya Waislamu ya siku za sikukuu huonyesha ukuu wa Uislamu: Mikutano kama Sala ya Idi huonyesha umoja, nguvu na utukufu (taadhima) ya umma wa Kiislamu.
- Dua ya kumuomba kheri mbali mbali za Mwenye Ezi Mungu kama alivyowapa wengine: Ni dua inayoonesha unyenyekevu na hamu ya kupata baraka mbali mbali kutoka kwa Mwenye Ezi Mungu.
- Umuhimu wa kutumia Majina na Sifa za Mwenye Ezi Mungu ipasavyo: Inapendekezwa kutumia Majina Mazuri ya Mungu (Asmaul Husna) katika dua ili kumuomba msaada kulingana na sifa zake.
- Kumjua Mwenye Ezi Mungu kunakopelekea kutumia vyema neema zaidi kwa: Kumjua Mungu (welewa wa kumjua Mungu) huongeza shukrani na husaidia kutumia neema Zake kwa njia sahihi.
- Pepo na vyeo vipo chini ya rehema za Mungu: Kuingia Peponi kunategemea fadhila na huruma ya Mwenye Ezi Mungu, na si kwa kutegemea matendo mema pekee.
- Kuomba Mtume Muhammad na Aali zake rehema zisizo na kikomo: Kumsalia bwana Mtume pamoja na Aali zake watoharifu (Ahlul Bait) ni moja ya ibada muhimu na yenye thawabu adhimu.
- Kutopendeza kuomba msaada kwa asiyekuwa Mwenye Ezi Mungu: Dhana hii inasisitiza ya kwamba; msaada wa kweli unapaswa kuombwa kutoka kwa Mwenye Ezi Mungu peke yake.
- Kutumainia rehema za Mungu kuliko matendo yako: Ni muhimu kuwa na matumaini makubwa katika msamaha wa Mungu kuliko kujivunia matendo binafsi.
- Rehema za Mwenye Ezi Mungu ni pana kuliko dhambi za waja: Hii ni dhana intoayo faraja, kwamba msamaha wa Mwenye Ezi Mungu ni mkubwa zaidi ya dhambi za yeyote yule anayetubu.
- Matumaini ya kupata ujira siku ya Idi al-Adha na Ijumaa: Siku mbili hizi ni siku zenye fadhila maalum, na matendo mema ndani yake yanaaminika kuwa na thawabu kubwa zaidi kuliko siku nyengine.
- Kheri na shari zote ziko chini ya uwezo wa Mwenye Ezi Mungu: Hakuna jambo linalotokea, liwe jema au baya, isipokuwa latokea kwa idhini na uwezo wa Mwenye Ezi Mungu.
- Kutarajia kheri za dunia na Akhera kutoka kwa Mwenye Ezi Mungu: Kumuomba Mwenye Ezi Mungu mafanikio na baraka katika maisha ya sasa na yajayo.
- Kiburi na kuachana na matendo mema huzuia dua kujibiwa: Majivuno na kuacha ibada ni miongoni mwa vizuizi vinavyoweza kuzuia maombi kukubaliwa.
- Mwenye Ezi Mungu hamhitaji mwanadamu, bali mwanadamu ndiye mhitaji wa Mola wake: Mungu ni Mkwasi (Al-Ghaniyy), na viumbe vyote vinamtegemea Yeye juu ya kila kitu.
- Kuomba maghufiri ni moja ya nyenzo za kumjua Mwenye Ezi Mungu: Kuomba msamaha (Istighfar) mara kwa mara husafisha moyo na kumkurubisha mja kwa Mola wake.
- Umuhimu wa kujiandaa kwa ajili ya Akhera: Maisha ya duniani ni fursa ya maandalizi kwa ajili ya maisha ya milele baada ya kifo.
- Matumaini ya uombezi (Shufaa) wa bwana Mtume na Ahlul Bait (a.s): Njia ya kukaribiana na bwana Mtume (s.a.w.w), ni kuamini kwamba; bwana Mtume na Aali zake ni wenye nafasi ya kumuombea shufaa muumini Siku ya Kiyama.
- Kufuata mwenendo wa Ahlul Bait (a.s) ili kupata uombezi wao: Ili kustahili uombezi wao, ni lazima kufuata mafundisho na mfano wao mwema.
- Kukiri na kuungama dhambi mbele ya Mwenye Ezi Mungu: Toba ya kweli inahitaji mja kukiri makosa yake kwa unyenyekevu mbele ya Mungu.
- Kukiri upana wa rehema na msamaha wa Mwenye Ezi Mungu: Moja ya nguzo muhimu za imani ni kutambua na kukubali kuwa, Mwenye Ezi Mungu ni Mwingi wa Rehema na Msamaha.
- Sala za Eid na Ijumaa ni kwa ajili ya viongozi wateule: Kwa mujibu wa iamni ya madhehebu ya Shia Ithna Asharia, uongozi wa sala hizi muhimu ni jukumu la Maimamu walioteuliwa na Mwenye Ezi Mungu.
- Laana juu ya maadui wa Ahlul Bait (a.s): Hii ni dua maalumu ya kuwaombea laana wale waliowadhulumu na kuwapinga viongozi pamoja na watu watokanao na familia ya bwana Mtume (s.a.w.w).
- Kuporwa kwa nafasi ya Maimamu ya kuongoza sala za Idi na Ijumaa: Huu ni mtazamo wa kihistoria usemao kwamba; viongozi halali walinyang'anywa mamlaka haya ya kidini.
- Dini kugeuzwa mchezo na watawala dhalimu: Ni ukosoaji kwa viongozi wanaotumia dini kwa manufaa yao ya kisiasa badala ya haki.
- Kuridhia dhuluma ni kushiriki katika dhuluma: Uislamu unafundisha kwamba kukubaliana na uovu na kuunyamazia ni sawa na kuutenda.
- Dua ya kuharakishwa kwa faraja ya umma kupitia kizazi cha bwana Mtume (s.a.w.w): Hii ni dua maalum (hasa katika madhehebu ya Shia) ya kuomba ujio wa haraka wa Imamu Mahdi (a.f).
- Dua ya kuwa miongoni mwa watu wa Tawhidi na Imani: Ni ombi la kudumishwa katika imani sahihi ya Mungu mmoja na kuwa miongoni mwa waumini wa kweli.
- Kuokolewa na adhabu ya Mungu kupitia unyenyekea: Kunyenyekea na kuomba kwa dhati (Tadharru) ndiyo njia ya kujiepusha na ghadhabu za Mwenye Ezi Mungu.
- Huzuni ya kuwa mbali na rehema za Mwenye Ezi Mungu: Kuhisi majuto na huzuni kwa kuwa mbali na Mwenye Ezi Mungu, ni hatua muhimu katika safari ya toba.
- Maombi ya kuomba kujibiwa kwa dua kabla ya kifo: Ni matumaini ya kila muumini kwamba maombi yake yatakubaliwa na Mola wake, huku akiwa bado yuhai.
- Kuomba afya njema hadi mwisho wa maisha: Afya ni neema muhimu inayomwezesha mja kutekeleza ibada na majukumu yake.
- Mungu haharakishi kuaadhibu waja wake: Mwenye Ezi Mungu ni Mpole (Al-Halim), na huwapa waja wake fursa ya kutubu badala ya kuwaadhibu papo hapo.
- Mungu ni mtakatifu na si mwenye kudhulumu: Mwenye Ezi Mungu ni Mwadilifu kabisa, na kamwe hana haja ya kumdhulumu kiumbe wake.
- Dua ya kulindwa dhidi ya majanga: Ni maombi ya kuomba hifadhi ya Mwenye Ezi Mungu dhidi ya mitihani, mabalaa na changamoto mbali mbali.
- Kuomba msaada wa Mungu katika kutatua shida na kuondoa huzuni: Dua hii inafungamana na imani ya kuamini kuwa; Mwenye Ezi Mungu pekee ndiye mwenye uwezo wa kuleta faraja na ufumbuzi.
- Kuokolewa na maumivu ya kifo (Sakaratul Maut) kupitia ukamilifu wa kiroho: Inaaminika kuwa kufikia daraja ya juu ya kiroho kunaweza kupunguza maumivu yanayojiri wakati wa kufa.
- Kuitumia siku za Ijumaa pamoja na Idi, katika kutafuta hifadhi ya Mungu dhidi ya ghadhabu zake: Kutumia siku hizi takatifu kama fursa maalum ya kuomba ulinzi dhidi ya hasira za Mwenye Ezi Mungu.
- Mungu ndiye tegemeo kuu: Hii ni dhana ya Tawakkul, yaani, kumtegemea Mwenye Ezi Mungu kikamilifu katika kila jambo.
- Kuondokana na matatizo kupitia nyenzo ya kunyenyekea ya Mungu: Unyenyekevu na utii kwa Mwenye Ezi Mungu, ndio ufunguo wa kupata msaada na faraja Yake.
- Dua ya kuomba usalama dhidi ya adhabu ya Mungu: Ni ombi la kuepushwa na adhabu ya Mwenye Ezi Mungu duniani na kesho Akhera.
- Dua ya kuomba uongofu wa Mungu: Kuomba mwongozo (Hidaya) ni jambo la msingi, kwani bila mwongozo huo mwanadamu hupotea.
- Dua ya kupata nusura (msaada) kutoka kwa Mungu: Kuomba ushindi na msaada kutoka kwa Mwenye Ezi Mungu dhidi ya changamoto na maadui mbali mbali.
- Kuomba rehema, msamaha na riziki ya kutosha: Ni dua inayojumuisha mahitaji makuu ya kiroho na kimwili ya mwanadamu.
- Kuomba msamaha dhidi ya dhambi (Istighfaru): Ni tendo muhimu la kuomba msamaha kwa makosa yote, yawe madogo au makubwa.
- Dua ya kuomba ulinzi dhidi ya shari na maafa mbali mbali: Ni maombi ya kuomba hifadhi ya Mungu dhidi ya uovu wa viumbe pamoja na majanga.
- Kuomba mafanikio mema kupitia fadhila za Mwenye Ezi Mungu: Ni dua ya kuomba baraka na mafanikio katika kila jambo jema analolifanya mwanadamu.
- Kuomba kheri katika majaaliwa (Qadar): Ni dua ya kumuomba Mwenye Ezi Mungu amjalie mja Wake kheri na baraka katika yale aliyomkadiria na kumuamulia.
- Kuwa na dhana ya kumtegemea Mwenye Ezi Mungu ni bora zaidi kuliko kuwa na dhana ya kujitegemea mwenyewe: Hii inasisitiza umuhimu wa Tawakkul (kumtegemea Mwenye Ezi Mungu) badala ya kutegemea nguvu na akili za kibinadamu pekee.[3]
Tafsiri Chambuzi za Dua ya Arubaini na Nane
Ufafanuzi wa Dua ya Arubaini na Nane ya Sahifa Sajjadiyya umewasilishwa kwa lugha mbali mbali, ikiwemo lugha ya Kiajemi pamoja na lugha ya Kiarabu. Miongoni mwa vitabu vilivyotoa tafsiri chambuzi za dua hii sambamba na dua nyengine za Sahisa Sajjadiyyya kwa lugha ya Kiajemi, ni pamoja na; Diare Ashiqan, kitabu kilichoandikwa na bwana Hussein Ansarian,[4] Shuhud wa Shenakht, kazi ya bwana Muhammad Hassan Mamduhi Kermanshahi,[5] pamoja na Sharh wa Tarjome-ye Sahife Sajjadiye, kilichoandikwa na Sayyid Ahmad Fahri.[6]
Kwa upande wa lugha ya Kiarabu, kuna juhudi kadhaa zilizchukuliwa kwa ajili kufikisha maana na makusudia kamili ya Dua hii kwa ajili ya wasomaji mbai mbali. Miongoni mwa tafsiri chambuzi za lugha ya Kiarabu zilizochambua dua hii sambamba na dua nyengine za Sahifa Sajjadiyya, ni pamoja na; Riadhu as-Salikin, kitabu cha bwana Sayyid Ali-Khan Madani,[7] Fi Dhilal as-Sahifa as-Sajjadiyya, cha Muhammad Jawad Maghniyah,[8] Riadhu al-Arifin, cha Muhammad ibn Muhammad Darabi,[9] na Afaqi ar-Ruh, cha Sayyid Muhammad Hussein Fadlallah.[10] Aidha, kuna kazi muhimu zilizofanywa kwa ajili ya kutoa maana ya maneno yaliyotumika katika dua hii. Miongoni mwa vitabu vilivyoshughulikia jukumu hili la kilugha ni kama vile; Ta'aliqat 'ala as-Sahifa as-Sajjadiyya, cha Faidhu Kashani[11] pamoja na Sharh as-Sahifa as-Sajjadiyya, cha Izzu Al-ddin Jaza’iri.[12]
Matini ya Dua ya Arubaini na Nane Pamoja na Maelezo Yake kwa Kiswahili
وَ كَانَ مِنْ دُعَائِهِ عَلَيْهِ السَّلَامُ يَوْمَ الْأَضْحَي وَ يَوْمَ الْجُمُعَةِ
اللَّهُمَّ هَذَا يَوْمٌ مُبَارَكٌ مَيْمُونٌ ، وَ الْمُسْلِمُونَ فِيهِ مُجْتَمِعُونَ فِي أَقْطَارِ أَرْضِكَ ، يَشْهَدُ السَّائِلُ مِنْهُمْ وَ الطَّالِبُ وَ الرَّاغِبُ وَ الرَّاهِبُ وَ أَنْتَ النَّاظِرُ فِي حَوَائِجِهِمْ ، فَأَسْأَلُكَ بِجُودِكَ وَ كَرَمِكَ وَ هَوَانِ مَا سَأَلْتُكَ عَلَيْكَ أَنْ تُصَلِّيَ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ .
وَ أَسْأَلُكَ اللَّهُمَّ رَبَّنَا بِأَنَّ لَكَ الْمُلْكَ ، وَ لَكَ الْحَمْدَ ، لَا إِلَهَ إِلَّا أَنْتَ ، الْحَلِيمُ الْكَرِيمُ الْحَنَّانُ الْمَنَّانُ ذُو الْجَلَالِ وَ الْإِكْرَامِ ، بَدِيعُ السَّمَاوَاتِ وَ الْأَرْضِ ، مَهْمَا قَسَمْتَ بَيْنَ عِبَادِكَ الْمُؤْمِنِينَ مِنْ خَيْرٍ أَوْ عَافِيَةٍ أَوْ بَرَكَةٍ أَوْ هُدًى أَوْ عَمَلٍ بِطَاعَتِكَ ، أَوْ خَيْرٍ تَمُنُّ بِهِ عَلَيْهِمْ تَهْدِيهِمْ بِهِ إِلَيْكَ ، أَوْ تَرْفَعُ لَهُمْ عِنْدَكَ دَرَجَةً ، أَوْ تُعْطِيهِمْ بِهِ خَيْراً مِنْ خَيْرِ الدُّنْيَا وَ الآْخِرَةِ أَنْ تُوَفِّرَ حَظِّي وَ نَصِيبِي مِنْهُ
وَ أَسْأَلُكَ اللَّهُمَّ بِأَنَّ لَكَ الْمُلْكَ وَ الْحَمْدَ ، لَا إِلَهَ إِلَّا أَنْتَ ، أَنْ تُصَلِّيَ عَلَى مُحَمَّدٍ عَبْدِكَ وَ رَسُولِكَ وَ حَبِيبِكَ وَ صِفْوَتِكَ وَ خِيَرَتِكَ مِنْ خَلْقِكَ ، وَ عَلَى آلِ مُحَمَّدٍ الْأَبْرَارِ الطَّاهِرِينَ الْأَخْيَارِ صَلَاةً لَا يَقْوَى عَلَى إِحْصَائِهَا إِلَّا أَنْتَ ، وَ أَنْ تُشْرِكَنَا فِي صَالِحِ مَنْ دَعَاكَ فِي هَذَا الْيَوْمِ مِنْ عِبَادِكَ الْمُؤْمِنِينَ ، يَا رَبَّ الْعَالَمِينَ ، وَ أَنْ تَغْفِرَ لَنَا وَ لَهُمْ ، إِنَّكَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ .
اللَّهُمَّ إِلَيْكَ تَعَمَّدْتُ بِحَاجَتِي ، وَ بِكَ أَنْزَلْتُ الْيَوْمَ فَقْرِي وَ فَاقَتِي وَ مَسْكَنَتِي ، وَ إِنِّي بِمَغْفِرَتِكَ وَ رَحْمَتِكَ أَوْثَقُ مِنِّي بِعَمَلِي ، وَ لَمَغْفِرَتُكَ وَ رَحْمَتُكَ أَوْسَعُ مِنْ ذُنُوبِي ، فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِ مُحَمَّدٍ ، وَ تَوَلَّ قَضَاءَ كُلِّ حَاجَةٍ هِيَ لِي بِقُدْرَتِكَ عَلَيْهَا ، وَ تَيْسِيرِ ذَلِكَ عَلَيْكَ ، وَ بِفَقْرِي إِلَيْكَ ، وَ غِنَاكَ عَنِّي ، فَإِنِّي لَمْ أُصِبْ خَيْراً قَطُّ إِلَّا مِنْكَ، وَ لَمْ يَصْرِفْ عَنِّي سُوءاً قَطُّ أَحَدٌ غَيْرُكَ ، وَ لَا أَرْجُو لِأَمْرِ آخِرَتِي وَ دُنْيَايَ سِوَاكَ .
اللَّهُمَّ من تَهَيَّأَ وَ تَعَبَّأَ وَ أَعَدَّ وَ اسْتَعَدَّ لِوَفَادَةٍ إِلَى مَخْلُوقٍ رَجَاءَ رِفْدِهِ وَ نَوَافِلِهِ وَ طَلَبَ نَيْلِهِ وَ جَائِزَتِهِ ، فَإِلَيْكَ يَا مَوْلَايَ كَانَتِ الْيَوْمَ تَهْيِئَتِي وَ تَعْبِئَتِي وَ إِعْدَادِي وَ اسْتِعْدَادِي رَجَاءَ عَفْوِكَ وَ رِفْدِكَ وَ طَلَبَ نَيْلِكَ وَ جَائِزَتِكَ.
اللَّهُمَّ فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِ مُحَمَّدٍ ، وَ لَا تُخَيِّبِ الْيَوْمَ ذَلِكَ مِنْ رَجَائِي ، يَا مَنْ لَا يُحْفِيهِ سَائِلٌ وَ لَا يَنْقُصُهُ نَائِلٌ ، فَإِنِّي لَمْ آتِكَ ثِقَةً مِنِّي بِعَمَلٍ صَالِحٍ قَدَّمْتُهُ ، وَ لَا شَفَاعَةِ مَخْلُوقٍ رَجَوْتُهُ إِلَّا شَفَاعَةَ مُحَمَّدٍ وَ أَهْلِ بَيْتِهِ عَلَيْهِ وَ عَلَيْهِمْ سَلَامُكَ.
أَتَيْتُكَ مُقِرّاً بِالْجُرْمِ وَ الْإِسَاءَةِ إِلَى نَفْسِي ، أَتَيْتُكَ أَرْجُو عَظِيمَ عَفْوِكَ الَّذِي عَفَوْتَ بِهِ عَنِ الْخَاطِئِينَ ، ثُمَّ لَمْ يَمْنَعْكَ طُولُ عُكُوفِهِمْ عَلَى عَظِيمِ الْجُرْمِ أَنْ عُدْتَ عَلَيْهِمْ بِالرَّحْمَةِ وَ الْمَغْفِرَةِ.
فَيَا مَنْ رَحْمَتُهُ وَاسِعَةٌ ، وَ عَفْوُهُ عَظِيمٌ ، يَا عَظِيمُ يَا عَظِيمُ ، يَا كَرِيمُ يَا كَرِيمُ ، صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِ مُحَمَّدٍ وَ عُدْ عَلَيَّ بِرَحْمَتِكَ وَ تَعَطَّفْ عَلَيَّ بِفَضْلِكَ وَ تَوَسَّعْ عَلَيَّ بِمَغْفِرَتِكَ .
اللَّهُمَّ إِنَّ هَذَا الْمَقَامَ لِخُلَفَائِكَ وَ أَصْفِيَائِكَ وَ مَوَاضِعَ أُمَنَائِكَ فِي الدَّرَجَةِ الرَّفِيعَةِ الَّتِي اخْتَصَصْتَهُمْ بِهَا قَدِ ابْتَزُّوهَا ، وَ أَنْتَ الْمُقَدِّرُ لِذَلِكَ ، لَا يُغَالَبُ أَمْرُكَ ، وَ لَا يُجَاوَزُ الَْمحْتُومُ مِنْ تَدْبِيرِكَ كَيْفَ شِئْتَ وَ أَنَّى شِئْتَ ، وَ لِمَا أَنْتَ أَعْلَمُ بِهِ غَيْرُ مُتَّهَمٍ عَلَى خَلْقِكَ وَ لَا لِإِرَادَتِكَ حَتَّى عَادَ صِفْوَتُكَ وَ خُلَفَاؤُكَ مَغْلُوبِينَ مَقْهُورِينَ مُبْتَزِّينَ ، يَرَوْنَ حُكْمَكَ مُبَدَّلًا ، وَ كِتَابَكَ مَنْبُوذاً ، وَ فَرَائِضَكَ مُحَرَّفَةً عَنْ جِهَاتِ أَشْرَاعِكَ ، وَ سُنَنَ نَبِيِّكَ مَتْرُوكَةً.
اللَّهُمَّ الْعَنْ أَعْدَاءَهُمْ مِنَ الْأَوَّلِينَ وَ الآْخِرِينَ ، وَ مَنْ رَضِيَ بِفِعَالِهِمْ وَ أَشْيَاعَهُمْ وَ أَتْبَاعَهُمْ .
اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِ مُحَمَّدٍ ، إِنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ ، كَصَلَوَاتِكَ وَ بَرَكَاتِكَ وَ تَحِيَّاتِكَ عَلَى أَصْفِيَائِكَ إِبْرَاهِيمَ وَ آلِ إِبْرَاهِيمَ ، وَ عَجِّلِ الْفَرَجَ وَ الرَّوْحَ وَ النُّصْرَةَ وَ الَّتمْكِينَ وَ التَّأْيِيدَ لَهُمْ .
اللَّهُمَّ وَ اجْعَلْنِي مِنْ أَهْلِ التَّوْحِيدِ وَ الْإِيمَانِ بِكَ ، وَ التَّصْدِيقِ بِرَسُولِكَ ، وَ الْأَئِمَّةِ الَّذِينَ حَتَمْتَ طَاعَتَهُمْ مِمَّنْ يَجْرِي ذَلِكَ بِهِ وَ عَلَى يَدَيْهِ ، آمِينَ رَبَّ الْعَالَمِينَ.
اللَّهُمَّ لَيْسَ يَرُدُّ غَضَبَكَ إِلَّا حِلْمُكَ ، وَ لَا يَرُدُّ سَخَطَكَ إِلَّا عَفْوُكَ ، وَ لَا يُجِيرُ مِنْ عِقَابِكَ إِلَّا رَحْمَتُكَ ، وَ لَا يُنْجِينِي مِنْكَ إِلَّا التَّضَرُّعُ إِلَيْكَ وَ بَيْنَ يَدَيْكَ ، فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِ مُحَمَّدٍ ، وَ هَبْ لَنَا يَا إِلَهِي مِنْ لَدُنْكَ فَرَجاً بِالْقُدْرَةِ الَّتِي بِهَا تُحْيِي أَمْوَاتَ الْعِبَادِ ، وَ بِهَا تَنْشُرُ مَيْتَ الْبِلَادِ .
وَ لَا تُهْلِكْنِي يَا إِلَهِي غَمّاً حَتَّى تَسْتَجِيبَ لِي ، وَ تُعَرِّفَنِي الْإِجَابَةَ فِي دُعَائِي ، وَ أَذِقْنِي طَعْمَ الْعَافِيَةِ إِلَى مُنْتَهَى أَجَلِي ، وَ لَا تُشْمِتْ بِي عَدُوِّي ، وَ لَا تُمَكِّنْهُ مِنْ عُنُقِي ، وَ لَا تُسَلِّطْهُ عَلَيَّ
إِلَهِي إِنْ رَفَعْتَنِي فَمَنْ ذَا الَّذِي يَضَعُنِي ، وَ إِنْ وَضَعْتَنِي فَمَنْ ذَا الَّذِي يَرْفَعُنِي ، وَ إِنْ أَكْرَمْتَنِي فَمَنْ ذَا الَّذِي يُهِينُنِي ، وَ إِنْ أَهَنْتَنِي فَمَنْ ذَا الَّذِي يُكْرِمُنِي ، وَ إِنْ عَذَّبْتَنِي فَمَنْ ذَا الَّذِي يَرْحَمُنِي ، وَ إِنْ أَهْلَكْتَنِي فَمَنْ ذَا الَّذِي يَعْرِضُ لَكَ فِي عَبْدِكَ ، أَوْ يَسْأَلُكَ عَنْ أَمْرِهِ ، وَ قَدْ عَلِمْتُ أَنَّهُ لَيْسَ فِي حُكْمِكَ ظُلْمٌ ، وَ لَا فِي نَقِمَتِكَ عَجَلَةٌ ، وَ إِنَّمَا يَعْجَلُ مَنْ يَخَافُ الْفَوْتَ ، وَ إِنَّمَا يَحْتَاجُ إِلَي الظُّلْمِ الضَّعِيفُ ، وَ قَدْ تَعَالَيْتَ يَا إِلَهِي عَنْ ذَلِكَ عُلُوّاً كَبِيراً .
اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِ مُحَمَّدٍ ، وَ لَا تَجْعَلْنِي لِلْبَلَاءِ غَرَضاً ، وَ لَا لِنَقِمَتِكَ نَصَباً ، وَ مَهِّلْنِي ، وَ نَفِّسْنِي ، وَ أَقِلْنِي عَثْرَتِي ، وَ لَا تَبْتَلِيَنِّي بِبَلَاءٍ عَلَى أَثَرِ بَلَاءٍ ، فَقَدْ تَرَى ضَعْفِي وَ قِلَّةَ حِيلَتِي وَ تَضَرُّعِي إِلَيْكَ .
أَعُوذُ بِكَ اللَّهُمَّ الْيَوْمَ مِنْ غَضَبِكَ ، فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ أَعِذْنِي.
وَ أَسْتَجِيرُ بِكَ الْيَوْمَ مِنْ سَخَطِكَ ، فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ أَجِرْنِي
وَ أَسْأَلُكَ أَمْناً مِنْ عَذَابِكَ ، فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ آمِنِّي .
وَ أَسْتَهْدِيكَ ، فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ اهْدِنِي
وَ أَسْتَنْصِرُكَ ، فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ انْصُرْنِي .
وَ أَسْتَرْحِمُكَ ، فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ ارْحَمْنِي
وَ أَسْتَكْفِيكَ ، فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ اكْفِنِي
وَ أَسْتَرْزِقُكَ ، فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ ارْزُقْنِي
وَ أَسْتَعِينُكَ ، فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ أَعِنِّي .
وَ أَسْتَغْفِرُكَ لِمَا سَلَفَ مِنْ ذُنُوبِي ، فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ اغْفِرْ لِي .
وَ أَسْتَعْصِمُكَ ، فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ اعْصِمْنِي ، فَإِنِّي لَنْ أَعُودَ لِشَيْءٍ كَرِهْتَهُ مِنِّي إِنْ شِئْتَ ذَلِكَ .
يَا رَبِّ يَا رَبِّ ، يَا حَنَّانُ يَا مَنَّانُ ، يَا ذَا الْجَلَالِ وَ الْإِكْرَامِ ، صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ اسْتَجِبْ لِي جَمِيعَ مَا سَأَلْتُكَ وَ طَلَبْتُ إِلَيْكَ وَ رَغِبْتُ فِيهِ إِلَيْكَ ، وَ أَرِدْهُ وَ قَدِّرْهُ وَ اقْضِهِ وَ أَمْضِهِ ، وَ خِرْ لِي فِيما تَقْضِي مِنْهُ ، وَ بَارِكْ لِي فِي ذَلِكَ ، وَ تَفَضَّلْ عَلَيَّ بِهِ ، وَ أَسْعِدْنِي بِمَا تُعْطِينِي مِنْهُ ، وَ زِدْنِي مِنْ فَضْلِكَ وَ سَعَةِ مَا عِنْدَكَ ، فَإِنَّكَ وَاسِعٌ كَرِيمٌ ، وَ صِلْ ذَلِكَ بِخَيْرِ الآْخِرَةِ وَ نَعِيمِهَا ، يَا أَرْحَمَ الرَّاحِمِينَ . (ثُمَّ تَدْعُو بِمَا بَدَا لَكَ ، وَ تُصَلِّي عَلَي مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ أَلْفَ مَرَّةٍ هَكَذَا كَانَ يَفْعَلُ عَلَيْهِ السَّلَامُ).
Na (ifuatayo ilikuwa ni) miongoni mwa dua zake, amani iwe juu yake, aliyokuwa akiisoma katika siku ya Idi al-Adha na siku ya Ijumaa:
Ewe Mwenye Ezi Mungu, hakika siku hii ni siku iliyobarikiwa na ni nadra (yenye taadhima maalumu), ambapo Waislamu hukusanyika ndani yake katika maeneo mbali mbali ya ardhi yako. Miongoni mwao kuna (watu mbali mbali akiwemo;) muombaji, mtafutaji, mwenye raghba pamoja na mwenye khofu, Nawe washuhudia haja zao (maombi ya matilaba yao). Basi (kwanza kabisa) nakuomba kwa ukarimu wako na fadhila zako, na wepesi wa maombi yangu (haya) kwako, umrehemu Muhammad na Aali zake.
Na nakuomba Ewe Allah, Mola wetu mlezi, kwa kuwa Wewe ndiye Mwenye ufalme, na sifa njema zote ni Zako, hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Wewe. Wewe ni Mpole, Mkarimu, Mwenye huruma, Mwingi wa kuneemesha, Mwenye utukufu na ukarimu, Muumba wa mbingu na ardhi. (Ninakuomba unikirimu hisa maalumu kutoka kwenye) Lolote lile ulilowakadiria waja Wako waumini miongoni mwa; kheri, au afya njema, au baraka, au uongofu, au amali za utiifu Kwako, au kheri unayowaneemesha kwayo ili kuwaongoza (ya kufika) Kwako, au kwa ajili ya kuwapandisha daraja mbele Yako, au kwa ajili ya kuwapa kheri za dunia na Akhera kupitia neema hiyo ya kheri Zako.
Na nakuomba Ewe Allah, Mola wetu mlezi, kwa kuwa Wewe ndiye Mwenye ufalme, na sifa njema zote ni Zako Wewe peke yako, hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Wewe tu. Nakuomba umteremshie swala na salamu (umrehemu) Muhammad, (ambaye ni) mja Wako, Mtume Wako, kipenzi Chako, na mteule Wako (Swafwatika) na ni chaguo Lako bora (Khiyaratika) miongoni mwa viumbe Wako. (Ninakuomba umsalie yeye pamoja) na Aali Muhammad (poja na Aali zake) watukufu (Al-Abrar), waliotakasika (Watoharifu) na walio bora (Al-Akhyar). (Ninakuomba uwarehemu) kwa rerema ambayo hakutakuwa na kiumbe awezaye kuidhibiti isipokuwa Wewe. Na (ninakuomba) utushirikishe katika kheri za wale waliokuomba ndani ya siku hii, miongoni mwa waja Wako Waumini, yaa Rabbal-‘Alamina (Ewe Mola wa walimwengu). Na (ninakuomba) utughufirie sisi pamoja na wao, hakika Wewe ni Muweza juu ya kila kitu.
Ewe Mwenye Ezi Mungu, nimekuja kwako na haja yangu, na leo hii (na wakati huu) nimekuwekea wazi shida yangu na umasikini wangu (mbele Yako). Nina matumaini makubwa zaidi juu ya msamaha Wako na rehema Zako, kuliko ninavyotegemea (kuliko matumaini yangu juu ya) matendo yangu. Hakika, msamaha Wako na rehema zako ni kubwa zaidi kuliko dhambi zangu. Hivyo basi, mswalie (mrehemu) Mtume Muhammad na Aali zake. Na ninakuomba, kwa uwezo wako, unisaidie (uchukue hatua ya) kunitimizia kila haja niliyo nayo, kwani hilo ni jepesi mno Kwako. Ninakuomba (unitimizie matilaba yangu haya) kutokana na uhitaji Kwako, na ukwasi (utajiri) Wako dhidi yangu. Hakika mimi sijawahi kupata kheri yoyote ile isipokuwa kutoka kwako, na hakuna yeyote aliyewahi kuniepusha na baya isipokuwa Wewe. Na wala hakujawahi kuokea mwingine yeyote yule aliyeniepusha na shari fulani isipokuwa Wewe. Na wala mimi simtumainii yeyote yule kunipa kheri za duniani na akhera isipokuwa Wewe.
Allahumma, kama vile waja wanavyojitayarisha na kujifunga nira (au mkaja) na kujiandaa kwa ajili ya safari ya kumtembelea kiumbe fulani kwa matarajio ya kupata fadhila pamoja na zawadi fulani kutoka kwake, nami nimejitayarisha kwa kujifunga mkaja kwa jitihada zangu, na nimejiandaa kwa maandalizi yangu yote, nikitaraji msamaha Wako na msaada Wako, na kwa ajili ya kupata neema Zako na zawadi (thawabu) Zako.
Ewe Mwenye Ezi Mungu, mrehema Muhammad na Aali zake. Na wala usinikatishe tamaa katika matarajio yangu haya ndani ya Siku hii ya leo. Ewe usiyejoshwa (asiyekanzwa) na ombi la mwenye kuomba, na (Ewe) asiyepungukiwa kutokana na uchukuaji wa mchukuaji fulani (uliyemruzuku kutoka ndany ya hazina Yako). Hakika, mimi sikukujia huku tegemeo langu likiwa ni yale matendo yangu mema niliyoyatenda, wala kwa kutumaini maombezi ya kiumbe fulani, bali nimekuja nikitumainia maombezi ya Muhammad na watu wa nyumba yake (Aali zake), amani yako iwe juu yake na juu yao.
Nimekuja kwako nikikiri kosa (langu) (pamoja) na kuitendea mabaya (kuidhulumu) nafsi yangu. Nimekuja kwako nikitumainia msamaha wako mkuu uliowasamehea (ulioutumia kuwasamehe) wakosaji. Na hata kudumu kwao katika kosa kubwa hakukukuzuia Wewe kuwarejea kwa rehema (Zako) na msamaha (Wako).
Ewe Yule mwenye rehema Zake ni kunjufu (enevu), na (Ewe Yule) mwenye msamaha adhimu (mkuu), Ewe Muadhamu, Ewe Muadhamu, Ewe Mkarimu, Ewe Mkarimu, mteremshie rehma (Zako) Mtume Muhammad pamoja na Aali zake, na unirudie (unitazame) kwa (jicho la) rehema Zako, na unihurumie kwa fadhila Zako, na unigubike (unitande kwa mtando) wa msamaha Wako.
Ewe Mwenye Ezi Mungu, bila shaka wadhifa huu adhimu (wa kusalisha Sala za Idi na Ijumaa), ni milki ya wasimamizi wako na wateule wako, na ni nafasi ya waaminifu wako (iliyoko) katika ngazi (daraja) ya juu uliyowatunuku, ambayo umekuja porwa kutoka kwao. Nawe Ndiye mpangaji wa matukio haya yote (Ndiye mkadiriaji wa hayo); amri yako haipingiki, na wala uamuzi wako usioepukika hauwezi kukiukwa, (bali maamuzi Yako hutimia) kwa namna yoyote ile upendayo na kwa wakati wowote ule uupangao. (Kwani) haya hutendeka kulingana na hekima yako kuu, bila kuwepo tuhuma yoyote ile juu ya uumbaji wako au matakwa yako (katika utendaji Wako). (Matokeo hayo yaliotendeka chini ya hekima na maamuzi Yako yameendelea hadi), wateule na Wako na viongozi Wako wakajikuta katika hali ya kushindwa, kukandamizwa na kunyang'anywa mamlaka yao. Wanashuhudia sheria Zako zikigeuzwa, maandiko Yako matakatifu yakipuuzwa, amri Zako za lazima zikipotoshwa kutoka kwenye misingi ya sheria Zako, na mwenendo wa Mtume wako ukiachwa (Sunna za Mtume Wako kitenguliwa na kutupiliwa mbali).
Ewe Mwenye Ezi Mungu, walaani maadui zao wote, kuanzia wa mwanzo hadi wa mwisho. Vilevile, mlaani yeyote yule aliyeridhika na matendo yao, pamoja na washirika wao na wafuasi wao.
Ewe Mwenye Ezi Mungu, mbariki Muhammad na Aali Zake. Hakika Wewe ni Mstahiki wa sifa njema (Mhimidiwa) na Mtukufu (Muadhamu). (Mbariki kwa) baraka zilizo sawa na zile sala na baraka Zako zilizo juu ya wateule Wako, (ambao ni) Ibrahim na Aali Ibrahim. Na uwaharakishie faraja, amani, ushindi, uwezo pamoja na msaada (pamoja na kuwaunga mkono).
Ewe Mwenye Ezi Mungu, (nakuomba nami mja wako) unijaawe niwe miongoni mwa watu wa Tawhidi na (miongoni mwa) wenye kukuamini, na niwe pamoja na wale wenye kusadiki Utume wa Mtume wako, pamoja na Maimamu uliofaradhisha (uliotufaradhishia) utiifu wao, ambao (mambo ya dini) hujiri kupitia wao na mikononi mwao. Amina, ya Rabbi-l-alamina.
Allahumma, hapana kirejeshecho (nyuma) ghadhabu Zako ila ni huruma Zako, na wala hakuna cha kurejesha nyuma (kiakhirishi cha) hasira Zako ila ni afuwa Yako (usamehevu Wako). Wala hakuna kiepushaji cha kuepusha adhabu Yako isipokuwa ni rehema Zako, na wala hakuna cha kuniokoa dhidi Yako (hakuna chakunitetea mbele Yako) isipokuwa unyenyekevu (kujipendekeza) mbele Yako Yako. Basi, mswalie Mtume Muhammad na Aali zake, na utupe, na utufariji Ewe Mola wangu, kwa faraja itokayo Kwako (faraja itakayotufikia) kwa ule uwezo unaoutumia katika kuwahuisha wafu miongoni mwa waja (Wako), na kwa kupitia uwezu unaoutumia katika kueneza uhai kwenye ardhi iliyo maiti (ardhi kame).
Ewe Mola wangu, na wala usiniangamize kwa huzuni kabla ya kunijibu (matilaba yangu), na unijulishe (usinifunulie) jawabu ya dua yangu. Na (nakuomba) unionjeshe ladha ya afya njema hadi mwisho wa maisha yangu. (Na nakuomba) usimfanye adui yangu kufurahi (kutokana na masumbuko pamoja na madhila yangu), wala usimpe nafasi ya kunidhuru, na wala usimpe mamlaka juu yangu.
Mwenyezi Mungu, iwapo utanipandisha hadhi, ni nani basi atakayekuwa na uwezo wa kunishusha? Na endapo utanidunisha, ni yupi yule atakayeweza kunipandisha? Na ukinitukuza, ni nani atakayekwa na uwezo wa kunifedhehesha? Na pindi utakaponifedhehesha, ni nani yule atakayekwa na uwezo wa kunitukuza? Pindi ukiniadhibu, ni nani atakayenihurumia? Na iwapo utaniangamiza, ni nani yule atakayekuwa na uwezo wa pinga maamuzi yako juu ya mtumishi wako, au atakayekuwa na uwezo wa kukuuliza juu ya suala la mja Wako? Nimekwisha fahamu kuwa hakuna udhalimu (dhulma) katika uamuzi wako, wala hakuna papara katika malipizi Yako (kisasi Chako). Kwa hakika, anayefanya haraka ni yule anayehofia kupoteza fursa, na anayehitaji kutenda dhuluma ni yule kiumbe dhaifu. Nawe, Ee Mungu wangu, umeukiuka udhaifu huo kwa taadhima ya daraja la juu kabisa.
Ewe Mwenye Ezi Mungu, mrehema Mtume Muhammad na Aali zake. Na wala usinifanye kuwa ndiyo shabaha ya majaribu (Yako), wala (usinijaalie kuwa ndiye) shabaha (mlengwa) wa adhabu Yako. (Ewe Mwenye Ezi Mungu,) Nipe muhula, pamoja na nafuu, na unisamehe makosa yangu. Usinipe mtihani juu ya mtihani mwingine, kwani bila shaka Wewe ni mwenye kunaona (kujua) udhaifu wangu, na uchache wa uwezo wangu, na (ni mwenye kushuhudia) unyenyekevu wangu Kwako.
Ee Mwenye Ezi Mungu, leo hii ninajilinda kwako kutokana na hasira yako (dhidi ya hasira Zako). Hivyo basi (ninakuomba), umrehemu Muhammad na Aali zake, na unikinge (na ghadhabu Zako).
Na ninatafuta hifadhi kwako siku hii ya leo dhidi ya ghadhabu Zako. Hivyo basi, mrehemu Muhammad na Aali zake, na unipe hifadhi (dhidi ya ghadhabu Zako).
Na nakuomba amani (Ewe Mola wangu) dhidi ya adhabu yako, hivyo basi, mbariki Muhammad na Aali zake, na unisalimu (unipe amani dhidi ya adhabu Yako).
Na (Ewe Mola wangu) ninakuomba hidaya (Yako), hivyo basi, mbariki Muhammad na Aali zake, na uniongoze (kwa hidaya Yako).
Na (Ewe Mola wangu) ninakuomba ushindi (msaada) Wako, hiyo basi, mbariki Muhammad na Aali zake, na unipe ushindi (na unisaidie kwa msaada Wako).
Na (Ewe Mola wangu) ninakuomba rehema Zako; hiyo basi, mrehemu Muhammad na Aali zake, na unirehemu (kwa rehema Zako).
Na (Ewe Mola wangu) ninakuomba utoshelezaji (Wako), hivyo basi mrehemu Muhammad na Aali zake na unitosheleze (kwa mtoshelezo Wako).
Na (Ewe Mola wangu) ninakuomba riziki (Zako), hivyo basi, mbariki Muhammad na Aali zake, na niruzuku (kwa rizki Zako).
Nami (Ewe Mola wangu) natafuta msaada kutoka Kwako; kwa hiyo, mrehemu Muhammad na Aali zake, na unipe msaada (na unisaidie kwa msaada Wako).
Nami (Ewe Mola wangu) ninatubu kwako kutokana na maasi yangu yaliyotangulia, hivyo basi, mrehemu Muhammad na Aali zake, na unighufirie (dhambi zangu kwa msamaha Wako)
Nami (Ewe Mola wangu) ninatafuta hifadhi kwako, hivyo basi mrehemu Muhammad na Aali zake, na unihifadhi (kwa hifadhi yako). Hakika mimi katu sitarudia tena jambo ulilolichukia kutoka kwangu, uwapo utaniunga mkono kwa taufiki ya matakwa Yako.
Ewe Mola wangu Mlezi! Ewe Mola wangu Mlezi! Ewe Mrehemevu Mwenye wingi wa Rehema, Ewe Mpaji (Mtoaji) kwa ukarimu usio na mipaka, Mwenye utukufu na taadhima. Mrehemu Muhammad na Aali zake, kisha (nakuomba) unijibie maombi yangu yote (ninayoyawasilisha Kwako), na matilaba yangu yote niliyoyafikisha mbele Yako, pamoja na raghaba zangu (zote) zilizonileta kwako. (Ewe Mola) Yawezeshe (yape maombi yangu haya msukumo wa matakwa Yako), kisha uyapange (uyakadirie na uyapitishe), na hatimae uyapige muhuri (wa utendekaji). Na (ninakuomba) unielekeze kwenye njia ya chaguo lako bora zaidi ndani ya maamuzi yako, na unibariki katika hilo. Na (ninakuomba) unifadhilishe kwa neema hizo, na unijalie kuwa na furaha katika yale unayonitunuku. Pia (ninakuomba) unipe nyongeza (maalumu) kutoka katika hazina ya fadhila zako na wasaa (ukunjufu) wa yale uliyonayo, kwani wewe ni Mwenye wasaa (Mkunjufu) na Mkarimu. Ewe Mrehemevu uliyewapindukia warehemevu wote! Ninakuomba uniunganishie baraka hizi na mafanikio haya, na zile neema (na baraka) za maisha ya baada ya kifo. (Ukiomba dua, Baada ya kufika katika kipengele hichi, omba haja zako binafsi uitakayo, kisha umtakie rehema Mtume Muhammad na Aali zake mara elfu moja; hivyo ndivyo alivyokuwa akitenda (Imamu Sajjad) amani iwe juu yake).
Rejea
- ↑ Mamduhi Kermanshahi, Shuhud wa Shenakht, 1388, juz. 4, uk. 223.
- ↑ Mamduhi Kermanshahi, Shuhud wa Shenakht, 1388, juz. 4, uk. 260.
- ↑ Mamduhi Kermanshahi, Shuhud wa Shenakht, 1388, juz. 4, uk. 341-362.
- ↑ Ansarian, Diyar Asheqan, 1373, juz. 7, uk. 557-576.
- ↑ Mamduhi, Kitab Shuhud wa Shenakht, 1388, juz. 3, uk. 215-267.
- ↑ Fahri, Sherh wa Tafsir Sahifa Sajjadih, 1388, juz. 3, uk. 505-516.
- ↑ Madani Shirazi, Riyadh al-Salikin, 1435 AH, juz. 7, uk. 163-242.
- ↑ Mughniyah, Fi Dhilal al-Sahifa, 1428 AH, uk. 611-624.
- ↑ Darabi, Riyadh al-Arifin, 1379 AH, uk. 661-680.
- ↑ Fadhlullah, Afaq al-Ruh, 1420 AH, juz. 2, uk. 545-572.
- ↑ Faydh Kashani, Ta'baqat al-Sahifa al-Sajjadiyyah, 1407 AH, uk. 98-99.
- ↑ Jazairi, Sharh al-Sahifa al-Sajjadiyyah, 1402 AH, uk. 270-277.
Vyanzo
- Ansarian, Hussein, Diyar Asheqan, Tafsir Jamii Sahifa Sajjadiyah, Tehran, Payam Azadi, 1374.
- Jazairi, Izu-Din, Sherh al-Sahifa al-Sajjadiyyah, Beirut, Dar al-Taaruf Lil-Matbuat, 1402 AH.
- Darabi, Muhammad bin Muhammad, Riyadh al-Arifin Fi Sherh Sahifa Sajjadiyah, Muhaqiq Hussein Dargahi, Tehran, Nashr Us-wah, 1379.
- Fadhlullah, Sayyid Muhammad Hussein, A'faq al-Ruh, Beirut, Dar al-Malik, 1420 AH.
- Fahri, Sayyid Ahmad, Sherh wa Tarjume Sahifa Sajjadiyeh, Tehran, Us-wah, 1388 S.
- Faidh Kashani, Muhammad bin Murtaza, Taaliqat Ala Sahifa Sajjadiyah, Tehran, Muasase al-Bahth wa al-Tahqiqat al-Thaqafiyah, 1407 AH.
- Mughniyeh, Muhammad Jawad, Fi Dhilal al-Sahifa al-Sajjadiyyah, Qom, Dar al-Kitab al-Islami, 1428 AH.
- Madani Shirazi, Sayyid Ali Khan, Riyadh al-Salikiin Fi Sherh Sahifa Sayyid al-Sajidin, Qom, Muasase al-Nashr al-Islami, 1435 AH.
- Mamduhi Kermanshahi, Hassan, Shuhud wa Shenakhte: Tarjume wa Sherh Sahifa al-Sajjadiyyah, Ba Muqadime Ayatullah Jawadi Amuli, Qom, Bostan Kitab, 1385 S.